MATENDO

Sura: 1, 2, 3, 4, 5, 6, 7, 8, 9, 10, 11, 12, 13, 14, 15, 16, 17, 18, 19, 20, 21, 22, 23, 24, 25, 26, 27, 28

MATENDO 1


1 Kitabu kile cha kwanza nalikiandika, Theofilo, katika habari ya mambo yote aliyoanza Yesu kufanya na kufundisha,
2 hata siku ile alipochukuliwa juu, alipokuwa amekwisha kuwaagiza kwa Roho Mtakatifu wale mitume aliowachagua;
3 wale aliowadhihirishia nafsi yake, kwa dalili nyingi, baada ya kuteswa kwake, ya kwamba yu hai, akiwatokea muda wa siku arobaini, na kuyanena mambo yaliyouhusu ufalme wa Mungu.
4 Hata alipokuwa amekutana nao aliwaagiza wasitoke Yerusalemu, bali waingoje ahadi ya Baba, ambayo mlisikia habari zake kwangu;
5 ya kwamba Yohana alibatiza kwa maji, bali ninyi mtabatizwa katika Roho Mtakatifu baada ya siku hizi chache.
6 Basi walipokutanika, wakamwuliza, wakisema, Je! Bwana, wakati huu ndipo unapowarudishia Israeli ufalme?
7 Akawaambia, Si kazi yenu kujua nyakati wala majira, Baba aliyoyaweka katika mamlaka yake mwenyewe.
8 Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.
9 Akiisha kusema hayo, walipokuwa wakitazama, akainuliwa, wingu likampokea kutoka machoni pao.
10 Walipokuwa wakikaza macho mbinguni, yeye alipokuwa akienda zake, tazama, watu wawili wakasimama karibu nao, wenye nguo nyeupe,
11 wakasema, Enyi watu wa Galilaya, mbona mmesimama mkitazama mbinguni? Huyu Yesu aliyechukuliwa kutoka kwenu kwenda juu mbinguni, atakuja jinsi iyo hiyo mlivyomwona akienda zake mbinguni.
12 Kisha wakarudi kwenda Yerusalemu kutoka mlima ulioitwa wa Mizeituni, ulio karibu na Yerusalemu, wapata mwendo wa sabato.
13 Hata walipoingia, wakapanda orofani, walipokuwa wakikaa; Petro, na Yohana, na Yakobo, na Andrea, Filipo na Tomaso, Bartholomayo na Mathayo, Yakobo wa Alfayo, na Simoni Zelote, na Yuda wa Yakobo.
14 Hawa wote walikuwa wakidumu kwa moyo mmoja katika kusali, pamoja nao wanawake, na Mariamu mama yake Yesu, na ndugu zake.
15 Siku zile akasimama Petro kati ya hao ndugu (jumla ya majina ilipata mia na ishirini), akasema,
16 Ndugu, ilipasa andiko litimizwe, alilolinena Roho Mtakatifu zamani kwa kinywa cha Daudi, katika habari za Yuda aliyewaongoza wao waliomkamata Yesu;
17 kwa sababu alikuwa amehesabiwa pamoja na sisi, akapata sehemu ya huduma hii.
18 (Basi mtu huyu alinunua konde kwa ijara ya udhalimu; akaanguka kwa kasi akapasuka matumbo yake yote yakatoka.
19 Ikajulikana na watu wote wakaao Yerusalemu; hata konde lile likaitwa kwa lugha yao Akeldama, maana yake, konde la damu.)
20 Kwa maana imeandikwa katika chuo cha Zaburi, Kikao chake na kiwe ukiwa, Wala asiwepo mtu mwenye kukaa humo;
21 Basi katika watu waliofuatana nasi wakati wote Bwana Yesu alipokuwa akiingia na kutoka kwetu,
22 kuanza tangu ubatizo wa Yohana, hata siku ile alipochukuliwa kwetu kwenda juu, inapasa mmoja wao awe shahidi wa kufufuka kwake pamoja nasi.
23 Wakaweka wawili, Yusufu, aitwaye Barsaba, aliyekuwa na jina la pili Yusto, na Mathiya.
24 Kisha wakaomba, wakasema, Wewe, Bwana, ujuaye mioyo ya watu wote, tuonyeshe ni nani uliyemchagua katika hawa wawili,
25 ashike mahali katika huduma hii na utume huu, alioukosa Yuda, aende zake mahali pake mwenyewe.
26 Wakawapigia kura; kura ikamwangukia Mathiya; naye akahesabiwa kuwa pamoja na mitume kumi na mmoja.

MATENDO 2


1 Hata ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja.
2 Kukaja ghafula toka mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi.
3 Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao.
4 Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka.
5 Na walikuwako Yerusalemu Wayahudi wakikaa, watu watauwa, watu wa kila taifa chini ya mbingu.
6 Basi sauti hii iliposikiwa makutano walikutanika, wakashikwa na fadhaa, kwa kuwa kila mmoja aliwasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe.
7 Wakashangaa wote, wakastaajabu wakiambiana, Tazama, hawa wote wasemao si Wagalilaya?
8 Imekuwaje basi sisi kusikia kila mtu lugha yetu tuliyozaliwa nayo?
9 Warparthi na Wamedi na Waelami, nao wakaao Mesopotamia, Uyahudi na Kapadokia, Ponto na Asia,
10 Frigia na Pamfilia, Misri na pande za Libia karibu na Kirene, na wageni watokao Rumi, Wayahudi na waongofu,
11 Wakrete na Waarabu; tunawasikia hawa wakisema kwa lugha zetu matendo makuu ya Mungu.
12 Wakashangaa wote wakaingiwa na shaka, wakiambiana, Maana yake nini mambo haya?
13 Wengine walidhihaki, wakisema, wamelewa kwa mvinyo mpya.
14 Lakini Petro akasimama pamoja na wale kumi na mmoja, akapaza sauti yake, akawaambia, Enyi watu wa Uyahudi, na ninyi nyote mkaao Yerusalemu, lijueni jambo hili, mkasikilize maneno yangu.
15 Sivyo mnavyodhani; watu hawa hawakulewa, kwa maana ni saa tatu ya mchana;
16 lakini jambo hili ni lile lililonenwa kwa kinywa cha nabii Yoeli,
17 Itakuwa siku za mwisho, asema Mungu, nitawamwagia watu wote Roho yangu, na wana wenu na binti zenu watatabiri; na vijana wenu wataona maono; na wazee wenu wataota ndoto.
18 Naam, na siku zile nitawamwagia watumishi wangu wanaume na wanawake Roho yangu, nao watatabiri.
19 Nami nitatoa ajabu katika mbingu juu, na ishara katika nchi chini, damu na moto, na mvuke wa moshi.
20 Jua litageuka kuwa giza, na mwezi kuwa damu, kabla ya kuja ile siku ya Bwana iliyo kuu na iliyo dhahiri.
21 Na itakuwa kila atakayeliitia jina la Bwana ataokolewa.
22 Enyi waume wa Israeli, sikilizeni maneno haya: Yesu wa Nazareti, mtu aliyedhihirishwa kwenu na Mungu kwa miujiza na ajabu na ishara, ambazo Mungu alizifanya kwa mkono wake kati yenu, kama ninyi wenyewe mnavyojua;
23 mtu huyu alipotolewa kwa shauri la Mungu lililokusudiwa, na kwa kujua kwake tangu zamani, ninyi mkamsulibisha kwa mikono ya watu wabaya, mkamwua;
24 ambaye Mungu alimfufua, akiufungua uchungu wa mauti, kwa sababu haikuwezekana ashikwe nao.
25 Maana Daudi ataja habari zake, Nalimwona Bwana mbele yangu siku zote, Kwa kuwa yuko upande wa mkono wangu wa kuume, nisitikisike.
26 Kwa hiyo moyo wangu ukapendezewa, ulimi wangu ukafurahi; Tena mwili wangu nao utakaa katika matumaini.
27 Kwa maana hutaiacha roho yangu katika kuzimu; Wala hutamtoa Mtakatifu wako aone uharibifu.
28 Umenijuvisha njia za uzima; Utanijaza furaha kwa uso wako.
29 Waume, ndugu zangu, mniwie radhi, niseme kwa ujasiri mbele yenu habari za baba yetu mkuu, Daudi, ya kuwa alifariki akazikwa, na kaburi lake liko kwetu hata leo.
30 Basi kwa kuwa ni nabii, akijua ya kuwa Mungu amemwapia kwa kiapo, ya kwamba katika uzao wa viuno vyake atamketisha mmoja katika kiti chake cha enzi;
31 yeye mwenyewe akitangulia kuyaona haya, alitaja habari za kufufuka kwake Kristo, ya kwamba roho yake haikuachwa kuzimu, wala mwili wake haukuona uharibifu.
32 Yesu huyo Mungu alimfufua, na sisi sote tu mashahidi wake.
33 Basi yeye, akiisha kupandishwa hata mkono wa kuume wa Mungu, na kupokea kwa Baba ile ahadi ya Roho Mtakatifu, amekimwaga kitu hiki mnachokiona sasa na kukisikia.
34 Maana Daudi hakupanda mbinguni; bali yeye mwenyewe anasema, Bwana alimwambia Bwana wangu, Keti upande wa mkono wangu wa kuume.
35 Hata nitakapowaweka adui zako chini ya miguu yako.
36 Basi nyumba yote ya Israeli na wajue yakini ya kwamba Mungu amemfanya Yesu huyo mliyemsulibisha kuwa Bwana na Kristo.
37 Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu?
38 Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.
39 Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie.
40 Akawashuhudia kwa maneno mengine mengi sana na kuwaonya, akisema, Jiokoeni na kizazi hiki chenye ukaidi.
41 Nao waliolipokea neno lake wakabatizwa; na siku ile wakaongezeka watu wapata elfu tatu.
42 Wakawa wakidumu katika fundisho la mitume, na katika ushirika, na katika kuumega mkate, na katika kusali.
43 Kila mtu akaingiwa na hofu; ajabu nyingi na ishara zikafanywa na mitume.
44 Na wote walioamini walikuwa mahali pamoja, na kuwa na vitu vyote shirika,
45 wakiuza mali zao, na vitu vyao walivyokuwa navyo, na kuwagawia watu wote kama kila mtu alivyokuwa na haja.
46 Na siku zote kwa moyo mmoja walidumu ndani ya hekalu, wakimega mkate nyumba kwa nyumba, na kushiriki chakula chao kwa furaha na kwa moyo mweupe,
47 wakimsifu Mungu, na kuwapendeza watu wote. Bwana akalizidisha kanisa kila siku kwa wale waliokuwa wakiokolewa.

MATENDO 3


1 Basi Petro na Yohana walikuwa wakikwea pamoja kwenda hekaluni, saa ya kusali, saa tisa.
2 Na mtu mmoja aliyekuwa kiwete toka tumboni mwa mamaye alichukuliwa na watu, ambaye walimweka kila siku katika mlango wa hekalu uitwao Mzuri, ili aombe sadaka kwa watu waingiao ndani ya hekalu.
3 Mtu huyu akiwaona Petro na Yohana wakiingia hekaluni aliomba apewe sadaka.
4 Na Petro, akimkazia macho, pamoja na Yohana, akasema, Tutazame sisi.
5 Akawaangalia, akitaraji kupata kitu kwao.
6 Lakini Petro akasema, Mimi sina fedha, wala dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho nikupacho. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, simama uende.
7 Akamshika mkono wa kuume, akamwinua, mara nyayo zake na vifundo vya miguu yake vikatiwa nguvu.
8 Akaondoka upesi akasimama, akaanza kwenda; akaingia ndani ya hekalu pamoja nao, akienda, akiruka-ruka, na kumsifu Mungu.
9 Watu wote wakamwona akienda, akimsifu Mungu.
10 Wakamtambua, ya kuwa yeye ndiye aliyekuwa akiketi na kuomba sadaka penye mlango Mzuri wa hekalu; wakajaa ushangao wakastaajabia mambo yale yaliyompata.
11 Basi alipokuwa akiwashika Petro na Yohana, watu wote wakawakusanyikia mbio katika tao lile lililoitwa tao la Sulemani, wakishangaa sana.
12 Hata Petro alipoyaona haya akawajibu wale watu, Enyi Waisraeli, mbona mnastaajabia haya, au mbona mnatukazia macho sisi, kana kwamba tumemfanya huyu aende kwa nguvu zetu sisi, au kwa utauwa wetu sisi?
13 Mungu wa Ibrahimu na wa Isaka na wa Yakobo, Mungu wa baba zetu, amemtukuza mtumishi wake Yesu, ambaye ninyi mlimsaliti na kumkana mbele ya Pilato, alipokuwa ametoa hukumu yake afunguliwe.
14 Bali ninyi mlimkana yule Mtakatifu, yule Mwenye haki, mkataka mpewe mwuaji;
15 mkamwua yule Mkuu wa uzima, ambaye Mungu amemfufua katika wafu; na sisi tu mashahidi wake.
16 Na kwa imani katika jina lake, jina lake limemtia nguvu mtu huyu mnayemwona na kumjua; na imani ile iliyo kwake yeye imempatia huyu uzima huu mkamilifu mbele yenu ninyi nyote.
17 Basi sasa, ndugu, najua ya kuwa mliyatenda haya kwa kutokujua kwenu, kama na wakuu wenu walivyotenda.
18 Lakini mambo yale aliyohubiri Mungu tangu zamani kwa kinywa cha manabii wake wote, ya kwamba Kristo wake atateswa, ameyatimiza hivyo.
19 Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake Bwana;
20 apate kumtuma Kristo Yesu mliyewekewa tangu zamani;
21 ambaye ilimpasa kupokewa mbinguni hata zije zamani za kufanywa upya vitu vyote, zilizonenwa na Mungu kwa kinywa cha manabii wake watakatifu tokea mwanzo wa ulimwengu.
22 Kwa maana Musa kweli alisema ya kwamba, Bwana Mungu wenu atawainulieni nabii, katika ndugu zenu, kama mimi; msikieni yeye katika mambo yote atakayonena nanyi.
23 Na itakuwa ya kwamba kila mtu asiyemsikiliza nabii huyo ataangamizwa na kutengwa na watu wake.
24 Naam, na manabii wote tangu Samweli na wale waliokuja baada yake, wote walionena, walihubiri habari za siku hizi.
25 Ninyi mmekuwa watoto wa manabii na wa maagano yale, ambayo Mungu aliagana na baba zenu, akimwambia Ibrahimu, Katika uzao wako kabila zote za ulimwengu zitabarikiwa.
26 Mungu, akiisha kumfufua mtumishi wake Yesu, alimtuma kwenu ninyi kwanza, ili kuwabarikia kwa kumwepusha kila mmoja wenu na maovu yake.

MATENDO 4


1 Hata walipokuwa wakisema na watu wale, makuhani na akida wa hekalu na Masadukayo wakawatokea,
2 wakifadhaika sana kwa sababu wanawafundisha watu na kuhubiri katika Yesu ufufuo wa wafu.
3 Wakawakamata, wakawaweka gerezani hata asubuhi; kwa kuwa imekwisha kuwa jioni.
4 Lakini wengi katika hao waliosikia lile neno waliamini; na hesabu ya watu waume ikawa kama elfu tano.
5 Hata asubuhi wakubwa na wazee na waandishi wakakusanyika Yerusalemu,
6 na Anasi Kuhani Mkuu, na Kayafa pia, na Yohana na Iskanda, na wote wale waliokuwa jamaa zake Kuhani Mkuu.
7 Walipowaweka katikati wakawauliza, Kwa nguvu gani na kwa jina la nani ninyi mmefanya haya?
8 Ndipo Petro, akijaa Roho Mtakatifu, akawaambia, Enyi wakubwa wa watu na wazee wa Israeli,
9 kama tukiulizwa leo habari ya jambo jema alilofanyiwa yule mtu dhaifu, jinsi alivyoponywa,
10 jueni ninyi nyote na watu wote wa Israeli ya kuwa kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, ambaye ninyi mlimsulibisha, na Mungu akamfufua katika wafu, kwa jina hilo mtu huyu anasimama ali mzima mbele yenu.
11 Yeye ndiye jiwe lile lililodharauliwa na ninyi waashi, nalo limewekwa kuwa jiwe kuu la pembeni.
12 Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.
13 Basi walipoona ujasiri wa Petro na Yohana, na kuwajua ya kuwa ni watu wasio na elimu, wasio na maarifa, wakastaajabu, wakawatambua ya kwamba walikuwa pamoja na Yesu.
14 Na wakimwona yule aliyeponywa akisimama pamoja nao hawakuwa na neno la kujibu.
15 Wakawaamuru kutoka katika baraza, wakafanya shauri wao kwa wao,
16 wakisema, Tuwafanyie nini watu hawa? Maana ni dhahiri kwa watu wote wakaao Yerusalemu ya kwamba ishara mashuhuri imefanywa nao, wala hatuwezi kuikana.
17 Lakini neno hili lisije likaenea katika watu, na tuwatishe wasiseme tena na mtu awaye yote kwa jina hili.
18 Wakawaita, wakawaamuru wasiseme kabisa wala kufundisha kwa jina la Yesu.
19 Petro na Yohana wakawajibu wakawaambia, Kwamba ni haki mbele za Mungu kuwasikiliza ninyi kuliko Mungu, hukumuni ninyi wenyewe;
20 maana sisi hatuwezi kuacha kuyanena mambo tuliyoyaona na kuyasikia.
21 Nao walipokwisha kuwatisha tena wakawafungua, wasione njia ya kuwaadhibu, kwa sababu ya watu; kwa kuwa watu wote walikuwa wakimtukuza Mungu kwa hayo yaliyotendeka;
22 maana umri wake yule mtu aliyefanyiwa ishara hii ya kuponya ulipita miaka arobaini.
23 Hata walipofunguliwa, wakaenda kwa watu wao, wakawapasha habari ya mambo yote waliyoambiwa na wakuu wa makuhani na wazee.
24 Nao waliposikia, wakampazia Mungu sauti zao kwa moyo mmoja, wakisema, Mola, wewe ndiwe Mungu, ndiwe uliyefanya mbingu na nchi na bahari na vitu vyote vilivyomo;
25 nawe ulinena kwa Roho Mtakatifu kwa kinywa cha babaetu Daudi, mtumishi wako, Mbona mataifa wamefanya ghasia, Na makabila wametafakari ubatili?
26 Wafalme wa dunia wamejipanga, Na wakuu wamefanya shauri pamoja Juu ya Bwana na juu ya Kristo wake.
27 Maana ni kweli, Herode na Pontio Pilato pamoja na Mataifa na watu wa Israeli, walikusanyika katika mji huu juu ya Mtumishi wako mtakatifu Yesu, uliyemtia mafuta,
28 ili wafanye yote ambayo mkono wako na mashauri yako yamekusudia tangu zamani yatokee.
29 Basi sasa, Bwana, yaangalie matisho yao; ukawajalie watumwa wako kunena neno lako kwa ujasiri wote,
30 ukinyosha mkono wako kuponya; ishara na maajabu vifanyike kwa jina la Mtumishi wako mtakatifu Yesu.
31 Hata walipokwisha kumwomba Mungu, mahali pale walipokusanyika pakatikiswa, wote wakajaa Roho Mtakatifu, wakanena neno la Mungu kwa ujasiri.
32 Na jamii ya watu walioamini walikuwa na moyo mmoja na roho moja; wala hapana mmoja aliyesema ya kuwa kitu cho chote alicho nacho ni mali yake mwenyewe; bali walikuwa na vitu vyote shirika.
33 Na mitume wakatoa ushuhuda wa kufufuka kwake Yesu kwa nguvu nyingi, na neema nyingi ikawa juu yao wote.
34 Wala hapakuwa na mtu mmoja miongoni mwao mwenye mahitaji; kwa sababu watu wote waliokuwa na viwanja au nyumba waliviuza, wakaileta thamani ya vitu vile vilivyouzwa,
35 wakaiweka miguuni pa mitume; kila mtu akagawiwa kwa kadiri ya alivyohitaji.
36 Na Yusufu, aliyeitwa na mitume Barnaba, (maana yake, Mwana wa faraja), Mlawi, asili yake ni mtu wa Kipro,
37 alikuwa na shamba akaliuza, akaileta fedha, akaiweka miguuni pa mitume.

MATENDO 5


1 Lakini mtu mmoja jina lake Anania, pamoja na Safira mkewe, aliuza mali,
2 akazuia kwa siri sehemu ya thamani yake, mkewe naye akijua haya, akaleta fungu moja akaliweka miguuni pa mitume.
3 Petro akasema, Anania, kwa nini Shetani amekujaza moyo wako kumwambia uongo Roho Mtakatifu, na kuzuia kwa siri sehemu ya thamani ya kiwanja?
4 Kilipokuwa kwako, hakikuwa mali yako? Na kilipokuwa kimekwisha kuuzwa, thamani yake haikuwa katika uwezo wako? Ilikuwaje hata ukaweka neno hili moyoni mwako? Hukumwambia uongo mwanadamu, bali Mungu.
5 Anania aliposikia maneno haya akaanguka, akafa. Hofu nyingi ikawapata watu wote walioyasikia haya.
6 Vijana wakaondoka, wakamtia katika sanda, wakamchukua nje, wakamzika.
7 Hata muda wa saa tatu baadaye mkewe akaingia, naye hana habari ya hayo yaliyotokea.
8 Petro akamjibu, Niambie, Mlikiuza kiwanja kwa thamani hiyo? Akasema, Ndiyo, kwa thamani hiyo.
9 Petro akamwambia, Imekuwaje hata mkapatana kumjaribu Roho wa Bwana? Angalia, miguu yao waliomzika mumeo ipo mlangoni, nao watakuchukua nje wewe nawe.
10 Mara akaanguka miguuni pake akafa; wale vijana wakaingia wakamkuta amekufa, wakamchukua nje, wakamzika pamoja na mumewe.
11 Hofu nyingi ikawapata kanisa lote na watu wote walioyasikia haya.
12 Na kwa mikono ya mitume zikafanyika ishara na maajabu mengi katika watu; nao wote walikuwako kwa nia moja katika ukumbi wa Sulemani;
13 na katika wote wengine hapana hata mmoja aliyethubutu kuambatana nao; ila watu waliwaadhimisha;
14 walioamini wakazidi kuongezeka kwa Bwana, wengi, wanaume na wanawake;
15 hata ikawa katika njia kuu hutoa nje wagonjwa, na kuwaweka juu ya majamvi na magodoro, ili Petro akija, ngawa kivuli chake kimwangukie mmojawapo wao.
16 Nayo makutano ya watu wa miji iliyoko kandokando ya Yerusalemu wakakutanika, wakileta wagonjwa, nao walioudhiwa na pepo wachafu; nao wote wakaponywa.
17 Akaondoka Kuhani Mkuu na wote waliokuwa pamoja naye, (hao ndio walio wa madhehebu ya Masadukayo), wamejaa wivu,
18 wakawakamata mitume wakawaweka ndani ya gereza;
19 lakini malaika wa Bwana akafungua milango ya gereza usiku, akawatoa, akasema,
20 Enendeni mkasimame hekaluni mkawaambie watu maneno yote ya Uzima huu.
21 Nao waliposikia wakaenda alfajiri hekaluni, wakaanza kufundisha. Akaja Kuhani Mkuu nao waliokuwa pamoja naye, wakawakutanisha watu wa baraza, na wazee wote wa wana wa Israeli, wakatuma watu gerezani ili wawalete.
22 Hata watumishi walipofika hawakuwaona gerezani, wakarudi wakatoa habari,
23 wakisema, Gereza tumeikuta imefungwa salama, nao walinzi wamesimama mbele ya mlango; lakini tulipoufungua hatukukuta mtu ndani.
24 Basi jemadari wa hekalu na wakuu wa makuhani waliposikia haya, wakaingiwa na shaka kwa ajili yao, litakuwaje jambo hilo.
25 Mtu mmoja akaja akawapasha habari ya kwamba, Watu wale mliowaweka gerezani wako ndani ya hekalu, wamesimama wakiwafundisha watu.
26 Ndipo yule jemadari akaenda pamoja na watumishi, wakawaleta, lakini si kwa nguvu, kwa maana waliogopa watu wasije wakawapiga kwa mawe.
27 Walipowaleta, wakawaweka katika baraza. Kuhani Mkuu akawauliza,
28 akisema, Je! Hatukuwaamuru ninyi kwa nguvu, msifundishe kwa jina hili? Nanyi, tazameni, mmeijaza Yerusalemu mafundisho yenu, na mnataka kuileta damu ya mtu yule juu yetu.
29 Petro na mitume wakajibu, wakisema, Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu.
30 Mungu wa baba zetu alimfufua Yesu, ambaye ninyi mlimwua mkimtundika katika mti.
31 Mtu huyo Mungu amemtukuza kwa mkono wake wa kuume, awe Mkuu na Mwokozi, awape Waisraeli toba na msamaha wa dhambi.
32 Na sisi tu mashahidi wa mambo haya, pamoja na Roho Mtakatifu ambaye Mungu amewapa wote wamtiio.
33 Wao waliposikia wakachomwa mioyo yao; wakafanya shauri kuwaua.
34 Lakini mtu mmoja, Farisayo, jina lake Gamalieli, mwalimu wa torati, mwenye kuheshimiwa na watu wote, akasimama katika baraza, akaamuru mitume wawekwe nje kitambo kidogo,
35 akawaambia, Enyi waume wa Israeli, jihadharini jinsi mtakavyowatenda watu hawa.
36 Kwa sababu kabla ya siku hizi aliondoka Theuda, akijidai ya kuwa yeye ni mtu mkuu, watu wapata mia nne wakashikamana naye; naye aliuawa na wote waliomsadiki wakatawanyika wakawa si kitu.
37 Baada ya mtu huyo aliondoka Yuda Mgalilaya, siku zile za kuandikiwa orodha, akawavuta watu kadha wa kadha nyuma yake, naye pia akapotea na wote waliomsadiki wakatawanyika.
38 Basi sasa nawaambia, Jiepusheni na watu hawa, waacheni; kwa kuwa shauri hili au kazi hii ikiwa imetoka kwa binadamu, itavunjwa,
39 lakini ikiwa imetoka kwa Mungu hamwezi kuivunja; msije mkaonekana kuwa mnapigana na Mungu.
40 Wakakubali maneno yake; nao walipowaita mitume, wakawapiga, wakawaamuru wasinene kwa jina lake Yesu; kisha wakawaacha waende zao.
41 Nao wakatoka katika ile baraza, wakifurahi kwa sababu wamehesabiwa kuwa wamestahili kuaibishwa kwa ajili ya Jina hilo.
42 Na kila siku, ndani ya hekalu na nyumbani mwao, hawakuacha kufundisha na kuhubiri habari njema za Yesu kwamba ni Kristo.

MATENDO 6


1 Hata siku zile wanafunzi walipokuwa wakiongezeka hesabu yao, palikuwa na manung'uniko ya Wayahudi wa Kiyunani juu ya Waebrania kwa sababu wajane wao walisahauliwa katika huduma ya kila siku.
2 Wale Thenashara wakawaita jamii ya wanafunzi, wakasema, Haipendezi sisi kuliacha neno la Mungu na kuhudumu mezani.
3 Basi ndugu, chagueni watu saba miongoni mwenu, walioshuhudiwa kuwa wema, wenye kujawa na Roho, na hekima, ili tuwaweke juu ya jambo hili;
4 na sisi tutadumu katika kuomba na kulihudumia lile Neno.
5 Neno hili likapendeza machoni pa mkutano wote; wakamchagua Stefano, mtu aliyejaa imani na Roho Mtakatifu, na Filipo, na Prokoro, na Nikanori, na Timoni, na Parmena, na Nikolao mwongofu wa Antiokia;
6 ambao wakawaweka mbele ya mitume, na walipokwisha kuomba wakaweka mikono yao juu yao.
7 Neno la Mungu likaenea; na hesabu ya wanafunzi ikazidi sana katika Yerusalemu; jamii kubwa ya makuhani wakaitii ile Imani.
8 Na Stefano, akijaa neema na uwezo, alikuwa akifanya maajabu na ishara kubwa katika watu.
9 Lakini baadhi ya watu wa sinagogi lililoitwa sinagogi la Mahuru, na la Wakirene, na la Waiskanderia, na la wale wa Kilikia na Asia, wakaondoka na kujadiliana na Stefano;
10 lakini hawakuweza kushindana na hiyo hekima na huyo Roho aliyesema naye.
11 Hata wakashawishi watu waliosema, Tumemsikia mtu huyu akinena maneno ya kumtukana Musa na Mungu.
12 Wakawataharakisha watu na wazee na waandishi, wakamwendea, wakamkamata, wakampeleka mbele ya baraza.
13 Wakasimamisha mashahidi wa uongo waliosema, Mtu huyu haachi kusema maneno ya kufuru juu ya mahali hapa patakatifu na juu ya torati;
14 maana tumemsikia akisema kwamba Yesu huyo Mnazareti atapaharibu mahali hapa, na kuzibadili desturi tulizopewa na Musa.
15 Watu wote walioketi katika ile baraza wakamkazia macho yao, wakamwona uso wake kuwa kama uso wa malaika.

MATENDO 7


1 Kuhani Mkuu akasema, Je! Mambo hayo ndivyo yalivyo?
2 Naye akasema, Ndugu zangu na baba zangu, sikilizeni: Mungu wa utukufu alimtokea baba yetu Ibrahimu, alipokuwa katika Mesopotamia, kabla hajakaa Harani,
3 akamwambia, Toka katika nchi yako na katika jamaa zako, ukaende hata nchi nitakayokuonyesha.
4 Ndipo alipotoka katika nchi ya Wakaldayo, akakaa Harani, akatoka huko baada ya kufa babaye, Mungu akamhamisha mpaka nchi hii mnayokaa ninyi sasa.
5 Wala hakumpa urithi humu hata kiasi cha kuweka mguu; akaahidi kwamba atampa, iwe milki yake, na ya uzao wake baadaye alipokuwa hana mtoto.
6 Mungu akanena hivi, ya kwamba wazao wake watakuwa wageni katika nchi ya watu wengine, nao watawafanya kuwa watumwa wao, na kuwatenda mabaya kwa muda wa miaka mia nne.
7 Na lile taifa watakaowafanya watumwa nitawahukumu mimi, alisema Mungu; na baada ya hayo watatoka, nao wataniabudu mahali hapa.
8 Akampa agano la tohara; basi Ibrahimu akamzaa Isaka, akamtahiri siku ya nane. Isaka akamzaa Yakobo. Yakobo akawazaa wale kumi na wawili, wazee wetu.
9 Wale wazee wetu wakimwonea wivu Yusufu, wakamwuza aende Misri. Mungu akawa pamoja naye,
10 akamtoa katika dhiki zake zote, akampa fadhili na hekima mbele ya Farao, mfalme wa Misri; naye akamfanya awe mtawala juu ya Misri na nyumba yake yote.
11 Basi kukawa njaa katika nchi yote ya Misri na Kanaani, na dhiki nyingi, wala baba zetu hawakupata chakula cha kuwatosha.
12 Hata Yakobo aliposikia ya kwamba huko Misri kuna nafaka, akawatuma baba zetu mara ya kwanza.
13 Hata safari ya pili Yusufu akajitambulisha kwa ndugu zake, jamaa ya Yusufu ikawa dhahiri kwa Farao.
14 Yusufu akatuma watu akamwita Yakobo babaye na jamaa zake wote pia, watu sabini na watano.
15 Basi Yakobo akashuka mpaka Misri; akafa yeye na baba zetu;
16 wakachukuliwa mpaka Shekemu wakazikwa katika kaburi lile, ambalo Ibrahimu alilinunua kwa kima cha fedha kwa wana wa Hamori, huko Shekemu.
17 Basi wakati wa ile ahadi ambayo Mungu alimpa Ibrahimu ulipokuwa unakaribia, wale watu wakazidi na kuongezeka sana huko Misri,
18 hata mfalme mwingine akainuka juu ya Misri, asiyemfahamu Yusufu.
19 Huyo akawafanyia hila kabila yetu, na kuwatenda mabaya baba zetu, akiwaamuru wawatupe watoto wao wachanga, ili wasiishi.
20 Wakati huo akazaliwa Musa, naye alikuwa mzuri sana, akalelewa muda wa miezi mitatu katika nyumba ya babaye.
21 Hata alipotupwa, binti Farao akamtwaa, akamlea awe kama mwanawe.
22 Musa akafundishwa hekima yote ya Wamisri, akawa hodari wa maneno na matendo.
23 Umri wake ulipopata kama miaka arobaini akaazimu moyoni mwake kwenda kuwatazama ndugu zake Waisraeli.
24 Akamwona mmoja akidhulumiwa, akamtetea, akamlipia kisasi yule aliyekuwa akionewa, akampiga huyo Mmisri.
25 Alidhani kwamba ndugu zake watafahamu ya kuwa Mungu anawapa wokovu kwa mkono wake, lakini hawakufahamu.
26 Siku ya pili yake akawatokea walipokuwa wakishindana, akataka kuwapatanisha, akisema, Enyi bwana zangu, ninyi ni ndugu. Mbona mnadhulumiana?
27 Lakini yeye aliyemdhulumu mwenziwe akamsukumia mbali, akisema, Ni nani aliyekuweka wewe kuwa mkuu na mwamuzi juu yetu?
28 Je! Wataka kuniua mimi kama ulivyomwua yule Mmisri jana?
29 Musa akakimbia kwa neno hilo, akakaa hali ya ugeni katika nchi ya Midiani, akazaa wana wawili huko.
30 Hata miaka arobaini ilipotimia, malaika wa Bwana akamtokea katika jangwa la mlima wa Sinai katika mwali wa moto, kijitini.
31 Musa alipouona, akastaajabia maono yale, na alipokaribia ili atazame, sauti ya Bwana ikamjia,
32 Mimi ni Mungu wa baba zako, Mungu wa Ibrahimu, na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo. Musa akatetemeka, asithubutu kutazama.
33 Bwana akamwambia, Vua viatu miguuni mwako, kwa maana mahali hapa unaposimama ni nchi takatifu.
34 Yakini nimeona mateso ya watu wangu waliomo Misri, nimesikia kuugua kwao, nami nimeshuka niwatoe. Basi sasa, nitakutuma mpaka Misri.
35 Musa huyo waliyemkataa, wakisema, Ni nani aliyekuweka kuwa mkuu na mwamuzi? Ndiye aliyetumwa na Mungu kuwa mkuu na mkombozi, kwa mkono wa yule malaika aliyemtokea katika kile kijiti.
36 Huyo ndiye aliyewatoa, akifanya ajabu na ishara katika nchi ya Misri, na katika bahari ya Shamu, na katika jangwa muda wa miaka arobaini.
37 Musa huyo ndiye aliyewaambia Waisraeli, Bwana Mungu wenu atawainulieni nabii, katika ndugu zenu, kama mimi; msikieni yeye.
38 Yeye ndiye aliyekuwa katika kanisa jangwani pamoja na yule malaika aliyesema naye katika mlima wa Sinai, tena pamoja na baba zetu; ndiye aliyepokea maneno ya uzima atupe sisi.
39 Mtu huyo baba zetu hawakutaka kumtii, bali wakamsukumia mbali, na kwa mioyo yao wakarejea Misri,
40 wakamwambia Haruni, Tufanyie miungu, watakaotutangulia; maana huyo Musa, aliyetutoa katika nchi ya Misri, hatujui lililompata.
41 Wakafanya ndama siku zile, wakaleta dhabihu kwa sanamu ile, wakafurahia kazi za mikono yao.
42 Basi Mungu akaghairi, akawaacha ili waliabudu jeshi la mbinguni, kama ilivyoandikwa katika chuo cha manabii, Je! Mlinitolea mimi dhabihu na sadaka Miaka arobaini katika jangwa, enyi nyumba ya Israeli?
43 Nanyi mlichukua hema ya Moleki, Na nyota za mungu wenu Refani, Sanamu mlizozifanya ili kuziabudu; Nami nitawafahamisha mwende mbali kupita Babeli.
44 Ile hema ya ushahidi ilikuwa pamoja na baba zetu jangwani, kama alivyoagiza yeye aliyesema na Musa, ya kwamba aifanye sawasawa na mfano ule aliouona;
45 ambayo baba zetu, kwa kupokezana, wakaiingiza pamoja na Yoshua katika milki ya Mataifa wale, ambao Mungu aliwafukuza mbele ya baba zetu, mpaka siku za Daudi;
46 aliyepata fadhili mbele za Mungu, naye aliomba ampatie Mungu wa Yakobo maskani.
47 Lakini Sulemani alimjengea nyumba.
48 Ila Yeye aliye juu hakai katika nyumba zilizofanywa kwa mikono, kama vile asemavyo nabii,
49 Mbingu ni kiti changu cha enzi, Na nchi ni pa kuwekea miguu yangu; Ni nyumba gani mtakayonijengea? Asema Bwana,
50 Au ni mahali gani nitakapostarehe? Si mkono wangu uliofanya haya yote?
51 Enyi wenye shingo gumu, msiotahiriwa mioyo wala masikio, siku zote mnampinga Roho Mtakatifu; kama baba zenu walivyofanya, na ninyi ni vivyo hivyo.
52 Ni yupi katika manabii ambaye baba zenu hawakumwudhi? Nao waliwaua wale waliotabiri habari za kuja kwake yule Mwenye Haki; ambaye ninyi sasa mmekuwa wasaliti wake, mkamwua;
53 ninyi mlioipokea torati kwa agizo la malaika msiishike.
54 Basi waliposikia maneno haya, wakachomwa mioyo, wakamsagia meno.
55 Lakini yeye akijaa Roho Mtakatifu, akakaza macho yake, akitazama mbinguni, akauona utukufu wa Mungu, na Yesu akisimama upande wa mkono wa kuume wa Mungu.
56 Akasema, Tazama! Naona mbingu zimefunguka, na Mwana wa Adamu amesimama mkono wa kuume wa Mungu.
57 Wakapiga kelele kwa sauti kuu, wakaziba masikio yao, wakamrukia kwa nia moja,
58 wakamtoa nje ya mji, wakampiga kwa mawe. Nao mashahidi wakaweka nguo zao miguuni pa kijana mmoja aliyeitwa Sauli.
59 Wakampiga kwa mawe Stefano, naye akiomba, akisema, Bwana Yesu, pokea roho yangu.
60 Akapiga magoti, akalia kwa sauti kuu, Bwana, usiwahesabie dhambi hii. Akiisha kusema haya akalala. Na Sauli alikuwa akiona vema kwa kuuawa kwake.

MATENDO 8


1 Siku ile kukatukia adha kuu ya kanisa lililokuwa katika Yerusalemu; wote wakatawanyika katika nchi ya Uyahudi na Samaria, isipokuwa hao mitume.
2 Watu watauwa wakamzika Stefano, wakamfanyia maombolezo makuu.
3 Sauli akaliharibu kanisa, akiingia kila nyumba, na kuwaburuta wanaume na wanawake na kuwatupa gerezani.
4 Lakini wale waliotawanyika wakaenda huko na huko wakilihubiri neno.
5 Filipo akatelemka akaingia mji wa Samaria, akawahubiri Kristo.
6 Na makutano kwa nia moja wakasikiliza maneno yale yaliyosemwa na Filipo walipoyasikia na kuziona ishara alizokuwa akizifanya.
7 Kwa maana pepo wachafu wakawatoka wengi waliopagawa nao, wakilia kwa sauti kuu; na watu wengi waliopooza, na viwete, wakaponywa.
8 Ikawa furaha kubwa katika mji ule.
9 Na mtu mmoja, jina lake Simoni, hapo kwanza alikuwa akifanya uchawi katika mji ule, akiwashangaza watu wa taifa la Wasamaria, akisema ya kuwa yeye ni mtu mkubwa.
10 Wote wakamsikiliza tangu mdogo hata mkubwa, wakisema, Mtu huyu ni uweza wa Mungu, ule Mkuu.
11 Wakamsikiliza, kwa maana amewashangaza muda mwingi kwa uchawi wake.
12 Lakini walipomwamini Filipo, akizihubiri habari njema za ufalme wa Mungu, na jina lake Yesu Kristo, wakabatizwa, wanaume na wanawake.
13 Na yeye Simoni mwenyewe aliamini akabatizwa, akashikamana na Filipo; akashangaa alipoziona ishara na miujiza mikubwa inayotendeka.
14 Na mitume waliokuwako Yerusalemu, waliposikia ya kwamba Samaria imelikubali neno la Mungu, wakawapelekea Petro na Yohana;
15 ambao waliposhuka, wakawaombea wampokee Roho Mtakatifu;
16 kwa maana bado hajawashukia hata mmoja wao, ila wamebatizwa tu kwa jina lake Bwana Yesu.
17 Ndipo wakaweka mikono yao juu yao, nao wakampokea Roho Mtakatifu.
18 Hata Simoni alipoona ya kuwa watu wanapewa Roho Mtakatifu kwa kuwekewa mikono ya mitume, akataka kuwapa fedha akisema,
19 Nipeni na mimi uwezo huu, ili kila mtu nitakayemweka mikono yangu, apokee Roho Mtakatifu.
20 Lakini Petro akamwambia, Fedha yako na ipotelee mbali pamoja nawe, kwa kuwa umedhania ya kuwa karama ya Mungu yapatikana kwa mali.
21 Huna fungu wala huna sehemu katika jambo hili, kwa kuwa moyo wako si mnyofu mbele za Mungu.
22 Basi, tubia uovu wako huu, ukamwombe Bwana, ili kama yamkini, usamehewe fikira hii ya moyo wako.
23 Kwa maana nakuona u katika uchungu kama nyongo, na tena u katika kifungo cha uovu.
24 Simoni akajibu, akasema, Niombeeni ninyi kwa Bwana, yasinifikilie mambo haya mliyosema hata moja.
25 Nao walipokwisha kushuhudia na kulihubiri neno la Bwana wakarudi Yerusalemu, wakaihubiri Injili katika vijiji vingi vya Wasamaria.
26 Malaika wa Bwana akasema na Filipo, akamwambia, Ondoka ukaende upande wa kusini hata njia ile itelemkayo kutoka Yerusalemu kwenda Gaza; nayo ni jangwa.
27 Naye akaondoka, akaenda; mara akamwona mtu wa Kushi, towashi, mwenye mamlaka chini ya Kandake malkia wa Kushi, aliyewekwa juu ya hazina yake yote; naye alikuwa amekwenda Yerusalemu kuabudu,
28 akawa akirejea, ameketi garini mwake akisoma chuo cha nabii Isaya.
29 Roho akamwambia Filipo, Sogea karibu na gari hili, ukashikamane nalo.
30 Basi Filipo akaenda mbio, akamsikia anasoma chuo cha nabii Isaya; akanena, Je! Yamekuelea haya unayosoma?
31 Akasema, Nitawezaje kuelewa, mtu asiponiongoza? Akamsihi Filipo apande na kuketi pamoja naye.
32 Na fungu la Maandiko alilokuwa akilisoma ni hili, Aliongozwa kwenda machinjoni kama kondoo, Na kama vile mwana-kondoo alivyo kimya mbele yake amkataye manyoya, Vivyo hivyo yeye naye hafunui kinywa chake.
33 Katika kujidhili kwake hukumu yake iliondolewa. Ni nani atakayeeleza kizazi chake? Kwa maana uzima wake umeondolewa katika nchi.
34 Yule towashi akamjibu Filipo, akasema, Nakuomba, nabii huyu; asema maneno haya kwa habari ya nani; ni habari zake mwenyewe au za mtu mwingine?
35 Filipo akafunua kinywa chake, naye, akianza kwa andiko lilo hilo, akamhubiri habari njema za Yesu.
36 Wakawa wakiendelea njiani, wakafika mahali penye maji; yule towashi akasema, Tazama, maji haya; ni nini kinachonizuia nisibatizwe?
37 Filipo akasema, Ukiamini kwa moyo wako wote, inawezekana. Akajibu, akanena, Naamini ya kwamba Yesu Kristo ndiye Mwana wa Mungu.]
38 Akaamuru lile gari lisimame; wakatelemka wote wawili majini, Filipo na yule towashi; naye akambatiza.
39 Kisha, walipopanda kutoka majini, Roho wa Bwana akamnyakua Filipo, yule towashi asimwone tena; basi alikwenda zake akifurahi.
40 Lakini Filipo akaonekana katika Azoto, na alipokuwa akipita akahubiri Injili katika miji yote, hata akafika Kaisaria.

MATENDO 9


1 Lakini Sauli, akizidi kutisha na kuwaza kuwaua wanafunzi wa Bwana, akamwendea Kuhani Mkuu,
2 akataka ampe barua za kuenda Dameski zilizoandikwa kwa masinagogi, ili akiona watu wa Njia hii, waume kwa wake, awafunge na kuwaleta Yerusalemu.
3 Hata alipokuwa akisafiri, ikawa anakaribia Dameski; ghafula ikamwangaza kote kote nuru kutoka mbinguni.
4 Akaanguka chini, akasikia sauti ikimwambia, Sauli, Sauli, mbona waniudhi?
5 Akasema, U nani wewe, Bwana? Naye akasema, Mimi ndimi Yesu unayeniudhi wewe.
6 Lakini simama, uingie mjini, nawe utaambiwa yakupasayo kutenda.
7 Na wale watu waliosafiri pamoja naye wakasimama kimya, wakiisikia sauti, wasione mtu.
8 Sauli akainuka katika nchi, na macho yake yalipofumbuka, hakuona kitu; wakamshika mkono wakamleta mpaka Dameski.
9 Akawa siku tatu haoni; hali, wala hanywi.
10 Basi palikuwapo Dameski mwanafunzi jina lake Anania. Bwana akamwambia katika maono, Anania. Akasema, Mimi hapa, Bwana.
11 Bwana akamwambia, Simama, enenda zako katika njia iitwayo Nyofu, ukaulize katika nyumba ya Yuda mtu aitwaye Sauli, wa Tarso; maana, angalia, anaomba;
12 naye amemwona mtu, jina lake Anania, akiingia, na kumwekea mikono juu yake, apate kuona tena.
13 Lakini Anania akajibu, Bwana, nimesikia habari za mtu huyu kwa watu wengi, mabaya mengi aliyowatenda watakatifu wako Yerusalemu;
14 hata hapa ana amri itokayo kwa wakuu wa makuhani awafunge wote wakuitiao Jina lako.
15 Lakini Bwana akamwambia, Nenda tu; kwa maana huyu ni chombo kiteule kwangu, alichukue Jina langu mbele ya Mataifa, na wafalme, na wana wa Israeli.
16 Maana nitamwonyesha yalivyo mengi yatakayompasa kuteswa kwa ajili ya Jina langu.
17 Anania akaenda zake, akaingia mle nyumbani; akamwekea mikono akisema, Ndugu Sauli, Bwana amenituma, Yesu, yeye aliyekutokea katika njia uliyoijia, upate kuona tena, ukajazwe Roho Mtakatifu.
18 Mara vikaanguka machoni pake vitu kama magamba, akapata kuona, akasimama, akabatizwa;
19 akala chakula, na kupata nguvu. Akawa huko siku kadha wa kadha pamoja na wanafunzi walioko Dameski.
20 Mara akamhubiri Yesu katika masinagogi, kwamba yeye ni Mwana wa Mungu.
21 Na wote waliosikia wakashangaa, wakasema, Siye huyu aliyewaharibu walioliitia Jina hili huko Yerusalemu? Na hapa alikuwa amekuja kwa kusudi hilo, awafunge na kuwapeleka kwa wakuu wa makuhani?
22 Sauli akazidi kuwa hodari, akawatia fadhaa Wayahudi waliokaa Dameski, akithibitisha ya kuwa huyu ndiye Kristo.
23 Hata siku nyingi zilipopita, Wayahudi wakafanya shauri ili wamwue;
24 lakini hila yao ikajulikana na Sauli. Wakamvizia malangoni mchana na usiku wapate kumwua.
25 Wanafunzi wake wakamtwaa usiku wakamshusha ukutani, wakimtelemsha katika kapu.
26 Na Sauli alipofika Yerusalemu, alijaribu kujiunga na wanafunzi, nao walikuwa wakimwogopa wote, wasisadiki ya kuwa yeye ni mwanafunzi.
27 Lakini Barnaba akamtwaa, akampeleka kwa mitume, akawaeleza jinsi alivyomwona Bwana njiani, na ya kwamba alisema naye, na jinsi alivyohubiri kwa ushujaa katika Dameski kwa jina la Yesu.
28 Naye akawa pamoja nao katika Yerusalemu akiingia na kutoka.
29 Akahubiri kwa jina la Bwana kwa ushujaa, akinena na kuhojiana na Wayahudi wa Kiyunani. Nao wakajaribu kumwua.
30 Lakini ndugu walipopata habari wakamchukua mpaka Kaisaria, wakampeleka aende Tarso.
31 Basi kanisa likapata raha katika Uyahudi wote na Galilaya na Samaria, likajengwa, likiendelea na kuongezeka katika kicho cha Bwana, na faraja ya Roho Mtakatifu.
32 Hata Petro alipokuwa akizunguka-zunguka pande zote akawatelemkia na watakatifu waliokaa Lida.
33 Akamwona mtu mmoja huko, jina lake Ainea, mtu huyo amelala kitandani miaka minane; maana alikuwa amepooza.
34 Petro akamwambia, Ainea, Yesu Kristo akuponya; ondoka, ujitandikie. Mara akaondoka.
35 Na watu wote waliokaa Lida na Sharoni wakamwona, wakamgeukia Bwana.
36 Na mwanafunzi mmoja alikuwako Yafa, jina lake Tabitha, tafsiri yake ni Dorkasi (yaani paa); mwanamke huyu alikuwa amejaa matendo mema na sadaka alizozitoa.
37 Ikawa siku zile akaugua, akafa; hata walipokwisha kumwosha, wakamweka orofani.
38 Na kwa kuwa mji wa Lida ulikuwa karibu na Yafa, nao wanafunzi wamesikia ya kwamba Petro yuko huko, wakatuma watu wawili kwake, kumsihi na kusema, Usikawie kuja kwetu.
39 Petro akaondoka akafuatana nao. Alipofika, wakampeleka juu orofani wajane wote wakasimama karibu naye, wakilia na kumwonyesha zile kanzu na nguo alizozishona Dorkasi wakati ule alipokuwa pamoja nao.
40 Petro akawatoa nje wote, akapiga magoti, akaomba, kisha akaelekea yule maiti, akanena, Tabitha, ondoka. Naye akafumbua macho yake, na alipomwona Petro akajiinua, akaketi.
41 Akampa mkono, akamwinua; hata akiisha kuwaita wale watakatifu na wajane akamweka mbele yao, hali yu hai.
42 Ikajulikana katika mji mzima wa Yafa; watu wengi wakamwamini Bwana.
43 Basi Petro akakaa siku kadha wa kadha huko Yafa, nyumbani mwa mtu mmoja, jina lake Simoni, mtengenezaji wa ngozi.

MATENDO 10


1 Palikuwa na mtu Kaisaria, jina lake Kornelio, akida wa kikosi kilichoitwa Kiitalia,
2 mtu mtauwa, mchaji wa Mungu, yeye na nyumba yake yote, naye alikuwa akiwapa watu sadaka nyingi, na kumwomba Mungu daima.
3 Akaona katika maono waziwazi, kama saa tisa ya mchana, malaika wa Mungu, akimjia na kumwambia, Kornelio!
4 Akamtazama sana, akaogopa akasema, Kuna nini, Bwana? Akamwambia, Sala zako na sadaka zako zimefika juu na kuwa ukumbusho mbele za Mungu.
5 Sasa basi, peleka watu Yafa, ukamwite Simoni, aitwaye Petro.
6 Yeye ni mgeni wa mtu mmoja, jina lake Simoni, mtengenezaji wa ngozi, ambaye nyumba yake iko pwani, atakuambia yakupasayo kutenda.
7 Na yule malaika aliyesema naye akiisha kuondoka, Kornelio akawaita wawili katika watumishi wake wa nyumbani, na askari mmoja, mtu mtauwa katika wale waliomhudumia daima;
8 na alipokwisha kuwaeleza mambo yote akawatuma kwenda Yafa.
9 Hata siku ya pili, walipokuwa wakisafiri na kuukaribia mji, Petro alipanda juu darini, kwenda kuomba, yapata saa sita ya mchana;
10 akaumwa na njaa sana, akataka kula; lakini walipokuwa wakiandaa, roho yake ikazimia,
11 akaona mbingu zimefunuka, na chombo kikishuka kama nguo kubwa, inatelemshwa kwa pembe zake nne hata nchi;
12 ambayo ndani yake walikuwamo aina zote za wanyama wenye miguu minne, na hao watambaao, na ndege wa angani.
13 Kisha sauti ikamjia, kusema, Ondoka, Petro, uchinje ule.
14 Lakini Petro akasema, Hasha, Bwana, kwa maana sijakula kamwe kitu kilicho kichafu au najisi.
15 Sauti ikamjia mara ya pili, ikimwambia, Vilivyotakaswa na Mungu, usiviite wewe najisi.
16 Jambo hili likatendeka mara tatu; kisha kile chombo kikapokewa tena mbinguni.
17 Hata Petro alipokuwa akiona shaka ndani ya nafsi yake, maana yake ni nini maono hayo aliyoyaona, wale watu waliotumwa na Kornelio, wakiisha kuiulizia nyumba ya Simoni, wakasimama mbele ya mlango,
18 wakaita; wakauliza kwamba Simoni aitwaye Petro anakaa humo.
19 Na Petro alikuwa akiyafikiri yale maono. Roho akamwambia, Wako watu watatu wanakutafuta.
20 Basi ondoka ushuke ufuatane nao, usione tashwishi, kwa maana ni mimi niliyewatuma.
21 Petro akawashukia wale watu, akanena, Mimi ndiye mnayemtafuta. Mmekuja kwa sababu gani?
22 Wakasema, Kornelio akida, mtu mwenye haki, mchaji wa Mungu, aliye na sifa njema kwa taifa lote la Wayahudi, alionywa na malaika mtakatifu kutuma watu kwako, uende nyumbani kwake, apate kusikiliza maneno kwako.
23 Akawakaribisha wawe wageni wake. Hata siku ya pili, Petro akaondoka akatoka pamoja nao, na baadhi ya ndugu waliokaa Yafa wakafuatana naye.
24 Siku ya pili yake wakaingia Kaisaria. Na Kornelio alikuwa akiwangojea, hali amekusanya jamaa zake na rafiki zake.
25 Petro alipokuwa akiingia Kornelio akatoka amlaki akamwangukia miguu, akamsujudia.
26 Lakini Petro akamwinua, akasema, Simama, mimi nami ni mwanadamu.
27 Na katika kusema naye akaingia ndani, akaona watu wengi wamekusanyika.
28 Akawaambia, Ninyi mnajua ya kuwa si halali mtu aliye Myahudi ashikamane na mtu aliye wa taifa lingine wala kumwendea, lakini Mungu amenionya, nisimwite mtu awaye yote mchafu wala najisi.
29 Kwa sababu hiyo nalikuja nilipoitwa, nisikatae; basi nawauliza, ni neno gani mliloniitia?
30 Kornelio akasema, Siku tatu zilizopita, katika saa ii hii, yaani saa tisa, nilikuwa nikisali nyumbani mwangu; nikamwona mtu amesimama mbele yangu, mwenye nguo zing'arazo,
31 akasema, Kornelio, kuomba kwako kumesikiwa, na sadaka zako zinakumbukwa mbele za Mungu.
32 Basi, tuma watu kwenda Yafa, ukamwite Simoni aitwaye Petro, anakaa katika nyumba ya Simoni, mtengenezaji wa ngozi, karibu na pwani; naye akija atasema nawe.
33 Mara nikatuma watu kwako, nawe umefanya vyema kuja. Basi sasa sisi sote tupo hapa mbele za Mungu, tupate kuyasikiliza maneno yote uliyoamriwa na Bwana.
34 Petro akafumbua kinywa chake, akasema, Hakika natambua ya kuwa Mungu hana upendeleo;
35 bali katika kila taifa mtu amchaye na kutenda haki hukubaliwa na yeye.
36 Neno lile alilowapelekea wana wa Israeli akihubiri habari njema ya amani kwa Yesu Kristo (ndiye Bwana wa wote),
37 jambo lile ninyi mmelijua, lililoenea katika Uyahudi wote likianzia Galilaya, baada ya ubatizo aliouhubiri Yohana;
38 habari za Yesu wa Nazareti, jinsi Mungu alivyomtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu naye akazunguka huko na huko, akitenda kazi njema na kuponya wote walioonewa na Ibilisi; kwa maana Mungu alikuwa pamoja naye.
39 Nasi tu mashahidi wa mambo yote aliyoyatenda katika nchi ya Wayahudi na katika Yerusalemu; ambaye walimwua wakamtundika mtini.
40 Huyo Mungu alimfufua siku ya tatu, akamjalia kudhihirika,
41 si kwa watu wote, bali kwa mashahidi waliokuwa wamekwisha kuchaguliwa na Mungu, ndio sisi, tuliokula na kunywa pamoja naye baada ya kufufuka kwake kutoka kwa wafu.
42 Akatuagiza tuwahubiri watu na kushuhudia ya kuwa huyu ndiye aliyeamriwa na Mungu awe Mhukumu wa walio hai na wafu.
43 Huyo manabii wote humshuhudia, ya kwamba kwa jina lake kila amwaminiye atapata ondoleo la dhambi.
44 Petro alipokuwa akisema maneno hayo Roho Mtakatifu akawashukia wote waliolisikia lile neno.
45 Na wale waliotahiriwa, walioamini, wakashangaa, watu wote waliokuja pamoja na Petro, kwa sababu Mataifa nao wamemwagiwa kipawa cha Roho Mtakatifu.
46 Kwa maana waliwasikia wakisema kwa lugha, na kumwadhimisha Mungu. Ndipo Petro akajibu,
47 Ni nani awezaye kuzuia maji, hawa wasibatizwe, watu waliopokea Roho Mtakatifu vile vile kama sisi?
48 Akaamuru wabatizwe kwa Jina lake Yesu Kristo. Ndipo wakamsihi azidi kukaa siku kadha wa kadha.

MATENDO 11


1 Basi mitume na ndugu waliokuwako katika Uyahudi wakapata habari ya kwamba watu wa Mataifa nao wamelipokea neno la Mungu.
2 Na Petro alipopanda kwenda Yerusalemu, wale walio wa tohara wakashindana naye,
3 wakisema, Uliingia kwa watu wasiotahiriwa ukala nao.
4 Petro akaanza kuwaeleza kwa taratibu, akasema,
5 Nalikuwa katika mji wa Yafa, nikiomba, roho yangu ikazimia, nikaona maono; chombo kinashuka, kama nguo kubwa inatelemshwa kutoka mbinguni kwa pembe zake nne, kikanifikilia.
6 Nikakitazama sana, nikifikiri, nikaona wanyama wa nchi wenye miguu minne, na wanyama wa mwituni, nao watambaao, na ndege wa angani.
7 Nikasikia na sauti ikiniambia, Ondoka, Petro, ukachinje ule.
8 Nikasema, Hasha, Bwana, kwa maana kitu kilicho kichafu au kilicho najisi hakijaingia kabisa kinywani mwangu.
9 Sauti ikanijibu mara ya pili kutoka mbinguni, Alivyovitakasa Mungu, usivinene wewe najisi.
10 Jambo hili likatendeka mara tatu, kisha vitu vyote vikavutwa tena juu mbinguni.
11 Na tazama, mara hiyo watu watatu wakasimama mbele ya nyumba tuliyokuwamo, waliotumwa kwangu kutoka Kaisaria.
12 Roho akaniambia nifuatane nao, nisione tashwishi. Ndugu hawa sita nao wakaenda pamoja nami, tukaingia katika nyumba ya mtu yule;
13 akatueleza jinsi alivyomwona malaika aliyesimama nyumbani mwake na kumwambia, Tuma watu kwenda Yafa ukamwite Simoni aitwaye Petro,
14 atakayekuambia maneno ambayo yatakuokoa, wewe na nyumba yako yote.
15 Ikawa nilipoanza kunena, Roho Mtakatifu akawashukia kama alivyotushukia sisi mwanzo.
16 Nikalikumbuka neno lile la Bwana, jinsi alivyosema, Yohana alibatiza kwa maji kweli, bali ninyi mtabatizwa kwa Roho Mtakatifu.
17 Basi ikiwa Mwenyezi Mungu amewapa wao karama ile ile aliyotupa sisi tuliomwamini Bwana Yesu Kristo, mimi ni nani niweze kumpinga Mungu?
18 Waliposikia maneno haya wakanyamaza, wakamtukuza Mungu, wakisema, Basi, Mungu amewajalia hata mataifa nao toba liletalo uzima.
19 Basi wale waliotawanyika kwa sababu ya ile dhiki iliyotukia kwa habari ya Stefano, wakasafiri hata Foinike na Kipro na Antiokia, wasilihubiri lile neno ila kwa Wayahudi peke yao.
20 Lakini baadhi ya hao walikuwa watu wa Kipro na Kirene, nao walipofika Antiokia wakasema na Wayahudi wa Kiyunani, wakihubiri habari njema za Bwana Yesu.
21 Mkono wa Bwana ukawa pamoja nao, watu wengi wakaamini, wakamwelekea Bwana.
22 Habari hizo za watu hao zikafika masikioni mwa kanisa lililokuwako katika Yerusalemu; wakamtuma Barnaba, aende hata Antiokia.
23 Naye, alipokwisha kufika na kuiona neema ya Mungu akafurahi, akawasihi wote waambatane na Bwana kwa kusudi la moyo.
24 Maana alikuwa mtu mwema amejaa Roho Mtakatifu na imani; watu wengi wakaongezeka upande wa Bwana.
25 Kisha akatoka akaenda Tarso kumtafuta Sauli;
26 hata alipokwisha kumwona akamleta Antiokia. Ikawa kwa muda wa mwaka mzima wakakusanyika pamoja na kanisa na kuwafundisha watu wengi. Na wanafunzi waliitwa Wakristo kwanza hapo Antiokia.
27 Siku zizo hizo manabii walitelemka kutoka Yerusalemu hata Antiokia.
28 Na tulipokusanyika akasimama mmoja wao, jina lake Agabo, akaonyesha kwa uweza wa Roho Mtakatifu kwamba njaa kubwa itakuja karibu katika dunia nzima, nayo ikatukia katika siku za Klaudio.
29 Na wale wanafunzi, kila mtu kwa kadiri ya alivyofanikiwa, wakaazimu kupeleka msaada kwa ndugu zao waliokaa Uyahudi.
30 Wakafanya hivyo, wakawapelekea wazee kwa mikono ya Barnaba na Sauli.

MATENDO 12


1 Panapo majira yale yale Herode mfalme akanyosha mikono yake kuwatenda mabaya baadhi ya watu wa kanisa.
2 Akamwua Yakobo, ndugu yake Yohana, kwa upanga.
3 Na akiona ya kuwa imewapendeza Wayahudi akaendelea akamshika na Petro. Siku hizo zilikuwa siku za mikate isiyochachwa.
4 Alipokwisha kumkamata, akamweka gerezani akamtia mikononi mwa vikosi vinne vya askari wanne wanne, wamlinde, akitaka baada ya Pasaka kumtoa na kumweka mbele ya watu.
5 Basi Petro akalindwa gerezani, nalo kanisa likamwomba Mungu kwa juhudi kwa ajili yake.
6 Hata wakati Herode alipotaka kumtoa, usiku ule ule Petro alikuwa analala katikati ya askari wawili, amefungwa minyororo miwili; walinzi mbele ya mlango wakailinda gereza.
7 Mara malaika wa Bwana akasimama karibu naye, nuru ikamulika mle chumbani, akampiga Petro ubavuni, akamwamsha, akisema, Ondoka upesi. Minyororo yake ikamwanguka mikononi.
8 Malaika akamwambia, Jifunge, kavae viatu vyako. Akafanya hivyo. Kisha akamwambia, Jivike nguo yako, ukanifuate.
9 Akatoka nje, akamfuata; wala hakujua ya kuwa ni kweli yaliyofanywa na malaika; bali alidhani kwamba anaona maono.
10 Na walipopita lindo la kwanza na la pili, wakaja hata mlango wa chuma wa kuingilia mjini, ukawafungukia wenyewe. Wakatoka nje, wakapita katika njia moja; mara malaika akamwacha.
11 Hata Petro alipopata fahamu akasema, Sasa nimejua yakini ya kuwa Bwana amempeleka malaika wake na kunitoa katika mkono wa Herode na katika kutazamia kote kwa taifa la Wayahudi.
12 Na alipokuwa akifikiri haya akafika nyumbani kwa Mariamu, mamaye Yohana, ambaye jina lake la pili ni Marko; na watu wengi walikuwa wamekutana humo wakiomba.
13 Naye alipobisha kilango cha lango, kijakazi, jina lake Roda, akaja kusikiliza.
14 Alipoitambua sauti ya Petro, hakukifungua lango, kwa ajili ya furaha, bali alipiga mbio, akaingia ndani akawaambia kwamba Petro anasimama mbele ya lango.
15 Wakamwambia, Una wazimu. Lakini yeye akakaza sana, akasema ya kwamba ndivyo hivyo. Wakanena, Ni malaika wake.
16 Petro akafuliza kugonga, hata walipokwisha kumfungulia wakamwona, wakastaajabu.
17 Naye akawapungia mkono wanyamaze, akawaeleza jinsi Bwana alivyomtoa katika gereza. Akasema, Kampasheni Yakobo na wale ndugu habari hizi. Akaondoka, akaenda mahali pengine.
18 Hata kulipopambauka askari wakaingiwa na fadhaa nyingi, amekuwaje Petro.
19 Na Herode alipomtafuta, asimwone, aliwauliza-uliza wale walinzi, akaamuru wauawe. Kisha akatelemkia kutoka Uyahudi kwenda Kaisaria, akakaa huko.
20 Naye Herode alikuwa amewakasirikia sana watu wa Tiro na Sidoni; wakamwendea kwa nia moja, na wakiisha kufanya urafiki na Blasto, mwenye kukitunza chumba cha mfalme cha kulalia, wakataka amani; kwa maana nchi yao ilipata riziki kwa nchi ya mfalme.
21 Basi siku moja iliyoazimiwa, Herode akajivika mavazi ya kifalme, akaketi katika kiti cha enzi, akatoa hotuba mbele yao.
22 Watu wakapiga kelele, wakisema, Ni sauti ya Mungu, si sauti ya mwanadamu.
23 Mara malaika wa Bwana akampiga, kwa sababu hakumpa Mungu utukufu; akaliwa na chango, akatokwa na roho.
24 Neno la Bwana likazidi na kuenea.
25 Na Barnaba na Sauli, walipokwisha kutimiza huduma yao, wakarejea kutoka Yerusalemu, wakamchukua pamoja nao Yohana aitwaye Marko.

MATENDO 13


1 Na huko Antiokia katika kanisa lililokuwako palikuwa na manabii na waalimu, nao ni Barnaba, na Simeoni aitwaye Nigeri, na Lukio Mkirene, na Manaeni aliyekuwa ndugu wa kunyonya wa mfalme Herode, na Sauli.
2 Basi hawa walipokuwa wakimfanyia Bwana ibada na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia.
3 Ndipo wakiisha kufunga na kuomba, wakaweka mikono yao juu yao, wakawaacha waende zao.
4 Basi watu hao, wakiisha kupelekwa na Roho Mtakatifu wakatelemkia Seleukia, na kutoka huko wakasafiri baharini hata Kipro.
5 Na walipokuwa katika Salami wakalihubiri neno la Mungu katika masinagogi ya Wayahudi, nao walikuwa naye Yohana kuwa mtumishi wao.
6 Walipokwisha kupita katikati ya kisiwa chote mpaka Pafo, wakaona mtu mmoja, mchawi, nabii wa uongo, Myahudi jina lake Bar-Yesu;
7 mtu huyu alikuwa pamoja na liwali Sergio Paulo, mtu mwenye akili. Yeye liwali akawaita Barnaba na Sauli waje kwake, akataka kulisikia neno la Mungu.
8 Lakini Elima, yule mchawi (maana ndiyo tafsiri ya jina lake), akashindana nao, akitaka kumtia yule liwali moyo wa kuiacha ile imani.
9 Lakini Sauli, ambaye ndiye Paulo, akijaa Roho Mtakatifu, akamkazia macho,
10 akasema, Ewe mwenye kujaa hila na uovu wote, mwana wa Ibilisi, adui wa haki yote, huachi kuzipotoa njia za Bwana zilizonyoka?
11 Basi, angalia, mkono wa Bwana u juu yako, nawe utakuwa kipofu, usilione jua kwa muda. Mara kiwi kikamwangukia na giza, akazunguka-zunguka na kumtafuta mtu wa kumshika mkono na kumwongoza.
12 Ndipo yule liwali, alipoyaona yaliyotendeka, akaamini, akiyastaajabia mafundisho ya Bwana.
13 Kisha Paulo na wenziwe wakang'oa nanga wakasafiri kutoka Pafo, wakafika Perge katika Pamfilia. Yohana akawaacha akarejea Yerusalemu.
14 Lakini wao wakatoka Perge, wakapita kati ya nchi, wakafika Antiokia, mji wa Pisidia, wakaingia katika sinagogi siku ya sabato, wakaketi.
15 Kisha, baada ya kusomwa torati na chuo cha manabii, wakuu wa sinagogi wakatuma mtu kwao, na kuwaambia, Ndugu, kama mkiwa na neno la kuwafaa watu hawa, lisemeni.
16 Paulo akasimama, akawapungia mkono, akasema, Enyi waume wa Israeli, nanyi mnaomcha Mungu, sikilizeni.
17 Mungu wa watu hawa Israeli aliwachagua baba zetu, akawatukuza watu hao, walipokuwa wakikaa kama wageni katika nchi ya Misri, na kwa mkono ulioinuliwa akawatoa, akawaongoza.
18 Na kwa muda wa miaka kama arobaini akawavumilia katika jangwa.
19 Na alipokwisha kuwaharibu mataifa saba katika nchi ya Kanaani akawapa nchi yao iwe urithi kwa muda wa miaka kama mia nne na hamsini;
20 baada ya hayo akawapa waamuzi hata zamani za nabii Samweli.
21 Hatimaye wakaomba kupewa mfalme; Mungu akawapa Sauli mwana wa Kishi, mtu wa kabila ya Benyamini, kwa muda wa miaka arobaini.
22 Na alipokwisha kumwondoa huyo, akamwinua Daudi awe mfalme wao ambaye alimshuhudia, akisema, Nimemwona Daudi, mwana wa Yese, mtu anayeupendeza moyo wangu, atakayefanya mapenzi yangu yote.
23 Katika uzao wake mtu huyo Mungu amewaletea Israeli Mwokozi, yaani, Yesu, kama alivyoahidi;
24 Yohana alipokuwa amekwisha kuwahubiri watu wote wa Israeli habari za ubatizo wa toba, kabla ya kuja kwake.
25 Naye Yohana alipokuwa akimaliza mwendo wake alinena, Mwanidhani mimi kuwa nani? Mimi siye. Lakini, angalieni, anakuja mmoja nyuma yangu ambaye mimi sistahili kumlegezea viatu vya miguu yake.
26 Ndugu zangu, wana wa ukoo wa Ibrahimu, na hao miongoni mwenu wanaomcha Mungu, kwetu sisi neno la wokovu huu limepelekwa.
27 Kwa maana wakaao Yerusalemu, na wakuu wao, kwa kuwa hawakumjua yeye, wala maneno ya manabii yanayosomwa kila sabato, wameyatimiza kwa kumhukumu.
28 Na ijapokuwa hawakuona sababu ya kumfisha wakamwomba Pilato auawe.
29 Hata walipokwisha kumaliza yote aliyoandikiwa, wakamtelemsha katika ule mti, wakamweka kaburini.
30 Lakini Mungu akamfufua katika wafu;
31 akaonekana siku nyingi na wale waliopanda naye kutoka Galilaya hata Yerusalemu, ambao sasa ndio walio mashahidi wake mbele ya watu.
32 Na sisi tunawahubiri habari njema ya ahadi ile waliyopewa mababa,
33 ya kwamba Mungu amewatimizia watoto wetu ahadi hiyo, kwa kumfufua Yesu; kama ilivyoandikwa katika Zaburi ya pili, Wewe ndiwe Mwanangu, mimi leo nimekuzaa.
34 Tena ya kuwa alimfufua katika wafu, asipate kurudia uharibifu, amenena hivi, Nitawapa ninyi mambo matakatifu ya Daudi yaliyo amini.
35 Kwa hiyo anena na pengine, Hutamwachia Mtakatifu wako kuona uharibifu,
36 Kwa maana Daudi, akiisha kulitumikia shauri la Mungu katika kizazi chake, alilala, akawekwa pamoja na baba zake, akaona uharibifu.
37 Bali huyu aliyefufuliwa na Mungu hakuona uharibifu.
38 Basi, na ijulikane kwenu, ndugu zangu, ya kuwa kwa huyo mnahubiriwa msamaha wa dhambi;
39 na kwa yeye kila amwaminiye huhesabiwa haki katika mambo yale yote asiyoweza kuhesabiwa haki kwa torati ya Musa.
40 Angalieni, basi, isiwajilie habari ile iliyonenwa katika manabii.
41 Tazameni, enyi mnaodharau, kastaajabuni, mkatoweke; kwa kuwa natenda kazi mimi siku zenu, kazi ambayo msingeisadiki kabisa, ijapo mtu akiwasimulia sana.
42 Na walipokuwa wakitoka, wakawasihi waambiwe maneno haya sabato ya pili.
43 Sinagogi ilipofumukana, Wayahudi na waongofu watauwa wengi wakashikamana na Paulo na Barnaba; ambao, wakisema nao, wakawatia moyo kudumu katika neema ya Mungu.
44 Hata sabato ya pili, watu wengi, karibu mji wote, wakakusanyika walisikie neno la Mungu.
45 Bali Wayahudi, walipowaona makutano, wakajaa wivu, wakayakanusha maneno yaliyonenwa na Paulo, wakibisha na kutukana.
46 Paulo na Barnaba wakanena kwa ushujaa wakasema, Ilikuwa lazima neno la Mungu linenwe kwenu kwanza; lakini kwa kuwa mnalisukumia mbali, na kujiona nafsi zenu kuwa hamkustahili uzima wa milele, angalieni, twawageukia Mataifa.
47 Kwa sababu ndivyo tulivyoamriwa na Bwana, Nimekuweka uwe nuru ya Mataifa, Upate kuwa wokovu hata mwisho wa dunia.
48 Mataifa waliposikia hayo wakafurahi, wakalitukuza neno la Bwana, nao waliokuwa wamekusudiwa uzima wa milele wakaamini.
49 Neno la Bwana likaenea katika nchi ile yote.
50 Lakini Wayahudi wakawafitinisha wanawake watauwa wenye cheo na wakuu wa mji, wakawataharakisha watu wawaudhi Paulo na Barnaba; wakawatoa katika mipaka yao.
51 Nao wakawakung'utia mavumbi ya miguu yao, wakaenda Ikonio.
52 Na wanafunzi walijaa furaha na Roho Mtakatifu.

MATENDO 14


1 Ikawa huko Ikonio wakaingia pamoja katika sinagogi la Wayahudi; na kwa vile walivyonena, kundi kubwa la Wayahudi na la Wayunani wakaamini.
2 Walakini Wayahudi wasioamini wakawataharakisha watu wa Mataifa na kuwatia nia mbaya juu ya ndugu.
3 Basi wakakaa huko wakati mwingi, wakinena kwa ushujaa katika Bwana, aliyelishuhudia neno la neema yake, akiwajalia ishara na maajabu yatendeke kwa mikono yao.
4 Lakini jamii ya watu wa mjini wakafarakana; hawa walikuwa upande wa Wayahudi, na hawa upande wa Mitume.
5 Hata palipotokea shambulio la watu wa Mataifa na Wayahudi pamoja na wakubwa wao juu yao, kuwatenda jeuri na kuwapiga kwa mawe,
6 wao wakapata habari wakakimbilia Listra na Derbe, miji ya Likaonia, na nchi zilizo kando kando;
7 wakakaa huko, wakiihubiri Injili.
8 Na huko Listra palikuwa na mtu mmoja, dhaifu wa miguu, kiwete tangu tumboni mwa mamaye, ambaye hajaenda kabisa.
9 Mtu huyo alimsikia Paulo alipokuwa akinena; ambaye akamkazia macho na kuona ya kuwa ana imani ya kuponywa,
10 akasema kwa sauti kuu, Simama kwa miguu yako sawasawa. Akasimama upesi akaenda.
11 Na makutano walipoona aliyoyafanya Paulo wakapaza sauti zao, wakisema kwa Kilikaonia, Miungu wametushukia kwa mifano ya wanadamu.
12 Wakamwita Barnaba, Zeu, na Paulo, Herme, kwa sababu ndiye aliyekuwa mnenaji.
13 Kuhani wa Zeu ambaye hekalu lake lilikuwa mbele ya mji, akaleta ng'ombe na taji za maua hata malangoni, akitaka kutoa dhabihu pamoja na makutano.
14 Walakini mitume Barnaba na Paulo, walipopata habari, wakararua nguo zao, wakaenda mbio wakaingia katika makutano, wakipiga kelele,
15 wakisema, Akina bwana, mbona mnafanya haya? Sisi nasi tu wanadamu hali moja na ninyi; twawahubiri habari njema, ili mgeuke na kuyaacha mambo haya ya ubatili na kumwelekea Mungu aliye hai, aliyeumba mbingu na nchi na bahari na vitu vyote vilivyomo;
16 ambaye zamani zilizopita aliwaacha mataifa yote waende katika njia zao wenyewe.
17 Lakini hakujiacha pasipo ushuhuda, kwa kuwa alitenda mema, akiwapeni mvua kutoka mbinguni, na nyakati za mavuno, akiwashibisha mioyo yenu chakula na furaha.
18 Na kwa maneno hayo wakawazuia makutano kwa shida, wasiwatolee dhabihu.
19 Lakini Wayahudi wakafika toka Antiokia na Ikonio, wakawashawishi makutano hata wakampiga kwa mawe Paulo, wakamburuta nje ya mji, wakidhania ya kuwa amekwisha kufa.
20 Lakini wanafunzi walipokuwa wakimzunguka pande zote, akasimama, akaingia ndani ya mji; na siku ya pili yake akatoka, akaenda zake pamoja na Barnaba mpaka Derbe.
21 Hata walipokwisha kuihubiri Injili katika mji ule, na kupata wanafunzi wengi, wakarejea mpaka Listra na Ikonio na Antiokia,
22 wakifanya imara roho za wanafunzi na kuwaonya wakae katika ile Imani, na ya kwamba imetupasa kuingia katika ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi.
23 Na walipokwisha kuwachagulia wazee katika kila kanisa, na kuomba pamoja na kufunga, wakawaweka katika mikono ya Bwana waliyemwamini.
24 Wakapita kati ya Pisidia wakaingia Pamfilia.
25 Na baada ya kuhubiri lile neno katika Perge wakatelemka mpaka Atalia.
26 Na kutoka huko wakaabiri kwenda Antiokia. Huko ndiko walikoombewa neema ya Mungu kwa ile kazi waliyokwisha kuitimiza.
27 Hata walipofika wakalikutanisha kanisa, wakawaeleza mambo yote aliyoyafanya Mungu pamoja nao, na ya kwamba amewafungulia Mataifa mlango wa imani.
28 Wakaketi huko wakati usiokuwa mchache, pamoja na wanafunzi.

MATENDO 15


1 Wakashuka watu waliotoka Uyahudi wakawafundisha wale ndugu ya kwamba, Msipotahiriwa kama desturi ya Musa hamwezi kuokoka.
2 Basi baada ya Paulo na Barnaba kushindana na watu hawa na kuhojiana nao sana, ndugu wakaamuru kwamba Paulo na Barnaba na wengine miongoni mwao wapande kwenda Yerusalemu kwa mitume na wazee kwa habari ya swali hilo.
3 Basi, wakisafirishwa na kanisa, wakapita kati ya nchi ya Foinike na Samaria, wakitangaza habari za kuongoka kwao Mataifa; wakawafurahisha ndugu sana.
4 Walipofika Yerusalemu wakakaribishwa na kanisa na mitume na wazee, nao wakawaeleza mambo yote Mungu aliyoyafanya pamoja nao.
5 Lakini baadhi ya madhehebu ya Mafarisayo walioamini wakasimama wakisema, Ni lazima kuwatahiri na kuwaagiza kuishika torati ya Musa.
6 Mitume na wazee wakakusanyika wapate kulifikiri neno hilo.
7 Na baada ya hoja nyingi Petro akasimama, akawaambia, Ndugu zangu, ninyi mnajua ya kuwa tangu siku za kwanza Mungu alichagua miongoni mwenu ya kwamba Mataifa walisikie neno la Injili kwa kinywa changu, na kuliamini.
8 Na Mungu, ajuaye mioyo ya watu, akawashuhudia, akiwapa Roho Mtakatifu vile vile kama alivyotupa sisi;
9 wala hakufanya tofauti kati yetu sisi na wao, akiwasafisha mioyo yao kwa imani.
10 Basi sasa mbona mnamjaribu Mungu na kuweka kongwa juu ya shingo za wanafunzi, ambalo baba zetu wala sisi hatukuweza kulichukua.
11 Bali twaamini kwamba tutaokoka kwa neema ya Bwana Yesu vile vile kama wao.
12 Basi mkutano wote wakanyamaza, wakawasikiliza Barnaba na Paulo wakiwapasha habari za ishara na maajabu, ambayo Mungu aliyafanya kwa ujumbe wao katika Mataifa.
13 Na hao walipokwisha kunyamaza Yakobo akajibu, akisema, Ndugu zangu, nisikilizeni.
14 Simeoni ametueleza jinsi Mungu hapo kwanza alivyowaangalia Mataifa ili achague watu katika hao kwa ajili ya jina lake.
15 Na maneno ya manabii yapatana na hayo, kama ilivyoandikwa,
16 Baada ya mambo haya nitarejea, Nami nitaijenga tena nyumba ya Daudi iliyoanguka. Nitajenga tena maanguko yake, Nami nitaisimamisha;
17 Ili wanadamu waliosalia wamtafute Bwana, Na mataifa yote ambao jina langu limetajwa kwao;
18 Asema Bwana, ajulishaye hayo tangu milele.
19 Kwa sababu hiyo mimi naamua hivi; Tusiwataabishe wale waliomgeukia Mungu katika Mataifa;
20 bali tuwaandikie kwamba wajiepushe na unajisi wa sanamu, na uasherati, na nyama zilizosongolewa, na damu.
21 Kwa maana tangu zamani za kale Musa anao watu wahubirio mambo yake; katika kila mji husomwa kila sabato katika masinagogi.
22 Basi ikawapendeza mitume na wazee na kanisa lote kuwachagua watu miongoni mwao na kuwapeleka Antiokia pamoja na Paulo na Barnaba; nao ni hawa, Yuda aliyeitwa Barsaba, na Sila, waliokuwa watu wakuu katika ndugu. Wakaandika hivi na kupeleka kwa mikono yao,
23 Mitume na ndugu wazee, kwa ndugu zetu walioko Antiokia na Shamu na Kilikia, walio wa Mataifa; Salamu.
24 Kwa kuwa tumesikia ya kwamba watu waliotoka kwetu wamewasumbua kwa maneno yao, wakipotosha roho zenu, ambao sisi hatukuwaagiza;
25 sisi tumeona vema, hali tumepatana kwa moyo mmoja, kuwachagua watu na kuwapeleka kwenu pamoja na wapendwa wetu Barnaba na Paulo,
26 watu waliohatirisha maisha yao kwa ajili ya jina la Bwana wetu Yesu Kristo.
27 Basi tumewatuma Yuda na Sila, watakaowaambia wenyewe maneno yayo hayo kwa vinywa vyao.
28 Kwa maana ilimpendeza Roho Mtakatifu na sisi, tusiwatwike mzigo ila hayo yaliyo lazima,
29 yaani, mjiepushe na vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na damu, na nyama zilizosongolewa, na uasherati. Mkijizuia na hayo, mtafanya vema. Wasalamu.
30 Hata hao wakiisha kupewa ruhusa wakatelemkia Antiokia; na baada ya kuwakusanya jamii yote wakawapa ile barua.
31 Nao walipokwisha kuisoma wakafurahi kwa ajili ya faraja ile.
32 Tena Yuda na Sila, kwa kuwa wao wenyewe ni manabii, wakawausia ndugu kwa maneno mengi, wakawathibitisha.
33 Na wakiisha kukaa huko muda, wakaruhusiwa na ndugu waende kwa amani kwa hao waliowatuma. [
34 Lakini Sila akaona vema kukaa huko.]
35 Na Paulo na Barnaba wakakaa huko Antiokia, wakifundisha na kulihubiri neno la Bwana, pamoja na watu wengine wengi.
36 Baada ya siku kadha wa kadha Paulo akamwambia Barnaba, Haya! Mrejee sasa tukawaangalie hao ndugu katika kila mji tulipolihubiri neno la Bwana, wa hali gani.
37 Barnaba akaazimu kumchukua Yohana aliyeitwa Marko pamoja nao.
38 Bali Paulo hakuona vema kumchukua huyo aliyewaacha huko Pamfilia, asiende nao kazini.
39 Basi palitokea mashindano baina yao hata wakatengana. Barnaba akamchukua Marko akatweka kwenda Kipro.
40 Lakini Paulo akamchagua Sila, akaondoka, akiombewa na wale ndugu apewe neema ya Bwana.
41 Akapita katika Shamu na Kilikia akiyathibitisha makanisa.

MATENDO 16


1 Basi akafika Derbe na Listra, na hapo palikuwa na mwanafunzi mmoja jina lake Timotheo, mwana wa mwanamke Myahudi aliyeamini; lakini babaye alikuwa Myunani.
2 Mtu huyo alishuhudiwa vema na ndugu waliokaa Listra na Ikonio.
3 Paulo akamtaka huyo afuatane naye, akamtwaa akamtahiri kwa ajili ya Wayahudi waliokuwako pande zile; kwa maana wote walijua ya kuwa babaye ni Myunani.
4 Basi walipokuwa wakipita kati ya miji ile, wakawapa zile amri zilizoamriwa na mitume na wazee walioko Yerusalemu, ili wazishike.
5 Makanisa yakatiwa nguvu katika ile Imani, hesabu yao ikaongezeka kila siku.
6 Wakapita katika nchi ya Frigia na Galatia, wakikatazwa na Roho Mtakatifu, wasilihubiri lile neno katika Asia.
7 Walipofika kukabili Misia wakajaribu kuenda Bithinia, lakini Roho wa Yesu hakuwapa ruhusa,
8 wakapita Misia wakatelemkia Troa.
9 Paulo akatokewa na maono usiku; alimwona mtu wa Makedonia amesimama, akimsihi, na kumwambia, Vuka, uje Makedonia utusaidie.
10 Basi alipokwisha kuyaona yale maono, mara tukataka kutoka kwenda Makedonia, kwa kuwa tuliona hakika ya kwamba Mungu ametuita tuwahubiri Habari Njema.
11 Basi tukang'oa nanga kutoka Troa, tukafika Samothrake kwa tanga moja, na siku ya pili tukafika Neapoli;
12 na kutoka hapo tukafika Filipi, mji wa Makedonia, mji ulio mkuu katika jimbo lile, mahali walipohamia Warumi; tukawa katika mji huu, tukikaa siku kadha wa kadha.
13 Hata siku ya sabato tukatoka nje ya lango, tukaenda kando ya mto, ambapo tukadhani ya kuwa pana mahali pa kusali; tukaketi, tukasema na wanawake waliokutana pale.
14 Mwanamke mmoja, jina lake Lidia, mwenye kuuza rangi ya zambarau, mwenyeji wa Thiatira, mcha Mungu, akatusikiliza, ambaye moyo wake ulifunguliwa na Bwana, ayatunze maneno yaliyonenwa na Paulo.
15 Hata alipokwisha kubatizwa, yeye na nyumba yake, akatusihi, akisema, Kama mmeniona kuwa mwaminifu kwa Bwana, ingieni nyumbani mwangu mkakae. Akatushurutisha.
16 Ikawa tulipokuwa tukienda mahali pale pa kusali, kijakazi mmoja aliyekuwa na pepo wa uaguzi akatukuta, aliyewapatia bwana zake faida nyingi kwa kuagua.
17 Akamfuata Paulo na sisi akipiga kelele, akisema, Watu hawa ni watumishi wa Mungu aliye juu, wenye kuwahubiria njia ya wokovu.
18 Akafanya hayo siku nyingi. Lakini Paulo akasikitika, akageuka akamwambia yule pepo, Nakuamuru kwa jina la Yesu Kristo, mtoke huyu. Akamtoka saa ile ile.
19 Basi bwana zake walipoona ya kuwa tumaini la faida yao limewapotea, wakawakamata Paulo na Sila, wakawakokota mpaka sokoni mbele ya wakuu wa mji;
20 wakawachukua kwa makadhi, wakasema, Watu hawa wanachafua sana mji wetu, nao ni Wayahudi;
21 tena wanatangaza habari ya desturi zisizokuwa halali kwetu kuzipokea wala kuzifuata, kwa kuwa sisi tu Warumi.
22 Makutano wote wakaondoka wakawaendea, makadhi wakawavua nguo zao kwa nguvu, wakatoa amri wapigwe kwa bakora.
23 Na walipokwisha kuwapiga mapigo mengi, wakawatupa gerezani, wakamwamuru mlinzi wa gereza awalinde sana.
24 Naye akiisha kupata amri hii akawatupa katika chumba cha ndani, akawafunga miguu kwa mkatale.
25 Lakini panapo usiku wa manane Paulo na Sila walikuwa wakimwomba Mungu na kumwimbia nyimbo za kumsifu, na wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza.
26 Ghafula pakawa tetemeko kuu la nchi, hata misingi ya gereza ikatikisika, na mara hiyo milango ikafunguka, vifungo vya wote vikalegezwa.
27 Yule mlinzi wa gereza akaamka, naye alipoona ya kuwa milango ya gereza imefunguka, alifuta upanga, akataka kujiua, akidhani ya kuwa wafungwa wamekimbia.
28 Ila Paulo akapaza sauti yake kwa nguvu, akisema, Usijidhuru, kwa maana sisi sote tupo hapa.
29 Akataka taa ziletwe, akarukia ndani, akitetemeka kwa hofu, akawaangukia Paulo na Sila;
30 kisha akawaleta nje akasema, Bwana zangu, yanipasa nifanye nini nipate kuokoka?
31 Wakamwambia, Mwamini Bwana Yesu, nawe utaokoka pamoja na nyumba yako.
32 Wakamwambia neno la Bwana, yeye na watu wote waliomo nyumbani mwake.
33 Akawakaribisha saa ile ile ya usiku, akawaosha mapigo yao, kisha akabatizwa, yeye na watu wake wote wakati uo huo.
34 Akawaleta juu nyumbani kwake, akawaandalia chakula, akafurahi sana, yeye na nyumba yake yote, maana amekwisha kumwamini Mungu.
35 Kulipopambauka makadhi wakawatuma wakubwa wa askari wakisema, Waacheni watu wale waende zao.
36 Yule mlinzi wa gereza akamwarifu Paulo maneno haya akisema, Makadhi wametuma watu ili mfunguliwe; basi, sasa tokeni nje, enendeni zenu kwa amani.
37 Paulo akawaambia, Wametupiga mbele ya watu wote bila kutuhukumu, na sisi tu Warumi, tena wametutupa gerezani; na sasa wanataka kututoa kwa siri? Sivyo, lakini na waje wenyewe wakatutoe.
38 Wakubwa wa askari wakawapasha makadhi habari za maneno haya; nao wakaogopa, waliposikia ya kwamba hao ni Warumi.
39 Wakaja wakawasihi; na walipokwisha kuwatoa nje, wakawaomba watoke katika mji ule.
40 Nao wakatoka gerezani wakaingia nyumbani mwa Lidia; na walipokwisha kuonana na ndugu wakawafariji, wakaenda zao.

MATENDO 17


1 Wakiisha kupita kati ya Amfipoli na Apolonia wakafika Thesalonike, ambapo palikuwa na sinagogi la Wayahudi.
2 Na Paulo, kama ilivyokuwa desturi yake, akaingia mle walimo, akahojiana nao kwa maneno ya maandiko sabato tatu,
3 akiyafunua na kuwaeleza ya kwamba ilimpasa Kristo kuteswa, na kufufuka katika wafu; na ya kwamba, Yesu huyu ninayewapasha ninyi habari zake ndiye Kristo.
4 Wengine miongoni mwao wakaamini, wakashikamana na Paulo na Sila; na Wayunani waliomcha Mungu, wengi sana, na wanawake wenye cheo si wachache.
5 Na Wayahudi wakaona wivu, wakajitwalia watu kadha wa kadha katika watu ovyo wasio na sifa njema, nao wakakutanisha mkutano, wakafanya ghasia mjini, wakawaendea watu wa nyumba ya Yasoni, wakataka kuwapeleka mbele ya watu wa mji;
6 na walipowakosa, wakamkokota Yasoni na baadhi ya ndugu mbele ya wakubwa wa mji, wakipiga kelele, wakisema, Watu hawa walioupindua ulimwengu wamefika huku nako,
7 na Yasoni amewakaribisha; na hawa wote wanatenda mambo yaliyo kinyume cha amri za Kaisari, wakisema na kwamba yupo mfalme mwingine, aitwaye Yesu.
8 Wakafadhaisha ule mkutano na wakubwa wa mji walipoyasikia hayo.
9 Nao walipokwisha kumtoza dhamana Yasoni na wenziwe wakawaacha waende zao.
10 Mara hao ndugu wakawapeleka Paulo na Sila usiku hata Beroya. Nao walipofika huko wakaingia katika sinagogi la Wayahudi.
11 Watu hawa walikuwa waungwana kuliko wale wa Thesalonike, kwa kuwa walilipokea lile neno kwa uelekevu wa moyo, wakayachunguza maandiko kila siku, waone kwamba mambo hayo ndivyo yalivyo.
12 Basi watu wengi miongoni mwao wakaamini, na wanawake wa Kiyunani wenye cheo, na wanaume si wachache.
13 Lakini Wayahudi wa Thesalonike walipopata habari ya kwamba neno la Mungu linahubiriwa na Paulo hata katika Beroya, wakaenda huko nako wakawachafua na kuwafadhaisha makutano.
14 Mara hiyo wale ndugu wakampeleka Paulo aende zake mpaka pwani; bali Sila na Timotheo wakasalia huko.
15 Lakini wale waliomsindikiza Paulo wakampeleka mpaka Athene; nao wakiisha kupokea maagizo kuwapelekea Sila na Timotheo, ya kwamba wasikawie kumfuata, wakaenda zao.
16 Paulo alipokuwa akiwangojea huko Athene na kuona jinsi mji ule ulivyojaa sanamu, roho yake ilichukizwa sana ndani yake.
17 Basi katika sinagogi akahojiana na Wayahudi na waliomcha Mungu, na wale waliokutana naye sokoni kila siku.
18 Na baadhi ya Waepikureo na Wastoiko, wenye ujuzi, wakakutana naye. Wengine wakasema, Mpuzi huyu anataka kusema nini? Wengine walisema, Anaonekana kuwa mtangaza habari za miungu migeni, kwa maana alikuwa akihubiri habari za Yesu na ufufuo.
19 Wakamshika, wakamchukua Areopago, wakisema, Je! Twaweza kujua maana ya elimu hii mpya unayoinena?
20 Kwa maana unaleta mambo mageni masikioni mwetu, tutapenda kujua, basi, maana ya mambo haya.
21 Kwa maana Waathene na wageni waliokaa huko walikuwa hawana nafasi kwa neno lo lote ila kutoa habari na kusikiliza habari za jambo jipya.
22 Paulo akasimama katikati ya Areopago, akasema, Enyi watu wa Athene, katika mambo yote naona ya kuwa ninyi ni watu wa kutafakari sana mambo ya dini.
23 Kwa sababu nilipokuwa nikipita huko na huko na kuyaona mambo ya ibada yenu, naliona madhabahu iliyoandikwa maneno haya, KWA MUNGU ASIYEJULIKANA. Basi mimi nawahubirini habari zake yeye ambaye ninyi mnamwabudu bila kumjua.
24 Mungu aliyeufanya ulimwengu na vitu vyote vilivyomo, yeye, kwa kuwa ni Bwana wa mbingu na nchi, hakai katika hekalu zilizojengwa kwa mikono;
25 wala hatumikiwi kwa mikono ya wanadamu kana kwamba anahitaji kitu cho chote; kwa maana ndiye anayewapa wote uzima na pumzi na vitu vyote.
26 Naye alifanya kila taifa la wanadamu kutoka katika mmoja, wakae juu ya uso wa nchi yote, akiisha kuwawekea nyakati alizoziamuru tangu zamani, na mipaka ya makazi yao;
27 ili wamtafute Mungu, ingawa ni kwa kupapasa-papasa, wakamwone, ijapokuwa hawi mbali na kila mmoja wetu.
28 Kwa maana ndani yake yeye tunaishi, tunakwenda, na kuwa na uhai wetu. Kama vile mmoja wenu, mtunga mashairi alivyosema, Maana sisi sote tu wazao wake.
29 Basi, kwa kuwa sisi tu wazao wa Mungu, haitupasi kudhani ya kuwa Uungu ni mfano wa dhahabu au fedha au jiwe, vitu vilivyochongwa kwa ustadi na akili za wanadamu.
30 Basi, zamani zile za ujinga Mungu alijifanya kama hazioni; bali sasa anawaagiza watu wote wa kila mahali watubu.
31 Kwa maana ameweka siku atakayowahukumu walimwengu kwa haki, kwa mtu yule aliyemchagua; naye amewapa watu wote uthabiti wa mambo haya kwa kumfufua katika wafu.
32 Basi waliposikia habari za ufufuo wa wafu wengine walifanya dhihaka; wengine wakasema, Tutakusikiliza tena katika habari hiyo.
33 Basi hivi Paulo akaondoka akawaacha.
34 Baadhi ya watu wakashikamana naye, wakaamini; katika hao alikuwamo Dionisio, Mwareopago, na mwanamke mmoja jina lake Damari, na watu wengine pamoja na hao.

MATENDO 18


1 Baada ya mambo hayo, Paulo akatoka Athene akafika Korintho.
2 Akamwona Myahudi mmoja, jina lake Akila, mzalia wa Ponto; naye amekuja kutoka nchi ya Italia siku za karibu, pamoja na Prisila mkewe, kwa sababu Klaudio amewaamuru Wayahudi wote watoke Rumi, naye akafikilia kwao;
3 na kwa kuwa kazi yao ya ufundi ilikuwa moja, akakaa kwao, wakafanya kazi pamoja, kwa maana walikuwa mafundi wa kushona hema.
4 Akatoa hoja zake katika sinagogi kila sabato, akajaribu kuwavuta Wayahudi na Wayunani.
5 Hata Sila na Timotheo walipotelemka kutoka Makedonia, Paulo akasongwa sana na lile neno, akiwashuhudia Wayahudi ya kwamba Yesu ni Kristo.
6 Walipopingamana naye na kumtukana Mungu, akakung'uta mavazi yake, akawaambia, Damu yenu na iwe juu ya vichwa vyenu; mimi ni safi; tangu sasa nitakwenda kwa watu wa Mataifa.
7 Akaondoka huko akaingia katika nyumba ya mtu mmoja jina lake Tito Yusto, mcha Mungu, ambaye nyumba yake ilikuwa mpaka mmoja na sinagogi.
8 Na Krispo, mkuu wa sinagogi, akamwamini Bwana pamoja na nyumba yake yote. Wakorintho wengi waliposikia, waliamini, wakabatizwa.
9 Bwana akamwambia Paulo kwa maono usiku, Usiogope, bali nena, wala usinyamaze,
10 kwa kuwa mimi ni pamoja nawe, wala hapana mtu atakayekushambulia ili kukudhuru; kwa maana mimi nina watu wengi katika mji huu.
11 Akakaa huko muda wa mwaka mmoja na miezi sita akifundisha kati yao neno la Mungu.
12 Hata Galio alipokuwa liwali wa Akaya, Wayahudi wakamwinukia Paulo kwa nia moja, wakamleta mbele ya kiti cha hukumu,
13 wakisema Mtu huyu huwavuta watu ili wamwabudu Mungu kinyume cha sheria.
14 Na Paulo alipotaka kufunua kinywa chake, Galio akawaambia Wayahudi, Kama lingekuwa jambo la dhuluma au la hila mbaya, enyi Wayahudi, ingekuwa haki mimi kuchukuliana nanyi;
15 bali ikiwa ni hoja juu ya maneno na majina na sheria yenu, liangalieni ninyi wenyewe, maana mimi sitaki kuwa mwamuzi wa mambo hayo.
16 Akawafukuza waondoke mbele ya kiti cha hukumu.
17 Nao wote wakamshika Sosthene, mkuu wa sinagogi, wakampiga mbele ya kiti cha hukumu. Wala Galio hakuyaona mambo hayo kuwa ni kitu.
18 Baada ya hayo Paulo akazidi kukaa huko siku nyingi, kisha akaagana na ndugu akaabiri kwenda Shamu; na Prisila na Akila wakaenda pamoja naye, alipokwisha kunyoa kichwa chake huko Kenkrea; maana alikuwa ana nadhiri.
19 Wakafika Efeso, akawaacha huko. Yeye mwenyewe akaingia katika sinagogi, akahojiana na Wayahudi.
20 Walipomtaka akae wakati mwingi zaidi, hakukubali;
21 bali aliagana nao, akisema, Nitarejea kwenu tena, Mungu akinijalia. Akatweka, akatoka Efeso,
22 na alipokwisha kushuka Kaisaria, akapanda juu, akawasalimu kanisa, kisha akatelemkia Antiokia.
23 Hata akiisha kukaa huko siku kadha wa kadha akaondoka, akapita kati ya nchi ya Galatia na Frigia, mji kwa mji, akiwathibitisha wanafunzi.
24 Basi Myahudi mmoja, jina lake Apolo, mzalia wa Iskanderia, mtu wa elimu, akafika Efeso; naye alikuwa hodari katika maandiko.
25 Mtu huyo alikuwa amefundishwa njia ya Bwana; na kwa kuwa roho yake ilikuwa ikimwaka, alianza kunena na kufundisha kwa usahihi habari za Yesu; naye alijua ubatizo wa Yohana tu.
26 Akaanza kunena kwa ujasiri katika sinagogi; hata Prisila na Akila walipomsikia wakamchukua kwao, wakamweleza njia ya Bwana kwa usahihi zaidi.
27 Na alipotaka kuvuka bahari aende mpaka Akaya, ndugu wakamhimiza, wakawaandikia wale wanafunzi wamkaribishe, naye alipofika akawasaidia sana wale waliokwisha kuamini kwa neema ya Mungu.
28 Kwa maana aliwashinda Wayahudi kabisa kabisa mbele ya watu wote, akionyesha kwa maneno ya maandiko ya kuwa Yesu ni Kristo.

MATENDO 19


1 Ikawa, Apolo alipokuwa Korintho, Paulo, akiisha kupita kati ya nchi za juu, akafika Efeso; akakutana na wanafunzi kadha wa kadha huko;
2 akawauliza, Je! Mlipokea Roho Mtakatifu mlipoamini? Wakamjibu, La, hata kusikia kwamba kuna Roho Mtakatifu hatukusikia.
3 Akawauliza, Basi mlibatizwa kwa ubatizo gani? Wakasema, Kwa ubatizo wa Yohana.
4 Paulo akasema, Yohana alibatiza kwa ubatizo wa toba, akiwaambia watu wamwamini yeye atakayekuja nyuma yake, yaani, Yesu.
5 Waliposikia haya wakabatizwa kwa jina la Bwana Yesu.
6 Na Paulo, alipokwisha kuweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akaja juu yao; wakaanza kunena kwa lugha, na kutabiri.
7 Na jumla yao walipata wanaume kumi na wawili.
8 Akaingia ndani ya sinagogi, akanena kwa ushujaa kwa muda wa miezi mitatu, akihojiana na watu, na kuwavuta katika mambo ya ufalme wa Mungu.
9 Lakini wengine walikaidi, wakakataa kuamini, wakiitukana ile Njia mbele ya mkutano; basi, akaondoka akawaacha, akawatenga wanafunzi, akahojiana na watu kila siku katika darasa ya mtu mmoja, jina lake Tirano.
10 Mambo haya yakaendelea kwa muda wa miaka miwili, hata wote waliokaa Asia wakalisikia neno la Bwana, Wayahudi kwa Wayunani.
11 Mungu akafanya kwa mikono ya Paulo miujiza ya kupita kawaida;
12 hata wagonjwa wakaletewa leso na nguo zilizotoka mwilini mwake, magonjwa yao yakawaondokea, pepo wachafu wakawatoka.
13 Baadhi ya Wayahudi wenye kutanga-tanga, nao ni wapunga pepo, wakajaribu kutaja jina la Bwana Yesu juu yao waliopagawa na pepo wachafu, wakisema, Nawaapisha kwa Yesu, yule anayehubiriwa na Paulo.
14 Walikuwako wana saba wa mtu mmoja Skewa, Myahudi, kuhani mkuu, waliofanya hivyo.
15 Yule pepo mchafu akawajibu, akawaambia, Yesu namjua na Paulo namfahamu, lakini ninyi ni nani?
16 Na yule mtu aliyepagawa na pepo mchafu akawarukia wawili, akawaweza, akawashinda, hata wakatoka mbio katika nyumba ile hali wa uchi na kujeruhiwa.
17 Habari hii ikajulikana na Wayahudi wote na Wayunani waliokaa Efeso, hofu ikawaingia wote, na jina la Bwana Yesu likatukuzwa.
18 Na wengi wa wale walioamini wakaja wakaungama, wakidhihirisha matendo yao.
19 Na watu wengi katika wale waliotumia mambo ya uganga wakakusanya vitabu vyao, wakavichoma moto mbele ya watu wote; wakafanya hesabu ya thamani yake, wakaona ya kwamba yapata fedha hamsini elfu.
20 Hivyo ndivyo neno la Bwana lilivyozidi na kushinda kwa nguvu.
21 Mambo hayo yalipokwisha kumalizika, Paulo akaazimu rohoni mwake, akiisha kupita katika Makedonia na Akaya, aende Yerusalemu, akisema, Baada ya kuwako huko, yanipasa kuuona na Rumi pia.
22 Akatuma watu wawili miongoni mwa wale waliomtumikia kwenda Makedonia, nao ni Timotheo na Erasto, yeye mwenyewe akakaa katika Asia kitambo.
23 Wakati huo kukatukia ghasia si haba katika habari ya Njia ile.
24 Kwa maana mtu mmoja, jina lake Demetrio, mfua fedha, aliyekuwa akifanya vihekalu vya fedha vya Artemi, alikuwa akiwapatia mafundi faida nyingi.
25 Akawakusanya hao, pamoja na wengine wenye kazi ile ile, akasema, Enyi wanaume, mnajua ya kuwa utajiri wetu hutoka katika kazi hii.
26 Tena mnaona na kusikia ya kwamba si katika Efeso tu, bali katika Asia yote pia Paulo huyo ameshawishi watu wengi na kuwageuza nia zao, akisema ya kwamba hiyo inayofanywa kwa mikono siyo miungu.
27 Si kwamba kazi hii yetu ina hatari ya kudharauliwa tu; bali na hekalu la mungu mke aliye mkuu, Artemi, kuhesabiwa si kitu, na kuondolewa utukufu wake, ambaye Asia yote pia na walimwengu wote humwabudu.
28 Waliposikia haya wakajaa ghadhabu, wakapiga kelele, wakisema, Artemi wa Waefeso ni mkuu.
29 Mji wote ukajaa ghasia, wakaenda mbio wakaingia mahali pa michezo kwa nia moja, wakiisha kuwakamata Gayo na Aristarko, watu wa Makedonia waliosafiri pamoja na Paulo.
30 Na Paulo alipotaka kuingia kati ya watu, wanafunzi hawakumwacha aingie.
31 Na baadhi ya wakuu wa Asia, walio rafiki zake, wakatuma watu kwake, wakimsihi asijihudhurishe nafsi yake ndani ya mahali pa michezo.
32 Basi wengine walikuwa wakilia hivi na wengine hivi; kwa maana ule mkutano ulikuwa umechafuka-chafuka, na wengi wao hawakuijua sababu ya kukusanyika kwao pamoja.
33 Wakamtoa Iskanda katika mkutano, Wayahudi wakimweka mbele ya watu. Iskanda akawapungia mkono, akitaka kujitetea mbele ya wale watu.
34 Lakini walipotambua ya kuwa yeye ni Myahudi, wakapiga kelele wote pia kwa sauti moja kwa muda wa kama saa mbili, wakisema, Artemi wa Waefeso ni mkuu.
35 Na karani wa mji alipokwisha kuwatuliza watu, akasema, Enyi wanaume wa Efeso, ni mtu gani asiyejua ya kuwa mji wa Efeso ni mtunzaji wa hekalu la Artemi, aliye mkuu, na wa kitu kile kilichoanguka kutoka mbinguni?
36 Basi kwa kuwa mambo haya hayawezi kukanushwa, imewapasa kutulia; msifanye neno la haraka haraka.
37 Kwa maana mmewaleta watu hawa, wasioiba vitu vya hekalu wala kumtukana mungu mke wetu.
38 Basi ikiwa Demetrio na mafundi walio pamoja naye wana neno juu ya mtu, baraza ziko, na maliwali wako; na washitakiane.
39 Bali mkitafuta neno lo lote katika mambo mengine, yatatengenezwa katika kusanyiko lililo halali.
40 Kwa maana tuna hatari ya kushitakiwa kwa ajili ya matata haya ya leo, ambayo hayana sababu; na katika neno hilo, hatutaweza kujiudhuru kwa mkutano huu.
41 Alipokwisha kusema haya akauvunja mkutano.

MATENDO 20


1 Kishindo kile kilipokoma, Paulo akatuma kuwaita wanafunzi akawaonya, akaagana nao, kisha akaondoka aende zake mpaka Makedonia.
2 Naye akiisha kupita pande zile na kuwafariji kwa maneno mengi, akafika Uyunani.
3 Alipokwisha kukaa huko miezi mitatu, na Wayahudi kumfanyia vitimvi, alipotaka kwenda Shamu kwa njia ya bahari; basi akaazimu kurejea kwa njia ya Makedonia.
4 Watu hawa wakafuatana naye, Sopatro Mberoya, mwana wa Piro, na Aristarko na Sekundo, watu wa Thesalonike; na Gayo mtu wa Derbe, na Timotheo; na Tikiko na Trofimo watu wa Asia.
5 Ila watu hao wamekwisha kutangulia wakamngojea Troa.
6 Sisi tukatweka baada ya siku za mikate isiyotiwa chachu, tukatoka Filipi, tukawafikia Troa, safari ya siku tano, tukakaa huko siku saba.
7 Hata siku ya kwanza ya juma, tulipokuwa tumekutana ili kumega mkate, Paulo akawahutubu, akiazimu kusafiri siku ya pili yake, naye akafuliza maneno yake hata usiku wa manane.
8 Palikuwa na taa nyingi katika orofa ile tulipokuwa tumekusanyika.
9 Kijana mmoja, jina lake Eutiko, alikuwa ameketi dirishani, akalemewa na usingizi sana; hata Paulo alipoendelea sana kuhubiri, akazidiwa na usingizi wake akaanguka toka orofa ya tatu; akainuliwa amekwisha kufa.
10 Paulo akashuka, akamwangukia, akamkumbatia, akasema, Msifanye ghasia, maana uzima wake ungalimo ndani yake.
11 Akapanda juu tena, akamega mkate, akala, akazidi kuongea nao hata alfajiri, ndipo akaenda zake.
12 Wakamleta yule kijana, yu mzima, wakafarijika faraja kubwa sana.
13 Lakini sisi tukatangulia kwenda merikebuni, tukaabiri kwenda Aso, tukikusudia kumpakia Paulo huko; kwa maana ndivyo alivyoagiza, yeye mwenyewe aliazimu kwenda kwa miguu.
14 Alipotufikia huko Aso, tukampakia, kisha tukafika Mitilene.
15 Tukatweka kutoka huko, na siku ya pili tukafika mahali panapokabili Kio; siku ya tatu tukawasili Samo, tukakaa Trogilio, siku ya nne tukafika Mileto.
16 Kwa sababu Paulo amekusudia kupita Efeso merikebuni, asije akakawia katika Asia; kwa maana alikuwa na haraka, akitaka kuwahi Yerusalemu siku ya Pentekoste, kama ikiwezekana.
17 Toka Mileto Paulo akatuma watu kwenda Efeso, akawaita wazee wa kanisa.
18 Walipofika kwake, akawaambia, Ninyi wenyewe mnajua tangu siku ya kwanza nilipokanyaga hapa Asia, jinsi nilivyokuwa kwenu wakati wote,
19 nikimtumikia Bwana kwa unyenyekevu wote, na kwa machozi, na majaribu yaliyonipata kwa hila za Wayahudi;
20 ya kuwa sikujiepusha katika kuwatangazia neno lo lote liwezalo kuwafaa bali naliwafundisha waziwazi, na nyumba kwa nyumba,
21 nikiwashuhudia Wayahudi na Wayunani wamtubie Mungu, na kumwamini Bwana wetu Yesu Kristo.
22 Basi sasa, angalieni, nashika njia kwenda Yerusalemu hali nimefungwa rohoni, nisiyajue mambo yatakayonikuta huko;
23 isipokuwa Roho Mtakatifu mji kwa mji hunishuhudia akisema, ya kwamba vifungo na dhiki vyaningoja.
24 Lakini siyahesabu maisha yangu kuwa kitu cha thamani kwangu kama kuumaliza mwendo wangu na huduma ile niliyopokea kwa Bwana Yesu, kuishuhudia Habari Njema ya neema ya Mungu.
25 Na sasa, tazameni, mimi najua ya kuwa ninyi nyote niliowahubiria ufalme wa Mungu, nikienda huko na huko, hamtaniona uso tena.
26 Kwa hiyo nawashuhudia wote siku hii ya leo, ya kuwa mimi sina hatia kwa damu ya mtu awaye yote.
27 Kwa maana sikujiepusha na kuwahubiria habari ya kusudi lote la Mungu.
28 Jitunzeni nafsi zenu, na lile kundi lote nalo, ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa waangalizi ndani yake, mpate kulilisha kanisa lake Mungu, alilolinunua kwa damu yake mwenyewe.
29 Najua mimi ya kuwa baada ya kuondoka kwangu mbwa-mwitu wakali wataingia kwenu, wasilihurumie kundi;
30 tena katika ninyi wenyewe watainuka watu wakisema mapotovu, wawavute hao wanafunzi wawaandamie wao.
31 Kwa hiyo kesheni, mkikumbuka ya kwamba miaka mitatu, usiku na mchana, sikuacha kumwonya kila mtu kwa machozi.
32 Basi, sasa nawaweka katika mikono ya Mungu, na kwa neno la neema yake, ambalo laweza kuwajenga na kuwapa urithi pamoja nao wote waliotakaswa.
33 Sikutamani fedha wala dhahabu, wala mavazi ya mtu.
34 Ninyi wenyewe mnajua ya kuwa mikono yangu hii imetumika kwa mahitaji yangu na ya wale waliokuwa pamoja nami.
35 Katika mambo yote nimewaonyesha ya kuwa kwa kushika kazi hivi imewapasa kuwasaidia wanyonge, na kuyakumbuka maneno ya Bwana Yesu, jinsi alivyosema mwenyewe, Ni heri kutoa kuliko kupokea.
36 Alipokwisha kunena haya akapiga magoti, akaomba pamoja nao wote.
37 Wakalia sana wote, wakamwangukia Paulo shingoni, wakambusu-busu,
38 wakihuzunika zaidi kwa sababu ya neno lile alilosema, ya kwamba hawatamwona uso tena. Wakamsindikiza hata merikebuni.

MATENDO 21


1 Ikawa tulipokwisha kujitenga nao na kuabiri, tukafika Kosi kwa tanga moja, na siku ya pili yake tukafika Rodo na kutoka huko tukafika Patara,
2 tukapata merikebu itakayovuka mpaka Foinike tukapanda tukatweka.
3 Na tulipoona Kipro tukaiacha upande wa kushoto; tukasafiri mpaka Shamu tukashuka Tiro. Kwa maana huko ndiko merikebu yetu itakakoshusha shehena yake.
4 Tukiisha kuwaona wanafunzi tukakaa huko siku saba, nao wakamwambia Paulo kwa uweza wa Roho asipande kwenda Yerusalemu.
5 Hata tulipotimiza siku zile tukaondoka tukaenda zetu, na watu wote, pamoja na wake zao na watoto wao, wakatusindikiza mpake nje ya mji, tukapiga magoti pwani tukaomba;
6 na baada ya kuagana tukapanda merikebuni, nao wakarudi kwao.
7 Hata tulipomaliza safari yetu kutoka Tiro tukafika Tolemai, tukawaamkua ndugu tukakaa kwao siku moja.
8 Asubuhi yake tukaondoka, tukafika Kaisaria, tukaingia nyumbani mwa Filipo, mhubiri wa Injili, aliyekuwa mmoja wa wale saba, tukakaa kwake.
9 Mtu huyu alikuwa na binti wanne, mabikira, waliokuwa wakitabiri.
10 Basi tulipokuwa tukikaa huko siku nyingi, nabii mmoja jina lake Agabo akashuka kutoka Uyahudi.
11 Alipotufikia akautwaa mshipi wa Paulo, akajifunga miguu na mikono, akasema, Roho Mtakatifu asema hivi, Hivyo ndivyo Wayahudi wa Yerusalemu watakavyomfunga mtu mwenye mshipi huu, nao watamtia katika mikono ya watu wa Mataifa.
12 Basi tuliposikia haya, sisi na watu wa mahali pale, tukamsihi asipande kwenda Yerusalemu.
13 Ndipo Paulo alipojibu, Mnafanya nini, kulia na kunivunja moyo? Kwa maana mimi, licha ya kufungwa, ni tayari hata kuuawa katika Yerusalemu kwa ajili ya jina lake Bwana Yesu.
14 Alipokataa shauri letu, tukanyamaza tukisema, Mapenzi ya Bwana na yatendeke.
15 Baada ya siku zile tukachukua vyombo vyetu tukapanda kwenda Yerusalemu.
16 Baadhi ya wanafunzi wa Kaisaria wakafuatana na sisi, wakamchukua na Mnasoni, mtu wa Kipro, mwanafunzi wa zamani ambaye ndiye tutakayekaa kwake.
17 Tulipofika Yerusalemu wale ndugu wakatukaribisha kwa furaha.
18 Hata siku ya pili yake Paulo akaingia kwa Yakobo pamoja nasi, na wazee wote walikuwako.
19 Na baada ya kuwaamkua, akawaeleza mambo yote moja moja Mungu aliyoyatenda katika Mataifa kwa huduma yake.
20 Nao waliposikia wakamtukuza Mungu, wakamwambia, Ndugu yetu, unaona jinsi Wayahudi walioamini walivyo elfu nyingi, nao wote wana wivu sana kwa ajili ya torati.
21 Nao wameambiwa habari zako, ya kwamba unawafundisha Wayahudi wote wakaao katika Mataifa kumwacha Musa, ukiwaambia wasiwatahiri watoto wao, wala wasizifuate desturi.
22 Basi, ni nini? Bila shaka watasikia kwamba umekuja.
23 Basi fanya neno hili tunalokuambia. Wako kwetu watu wanne waliofungwa na nadhiri.
24 Wachukue watu hao, ujitakase pamoja nao, na kuwagharimia ili wanyoe vichwa vyao, watu wote wapate kujua ya kuwa habari zile walizoambiwa juu yako si kitu, bali wewe mwenyewe unaenenda vizuri na kuishika torati.
25 Lakini kwa habari za watu wa Mataifa walioamini, tuliandika na kutoa hukumu yetu ya wao kujilinda nafsi zao na vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na damu, na kitu kilichosongolewa, na uasherati.
26 Ndipo Paulo akawatwaa wanaume wale, na siku ya pili yake akajitakasa nafsi yake pamoja nao, akaingia ndani ya hekalu, akitangaza habari ya kutimiza siku za utakaso, hata sadaka itolewe kwa ajili ya kila mmoja wao.
27 Basi zile siku saba zilipokuwa karibu kutimia, Wayahudi waliotoka Asia wakamwona ndani ya hekalu, wakawataharakisha watu wote, wakamkamata,
28 wakapiga kelele, na kusema, Enyi wanaume wa Israeli, tusaidieni. Huyu ndiye mtu yule afundishaye watu wote kila mahali kinyume cha taifa letu na torati na mahali hapa. Tena, zaidi ya haya, amewaingiza Wayunani katika hekalu, akapatia unajisi mahali hapa patakatifu.
29 Kwa maana walikuwa wamemwona Trofimo, Mwefeso, pamoja naye mjini, ambaye walidhania ya kuwa Paulo amemwingiza katika hekalu.
30 Mji wote ukataharuki, watu wakakutanika mbio mbio, wakamkamata Paulo, wakamkokota, wakamtoa hekaluni; mara milango ikafungwa.
31 Na walipokuwa wakitafuta njia ya kumwua, habari zikamfikilia jemadari wa kikosi ya kwamba Yerusalemu imechafuka, mji mzima.
32 Mara akatwaa askari na maakida, akawashukia mbio. Nao walipomwona jemadari na askari wakaacha kumpiga Paulo.
33 Kisha jemadari akakaribia, akamshika, akaamuru afungwe kwa minyororo miwili; akauliza, Nani huyu? Tena, amefanya nini?
34 Wengine katika makutano wakapiga kelele wakisema hivi, na wengine hivi. Basi alipokuwa hawezi kupata hakika ya habari kwa sababu ya zile kelele, akatoa amri aletwe ndani ya ngome.
35 Basi Paulo alipofika darajani ilikuwa kuchukuliwa na askari kwa sababu ya nguvu ya makutano.
36 Maana kundi kubwa la watu wakamfuata, wakipiga kelele, na kusema, Mwondoe huyu.
37 Naye alipokuwa analetwa ndani ya ngome, Paulo akamwambia jemadari, Nina ruhusa nikuambie neno? Naye akasema, Je! Unajua Kiyunani?
38 Wewe si yule Mmisri ambaye kabla ya siku hizi aliwafitinisha wale watu elfu nne, walioitwa Wauaji, akawaongoza jangwani?
39 Paulo akasema, Mimi ni mtu wa Kiyahudi, mtu wa Tarso, mji wa Kilikia, mwenyeji wa mji usiokuwa mnyonge. Nakuomba, nipe ruhusa niseme na wenyeji hawa.
40 Basi, alipompa ruhusa, Paulo akasimama madarajani, akawapungia mkono wale wenyeji; na ilipokuwa kimya kabisa, akanena nao kwa lugha ya Kiebrania, akisema,

MATENDO 22


1 Enyi wanaume, ndugu zangu na baba zangu, nisikilizeni, nikijitetea mbele yenu sasa.
2 Waliposikia kwamba anasema nao kwa lugha ya Kiebrania wakazidi kunyamaza; akasema,
3 Mimi ni mtu wa Kiyahudi, nalizaliwa Tarso, mji wa Kilikia, ila nililelewa katika mji huu, miguuni pa Gamalieli, nikafundishwa sheria ya baba zetu kwa usahihi, nikawa mtu wa jitihadi kwa Mungu kama ninyi nyote mlivyo leo hivi;
4 nikawaudhi watu wa Njia hii hata kuwaua, nikawafunga, nikiwatia gerezani, wanaume na wanawake.
5 Kama Kuhani Mkuu naye anishuhudiavyo, na wazee wa baraza wote pia, ambao nalipokea barua kwao kuwapelekea ndugu wale, nikaenda Dameski, ili niwalete wale waliokuwa huko hata Yerusalemu, hali wamefungwa, ili waadhibiwe.
6 Ikawa nilipokuwa nikisafiri, nikikaribia Dameski, wakati wa adhuhuri, ghafula nuru kuu ilitoka mbinguni, ikanimulikia pande zote.
7 Nikaanguka nchi, nikasikia sauti ikiniambia, Sauli, Sauli, mbona unaniudhi?
8 Nikajibu, Wewe u nani, Bwana? Akaniambia, Mimi ni Yesu Mnazareti, ambaye wewe unaniudhi.
9 Na wale waliokuwa pamoja nami waliiona ile nuru, lakini hawakuisikia ile sauti ya yule aliyesema nami.
10 Nikasema, Nifanye nini, Bwana? Bwana akaniambia, Simama, uingie Dameski, na huko utaambiwa habari za mambo yote yaliyoamriwa uyafanye.
11 Na nilipokuwa sioni kwa sababu ya fahari ya nuru ile, nikaongozwa na mikono yao waliokuwa pamoja nami, nikaingia Dameski.
12 Basi mtu mmoja, Anania, mtauwa kwa kuifuata sheria, aliyeshuhudiwa wema na Wayahudi wote waliokaa huko,
13 Akanijia, akasimama karibu nami, akaniambia, Ndugu yangu Sauli, uone. Nikamwinulia macho yangu saa ile ile.
14 Akasema, Mungu wa baba zetu amekuchagua wewe upate kujua mapenzi yake, na kumwona yule Mwenye haki, na kuisikia sauti itokayo katika kinywa chake.
15 Kwa maana utakuwa shahidi wake kwa watu wote, wa mambo hayo uliyoyaona na kuyasikia.
16 Basi sasa, unakawilia nini? Simama, ubatizwe, ukaoshe dhambi zako, ukiliitia jina lake.
17 Ikawa nilipokwisha kurudi Yerusalemu, nilipokuwa nikisali ndani ya hekalu, nikawa hali ya kuzimia roho,
18 nikamwona, naye akiniambia, Hima, utoke Yerusalemu upesi, kwa sababu hawatakubali ushuhuda wako katika habari zangu.
19 Nami nikasema, Bwana, wanajua hao ya kuwa mimi nalikuwa nikiwafunga gerezani wale wanaokuamini na kuwapiga katika kila sinagogi.
20 Na damu ya Stefano shahidi wako ilipomwagwa, mimi nami nilikuwa nikisimama karibu, nikikubali, na kuzitunza nguo zao waliomwua.
21 Naye akaniambia, Enenda zako; kwa kuwa mimi nitakutuma uende mbali kwa watu wa Mataifa.
22 Wakamsikiliza mpaka neno lile, wakapaza sauti zao, wakisema, Mwondoe huyu katika nchi, kwa maana haifai aishi.
23 Walipokuwa wakipiga kelele na kutupa mavazi yao na kurusha-rusha mavumbi juu,
24 yule jemadari akaamuru aletwe ndani ya ngome, akisema aulizwe habari zake kwa kupigwa mijeledi, ili ajue sababu hata wakampigia kelele namna hii.
25 Hata walipokwisha kumfunga kwa kamba, Paulo akamwambia yule akida aliyesimama karibu, Je! Ni halali ninyi kumpiga mtu aliye Mrumi naye hajakuhumiwa bado?
26 Yule akida aliposikia, akaenda akamwarifu yule jemadari, akisema, Unataka kufanya nini? Kwa maana mtu huyu ni Mrumi.
27 Jemadari akaja, akamwuliza, Niambie, u Mrumi? Akasema, Ndiyo.
28 Jemadari akajibu, Mimi nalipata wenyeji huu kwa mali nyingi. Paulo akasema, Na mimi ni Mrumi wa kuzaliwa.
29 Basi wale waliokuwa tayari kumwuliza wakaondoka wakamwacha. Na yule jemadari naye akaogopa, alipojua ya kuwa ni Mrumi, na kwa sababu amemfunga.
30 Siku ya pili yake akitaka kujua hakika, ni kwa sababu gani ameshitakiwa na Wayahudi, akamfungua, akawaamuru wakuu wa makuhani na baraza yote wakutane. Akamleta Paulo chini, akamweka mbele yao.

MATENDO 23


1 Paulo akawakazia macho watu wa baraza, akasema, Ndugu zangu, mimi kwa dhamiri safi kabisa nimeishi mbele za Mungu hata leo hivi.
2 Kuhani Mkuu Anania akawaamuru wale waliosimama karibu naye wampige kinywa chake.
3 Ndipo Paulo akamwambia, Mungu atakupiga wewe, ukuta uliopakwa chokaa. Wewe umeketi kunihukumu sawasawa na sheria, nawe unaamuru nipigwe kinyume cha sheria?
4 Wale waliosimama karibu wakasema, Je! Unamtukana Kuhani Mkuu wa Mungu?
5 Paulo akasema, Sikujua, ndugu zangu, ya kuwa yeye ni Kuhani Mkuu; maana imeandikwa, Usimnenee mabaya mkuu wa watu wako.
6 Paulo alipotambua ya kuwa sehemu moja ni Masadukayo, na sehemu ya pili ni Mafarisayo, akapaza sauti yake katika ile baraza, Ndugu zangu, mimi ni Farisayo mwana wa Farisayo; mimi ninahukumiwa kwa ajili ya tumaini la ufufuo wa wafu.
7 Alipokwisha kunena hayo palikuwa na mashindano baina ya Mafarisayo na Masadukayo, mkutano ukafarakana.
8 Kwa maana Masadukayo husema ya kwamba hakuna kiyama wala malaika wala roho; bali Mafarisayo hukiri yote.
9 Pakawa na makelele mengi. Waandishi wengine wa upande wa Mafarisayo wakasimama, wakateta, wakisema, Hatuoni uovu wo wote katika mtu huyu; bali ikiwa roho au malaika amesema naye, ni nini?
10 Ugomvi mkubwa ulipotokea, yule jemadari akachelea Paulo asije akararuliwa nao, akaamuru askari washuke na kumwondoa kwa nguvu mikononi mwao, na kumleta ndani ya ngome.
11 Usiku ule Bwana akasimama karibu naye, akasema, Uwe na moyo mkuu; kwa sababu, kama ulivyonishuhudia habari zangu Yerusalemu, imekupasa kunishuhudia vivyo hivyo Rumi nako.
12 Kulipopambauka, Wayahudi wakafanya mapatano, wakajifunga kwa kiapo kwamba hawatakula wala hawatakunywa hata wamwue Paulo.
13 Na hao walioapiana hivyo walipata zaidi ya watu arobaini.
14 Nao wakaenda kwa wakuu wa makuhani na wazee, wakasema, Tumejifunga kwa kiapo tusionje kitu hata tumwue Paulo.
15 Basi sasa ninyi pamoja na wazee wa baraza mwambieni jemadari amlete chini kwenu, kana kwamba mnataka kujua habari zake vizuri zaidi; na sisi tu tayari kumwua kabla hajakaribia.
16 Mjomba wake Paulo akasikia habari za kuotea kwao, akaenda akaingia ndani ya ngome akampasha Paulo habari.
17 Paulo akamwita akida mmoja, akasema, Mchukue kijana huyu kwa jemadari; maana ana neno la kumwarifu.
18 Basi akamchukua, akampeleka kwa jemadari, akamwambia, Paulo, yule mfungwa, aliniita akataka nikuletee kijana huyu kwa kuwa ana neno la kukuambia.
19 Yule jemadari akamshika mkono akajitenga pamoja naye kando, akamwuliza kwa faragha, Una neno gani utakalo kuniarifu?
20 Akasema Wayahudi wamepatana kukuomba umlete Paulo chini kesho, ukamweke mbele ya baraza, kana kwamba wanataka kupata habari zake kwa usahihi zaidi.
21 Basi wewe usikubali; kwa maana watu zaidi ya arobaini wanamwotea, wamejifunga kwa kiapo wasile wala wasinywe hata watakapomwua; nao sasa wako tayari, wakiitazamia ahadi kwako.
22 Basi yule jemadari akamwacha kijana aende zake, akimwagiza, Usimwambie mtu awaye yote ya kwamba umeniarifu haya.
23 Akawaita maakida wawili, akasema, Wekeni tayari askari mia mbili kwenda Kaisaria, na askari wapanda farasi sabini, na wenye mikuki mia mbili, kwa saa tatu ya usiku.
24 Akawaambia kuweka wanyama tayari wampandishe Paulo, na kumchukua salama kwa Feliki liwali.
25 Akaandika barua, kwa namna hii,
26 Klaudio Lisia kwa liwali mtukufu Feliki, Salamu!
27 Mtu huyu alikamatwa na Wayahudi, wakawa karibu kumwua, ndipo nikaenda pamoja na kikosi cha askari nikamwokoa, nilipopata habari ya kuwa yeye ni Mrumi.
28 Nami nikitaka kulijua lile neno walilomshitakia, nikamtelemsha nikamweka mbele ya baraza;
29 nikaona kwamba ameshitakiwa kwa ajili ya maswali ya sheria yao, wala hakushitakiwa neno lo lote la kustahili kuuawa wala kufungwa.
30 Hata nilipopewa habari kwamba patakuwa na vitimvi juu ya mtu huyu, mara nikampeleka kwako, nikawaagiza na wale waliomshitaki, wanene habari zake mbele yako. Wasalamu.
31 Basi, wale askari wakamchukua Paulo kama walivyoamriwa, wakampeleka hata Antipatri usiku;
32 hata asubuhi wakawaacha wale wapanda farasi waende pamoja naye, nao wakarudi zao ngomeni.
33 Na wale walipofika Kaisaria, na kumpa liwali ile barua, wakamweka Paulo mbele yake.
34 Naye alipokwisha kuisoma, akawauliza, Mtu huyu ni wa jimbo gani? Alipoarifiwa ya kuwa ni mtu wa Kilikia,
35 akasema, Nitakusikia wewe watakapokuja wale waliokushitaki; akaamuru alindwe katika nyumba ya uliwali ya Herode.

MATENDO 24


1 Baada ya siku tano, Anania, Kuhani Mkuu, akatelemka na baadhi ya wazee pamoja naye, na msemi mmoja, Tertulo, nao wakamweleza liwali habari za Paulo.
2 Naye alipoitwa, Tertulo akaanza kumshitaki, akisema, Kwa kuwa mnapata amani nyingi chini yako, Feliki mtukufu, na kwa maangalizi yako mambo mabaya yanatengenezwa kwa ajili ya taifa hili,
3 basi tunayapokea kila wakati na kila mahali, kwa shukrani yote.
4 Lakini nisikuudhi zaidi, nakusihi utusikilize maneno machache kwa fadhili zako.
5 Kwa maana tumemwona mtu huyu mkorofi, mwanzilishi wa fitina katika Wayahudi wote duniani, tena ni kichwa cha madhehebu ya Wanazorayo.
6 Na tena alijaribu kulitia hekalu unajisi; tukamkamata; [tukataka kumhukumu kwa sheria yetu.
7 Lakini Lisia jemadari akafika akamwondoa mikononi mwetu kwa nguvu,
8 Akawaamuru wale waliomshitaki waje kwako.] Wewe mwenyewe kwa kumwuliza-uliza utaweza kupata habari ya mambo yale yote tunayomshitaki sisi.
9 Wayahudi nao wakamshitaki, wakisema ya kuwa ndivyo yalivyo.
10 Na liwali alipompungia mkono ili anene, Paulo akajibu, Kwa kuwa ninajua ya kwamba wewe umekuwa mwamuzi wa taifa hili kwa muda wa miaka mingi, najitetea mwenyewe kwa moyo wa furaha.
11 Maana waweza kujua ya kuwa hazijapita siku zaidi ya kumi na mbili tangu nilipopanda kwenda Yerusalemu ili kuabudu.
12 Watu hawa hawakuniona ndani ya hekalu, nikihojiana na mtu, au kufanya fujo katika mkutano, wala katika masinagogi wala ndani ya mji.
13 Wala hawawezi kuyahakikisha mambo haya wanayonishitaki sasa.
14 Ila neno hili naungama kwako ya kwamba kwa Njia ile ambayo waiita uzushi, ndivyo ninavyomwabudu Mungu wa baba zetu, nikiyaamini yote yanayopatana na torati na yaliyoandikwa katika vyuo vya manabii.
15 Nina tumaini kwa Mungu, ambalo hata hao nao wanalitazamia, ya kwamba kutakuwa na ufufuo wa wafu, wenye haki na wasio haki pia.
16 Nami ninajizoeza katika neno hili niwe na dhamiri isiyo na hatia mbele za Mungu na mbele ya watu siku zote.
17 Baada ya miaka mingi nalifika niwaletee watu wa taifa langu sadaka na matoleo.
18 Wakaniona ndani ya hekalu nikishughulika na mambo haya, hali nimetakaswa, wala sikuwa na mkutano wala ghasia; lakini walikuwako baadhi ya Wayahudi waliotoka Asia,
19 ambao imewapasa hao kuwapo hapa mbele yako na kunishitaki, kama wana neno lo lote juu yangu.
20 Au watu hawa wenyewe na waseme, ni kosa gani waliloliona kwangu niliposimama mbele ya baraza,
21 isipokuwa kwa ajili ya sauti hii moja, nilipolia nikisimama katikati yao, na kusema, Kwa ajili ya ufufuo wa wafu ninahukumiwa mbele yenu hivi leo.
22 Basi Feliki aliwaahirisha, kwa sababu alijua habari za Njia ile kwa usahihi zaidi, akasema, Lisia jemadari atakapotelemka nitakata maneno yenu.
23 Akamwamuru yule akida kwamba Paulo alindwe; ila awe na nafasi, wala asimkataze mmojawapo wa rafiki zake kumtumikia.
24 Baada ya siku kadha wa kadha, Feliki akafika pamoja na Drusila mkewe aliyekuwa Myahudi, akatuma kumwita Paulo akamsikiliza habari za imani iliyo kwa Kristo Yesu.
25 Na Paulo alipokuwa akitoa hoja zake katika habari ya haki, na kuwa na kiasi, na hukumu itakayokuja, Feliki akafanya hofu akajibu, Sasa enenda zako, nami nikipata nafasi nitakuita.
26 Pamoja na hayo alitaraji kwamba atapewa fedha na Paulo; kwa hiyo alimwita mara nyingi akaongea naye.
27 Na miaka miwili ilipotimia, Feliki akampokea Porkio Festo atawale badala yake. Na Feliki, akitaka kuwafanyia Wayahudi fadhili, akamwacha Paulo amefungwa.

MATENDO 25


1 Hata Festo alipokwisha kuingia katika uliwali, baada ya siku tatu akapanda kwenda Yerusalemu kutoka Kaisaria.
2 Kuhani Mkuu na wakuu wa Wayahudi wakampasha habari za Paulo, wakamsihi,
3 na kumwomba fadhili juu yake, kwamba atoe amri aletwe Yerusalemu, wapate kumwotea na kumwua njiani.
4 Lakini Festo akajibu ya kwamba Paulo analindwa Kaisaria; naye mwenyewe yu tayari kwenda huko karibu.
5 Akasema, Wale walio na mamlaka kwenu na watelemke pamoja nami wakamshitaki, ikiwa liko neno baya katika mtu huyu.
6 Alipokwisha kukaa kwao siku nane au kumi si zaidi, akatelemkia Kaisaria; hata siku ya pili akaketi katika kiti cha hukumu akaamuru Paulo aletwe.
7 Alipokuja, wale Wayahudi walioshuka kutoka Yerusalemu wakasimama karibu yake wakaleta mashitaka mengi mazito juu yake, wasiyoweza kuyayakinisha.
8 Paulo akasema akijitetea, Mimi sikukosa neno juu ya sheria ya Wayahudi, wala juu ya hekalu, wala juu ya Kaisari.
9 Lakini Festo akitaka kujipendekeza kwa Wayahudi akamjibu Paulo, akisema, Je! Wataka kwenda Yerusalemu, ukahukumiwe huko mbele yangu kwa ajili ya mambo hayo?
10 Paulo akasema, Mimi ninasimama hapa mbele ya kiti cha hukumu cha Kaisari, ndipo panipasapo kuhukumiwa; sikuwakosa Wayahudi neno, kama wewe ujuavyo sana.
11 Basi ikiwa ni mkosa au nimetenda neno la kustahili kufa, sikatai kufa; bali, kama si kweli neno hili wanalonishitaki, hapana awezaye kunitia mikononi mwao. Nataka rufani kwa Kaisari.
12 Basi Festo alipokwisha kusema na watu wa baraza, akajibu, Umetaka rufani kwa Kaisari! Basi, utakwenda kwa Kaisari.
13 Siku kadha wa kadha zilipokwisha kupita, Agripa mfalme na Bernike wakafika Kaisaria, wakimwamkia Festo.
14 Na walipokuwa wakikaa huko siku nyingi, Festo akamweleza mfalme habari za Paulo, akisema, Yupo hapa mtu mmoja aliyeachwa na Feliki kifungoni;
15 ambaye nilipokuwa Yerusalemu wakuu wa makuhani na wazee wa Wayahudi wakaniarifu habari zake, wakinitaka hukumu juu yake.
16 Nikawajibu kwamba si desturi ya Warumi kumtoa mtu awaye yote, kabla mtu yule aliyeshitakiwa hajaonana na washitaki wake uso kwa uso, na kupewa nafasi ya kujitetea katika mashitaka yake.
17 Basi walipokutanika hapa sikukawia; bali siku ya pili nikaketi katika kiti cha hukumu nikaamuru mtu huyo aletwe.
18 Na wale waliomshitaki waliposimama hawakuleta neno lo lote baya, kama nilivyodhani,
19 bali walikuwa na maswali mengine mengine juu yake katika dini yao wenyewe, na katika habari ya mtu mmoja Yesu, aliyekuwa amekwisha kufa, ambaye Paulo alikaza kusema kwamba yu hai.
20 Nami nikaona shaka jinsi ya kutafuta hakika ya habari hii, nikamwuliza kama anataka kwenda Yerusalemu ahukumiwe huko katika mambo haya.
21 Lakini Paulo alipodai kuwekwa ahukumiwe na Kaisari, nikaamuru alindwe hata nitakapompeleka kwa Kaisari.
22 Agripa akamwambia Festo, Mimi nami nalikuwa nikitaka kumsikia mtu huyu. Akasema, Utamsikia kesho.
23 Hata asubuhi Agripa akaja pamoja na Bernike kwa fahari nyingi, wakaingia mahali pa kusikia maneno, pamoja na maakida wakuu na watu wakuu wa mji; Festo akatoa amri, Paulo akaletwa.
24 Festo akasema, Mfalme Agripa, na ninyi nyote mliopo hapa pamoja nasi, mnamwona mtu huyu, ambaye jamii yote ya Wayahudi huko Yerusalemu na hapa pia wamenitaka niwasaidie, wakipiga kelele kwamba haimpasi kuishi zaidi.
25 Lakini mimi naliona kwamba hakutenda neno la kustahili kuuawa, na yeye mwenyewe alipotaka kuhukumiwa na Kaisari, nalikusudia kumpeleka kwake.
26 Nami katika habari yake sina neno la hakika la kumwandikia bwana. Kwa hiyo nimemleta hapa mbele yenu, hasa mbele yako wewe, mfalme Agripa, ili akiisha kuulizwa-ulizwa nipate neno la kuandika.
27 Kwa maana naona ni neno lisilo maana kumpeleka mfungwa, bila kuonyesha mashitaka yale aliyoshitakiwa.

MATENDO 26


1 Agripa akamwambia Paulo, Una ruhusa kusema maneno yako. Ndipo Paulo akanyosha mkono wake, akajitetea,
2 Najiona nafsi yangu kuwa na heri, Ee mfalme Agripa, kwa kuwa nitajitetea mbele yako leo, katika mambo yale yote niliyoshitakiwa na Wayahudi.
3 Hasa kwa sababu wewe unajua sana desturi na maswali yote waliyo nayo Wayahudi; kwa sababu hiyo nakuomba unisikilize kwa uvumilivu.
4 Kwa maana Wayahudi wote wanajua maisha yangu tangu ujana, yaliyokuwa tangu mwanzo katika taifa langu huko Yerusalemu,
5 wakinijua sana tangu mwanzo, kama wakipenda kushuhudia, ya kwamba nalikuwa Farisayo kwa kuifuata madhehebu ya dini yetu iliyo sahihi kabisa.
6 Na sasa ninasimama hapa nihukumiwe kwa ajili ya tumaini la ahadi baba zetu waliyopewa na Mungu,
7 ambayo kabila zetu kumi na mbili wanataraji kuifikia, wakimwabudu Mungu kwa bidii mchana na usiku. Nami ninashitakiwa na Wayahudi kwa ajili ya tumaini hilo, Ee Mfalme.
8 Kwa nini limedhaniwa kwenu kuwa ni neno lisilosadikika, kwamba Mungu awafufua wafu?
9 Kweli, mimi mwenyewe naliona ndani ya nafsi yangu kwamba yanipasa kutenda mambo mengi yaliyopingamana na jina lake Yesu Mnazareti;
10 nami nikayafanya hayo Yerusalemu; niliwafunga wengi miongoni mwa watakatifu ndani ya magereza, nikiisha kupewa amri na wakuu wa makuhani; na walipouawa nalitoa idhini yangu.
11 Na mara nyingi katika masinagogi yote naliwaadhibu, nikawashurutisha kukufuru; nikawaonea hasira kama mwenye wazimu, nikawaudhi hata katika miji ya ugenini.
12 Basi katika kazi hiyo nilipokuwa nikienda Dameski, mwenye mamlaka na maagizo ya wakuu wa makuhani;
13 Ee Mfalme, ndipo wakati wa adhuhuri njiani naliona nuru inatoka mbinguni ipitayo mwangaza wa jua, ikinimulikia mimi, na wale waliofuatana nami pande zote.
14 Tukaanguka nchi sote, nikasikia sauti ikisema nami kwa lugha ya kiebrania, Sauli! Sauli! Mbona waniudhi? Ni vigumu kwako kuupiga mateke mchokoo.
15 Nami nikasema, Wewe u nani, Bwana? Bwana akaniambia, Mimi ni Yesu, ambaye wewe unaniudhi.
16 Lakini inuka, usimame kwa miguu yako, maana nimekutokea kwa sababu hii, nikuweke wewe uwe mtumishi na shahidi wa mambo haya uliyoyaona, na wa mambo ambayo katika hayo nitajidhihirisha kwako;
17 nikikuokoa na watu wako, na watu wa Mataifa, ambao nakutuma kwao;
18 uwafumbue macho yao, na kuwageuza waiache giza na kuielekea nuru, waziache na nguvu za Shetani na kumwelekea Mungu; kisha wapate msamaha wa dhambi zao, na urithi miongoni mwao waliotakaswa kwa imani iliyo kwangu mimi.
19 Kwa hiyo, Ee Mfalme Agripa, sikuyaasi yale maono ya mbinguni,
20 bali kwanza niliwahubiri wale wa Dameski na Yerusalemu, na katika nchi yote ya Uyahudi, na watu wa Mataifa, kwamba watubu na kumwelekea Mungu, wakiyatenda matendo yanayopatana na kutubu kwao.
21 Kwa sababu ya hayo Wayahudi wakanikamata ndani ya hekalu wakajaribu kuniua.
22 Basi kwa kuwa nimeupata msaada utokao kwa Mungu nimesimama hata leo hivi nikiwashuhudia wadogo kwa wakubwa, wala sisemi neno ila yale ambayo manabii na Musa waliyasema, kwamba yatakuwa;
23 ya kwamba Kristo hana budi kuteswa na ya kwamba yeye kwanza kwa kufufuliwa katika wafu atatangaza habari za nuru kwa watu wake na kwa watu wa Mataifa.
24 Alipokuwa akijitetea hivi, Festo akasema kwa sauti kuu, Paulo, una wazimu, kusoma kwako kwingi kumekugeuza akili.
25 Lakini Paulo akasema, Sina wazimu, Ee Festo mtukufu, bali nanena maneno ya kweli na ya akili kamili.
26 Kwa maana mfalme anajua habari za mambo haya, nami naweza kusema naye kwa ujasiri, kwa sababu najua sana ya kuwa hapana neno moja katika hayo asilolijua; kwa maana jambo hilo halikutendeka pembeni.
27 Mfalme Agripa, je! Wawaamini manabii? Najua ya kuwa wawaamini.
28 Agripa akamwambia Paulo, Kwa maneno machache wadhani kunifanya mimi kuwa Mkristo.
29 Paulo akamjibu, Namwomba Mungu kwamba, ikiwa kwa machache au ikiwa kwa mengi, si wewe tu ila na hao wote wanaonisikia leo wawe kama mimi, isipokuwa vifungo hivi.
30 Mfalme na liwali na Bernike na wale walioketi pamoja nao wakasimama;
31 hata walipoondoka wakasemezana, wakisema, Mtu huyu hatendi neno linalostahili kifo wala kufungwa.
32 Agripa akamwambia Festo, Mtu huyo angeweza kufunguliwa, kama asingalitaka rufani kwa Kaisari.

MATENDO 27


1 Basi ilipoamriwa tuabiri hata Italia, wakamtia Paulo na wafungwa wengine katika mikono ya akida mmoja, jina lake Yulio, wa kikosi cha Augusto.
2 Tukapanda katika merikebu ya Adramitio iliyokuwa tayari kusafiri mpaka miji ya pwani za Asia, tukatweka; Aristarko, Mmakedonia wa Thesalonike, akiwa pamoja nasi.
3 Siku ya pili tukawasili Sidoni; Yulio akamfadhili sana Paulo akampa ruhusa kwenda kwa rafiki zake, apate kutunzwa.
4 Kutoka huko tukatweka, tukasafiri chini ya Kipro ili kuukinga upepo, kwa maana pepo zilikuwa za mbisho.
5 Tulipopita bahari ya upande wa Kilikia na Pamfilia, tukafika Mira, mji wa Likia.
6 Na huko yule akida akakuta merikebu ya Iskanderia, tayari kusafiri kwenda Italia, akatupandisha humo.
7 Tukasafiri polepole kwa muda wa siku nyingi, tukafika mpaka Nido kwa shida; na kwa sababu upepo ulikuwa ukituzuia tukapita chini ya Krete, tukaikabili Salmone.
8 Tukaipita kwa shida, pwani kwa pwani, tukafika mahali paitwapo Bandari Nzuri. Karibu na hapo pana mji uitwao Lasea.
9 Na wakati mwingi ulipokwisha kupita, na safari ikiwa ina hatari sasa, kwa sababu siku za kufunga zilikuwa zimekwisha kupita, Paulo akawaonya,
10 akawaambia, Wanaume, naona kwamba safari hii itakuwa na madhara na hasara nyingi, si ya shehena na merikebu tu, ila na ya maisha yetu pia.
11 Lakini yule akida akawasikiliza nahodha na mwenye merikebu zaidi ya yale aliyoyasema Paulo.
12 Na kwa sababu bandari ile ilikuwa haifai kukaa wakati wa baridi, wengi wao wakatoa shauri la kutweka kutoka huko ili wapate kufika Foinike, kama ikiwezekana, na kukaa huko wakati wa baridi; nayo ni bandari ya Krete, inaelekea kaskazini-mashariki na kusini-mashariki.
13 Na upepo wa kusi ulipoanza kuvuma kidogo, wakidhani ya kuwa wamepata waliyoazimu kupata, wakang'oa nanga, wakasafiri karibu na Krete pwani kwa pwani.
14 Baada ya muda mchache ukavuma upepo wa nguvu wa namna ya tufani, uitwao Eurakilo,
15 merikebu iliposhikwa, na kutoweza kushindana na upepo, tukaiacha tukachukuliwa.
16 Na tukipita upesi karibu na kisiwa kidogo kiitwacho Kauda tukadiriki kuikweza mashua; lakini kwa shida.
17 Walipokwisha kuikweza wakatumia misaada, wakaikaza merikebu kwa kupitisha kamba chini yake, nao wakiogopa wasije wakakwama katika fungu liitwalo Sirti, wakatua matanga wakachukuliwa vivi hivi.
18 Na kwa maana tulikuwa tukipigwa sana na ile tufani, siku ya pili yake wakaanza kuitupa shehena baharini.
19 Siku ya tatu wakatupa vyombo vya merikebu kwa mikono yao wenyewe.
20 Jua wala nyota hazikuonekana kwa muda wa siku nyingi, na tufani kuu ikatushika, basi tukakata tamaa ya kuokoka.
21 Na walipokuwa wamekaa wakati mwingi bila kula chakula, Paulo akasimama katikati yao, akasema, Wanaume, iliwapasa kunisikiliza mimi na kutokung'oa nanga huko Krete, na kupata madhara haya na hasara hii.
22 Sasa nawapeni shauri, iweni na moyo mkuu, kwa maana hapana hata nafsi mmoja miongoni mwenu atakayepotea, ila merikebu tu.
23 Kwa maana usiku huu wa leo malaika wa Mungu yule ambaye mimi ni wake, naye ndiye nimwabuduye, alisimama karibu nami,
24 akaniambia, Usiogope, Paulo, huna budi kusimama mbele ya Kaisari; tena, tazama, Mungu amekupa watu wote wanaosafiri pamoja nawe.
25 Basi, wanaume, changamkeni; kwa sababu namwamini Mungu, ya kwamba yatakuwa vile vile kama nilivyoambiwa.
26 Lakini hatuna budi kupwelewa katika kisiwa kimoja.
27 Hata usiku wa kumi na nne ulipofika, tulipokuwa tukichukuliwa huko na huko katika bahari ya Adria, kama usiku wa manane baharia wakadhani ya kuwa wanaikaribia nchi kavu.
28 Wakatupa bildi wakapata pima ishirini, wakaendelea kidogo wakatupa bildi tena, wakapata pima kumi na tano.
29 Wakachelea tusije tukapwelewa mahali penye miamba, wakatupa nanga nne za tezi, wakaomba kuche.
30 Na baharia walipotaka kukimbia na kuiacha merikebu, wakiishusha mashua baharini kana kwamba wanataka kutupa nanga za omo,
31 Paulo akawaambia akida na askari, Hawa wasipokaa ndani ya merikebu hamtaweza kuokoka.
32 Basi askari wakazikata kamba za mashua, wakaiacha ianguke.
33 Na kulipokuwa kukipambauka Paulo akawasihi wote wale chakula, akisema, Leo ni siku ya kumi na nne kungoja na kufunga, hamkula kitu cho chote.
34 Basi nawasihi mle chakula, maana itakuwa kwa wokovu wenu; kwa maana hapana hata unywele wa kichwa cha mmoja wenu utakaopotea.
35 Alipokwisha kusema hayo akatwaa mkate, akamshukuru Mungu mbele yao wote akaumega akaanza kula.
36 Ndipo wakachangamka wote, wakala chakula wenyewe.
37 Na sisi tuliokuwa ndani ya merikebu tulipata watu mia mbili na sabini na sita.
38 Walipokwisha kushiba wakaipunguza shehena ya merikebu, wakiitupa ngano baharini.
39 Kulipokucha hawakuitambua ile nchi, ila waliona hori yenye ufuo, wakashauriana kuiegesha merikebu huko, kama ikiwezekana.
40 Wakazitupilia mbali zile nanga, na kuziacha baharini, pamoja na kuzilegeza kamba za sukani, wakalitweka tanga dogo ili liushike upepo, wakauendea ule ufuo.
41 Lakini wakafikia mahali palipokutana bahari mbili, wakaiegesha merikebu, omo ikakwama ikakaa isitikiswe, bali tezi ilikuwa imefumuliwa kwa nguvu za mawimbi.
42 Shauri la askari lilikuwa kuwaua wafungwa, mtu asiogelee na kukimbia.
43 Bali akida, akitaka kumponya Paulo, akawazuia, wasifanye kama walivyokusudia, akawaamuru wale wawezao kuogelea wajitupe kwanza baharini, wafike nchi kavu;
44 nao waliosalia, hawa juu ya mbao na hawa juu ya vitu vingine vya merikebu. Na hivyo watu wote wakapata kuifikilia nchi kavu salama.

MATENDO 28


1 Tulipokwisha kuokoka, ndipo tulipojua ya kuwa kisiwa kile chaitwa Melita.
2 Wenyeji wakatufanyia fadhili zisizokuwa za kawaida. Kwa maana waliwasha moto, wakatukaribisha sote, kwa sababu ya mvua iliyonyesha na kwa sababu ya baridi.
3 Paulo alipokuwa amekusanya mzigo wa kuni, na kuuweka motoni, nyoka akatoka kwa ajili ya ule moto akamzonga-zonga mkononi.
4 Wenyeji walipomwona yule nyoka akilewa-lewa mkononi, wakaambiana, Hakosi mtu huyu ni mwuaji; ambaye ijapokuwa ameokoka katika bahari haki haimwachi kuishi.
5 Lakini yeye akamtukusia motoni asipate madhara.
6 Wao wakadhani ya kuwa atavimba au kuanguka chini kwa kufa ghafula; na wakiisha kumwangalia sana, na kuona kwamba halimpati dhara lo lote, wakageuka, wakasema kwamba yeye ni mungu.
7 Karibu na mahali pale palikuwa na mashamba ya mkuu wa kisiwa, jina lake Publio; mtu huyu akatukaribisha kwa moyo wa urafiki, akatufanya wageni wake kwa muda wa siku tatu.
8 Ikawa babaake Publio alikuwa hawezi homa na kuhara damu. Paulo akaingia kwake, akaomba, akaweka mikono yake juu yake, na kumpoza.
9 Yalipokwisha kutendeka hayo wengine waliokuwa na magonjwa katika kisiwa wakaja wakapozwa;
10 nao wakatuheshimu kwa heshima nyingi; basi tulipoabiri wakatupakilia vitu vile tulivyokuwa na haja navyo.
11 Baada ya miezi mitatu tukasafiri katika merikebu ya Iskanderia iliyokuwa imekaa pale kisiwani wakati wa baridi; na alama yake ni Ndugu Pacha.
12 Tukafika Sirakusa, tukakaa siku tatu.
13 Kutoka huko tukazunguka tukafikia Regio; baada ya siku moja upepo wa kusi ukavuma, na siku ya pili tukawasili Puteoli.
14 Huko tukakuta ndugu, wakatusihi tukae nao siku saba; na hivi tukafika Rumi.
15 Na kutoka huko ndugu, waliposikia habari zetu, wakaja kutulaki mpaka Soko la Apio na Mikahawa Mitatu. Paulo alipowaona alimshukuru Mungu, akachangamka.
16 Tulipoingia Rumi Paulo alipewa ruhusa kukaa kwake mwenyewe pamoja na askari aliyemlinda.
17 Ikawa baada ya siku tatu akawaita wakuu wa Wayahudi wakutane, hata walipokutanika akawaambia, Ndugu zangu, ningawa sikufanya neno kinyume cha watu wetu wala neno lililopingamana na desturi za baba zetu, nalitiwa katika mikono ya Warumi, hali nimefungwa, tokea Yerusalemu.
18 Na hao walipokwisha kuniuliza-uliza walitaka kunifungua, kwa maana hapakuwa na sababu yo yote kwangu ya kuuawa.
19 Lakini Wayahudi walipotoa hoja juu ya shauri hili nalishurutishwa kutaka rufani kwa Kaisari. Si kwamba nalikuwa na neno la kuwashitaki watu wa taifa langu.
20 Basi kwa ajili ya hayo, nimewaita mje kunitazama na kusema nami; kwa maana nimefungwa kwa mnyororo huu kwa ajili ya tumaini la Israeli.
21 Wale wakamwambia, Sisi hatukupata nyaraka zenye habari zako kutoka Uyahudi, wala hapana ndugu hata mmoja aliyefika hapa na kutupasha habari, au kunena neno baya juu yako.
22 Lakini tunataka kusikia kwako uonavyo wewe; kwa maana katika habari za madhehebu hiyo imejulikana kwetu kwamba inanenwa vibaya kila mahali.
23 Wakiisha kuagana naye siku, wakamjia katika nyumba aliyokaa, watu wengi sana, akawaeleza kwa taratibu na kuushuhudia ufalme wa Mungu, akiwaonya mambo yake Yesu, kwa maneno ya sheria ya Musa na ya manabii, tangu asubuhi hata jioni.
24 Wengine waliamini yale yaliyonenwa, wengine hawakuyaamini.
25 Na walipokuwa hawapatani wao kwa wao, wakaenda zao, Paulo alipokwisha kusema neno hili moja, ya kwamba, Roho Mtakatifu alinena vema na baba zetu, kwa kinywa cha nabii Isaya,
26 akisema, Enenda kwa watu hawa, ukawaambie, Kusikia, mtasikia wala hamtafahamu; Na kuona, mtaona wala hamtatambua;
27 Kwa maana mioyo ya watu hawa imepumbaa, Na masikio yao ni mazito ya kusikia, Na macho yao wameyafumba; Wasije wakaona kwa macho yao, Na kusikia kwa masikio yao, Na kufahamu kwa mioyo yao, Na kubadili nia zao, nikawaponya.
28 Basi ijulikane kwenu ya kwamba wokovu huu wa Mungu umepelekwa kwa Mataifa, nao watasikia!
29 Alipokwisha kusema hayo, Wayahudi wakaenda zao, wakiulizana mengi wao kwa wao.]
30 Akakaa muda wa miaka miwili mizima katika nyumba yake aliyokuwa ameipanga, akawakaribisha watu wote waliokuwa wakimwendea,
31 akihubiri habari za ufalme wa Mungu, na kuyafundisha mambo ya Bwana Yesu Kristo, kwa ujasiri mwingi, asikatazwe na mtu.