1 TIMOTHEO

Sura: 1, 2, 3, 4, 5, 6

1 TIMOTHEO 1


1 Paulo, mtume wa Kristo Yesu, kwa amri ya Mungu Mwokozi wetu na Kristo Yesu, taraja letu;
2 kwa Timotheo, mwanangu hasa katika imani. Neema na iwe kwako, na rehema, na amani, zitokazo kwa Mungu Baba na kwa Kristo Yesu Bwana wetu.
3 Kama vile nilivyokusihi ukae Efeso, nilipokuwa nikisafiri kwenda Makedonia, ili uwakataze wengine wasifundishe elimu nyingine;
4 wala wasiangalie hadithi na nasaba zisizo na ukomo, ziletazo maswali wala si madaraka ya Mungu yaliyo katika imani; basi ufanye hivyo.
5 Walakini mwisho wa agizo hilo ni upendo utokao katika moyo safi na dhamiri njema, na imani isiyo na unafiki.
6 Wengine wakiyakosa hayo wamegeukia maneno ya ubatili;
7 wapenda kuwa waalimu wa sheria, ingawa hawayafahamu wasemayo wala mambo yale wayanenayo kwa uthabiti.
8 Lakini twajua ya kuwa sheria ni njema, kama mtu akiitumia kwa njia iliyo halali;
9 akilifahamu neno hili, ya kuwa sheria haimhusu mtu wa haki, bali waasi, na wasio wataratibu, na makafiri, na wenye dhambi, na wanajisi, na wasiomcha Mungu, na wapigao baba zao, na wapigao mama zao, na wauaji,
10 na wazinifu, na wafiraji, na waibao watu, na waongo, nao waapao kwa uongo; na likiwapo neno lo lote linginelo lisilopatana na mafundisho yenye uzima;
11 kama vile ilivyonenwa katika Habari Njema ya utukufu wa Mungu ahimidiwaye, niliyowekewa amana.
12 Nami namshukuru Kristo Yesu Bwana wetu, aliyenitia nguvu kwa sababu aliniona kuwa mwaminifu, akaniweka katika utumishi wake;
13 ingawa hapo kwanza nalikuwa mtukanaji, mwenye kuudhi watu, mwenye jeuri, lakini nalipata rehema kwa kuwa nalitenda hivyo kwa ujinga, na kwa kutokuwa na imani.
14 Na neema ya Bwana wetu ilizidi sana, pamoja na imani na pendo lililo katika Kristo Yesu.
15 Ni neno la kuaminiwa, tena lastahili kukubalika kabisa, ya kwamba Kristo Yesu alikuja ulimwenguni awaokoe wenye dhambi; ambao wa kwanza wao ni mimi.
16 Lakini kwa ajili hii nalipata rehema, ili katika mimi wa kwanza, Yesu Kristo audhihirishe uvumilivu wake wote; niwe kielelezo kwa wale watakaomwamini baadaye, wapate uzima wa milele.
17 Sasa kwa Mfalme wa milele, asiyeweza kuona uharibifu, asiyeonekana, Mungu peke yake, na iwe heshima na utukufu milele na milele. Amina.
18 Mwanangu Timotheo, nakukabidhi agizo hilo liwe akiba, kwa ajili ya maneno ya unabii yaliyotangulia juu yako, ili katika hayo uvipige vile vita vizuri;
19 uwe mwenye imani na dhamiri njema, ambayo wengine wameisukumia mbali, wakaangamia kwa habari ya Imani.
20 Katika hao wamo Himenayo na Iskanda, ambao nimempa Shetani watu hao, ili wafundishwe wasimtukane Mungu.

1 TIMOTHEO 2


1 Basi, kabla ya mambo yote, nataka dua, na sala, na maombezi, na shukrani, zifanyike kwa ajili ya watu wote;
2 kwa ajili ya wafalme na wote wenye mamlaka, tuishi maisha ya utulivu na amani, katika utauwa wote na ustahivu.
3 Hili ni zuri, nalo lakubalika mbele za Mungu Mwokozi wetu;
4 ambaye hutaka watu wote waokolewe, na kupata kujua yaliyo kweli.
5 Kwa sababu Mungu ni mmoja, na mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu ni mmoja, Mwanadamu Kristo Yesu;
6 ambaye alijitoa mwenyewe kuwa ukombozi kwa ajili ya wote, utakaoshuhudiwa kwa majira yake.
7 Nami kwa ajili ya huo naliwekwa niwe mhubiri na mtume, (nasema kweli, sisemi uongo), mwalimu wa Mataifa katika imani na kweli.
8 Basi, nataka wanaume wasalishe kila mahali, huku wakiinua mikono iliyotakata pasipo hasira wala majadiliano.
9 Vivyo hivyo wanawake na wajipambe kwa mavazi ya kujisitiri, pamoja na adabu nzuri, na moyo wa kiasi; si kwa kusuka nywele, wala kwa dhahabu na lulu, wala kwa nguo za thamani;
10 bali kwa matendo mema, kama iwapasavyo wanawake wanaoukiri uchaji wa Mungu.
11 Mwanamke na ajifunze katika utulivu, akitii kwa kila namna.
12 Simpi mwanamke ruhusa ya kufundisha, wala kumtawala mwanamume, bali awe katika utulivu.
13 Kwa maana Adamu ndiye aliyeumbwa kwanza, na Hawa baadaye.
14 Wala Adamu hakudanganywa, ila mwanamke alidanganywa kabisa akaingia katika hali ya kukosa.
15 Walakini ataokolewa kwa uzazi wake, kama wakidumu katika imani na upendo na utakaso, pamoja na moyo wa kiasi.

1 TIMOTHEO 3


1 Ni neno la kuaminiwa; mtu akitaka kazi ya askofu, atamani kazi njema.
2 Basi imempasa askofu awe mtu asiyelaumika, mume wa mke mmoja, mwenye kiasi na busara, mtu wa utaratibu, mkaribishaji, ajuaye kufundisha;
3 si mtu wa kuzoelea ulevi, si mpiga watu; bali awe mpole; si mtu wa kujadiliana, wala asiwe mwenye kupenda fedha;
4 mwenye kuisimamia nyumba yake vema, ajuaye kutiisha watoto katika ustahivu;
5 (yaani, mtu asiyejua kuisimamia nyumba yake mwenyewe, atalitunzaje Kanisa la Mungu?)
6 Wala asiwe mtu aliyeongoka karibu, asije akajivuna akaanguka katika hukumu ya Ibilisi.
7 Tena imempasa kushuhudiwa mema na watu walio nje; ili asianguke katika lawama na mtego wa Ibilisi.
8 Vivyo hivyo mashemasi na wawe wastahivu; si wenye kauli mbili, si watu wa kutumia mvinyo sana,si watu wanaotamani fedha ya aibu.
9 wakiishika siri ya imani katika dhamiri safi.
10 Hawa pia na wajaribiwe kwanza; baadaye waitende kazi ya shemasi, wakiisha kuonekana kuwa hawana hatia.
11 Vivyo hivyo wake zao na wawe wastahivu; si wasingiziaji; watu wa kiasi, waaminifu katika mambo yote.
12 Mashemasi na wawe waume wa mke mmoja, wakiwasimamia watoto wao vizuri, na nyumba zao.
13 Kwa maana watendao vema kazi ya shemasi hujipatia daraja nzuri, na ujasiri mwingi katika imani iliyo katika Kristo Yesu.
14 Nakuandikia hayo nikitaraji kuja kwako hivi karibu.
15 Lakini nikikawia, upate kujua jinsi iwapasavyo watu kuenenda katika nyumba ya Mungu, iliyo kanisa la Mungu aliye hai, nguzo na msingi wa kweli.
16 Na bila shaka siri ya utauwa ni kuu. Mungu alidhihirishwa katika mwili, Akajulika kuwa na haki katika roho, Akaonekana na malaika, Akahubiriwa katika mataifa, Akaaminiwa katika ulimwengu, Akachukuliwa juu katika utukufu.

1 TIMOTHEO 4


1 Basi Roho anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani;
2 kwa unafiki wa watu wasemao uongo, wakichomwa moto dhamiri zao wenyewe;
3 wakiwazuia watu wasioe, na kuwaamuru wajiepushe na vyakula, ambavyo Mungu aliviumba vipokewe kwa shukrani na walio na imani wenye kuijua hiyo kweli.
4 Kwa maana kila kiumbe cha Mungu ni kizuri, wala hakuna cha kukataliwa, kama kikipokewa kwa shukrani;
5 kwa kuwa kimetakaswa kwa neno la Mungu na kwa kuomba.
6 Uwakumbushe ndugu mambo hayo, nawe utakuwa mtumishi mwema wa Kristo Yesu, na mzoevu wa maneno ya imani, na mafundisho mazuri yale uliyoyafuata.
7 Bali hadithi za kizee, zisizokuwa za dini, uzikatae; nawe ujizoeze kupata utauwa.
8 Kwa maana kujizoeza kupata nguvu za mwili kwafaa kidogo, lakini utauwa hufaa kwa mambo yote; yaani, unayo ahadi ya uzima wa sasa, na ya ule utakaokuwapo baadaye.
9 Ni neno la kuaminiwa, tena lastahili kukubalika kabisa;
10 kwa maana twajitaabisha na kujitahidi kwa kusudi hili, kwa sababu tunamtumaini Mungu aliye hai, aliye Mwokozi wa watu wote, hasa wa waaminio.
11 Mambo hayo uyaagize na kuyafundisha.
12 Mtu awaye yote asiudharau ujana wako, bali uwe kielelezo kwao waaminio, katika usemi na mwenendo, na katika upendo na imani na usafi.
13 Hata nitakapokuja, ufanye bidii katika kusoma na kuonya na kufundisha.
14 Usiache kuitumia karama ile iliyomo ndani yako, uliyopewa kwa unabii na kwa kuwekewa mikono ya wazee.
15 Uyatafakari hayo; ukae katika hayo; ili kuendelea kwako kuwe dhahiri kwa watu wote.
16 Jitunze nafsi yako, na mafundisho yako. Dumu katika mambo hayo; maana kwa kufanya hivyo utajiokoa nafsi yako na wale wakusikiao pia.

1 TIMOTHEO 5


1 Mzee usimkemee, bali umwonye kama baba; na vijana kama ndugu;
2 wanawake wazee kama mama; wanawake vijana kama ndugu wa kike; katika usafi wote.
3 Uwaheshimu wajane walio wajane kweli kweli.
4 Lakini mjane akiwa ana watoto au wajukuu, na wajifunze kwanza kuyatenda yaliyo wajibu wao kwa jamaa zao wenyewe, na kuwalipa wazazi wao. Kwa kuwa hili lakubalika mbele za Mungu.
5 Basi yeye aliye mjane kweli kweli, ameachwa peke yake, huyo amemwekea Mungu tumaini lake, naye hudumu katika maombi na sala mchana na usiku.
6 Bali, yeye asiyejizuia nafsi yake amekufa ingawa yu hai.
7 Mambo hayo pia uyaagize, ili wasiwe na lawama.
8 Lakini mtu ye yote asiyewatunza walio wake, yaani, wale wa nyumbani mwake hasa, ameikana Imani, tena ni mbaya kuliko mtu asiyeamini.
9 Mjane asiandikwe isipokuwa umri wake amepata miaka sitini; naye amekuwa mke wa mume mmoja;
10 naye ameshuhudiwa kwa matendo mema; ikiwa amelea watoto, ikiwa amekaribisha wageni, ikiwa amewaosha watakatifu miguu, ikiwa amewasaidia wateswao, ikiwa amefuata kwa bidii kila tendo jema.
11 Bali wajane walio vijana ukatae kuwaandika hao, maana, wakizidiwa na tamaa kinyume cha Kristo, wataka kuolewa;
12 nao wana hukumu kwa kuwa wameiacha imani yao ya kwanza.
13 Tena, pamoja na hayo, hujifunza kuwa wavivu, wakizunguka-zunguka nyumba kwa nyumba; wala si wavivu tu, lakini ni wachongezi na wadadisi, wakinena maneno yasiyowapasa.
14 Basi napenda wajane, ambao si wazee, waolewe, wazae watoto, wawe na madaraka ya nyumbani; ili wasimpe adui nafasi ya kulaumu.
15 Kwa maana wengine wamekwisha kugeuka na kumfuata Shetani.
16 Mwanamke aaminiye, akiwa ana wajane, na awasaidie mwenyewe, Kanisa lisilemewe; ili liwasaidie wale walio wajane kweli kweli.
17 Wazee watawalao vema na wahesabiwe kustahili heshima maradufu; hasa wao wajitaabishao kwa kuhutubu na kufundisha.
18 Kwa maana andiko lasema, Usimfunge kinywa ng'ombe apurapo nafaka. Na tena, Mtenda kazi astahili ujira wake.
19 Usikubali mashitaka juu ya mzee, ila kwa vinywa vya mashahidi wawili au watatu.
20 Wale wadumuo kutenda dhambi uwakemee mbele ya wote, ili na wengine waogope.
21 Nakuagiza mbele za Mungu, na mbele za Kristo Yesu, na mbele za malaika wateule, uyatende hayo pasipo kuhukumu kwa haraka; usifanye neno lo lote kwa upendeleo.
22 Usimwekee mtu mikono kwa haraka, wala usizishiriki dhambi za watu wengine. Ujilinde nafsi yako uwe safi.
23 Tokea sasa usinywe maji tu lakini tumia mvinyo kidogo, kwa ajili ya tumbo lako, na magonjwa yakupatayo mara kwa mara.
24 Dhambi za watu wengine zi dhahiri, zatangulia kwenda hukumuni; wengine dhambi zao zawafuata.
25 Vivyo hivyo matendo yaliyo mazuri ya dhahiri; wala yale yasiyo dhahiri hayawezi kusitirika.

1 TIMOTHEO 6


1 Wo wote walio chini ya kongwa, hali ya utumwa, na wawahesabie bwana zao kuwa wamestahili heshima yote, jina la Mungu lisitukanwe wala mafundisho yetu.
2 Na wale walio na bwana waaminio wasiwadharau kwa kuwa ni ndugu; bali afadhali wawatumikie, kwa sababu hao waishirikio faida ya kazi yao wamekuwa wenye imani na kupendwa. Mambo hayo uyafundishe na kuonya.
3 Mtu awaye yote akifundisha elimu nyingine, wala hayakubali maneno yenye uzima ya Bwana wetu Yesu Kristo, wala mafundisho yapatanayo na utauwa,
4 amejivuna; wala hafahamu neno lo lote; bali ana wazimu wa kuwazia habari za maswali, na mashindano ya maneno, ambayo katika hayo hutoka husuda, na ugomvi, na matukano, na shuku mbaya;
5 na majadiliano ya watu walioharibika akili zao, walioikosa kweli, huku wakidhani ya kuwa utauwa ni njia ya kupata faida.
6 Walakini utauwa pamoja na kuridhika ni faida kubwa.
7 Kwa maana hatukuja na kitu duniani, tena hatuwezi kutoka na kitu;
8 ila tukiwa na chakula na nguo tutaridhika na vitu hivyo.
9 Lakini hao watakao kuwa na mali huanguka katika majaribu na tanzi, na tamaa nyingi zisizo na maana, zenye kudhuru, ziwatosazo wanadamu katika upotevu na uharibifu.
10 Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi.
11 Bali wewe, mtu wa Mungu, uyakimbie mambo hayo; ukafuate haki, utauwa, imani, upendo, saburi, upole.
12 Piga vita vile vizuri vya imani; shika uzima ule wa milele ulioitiwa, ukaungama maungamo mazuri mbele ya mashahidi wengi.
13 Nakuagiza mbele za Mungu anayevihifadhi hai vitu vyote, na mbele za Kristo Yesu, aliyeyaungama maungamo mazuri yale mbele ya Pontio Pilato,
14 kwamba uilinde amri hii pasipo mawaa, pasipo lawama, hata kufunuliwa kwake Bwana wetu Yesu Kristo;
15 ambako yeye kwa majira yake atakudhihirisha, yeye aliyehimidiwa, Mwenye uweza peke yake, Mfalme wa wafalme, Bwana wa mabwana;
16 ambaye yeye peke yake hapatikani na mauti, amekaa katika nuru isiyoweza kukaribiwa; wala hakuna mwanadamu aliyemwona, wala awezaye kumwona. Heshima na uweza una yeye hata milele. Amina.
17 Walio matajiri wa ulimwengu wa sasa uwaagize wasijivune, wala wasiutumainie utajiri usio yakini, bali wamtumaini Mungu atupaye vitu vyote kwa wingi ili tuvitumie kwa furaha.
18 Watende mema, wawe matajiri kwa kutenda mema, wawe tayari kutoa mali zao, washirikiane na wengine kwa moyo;
19 huku wakijiwekea akiba iwe msingi mzuri kwa wakati ujao, ili wapate uzima ulio kweli kweli.
20 Ee Timotheo, ilinde hiyo amana; ujiepushe na maneno yasiyo ya dini, yasiyo na maana, na mashindano ya elimu iitwayo elimu kwa uongo;
21 ambayo wengine wakiikiri hiyo wameikosa Imani. Neema na iwe pamoja nanyi.