WAGALATIA

Sura: 1, 2, 3, 4, 5, 6

WAGALATIA 1


1 Paulo, mtume, (si mtume wa wanadamu, wala kutumwa na mwanadamu, bali na Yesu Kristo, na Mungu Baba aliyemfufua kutoka kwa wafu),
2 na ndugu wote walio pamoja nami, kwa makanisa ya Galatia;
3 Neema na iwe kwenu, na amani, zitokazo kwa Mungu Baba, na kwa Bwana wetu Yesu Kristo;
4 ambaye alijitoa nafsi yake kwa ajili ya dhambi zetu, ili atuokoe na dunia hii mbovu iliyopo sasa, kama alivyopenda Mungu, Baba yetu.
5 Utukufu una yeye milele na milele, Amina.
6 Nastaajabu kwa kuwa mnamwacha upesi hivi yeye aliyewaita katika neema ya Kristo, na kugeukia injili ya namna nyingine.
7 Wala si nyingine; lakini wapo watu wawataabishao na kutaka kuigeuza injili ya Kristo.
8 Lakini ijapokuwa sisi au malaika wa mbinguni atawahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo tuliyowahubiri, na alaaniwe.
9 Kama tulivyotangulia kusema, na sasa, nasema tena, mtu awaye yote akiwahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo mliyoipokea, na alaaniwe.
10 Maana, sasa je! Ni wanadamu ninaowashawishi, au Mungu? Au nataka kuwapendeza wanadamu? Kama ningekuwa hata sasa nawapendeza wanadamu, singekuwa mtumwa wa Kristo.
11 Kwa maana, ndugu zangu, injili hiyo niliyowahubiri, nawajulisha ya kuwa siyo ya namna ya kibinadamu.
12 Kwa kuwa sikuipokea kwa mwanadamu wala sikufundishwa na mwanadamu, bali kwa ufunuo wa Yesu Kristo.
13 Maana mmesikia habari za mwenendo wangu zamani katika dini ya Kiyahudi, kwamba naliliudhi kanisa la Mungu kupita kiasi, nikaliharibu.
14 Nami naliendelea katika dini ya Kiyahudi kuliko wengi walio hirimu zangu katika kabila yangu, nikajitahidi sana katika kuyashika mapokeo ya baba zangu.
15 Lakini Mungu, aliyenitenga tangu tumboni mwa mama yangu, akaniita kwa neema yake,
16 alipoona vema kumdhihirisha Mwanawe ndani yangu, ili niwahubiri Mataifa habari zake; mara sikufanya shauri na watu wenye mwili na damu;
17 wala sikupanda kwenda Yerusalemu kwa hao waliokuwa mitume kabla yangu; bali nalikwenda zangu Arabuni, kisha nikarudi tena Dameski.
18 Kisha, baada ya miaka mitatu, nalipanda kwenda Yerusalemu ili nionane na Kefa, nikakaa kwake siku kumi na tano.
19 Lakini sikumwona mtume mwingine, ila Yakobo, ndugu yake Bwana.
20 Na hayo ninayowaandikia, angalieni, mbele za Mungu, sisemi uongo.
21 Baadaye nalikwenda pande za Shamu na Kilikia.
22 Lakini sikujulikana uso wangu na makanisa ya Uyahudi yaliyokuwa katika Kristo;
23 ila wamesikia tu ya kwamba huyo aliyetuudhi hapo kwanza, sasa anaihubiri imani ile aliyoiharibu zamani.
24 Wakamtukuza Mungu kwa ajili yangu.

WAGALATIA 2


1 Kisha, baada ya miaka kumi na minne, nalipanda tena kwenda Yerusalemu pamoja na Barnaba, nikamchukua na Tito pamoja nami.
2 Nami nalikwenda kwa kuwa nalifunuliwa, nikawaeleza injili ile niihubiriyo katika Mataifa, lakini kwa faragha kwa hao walio wenye sifa, isiwe labda napiga mbio bure, au nalipiga mbio bure.
3 Lakini Tito aliyekuwa pamoja nami, naye ni Myunani, hakulazimishwa kutahiriwa.
4 Bali kwa ajili ya ndugu za uongo walioingizwa kwa siri; ambao waliingia kwa siri ili kuupeleleza uhuru wetu tulio nao katika Kristo Yesu, ili watutie utumwani;
5 ambao hata saa moja hatukujitia chini yao, ili kwamba kweli ya Injili ikae pamoja nanyi.
6 Lakini wale wenye sifa ya kuwa wana cheo; (walivyokuwa vyo vyote ni mamoja kwangu; Mungu hapokei uso wa mwanadamu); nasema, hao wenye sifa hawakuniongezea kitu;
7 bali, kinyume cha hayo, walipoona ya kuwa nimekabidhiwa injili ya wasiotahiriwa, kama vile Petro ya waliotahiriwa;
8 (maana yeye aliyemwezesha Petro kuwa mtume wa waliotahiriwa ndiye aliyeniwezesha mimi kwenda kwa Mataifa);
9 tena walipokwisha kuijua ile neema niliyopewa; Yakobo, na Kefa, na Yohana, wenye sifa kuwa ni nguzo, walinipa mimi na Barnaba mkono wa kuume wa shirika; ili sisi tuende kwa Mataifa, na wao waende kwa watu wa tohara;
10 ila neno moja tu walitutakia, tuwakumbuke maskini; nami neno lilo hilo nalikuwa na bidii kulifanya.
11 Lakini Kefa alipokuja Antiokia, nalishindana naye uso kwa uso, kwa sababu alistahili hukumu.
12 Kwa maana kabla hawajaja watu kadha wa kadha waliotoka kwa Yakobo, alikuwa akila pamoja na watu wa Mataifa; lakini walipokuja wao, akarudi nyuma akajitenga, huku akiwaogopa waliotahiriwa.
13 Na hao Wayahudi wengine wakajigeuza pamoja naye, hata na Barnaba pia akachukuliwa na unafiki wao.
14 Walakini, nilipoona ya kuwa njia yao haiendi sawasawa na ile kweli ya Injili, nalimwambia Kefa mbele ya wote, Ikiwa wewe uliye Myahudi wafuata desturi za Mataifa, wala si za Wayahudi, kwa nini unawashurutisha Mataifa kufuata desturi za Wayahudi?
15 Sisi tulio Wayahudi kwa asili, wala si wakosaji wa Mataifa,
16 hali tukijua ya kuwa mwanadamu hahesabiwi haki kwa matendo ya sheria, bali kwa imani ya Kristo Yesu; sisi tulimwamini Kristo Yesu ili tuhesabiwe haki kwa imani ya Kristo, wala si kwa matendo ya sheria; maana kwa matendo ya sheria hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki.
17 Lakini ikiwa sisi wenyewe, kwa kutafuta kuhesabiwa haki katika Kristo, tulionekana kuwa wenye dhambi, je! Kristo amekuwa mtumishi wa dhambi? Hasha!
18 Maana nikiyajenga tena yale niliyoyabomoa, naonyesha ya kuwa mimi mwenyewe ni mkosaji.
19 Maana mimi kwa njia ya sheria naliifia sheria ili nimwishie Mungu.
20 Nimesulibiwa pamoja na Kristo; lakini ni hai; wala si mimi tena, bali Kristo yu hai ndani yangu; na uhai nilio nao sasa katika mwili, ninao katika imani ya Mwana wa Mungu, ambaye alinipenda, akajitoa nafsi yake kwa ajili yangu.
21 Siibatili neema ya Mungu; maana, ikiwa haki hupatikana kwa njia ya sheria, basi Kristo alikufa bure.

WAGALATIA 3


1 Enyi Wagalatia msio na akili, ni nani aliyewaloga, ninyi ambao Yesu Kristo aliwekwa wazi mbele ya macho yenu ya kuwa amesulibiwa?
2 Nataka kujifunza neno hili moja kwenu. Je! Mlipokea Roho kwa matendo ya sheria, au kwa kusikia kunakotokana na imani?
3 Je! Mmekuwa wajinga namna hii? Baada ya kuanza katika Roho, mnataka kukamilishwa sasa katika mwili?
4 Mmepatikana na mateso makubwa namna hii bure? Ikiwa ni bure kweli.
5 Basi, yeye awapaye Roho na kufanya miujiza kati yenu, je! Afanya hayo kwa matendo ya sheria, au kwa kusikia kunakotokana na imani?
6 Kama vile Ibrahimu alivyomwamini Mungu akahesabiwa haki.
7 Fahamuni basi, ya kuwa wale walio wa imani, hao ndio wana wa Ibrahimu.
8 Na andiko, kwa vile lilivyoona tangu zamani kwamba Mungu atawahesabia haki Mataifa kwa imani, lilimhubiri Ibrahimu habari njema zamani, kusema, Katika wewe Mataifa yote watabarikiwa.
9 Basi hao walio wa imani hubarikiwa pamoja na Ibrahimu aliyekuwa mwenye imani.
10 Kwa maana wale wote walio wa matendo ya sheria, wako chini ya laana; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu asiyedumu katika yote yaliyoandikwa katika kitabu cha torati, ayafanye.
11 Ni dhahiri ya kwamba hakuna mtu ahesabiwaye haki mbele za Mungu katika sheria; kwa sababu Mwenye haki ataishi kwa imani.
12 Na torati haikuja kwa imani, bali, Ayatendaye hayo ataishi katika hayo.
13 Kristo alitukomboa katika laana ya torati, kwa kuwa alifanywa laana kwa ajili yetu; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu aangikwaye juu ya mti;
14 ili kwamba baraka ya Ibrahimu iwafikilie Mataifa katika Yesu Kristo, tupate kupokea ahadi ya Roho kwa njia ya imani.
15 Ndugu zangu, nanena kwa jinsi ya kibinadamu. Lijapokuwa ni agano la mwanadamu, hata hivyo likiisha kuthibitika, hakuna mtu alibatilishaye, wala kuliongeza neno.
16 Basi ahadi zilinenwa kwa Ibrahimu na kwa mzao wake. Hasemi, Kwa wazao, kana kwamba ni wengi, bali kana kwamba ni mmoja, Kwa mzao wako, yaani, Kristo.
17 Nisemalo ni hili; agano lililothibitishwa kwanza na Mungu, torati iliyotokea miaka mia nne na thelathini baadaye hailitangui, hata kuibatilisha ile ahadi.
18 Kwa maana urithi ukiwa kwa sheria, hauwi tena kwa ahadi; lakini Mungu alimkirimia Ibrahimu kwa njia ya ahadi.
19 Torati ni nini basi? Iliingizwa kwa sababu ya makosa, hata aje huyo mzao aliyepewa ile ahadi; iliamriwa kwa utumishi wa malaika kwa mkono wa mjumbe.
20 Basi aliye mjumbe si mjumbe wa mmoja; bali Mungu ni mmoja.
21 Basi je! Torati haipatani na ahadi za Mungu? Hasha! Kwa kuwa, kama ingalitolewa sheria iwezayo kuhuisha, yakini haki ingalipatikana kwa sheria.
22 Lakini andiko limeyafunga yote chini ya nguvu ya dhambi, makusudi hao waaminio wapewe ile ahadi kwa imani ya Yesu Kristo.
23 Lakini kabla ya kuja ile imani tulikuwa tumewekwa chini ya sheria, tumefungwa mpaka ije ile imani itakayofunuliwa.
24 Hivyo torati imekuwa kiongozi kutuleta kwa Kristo, ili tuhesabiwe haki kwa imani.
25 Lakini, iwapo imani imekuja, hatupo tena chini ya kiongozi.
26 Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa Mungu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu.
27 Maana ninyi nyote mliobatizwa katika Kristo mmemvaa Kristo.
28 Hapana Myahudi wala Myunani. Hapana mtumwa wala huru. Hapana mtu mume wala mtu mke. Maana ninyi nyote mmekuwa mmoja katika Kristo Yesu.
29 Na kama ninyi ni wa Kristo, basi, mmekuwa uzao wa Ibrahimu, na warithi sawasawa na ahadi.

WAGALATIA 4


1 Lakini nasema ya kuwa mrithi, wakati wote awapo mtoto, hana tofauti na mtumwa, angawa ni bwana wa yote;
2 bali yu chini ya mawakili na watunzaji, hata wakati uliokwisha kuamriwa na baba.
3 Kadhalika na sisi, tulipokuwa watoto, tulikuwa tukitumikishwa na kawaida za kwanza za dunia.
4 Hata ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke, amezaliwa chini ya sheria,
5 kusudi awakomboe hao waliokuwa chini ya sheria, ili sisi tupate kupokea hali ya kuwa wana.
6 Na kwa kuwa ninyi mmekuwa wana, Mungu alimtuma Roho wa Mwanawe mioyoni mwetu, aliaye, Aba, yaani, Baba.
7 Kama ni hivyo, wewe si mtumwa tena bali u mwana; na kama u mwana, basi, u mrithi kwa Mungu.
8 Lakini wakati ule, kwa kuwa hamkumjua Mungu, mliwatumikia wao ambao kwa asili si miungu.
9 Bali sasa mkiisha kumjua Mungu, au zaidi kujulikana na Mungu, kwa nini kuyarejea tena mafundisho ya kwanza yaliyo manyonge, yenye upungufu, ambayo mnataka kuyatumikia tena?
10 Mnashika siku, na miezi, na nyakati, na miaka.
11 Nawachelea, isiwe labda nimejitaabisha bure kwa ajili yenu.
12 Ndugu zangu, nawasihi, iweni kama mimi, maana mimi ni kama ninyi. Hamkunidhulumu kwa lo lote.
13 Lakini mwajua ya kuwa naliwahubiri Injili mara ya kwanza kwa sababu ya udhaifu wa mwili;
14 na jaribu lililowapata katika mwili wangu hamkulidharau wala kulikataa, bali mlinipokea kama malaika wa Mungu, kama Kristo Yesu.
15 Ku wapi, basi, kule kujiita heri? Maana nawashuhudu kwamba, kama ingaliwezekana, mngaling'oa macho yenu, mkanipa mimi.
16 Je! Nimekuwa adui wenu kwa sababu nawaambia yaliyo kweli?
17 Hao wana shauku nanyi, lakini si kwa njia nzuri, bali wanataka kuwafungia nje, ili kwamba ninyi mwaonee wao shauku.
18 Navyo ni vizuri kuonewa shauku katika neno jema sikuzote, wala si wakati nikiwapo mimi pamoja nanyi tu.
19 Vitoto vyangu, ambao kwamba nawaonea utungu tena mpaka Kristo aumbike ndani yenu;
20 laiti ningekuwapo pamoja nanyi sasa, na kuigeuza sauti yangu! Maana naona shaka kwa ajili yenu.
21 Niambieni, ninyi mnaotaka kuwa chini ya sheria, je! Hamwisikii sheria?
22 Kwa maana imeandikwa ya kuwa, Ibrahimu alikuwa na wana wawili mmoja kwa mjakazi, na mmoja kwa mwungwana.
23 Lakini yule wa mjakazi alizaliwa kwa mwili, yule wa mwungwana kwa ahadi.
24 Mambo haya husemwa kwa mfano; kwa maana hawa ndio kama maagano mawili, moja kutoka mlima Sinai, lizaalo kwa utumwa, ambalo ni Hajiri.
25 Maana Hajiri ni kama mlima Sinai ulioko Arabuni, umelingana na Yerusalemu wa sasa; kwa kuwa anatumika pamoja na watoto.
26 Bali Yerusalemu wa juu ni mwungwana, naye ndiye mama yetu sisi.
27 Kwa maana imeandikwa, Furahi, wewe uliye tasa, usiyezaa; Paza sauti, ulie, wewe usiye na utungu; Maana watoto wake aliyeachwa pekee ni wengi Kuliko wa huyo aliye na mume.
28 Basi, ndugu zangu, kama Isaka sisi tu watoto wa ahadi.
29 Lakini kama vile siku zile yule aliyezaliwa kwa mwili alivyomwudhi yule aliyezaliwa kwa Roho, ndivyo ilivyo na sasa.
30 Lakini lasemaje andiko? Mfukuze mjakazi na mwanawe, kwa maana mwana wa mjakazi hatarithi kabisa pamoja na mwana wa mwungwana.
31 Ndiposa, ndugu zangu, sisi si watoto wa mjakazi, bali tu watoto wa huyo aliye mwungwana.

WAGALATIA 5


1 Katika ungwana huo Kristo alituandika huru; kwa hiyo simameni, wala msinaswe tena chini ya kongwa la utumwa.
2 Tazama, mimi Paulo nawaambia ninyi ya kwamba, mkitahiriwa, Kristo hatawafaidia neno.
3 Tena namshuhudia kila mtu atahiriwaye, kwamba ni wajibu wake kuitimiza torati yote.
4 Mmetengwa na Kristo, ninyi mtakao kuhesabiwa haki kwa sheria; mmeanguka na kutoka katika hali ya neema.
5 Maana sisi kwa Roho tunalitazamia tumaini la haki kwa njia ya imani.
6 Maana katika Kristo Yesu kutahiriwa hakufai neno, wala kutokutahiriwa, bali imani itendayo kazi kwa upendo.
7 Mlikuwa mkipiga mbio vizuri; ni nani aliyewazuia msiitii kweli?
8 Kushawishi huku hakukutoka kwake yeye anayewaita ninyi.
9 Chachu kidogo huchachua donge zima.
10 Nina matumaini kwenu katika Bwana, ya kwamba hamtakuwa na nia ya namna nyingine. Lakini yeye anayewafadhaisha atachukua hukumu yake, awaye yote.
11 Nami, ndugu zangu ikiwa ninahubiri habari ya kutahiriwa, kwa nini ningali ninaudhiwa? Hapo kwazo la msalaba limebatilika!
12 Laiti hao wanaowatia mashaka wangejikata nafsi zao!
13 Maana ninyi, ndugu, mliitwa mpate uhuru; lakini uhuru wenu usiwe sababu ya kuufuata mwili, bali tumikianeni kwa upendo.
14 Maana torati yote imetimilika katika neno moja, nalo ni hili, Umpende jirani yako kama nafsi yako.
15 Lakini mkiumana na kulana, angalieni msije mkaangamizana.
16 Basi nasema, Enendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili.
17 Kwa sababu mwili hutamani ukishindana na Roho, na Roho kushindana na mwili; kwa maana hizi zimepingana, hata hamwezi kufanya mnayotaka.
18 Lakini mkiongozwa na Roho, hampo chini ya sheria.
19 Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi,
20 ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi,
21 husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu.
22 Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu,
23 upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria.
24 Na hao walio wa Kristo Yesu wameusulibisha mwili pamoja na mawazo yake mabaya na tamaa zake.
25 Tukiishi kwa Roho, na tuenende kwa Roho.
26 Tusijisifu bure, tukichokozana na kuhusudiana.

WAGALATIA 6


1 Ndugu zangu, mtu akighafilika katika kosa lo lote, ninyi mlio wa Roho mrejezeni upya mtu kama huyo kwa roho ya upole, ukijiangalia nafsi yako usije ukajaribiwa wewe mwenyewe.
2 Mchukuliane mizigo na kuitimiza hivyo sheria ya Kristo.
3 Maana mtu akijiona kuwa ni kitu, naye si kitu, ajidanganya nafsi yake.
4 Lakini kila mtu na aipime kazi yake mwenyewe, ndipo atakapokuwa na sababu ya kujisifu ndani ya nafsi yake tu, wala si kwa mwenzake.
5 Maana kila mtu atalichukua furushi lake mwenyewe.
6 Mwanafunzi na amshirikishe mkufunzi wake katika mema yote.
7 Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi; kwa kuwa cho chote apandacho mtu, ndicho atakachovuna.
8 Maana yeye apandaye kwa mwili wake, katika mwili wake atavuna uharibifu; bali yeye apandaye kwa Roho, katika Roho atavuna uzima wa milele.
9 Tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho.
10 Kwa hiyo kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema; na hasa jamaa ya waaminio.
11 Tazameni ni kwa herufi gani kubwa nimewaandikia kwa mkono wangu mimi mwenyewe!
12 Wote watakao kuonekana ni wazuri kwa mambo ya mwili, ndio wanaowashurutisha kutahiriwa; makusudi wasiudhiwe kwa ajili ya msalaba wa Kristo, hilo tu.
13 Kwa maana hata wao wenyewe waliotahiriwa hawaishiki sheria; bali wanataka ninyi mtahiriwe, wapate kuona fahari katika miili yenu.
14 Lakini mimi, hasha, nisione fahari juu ya kitu cho chote ila msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambao kwa huo ulimwengu umesulibishwa kwangu, na mimi kwa ulimwengu.
15 Kwa sababu kutahiriwa si kitu, wala kutokutahiriwa, bali kiumbe kipya.
16 Na wote watakaoenenda kwa kanuni hiyo, amani na iwe kwao na rehema, naam, kwa Israeli wa Mungu.
17 Tangu sasa mtu asinitaabishe; kwa maana ninachukua mwilini mwangu chapa zake Yesu.
18 Ndugu zangu, neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na iwe pamoja na roho zenu. Amina.