Ezekieli

Sura: 1, 2, 3, 4, 5, 6, 7, 8, 9, 10, 11, 12, 13, 14, 15, 16, 17, 18, 19, 20, 21, 22, 23, 24, 25, 26, 27, 28, 29, 30, 31, 32, 33, 34, 35, 36, 37, 38, 39, 40, 41, 42, 43, 44, 45, 46, 47, 48

Ezekieli 1


1 Ikawa katika mwaka wa thelathini, mwezi wa nne, siku ya tano ya mwezi, nilipokuwa pamoja na watu waliohamishwa, karibu na mto Kebari, mbingu zilifunuka, nikaona maono ya Mungu.
2 Siku ya tano ya mwezi, nao ulikuwa ni mwaka wa tano wa kuhamishwa kwake mfalme Yehoyakini,
3 neno la Bwana lilimjia Ezekielii, kuhani, mwana wa Buzi, kwa dhahiri, katika nchi ya Wakaldayo, karibu na mto Kebari; na mkono wa Bwana ulikuwa hapo juu yake.
4 Nikaona, na tazama, upepo wa dhoruba ulitoka upande wa kaskazini, wingu kubwa sana, pamoja na moto, ukifanya duara ya nuru, na mwangaza pande zote, na katikati yake kitu kama rangi ya kaharabu, katikati ya moto huo.
5 Kukatokea katikati yake mfano wa viumbe hai vinne. Kuonekana kwao kulikuwa hivi; walikuwa na sura ya mwanadamu.
6 Na kila mmoja alikuwa na nyuso nne, na kila mmoja alikuwa na mabawa manne.
7 Na miguu yao ilikuwa miguu iliyonyoka; na nyayo za miguu yao zilikuwa kama nyayo za miguu ya ndama; zikimetameta kama rangi ya shaba iliyosuguliwa sana.
8 Nao walikuwa na mikono ya mwanadamu chini ya mabawa yao, pande zote nne; na wote wanne walikuwa na nyuso zao na mabawa yao hivi;
9 mabawa yao yaliungana, hili na hili; nao hawakugeuka walipokwenda, walikwenda kila mmoja kuelekea mbele.
10 Kwa habari za mfano wa nyuso zao; walikuwa na uso wa mwanadamu; na hao wanne walikuwa na uso wa simba upande wa kuume; na hao wanne walikuwa na uso wa ng'ombe upande wa kushoto; na hao wanne walikuwa na uso wa tai pia.
11 Na nyuso zao na mabawa yao yalikuwa yametengana kwa juu; mabawa mawili ya kila mmoja yaliungana, hili na hili, na mawili yalifunika miili yao.
12 Nao walikwenda kuelekea mbele, kila mmoja wao; roho ilikotaka kwenda ndiko walikokwenda; hawakugeuka walipokwenda.
13 Kwa habari za kuonekana kwao vile viumbe hai; kuonekana kwao kulikuwa kama makaa ya moto yawakayo, kama kuonekana kwa vinga vya moto; moto ule ulikuwa ukienda juu na kushuka chini, katikati ya vile viumbe hai; na ule moto ulikuwa na mwangaza mwingi, na katika ule moto ulitoka umeme.
14 Na vile viumbe hai walipiga mbio, kwenda na kurudi, kama kuonekana kwa kumulika kwa umeme.
15 Basi, nilipokuwa nikivitazama vile viumbe hai, tazama, gurudumu moja juu ya nchi, karibu na kila kimoja cha vile viumbe hai, pande zake zote nne.
16 Kuonekana kwake magurudumu hayo na kazi yake kulikuwa kama rangi ya zabarajadi; nayo yote manne yalikuwa na mfano mmoja; na kuonekana kwake na kazi yake kulikuwa kana kwamba ni gurudumu ndani ya gurudumu lingine.
17 Yalipokwenda yalikwenda pande zote nne; hayakugeuka yalipokwenda.
18 Katika habari za vivimbe vyake; vilikuwa virefu, vya kutisha; nayo yote manne, vivimbe vyake vimejaa macho pande zote.
19 Na viumbe hao walipokwenda, magurudumu yalikwenda kandokando yao, na viumbe hao walipoinuliwa, magurudumu nayo yaliinuliwa.
20 Kila mahali ambako roho hiyo ilitaka kwenda, walikwenda; walikuwa na roho ya kwenda huko; nayo magurudumu yaliinuliwa karibu nao; kwa maana roho ya viumbe hai ilikuwa ndani ya magurudumu.
21 Walipokwenda hao, yalikwenda hayo nayo; na waliposimama hao, yalisimama hayo nayo; na walipoinuliwa hao juu ya nchi, magurudumu yaliinuliwa karibu nao; maana roho ya viumbe hai ilikuwa ndani ya magurudumu.
22 Tena juu ya vichwa vya viumbe hai palikuwa na kitu mfano wa anga, kama rangi ya bilauri, lenye kutisha, limetandwa juu ya vichwa vyao.
23 Na chini ya anga mabawa yao yamenyoshwa, moja kulielekea la pili; kila mmoja alikuwa na mawili yaliyowafunika miili yao upande mmoja, na kila mmoja alikuwa na mawili yaliyowafunika miili yao upande wa pili.
24 Nao walipokwenda nalisikia mshindo wa mabawa yao, kama mshindo wa maji makuu, kama sauti yake Mwenyezi, mshindo wa mvumo, kama mshindo wa jeshi; hapo waliposimama walishusha mabawa yao.
25 Tena palikuwa na sauti juu ya anga lile, lililokuwa juu ya vichwa vyao; hapo waliposimama walishusha mabawa yao.
26 Na juu ya anga, lililokuwa juu ya vichwa vyao, palikuwa na mfano wa kiti cha enzi, kuonekana kwake kama yakuti samawi; na juu ya mfano huo wa kiti cha enzi, ulikuwako mfano kama kuonekana kwa mfano wa mwanadamu juu yake.
27 Nikaona kana kwamba ni rangi ya kaharabu, kama kuonekana kwa moto ndani yake pande zote, tangu kuonekana kwa viuno vyake na juu; na tangu kuonekana kwa viuno vyake na chini, naliona kana kwamba ni kuonekana kwa moto; tena palikuwa na mwangaza pande zake zote.
28 Kama kuonekana kwa upinde wa mvua, ulio katika mawingu siku ya mvua, ndivyo kulivyokuwa kuonekana kwa mwangaza ule pande zote. Ndivyo kulivyokuwa kuonekana kwake mfano huo wa utukufu wa Bwana. Nami nilipoona nalianguka kifudifudi, nikasikia sauti ya mmoja anenaye.

Ezekieli 2


1 Akaniambia, Mwanadamu, simama kwa miguu yako, nami nitasema nawe.
2 Naye aliposema nami, roho ikaniingia, ikanisimamisha; nikamsikia yeye aliyesema nami.
3 Akaniambia, Mwanadamu, nakutuma kwa wana wa Israeli, kwa mataifa wanaoasi, walioniasi mimi; wao na baba zao wamekosa juu yangu, naam, hata hivi leo.
4 Na wana hao wana nyuso zisizo na haya, na mioyo yao ni migumu. Mimi nakutuma kwa hao; nawe utawaambia, Bwana MUNGU asema hivi.
5 Nao, kwamba watasikia, au kwamba hawataki kusikia, (maana ndio nyumba ya kuasi hao), hata hivyo watajua ya kuwa nabii amekuwako miongoni mwao.
6 Na wewe, mwanadamu, usiwaogope hao, wala usiyaogope maneno yao, ijapokuwa miiba na michongoma i pamoja nawe, nawe unakaa katikati ya nge; usiyaogope maneno yao, wala usifadhaike kwa sababu ya nyuso zao, wajapokuwa ni nyumba yenye kuasi.
7 Nawe utawaambia maneno yangu, kwamba watasikia, au kwamba hawataki kusikia; maana hao wanaasi sana.
8 Bali wewe, mwanadamu, sikia neno hili ninalokuambia; usiwe wewe mwenye kuasi kama nyumba ile yenye kuasi; funua kinywa chako, ule nikupacho.
9 Nami nilipotazama, mkono ulinyoshwa kunielekea; na tazama, gombo la chuo lilikuwa ndani yake.
10 Akalikunjua mbele yangu; nalo lilikuwa limeandikwa ndani na nje; ndani yake yalikuwa yameandikwa maombolezo, na vilio, na ole!

Ezekieli 3


1 Akaniambia, Mwanadamu, kula uonacho; kula gombo hili, kisha enenda ukaseme na wana wa Israeli.
2 Basi nikafunua kinywa changu, naye akanilisha lile gombo.
3 Akaniambia, Mwanadamu, lisha tumbo lako, ulijaze tumbo lako kwa hili gombo nikupalo. Ndipo nikalila, nalo kinywani mwangu lilikuwa tamu, kama utamu wa asali.
4 Akaniambia, Mwanadamu, haya! Waendee wana wa Israeli ukawaambie maneno yangu.
5 Maana wewe hukutumwa kwa watu wa maneno mageni, ama wa lugha ngumu, bali kwa nyumba ya Israeli;
6 si kwa watu wa kabila nyingi wenye maneno mageni, na lugha ngumu, ambao huwezi kufahamu maneno yao. Bila shaka, kama ningekutuma kwa watu hao, wangekusikiliza.
7 Bali nyumba ya Israeli hawatakusikiliza wewe; kwa kuwa hawanisikilizi mimi; maana nyumba yote ya Israeli wana vipaji vigumu, na mioyo yenye ukaidi.
8 Tazama, nimeufanya uso wako kuwa mgumu juu ya nyuso zao, na kipaji cha uso chako kuwa kigumu juu ya vipaji vya nyuso vyao.
9 Kama almasi ilivyo ngumu kuliko gumegume, ndivyo nilivyokifanya kipaji chako; usiwaogope, wala usifadhaike kwa sababu ya nyuso zao, wajapokuwa ni nyumba ya kuasi.
10 Tena akaniambia, Mwanadamu, maneno yangu yote nitakayokuambia, yapokee moyoni mwako, na kuyasikia kwa masikio yako.
11 Haya! Enenda uwafikilie watu hao waliohamishwa, kwa wana wa watu wako, ukaseme nao, na kuwaambia, Bwana MUNGU asema hivi; kwamba watasikia, au kwamba hawataki kusikia.
12 Ndipo roho ikaniinua, nami nikasikia nyuma yangu sauti kama mshindo wa radi kuu, ikisema, Na uhimidiwe utukufu wa Bwana tokea mahali pake.
13 Nikasikia mshindo wa mabawa ya vile viumbe hai, walipogusana, na mshindo wa yale magurudumu kando yao, mshindo wa radi kuu.
14 Basi roho ikaniinua, ikanichukua mahali pengine; nami nikaenda kwa uchungu, na hasira kali rohoni mwangu, na mkono wa Bwana ulikuwa juu yangu kwa nguvu.
15 Ndipo nikawafikia watu waliohamishwa, huko Tel-abibu, waliokuwa wakikaa karibu na mto Kebari, nikafika huko walikokuwa wakikaa; nikaketi huko miongoni mwao muda wa siku saba, katika hali ya ushangao mwingi.
16 Hata ikawa, mwisho wa siku saba, neno la Bwana likanijia, kusema,
17 Mwanadamu, nimekuweka kuwa mlinzi wa nyumba ya Israeli; basi, sikia neno hili litokalo katika kinywa changu, ukawape maonyo haya yatokayo kwangu.
18 Nimwambiapo mtu mbaya, Hakika utakufa; wewe usimpe maonyo, wala husemi na huyo mtu mbaya ili kumwonya, kusudi aache njia yake mbaya na kujiokoa roho yake; mtu yule mbaya atakufa katika uovu wake; lakini damu yake nitaitaka mkononi mwako.
19 Lakini ukimwonya mtu mbaya, wala yeye hauachi ubaya wake, wala njia yake mbaya, atakufa katika uovu wake; bali wewe umejiokoa roho yako.
20 Tena mtu mwenye haki aiachapo haki yake, na kutenda uovu, nami nikiweka kikwazo mbele yake, atakufa; kwa sababu hukumwonya, atakufa katika uovu wake, wala matendo yake ya haki aliyoyatenda hayatakumbukwa; lakini damu yake nitaitaka mkononi mwako.
21 Bali ukimwonya mwenye haki, kwamba yule mwenye haki asitende dhambi, tena ikiwa yeye hatendi dhambi, hakika ataishi, kwa sababu alikubali kuonywa; nawe umejiokoa roho yako.
22 Na mkono wa Bwana ulikuwako juu yangu huko; akaniambia, Ondoka, enenda uwandani; nami nitasema nawe huko.
23 Basi, nikaondoka, nikaenda uwandani, na tazama, utukufu wa Bwana ulisimama huko, kama utukufu ule niliouona karibu na mto Kebari; nami nikaanguka kifudifudi.
24 Ndipo roho ile ikaniingia, ikanisimamisha kwa miguu yangu; akasema nami, akaniambia, Enenda ukajifungie nyumbani mwako.
25 Lakini wewe, mwanadamu, tazama, watakutia pingu, nao watakufunga kwazo, wala hutakwenda nje kati yao;
26 nami nitaufanya ulimi wako ugandamane na kaakaa lako, hata utakuwa bubu, wala hutakuwa mwonyaji kwao; kwa kuwa wao ni nyumba yenye kuasi.
27 Lakini hapo nitakaposema nawe, nitafumbua kinywa chako, nawe utawaambia, Bwana MUNGU asema hivi. Yeye asikiaye na asikie; naye akataaye na akatae; maana wao ni nyumba yenye kuasi.

Ezekieli 4


1 Wewe nawe, mwanadamu, jipatie tofali uliweke mbele yako, kisha, chora juu yake mfano wa mji, yaani, Yerusalemu;
2 ukauhusuru, ukajenge ngome juu yake, na kufanya boma juu yake; ukaweke makambi juu yake, na kuweka magogo ya kuubomoa yauzunguke pande zote.
3 Kisha ukajipatie bamba la chuma, ukalisimamishe liwe ukuta wa chuma kati ya wewe na mji huo; ukaelekeze uso wako juu yake, nao utahusuriwa, nawe utauhusuru. Hili litakuwa ishara kwa nyumba ya Israeli.
4 Tena lala chini kwa ubavu wako wa kushoto, ukaweke huo uovu wa nyumba ya Israeli juu yake; kwa kadiri ya hesabu ya siku utakazolala juu yake, kwa kadiri hiyo utauchukua uovu wao.
5 Maana nimekuagizia miaka ya uovu wao iwe kwako hesabu ya siku, yaani, siku mia tatu na tisini; ndivyo utakavyouchukua uovu wa nyumba ya Israeli.
6 Tena utakapozitimiza hizo, utalala kwa ubavu wako wa kuume, nawe utauchukua uovu wa nyumba ya Yuda; siku arobaini, siku moja kwa mwaka mmoja, nimekuagizia.
7 Nawe utauelekeza uso wako, uelekee mazingiwa ya Yerusalemu, na mkono wako utakuwa haukuvikwa nguo, nawe utatoa unabii juu yake.
8 Na tazama, nitakutia pingu, wala hutageuka toka upande mmoja hata upande wa pili, hata utakapozitimiza siku za mazingiwa yako.
9 Pia ujipatie ngano, na shayiri, na kunde, na dengu, na mtama, na kusemethi, ukavitie vyote katika chombo kimoja, ukajifanyie mkate kwa vitu hivyo; kwa kadiri ya hesabu ya siku utakazolala ubavuni mwako; yaani, siku mia tatu na tisini utaula.
10 Na chakula chako utakachokula kitapimwa, shekeli ishirini kwa siku moja; utakila kwa wakati wake.
11 Nawe utakunywa maji kwa kuyapima, sehemu ya sita ya hini; utayanywa kwa wakati wake.
12 Nawe utakila kama mkate wa shayiri, nawe utakioka mbele ya macho yao juu ya mashonde yatokayo katika mwanadamu.
13 Bwana akasema, Hivyo ndivyo wana wa Israeli watakavyokula chakula chao, hali kimetiwa unajisi, kati ya mataifa nitakakowafukuza.
14 Ndipo nikasema, Ee Bwana MUNGU, tazama, roho yangu haikutiwa unajisi; maana tangu ujana wangu hata sasa sijala nyamafu, wala iliyoraruliwa na hayawani; wala nyama ichukizayo haikuingia kinywani mwangu.
15 Ndipo akaniambia, Tazama, nimekupa mashonde ya ng'ombe badala ya mashonde ya mwanadamu, nawe utakipika chakula chako juu ya hayo.
16 Tena akaniambia, Mwanadamu, tazama, nitalivunja tegemeo la chakula katika Yerusalemu; nao watakula mkate kwa kuupima, na kwa kuutunza sana; nao watakunywa maji kwa kuyapima, na kwa kushangaa;
17 wapate kupungukiwa na mkate na maji, na kustaajabiana, na kukonda kwa sababu ya uovu wao.

Ezekieli 5


1 Nawe, mwanadamu, ujipatie upanga mkali, kama wembe wa kinyozi ujipatie, ukaupitishe juu ya kichwa chako na ndevu zako; kisha ujipatie mizani ya kupimia, ukazigawanye nywele hizo.
2 Theluthi ya hizo utaiteketeza katikati ya mji, siku za mazingiwa zitakapotimia; nawe utatwaa theluthi, na kuipiga kwa upanga pande zote; nawe utatawanya theluthi ichukuliwe na upepo, nami nitafuta upanga nyuma yake.
3 Nawe twaa nywele chache katika hizo, na kuzifunga katika upindo wa mavazi yako.
4 Nawe utatwaa tena baadhi ya hizo, na kuzitupa katikati ya moto, na kuziteketeza katika moto huo; kutoka nywele hizo moto utakuja na kuingia katika nyumba yote ya Israeli.
5 Bwana MUNGU asema hivi; Huu ndio Yerusalemu; nimeuweka kati ya mataifa, na nchi zauzunguka pande zote.
6 Nao umeasi hukumu zangu, kwa kutenda mabaya kuliko mataifa hayo, nao umeasi sheria kuliko nchi hizo ziuzungukazo; maana wamezikataa hukumu zangu, wala hawakuenda katika sheria zangu.
7 Basi, kwa hiyo Bwana MUNGU asema hivi; Kwa sababu ninyi mmefanya ghasia kuliko mataifa wawazungukao ninyi, wala hamkuenda katika sheria zangu, wala hamkuzishika hukumu zangu, wala hamkutenda kama kawaida za mataifa wawazungukao;
8 basi, Bwana MUNGU asema hivi; Angalia, mimi, naam, mimi, ni juu yako; nami nitafanya hukumu kati yako machoni pa mataifa.
9 Nami nitakutenda nisiyoyatenda zamani, wala sitafanya tena mambo kama hayo, kwa sababu ya machukizo yako yote.
10 Kwa sababu hiyo baba za watu watawala wana wao kati yako, nao wana watawala baba zao; nami nitafanya hukumu ndani yako, na hao wote waliosalia kwako nitawatawanya kwa pepo zote.
11 Kwa sababu hiyo, kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, hakika kwa kuwa umepatia unajisi patakatifu pangu, kwa matendo yako yote niyachukiayo, na kwa machukizo yako yote, kwa sababu hiyo mimi nami nitakupunguza; wala jicho langu halitaachilia, wala sitaona huruma.
12 Theluthi yenu mtakufa kwa tauni, na kwa njaa watakomeshwa ndani yako; na theluthi yenu wataanguka kwa upanga pande zako zote; na theluthi yenu nitawatawanya kwa pepo zote, kisha nitafuta upanga nyuma yao.
13 Hivyo ndivyo ghadhabu yangu itakavyotimia, nami nitatosheleza hasira yangu juu yao, nami nitafarijika; nao watajua ya kuwa mimi, Bwana, nimenena kwa wivu wangu, nitakapokuwa nimeitimiza ghadhabu yangu juu yao.
14 Tena nitakufanya kuwa ukiwa, na aibu, kati ya mataifa wakuzungukao, machoni pa watu wote wapitao.
15 Nayo itakuwa tukano na aibu, na mafundisho na ajabu, kwa mataifa wakuzungukao, hapo nitakapotekeleza hukumu ndani yako, kwa hasira, na kwa ghadhabu, na kwa malaumu ya ghadhabu; mimi, Bwana, nimeyanena hayo;
16 hapo nitakapopeleka mishale mibaya ya njaa juu yao, iletayo uharibifu, nitakayoipeleka ili kuwaharibu ninyi; nami nitaiongeza njaa juu yenu, na tegemeo lenu la mkate nitalivunja.
17 Nami nitapeleka juu yenu njaa na wanyama wabaya, nao watakunyang'anya watu wako; na tauni na damu zitapita ndani yako; nami nitauleta upanga juu yako; mimi Bwana, nimeyanena hayo.

Ezekieli 6


1 Neno la Bwana likanijia, kusema,
2 Mwanadamu, uelekeze uso wako uitazame milima ya Israeli, ukaitabirie,
3 ukisema, Enyi milima ya Israeli, lisikieni neno la Bwana MUNGU; Bwana MUNGU aiambia hivi milima na vilima, na vijito na mabonde; Tazama, mimi, naam, mimi, nitaleta upanga juu yenu, nami nitapaharibu mahali penu palipoinuka,
4 Na madhabahu zenu zitakuwa ukiwa, na sanamu zenu za jua zitavunjika; nami nitawatupa wana wenu waliouawa mbele ya vinyago vyenu.
5 Nami nitaiweka mizoga ya wana wa Israeli mbele ya vinyago vyao; nami nitaitawanya mifupa yenu pande zote za madhabahu zenu.
6 Kila mahali mkaapo miji itaharibika, na mahali palipoinuka patakuwa ukiwa; ili madhabahu zenu ziharibiwe, na kufanywa ukiwa, na vinyago vyenu vivunjwe, na kukoma, na sanamu zenu za jua zikatwe, na kuangushwa, na kazi zenu zifutwe kabisa.
7 Na hao waliouawa wataanguka katikati yenu; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.
8 Lakini nitasaza mabaki; maana mtakuwa na baadhi ya watu watakaoukimbia upanga kati ya mataifa, mtakapokuwa mmetawanyika katika nchi za watu.
9 Na hao wa kwenu watakaookoka watanikumbuka kati ya mataifa, watakakochukuliwa mateka, jinsi nilivyoiponda mioyo yao ya kikahaba, iliyoniacha, na macho yao, yaendayo kufanya uasherati na vinyago vyao; nao watajichukia nafsi zao machoni pao wenyewe, kwa sababu ya mabaya yao yote, waliyoyatenda kwa machukizo yao yote.
10 Nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana; sikusema bure kama nitawatenda mabaya hayo.
11 Bwana MUNGU asema hivi; Piga kwa mkono wako, ipige nchi kwa mguu wako, ukaseme, Ole! Kwa sababu ya machukizo maovu yote ya nyumba ya Israeli; maana wataanguka kwa upanga, na kwa njaa, na kwa tauni.
12 Yeye aliye mbali sana atakufa kwa tauni; na yeye aliye karibu atakufa kwa upanga; na yeye atakayesalia, na kuhusuriwa katika mji, atakufa kwa njaa, hivyo ndivyo nitakavyoitimiza ghadhabu yangu juu yao.
13 Nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, watu wa kwao waliouawa watakapokuwa kati ya vinyago vyao, pande zote za madhabahu zao, juu ya kila kilima kirefu, juu ya vilele vya milima, na chini ya kila mti wenye majani mabichi, na chini ya kila mwaloni mnene, pale pale walipovifukizia uvumba mzuri vinyago vyao vyote.
14 Nami nitanyosha mkono wangu juu yao, na kuifanya nchi kuwa maganjo, tena ukiwa mbaya kuliko jangwa upande wa Dibla, katika makao yao yote; nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.

Ezekieli 7


1 Tena neno la Bwana likanijia, kusema,
2 Na wewe, mwanadamu, Bwana MUNGU aiambia hivi nchi ya Israeli; Ni mwisho; mwisho umezijia pembe nne za nchi.
3 Sasa mwisho huu unakupata, nami nitakuletea hasira yangu, nitakuhukumu sawasawa na njia zako; nami nitakupatiliza machukizo yako yote.
4 Jicho langu halitakuachilia, wala sitaona huruma; bali nitakupatiliza njia zako, na machukizo yako yatakuwa katikati yako; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.
5 Bwana MUNGU asema hivi; Ni jambo baya, jambo baya la namna ya peke yake; angalia, linakuja.
6 Mwisho umekuja, mwisho huu umekuja; unaamka ukupate; angalia, unakuja.
7 Ajali yako imekujia, wewe ukaaye katika nchi hii; majira yamewadia, siku ile inakaribia; siku ya fujo, wala si ya shangwe milimani.
8 Basi hivi karibu nitamwaga ghadhabu yangu juu yako, nitazitimiza hasira zangu juu yako, nami nitakuhukumu sawasawa na njia zako; nami nitakupatiliza machukizo yako yote.
9 Jicho langu halitaachilia, wala sitaona huruma; nitakupatiliza njia zako na machukizo yako yote yatakuwa katikati yako; nanyi mtajua ya kuwa mimi, Bwana, napiga.
10 Angalia, siku hiyo; angalia, inakuja; ajali yako imetokea; fimbo imechanua, kiburi kimechipuka.
11 Udhalimu umeinuka, ukawa fimbo ya uovu; hapana mtu atakayesalia miongoni mwao, wala katika jamii yao, wala kitu katika utajiri wao; wala hakutakuwa kutukuka kati yao.
12 Majira yamewadia, siku ile inakaribia; huyo anunuaye asifurahi, wala asihuzunike auzaye; maana ghadhabu imewapata wote jamii.
13 Kwa maana auzaye hatakirudia kilichouzwa, wajapokuwa wangali hai; kwa sababu maono haya yawahusu wote jamii; hapana mmoja atakayerudi; wala hapana mtu atakayejitia nguvu katika uovu wa maisha yake.
14 Wamepiga tarumbeta, wameweka vitu vyote tayari; lakini hapana aendaye vitani; maana ghadhabu yangu imewapata wote jamii.
15 Upanga uko nje, na tauni na njaa zimo ndani; yeye aliye nje mashambani atakufa kwa upanga; na yeye aliye ndani ya mji, njaa na tauni zitamla.
16 Lakini watakaokimbia watakimbia, nao watakuwa juu ya milima kama hua wa bondeni, wote wakilia, kila mmoja katika uovu wake.
17 Mikono yote itakuwa dhaifu, na magoti yote yatalegea kama maji.
18 Tena watajifungia nguo za magunia, na utisho utawafunika; na aibu itakuwa juu ya nyuso zote, na upaa juu ya vichwa vyao vyote.
19 Watatupa fedha yao katika njia kuu za mji, na dhahabu yao itakuwa kama kitu cha unajisi; fedha yao na dhahabu yao hazitaweza kuwaokoa siku ya ghadhabu ya Bwana; hawatajishibisha roho zao, wala hawatajijaza matumbo yao; kwa sababu zilikuwa kwazo la uovu wao.
20 Na uzuri wa pambo lake, yeye aliuweka katika enzi, lakini wao walifanya sanamu za machukizo yao, na vitu vyao vichukizavyo, ndani yake; ndiyo maana nimeifanya kuwa kama kitu cha unajisi kwao.
21 Nami nitapatia katika mikono ya wageni pawe mateka yao, na katika mikono ya waovu wa duniani pawe mawindo yao, nao watapanajisi.
22 Tena nitaugeuza uso wangu usiwaelekee, nao watapatia unajisi mahali pangu pa siri; na wanyang'anyi wataingia humo na kupatia unajisi.
23 Ufue mnyororo; kwa maana nchi hii imejaa hukumu za damu, nao mji umejaa udhalimu.
24 Kwa sababu hiyo nitawaleta watu wa mataifa walio wabaya kabisa, nao watazimiliki nyumba zao; tena nitakikomesha kiburi chao wenye nguvu; na mahali pao patakatifu patatiwa unajisi.
25 Uharibifu unakuja; nao watatafuta amani, lakini haitapatikana.
26 Madhara yatakuja juu ya madhara, na habari ya shari juu ya habari ya shari; nao watakwenda kwa nabii kutaka maono; lakini hiyo sheria itampotea kuhani, na mashauri yatawapotea wazee.
27 Mfalme ataomboleza, na mkuu atavikwa ukiwa, na mikono ya watu wa nchi itataabika; nitawatenda sawasawa na njia yao; nami nitawahukumu sawasawa na kustahili kwao; nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.

Ezekieli 8


1 Ikawa katika mwaka wa sita, mwezi wa sita, siku ya tano ya mwezi, nilipokuwa nikikaa nyumbani mwangu, wazee wa Yuda nao wali wamekaa mbele yangu, mkono wa Bwana MUNGU ukaniangukia huko.
2 Ndipo nikaangalia, na tazama, kana kwamba ni mfano wa moto; tangu mfano wa viuno vyake na chini, moto; na tangu mfano wa viuno vyake na juu, kana kwamba ni mfano wa mwangaza, kama rangi ya kaharabu.
3 Naye akanyosha mfano wa mkono, akanishika kwa kishungi kimoja cha nywele za kichwa changu; nayo roho ikaniinua kati ya dunia na mbingu, ikanileta katika maono ya Mungu mpaka Yerusalemu, mpaka mlango wa kuingilia ua wa ndani uelekeao upande wa kaskazini; mahali palipokuwa pamewekwa sanamu ya wivu, itiayo wivu.
4 Na tazama, huo utukufu wa Mungu wa Israeli ulikuwapo hapo, sawasawa na maono yale niliyoyaona katika uwanda.
5 Ndipo akaniambia, Mwanadamu, inua macho yako sasa, uangalie upande wa kaskazini. Basi nikainua macho yangu, nikaangalia upande wa kaskazini, na tazama, upande wa kaskazini wa mlango, ilikuwako sanamu ile ya wivu, mahali pale pa kuingilia.
6 Akaniambia, Mwanadamu, je! Unayaona wanayoyafanya, yaani, haya machukizo makubwa wanayoyafanya nyumba ya Israeli hapa, hata niende zangu mbali na patakatifu pangu? Lakini utaona tena machukizo makubwa mengine.
7 Akanileta hata mlango wa ua; nami nilipoangalia, tazama, pana tundu katika ukuta.
8 Ndipo akaniambia, Mwanadamu, toboa sasa katika ukuta huu; nami nilipotoboa, tazama, pana mlango.
9 Akaniambia, Ingia uyaone machukizo mabaya wanayoyafanya hapa.
10 Basi, nikaingia, nikaona; na tazama, kila namna ya wadudu, na wanyama wachukizao, na taswira za vinyago vyote vya nyumba ya Israeli, zimepigwa ukutani pande zote.
11 Na watu sabini wa wazee wa Israeli walikuwa wamesimama na kuzielekea, na katikati yao alisimama Yaazania, mwana wa Shafani; kila mmoja ana chetezo mkononi mwake, na harufu ya moshi wa uvumba ilipaa juu.
12 Kisha akaniambia, Mwanadamu, umeyaona wanayotenda wazee wa nyumba ya Israeli gizani, kila mtu ndani ya vyumba vyake vya sanamu? Maana husema, Bwana hatuoni; Bwana ameiacha nchi hii.
13 Akaniambia tena, Utaona tena machukizo makubwa mengine wanayoyatenda.
14 Ndipo akanileta mpaka mlango wa kuingilia katika nyumba ya Bwana, ulioelekea upande wa kaskazini, na tazama, wanawake wameketi wakimlilia Tamuzi.
15 Akaniambia, Mwanadamu umeyaona haya? Utaona tena machukizo makubwa kuliko hayo.
16 Akanileta mpaka ua wa ndani wa nyumba ya Bwana, na tazama, mlangoni pa hekalu la Bwana, kati ya ukumbi na madhabahu, walikuwako watu kama ishirini na watano, wamelipa kisogo hekalu la Bwana, na nyuso zao zimeelekea upande wa mashariki, nao wanaliabudu jua, kwa kuuelekea upande wa mashariki.
17 Basi, akaniambia, Umeyaona haya, Ee mwanadamu? Je! Ni jambo dogo sana kwa nyumba ya Yuda, wayafanye machukizo wanayoyafanya hapa? Kwa maana wameijaza nchi hii udhalimu, tena wamerejea nyuma ili kunikasirisha; na, tazama, wanaliweka tawi puani.
18 Kwa sababu hiyo mimi nami nitatenda kwa ghadhabu; jicho langu halitaachilia, wala sitaona huruma, na wajapolia masikioni mwangu kwa sauti kuu, sitawasikiliza.

Ezekieli 9


1 Kisha akalia kwa sauti kuu masikioni mwangu, akisema, Waamuru wale wanaousimamia mji wakaribie, kila mmoja na awe na kitu chake cha kuangamiza mkononi mwake.
2 Na tazama, watu sita wakaja, wakitokea kwa njia ya lango la juu, lielekealo upande wa kaskazini, kila mmoja ana kitu chake cha kufisha mkononi mwake; na mtu mmoja kati yao amevaa bafta, naye ana kidau cha wino cha mwandishi kiunoni. Wakaingia, wakasimama karibu na madhabahu ya shaba.
3 Na huo utukufu wa Bwana wa Israeli ulikuwa umepanda juu kutoka kwa kerubi, ambaye ulikuwa juu yake, mpaka kizingiti cha nyumba; akamwita mtu yule aliyekuwa amevaa bafta, mwenye kidau cha wino cha mwandishi kiunoni.
4 Bwana akamwambia, Pita kati ya mji, kati ya Yerusalemu, ukatie alama katika vipaji vya nyuso vya watu wanaougua na kulia kwa sababu ya machukizo yote yanayofanyika kati yake.
5 Na hao wengine aliwaambia, nami nalisikia, Piteni kati ya mji nyuma yake, mkapige; jicho lenu lisiachilie, wala msione huruma;
6 Waueni kabisa, mzee, na kijana, na msichana, na watoto wachanga, na wanawake; lakini msimkaribie mtu ye yote mwenye hiyo alama; tena anzeni katika patakatifu pangu. Basi, wakaanza kwa wazee waliokuwa mbele ya nyumba.
7 Akawaambia, itieni nyumba unajisi, mkazijaze nyua mizoga ya hao waliouawa; haya, enendeni. Wakaenenda, wakapiga-piga katika mji.
8 Tena ikawa, walipokuwa wakipiga, nami nikiachwa, nalianguka kifudifudi, nikalia, nikasema, Ee Bwana MUNGU! Utaangamiza mabaki yote ya Israeli, wakati wa kumwaga ghadhabu yako juu ya Yerusalemu?
9 Ndipo akaniambia, Uovu wa nyumba ya Israeli na Yuda ni mwingi sana, nayo nchi imejaa damu, nao mji umejaa kupotosha hukumu; maana husema, Bwana ameiacha nchi hii, naye Bwana haoni.
10 Nami, jicho langu halitaachilia, wala sitaona huruma; lakini nitaleta njia yao juu ya vichwa vyao.
11 Na tazama, mtu yule aliyevaa bafta, mwenye kidau cha wino kiunoni, akaleta habari, akisema, Nimefanya kama ulivyoniamuru.

Ezekieli 10


1 Ndipo nikaangalia, na tazama, katika anga lililokuwa juu ya vichwa vya makerubi, kulionekana juu yao kana kwamba ni yakuti samawi, kuonekana kama mfano wa kiti cha enzi.
2 Naye akamwambia mtu yule aliyevaa bafta, akasema, Ingia kati ya magurudumu yazungukayo, yaani, chini ya kerubi, ukaijaze mikono yako yote miwili makaa ya moto, toka katikati ya makerubi, ukayamwage juu ya mji. Akaingia ndani mbele ya macho yangu.
3 Basi, makerubi walisimama upande wa kuume wa nyumba, hapo alipoingia mtu yule; nalo wingu likaujaza ua wa ndani.
4 Utukufu wa Bwana ukapaa kutoka kwa kerubi yule, ukasimama juu ya kizingiti cha nyumba; nayo nyumba ikajazwa na lile wingu, na ua ulikuwa umejaa mwangaza wa utukufu wa Bwana.
5 Na sauti ya mabawa ya makerubi ikasikiwa, hata katika ua wa nje, kama sauti ya Mungu Mwenyezi, asemapo.
6 Ikawa, hapo alipomwagiza huyo mtu aliyevaa bafta, akisema, Twaa moto kutoka katikati ya magurudumu yazungukayo katikati ya hao makerubi, akaingia, akasimama karibu na gurudumu moja.
7 Na kerubi yule akanyosha mkono wake toka katikati ya makerubi, kwa moto ule uliokuwa katikati ya makerubi, akatwaa baadhi ya moto ule, akautia katika mikono ya mtu yule aliyevaa bafta; naye akautwaa, akatoka.
8 Kukaonekana katika makerubi mfano wa mkono wa mwanadamu chini ya mabawa yao.
9 Nami nikaangalia, na tazama, yalikuwako magurudumu manne karibu na makerubi, gurudumu moja karibu na kerubi mmoja, na gurudumu lingine karibu na kerubi mwingine; na kuonekana kwa magurudumu kulikuwa kana kwamba ni zabarajadi.
10 Na kuonekana kwake, yote manne yalikuwa na mfano mmoja, kana kwamba gurudumu moja lilikuwa ndani ya gurudumu lingine.
11 Walipokwenda, walikwenda kwa pande zao nne; hawakugeuka walipokwenda, lakini walifuata mpaka mahali pale kilipopaelekea kichwa; hawakugeuka walipokwenda.
12 Na mwili wao mzima, na maungo yao, na mikono yao, na mabawa yao, na magurudumu, wamejaa macho pande zote, hata magurudumu waliyokuwa nayo wale wanne.
13 Na magurudumu hayo yaliitwa Kisulisuli, nami nalisikia.
14 Kila mmoja alikuwa na nyuso nne; uso wa kwanza ulikuwa uso wa kerubi, na uso wa pili ulikuwa uso wa mwanadamu, na uso wa tatu ulikuwa uso wa simba, na uso wa nne ulikuwa uso wa tai.
15 Makerubi wakapaa juu; huyo ndiye kiumbe hai niliyemwona karibu na mto Kebari.
16 Na makerubi walipokwenda, magurudumu yale yalikwenda kando yao; na makerubi walipoinua mabawa yao, wapate kupaa juu kutoka katika dunia, magurudumu yale hayakugeuka wala kutoka kando yao.
17 Waliposimama hao, hayo nayo yalisimama; na walipopaa juu hao, hayo nayo yalipaa juu pamoja nao; maana roho ya huyo kiumbe hai ilikuwa ndani yao.
18 Kisha huo utukufu wa Bwana ukatoka pale juu ya kizingiti cha nyumba, ukasimama juu ya makerubi.
19 Nao makerubi wakainua mabawa yao, wakapaa juu kutoka katika dunia machoni pangu, hapo walipotoka nje, nayo magurudumu yakawa kando yao; wakasimama mahali pa kuingilia pa mlango wa upande wa mashariki wa nyumba ya Bwana; na utukufu wa Mungu wa Israeli ulikuwa juu yao.
20 Huyu ndiye kiumbe hai niliyemwona, chini ya Mungu wa Israeli, karibu na mto Kebari; nikajua ya kuwa hao ni makerubi.
21 Kila mmoja alikuwa na nyuso nne, na kila mmoja alikuwa na mabawa manne; na mifano ya mikono ya mwanadamu ilikuwa chini ya mabawa yao.
22 Na mfano wa nyuso zao, ni nyuso zile zile nilizoziona karibu na mto Kebari; kuonekana kwao, na wao wenyewe; kila mmoja walikwenda mbele moja kwa moja.

Ezekieli 11


1 Tena roho ikaniinua, ikanileta hata lango la upande wa mashariki wa nyumba ya Bwana, lililoelekea upande wa mashariki; na tazama, mahali pa kuingilia pa lango walikuwako watu ishirini na watano; na katikati yao nikamwona Yaazania, mwana wa Azuri, na Pelatia, mwana wa Benaya, nao ni wakuu wa watu.
2 Akaniambia, Mwanadamu, hawa ndio watu wale watungao uovu, na kutoa mashauri mabaya ndani ya mji huu;
3 wasemao, Wakati wa kujenga nyumba si karibu; mji huu ni sufuria na sisi ni nyama.
4 Basi toa unabii juu yao, Ee mwanadamu, toa unabii.
5 Roho ya Bwana ikaniangukia, naye akaniambia, Nena, Bwana asema hivi; Mmesema maneno hayo, Enyi nyumba ya Israeli; maana mimi nayajua yaingiayo katika mioyo yenu.
6 Mmewaongeza watu wenu waliouawa ndani ya mji wenu, nanyi mmezijaza njia kuu zake waliouawa.
7 Basi Bwana MUNGU asema hivi; Watu wenu waliouawa, ambao mmewalaza katikati yake, hao ndio nyama hiyo, na mji huu ndio sufuria; lakini ninyi mtatolewa nje kutoka katikati yake.
8 Ninyi mmeuogopa upanga; nami nitauleta upanga juu yenu, asema Bwana MUNGU.
9 Nami nitawatoa ninyi nje kutoka katikati yake, na kuwatia katika mikono ya wageni, nami nitafanya hukumu kati yenu.
10 Mtaanguka kwa upanga; nitawahukumu katika mpaka wa Israeli; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.
11 Mji huu hautakuwa sufuria lenu, wala ninyi hamtakuwa nyama ndani yake; nitawahukumu katika mpaka wa Israeli;
12 nanyi mtajua ya kuwa mimi ni Bwana; kwa maana hamuendi katika amri zangu, wala hamkuzishika hukumu zangu, bali mmetenda mambo kama hukumu za mataifa wanaowazunguka.
13 Ikawa, nilipotoa unabii, Pelatia, mwana wa Benaya, akafa. Ndipo nikaanguka kifudifudi, nikalia kwa sauti kuu, nikasema, Ee Bwana MUNGU, je! Utawakomesha kabisa mabaki ya Israeli?
14 Neno la Bwana likanijia, kusema,
15 Mwanadamu, ndugu zako, naam, ndugu zako, watu wa jamaa zako, na nyumba yote ya Israeli, wote pia, ndio hao ambao wenyeji wa Yerusalemu wamewaambia, Jitengeni mbali na Bwana, nchi hii tumepewa sisi, iwe milki yetu;
16 basi nena, Bwana MUNGU asema hivi, Ikiwa mimi nimewahamisha, wakae katika mataifa, na ikiwa mimi nimewatawanya katika nchi kadha wa kadha, pamoja na hayo nitakuwa patakatifu kwao kwa muda mchache, katika nchi zile walizozifikilia.
17 Basi nena, Bwana MUNGU asema hivi; Nitawakusanya ninyi toka kati ya kabila za watu, na kuwakutanisha toka nchi zile mlizotawanyika, nami nitawapeni nchi ya Israeli.
18 Nao watafika huko, nao wataondolea mbali vitu vyake vyote vichukizavyo, na machukizo yake yote.
19 Nami nitawapa moyo mmoja, nami nitatia roho mpya ndani yao; nami nitauondoa moyo wa kijiwe katika miili yao, nami nitawapa moyo wa nyama;
20 ili waende katika amri zangu, na kuyashika maagizo yangu, na kuyatenda; nao watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao.
21 Bali wao ambao mioyo yao huenda kwa kuufuata moyo wa vitu vyao vichukizavyo, na machukizo yao, nitaileta njia yao iwajilie juu ya vichwa vyao, asema Bwana MUNGU.
22 Ndipo hao makerubi wakainua mabawa yao, nayo magurudumu yalikuwa karibu nao, nao utukufu wa Mungu wa Israeli ulikuwa juu yao.
23 Utukufu wa Bwana ukapaa juu toka katikati ya mji, ukasimama juu ya mlima wa upande wa mashariki wa mji.
24 Na roho hiyo ikaniinua, ikanichukua katika maono, kwa nguvu za roho ya Mungu, hata Ukaldayo, kwa watu wale wa uhamisho. Basi maono niliyoyaona yakaniacha.
25 Ndipo nikawaambia watu wa uhamisho habari ya mambo yote aliyonionyesha Bwana.

Ezekieli 12


1 Neno la Bwana likanijia tena, kusema,
2 Mwanadamu, wewe unakaa kati ya nyumba iliyoasi, watu ambao wana macho ya kuona, ila hawaoni, wana masikio ya kusikia, ila hawasikii; kwa maana ni nyumba iliyoasi.
3 Basi, mwanadamu, funga tayari vyombo kwa uhamisho, ukahame wakati wa mchana mbele ya macho yao; nawe utahama toka mahali pako hapa mpaka mahali pengine mbele ya macho yao; labda watafahamu, wajapokuwa ni nyumba iliyoasi.
4 Nawe utatoa vyombo vyako, wakati wa mchana, mbele ya macho yao, kana kwamba ni vyombo vya kuhamishwa; nawe mwenyewe utatoka, wakati wa jioni, mbele ya macho yao, kama watu watokavyo katika kuhamishwa.
5 Toboa mahali ukutani mbele ya macho yao, ukachukue vitu kwa kuvipitisha pale.
6 Mbele ya macho yao utajitwika begani pako, na kuvichukua nje gizani; utafunika uso wako, hata usiione nchi; kwa maana nimekuweka uwe ishara kwa nyumba ya Israeli.
7 Nikafanya vile vile kama nilivyoamriwa; nalitoa vyombo vyangu wakati wa mchana kana kwamba ni vyombo vya kuhamishwa, na wakati wa jioni nikautoboa ukuta kwa mkono wangu; nikavitoa gizani, nikavichukua begani, mbele ya macho yao.
8 Asubuhi neno la Bwana likanijia, kusema,
9 Mwanadamu, nyumba ya Israeli, je! Nyumba ile iliyoasi, hawakukuambia, Unafanya nini wewe?
10 Waambie, Bwana MUNGU asema hivi; Ufunuo huu wamhusu mkuu wa Yerusalemu, na nyumba yote ya Israeli walio kati yao.
11 Sema, Mimi ni ishara kwenu; kama mimi nilivyotenda, wao nao watatendwa vile vile; watahamishwa, watakwenda kufungwa.
12 Naye mkuu aliye kati yao atachukua begani katika giza; naye atatoka kwenda zake; watatoboa mahali ukutani, wapate kuvichukua vyombo vyao nje; atafunika uso wake, kwa sababu hataiona nchi kwa macho yake.
13 Tena wavu wangu nitautandika juu yake, naye atanaswa kwa mtego wangu; nami nitampeleka Babeli, mpaka nchi ya Wakaldayo; lakini hataiona, angawa atakufa huko.
14 Nami nitawatawanya kwa pepo zote wote wamzungukao ili wamsaidie, na vikosi vyake vyote; nami nitaufuta upanga nyuma yao.
15 Nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana; nitakapowatawanya kati ya mataifa, na kuwatupa-tupa katika nchi zote.
16 Lakini nitawasaza watu wachache miongoni mwao na kuwaokoa na upanga, na njaa, na tauni ili watangaze habari ya machukizo yao yote, kati ya mataifa huko waendako; nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.
17 Tena neno la Bwana likanijia, kusema,
18 Mwanadamu, ule chakula chako kwa matetemo, ukanywe maji yako kwa kutetemeka na kwa kuyatunza sana;
19 ukawaambie watu wa nchi, Bwana MUNGU asema hivi, katika habari zao wakaao Yerusalemu, na katika nchi ya Israeli; Watakula chakula chao kwa kukitunza sana, na maji yao watayanywa kwa ushangao, nchi yao iwe ukiwa, kwa kukosa vitu vyote viijazavyo, kwa sababu ya udhalimu wao wote wakaao ndani yake.
20 Na miji yote yenye watu itakuwa maganjo, nayo nchi itakuwa ukiwa; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.
21 Neno la Bwana likanijia, kusema,
22 Mwanadamu, ni mithali gani hii mliyo nayo katika nchi ya Israeli, mkisema, Siku hizo zinakawia na maono yote hayatimizwi.
23 Basi uwaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Nitaikomesha mithali hii, wasiitumie tena kama mithali katika Israeli; lakini uwaambie, Siku hizo ni karibu, na utimilizo wa maono yote.
24 Kwa maana hayatakuwapo tena maono yo yote ya ubatili, wala ubashiri wa kujipendekeza, katika nyumba ya Israeli.
25 Maana mimi ni Bwana; mimi nitanena, na neno lile nitakalolinena litatimizwa; wala halitakawilishwa tena; maana katika siku zenu, Ewe nyumba iliyoasi, nitalinena neno hilo na kulitimiza, asema Bwana MUNGU.
26 Neno la Bwana likanijia tena, kusema,
27 Mwanadamu, tazama, hao wa nyumba ya Israeli husema, Maono hayo ayaonayo ni ya siku nyingi zijazo, naye anatabiri habari ya nyakati zilizo mbali sana.
28 Basi uwaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Maneno yangu hayatakawilishwa tena hata moja, bali neno nitakalolinena litatimizwa, asema Bwana MUNGU.

Ezekieli 13


1 Kisha neno la Bwana likanijia, kusema,
2 Mwanadamu, tabiri juu ya manabii wa Israeli wanaotabiri, uwaambie wanaotabiri kwa mioyo yao wenyewe, Lisikieni neno la Bwana;
3 Bwana MUNGU asema hivi; Ole wao manabii wajinga, wanaoifuata roho yao wenyewe, wala hawakuona neno lo lote!
4 Ee Israeli, manabii wako wamekuwa kama mbweha, mahali palipo ukiwa.
5 Hamkupanda kwenda mahali palipobomolewa, wala hamkuitengenezea nyumba ya Israeli boma, wapate kusimama vitani katika siku ya Bwana.
6 Wameona ubatili, na uganga wa uongo, hao wasemao, Bwana asema; lakini Bwana hakuwatuma; nao wamewatumainisha watu ya kuwa neno lile litatimizwa.
7 Je! Hamkuona maono ya bure, hamkunena mabashiri ya uongo? Nanyi mwasema, Bwana asema; ila mimi sikusema neno.
8 Basi tazama, Bwana MUNGU asema hivi; Kwa sababu mmenena ubatili, na kuona uongo, basi, kwa sababu hiyo, mimi ni juu yenu, asema Bwana MUNGU.
9 Na mkono wangu utakuwa juu ya manabii wanaoona ubatili, na kutabiri uongo; hawatakuwa katika mashauri ya watu wangu, wala hawataandikwa katika maandiko ya nyumba ya Israeli, wala hawataingia katika nchi ya Israeli; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana MUNGU.
10 Kwa sababu hiyo, kwa sababu wameshawishi watu wangu, wakisema, Amani; wala hapana amani; na mtu mmoja ajengapo ukuta, tazama, waupaka chokaa isiyokorogwa vema;
11 basi waambie hao wanaoupaka ukuta chokaa isiyokorogwa vema, ya kwamba utaanguka; kutakuwa mvua ya kufurika; nanyi, enyi mvua ya mawe makubwa ya barafu, mtaanguka; na upepo wa dhoruba utaupasua.
12 Na huo ukuta utakapoanguka, je! Hamtaambiwa, Ku wapi kupaka kwenu mlikoupaka?
13 Basi Bwana MUNGU asema hivi; Nitaupasua kwa upepo wa dhoruba, katika ghadhabu yangu; tena kutakuwa mvua ya barafu ya kufurika katika hasira yangu; na mawe makubwa ya barafu katika hasira ya kuukomesha.
14 Ndivyo nitakavyoubomoa ukuta mlioupaka chokaa isiyokorogwa vema, na kuuangusha chini, hata misingi yake itafunuliwa; nao utaanguka, nanyi mtaangamizwa katikati yake; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.
15 Ndivyo nitakavyotimiza ghadhabu yangu juu ya ukuta ule, na juu yao walioupaka chokaa isiyokorogwa vema; nami nitawaambieni, Ukuta huo hauko sasa, wala wao walioupaka hawako;
16 yaani, manabii wa Israeli, watabirio habari za Yerusalemu, na kuona maono ya amani katika habari zake; wala hapana amani, asema Bwana MUNGU.
17 Na wewe, mwanadamu, kaza uso wako juu ya binti za watu wako, watabirio kwa akili zao wenyewe; ukatabiri juu yao,
18 useme, Bwana MUNGU asema hivi; Ole wao wanawake wale, washonao hirizi katika viungo vyote vya mikono, wawekao leso juu ya vichwa vya kila kimo, ili wawinde roho za watu; je! Mtaziwinda roho za watu wangu, na kuzihifadhi hai roho zenu wenyewe?
19 Nanyi mmeninajisi kati ya watu wangu, kwa ajili ya makonzi ya shayiri na vipande vya mkate, ili kuziua roho za watu ambao haiwapasi kufa, na kuzihifadhi hai roho za watu ambao haikuwapasa kuwa hai, kwa kuwaambia uongo watu wangu wasikilizao uongo.
20 Basi Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi ni kinyume cha hirizi zenu, ambazo kwa hizo mnaziwinda roho za watu kama ndege, nami nitazitoa katika mikono yenu kwa nguvu; nami nitaziachilia roho zile mnazoziwinda kama ndege.
21 Na leso zenu nazo nitazirarua, na kuwaokoa watu wangu katika mikono yenu, wala hawatakuwa katika mikono yenu tena kuwindwa; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.
22 Kwa kuwa ninyi mmemhuzunisha moyo mwenye haki kwa uongo, ambaye mimi sikumhuzunisha; na kuitia nguvu mikono ya mtu mbaya, hata asigeuke, na kuiacha njia yake mbaya, na kuhifadhika;
23 basi, kwa sababu hiyo ninyi hamtaona tena ubatili, wala kutabiri mambo; nami nitawaokoa watu wangu katika mikono yenu; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.

Ezekieli 14


1 Ndipo baadhi ya wazee wa Israeli wakanijia, wakaketi mbele yangu.
2 Ndipo neno la Bwana likanijia, kusema,
3 Mwanadamu, watu hawa wametwaa vinyago vyao na kuvitia mioyoni mwao, nao wameweka kwazo la uovu wao mbele ya nyuso zao. Je! Ni laiki yangu niulizwe na wao katika neno lo lote?
4 Basi sema nao, uwaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Kila mtu wa nyumba ya Israeli atwaaye vinyago vyake na kuvitia moyoni mwake, na kuliweka kwazo la uovu wake mbele ya uso wake, na kumwendea nabii; mimi, Bwana, nitamjibu neno lake sawasawa na wingi wa sanamu zake;
5 ili niwakamate nyumba ya Israeli kwa mioyo yao wenyewe, kwa sababu wamefarakana nami kwa vinyago vyao.
6 Kwa sababu hiyo uwaambie nyumba ya Israeli, Bwana MUNGU asema hivi; Rudini ninyi, mkageuke na kuviacha vinyago vyenu; mkageuze nyuso zenu zisielekee machukizo yenu yote.
7 Kwa maana kila mtu wa nyumba ya Israeli, au wa wageni wakaao katika Israeli, ajitengaye nami, na kuvitwaa vinyago vyake na kuvitia moyoni mwake, na kuliweka kwazo la uovu wake mbele ya uso wake, kisha kumwendea nabii, na kuniuliza neno kwa ajili ya nafsi yake; mimi, Bwana, nitamjibu, mimi mwenyewe;
8 nami nitaukaza uso wangu juu ya mtu yule, na kumfanya kuwa ajabu, awe ishara na mithali, nami nitamkatilia mbali, asiwe kati ya watu wangu; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.
9 Na nabii akidanganyika, na kusema neno, mimi, Bwana, nimemdanganya nabii yule, nami nitaunyosha mkono wangu juu yake, na kumwangamiza, asiwe kati ya watu wangu Israeli.
10 Nao watauchukua uovu wao; uovu wa nabii utakuwa sawasawa na uovu wake yule amwendeaye aulize neno;
11 ili nyumba ya Israeli wasipotee mbali nami, wala wasijitie unajisi tena kwa makosa yao yote; bali wawe watu wangu, nami niwe Mungu wao, asema Bwana MUNGU.
12 Neno la Bwana likanijia, kusema,
13 Mwanadamu, nchi itakapofanya dhambi na kuniasi, kwa kukosa, nikaunyosha mkono wangu juu yake, na kulivunja tegemeo la chakula chake, na kuipelekea njaa, na kukatilia mbali mwanadamu na mnyama;
14 wajapokuwa watu hawa watatu, Nuhu, na Danieli, na Ayubu, kuwamo ndani yake, wangejiokoa nafsi zao wenyewe tu kwa haki yao, asema Bwana MUNGU.
15 Nikipitisha wanyama wabaya ndani ya nchi ile, wakaiharibu hata ikawa ukiwa, mtu awaye yote asiweze kupita ndani yake, kwa sababu ya wanyama hao;
16 wajapokuwamo watu hawa watatu ndani yake, kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, hawataokoa wana wala binti; wao wenyewe tu wataokoka, bali nchi ile itakuwa ukiwa.
17 Au nikileta upanga juu ya nchi ile, na kusema, Upanga, pita kati ya nchi hii, hata nikawakatilia mbali na nchi hiyo wanadamu na wanyama;
18 wajapokuwamo watu hawa watatu ndani yake, kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, hawataokoa wana wala binti; bali wao wenyewe tu wataokoka.
19 Au nikipeleka tauni katika nchi ile, na kumwaga ghadhabu yangu juu yake, kwa damu; ili kuwakatilia mbali nayo wanadamu na wanyama;
20 wajapokuwamo ndani yake Nuhu, na Danieli, na Ayubu, kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, hawataokoa wana wala binti; watajiokoa nafsi zao tu kwa haki yao.
21 Maana Bwana MUNGU asema hivi; Je! U zaidi sana nitakapoleta hukumu zangu nne zilizo kali juu ya Yerusalemu, yaani, upanga, na njaa, na wanyama wabaya, na tauni, niwakatilie mbali nayo wanadamu na wanyama?
22 Lakini, tazama, watasalia mabaki watakaochukuliwa nje, wana na binti; tazama, watawatokea ninyi, nanyi mtaiona njia yao na matendo yao; nanyi mtafarijika katika habari ya mabaya niliyoleta juu ya Yerusalemu, naam, katika habari ya mambo yote niliyoleta juu yake.
23 Nao watawafariji ninyi, mtakapoona njia yao na matendo yao; nanyi mtajua ya kuwa sikufanya bila sababu mambo yote niliyoutenda, asema Bwana MUNGU.

Ezekieli 15


1 Neno la Bwana likanijia, kusema,
2 Mwanadamu, mzabibu una sifa gani kuliko mti mwingine, au tawi la mzabibu lililokuwa kati ya miti ya msituni?
3 Je! Mti wake waweza kutwaliwa, ili kufanya kazi yo yote? Watu waweza kufanya chango kwa huo, ili kutundika chombo cho chote?
4 Tazama, watupwa motoni kwa kuni moto umeziteketeza ncha zake zote mbili, nao umeteketea katikati, je! Wafaa kwa kazi yo yote?
5 Tazama, ulipokuwa mzima, haukufaa kwa kazi yo yote; sembuse ukiisha kuliwa na moto, na kuteketea; je! Waweza kufaa kwa kazi yo yote?
6 Basi Bwana MUNGU asema hivi; Kama mzabibu kati ya miti ya msituni, niliyoupa moto uwe kuni, ndivyo nitakavyowatoa wakaao Yerusalemu.
7 Nami nitaukaza uso wangu juu yao; nao watatoka motoni, lakini moto utawateketeza; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, nitakapoukaza uso wangu juu yao.
8 Nami nitaifanya nchi kuwa ukiwa, kwa sababu wamekosa, asema Bwana MUNGU.

Ezekieli 16


1 Neno la Bwana likanijia tena, kusema,
2 Mwanadamu, uujulishe Yerusalemu machukizo yake,
3 useme, Bwana MUNGU auambia Yerusalemu hivi; Asili yako na kuzaliwa kwako kwatoka katika nchi ya Mkanaani; Mwamori alikuwa baba yako, na mama yako alikuwa Mhiti.
4 Na katika habari za kuzaliwa kwako, siku ile uliyozaliwa, kitovu chako hakikukatwa, wala hukuoshwa kwa maji usafishwe; hukutiwa chumvi hata kidogo, wala hukutiwa katika nguo kabisa.
5 Hapana jicho lililokuhurumia, ili kukutendea lo lote la mambo hayo kwa kukuhurumia; lakini ulitupwa nje uwandani, kwa kuwa nafsi yako ilichukiwa, katika siku ile uliyozaliwa.
6 Nami nilipopita karibu nawe, nikakuona ukigaagaa katika damu yako, nalikuambia, Ujapokuwa katika damu yako, uwe hai; naam, nalikuambia, Ujapokuwa katika damu yako, uwe hai.
7 Nalikufanya kuwa maelfu-elfu, kama mimea ya mashamba, ukaongezeka, na kuzidi kuwa mkubwa, ukapata kuwa na uzuri mno; matiti yako yakaumbwa, nywele zako zikawa zimeota; lakini ulikuwa uchi, huna nguo.
8 Basi, nilipopita karibu nawe, nikakutazama; tazama, wakati wako ulikuwa wakati wa upendo; nikatandika upindo wa vazi langu juu yako, nikakufunika uchi wako; naam, nalikuapia, nikafanya agano nawe, asema Bwana MUNGU, ukawa wangu.
9 Kisha nikakuosha kwa maji; naam, nalikuosha kabisa damu yako, nikakupaka mafuta;
10 nikakuvika nguo ya taraza, nikakupa viatu vya ngozi ya pomboo, nikakufunga nguo ya kitani safi kiunoni mwako, nikakufunika kwa hariri.
11 Nikakupamba kwa mapambo pia, nikatia vikuku mikononi mwako, na mkufu shingoni mwako.
12 Nikatia hazama puani mwako, na pete masikioni mwako, na taji nzuri juu ya kichwa chako.
13 Hivyo ulipambwa kwa dhahabu na fedha; na mavazi yako yalikuwa ya kitani safi, na hariri, na kazi ya taraza; ulikula unga mzuri, na asali, na mafuta; nawe ulikuwa mzuri mno, ukafanikiwa hata kufikilia hali ya kifalme.
14 Sifa zako zikaenea kati ya mataifa kwa sababu ya uzuri wako; kwa maana ulikuwa mkamilifu, kwa sababu ya utukufu wangu niliokutia, asema Bwana MUNGU.
15 Lakini uliutumainia uzuri wako, ukafanya mambo ya kikahaba kwa sababu ya sifa zako, ukamwaga mambo yako ya kikahaba juu ya kila mtu aliyepita; ulikuwa wake.
16 Ukatwaa baadhi ya mavazi yako, ukajifanyia mahali palipoinuka, palipopambwa kwa rangi mbalimbali, ukafanya mambo ya kikahaba juu yake; mambo kama hayo hayatakuja wala hayatakuwako.
17 Pia ulivitwaa vyombo vyako vya uzuri, vya dhahabu yangu na vya fedha yangu, nilivyokupa, ukajifanyia sanamu za wanaume, ukafanya mambo ya kikahaba pamoja nazo;
18 ukatwaa nguo zako za kazi ya taraza, ukawafunika, ukaweka mafuta yangu na uvumba wangu mbele yao.
19 Mkate wangu niliokupa, unga mzuri, na mafuta, na asali, nilivyokulisha, ukaviweka mbele yao viwe harufu ya kupendeza; na ndivyo vilivyokuwa; asema Bwana MUNGU.
20 Pamoja na hayo uliwatwaa wana wako na binti zako, ulionizalia, ukawatoa sadaka kwao ili waliwe. Je! Mambo yako ya kikahaba ni kitu kidogo tu,
21 hata ukawaua watoto wangu, na kuwatoa kwa kuwapitisha motoni kwa hao?
22 Na katika machukizo yako yote, na mambo yako ya kikahaba, hukuzikumbuka siku za ujana wako, ulipokuwa uchi, huna nguo, ukawa ukigaagaa katika damu yako.
23 Tena, imekuwa baada ya uovu wako wote, (ole wako! ole wako! Asema Bwana MUNGU,)
24 ulijijengea mahali palipoinuka, ukajifanyia mahali palipoinuka katika kila njia kuu.
25 Umejenga mahali pako palipoinuka penye kichwa cha kila njia, ukaufanya uzuri wako kuwa chukizo, ukatanua miguu yako kwa kila mtu aliyepita karibu, ukaongeza mambo yako ya kikahaba.
26 Tena umezini na Wamisri, jirani zako, wakuu wa mwili; ukaongeza mambo yako ya kikahaba, ili kunikasirisha.
27 Basi, tazama, kwa ajili ya hayo nimenyosha mkono wangu juu yako, nami nimelipunguza posho lako, na kukutoa kwa mapenzi yao wanaokuchukia, binti za Wafilisti, walioyaonea haya mambo yako ya uasherati.
28 Pia umefanya mambo ya kikahaba pamoja na Waashuri, kwa sababu ulikuwa huwezi kushibishwa; naam, umefanya mambo ya kikahaba pamoja nao, wala hujashiba bado.
29 Pamoja na hayo umeongeza mambo yako ya kikahaba katika nchi ya Kanaani, mpaka Ukaldayo, wala hujashibishwa kwa hayo.
30 Jinsi moyo wako ulivyokuwa dhaifu, asema Bwana MUNGU, ikiwa unafanya mambo hayo yote, kazi ya mwanamke mzinzi,
31 apendaye kutawala watu; kwa kuwa wajijengea mahali pako pakuu penye kichwa cha kila njia, na kufanya mahali pako palipoinuka katika kila njia kuu; lakini hukuwa kama kahaba, kwa maana ulidharau kupokea ujira.
32 Mke wa mtu, aziniye! Akaribishaye wageni badala ya mumewe!
33 Watu huwapa makahaba wote zawadi, bali wewe unawapa wapenzi wako wote zawadi zako, na kuwapa rushwa ili waje kwako pande zote, kwa ajili ya mambo yako ya kikahaba.
34 Tena, katika mambo yako ya kikahaba, wewe na wanawake wengine ni mbalimbali, kwa kuwa hapana akufuataye katika mambo yako ya kikahaba; tena kwa kuwa unatoa ujira, wala hupewi ujira; basi, njia yako na njia yao ni mbalimbali.
35 Kwa sababu hiyo, Ewe kahaba, lisikie neno la Bwana;
36 Bwana MUNGU asema hivi; Kwa sababu uchafu wako umemwagwa, na uchi wako umefunuliwa, kwa njia ya uzinzi wako pamoja na wapenzi wako; na kwa sababu ya vinyago vyote vya machukizo yako; na kwa sababu ya damu ya watoto wako, uliyowapa;
37 basi, tazama, nitawakusanya wapenzi wako wote ambao umejifurahisha pamoja nao, nao wote uliowapenda, pamoja na watu wote uliowachukia; naam, nitawakusanya juu yako pande zote, na kuwafunulia uchi wako, wapate kuuona uchi wako wote.
38 Nami nitakuhukumu, kama wahukumiwavyo wake walioolewa wazinio, na kumwaga damu, nami nitakupatiliza damu ya ghadhabu na wivu.
39 Tena nitakutia katika mikono yao, nao watapaangusha mahali pako pakuu, na kupabomoa mahali pako palipoinuka, nao watakuvua nguo zako, na kutwaa vyombo vyako vya uzuri, nao watakuacha uchi, huna nguo.
40 Tena wataleta mkutano wa watu juu yako, nao watakupiga kwa mawe, na kukuchoma kwa panga zao.
41 Nao watazipiga moto nyumba zako, na kutekeleza hukumu juu yako mbele ya wanawake wengi, nami nitakulazimisha kuacha mambo ya kikahaba, wala hutatoa ujira tena.
42 Hivyo ndivyo nitakavyoshibisha ghadhabu yangu juu yako, na wivu wangu utanitoka, nami nitatulia wala sitaona hasira tena.
43 Kwa sababu hukuzikumbuka siku za ujana wako, bali umenikasirisha kwa mambo hayo yote; basi, tazama, mimi nami nitaleta njia yako juu ya kichwa chako, asema Bwana MUNGU; wala hutafanya uasherati zaidi ya machukizo yako yote.
44 Tazama, kila mtu atumiaye mithali atatumia mithali hii kinyume chako, akisema, Kama mama ya mtu alivyo, ndivyo alivyo binti yake.
45 Wewe u binti ya mama yako, amchukiaye mume wake na watoto wake; nawe u umbu la maumbu yako, waliowachukia waume zao na watoto wao; mama yako alikuwa Mhiti, na baba yako Mwamori.
46 Na umbu lako mkubwa ni Samaria, akaaye mkono wako wa kushoto, yeye na binti zake; na umbu lako mdogo, akaaye mkono wako wa kuume, ni Sodoma na binti zake.
47 Lakini hukuenda katika njia zao, wala hukutenda sawasawa na machukizo yao; lakini kana kwamba hilo ni jambo dogo sana, ulikuwa umeharibika kuliko wao katika njia zako zote.
48 Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, Sodoma, umbu lako, yeye na binti zake, hawakutenda kama wewe ulivyotenda, wewe na binti zako.
49 Tazama, uovu wa umbu lako, Sodoma, ulikuwa huu; kiburi, na kushiba chakula, na kufanikiwa, hayo yalikuwa ndani yake na binti zake; tena hakuutia nguvu mkono wa maskini na mhitaji.
50 Nao walijivuna, wakafanya machukizo mbele zangu; kwa sababu hiyo naliwaondoa hapo nilipoyaona.
51 Samaria naye hakutenda nusu ya dhambi zako; bali wewe umeyaongeza machukizo yako zaidi ya hao, nawe umewapa haki maumbu yako kwa machukizo yako yote uliyoyatenda.
52 Wewe nawe, ichukue aibu yako mwenyewe, kwa kuwa umetoa hukumu juu ya maumbu yako; kwa dhambi zako ulizozitenda, zilizochukiza kuliko hao, wao wana haki kuliko wewe; naam, ufedheheke wewe nawe, ukaichukue aibu yako, kwa kuwa umewapa haki maumbu yako.
53 Nami nitawarudisha watu wao waliofungwa; wafungwa wa Sodoma na binti zake, na wafungwa wa Samaria na binti zake na wafungwa wako waliofungwa kati yao;
54 upate kuichukua aibu yako mwenyewe, na kutahayari, kwa sababu ya mambo yote uliyoyatenda, kwa kuwa umekuwa faraja kwao.
55 Na maumbu yako, Sodoma na binti zake, watairudia hali yao ya kwanza, na Samaria na binti zake watairudia hali yao ya kwanza, na wewe na binti zako mtairudia hali yenu ya kwanza.
56 Kwa maana umbu lako, Sodoma, hakutajwa kwa kinywa chako katika siku ya kiburi chako;
57 kabla uovu wako haujafunuliwa bado, kama vile wakati ule walipokutukana binti za Shamu, na wale wote waliomzunguka, binti za Wafilisti wanaokudharau pande zote.
58 Umeuchukua uasherati wako, na machukizo yako, asema Bwana.
59 Maana Bwana MUNGU asema hivi; Nitakutenda vile vile kama ulivyotenda, uliyekidharau kiapo kwa kulivunja agano.
60 Walakini nitalikumbuka agano langu nililolifanya pamoja nawe, katika siku za ujana wako, nami nitaweka imara agano la milele pamoja nawe.
61 Hapo ndipo utakapozikumbuka njia zako, na kutahayarika, hapo utakapowakaribisha maumbu yako, walio wakubwa wako na wadogo wako; nami nitakupa hao wawe binti zako, lakini si kwa agano lako.
62 Nami nitaweka imara agano langu nawe; nawe utajua ya kuwa mimi ndimi Bwana;
63 upate kukumbuka, na kufadhaika, usifumbue kinywa chako tena, kwa sababu ya aibu yako; hapo nitakapokusamehe yote uliyoyatenda, asema Bwana MUNGU.

Ezekieli 17


1 Neno la Bwana likanijia, kusema,
2 Mwanadamu, tega kitendawili, ukawaambie nyumba ya Israeli mithali;
3 useme, Bwana MUNGU asema hivi; Tai mkubwa, mwenye mabawa makubwa na manyoya marefu katika mabawa, mwenye kujaa manyoya, yaliyo ya rangi mbalimbali, alifika Lebanoni, akakitwaa kilele cha mwerezi;
4 akakikata kitawi kilicho juu katika vitawi vyake, akakichukua mpaka nchi ya biashara, akakiweka katika mji wa wachuuzi.
5 Akatwaa tena mbegu katika mbegu za nchi hiyo, akaipanda katika udongo uzaao sana, akaiweka kando ya maji mengi; aliipandikiza kama mti ukuao karibu na mto.
6 Ikakua, ikawa mzabibu wenye kuenea sana, wa kimo kifupi, ambao matawi yake yalimgeukia, na mizizi yake ilikuwa chini yake; basi ukawa mzabibu, ukatoa matawi, ukachipuza vichipuko.
7 Kulikuwa na tai mwingine mkubwa, mwenye mabawa makubwa na manyoya mengi; na tazama, mzabibu huo ukapinda mizizi yake imwelekee yeye, ukachipuza matawi yake yamwelekee yeye, toka matuta yake ulipopandwa; ili yeye apate kuunywesha.
8 Ulikuwa umepandwa katika udongo mwema, kando ya maji mengi, upate kutoa matawi, na kuzaa matunda, uwe mzabibu mzuri.
9 Basi nena wewe, Bwana MUNGU asema hivi; Je! Huo utafanikiwa? Yeye hataing'oa mizizi yake na kuyakata matunda yake, ili ukauke? Kwamba majani mabichi yake yote yachipukayo yakauke, hata ikiwa hana nguvu nyingi, wala watu wengi wa kuung'oa na mizizi yake?
10 Naam, tazama, ingawa umepandwa, je! Utafanikiwa? Hautakauka kabisa, upepo wa mashariki utakapoupiga? Naam, utakauka katika matuta hapo ulipopandwa.
11 Tena neno la Bwana likanijia, kusema,
12 Waambie sasa nyumba hii iliyoasi, Hamjui maana ya mambo haya? Waambie, Tazama, mfalme wa Babeli alifika Yerusalemu, akamtwaa mfalme wake, na wakuu wake, akawachukua pamoja naye mpaka Babeli;
13 akawatwaa baadhi ya wazao wa kifalme; kisha akafanya agano naye, akamwapisha; akawaondoa watu wa nchi wenye nguvu;
14 ili ufalme huo uwe duni usijiinue, lakini usimame kwa kulishika agano lake.
15 Lakini alimwasi kwa kupeleka wajumbe huko Misri, wampe farasi na watu wengi. Je! Atafanikiwa? Afanyaye mambo hayo ataokoka? Atalivunja agano, kisha akaokoka?
16 Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, hakika mahali pale akaapo mfalme aliyemmilikisha, ambaye alikidharau kiapo chake, na kulivunja agano lake, ndipo atakapokufa pamoja naye kati ya Babeli.
17 Wala Farao na jeshi lake kubwa, na kusanyiko lake kuu la watu, hawatamfaa kitu vitani, watakapofanya maboma, na kujenga ngome, ili kukatilia mbali watu wengi.
18 Kwa maana amekidharau kiapo kwa kulivunja agano; na tazama, ametia mkono wake, na pamoja na hayo ameyatenda mambo hayo yote; hataokoka.
19 Basi Bwana MUNGU asema hivi; Kama mimi niishivyo, hakika kiapo changu alichokidharau, na agano langu alilolivunja, nitampatiliza kichwani pake.
20 Nami nitatandika wavu wangu juu yake, naye atanaswa katika mtego wangu, nami nitamleta hata Babeli; nami nitateta naye huko kwa sababu ya kosa lake alilonikosa.
21 Na wakimbizi wake wote wa vikosi vyake vyote wataanguka kwa upanga, na hao watakaosalia watatawanyika kwenye kila upepo; nanyi mtajua ya kuwa mimi, Bwana, nimenena neno hili.
22 Bwana MUNGU asema hivi; Mimi nami nitakitwaa kilele kirefu cha mwerezi, na kukipandikiza mahali; na katika vitawi vyake vilivyo juu nitatwaa kitawi kimoja kilicho chororo, nami nitakipanda juu ya mlima mrefu ulioinuka sana;
23 juu ya mlima wa mahali palipoinuka pa Israeli nitakipanda; nacho kitatoa matawi, na kuzaa matunda, nao utakuwa mwerezi mzuri; na chini yake watakaa ndege wa kila namna ya mbawa; katika uvuli wa matawi yake watakaa.
24 Na miti yote ya mashamba itajua ya kuwa mimi, Bwana, nimeushusha chini mti mrefu, na kuuinua mti mfupi, na kuukausha mti mbichi, na kuusitawisha mti mkavu; mimi, Bwana, nimenena, nami nimelitenda jambo hili.

Ezekieli 18


1 Neno la Bwana likanijia tena, kusema,
2 Je! Maana yake ni nini hata mkatumia mithali hii katika Israeli, mkisema, Baba wamekula zabibu mbichi, nao watoto wakatiwa ganzi la meno?
3 Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, hamtakuwa na sababu ya kuitumia tena mithali hii katika Israeli.
4 Tazama, roho zote ni mali yangu; kama vile roho ya baba ni mali yangu, ndivyo ilivyo roho ya mwana mali yangu; roho ile itendayo dhambi itakufa.
5 Bali kama mtu ni mwenye haki, na kuyatenda yaliyo halali na haki;
6 hakula juu ya milima, wala hakuviinulia macho vinyago vya nyumba ya Israeli, wala hakumtia unajisi mke wa jirani yake, wala hakumkaribia mwanamke wakati wa kutengwa kwake;
7 wala hakumdhulumu mtu, bali amemrudishia mdeni wake rehani yake, wala hakumnyang'anya mtu mali yake kwa nguvu, naye amewapa wenye njaa chakula chake, na kuwavika nguo walio uchi;
8 ambaye hakumkopesha mtu ili apate faida, wala hakupokea ziada ya namna yo yote; naye ameuepusha mkono wake na uovu, na kufanya hukumu ya haki kati ya mtu na mwenzake;
9 tena ikiwa amezifuata sheria zangu, na kuzishika hukumu zangu; mtu huyu ni mwenye haki; hakika ataishi, asema Bwana MUNGU.
10 Walakini akizaa mwana aliye mnyang'anyi, mmwaga damu, atendaye mambo hayo mojawapo;
11 wala hakutenda mojawapo la mambo hayo yampasayo, bali amekula juu ya milima, na kumtia unajisi mke wa jirani yake,
12 na kuwadhulumu maskini na wahitaji, na kuwanyang'anya watu mali yao kwa nguvu, wala hakurudisha rehani, naye ameviinulia macho vinyago, na kufanya machukizo,
13 naye amekopesha watu ili apate faida, na kupokea ziada; je! Ataishi baada ya hayo? La, hataishi; amefanya machukizo hayo yote; hakika atakufa; damu yake itakuwa juu yake.
14 Na kama yeye huyo akizaa mwana, naye ameona dhambi zote za baba yake alizozitenda, akaogopa, asifanye neno lo lote kama hayo;
15 hakula juu ya milima, wala hakuviinulia macho vinyago vya nyumba ya Israeli, wala hakumtia unajisi mke wa jirani yake,
16 wala hakumdhulumu mtu, wala hakutwaa kitu kiwekwe rehani, wala hakumnyang'anya mtu mali yake kwa nguvu, bali amewapa wenye njaa chakula chake, na kuwafunika nguo walio uchi;
17 tena ikiwa ameuzuia mkono wake asimwonee maskini, wala hakupokea faida na ziada, naye amezifanya hukumu zangu, na kuzifuata sheria zangu; hatakufa huyu kwa sababu ya uovu wa baba yake, hakika ataishi.
18 Kwa habari za yule baba yake, kwa sababu aliwaonea watu kwa ukali mwingi, na kumnyang'anya ndugu yake mali yake kwa nguvu; na kuyatenda yasiyo mema kati ya watu wake, tazama, atakufa katika uovu wake.
19 Lakini ninyi mwasema, Kwani yule mwana asiuchukue uovu wa baba yake? Yule mwana atakapofanya yaliyo halali na haki, na kuzishika amri zangu na kuzitenda, hakika ataishi.
20 Roho itendayo dhambi, ndiyo itakayokufa; mwana hatauchukua uovu wa baba yake, wala baba hatauchukua uovu wa mwanawe, haki yake mwenye haki itakuwa juu yake, na uovu wake mwenye uovu utakuwa juu yake.
21 Lakini mtu mbaya akighairi, na kuacha dhambi zake zote alizozitenda, na kuzishika amri zangu zote, na kutenda yaliyo halali na haki, hakika ataishi, hatakufa.
22 Dhambi zake zote alizozitenda hazitakumbukwa juu yake hata mojawapo; katika haki yake aliyoitenda ataishi.
23 Je! Mimi ninafurahia kufa kwake mtu mwovu? Asema Bwana MUNGU; si afadhali kwamba aghairi, na kuiacha njia yake, akaishi?
24 Bali mwenye haki atakapoghairi, na kuiacha haki yake, na kutenda uovu, na kufanya machukizo yote kama yale afanyayo mtu mwovu, je, ataishi? Katika matendo yake yote ya haki aliyoyatenda halitakumbukwa hata mojawapo. Katika kosa lile alilolikosa, naam, katika dhambi yake aliyoitenda, atakufa.
25 Lakini ninyi mwasema, Njia ya Bwana si sawa. Sikilizeni sasa, Enyi nyumba ya Israeli; Je! Njia yangu siyo iliyo sawa? Njia zenu sizo zisizo sawa?
26 Mwenye haki atakapoghairi, na kuiacha haki yake, na kutenda uovu, akafa katika uovu huo; katika uovu wake alioutenda atakufa.
27 Tena, mtu mwovu atakapoghairi, na kuuacha uovu wake alioutenda, na kutenda yaliyo halali na haki, ataponya roho yake, nayo itakuwa hai.
28 Kwa sababu atafakari, na kughairi, na kuyaacha makosa yake yote aliyoyatenda, hakika ataishi, hatakufa.
29 Lakini nyumba ya Israeli husema, Njia ya Bwana si sawa. Ee nyumba ya Israeli, je! Njia zangu sizo zilizo sawa? Njia zenu sizo zisizo sawa?
30 Basi, nitawahukumu ninyi, nyumba ya Israeli, kila mmoja kwa kadiri ya njia zake, asema Bwana MUNGU. Rudini, mkaghairi, na kuyaacha makosa yenu yote; basi hivyo uovu wenu hautakuwa uharibifu wenu.
31 Tupilieni mbali nanyi makosa yenu yote mliyoyakosa; jifanyieni moyo mpya na roho mpya; mbona mnataka kufa, enyi nyumba ya Israeli?
32 Maana mimi sikufurahii kufa kwake afaye, asema Bwana MUNGU; basi ghairini, mkaishi.

Ezekieli 19


1 Tena uwaombolezee wakuu wa Israeli,
2 useme, Mama yako alikuwa nini? Simba mke; alijilaza kati ya simba, kati ya wana-simba aliwalisha watoto wake.
3 Akamlea mtoto mmoja katika watoto wake, akawa mwana-simba, akajifunza kuwinda mawindo, akala watu.
4 Mataifa nao wakapata habari zake, akanaswa katika rima lao, wakamchukua kwa kulabu mpaka nchi ya Misri.
5 Basi mamaye alipoona kwamba amemngoja, na tumaini lake limepotea, akatwaa mtoto mwingine katika watoto wake, akamfanya mwana-simba.
6 Naye akaenda huko na huko kati ya simba, akawa mwana-simba, akajifunza kuwinda mawindo, akala watu.
7 Akayajua majumba yao, akaiharibu miji yao; nchi ikawa ukiwa, navyo vitu vilivyoijaza, kwa sababu ya mshindo wa kunguruma kwake.
8 Ndipo mataifa wakajipanga juu yake pande zote toka nchi zote; wakaunda wavu wao juu yake; akanaswa katika rima lao.
9 Wakamtia katika tundu kwa kulabu, wakamleta kwa mfalme wa Babeli wakamtia ndani ya ngome, sauti yake isisikiwe tena juu ya milima ya Israeli.
10 Mama yako alikuwa kama mzabibu, katika damu yako, uliopandwa karibu na maji; akazaa sana na kujaa matawi, kwa sababu ya maji mengi.
11 Naye alikuwa na vijiti vya nguvu, kwa fimbo za enzi zao watawalao, na kimo chao kiliinuka kati ya matawi manene, wakaonekana kwa urefu wao, pamoja na wingi wa matawi yao.
12 Lakini aling'olewa kwa ghadhabu, akaangushwa chini, upepo wa mashariki ukakausha matunda yake; vijiti vyake vya nguvu vikavunjika, vikakauka; moto ulivila.
13 Na sasa umepandwa jangwani, katika nchi kavu, ya ukame.
14 Na moto umetoka katika vijiti vya matawi yake, umekula matunda yake, hata hana tena kijiti cha nguvu kifaacho kwa fimbo ya enzi ya kutawala. Na hayo ni maombolezo, nayo yatakuwa maombolezo.

Ezekieli 20


1 Ikawa katika mwaka wa saba, mwezi wa tano, siku ya kumi ya mwezi, baadhi ya wazee wa Israeli walikuja ili kuuliza kwa Bwana, wakaketi mbele yangu.
2 Neno la Bwana likanijia, kusema,
3 Mwanadamu, sema na wazee wa Israeli, uwaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Je! Mmekuja kuniuliza neno? Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, sitaulizwa neno na ninyi.
4 Je! Utawahukumu, mwanadamu, utawahukumu? Uwajulishe machukizo ya baba zao;
5 uwaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Katika siku ile nilipochagua Israeli, na kuwainulia wazao wa nyumba ya Yakobo mkono wangu, na kujidhihirisha kwao katika nchi ya Misri, hapo nilipowainulia mkono wangu, nikisema, Mimi ni Bwana, Mungu wenu;
6 katika siku ile naliwainulia mkono wangu, kuwatoa katika nchi ya Misri, na kuwaingiza katika nchi niliyowapelelezea, ijaayo maziwa na asali, ambayo ni utukufu wa nchi zote;
7 nikawaambia, Kila mtu kwenu na atupilie mbali machukizo ya macho yake, wala msijitie unajisi kwa vinyago vya Misri, Mimi ni Bwana, Mungu wenu.
8 Lakini waliniasi, wala hawakutaka kunisikiliza; hawakutupilia mbali kila mtu machukizo ya macho yake, wala hawakuviacha vinyago vya Misri; ndipo nikasema kwamba nitamwaga ghadhabu yangu juu yao, ili kuitimiza hasira yangu juu yao, katikati ya nchi ya Misri.
9 Lakini nalitenda kwa ajili ya jina langu, ili lisitiwe unajisi mbele ya macho ya mataifa, ambao walikaa pamoja nao, ambao machoni pao nalijidhihirisha kwao, kwa kuwatoa katika nchi ya Misri.
10 Basi nikawatoa katika nchi ya Misri, nikawaleta jangwani.
11 Nikawapa amri zangu, na kuwaonyesha hukumu zangu, ambazo mwanadamu ataishi kwazo, kama akizitenda.
12 Tena naliwapa sabato zangu, ziwe ishara kati ya mimi na wao, wapate kujua ya kuwa mimi, Bwana, ndimi niwatakasaye.
13 Lakini nyumba ya Israeli waliniasi jangwani; hawakuenda katika amri zangu, wakazikataa hukumu zangu, ambazo mwanadamu ataishi kwazo, kama akizitenda; na sabato zangu walizitia unajisi sana; ndipo nikasema, Nitamwaga hasira yangu juu yao jangwani, ili niwaangamize.
14 Lakini nalitenda kwa ajili ya jina langu, lisitiwe unajisi machoni pa mataifa, ambao naliwatoa mbele ya macho yao.
15 Tena naliwainulia mkono wangu jangwani, ya kwamba sitawaingiza katika nchi ile niliyokuwa nimewapa, ijaayo maziwa na asali, ambayo ni utukufu wa nchi zote;
16 kwa sababu walizikataa hukumu zangu, wala hawakuenda katika amri zangu, wakazitia unajisi sabato zangu, kwa maana mioyo yao iliandama vinyago vyao.
17 Walakini jicho langu likawahurumia nisiwaangamize kabisa, wala sikuwakomesha kabisa jangwani.
18 Kisha nikawaambia watoto wao jangwani, Msiende katika amri za baba zenu, wala msizishike hukumu zao, wala msijitie unajisi kwa vinyago vyao.
19 Mimi ni Bwana, Mungu wenu; endeni katika amri zangu, mkazishike hukumu zangu, na kuzitenda;
20 zitakaseni sabato zangu; zitakuwa ishara kati ya mimi na ninyi, mpate kujua ya kuwa mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.
21 Lakini watoto hao waliniasi; hawakuenda katika amri zangu, wala hawakuzishika hukumu zangu kuzitenda, ambazo mwanadamu ataishi kwazo kama akizitenda; walizitia unajisi sabato zangu, ndipo nikasema, kwamba nitamwaga ghadhabu yangu juu yao, ili kuitimiza hasira yangu juu yao jangwani.
22 Lakini naliuzuia mkono wangu, nikatenda kwa ajili ya jina langu, lisitiwe unajisi mbele ya macho ya mataifa, ambao mbele ya macho yao naliwatoa.
23 Tena naliwainulia mkono wangu jangwani, kwamba nitawatawanya kati ya mataifa, na kuwatapanya katika nchi mbalimbali;
24 kwa sababu hawakuzitekeleza hukumu zangu, bali walizikataa amri zangu, nao walizitia unajisi sabato zangu, na macho yao yaliandama vinyago vya baba zao.
25 Tena naliwapa amri zisizokuwa njema, na hukumu ambazo hawakuweza kuishi kwazo;
26 nami nikawatia unajisi kwa matoleo yao wenyewe, kwa kuwa walipitisha motoni wote waliofungua tumbo; ili kuwafanya kuwa ukiwa, wakapate kujua ya kuwa mimi ndimi Bwana.
27 Basi, mwanadamu, sema na nyumba ya Israeli, uwaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Baba zenu wamenitukana kwa jambo hili, kwa kuwa wamekosa kosa juu yangu.
28 Kwa maana nilipokuwa nimekwisha kuwaingiza katika nchi ile, ambayo naliuinua mkono wangu kuwapa, wakati huo walipoona kila mlima mrefu, na kila mti wenye majani mengi, walitoa matoleo yao huko, na huko walitoa chukizo la sadaka zao, na huko walifanya nukato la kupendeza, na huko walimimina sadaka zao za kunywewa.
29 Ndipo nikawauliza, Nini maana yake mahali palipoinuka mnapopaendea? Basi, jina lake mahali pale ni Bama hata leo.
30 Basi, uwaambie nyumba ya Israeli, Bwana MUNGU asema hivi; Je! Mnajitia unajisi kwa kuzifuata njia za baba zenu? Mnakwenda kufanya uasherati kwa kuyafuata machukizo yao?
31 Tena mtoapo matoleo yenu, na kuwapitisha watoto wenu motoni, je! Mnajitia unajisi kwa vinyago vyenu vyote hata leo? Na mimi je! Niulizwe neno nanyi, Enyi nyumba ya Israeli? Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, sitaulizwa neno na ninyi.
32 Na haya yote yaingiayo katika nia zenu hayatakuwa kamwe; ikiwa mmesema, Sisi tutakuwa sawasawa na mataifa, sawasawa na jamaa za nchi nyingine, kutumikia miti na mawe.
33 Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, hakika kwa mkono hodari, na kwa mkono ulionyoshwa, na kwa ghadhabu iliyomwagika, nitakuwa mfalme juu yenu;
34 nami nitawatoa katika mataifa, na kuwakusanya, na kuwatoa katika nchi mlizotawanyika ndani yake, kwa mkono hodari, na kwa mkono ulionyoshwa, na kwa ghadhabu iliyomwagika;
35 nami nitawaingiza katika jangwa la mataifa, na huko ndiko nitakakoteta nanyi uso kwa uso.
36 Kama nilivyoteta na baba zenu katika jangwa la Misri, ndivyo nitakavyoteta nanyi, asema Bwana MUNGU.
37 Nami nitawapitisha chini ya fimbo, nami nitawaingiza katika mafungo ya agano.
38 Nami nitawasafisha kwa kuwatoa waasi, na hao walionikosa; nitawatoa katika nchi wanayokaa ugenini, lakini hawataingia katika nchi ya Israeli; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.
39 Na katika habari zenu, enyi nyumba ya Israeli, Bwana MUNGU asema hivi, Enendeni, mkavitumikie vinyago vyenu kila mmoja wenu; na wakati wa baadaye pia, kama hamtaki kunisikiliza; lakini jina langu takatifu hamtalitia unajisi tena, kwa matoleo yenu, na kwa vinyago wenu.
40 Kwa maana katika mlima wangu mtakatifu, katika mlima mrefu sana wa Israeli, asema Bwana MUNGU, ndiko watakakonitumikia nyumba yote ya Israeli, wote pia katika nchi ile; nami nitawatakabali huko, na huko nitataka matoleo yenu, na malimbuko ya dhabihu zenu, pamoja na vitu vyenu vitakatifu vyote.
41 Nitawatakabali kama harufu ipendezayo, nitakapowatoa katika mataifa, na kuwakusanya toka nchi zile mlizotawanyika; nami nitatakaswa kwenu machoni pa mataifa.
42 Nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, nitakapowaingiza katika nchi ya Israeli, katika nchi ile ambayo niliuinua mkono wangu kwamba nitawapa baba zenu.
43 Na huko mtazikumbuka njia zenu, na matendo yenu yote, ambayo mmejitia unajisi kwayo; nanyi mtajichukia katika macho yenu wenyewe, kwa sababu ya maovu yenu yote mliyoyatenda.
44 Nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, nitakapokuwa nimetenda nanyi kwa ajili ya jina langu, si sawasawa na njia zenu mbaya, wala si sawasawa na matendo yenu mabovu, enyi nyumba ya Israeli, asema Bwana MUNGU.
45 Neno la Bwana likanijia, kusema,
46 Mwanadamu, uelekeze uso wako kusini, ukadondoze neno lako upande wa kusini, ukatabiri juu ya msitu wa uwanda wa Negebu,
47 ukauambie msitu wa Negebu, Lisikie neno la Bwana; Bwana MUNGU asema hivi; Tazama nitawasha moto ndani yako, nao utakula kila mti mbichi ndani yako, na kila mti mkavu; miali ya moto ule haitazimika, na nyuso zote toka kusini hata kaskazini zitateketezwa kwa moto huo.
48 Na watu wote wenye mwili wataona ya kuwa mimi, Bwana, nimeuwasha; hautazimika.
49 Ndipo nikasema, Ee Bwana MUNGU, wao hunisema; Je! Mtu huyu si mtu mwenye kupiga mithali?

Ezekieli 21


1 Neno la Bwana likanijia, kusema,
2 Mwanadamu, uelekeze uso wako kuelekea Yerusalemu, ukadondoze neno lako upande wa mahali patakatifu, ukatabiri juu ya nchi ya Israeli;
3 uiambie nchi ya Israeli, Bwana asema hivi; Tazama, mimi ni juu yako, nami nitautoa upanga wangu alani, nami nitamkatilia mbali nawe mtu mwenye haki na mtu mbaya.
4 Basi, kwa kuwa nitamkatilia mbali nawe mtu mwenye haki na mtu mbaya, upanga wangu utatoka alani mwake, uwe juu ya watu wote wenye mwili toka kusini hata kaskazini,
5 na watu wote wenye mwili watajua ya kuwa mimi, Bwana, nimeufuta upanga wangu alani mwake; hautarudi tena.
6 Ugua, basi, Ee mwanadamu; kwa kuvunjika kwake viuno vyako, na kwa uchungu, utaugua mbele ya macho yao.
7 Na itakuwa, wakuambiapo, Mbona unaugua? Ndipo utakaposema, Kwa sababu ya habari hizo, maana linakuja; na kila moyo utayeyuka, na mikono yote itakuwa dhaifu, na kila roho itazimia, na magoti yote yatalegea kama maji; tazama, linakuja, nalo litatendeka, asema Bwana MUNGU.
8 Neno la Bwana likanijia, kusema,
9 Mwanadamu, tabiri, useme, Bwana asema hivi; Nena, Upanga, upanga, umenolewa na kusuguliwa,
10 umenolewa ili kufanya machinjo; umesuguliwa ili uwe kama umeme; basi je! Tufanye furaha? Upanga unadharau fimbo ya mwanangu, kama unavyodharau kila mti.
11 Nao umenolewa usuguliwe, upate kushikwa mkononi; upanga umenolewa, naam, umesuguliwa, ili kutiwa katika mkono wake auaye.
12 Piga kelele, utoe sauti ya uchungu, Ee mwanadamu, kwa maana upanga u juu ya watu wangu, u juu ya wakuu wote wa Israeli; wametolewa wauawe na upanga pamoja na watu wangu, basi, jipige pajani.
13 Kwa maana kuna kujaribiwa; itakuwaje, basi, ikiwa upanga unaidharau hiyo fimbo? Haitakuwapo tena; asema Bwana MUNGU.
14 Basi, wewe mwanadamu, tabiri, ukapige makofi; upanga huo na uongezwe mara mbili, hata mara tatu; upanga wao waliotiwa jeraha kiasi cha kuwaua; ni upanga wa mkuu aliyetiwa jeraha kiasi cha kumwua; uwazungukao pande zote.
15 Nimeweka ncha ya upanga huo juu ya malango yao yote, ili mioyo yao iyeyuke, yakaongezeke makwazo yao; aha! Umefanywa kuwa kama umeme, umenolewa, ili uchinje.
16 Jiweke tayari, enenda upande wa kuume; jipange, enenda upande wa kushoto; mahali po pote utakapouelekeza uso wako.
17 Mimi nami nitapiga makofi, mimi nami nitashibisha ghadhabu yangu; mimi, Bwana, nimenena neno hili.
18 Neno la Bwana likanijia tena, kusema,
19 Tena, mwanadamu, ujiwekee njia mbili, upanga wa mfalme wa Babeli upate kuja; hizo mbili zitatoka katika nchi moja; ukaandike mahali, upaandike penye kichwa cha njia iendayo mjini.
20 Utaagiza njia, upanga upate kufikilia Raba wa wana wa Amoni, na kufikilia Yuda katika Yerusalemu, wenye maboma.
21 Maana mfalme wa Babeli alisimama penye njia panda, penye kichwa cha njia hizo mbili, ili atumie uganga; aliitikisa mishale huko na huko, akaziuliza terafi, akayatazama maini.
22 Katika mkono wake wa kuume alikuwa na kura ya Yerusalemu, kuviweka vyombo vya kubomolea, kufumbua kinywa katika machinjo, kuiinua sauti kwa kupiga kelele sana, kuweka vyombo vya kubomolea juu ya malango, kufanya maboma, na kujenga ngome.
23 Jambo hili litakuwa kwao kama uganga wa ubatili, mbele ya macho yao waliowaapia viapo lakini ataufanya uovu ukumbukwe, ili kwamba wakamatwe.
24 Basi Bwana MUNGU asema hivi; Kwa kuwa mmeufanya uovu wenu ukumbukwe, kwa maana makosa yenu yamefunuliwa, hata dhambi zenu zikaonekana kwa matendo yenu; kwa sababu mmekumbukwa, mtakamatwa kwa mkono.
25 Na wewe, Ewe mtu mwovu, uliyetiwa jeraha kiasi cha kukuua, mkuu wa Israeli, ambaye siku yako imekuja, katika wakati wa uovu wa mwisho;
26 Bwana MUNGU asema hivi; Kiondoe kilemba, ivue taji; haya hayatakuwa tena kama yalivyo; kikweze kilicho chini, kakishushe kilichoinuka.
27 Nitakipindua, nitakipindua, nitakipindua; hiki nacho hakitakuwa tena, hata atakapokuja yeye ambaye ni haki yake; nami nitampa.
28 Nawe, mwanadamu, tabiri useme, Bwana MUNGU asema hivi, katika habari za wana wa Amoni, na katika habari za aibu yao; Nena, Upanga; upanga umefutwa; umesuguliwa, ili kuua, ili kuufanya uue sana, upate kuwa kama umeme;
29 wakati wakuoneapo ubatili, wakati wakufanyiao uganga wa uongo, ili kukuweka juu ya shingo zao waliotiwa jeraha kiasi cha kuwaua, ambao siku yao imekuja, katika wakati wa uovu wa mwisho.
30 Uurudishe alani mwake. Mahali pale ulipoumbwa, katika nchi uliyozaliwa; nitakuhukumu wewe.
31 Nami nitamwaga ghadhabu yangu juu yako; nitakupulizia moto wa hasira yangu; nami nitakutia katika mikono ya watu walio kama hayawani, wajuao sana kuangamiza.
32 Utakuwa kuni za kutiwa motoni; damu yako itakuwa katikati ya nchi; hutakumbukwa tena; maana mimi, Bwana, nimenena neno hili.

Ezekieli 22


1 Neno la Bwana likanijia tena, kusema,
2 Na wewe, mwanadamu, je! Utauhukumu, utauhukumu mji huu wa damu? Basi uujulishe machukizo yake yote.
3 Nawe utasema, Bwana MUNGU asema hivi; Mji umwagao damu ndani yake, ili wakati wake upate kuja; mji ufanyao vinyago juu ya nafsi yake, ili ujitie unajisi!
4 Umekuwa na hatia katika damu yako uliyomwaga, nawe umekuwa na unajisi kwa vinyago vyako ulivyovifanya; nawe umezileta karibu siku zako, nawe umefika karibu na miaka yako; basi, kwa sababu ya hayo, nimekufanya kuwa lawama kwa mataifa, na kuwa dhihaka katika nchi zote.
5 Zilizo karibu, na zilizo mbali nawe, zitakudhihaki, Ewe mchafu, uliyejaa fujo.
6 Tazama, wakuu wa Israeli, kila mmoja kwa kadiri ya nguvu zake, wamekuwamo ndani yako, ili kumwaga damu.
7 Ndani yako wamedharau baba na mama; kati yako wamewatenda wageni udhalimu; ndani yako wamewaonea yatima na mjane.
8 Umevidharau vitu vyangu vitakatifu, umezitia unajisi sabato zangu.
9 Wasingiziaji wamekuwamo ndani yako, ili kumwaga damu; na ndani yako wamekula juu ya milima; kati yako wamefanya uasherati.
10 Ndani yako wamefunua uchi wa baba zao; ndani yako wamemfanyia nguvu mwanamke asiye safi wakati wa kutengwa kwake.
11 Na mtu mmoja amefanya chukizo pamoja na mke wa jirani yake; na mtu mwingine amemharibu mke wa mwanawe kwa uasherati; na mtu mwingine ndani yako amemfanyia nguvu umbu lake, binti ya babaye.
12 Ndani yako wamepokea rushwa ili kumwaga damu; umepokea riba na faida; nawe kwa choyo umepata mapato kwa kuwadhulumu jirani zako, nawe umenisahau mimi, asema Bwana MUNGU.
13 Basi, tazama, nimeipigia kofi hiyo faida uliyopata kwa njia isiyo haki, na hiyo damu yako iliyokuwa kati yako.
14 Je! Moyo wako waweza kuvumilia, au mkono wako waweza kuwa hodari, katika siku zile nitakapokutenda mambo? Mimi, Bwana, nimenena neno hili, tena nitalitenda.
15 Nami nitakutawanya kati ya mataifa, na kukutapanya kati ya nchi mbalimbali; nami nitauteketeza uchafu wako, ili ukutoke.
16 Nawe utatiwa unajisi ndani ya nafsi yako, mbele ya macho ya mataifa; nawe utajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.
17 Neno la Bwana likanijia, kusema,
18 Mwanadamu, nyumba ya Israeli imekuwa taka za fedha kwangu; wote wamekuwa shaba, na bati, na chuma, na risasi, kati ya tanuu; wamekuwa taka za fedha.
19 Basi Bwana MUNGU asema hivi; Kwa sababu ninyi nyote mmekuwa taka za fedha, tazama, nitawakusanya kati ya Yerusalemu.
20 Kama vile watu wakusanyavyo fedha, na shaba, na chuma, na risasi, na bati, kati ya tanuu, ili kuvifukutia moto na kuviyeyusha; ndivyo nitakavyowakusanya ninyi katika hasira yangu, na ghadhabu yangu, nami nitawalaza huko, na kuwayeyusha.
21 Naam, nitawakusanya, na kuwafukutia moto wa ghadhabu yangu, nanyi mtayeyushwa kati yake.
22 Kama fedha iyeyushwavyo kati ya tanuu, ndivyo mtakavyoyeyushwa kati yake; nanyi mtajua ya kuwa mimi, Bwana, nimemwaga ghadhabu yangu juu yenu.
23 Neno la Bwana likanijia, kusema,
24 Mwanadamu, uiambie nchi, Wewe u nchi isiyosafika, wala kunyeshewa mvua siku ya ghadhabu.
25 Fitina ya manabii wake imo ndani yake, kama simba angurumaye akirarua mawindo; wamekula roho za watu; hutwaa kwa nguvu hazina na vitu vya thamani; wameongeza hesabu ya wajane wake ndani yake.
26 Makuhani wake wameihalifu sheria yangu, wametia unajisi vitu vyangu vitakatifu; hawakuweka tofauti ya vitu vitakatifu na vitu vya kutumiwa sikuzote; wala hawakuwafundisha watu kupambanua vitu vichafu na vitu vilivyo safi, nao wamefumba macho yao, wasiziangalie sabato zangu, nami nimetiwa unajisi kati yao.
27 Wakuu wake kati yake wamekuwa kama mbwa-mwitu wakirarua mawindo; ili kumwaga damu, na kuharibu roho za watu, wapate faida kwa njia isiyo halali.
28 Na manabii wake wamewapakia chokaa isiyokorogwa vema, wakiona ubatili, na kuwatabiria maneno ya uongo, wakisema, Bwana MUNGU asema hivi; iwapo Bwana hakusema neno.
29 Watu wa nchi wametumia udhalimu, wamenyang'anya kwa nguvu; naam, wamewatenda jeuri maskini na wahitaji, nao wamewaonea wageni bila haki.
30 Nami nikatafuta mtu miongoni mwao, atakayelitengeneza boma, na kusimama mbele zangu mahali palipobomoka, kwa ajili ya nchi, nisije nikaiharibu, lakini sikuona mtu.
31 Kwa sababu hiyo nimemwaga ghadhabu yangu juu yao; nimewateketeza kwa moto wa hasira yangu; nami nimeileta njia yao wenyewe juu ya vichwa vyao, asema Bwana MUNGU.

Ezekieli 23


1 Neno la Bwana likanijia tena, kusema,
2 Mwanadamu, palikuwa na wanawake wawili, binti za mama mmoja;
3 nao walizini huko Misri; walizini wakati wa ujana wao; huko vifua vyao vililemewa, na huko waliyabana matiti ya ubikira wao.
4 Na majina yao, mkubwa aliitwa Ohola, na umbu lake Oholiba; wakawa wangu, wakazaa wana na binti. Na katika hayo majina yao, Samaria ni Ohola, na Yerusalemu ni Oholiba.
5 Na Ohola alifanya mambo ya kikahaba alipokuwa wangu; naye alipenda mno wapenzi wake, Waashuri, jirani zake,
6 waliovikwa samawi, maliwali na mawaziri, wote vijana wa kutamanika, wapanda farasi wakipanda farasi zao.
7 Akawagawia mambo yake ya kikahaba, watu wateule wa Ashuru, wote pia; akajitia unajisi kwa vinyago vyote vya kila mmoja wa hao aliowapenda.
8 Wala hakuyaacha mambo yake ya kikahaba tangu siku za Misri, kwa maana wakati wa ujana wake walilala naye, wakayabana matiti ya ubikira wake wakamwaga uzinzi wao juu yake.
9 Kwa sababu hiyo nalimtia katika mikono ya wapenzi wake, katika mikono ya Waashuri, aliowapendelea.
10 Na hawa wakaufunua uchi wake, wakatwaa wanawe na binti zake, wakamwua yeye kwa upanga; akawa jina la aibu kati ya wanawake; kwa maana walitoa hukumu juu yake.
11 Na umbu lake, Oholiba, akayaona hayo walakini alizidi kuharibika kuliko yeye, kwa kupendelea kwake, na kwa uzinzi wake, uliokuwa mwingi kuliko uzinzi wa umbu lake.
12 Aliwapendelea Waashuri, maliwali na mawaziri, jirani zake, waliovikwa nguo za shani, wapanda farasi wakipanda farasi zao, wote pia vijana wa kutamanika.
13 Nikaona ya kuwa ametiwa unajisi; wote wawili walifuata njia moja.
14 Naye akaongeza uzinzi wake; kwa maana aliona watu waume, ambao sura zao zimeandikwa ukutani, sura za Wakaldayo zilizoandikwa kwa rangi nyekundu;
15 waliofungiwa mikumbuu viunoni mwao, na vilemba vilivyotiwa rangi vichwani mwao; wote wakuu wa kuangaliwa, kwa mfano wa wana wa Babeli katika Ukaldayo, katika nchi ya kuzaliwa kwao.
16 Na mara alipowaona aliwapendelea, akatuma wajumbe kwao hata Ukaldayo.
17 Na watu wa Babeli wakamwendea katika kitanda cha mapenzi, wakamtia unajisi kwa uzinzi wao, akatiwa unajisi nao, kisha roho yake ikafarakana nao.
18 Basi alifunua uzinzi wake, na kufunua uchi wake; ndipo roho yangu ikafarakana naye, kama ilivyofarakana na umbu lake.
19 Lakini aliongeza uzinzi wake, akikumbuka siku za ujana wake, alipofanya mambo ya kikahaba katika nchi ya Misri.
20 Akawapendelea wapenzi wao, ambao nyama ya mwili wao ni kama nyama ya mwili wa punda, nacho kiwatokacho ni kama kiwatokacho farasi.
21 Ndivyo ulivyokumbuka uasherati wa ujana wako, yalipobanwa matiti yako na Wamisri, kwa maziwa ya ujana wako.
22 Kwa sababu hiyo, Ewe Oholiba, Bwana MUNGU asema hivi, Tazama, nitawainua wapenzi wako juu yako, ambao roho yako imefarakana nao, nami nitawaleta juu yako pande zote;
23 watu wa Babeli, na Wakaldayo wote, Pekodi na Shoa na Koa, na Waashuri wote pamoja nao; vijana wa kutamanika, wote pia, maliwali na mawaziri, wakuu, na watu wenye sifa, wote wenye kupanda farasi.
24 Nao watakuja kwako na silaha zao, na magari ya vita, na magurudumu, na wingi wa mataifa; watajipanga juu yako kwa ngao, na vigao, na chapeo za shaba, pande zote; nami nitawapa uwezo wa kuhukumu, nao watakuhukumu sawasawa na hukumu zao.
25 Nami nitaweka wivu wangu juu yako, nao watakutenda mambo kwa ghadhabu; watakuondolea pua yako na masikio yako; na mabaki yako wataanguka kwa, upanga; watawatwaa wanao na binti zako; na mabaki yako watateketea motoni.
26 Pia watakuvua nguo zako, na kukuondolea vyombo vyako vya uzuri.
27 Hivyo ndivyo nitakavyoukomesha uasherati wako, na uzinzi wako, ulioletwa toka nchi ya Misri; usije ukawainulia macho yako, na kukumbuka Misri tena.
28 Maana Bwana MUNGU asema hivi, Tazama nitakutia katika mikono yao unaowachukia, katika mikono yao, ambao roho imefarakana nao;
29 nao watakutenda mambo kwa chuki, watakuondolea kazi zako zote, watakuacha uchi, huna nguo na aibu ya mambo yako ya kikahaba itafunuliwa, uasherati wako na uzinzi wako.
30 Utatendwa mambo hayo kwa sababu umezini na hao wasioamini, na kwa sababu umetiwa unajisi kwa vinyago vyao.
31 Umekwenda katika njia ya umbu lako; basi nitatia kikombe chake katika mkono wako.
32 Bwana MUNGU asema hivi; Utakinywea kikombe cha umbu lako; chenye nafasi nyingi kikubwa; utadhihakiwa na kudharauliwa; kimejaa sana.
33 Utajazwa ulevi na sikitiko, kwa kikombe cha ushangao na ukiwa, kikombe cha umbu lako Samaria.
34 Naam, utakinywea hata hakitabaki kitu ndani yake, utavitafuna vigae vyake, utayararua maziwa yako; maana mimi, Bwana MUNGU, nimenena neno hili.
35 Basi Bwana MUNGU asema hivi; Kwa kuwa umenisahau, na kunitupa nyuma yako, basi kwa hiyo, uchukue uasherati wako na uzinzi wako.
36 Tena Bwana akaniambia, Mwanadamu, utawahukumu Ohola na Oholiba? Basi uwahubiri machukizo yao.
37 Maana wamezini, na damu imo mikononi mwao, nao wamezini na vinyago vyao; tena wana wao walionizalia wamewapitisha katika moto ili waliwe nao.
38 Tena wamenitenda haya; wamepatia unajisi mahali pangu patakatifu, siku ile ile, nao wamezitangua sabato zangu.
39 Kwa maana walipokuwa wamekwisha kuvichinjia vinyago vyao watoto wao, ndipo walipoingia patakatifu pangu, siku ile ile, wapatie unajisi, na tazama, wamefanya hivyo kati ya nyumba yangu.
40 Tena mmewatuma watu kuwaita watokao mbali; ambao mjumbe alitumwa kwao, na tazama, wakaja; nawe ulijiosha kwa ajili yao, ulitia rangi macho yako, na kujipamba vyombo vya uzuri;
41 ukaketi juu ya kitanda cha enzi, na meza imeandikwa tayari mbele yake, ambayo juu yake uliweka uvumba wangu na mafuta yangu.
42 Na sauti za wingi wa watu wenye hali ya raha zilikuwa pamoja naye; na pamoja na watu wasio na adabu, waliletwa walevi toka jangwani; wakawatia vikuku mikononi, na taji nzuri juu ya vichwa vyao.
43 Ndipo nikasema, Huyo aliye mkongwe atafanya uzinzi! Sasa hao watazini naye, naam, na yeye!
44 Wakamwingilia kama watu wamwingiliavyo kahaba; ndivyo walivyowaingilia Ohola na Oholiba, wanawake wale waasherati.
45 Basi watu wenye haki watawahukumu, kwa hukumu iwapasayo wazinzi, na kwa hukumu iwapasayo wanawake wamwagao damu; kwa sababu wao ndio wazinzi, na mikononi mwao mna damu.
46 Maana Bwana MUNGU asema hivi; Nitaleta kusanyiko la watu juu yao, nami nitawatoa warushwe huko na huko, na kutekwa nyara.
47 Na kusanyiko hilo watawapiga kwa mawe, na kuwaua kwa panga zao; watawaua wana wao na binti zao, na kuziteketeza nyumba zao kwa moto.
48 Hivyo nitaukomesha uasherati katika nchi hii, ili wanawake wote wafundishwe, wasifanye mambo ya uasherati wenu.
49 Nao watawalipa ninyi malipo ya uasherati wenu, nanyi mtachukua dhambi za vinyago vyenu; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana MUNGU.

Ezekieli 24


1 Tena, katika mwaka wa kenda, mwezi wa kumi, siku ya kumi ya mwezi, neno la Bwana likanijia, kusema,
2 Mwanadamu, liandike jina la siku hii, naam, la siku ii hii; mfalme wa Babeli ameukaribia Yerusalemu siku iyo hiyo.
3 Ukawatungie mithali nyumba ya kuasi, ukawaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Teleka sufuria, liteleke; ukatie maji ndani yake;
4 vikusanye vipande vyake ndani yake, naam, kila kipande chema, paja na bega; lijaze mifupa iliyochaguliwa.
5 Uwatwae wateule wa kundi la kondoo, ukafanye chungu ya mifupa chini yake; ukalitokose sana; naam, mifupa yake itokoswe ndani yake.
6 Basi Bwana MUNGU asema hivi; Ole wake mji wa damu! Hilo sufuria ambalo kutu yake i ndani yake, ambalo kutu yake haikulitoka; litoe kipande kipande; hapana kura iliyoanguka juu yake.
7 Maana damu yake imo ndani yake; aliiweka juu ya jabali lililo wazi; hakuimwaga juu ya nchi, apate kuifunika kwa mavumbi;
8 ili ipandishe ghadhabu ya kulipa kisasi, nimeiweka damu yake juu ya jabali lililo wazi, isipate kufunikwa.
9 Basi Bwana MUNGU asema hivi; Ole wake mji wa damu! Mimi nami nitaiongeza chungu.
10 Tia kuni nyingi, uchochee moto, itokose nyama sana, fanyiza mchuzi mzito, mifupa ikateketee.
11 Kisha litie juu ya makaa yake, tupu, lipate moto, na shaba yake iteketee, uchafu wake uyeyushwe, na kutu yake iteketee.
12 Amejidhoofisha kwa taabu, lakini kutu yake nyingi haikumtoka; kutu yake haitoki kwa moto.
13 Katika uchafu wako mna uasherati, kwa maana nimekusafisha, ila wewe hukusafika; hutasafishwa tena uchafu wako ukutoke, hata nitakapokuwa nimeituliza hasira yangu kwako.
14 Mimi, Bwana, nimenena neno hili, nalo litakuwa; nami nitalifanya; sitaachilia, wala sitahurumia, wala sitajuta; sawasawa na njia zako, na sawasawa na matendo yako, ndivyo watakavyokuhukumu, asema Bwana MUNGU.
15 Neno la Bwana likanijia tena, kusema,
16 Mwanadamu, tazama, ninakuondolea kwa pigo moja tunu, mteule wa macho yako; walakini hutaomboleza wala kulia, wala yasichuruzike machozi yako.
17 Ugua lakini si kwa sauti ya kusikiwa; usifanye matanga kwa ajili yake yeye aliyekufa; jipige kilemba chako, ukavae viatu vyako, wala usiifunike midomo yako, wala usile chakula cha watu.
18 Basi nalisema na watu asubuhi, na jioni mke wangu akafa; nami nalifanya asubuhi kama nilivyoagizwa.
19 Watu hao wakaniambia, Je! Hutaki kutuambia maana ya mambo haya kwetu, hata umefanya kama vile ufanyavyo.
20 Nikawaambia, Neno la Bwana lilinijia, kusema,
21 Uwaambie nyumba ya Israeli, Bwana MUNGU asema hivi; Angalieni, nitapatia unajisi patakatifu pangu, fahari ya uwezo wenu, mahali pa kutamaniwa na macho yenu, ambapo roho zenu zinapahurumia na wana wenu na binti zenu, mliowaacha nyuma, wataanguka kwa upanga.
22 Nanyi mtafanya kama mimi nilivyofanya; hamtaifunika midomo yenu, wala kula chakula cha watu.
23 Na vilemba vyenu vitakuwa juu ya vichwa vyenu, na viatu vyenu miguuni mwenu; hamtaomboleza wala kulia; lakini mtafifia katika maovu yenu, na kuugua kila mtu pamoja na mwenziwe.
24 Basi ndivyo Ezekielii atakavyokuwa ishara kwenu; ninyi mtatenda sawasawa na yote aliyoyatenda yeye; litakapokuja jambo hili, ndipo mtakapojua ya kuwa mimi ndimi Bwana MUNGU.
25 Nawe, mwanadamu, je! Haitakuwa hivi katika siku hiyo nitakapowaondolea nguvu zao, na furaha ya utukufu wao, na kilichotamaniwa na macho yao, ambacho walikiinulia mioyo yao, wana wao na binti zao,
26 kwamba katika siku iyo hiyo yeye atakayeokoka atakuja kwako, akusikize jambo hili kwa masikio yako?
27 Siku hiyo kinywa chako kitafumbuliwa kwake aliyeokoka, nawe utasema; hutakuwa bubu tena; ndivyo utakavyokuwa ishara kwao; nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.

Ezekieli 25


1 Neno la Bwana likanijia, kusema,
2Mwanadamu, uwaelekezee wana wa Amoni uso wako, ukatabiri juu yao.
3Uwaambie hao wana wa Amoni, Lisikieni neno la Bwana MUNGU; Bwana MUNGU asema hivi; Kwa sababu umesema, Aha! Juu ya patakatifu pangu, palipotiwa unajisi; na juu ya nchi ya Israeli, ilipoharibiwa; na juu ya nyumba ya Israeli, walipokwenda kifungoni;
4basi, kwa sababu hiyo, nitakutia katika mikono ya wana wa mashariki uwe milki yao, nao wataweka marago yao ndani yako, kufanya maskani zao ndani yako; watakula matunda yako, na kunywa maziwa yako.
5Nami nitafanya Raba kuwa banda la ngamia, na wana wa Amoni kuwa mahali pa kulaza makundi; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.
6Maana Bwana MUNGU asema hivi; Kwa sababu umepiga makofi, na kupiga mshindo kwa miguu yako, na kufurahi juu ya nchi ya Israeli, jeuri yote ya roho yako;
7basi, tazama, nimenyosha mkono wangu juu yako, nami nitakutoa uwe mateka ya mataifa; nami nitakukatilia mbali na kabila za watu, nami nitakuangamiza, usiwe katika nchi hizo; nitakukomesha; nawe utajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.
8Bwana MUNGU asema hivi; Kwa sababu Moabu na Seiri husema, Tazama, nyumba ya Israeli ni sawasawa na mataifa yote;
9basi, tazama, nitawafunulia wana wa mashariki ubavu wa Moabu toka miji yake, toka miji yake iliyo mipakani mwake, utukufu wa nchi hiyo, Beth-yeshimothi, na Baal-meoni, na Kiriathaimu,
10pamoja na wana wa Amoni, nami nitawatoa kuwa milki, ili wana wa Amoni wasikumbukwe kati ya mataifa,
11nami nitatoa hukumu juu ya Moabu; nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.
12Bwana MUNGU asema hivi; Kwa kuwa Edomu wametenda kinyume cha nyumba ya Yuda, kwa kujilipiza kisasi, nao wamekosa sana, na kujilipiza kisasi juu yao;
13kwa sababu hiyo, Bwana MUNGU asema hivi; Nitanyosha mkono wangu juu ya Edomu, nitakatilia mbali nayo wanadamu na wanyama; nami nitaifanya kuwa ukiwa toka Temani; na mpaka Dedani wataanguka kwa upanga.
14Nami nitaweka kisasi changu juu ya Edomu, kwa mkono wa watu wangu Israeli; nao watatenda mambo katika Edomu, kwa kadiri ya hasira yangu, na ghadhabu yangu, nao watakijua kisasi changu, asema Bwana MUNGU.
15Bwana MUNGU asema hivi; Kwa kuwa Wafilisti wametenda mambo kwa kujilipiza kisasi, nao wamejilipiza kisasi kwa jeuri ya roho, ili kupaangamiza kwa uadui wa daima;
16kwa sababu hiyo, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, nitanyosha mkono wangu juu ya Wafilisti, nami nitawakatilia mbali Wakerethi, na kuwaharibu wabakio pande za pwani.
17Nami nitajilipiza kisasi kikuu, nikiwakemea kwa ukali; nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, nitakapojilipiza kisasi juu yao.

Ezekieli 26


1 Ikawa katika mwaka wa kumi na mmoja, siku ya kwanza ya mwezi, neno la Bwana likanijia, kusema,
2 Mwanadamu, Kwa sababu Tiro amesema juu ya Yerusalemu, Aha! Yeye amevunjika aliyekuwa lango la kabila za watu; amenigeukia; nitajazwa kwa kuwa sasa ameharibika;
3 basi Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi ni juu yako, Ee Tiro, nami nitaleta mataifa mengi kupigana nawe, kama bahari iinuavyo mawimbi yake.
4 Nao wataziharibu kuta za Tiro, na kuibomoa minara yake; tena nitakwangua hata mavumbi yake yamtoke, na kumfanya kuwa jabali tupu.
5 Naye atakuwa mahali pa kutandazia nyavu za wavuvi kati ya bahari; maana mimi nimenena neno hili, asema Bwana MUNGU; naye atakuwa mateka ya mataifa.
6 Na binti zake walio katika mashamba watauawa kwa upanga; nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.
7 Maana Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, nitamleta Nebukadreza, mfalme wa Babeli, mfalme wa wafalme, juu ya Tiro toka kaskazini, pamoja na farasi, na magari ya vita, na wapanda farasi, na jeshi, na watu wengi.
8 Atawaua binti zako kwa upanga katika mashamba; naye atafanya ngome juu yako, na kufanya maboma juu yako, na kuiinua ngao juu yako.
9 Naye ataweka vyombo vyake vya kubomolea mbele za kuta zako, na kwa mashoka yake ataiangusha chini minara yako.
10 Kwa sababu wingi wa farasi zake, mavumbi yao yatakufunika; kuta zako zitatetemeka kwa sababu ya mshindo wa wapanda farasi, na wa magurudumu, na wa magari ya vita, atakapoingia katika malango yako, kama watu waingiavyo katika mji uliobomolewa mahali.
11 Kwa kwato za farasi zake atazikanyaga njia zako zote; atawaua watu wako kwa upanga, na minara ya nguvu zako itashuka hata nchi.
12 Nao wataufanya utajiri wako kuwa mateka, na bidhaa yako kuwa mawindo; nao watazibomoa kuta zako, na kuziharibu nyumba zako zipendezazo; nao wataweka mawe yako, na miti yako, na mavumbi yako, kati ya maji.
13 Nami nitaikomesha sauti ya nyimbo zako, wala sauti ya vinubi vyako haitasikiwa tena.
14 Nami nitakufanya kuwa jabali tupu; utakuwa mahali pa kutandazia nyavu za wavuvi; hutajengwa tena; maana mimi, Bwana, nimenena neno hili, asema Bwana MUNGU.
15 Bwana MUNGU amwambia Tiro neno hili; Je! Visiwa havitatikisika kwa mshindo wa kuanguka kwako, watakapougua waliojeruhiwa, yatakapofanyika machinjo kati yako.
16 Ndipo wakuu wote wa bahari watashuka kutoka viti vyao vya enzi, na kuweka upande mavazi yao, na kuvua nguo zao zilizotiwa taraza; watajivika matetemeko; wataketi na kutetemeka kila dakika, na kukustaajabia,
17 Nao watakufanyia maombolezo, na kukuambia, Imekuwaje wewe kuharibika, wewe uliyekaliwa na wana-maji, mji wenye sifa, uliyekuwa na nguvu katika bahari, mji huo, na hao waliokaa ndani yake, waliowatia hofu wote waliokaa ndani yake!
18 Sasa visiwa vitatetemeka katika siku ya kuanguka kwako; naam, visiwa vilivyo katika bahari vitafadhaika, kwa sababu ya kuondoka kwako.
19 Maana Bwana MUNGU asema hivi; Nitakapokufanya kuwa mji wa ukiwa, kama miji isiyokaliwa na watu; nitakapoleta vilindi vya bahari juu yako, na maji makuu yatakapokufunika;
20 ndipo nitakapokushusha pamoja nao washukao shimoni, uende kwa watu wa kale; nami nitakukalisha pande za chini za nchi; mahali palipokuwa ukiwa tangu zamani, pamoja nao washukao shimoni; ili usikaliwe na watu, wala usiweke utukufu wako katika nchi yao walio hai.
21 Nitakufanya kuwa kitu cha kutisha, wala hutakuwako tena; ujapotafutwa, lakini hutaonekana tena kabisa, asema Bwana MUNGU.

Ezekieli 27


1 Neno la Bwana likanijia tena, kusema,
2 Na wewe, mwanadamu, mfanyie Tiro maombolezo;
3 umwambie Tiro, Ewe ukaaye penye maingilio ya bahari, uliye mchuuzi wa watu wa kabila nyingi, mpaka visiwa vingi, Bwana MUNGU asema hivi; Wewe, Tiro, umesema, Mimi ni ukamilifu wa uzuri.
4 Mipaka yako i kati ya moyo wa bahari; wajenzi wako wameukamilisha uzuri wako.
5 Mbao zako zote wamezifanya kwa misunobari itokayo Seniri; wametwaa mierezi ya Lebanoni ili kukufanyia mlingoti;
6 kwa mialoni ya Bashani wamefanya makasia yako; na sitaha zako wamezifanya kwa pembe iliyotiwa kazi ya njumu katika mti wa mihugu itokayo Kitimu.
7 Tanga lako lilikuwa la kitani safi itokayo Misri, iliyotiwa taraza, ili iwe bendera kwako; na chandalua chako kilikuwa cha rangi ya samawi na urujuani toka visiwa vya Elisha.
8 Wakaao Sidoni na Arvadi ndio waliovuta makasia yako; wana wako wenye akili, Ee Tiro, walikuwa ndani yako, ndio waliokuwa rubani zako.
9 Wazee wa Gebali na wenye akili wake walikuwa ndani yako, wenye kutia kalafati; merikebu zote za bahari na mabaharia wao walikuwa ndani yako, ili kubadiliana biashara yako.
10 Watu wa Uajemi na Ludi na Putu walikuwa katika jeshi lako, watu wako wa vita; walitungika ngao na chapeo ndani yako; wakadhihirisha uzuri wako.
11 Watu wa Arvadi, pamoja na jeshi lako, walikuwa juu ya kuta zako pande zote, na Wagamadi walikuwa ndani ya minara yako; walitungika ngao zao juu ya kuta zako pande zote; wakaukamilisha uzuri wako.
12 Tarshishi alikuwa mfanya biashara kwako, kwa sababu ya wingi wa utajiri wa kila aina; kwa fedha, na chuma, na bati, na risasi, walifanya biashara, wapate vitu vyako vilivyouzwa.
13 Uyunani na Tubali na Mesheki ndio waliokuwa wachuuzi wako; walitoa wanadamu, na vyombo vya shaba, kwa biashara yako.
14 Watu wa nyumba ya Togarma walifanya biashara, kwa farasi, naam, farasi za vita, na nyumbu, wapate vitu vyako vilivyouzwa.
15 Wadedani walikuwa wachuuzi wako, visiwa vingi vilikuwa soko la mkono wako; walikuletea pembe, na mpingo, ili kuvibadili.
16 Shamu alikuwa mfanya biashara kwako, kwa sababu ya wingi wa kazi za mkono wako walifanya biashara kwa zumaridi, na urujuani, na kazi ya taraza, na kitani safi, na marijani, na akiki, wapate vitu vyako vilivyouzwa.
17 Yuda, na nchi ya Israeli, walikuwa wachuuzi wako; walitoa badala ya bidhaa yako ngano ya Minithi, na mtama, na asali, na mafuta, na zeri.
18 Dameski alikuwa mfanya biashara kwako, kwa habari ya wingi wa kazi za mkono wako, kwa ajili ya wingi wa aina zote za utajiri; akaleta divai ya Helboni, na sufu nyeupe.
19 Wedani, na Yavani, walifanya biashara toka Uzali kwa vitu vyako; chuma kilichofuliwa, na mdalasini, na mchai, vilikuwa katika bidhaa yako.
20 Dedani alikuwa mchuuzi wako, kwa nguo za thamani za kutandikia farasi.
21 Arabuni, na wakuu wote wa Kedari, ndio waliokuwa wafanya biashara wa mkono wako; kwa wana-kondoo, na kondoo waume, na mbuzi; kwa hao walifanya biashara nawe.
22 Wachuuzi wa Sheba, na Raama, ndio waliokuwa wachuuzi wako; badala ya vitu vyako walitoa manukato yaliyo mazuri, na kila aina ya vito vya thamani, na dhahabu.
23 Harani, na Kane, na Adini, wachuuzi wa Sheba, na Ashuru, na Kilmadi, walikuwa wachuuzi wako.
24 Hao ndio waliokuwa wachuuzi wako, kwa vitu vya tunu, kwa vitumba vya nguo za samawi na kazi ya taraza, na masanduku ya mavazi ya thamani, yaliyofungwa kwa kamba, na kufanyizwa kwa mti wa mierezi, katika bidhaa yako.
25 Merikebu za Tarshishi zilikuwa misafara yako, kwa bidhaa yako; nawe ulijazwa sana, ukawa mtukufu sana, katika moyo wa bahari.
26 Wavuta makasia wako walikuleta katika maji makuu; upepo wa mashariki umekuvunja moyoni mwa bahari.
27 Mali zako, na bidhaa yako, na utajiri wako, wana-maji wako, na rubani zako, na wenye kutia kalafati wako, na wafanya biashara wako, na watu wako wa vita wote, walio ndani yako, pamoja na jeshi lako lote lililo ndani yako, wataanguka katika moyo wa bahari katika siku ya kuangamia kwako.
28 Kwa sauti ya vilio vya rubani zako viunga vyako vitatetema.
29 Na wote wavutao kasia, wana-maji, na rubani zote wa baharini, watashuka katika merikebu zao, na kusimama katika nchi kavu;
30 nao watasikizisha watu sauti zao juu yako, nao watalia kwa uchungu, na kutupa mavumbi juu ya vichwa vyao, na kugaagaa katika majivu;
31 nao watajifanya kuwa na upaa kwa ajili yako, na kujifunga nguo za magunia viunoni, nao watakulilia kwa uchungu wa roho, kwa maombolezo ya uchungu.
32 Na katika kulia kwao watakufanyia maombolezo, na kukuombolezea, wakisema, Ni nani aliye kama Tiro, kama yeye aliyenyamazishwa kati ya bahari?
33 Bidhaa zako zilipotoka katika bahari, uliwajaza watu wa kabila nyingi; uliwatajirisha wafalme wa dunia, kwa wingi wa mali zako, na kwa utajiri wako.
34 Wakati ulipovunjwa na bahari, katika vilindi vya maji, bidhaa zako na jeshi lako lote walianguka kati yako.
35 Wote wakaao katika visiwa vile watakustaajabia, na wafalme wao wameogopa sana, wamefadhaika nyuso zao.
36 Wafanya biashara kati ya kabila za watu wakuzomea; umekuwa kitu cha kutisha, wala hutakuwapo tena milele.

Ezekieli 28


1 Neno la Bwana likanijia tena, kusema,
2 Mwanadamu, mwambie mkuu wa Tiro, Bwana MUNGU asema hivi; Kwa kuwa moyo wako umeinuka, nawe umesema, Mimi ni Mungu, nami nimeketi katika kiti cha Mungu, kati ya bahari; lakini u mwanadamu wala si Mungu, ujapokuwa umeweka moyo wako kama moyo wa Mungu.
3 Tazama, una hekima kuliko Danieli; hapana neno la siri watu wawezalo kukuficha;
4 kwa hekima yako na kwa fahamu zako umejipatia utajiri, nawe umepata dhahabu na fedha katika hazina zako;
5 kwa hekima yako nyingi, na kwa biashara yako, umeongeza utajiri wako, na moyo wako umeinuka kwa sababu ya utajiri wako;
6 basi, kwa hiyo, Bwana MUNGU asema hivi; Kwa kuwa umeweka moyo wako kama moyo wa Mungu;
7 basi, tazama, nitaleta wageni juu yako, watu wa mataifa wenye kutisha; nao watafuta panga zao juu ya uzuri wa hekima yako, nao watautia uchafu mwangaza wako.
8 Watakushusha hata shimoni; nawe utakufa kifo chao waliouawa kati ya bahari.
9 Je! Utazidi kusema mbele yake huyo akuuaye, Mimi ni Mungu? Lakini u mwanadamu, wala si Mungu, mkononi mwake akutiaye jeraha.
10 Utakufa kifo cha hao wasiotahiriwa, kwa mikono ya wageni; kwa maana mimi nimenena neno hili, asema Bwana MUNGU.
11 Tena neno la Bwana likanijia, kusema,
12 Mwanadamu, umfanyie maombolezo mfalme wa Tiro, umwambie, Bwana MUNGU asema hivi; Wewe wakitia muhuri kipimo, umejaa hekima, na ukamilifu wa uzuri.
13 Ulikuwa ndani ya Adeni, bustani ya Mungu; kila jiwe la thamani lilikuwa kifuniko chako, akiki, na yakuti manjano, na almasi, na zabarajadi, na shohamu, na yaspi, na yakuti samawi, na zumaridi, na baharamani, na dhahabu; kazi ya matari yako na filimbi zako ilikuwa ndani yako; katika siku ya kuumbwa kwako zilitengenezwa tayari.
14 Wewe ulikuwa kerubi mwenye kutiwa mafuta afunikaye; nami nalikuweka hata ukawa juu ya mlima mtakatifu wa Mungu, umetembea huko na huko kati ya mawe ya moto.
15 Ulikuwa mkamilifu katika njia zako tangu siku ile ulipoumbwa, hata uovu ulipoonekana ndani yako.
16 Kwa wingi wa uchuuzi wako watu walikujaza udhalimu ndani yako, nawe umetenda dhambi; kwa sababu hiyo nimekutoa kwa nguvu katika mlima wa Mungu, kama kitu kilicho najisi; nami nimekuangamiza, Ewe kerubi ufunikaye, utoke katika mawe hayo ya moto.
17 Moyo wako uliinuka kwa sababu ya uzuri wako; umeiharibu hekima yako kwa sababu ya mwangaza wako; nimekutupa chini, nimekulaza mbele ya wafalme, wapate kukutazama.
18 Kwa wingi wa maovu yako, katika uovu wa uchuuzi wako, umepatia unajisi patakatifu pako; basi nimetokeza moto kutoka ndani yako, nao umekuteketeza, nami nimekufanya kuwa majivu juu ya nchi, machoni pa watu wote wakutazamao.
19 Wote wakujuao kati ya kabila za watu watakustaajabia; umekuwa kitu cha kutisha, wala hutakuwapo tena hata milele.
20 Neno la Bwana likanijia, kusema,
21 Mwanadamu, uuelekezee Sidoni uso wako, ukatabiri juu yake,
22 useme, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi ni juu yako, Ee Sidoni, nami natukuzwa kati yako; nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, nitakapokuwa nimetekeleza hukumu zangu ndani yake, na kutakasika ndani yake.
23 Maana nitampelekea tauni, na damu, katika njia kuu zake, na hao waliotiwa jeraha wataanguka kati yake, kwa upanga juu yake pande zote; nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.
24 Wala hautakuwapo mchongoma uchomao kwa nyumba ya Israeli; wala mwiba uumizao miongoni mwa wote wamzungukao, waliowatenda mambo ya jeuri; nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana MUNGU.
25 Bwana MUNGU asema hivi; Nitakapokuwa nimewakusanya nyumba ya Israeli, na kuwatoa katika watu ambao wametawanyika kati yao, na kutakasika kati yao machoni pa mataifa, ndipo watakapokaa katika nchi yao wenyewe, niliyompa mtumishi wangu, Yakobo.
26 Nao watakaa humo salama; naam, watajenga nyumba, na kupanda mashamba ya mizabibu, na kukaa salama; nitakapokuwa nimetekeleza hukumu zangu juu ya watu wote, wanaowatenda mambo ya jeuri pande zote; nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, Mungu wao.

Ezekieli 29


1 Katika mwaka wa kumi, mwezi wa kumi, siku ya kumi na mbili ya mwezi, neno la Bwana likanijia, kusema,
2 Mwanadamu, elekeza uso wako juu ya Farao, mfalme wa Misri, ukatabiri juu yake, na juu ya Misri yote;
3 nena, useme, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi ni juu yako, Ewe Farao, mfalme wa Misri, joka kubwa aoteaye kati ya mito yake, aliyesema, Mto wangu ni wangu mwenyewe, nami nimeufanya kwa ajili ya nafsi yangu.
4 Nami nitatia kulabu katika taya zako, nami nitawashikamanisha samaki wa mito yako na magamba yako; nami nitakutoa katika mito yako, pamoja na samaki wa mito yako walioshikamana na magamba yako.
5 Nami nitakuacha hali umetupwa jangwani, wewe na samaki wote wa mito yako; utaanguka juu ya uso wa uwanda; hutakusanywa, wala kuwekwa pamoja; nimekutoa uwe chakula cha wanyama wa nchi, na cha ndege wa angani.
6 Na watu wote wakaao Misri watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, kwa sababu wamekuwa mwanzi wa kutegemewa kwa nyumba ya Israeli.
7 Walipokushika kwa mkono wako, ulivunjika, ukawararua mabega yao yote; nao walipokutegemea, ulivunjika, ukawatetemesha viuno vyao vyote.
8 Basi, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, nitaleta upanga juu yako, nami nitakatilia mbali nawe wanadamu na wanyama.
9 Nayo nchi ya Misri itakuwa ukiwa na jangwa; nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana; kwa sababu amesema, Mto huu ni wangu, nami nimeufanya.
10 Basi, tazama, mimi ni juu yako, na juu ya mito yako, nami nitaifanya nchi ya Misri kuwa jangwa tupu, na ukiwa, toka Migdoli hata Sewene, hata mpaka wa Kushi.
11 Hautapita kati yake mguu wa mwanadamu, wala hautapita kati yake mguu wa mnyama, wala haitakaliwa na watu, muda wa miaka arobaini.
12 Nami nitaifanya nchi ya Misri kuwa ukiwa, kati ya nchi zilizo ukiwa, na miji yake, kati ya miji iliyoharibika, itakuwa maganjo muda wa miaka arobaini; nami nitawatawanya Wamisri kati ya mataifa, nami nitawatapanya kati ya nchi mbalimbali.
13 Maana Bwana MUNGU asema hivi; Mwisho wa miaka arobaini nitawakusanya Wamisri, na kuwatoa katika hizo kabila za watu, ambazo walitawanyika kati yao;
14 nami nitawarejeza Wamisri walio katika hali ya kufungwa, nami nitawarudisha hata nchi ya Pathrosi, hata nchi ya kuzaliwa kwao; na huko watakuwa ufalme duni.
15 Utakuwa duni kuliko falme zote; wala hautajiinua tena juu ya mataifa; nami nitawapunguza, ili wasitawale tena juu ya mataifa.
16 Wala hautakuwa tena tumaini la nyumba ya Israeli, kufanya maovu yakumbukwe, watakapogeuka kuangalia nyuma yao; nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana MUNGU.
17 Ikawa katika mwaka wa ishirini na saba, mwezi wa kwanza, siku ya kwanza ya mwezi, neno la Bwana likanijia, kusema,
18 Mwanadamu, Nebukadreza, mfalme wa Babeli, alilihudumisha jeshi lake huduma kuu juu ya Tiro; kila kichwa kilitiwa upaa, na kila bega liliambuliwa ngozi, lakini alikuwa hana mshahara uliotoka Tiro, wala yeye wala jeshi lake, kwa huduma ile aliyohudumu juu yake.
19 Basi, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, nitampa Nebukadreza, mfalme wa Babeli, hiyo nchi ya Misri; naye atawachukua watu wake jamii yote pia, na kutwaa mateka yake, na kutwaa mawindo yake, nayo yatakuwa ndio mshahara wa jeshi lake.
20 Nimempa nchi ya Misri kuwa malipo ya huduma aliyohudumu, kwa sababu walifanya kazi kwa ajili yangu; asema Bwana MUNGU.
21 Siku ile nitawachipushia nyumba ya Israeli pembe, nami nitakujalia kufumbua kinywa kati yao; nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.

Ezekieli 30


1 Neno la Bwana likanijia tena, kusema,
2 Mwanadamu, tabiri, useme, Bwana MUNGU asema hivi; Pigeni makelele ya uchungu, Ole wa siku ile!
3 Kwa maana siku ile i karibu, siku ile ya Bwana i karibu, siku ya mawingu; itakuwa wakati wa mataifa.
4 Na upanga utakuja juu ya Misri, na dhiki itakuwa katika Kushi, watakapoanguka watu waliouawa katika Misri, nao watauondoa wingi wa watu wake, na misingi yake itabomolewa.
5 Kushi, na Putu, na Ludi, na watu wote waliochanganyika, na Kubu, na wana wa nchi ya agano, wataanguka kwa upanga pamoja nao.
6 Bwana asema hivi; Nao pia wanaoitegemeza Misri wataanguka, na kiburi cha uwezo wake kitashuka; toka Migdoli hata Sewene, wataanguka ndani yake kwa upanga, asema Bwana MUNGU.
7 Nao watakuwa ukiwa, kati ya nchi zilizo ukiwa, na miji yake itakuwamo kati ya miji iliyoharibika.
8 Nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, nitakapoweka moto katika Misri, na hao wote wamsaidiao watakapoangamia.
9 Katika siku hiyo watatoka wajumbe mbele zangu katika merikebu, ili kuwatia hofu Wakushi, wanaojiona kuwa salama, na dhiki itakuwa juu yao, vile vile kama katika siku ya Misri; kwa maana, tazama, inakuja.
10 Bwana MUNGU asema hivi; Pia nitaukomesha wingi wa watu wa Misri, kwa mkono wa Nebukadreza, mfalme wa Babeli.
11 Yeye, na watu wake pamoja naye, watu wa mataifa watishao, wataletwa waingie katika nchi waiharibu, nao watafuta panga zao wapigane na Misri, na kuijaza nchi wale waliouawa.
12 Nami nitaikausha mito, na kuiuza nchi, na kuitia katika mikono ya watu wabaya; nami nitaifanya nchi kuwa ukiwa, na watu wote walio ndani yake, kwa mkono wa wageni; mimi, Bwana, nimenena neno hili.
13 Bwana MUNGU asema hivi; Pia nitaviharibu vinyago, nami nitavikomesha vitu vya ubatili katika Nofu, wala hapatakuwa na mkuu tena atokaye katika nchi ya Misri, nami nitatia hofu katika nchi ya Misri.
14 Nami nitaifanya Pathrosi kuwa ukiwa, nami nitatia moto katika Soani, nami nitatekeleza hukumu katika No.
15 Nami nitamwaga ghadhabu yangu juu ya Sini, ngome ya Misri, nami nitakatilia mbali wingi wa watu wa No.
16 Nami nitatia moto katika Misri; Sini itakuwa katika dhiki kuu, na No itavunjika kabisa; na Nofu itakuwa na adui wakati wa mchana.
17 Vijana wa Oni, na wa Pi-besethi, wataanguka kwa upanga; na miji hiyo itakwenda utumwani.
18 Huko Tapanesi nako mchana utakuwa giza, nitakapovunja huko kongwa za Misri, na kiburi cha uwezo wake kitakoma ndani yake, na katika habari zake, wingu litaifunika, na binti zake watakwenda utumwani.
19 Hivyo ndivyo nitakavyotekeleza hukumu katika Misri; nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.
20 Ikawa katika mwaka wa kumi na mmoja, mwezi wa kwanza, siku ya saba ya mwezi, neno la Bwana likanijia, kusema,
21 Mwanadamu, nimeuvunja mkono wa Farao, mfalme wa Misri, na tazama, haukufungwa ili kuutia dawa, haukuzongwa kwa kitambaa, upate kuwa na nguvu za kushika upanga.
22 Basi Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi ni juu ya Farao, mfalme wa Misri, nami nitamvunja mikono yake, mkono ulio wenye nguvu, na huo uliovunjika, nami nitauangusha upanga ulio katika mkono wake.
23 Nami nitawatawanya Wamisri kati ya mataifa, na kuwatapanya kati ya nchi mbalimbali.
24 Nami nitaitia nguvu mikono ya mfalme wa Babeli, na kuutia upanga wangu katika mkono wake, bali mikono ya Farao nitaivunja, naye ataugua mbele yake, kwa mauguzi ya mtu aliyetiwa jeraha ya kumfisha.
25 Nami nitaitegemeza mikono ya mfalme wa Babeli, na mikono ya Farao itaanguka; nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, nitakapoutia upanga wangu katika mkono wa mfalme wa Babeli, naye ataunyosha juu ya nchi ya Misri.
26 Nami nitawatawanya Wamisri kati ya mataifa, na kuwatapanya kati ya nchi mbalimbali; nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.

Ezekieli 31


1 Ikawa katika mwaka wa kumi na mmoja, mwezi wa tatu, siku ya kwanza ya mwezi, neno la Bwana likanijia, kusema,
2 Mwanadamu, mwambie Farao mfalme wa Misri, na jamii ya watu wake, Je! Umefanana na nani katika ukuu wako?
3 Tazama, Mwashuri alikuwa mwerezi katika Lebanoni, wenye matawi mazuri, na kifuniko chenye uvuli, na kimo kirefu; na kilele chake kilikuwa kati ya matawi mapana.
4 Maji yalimlisha, vilindi vilimsitawisha; mito yake ilipita pande zote za miche yake; naye akapeleka mifereji yake kwa miti yote ya kondeni.
5 Basi kimo chake kilitukuzwa kuliko miti yote ya kondeni, na vitanzu vyake viliongezeka; matawi yake yakawa marefu, kwa sababu ya maji mengi, alipoyachipuza.
6 Ndege wote wa angani walifanya vioto vyao katika vitanzu vyake, na chini ya matawi yake wanyama wote wa kondeni walizaa watoto wao, na chini ya uvuli wake mataifa makuu yote walikaa.
7 Basi hivyo alikuwa mzuri katika ukuu wake, katika urefu wa matawi yake; maana mizizi yake ilikuwa karibu na maji mengi.
8 Mierezi ya bustani ya Mungu haikuweza kumficha; misunobari haikuwa kama vitanzu vyake, na miamori haikuwa kama matawi yake, wala bustanini mwa Mungu hamkuwa na mti wo wote uliofanana naye kwa uzuri.
9 Nalimfanya kuwa mzuri kwa wingi wa matawi yake; hata miti yote ya Adeni, iliyokuwa ndani ya bustani ya Mungu, ilimwonea wivu.
10 Basi Bwana MUNGU asema hivi; kwa kuwa umetukuzwa kimo chako, naye ameweka kilele chake kati ya mawingu, na moyo wake umeinuka kwa urefu wake;
11 mimi nitamtia katika mikono yake aliye mkuu kati ya mataifa; naye atamtenda mambo; nimemfukuza kwa sababu ya uovu wake.
12 Na wageni, watu wa mataifa watishao, wamemkatilia mbali na kumwacha; juu ya milima na katika mabonde yote matawi yake yameanguka, na vitanzu vyake vimevunjika karibu na mifereji yote ya nchi; na watu wote wa dunia wameshuka, wakitoka katika uvuli wake na kumwacha.
13 Juu ya magofu yake ndege wote wa angani watakaa, na wanyama wote wa jangwani watakuwa juu ya matawi yake;
14 kusudi mti wo wote, ulio karibu na maji, usijitukuze kwa sababu ya kimo chake, wala usitie kilele chake kati ya mawingu, wala mashujaa wake wasisimame katika kimo chao kirefu, naam, wote wanywao maji; maana wote wametolewa wafe, waende pande za chini za nchi, kati ya wanadamu, pamoja nao washukao shimoni.
15 Bwana MUNGU asema hivi, Katika siku ile alipotelemka mpaka kuzimu naliamuru matanga, nalikifunika kilindi kwa ajili yake, nikiizuia mito yake, nayo maji makuu yalizuiwa; naliamuru Lebanoni kumwombolezea, na miti yote ya kondeni ilizimia kwa ajili yake.
16 Niliwatetemesha mataifa kwa mshindo wa kuanguka kwake, hapo nilipomtupa chini mpaka kuzimu, pamoja nao washukao shimoni; na miti yote ya Adeni, miti iliyo miteule na iliyo mizuri ya Lebanoni, yote inywayo maji, ilifarijika pande za chini za nchi.
17 Hao nao walitelemka kuzimuni pamoja naye kwa watu waliouawa kwa upanga; naam, wale waliokuwa mkono wake, waliokaa chini ya uvuli wake kati ya mataifa.
18 Umefanana na nani, hivi katika utukufu na ukuu, kati ya miti ya Adeni? Lakini utashushwa pamoja na miti ya Adeni, hata pande za chini za nchi; utalala kati ya hao wasiotahiriwa; pamoja na hao waliouawa kwa upanga. Huyu ndiye Farao, na jamii yote ya watu wake, asema Bwana MUNGU.

Ezekieli 32


1 Ikawa katika mwaka wa kumi na mbili, mwezi wa kumi na mbili, siku ya kwanza ya mwezi, neno la Bwana likanijia, kusema,
2 Mwanadamu, mfanyie Farao, mfalme wa Misri, maombolezo, umwambie, Ulifananishwa na mwana-simba wa mataifa; lakini umekuwa kama joka katika bahari; nawe watoka kwa nguvu pamoja na mito yako, na kuyachafua maji kwa miguu yako, na kuitia uchafu mito yao.
3 Bwana MUNGU asema hivi; Nitautanda wavu wangu juu yako, kwa kusanyiko la watu wa kabila nyingi; nao watakuvua katika jarife langu.
4 Nami nitakuacha juu ya nchi kavu, nitakutupa juu ya uso wa uwanda, nami nitawaleta ndege wote wa angani watue juu yako, nami nitawashibisha wanyama wa dunia yote kwako wewe.
5 Nami nitaweka nyama yako juu ya milima, na kuyajaza mabonde kwa urefu wako.
6 Tena kwa damu yako nitainywesha nchi, ambayo waogelea juu yake, hata milimani; na mifereji ya maji itajawa nawe.
7 Nami nitakapokuzimisha, nitazifunikiza mbingu, na kuzifanya nyota zake kuwa giza; nami nitalifunika jua kwa wingu, wala mwezi hautatoa nuru yake.
8 Mianga yote ya mbinguni iangazayo nitaifanya kuwa giza juu yako, nami nitatia giza katika nchi yako, asema Bwana MUNGU.
9 Tena nitawakasirisha watu wengi mioyo yao, nitakapoleta uangamivu wako kati ya mataifa, uingie katika nchi ambazo hukuzijua.
10 Nami nitawashangaza watu wa kabila nyingi kwa habari zako, na wafalme wao wataogopa sana kwa ajili yako, nitakapoutikisa upanga wangu mbele yao; nao watatetemeka kila dakika, kila mtu kwa ajili ya uhai wake, katika siku ya kuanguka kwako.
11 Maana Bwana MUNGU asema hivi; Upanga wa mfalme wa Babeli utakujilia.
12 Kwa panga za mashujaa nitawaangusha watu wako wote jamii; hao wote ni watu wa mataifa watishao, nao watakiharibu kiburi cha Misri, na jamii ya watu wake wengi wataangamia.
13 Tena nitawaharibu wanyama wake wote, toka kando ya maji mengi; na mguu wa mwanadamu hautayatibua tena, wala kwato za mnyama hazitayatibua.
14 Ndipo nitakapoyafanya maji yao kuwa safi, na kuiendesha mito yao kama mafuta, asema Bwana MUNGU.
15 Nitakapoifanya nchi ya Misri kuwa ukiwa na jangwa, nchi iliyopungukiwa na vitu vilivyoijaza, nitakapowapiga watu wote wakaao ndani yake, ndipo watakapojua ya kuwa mimi ndimi Bwana.
16 Hayo ndiyo maombolezo watakayoomboleza; binti za mataifa wataomboleza kwa hayo; kwa hayo wataomboleza kwa ajili ya Misri, na kwa ajili ya watu wake wote jamii, asema Bwana MUNGU.
17 Ikawa katika mwaka wa kumi na mbili, siku ya kumi na tano ya mwezi, neno la Bwana likanijia kusema,
18 Mwanadamu, walilie watu wa Misri. Wote jamii ukawabwage, naam, yeye, na binti za mataifa mashuhuri, hata pande za chini za nchi, pamoja na watu washukao shimoni.
19 Umemshinda nani kwa uzuri? Shuka, ukalazwe pamoja na wasiotahiriwa.
20 Wataanguka kati ya watu waliouawa kwa upanga; ametokwa apigwe na upanga; mvuteni aende mbali pamoja na watu wake wote jamii.
21 Walio hodari watasema naye, toka kati ya kuzimu pamoja nao wamsaidiao; wameshuka wamelala kimya, hata wasiotahiriwa, hali wameuawa kwa upanga.
22 Ashuru yuko huko, na watu wake wote jamii; makaburi yake yamzunguka; wote pia wameuawa, wameanguka kwa upanga,
23 ambao makaburi yao yamewekwa pande za shimo zilizo mbali sana, wote jamii wamezunguka kaburi lake; wote pia wameuawa, wameanguka kwa upanga, waliofanya utisho katika nchi yao walio hai.
24 Elamu yuko huko, na watu wake wote jamii, pande zote za kaburi lake; wote pia wameuawa, wameanguka kwa upanga, walioshuka hali hawana tohara hata pande za chini ya nchi; ambao waliwatia watu hofu katika nchi ya walio hai, nao wamechukua aibu yao, pamoja nao washukao shimoni.
25 Wamemwekea kitanda kati ya hao waliouawa, pamoja na watu wake wote jamii; makaburi yake yamzunguka; wote pia hawakutahiriwa, wameuawa kwa upanga; maana maogofyo yao yalifanyika katika nchi ya walio hai, nao wamechukua aibu yao, pamoja nao washukao shimoni; amewekwa kati ya hao waliouawa.
26 Mesheki yuko huko, na Tubali, na watu wake wote jamii; makaburi yake yamzunguka; wote pia hawakutahiriwa, wameuawa kwa upanga; maana walifanya utisho wao katika nchi ya walio hai.
27 Je! Wasilale pamoja na mashujaa wao wasiotahiriwa, walioanguka, walioshuka kuzimu pamoja na silaha zao za vita, ambao wameweka panga zao chini ya vichwa vyao, na maovu yao mifupani mwao? Maana waliwatisha mashujaa katika nchi ya walio hai.
28 Lakini utavunjika kati ya hao wasiotahiriwa, nawe utalala pamoja nao waliouawa kwa upanga.
29 Edomu yuko huko, wafalme wake, na wakuu wake wote, ambao katika uwezo wao wamelazwa pamoja nao waliouawa kwa upanga; watalala pamoja na hao wasiotahiriwa, na pamoja na hao washukao shimoni.
30 Wakuu wa kaskazini wako huko, wote pia, na Wasidoni, wote walioshuka pamoja na hao waliouawa; kwa sababu ya utisho walioufanya katika uwezo wao wamefedheheka, nao wamelala hali hawana tohara, pamoja nao waliouawa kwa upanga, nao wanachukua aibu yao, pamoja nao washukao shimoni.
31 Farao atawaona, naye atapata faraja juu ya watu wake wote jamii; naam, Farao, jeshi lake lote waliouawa kwa upanga, asema Bwana MUNGU.
32 Kwa maana nimeweka utisho wake katika nchi ya walio hai; naye atalazwa kati yao wasiotahiriwa, pamoja na hao waliouawa kwa upanga; yeye Farao na watu wake wote jamii, asema Bwana MUNGU.

Ezekieli 33


1 Neno la Bwana likanijia, kusema,
2 Mwanadamu, sema na wana wa watu wako, uwaambie, Hapo nitakapoleta upanga juu ya nchi, watu wa nchi hiyo wakimtwaa mtu mmoja miongoni mwao, na kumweka awe mlinzi wao;
3 ikiwa, aonapo upanga unakuja juu ya nchi hiyo, apiga tarumbeta na kuwaonya watu;
4 basi mtu awaye yote aisikiaye sauti ya tarumbeta, wala haonywi, upanga ukija na kumwondoa, damu yake itakuwa juu ya kichwa chake mwenyewe.
5 Aliisikia sauti ya tarumbeta, wala hakuonywa; damu yake itakuwa juu yake; lakini kama angalionywa, angalijiokoa roho yake.
6 Bali mlinzi akiona upanga unakuja, kama hapigi tarumbeta, wala watu hawakuonywa, na upanga ukaja ukamwondoa mtu awaye yote miongoni mwao; ameondolewa huyo katika uovu wake, lakini damu yake nitaitaka mkononi mwa mlinzi huyo.
7 Basi wewe, mwanadamu, nimekuweka kuwa mlinzi kwa nyumba ya Israeli; basi ulisikie neno hili kinywani mwangu, ukawape maonyo yangu.
8 Nimwambiapo mtu mbaya, Ewe mtu mbaya, hakika utakufa, nawe husemi neno la kumwonya mtu huyo, aiache njia yake, mtu mbaya huyo atakufa katika uovu wake, lakini damu yake nitaitaka mkononi mwako.
9 Walakini ukimwonya mtu mbaya kwa sababu ya njia yake, kusudi aiache; wala yeye asiiache; atakufa huyo katika uovu wake, lakini wewe umejiokoa roho yako.
10 Na wewe, mwanadamu, sema na nyumba ya Israeli; Ninyi mwasema hivi, kwamba, Makosa yetu na dhambi zetu ni juu yetu, nasi tumedhoofika katika dhambi hizo; basi tungewezaje kuwa hai?
11 Waambie, Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, sikufurahii kufa kwake mtu mwovu; bali aghairi mtu mwovu, na kuiacha njia yake mbaya, akaishi. Ghairini, ghairini, mkaache njia zenu mbaya; mbona mnataka kufa, Enyi nyumba ya Israeli?
12 Na wewe, mwanadamu, waambie wana wa watu wako, Haki yake mwenye haki haitamwokoa, katika siku ya kukosa kwake; na kwa habari ya uovu wake mtu mwovu, hataanguka kwa ajili ya uovu huo, siku ile atakapoghairi na kuuacha uovu wake; wala yeye aliye mwenye haki hataweza kuishi kwa haki yake, siku ile atakapotenda dhambi.
13 Nimwambiapo mwenye haki, ya kwamba hakika ataishi; kama akiitumainia haki yake, akatenda uovu, basi katika matendo yake ya haki, hata mojawapo halitakumbukwa; bali katika uovu wake alioutenda, atakufa katika uovu huo.
14 Tena, nimwambiapo mtu mwovu, Hakika utakufa; kama akighairi, na kuiacha dhambi yake, na kutenda yaliyo halali na haki;
15 kama mtu mwovu akirudisha rehani, na kumrudishia mtu mali yake aliyomnyang'anya, akizifuata sheria za uzima, asitende uovu wo wote; hakika ataishi, hatakufa.
16 Katika dhambi zake zote alizozitenda, hata mojawapo haitakumbukwa juu yake; ametenda yaliyo halali na haki; hakika ataishi.
17 Walakini wana wa watu wako husema, Njia ya Bwana si sawa; lakini watu hao, njia yao si sawa.
18 Mwenye haki ageukapo, na kuiacha haki yake, na kutenda maovu, atakufa katika maovu hayo.
19 Na mtu mbaya ageukapo, na kuuacha ubaya wake, na kutenda yaliyo halali na haki, ataishi kwa matendo hayo.
20 Lakini ninyi husema, Njia ya Bwana si sawa. Ee nyumba ya Israeli, nitawahukumu ninyi; kila mtu kwa kadiri ya njia zake.
21 Ikawa, katika mwaka wa kumi na mbili wa kuhamishwa kwetu, mwezi wa kumi, siku ya tano ya mwezi, mtu mmoja aliyekuwa ametoroka toka Yerusalemu akanijia, akisema, Mji umepigwa.
22 Basi mkono wa Bwana umekuwa juu yangu wakati wa jioni, kabla hajafika yeye aliyetoroka; naye alikuwa amenifumbua kinywa changu, hata aliponijia wakati wa asubuhi; na kinywa changu kilikuwa wazi, wala sikuwa bubu tena.
23 Neno la Bwana likanijia, kusema,
24 Mwanadamu, watu wale wakaao mahali palipoharibika katika nchi ya Israeli husema ya kwamba, Ibrahimu alikuwa mmoja, akairithi nchi hii; lakini sisi tu watu wengi; tumepewa nchi hii iwe urithi wetu.
25 Basi, waambie, Bwana MUNGU asema hivi; Mnakula nyama pamoja na damu yake, na kuviinulia vinyago vyenu macho yenu, na kumwaga damu; je, mtaimiliki nchi hii?
26 Mnategemea upanga wenu, mnatenda machukizo, mnanajisi kila mtu mke wa jirani yake; je! Mtaimiliki nchi hii?
27 Hivi ndivyo utakavyowaambia, Bwana MUNGU asema hivi; Kama mimi niishivyo, hakika watu wale wakaao mahali palipoharibika wataanguka kwa upanga, naye mtu aliye katika uwanda, nitamtoa na kuwapa wanyama wakali, ili aliwe; na hao walio ndani ya ngome na mapango watakufa kwa tauni.
28 Nami nitaifanya nchi kuwa ukiwa na ajabu, na kiburi cha uwezo wake kitakoma; nayo milima ya Israeli itakuwa ukiwa, asipite mtu.
29 Ndipo watakapojua ya kuwa mimi ndimi Bwana, nitakapoifanya nchi kuwa ukiwa na ajabu, kwa sababu ya machukizo yao yote waliyoyatenda.
30 Nawe, mwanadamu, wana wa watu wako husimulia habari zako karibu na kuta, na ndani ya milango ya nyumba zao, na kuambiana, kila mtu na ndugu yake, wakisema, Haya! Twende tukasikie ni neno gani hilo litokalo kwa Bwana.
31 Nao huja kwako kama watu wajavyo, nao hukaa mbele yako kama watu wangu, nao husikia maneno yako, wasiyatende; maana kwa vinywa vyao hujifanya kuwa wenye upendo mwingi, lakini mioyo yao inatafuta faida yao.
32 Na tazama, wewe umekuwa kwao kama wimbo mzuri sana, wa mtu mwenye sauti ipendezayo, awezaye kupiga kinanda vizuri; maana, wasikia maneno yako, lakini hawayatendi.
33 Na hayo yatakapokuwapo (tazama, yanakuja), ndipo watakapojua ya kuwa nabii amekuwapo kati yao.

Ezekieli 34


1 Neno la Bwana likanijia, kusema,
2 Mwanadamu, toa unabii juu ya wachungaji wa Israeli, toa unabii, uwaambie, naam, hao wachungaji, Bwana MUNGU asema hivi; Ole wao wachungaji wa Israeli, wanaojilisha wenyewe; je! Haiwapasi wachungaji kuwalisha kondoo?
3 Mnawala walionona, mnajivika manyoya, mnawachinja walionona; lakini hamwalishi kondoo.
4 Wagonjwa hamkuwatia nguvu, wala hamkuwaponya wenye maradhi, wala hamkuwafunga waliovunjika, wala hamkuwarudisha waliofukuzwa, wala hamkuwatafuta waliopotea; bali kwa nguvu na kwa ukali mmewatawala.
5 Nao wakatawanyika, kwa sababu hapakuwa na mchungaji; wakawa chakula cha wanyama- mwitu, wakatawanyika.
6 Kondoo zangu walitanga-tanga katika milima yote, na juu ya kila kilima kirefu; naam, kondoo zangu walitawanyika juu ya uso wote wa dunia; wala hapakuwa na mtu aliyewaulizia, wala kuwatafuta.
7 Basi, enyi wachungaji, lisikieni neno la Bwana;
8 Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, kwa sababu kondoo zangu walikuwa mateka, kondoo zangu wakawa chakula cha wanyama-mwitu wote, kwa sababu hapakuwa na mchungaji, wala wachungaji wangu hawakutafuta kondoo zangu, bali wachungaji walijilisha wenyewe wala hawakuwalisha kondoo zangu;
9 kwa sababu hiyo, enyi wachungaji, lisikieni neno la Bwana;
10 Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi ni juu ya wachungaji; nami nitawataka kondoo zangu mikononi mwao, nami nitawaachisha hiyo kazi ya kuwalisha kondoo; nao wachungaji hawatajilisha wenyewe tena; nami nitawaokoa kondoo zangu vinywani mwao, wasiwe tena chakula chao.
11 Maana, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi mwenyewe, naam, mimi, nitawatafuta kondoo zangu, na kuwaulizia.
12 Kama vile mchungaji atafutavyo kondoo zake, siku ile anapokuwa kati ya kondoo zake waliotawanyika; ndivyo nitakavyowatafuta kondoo zangu; nami nitawaokoa katika mahali pote walipotawanyika, katika siku ya mawingu na giza.
13 Nami nitawatoa katika watu wa mataifa, na kuwakusanya katika nchi zote, nami nitawarudisha katika nchi yao wenyewe; nami nitawalisha juu ya milima ya Israeli, kando ya mifereji ya maji; na katika mahali pote pa nchi panapokaliwa na watu.
14 Nami nitawalisha malisho mema, pa juu ya milima ya mahali palipoinuka pa Israeli litakuwa zizi lao; huko watalala katika zizi jema; nao watakula malisho mema, juu ya milima ya Israeli.
15 Mimi mwenyewe nitawalisha kondoo zangu, nami nitawalaza, asema Bwana MUNGU.
16 Nami nitawatafuta waliopotea, nitawarudisha waliofukuzwa, nitawafunga waliovunjika, nitawatia nguvu wagonjwa; nao wanono na wenye nguvu nitawaharibu; nitawalisha hukumu.
17 Na kwa habari zenu, Enyi kundi langu, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, nahukumu kati ya mnyama na mnyama, kondoo waume na mbuzi waume pia.
18 Je! Mwaona ya kuwa ni neno dogo ninyi kulishwa malisho mema, hata mkawa hamna budi hukanyaga kwa miguu yenu yaliyosalia? Na kuwa mmekunywa maji yaliyo safi, nanyi hamna budi kuyatibua kwa miguu yaliyobaki?
19 Na kwa habari za kondoo zangu, wao wanakula hayo mliyoyakanyaga kwa miguu yenu, nao wanakunywa maji mliyoyatibua kwa miguu yenu.
20 Kwa sababu hiyo, Bwana MUNGU awaambia hivi; Tazama, mimi, naam, mimi, nitahukumu kati ya wanyama walionona na wanyama waliokonda.
21 Kwa kuwa mmesukuma kwa ubavu, na kwa mabega, na kuwapiga wenye maradhi kwa pembe zenu, hata mkawatawanyia mbali;
22 basi mimi nitaliokoa kundi langu, wala hawatakuwa mateka tena; nami nitahukumu kati ya mnyama na mnyama.
23 Nami nitaweka mchungaji mmoja juu yao, naye atawalisha, naam, mtumishi wangu, Daudi; yeye atawalisha, naye atakuwa mchungaji wao.
24 Na mimi, Bwana, nitakuwa Mungu wao, na mtumishi wangu, Daudi, atakuwa mkuu kati yao; mimi, Bwana, nimesema haya.
25 Nami nitafanya agano la amani nao, nami nitawakomesha wanyama wakali kati yao; nao watakaa salama jangwani, na kulala misituni.
26 Nami nitawafanya wao, na mahali palipo pande zote za mlima wangu, kuwa baraka, nami nitaleta manyunyu kwa wakati wake; yatakuwako manyunyu ya baraka.
27 Na mti wa kondeni utazaa matunda yake, nayo ardhi itatoa mazao yake, nao watakuwa salama katika nchi yao; nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, nitakapovunja vifungo vya kongwa lao, na kuwaokoa katika mikono ya watu wale waliowatumikisha.
28 Hawatakuwa mateka ya makafiri tena, wala mnyama wa nchi hatawala; bali watakaa salama salimini, wala hapana mtu atakayewatia hofu.
29 Nami nitawainulia miche iwe sifa njema, wala hawataangamizwa kwa njaa katika nchi yao tena, wala hawatachukua tena aibu ya makafiri.
30 Nao watajua ya kuwa mimi, Bwana, Mungu wao, ni pamoja nao, na ya kuwa wao, nyumba ya Israeli, ni watu wangu, asema Bwana MUNGU.
31 Na ninyi, kondoo zangu, kondoo za malisho yangu, ni wanadamu, na mimi ni Mungu wenu, asema Bwana MUNGU.

Ezekieli 35


1 Tena neno la Bwana likanijia, kusema,
2 Mwanadamu, kaza uso wako juu ya mlima Seiri, ukatabiri juu yake,
3 uuambie, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi ni juu yako, Ee mlima Seiri, nami nitaunyosha mkono wangu juu yako, nami nitakufanya kuwa ukiwa na ajabu.
4 Miji yako nitaiharibu, nawe utakuwa ukiwa; nawe utajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.
5 Kwa kuwa umekuwa na uadui usiokoma, nawe umewatoa wana wa Israeli wapigwe kwa nguvu za upanga, wakati wa msiba wao, wakati wa mwisho wa uovu.
6 Basi, kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, nitakuweka tayari kwa damu, na damu itakufuatia; ikiwa hukuchukia damu, basi damu itakufuatia.
7 Hivyo ndivyo nitakavyoufanya mlima Seiri kuwa ajabu na ukiwa; nami nitakatilia mbali nao mtu apitaye, na mtu arejeaye.
8 Nami nitaijaza milima yake watu wake waliouawa; katika milima yako, na katika mabonde yako, na katika mifereji yako ya maji yote, wataanguka wao watakaouawa kwa upanga.
9 Nitakufanya kuwa ukiwa wa daima, na miji yako haitakaliwa na watu; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.
10 Kwa sababu umesema, Mataifa haya mawili na nchi hizi mbili zitakuwa zangu, nasi tutazimiliki, ijapokuwa Bwana alikuwako huko.
11 Basi, kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, nitatenda kwa kadiri ya hasira yako, na kwa kadiri ya wivu wako, ulioudhihirisha kwa kuwachukia; nami nitajidhihirisha kwao, nitakapokuhukumu wewe.
12 Nawe utajua ya kuwa mimi, Bwana, nimeyasikia matukano yako yote, uliyoyanena juu ya milima ya Israeli, ukisema, Wamefanyika ukiwa, wametiwa katika mikono yetu tuwale.
13 Nanyi mmejitukuza juu yangu kwa vinywa vyenu, na kuyaongeza maneno juu yangu; nimesikia mimi.
14 Bwana MUNGU asema hivi; Dunia yote itakapofurahi, nitakufanya kuwa ukiwa.
15 Kama vile ulivyofurahi juu ya urithi wa nyumba ya Israeli, kwa sababu ilikuwa ukiwa, ndivyo nitakavyokutenda wewe; utakuwa ukiwa, Ee mlima Seiri, na Edomu yote, naam, yote pia; nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.

Ezekieli 36


1 Na wewe, mwanadamu, itabirie milima ya Israeli, useme, Enyi milima ya Israeli, lisikieni neno la Bwana.
2 Bwana MUNGU asema hivi; Kwa sababu adui amesema juu yenu, Aha! Na, Mahali pa juu pa zamani pamekuwa petu tupamiliki;
3 basi tabiri useme, Bwana MUNGU asema hivi; Kwa sababu, naam, kwa sababu wamewafanya ninyi kuwa ukiwa, na kuwameza pande zote, mpate kuwa milki kwa mabaki ya mataifa, nanyi mmeambwa kwa midomo yao waongeao, na kwa masingizio ya watu;
4 kwa sababu hiyo, enyi milima ya Israeli, lisikieni neno la Bwana MUNGU; Bwana MUNGU aiambia hivi hiyo milima na vilima, mifereji ya maji na mabonde, mahali palipoharibika na kuwa ukiwa, na miji iliyoachwa na watu, ambayo imekuwa mateka, na kuzomewa na mabaki ya mataifa, walio karibu pande zote;
5 basi Bwana MUNGU asema hivi; Hakika kwa moto wa wivu wangu nimenena juu ya mabaki ya mataifa, na juu ya Edomu yote, waliojiandikia nchi yangu kuwa milki yao, kwa furaha ya mioyo yao yote, kwa jeuri ya roho zao, ili waitupe nje kuwa mawindo;
6 basi katika kutabiri habari za nchi ya Israeli, uiambie milima na vilima, mifereji ya maji na mabonde, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, nimenena katika wivu wangu na hasira yangu, kwa sababu mmechukua aibu ya mataifa;
7 basi Bwana MUNGU asema hivi; Nimeinua mkono wangu, kusema, Hakika, mataifa walio karibu nanyi pande zote, wao watachukua aibu yao.
8 Lakini ninyi, enyi milima ya Israeli, mtachipuza matawi yenu na kuwapa watu wangu Israeli matunda yenu; maana wa karibu kuja.
9 Maana, tazama, mimi nasimama upande wenu, nami nitawaelekea, nanyi mtalimwa na kupandwa mbegu;
10 nami nitaongeza watu juu yenu, nyumba yote ya Israeli, naam, yote pia; nayo miji itakaliwa na watu, na mahali palipoharibika patajengwa.
11 Nami nitaongeza juu yenu mwanadamu na mnyama, nao watazidi na kuzaa; nami nitawakalisha watu ndani yenu, kwa kadiri ya hali yenu ya kwanza, nami nitawatendea mema kuliko mema ya mianzo yenu; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.
12 Naam, nitaleta watu watembee juu yenu, naam, watu wangu Israeli; nao watakumiliki, nawe utakuwa urithi wao, wala hutawafisha watoto wao tena tangu leo.
13 Bwana MUNGU asema hivi; Kwa kuwa watu hukuambia, wewe nchi u mwenye kula watu, nawe umekuwa mwenye kufisha watu wa taifa lako;
14 basi hutakula watu tena, wala hutafisha watu wa taifa lako tena, asema Bwana MUNGU;
15 wala sitakusikizisha tena aibu yao wasioamini, wala hutachukua matukano ya watu tena; wala hutalikwaza taifa lako tena, asema Bwana MUNGU.
16 Tena, neno la Bwana likanijia, kusema,
17 Mwanadamu, nyumba ya Israeli walipokaa katika nchi yao wenyewe, waliitia uchafu kwa njia yao na kwa matendo yao. Njia yao mbele zangu ilikuwa kama uchafu wa mwanamke wakati wa kutengwa kwake.
18 Kwa hiyo nalimwaga hasira yangu juu yao, kwa ajili ya damu waliyoimwaga juu ya nchi, na kwa sababu wameitia uchafu kwa vinyago vyao.
19 Nikawatawanya katika mataifa, wakatapanyika katika nchi nyingi; kwa kadiri ya njia yao, na kwa kadiri ya matendo yao, naliwahukumu.
20 Nao walipoyafikilia mataifa yale waliyoyaendea, walilitia unajisi jina langu takatifu; kwa kuwa watu waliwanena, wakisema, Watu hawa ni watu wa Bwana, nao wametoka katika nchi yake.
21 Lakini, naliwahurumia kwa ajili ya jina langu takatifu, ambalo nyumba ya Israeli walikuwa wamelitia unajisi katika mataifa waliyoyaendea.
22 Kwa hiyo; waambieni nyumba ya Israeli, Bwana MUNGU asema hivi Sitendi hili kwa ajili yenu, Ee nyumba ya Israeli, bali kwa ajili ya jina langu takatifu, mlilolitia unajisi katika mataifa mliyoyaendea.
23 Nami nitalitakasa jina langu kuu, lililotiwa unajisi katika mataifa, mlilolitia unajisi kati yao; nao mataifa watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, asema Bwana MUNGU, nitakapotakaswa kati yenu mbele ya macho yao.
24 Maana nitawatwaa kati ya mataifa, nami nitawakusanya na kuwatoa katika nchi zote, na kuwarudisha katika nchi yenu wenyewe.
25 Nami nitawanyunyizia maji safi, nanyi mtakuwa safi; nitawatakaseni na uchafu wenu wote, na vinyago vyenu vyote.
26 Nami nitawapa ninyi moyo mpya, nami nitatia roho mpya ndani yenu, nami nitatoa moyo wa jiwe uliomo ndani ya mwili wenu, nami nitawapa moyo wa nyama.
27 Nami nitatia roho yangu ndani yenu, na kuwaendesha katika sheria zangu, nanyi mtazishika hukumu zangu, na kuzitenda.
28 Nanyi mtakaa katika nchi ile niliyowapa baba zenu, nanyi mtakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wenu.
29 Nami nitawaokoeni na uchafu wenu wote; nitaiita ngano, na kuiongeza, wala sitaweka njaa juu yenu tena.
30 Nami nitazidisha matunda ya miti, na mazao ya mashamba, msipate tena kutukanwa na mataifa kwa sababu ya njaa.
31 Ndipo mtazikumbuka njia zenu mbaya, na matendo yenu yasiyokuwa mema, nanyi mtajichukia nafsi zenu kwa macho yenu, kwa sababu ya maovu yenu na machukizo yenu.
32 Ijulikane kwenu ya kuwa silitendi neno hili kwa ajili yenu, asema Bwana MUNGU; tahayarikeni, na kufadhaika, kwa sababu ya njia zenu, Enyi nyumba ya Israeli.
33 Bwana MUNGU asema hivi; Siku ile nitakapowatakaseni na maovu yenu yote, nitaifanya miji ikaliwe na watu, na palipobomolewa pajengwe tena.
34 Nchi iliyokuwa ukiwa italimwa, ijapokuwa ilikuwa ukiwa mbele ya macho ya watu wote waliopita.
35 Nao watasema, Nchi hii, iliyokuwa ukiwa, imekuwa kama bustani ya Adeni; nayo miji iliyokuwa mahame, na ukiwa, na magofu, sasa ina maboma, inakaliwa na watu.
36 Ndipo mataifa, waliobaki karibu yenu pande zote, watajua ya kuwa mimi, Bwana, nimejenga mahali palipoharibika, nami nimepanda mbegu katika nchi iliyokuwa ukiwa; mimi, Bwana, nimesema hayo; tena nitayatenda.
37 Bwana MUNGU asema hivi, Tena kwa ajili ya jambo hili nitaulizwa na nyumba ya Israeli, ili niwatendee; nami nitawaongeza kwa watu kama kundi la kondoo.
38 Kama kundi lililo tayari kutolewa sadaka, kama kundi la Yerusalemu katika sikukuu zake zilizoamriwa; ndivyo itakavyojazwa watu, miji ile iliyokuwa maganjo; nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.

Ezekieli 37


1 Mkono wa Bwana ulikuwa juu yangu, naye akanichukua nje katika roho ya Bwana, akaniweka chini, katikati ya bonde; nalo limejaa mifupa;
2 akanipitisha karibu nayo pande zote; na tazama, palikuwa na mifupa mingi katika ule uwanda! Nayo, tazama, ilikuwa mikavu sana.
3 Akaniambia, Mwanadamu, je! Mifupa hii yaweza kuishi? Nami nikajibu, Ee Bwana MUNGU, wajua wewe.
4 Akaniambia tena, Toa unabii juu ya mifupa hii, uiambie, Enyi mifupa mikavu, lisikieni neno la Bwana.
5 Bwana MUNGU aiambia mifupa hii maneno haya; Tazama, nitatia pumzi ndani yenu, nanyi mtaishi.
6 Nami nitatia mishipa juu yenu, nami nitaleta nyama iwe juu yenu, na kuwafunika ngozi, na kutia pumzi ndani yenu, nanyi mtaishi; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.
7 Basi nikatoa unabii kama nilivyoamriwa; hata nilipokuwa nikitoa unabii, palikuwa na mshindo mkuu; na tazama, tetemeko la nchi, na ile mifupa ikasogeleana, mfupa kwa mfupa mwenziwe.
8 Nikatazama, kumbe! Kulikuwa na mishipa juu yake, nyama ikatokea juu yake, ngozi ikaifunika juu yake; lakini haikuwamo pumzi ndani yake.
9 Ndipo akaniambia, Tabiri, utabirie upepo, mwanadamu, ukauambie upepo, Bwana MUNGU asema hivi; Njoo, kutoka pande za pepo nne, Ee pumzi, ukawapuzie hawa waliouawa, wapate kuishi.
10 Basi nikatabiri kama alivyoniamuru; pumzi ikawaingia, wakaishi, wakasimama kwa miguu yao, jeshi kubwa mno.
11 Kisha akaniambia, Mwanadamu, mifupa hii ni nyumba yote ya Israeli; tazama, wao husema, Mifupa yetu imekauka, matumaini yetu yametupotea; tumekatiliwa mbali kabisa.
12 Basi tabiri, uwaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, nitafunua makaburi yenu, na kuwapandisha kutoka katika makaburi yenu, enyi watu wangu, nami nitawaingizeni katika nchi ya Israeli.
13 Nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, nitakapoyafunua makaburi yenu, na kuwatoa ninyi katika makaburi yenu, enyi watu wangu.
14 Nami nitatia roho yangu ndani yenu, nanyi mtaishi, nami nitawawekeni katika nchi yenu, nanyi mtajua ya kuwa mimi, Bwana, nimesema hayo, na kuyatimiza, asema Bwana.
15 Neno la Bwana likanijia tena, kusema,
16 Na wewe mwanadamu, twaa kijiti kimoja; ukaandike juu yake, Kwa Yuda, na kwa wana wa Israeli wenzake; kisha, twaa kijiti cha pili; ukaandike juu yake, Kwa Yusufu, kijiti cha Efraimu, na kwa nyumba yote ya Israeli wenzake;
17 ukaviunge pamoja kwa ajili yako hiki na hiki viwe kijiti kimoja, viwe kimoja katika mkono wako.
18 Na wana wa watu wangu watakapokuambia, wakisema, Je! Hutatuonyesha maana ya mambo hayo utendayo?
19 Waambie, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, nitakitwaa kijiti cha Yusufu, kilicho mkononi mwa Efraimu, na kabila za Israeli wenzake, nami nitawaweka pamoja nacho, yaani, pamoja na kijiti cha Yuda, na kuvifanya kuwa kijiti kimoja; navyo vitakuwa kimoja mkononi mwangu.
20 Navyo vijiti, ambavyo uliandika juu yake, vitakuwa mkononi mwako mbele ya macho yao.
21 Ukawaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, nitawatwaa wana wa Israeli toka kati ya mataifa walikokwenda, nami nitawakusanya pande zote, na kuwaleta katika nchi yao wenyewe;
22 nami nitawafanya kuwa taifa moja katika nchi hiyo, juu ya milima ya Israeli; na mfalme mmoja atakuwa mfalme wao wote; wala hawatakuwa tena mataifa mawili, wala hawatagawanyikana kuwa falme mbili tena, hata milele.
23 Wala hawatajitia uchafu tena kwa vinyago vyao, wala kwa vitu vyao vichukizavyo, wala kwa makosa yao mojawapo; lakini nitawaokoa, na kuwatoa katika makao yao yote, ambayo wamefanya dhambi ndani yake, nami nitawatakasa; basi watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao.
24 Na mtumishi wangu, Daudi, atakuwa mfalme juu yao, nao wote watakuwa na mchungaji mmoja; nao wataenenda katika hukumu zangu, na kuzishika amri zangu, na kuzitenda.
25 Nao watakaa katika nchi niliyompa Yakobo, mtumishi wangu, walimokaa baba zenu; nao watakaa humo, wao na watoto wao, na watoto wa watoto wao, milele; na Daudi, mtumishi wangu, atakuwa mkuu wao milele.
26 Tena nitafanya agano la amani pamoja nao; litakuwa agano la milele pamoja nao; nami nitawaweka na kuwazidisha, na patakatifu pangu nitapaweka katikati yao milele.
27 Tena maskani yangu itakuwa pamoja nao; nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.
28 Na mataifa watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, mimi niwatakasaye Israeli, patakatifu pangu patakapokuwa katikati yao milele.

Ezekieli 38


1 Neno la Bwana likanijia, kusema,
2 Mwanadamu, kaza uso wako, umwelekee Gogu, wa nchi ya Magogu, mkuu wa Roshi, Mesheki, na Tubali, ukatabiri juu yake,
3 useme, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi ni juu yako, Ewe Gogu, mkuu wa Roshi, na Mesheki, na Tubali;
4 nami nitakugeuza na kutia kulabu katika mataya yako, nami nitakutoa, pamoja na jeshi lako lote, farasi na hao wapandao farasi, wote wamevaa silaha za namna zote, jeshi kubwa sana, wenye ngao na kigao, wote wakishika upanga;
5 Uajemi, na Kushi, na Putu, pamoja nao; wote wana ngao na chapeo;
6 Gomeri, na vikosi vyake vyote; nyumba ya Togarma, pande za mwisho za kaskazini, na vikosi vyake vyote; naam, watu wengi pamoja nawe.
7 Ujiweke tayari, naam, jiweke tayari, wewe na majeshi yako yote waliokukusanyikia, nawe uwe jemadari wao.
8 Na baada ya siku nyingi utajiliwa; katika miaka ya mwisho, utaingia nchi iliyorudishiwa hali yake ya kwanza, baada ya kupigwa kwa upanga, iliyokusanywa toka kabila nyingi za watu, juu ya milima ya Israeli, iliyokuwa ukiwa wa daima; lakini imetolewa katika kabila za watu, nao watakaa salama salimini wote pia.
9 Nawe utapaa juu, utakuja kama tufani, utakuwa kama wingu kuifunika nchi, wewe, na vikosi vyako vyote, na kabila nyingi za watu pamoja nawe.
10 Bwana MUNGU asema hivi; Itakuwa katika siku hiyo, mawazo yataingia moyoni mwako, nawe utakusudia kusudi baya;
11 nawe utasema, Nitapanda juu niiendee nchi yenye vijiji visivyo na maboma; nitawaendea watu wanaostarehe, wanaokaa salama, wote wakikaa pasipo kuta, ambao hawana makomeo wala malango;
12 ili kuteka mateka, na kuwinda mawindo; uugeuze mkono wako juu ya mahali palipoharibika, ambapo sasa panakaliwa na watu, na juu ya watu waliokusanyika toka mataifa, waliopata ng'ombe na mali, wakaao katikati ya dunia.
13 Sheba, na Dedani, na wafanya biashara wa Tarshishi, pamoja na wana-simba wake wote, watakuambia, Je! Umekuja kuteka mateka? Umekusanya jeshi lako, ili kuwinda mawindo? Kuchukua fedha na dhahabu, kuchukua ng'ombe na mali, kuteka mateka mengi sana?
14 Basi, mwanadamu, tabiri, umwambie Gogu, Bwana MUNGU asema hivi; Katika siku ile watu wangu, Israeli, watakapokaa salama, hutapata habari?
15 Nawe utakuja kutoka mahali pako, kutoka pande za mwisho za kaskazini, wewe, na watu wa kabila nyingi pamoja nawe, wote wamepanda farasi, kusanyiko kubwa, na jeshi kuu;
16 nawe utapanda juu uwajilie watu wangu, Israeli, kama wingu kuifunika nchi; itakuwa katika siku za mwisho, nitakuleta upigane na nchi yangu, ili mataifa wanijue, nitakapotakaswa kwako, Ewe Gogu, mbele ya macho yao.
17 Bwana MUNGU asema hivi; Je! Wewe ndiwe niliyemnena zamani za kale, kwa vinywa vya watumishi wangu, manabii wa Israeli, waliotabiri siku zile kwa muda wa miaka mingi, ya kwamba nitakuleta upigane nao?
18 Itakuwa katika siku hiyo, Gogu atakapokuja kupigana na nchi ya Israeli, asema Bwana MUNGU, ghadhabu yangu itapanda katika mianzi ya pua yangu.
19 Kwa maana katika wivu wangu, na katika moto wa ghadhabu yangu, nimenena, Hakika katika siku ile kutakuwako tetemeko kubwa katika nchi ya Israeli;
20 hata samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama wa kondeni, na vitu vyote vitambaavyo juu ya nchi, na wanadamu wote walio juu ya uso wa nchi, watatetemeka mbele ya uso wangu; nayo milima itatupwa chini, na magenge yataanguka, na kila ukuta utaanguka chini.
21 Nami nitaita upanga, uje juu yake katika milima yangu yote, asema Bwana MUNGU; nao upanga wa kila mtu utakuwa juu ya ndugu yake.
22 Nami nitamhukumu kwa tauni, na kwa damu; nami nitanyesha mvua ifurikayo, na mvua ya mawe makubwa sana, na moto na kiberiti juu yake, na vikosi vyake, na watu wa kabila nyingi walio pamoja naye.
23 Nami nitajitukuza, na kujitakasa, na kujidhihirisha, mbele ya macho ya mataifa mengi; nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.

Ezekieli 39


1 Na wewe, mwanadamu, tabiri juu ya Gogu, useme, Bwana MUNGU asema hivi, Tazama, mimi ni juu yako, Ewe Gogu, mkuu wa Roshi, Mesheki, na Tubali;
2 nami nitakugeuza na kukuongoza, nami nitakupandisha toka pande za mwisho za kaskazini; nami nitakuleta juu ya milima ya Israeli;
3 nami nitaupiga upinde wako, utoke katika mkono wako wa kushoto, na mishale yako nitaiangusha, itoke katika mkono wako wa kulia.
4 Utaanguka juu ya milima ya Israeli, wewe, na vikosi vyako vyote, na watu wa kabila nyingi walio pamoja nawe; nami nitakutoa na kuwapa ndege wa kila namna walao nyama, na wanyama wa nchi, uliwe na wao.
5 Utaanguka katika uwanda; kwa maana mimi nimenena neno hili, asema Bwana MUNGU.
6 Nami nitapeleka moto juu ya Magogu; na juu ya watu wote wakaao salama katika visiwa; nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.
7 Na jina langu takatifu nitalifanya kuwa limejulika kati ya watu wangu Israeli; wala sitaliacha jina langu takatifu kutiwa unajisi tena; nao mataifa watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, na Aliye Mtakatifu katika Israeli.
8 Tazama, linakuja, nalo litatendeka, asema Bwana MUNGU; hii ndiyo siku ile niliyoinena.
9 Hao wakaao katika miji ya Israeli watatoka, nao watafanya mioto kwa silaha za vita na kuziteketeza, ngao, na vigao, na pinde, na mishale, na mafumo, na mikuki, nao watazitumia kama kuni kwa muda wa miaka saba;
10 hata hawataokota kuni mashambani, wala hawatakata kuni msituni; maana watafanya mioto kwa silaha zile; nao watawateka nyara watu waliowateka wao, na kunyang'anya vitu vya watu walionyang'anya vitu vyao, asema Bwana MUNGU.
11 Tena, itakuwa katika siku hiyo, nitampa Gogu pa kuzikia katika Israeli, bonde la wapitao, upande wa mashariki wa bahari; nalo litawazuia wapitao; na huko watamzika Gogu na watu wake jamii yote; nao wataliita, Bonde la Hamon-Gogu.
12 Na kwa muda wa miezi saba nyumba ya Israeli watakuwa wakiwazika, wapate kuisafisha nchi.
13 Naam, watu wote wa nchi hiyo watawazika; itakuwa ni sifa kwao katika siku ile nitakapotukuzwa, asema Bwana MUNGU.
14 Nao watawachagua watu wa kufanya kazi ya daima, watakaopita kati ya nchi, ili kuwazika waliosalia juu ya uso wa nchi, ili kuisafisha; miezi saba itakapokwisha kupita watatafuta.
15 Na hao wapitao kati ya nchi watatafuta; na mtu ye yote aonapo mfupa wa mtu, ndipo atakapoweka alama karibu nao, hata wazishi watakapouzika katika bonde la Hamon- Gogu.
16 Tena, Hamona litakuwa jina la mji. Hivyo ndivyo watakavyosafisha nchi.
17 Na wewe, mwanadamu, Bwana MUNGU asema hivi; Sema na ndege wa kila namna, na kila mnyama wa kondeni, Jikusanyeni, mje; jikusanyeni pande zote mwijilie sadaka yangu niifanyayo kwa ajili yenu, naam, sadaka kubwa juu ya milima ya Israeli, mpate kula nyama na kunywa damu.
18 Mtakula nyama yao walio hodari, na kunywa damu ya wakuu wa dunia, ya kondoo waume na ya wana-kondoo, na ya mbuzi, na ya ng'ombe, wote na wanono wa Bashani.
19 Nanyi mtakula mafuta na kushiba, mtakunywa damu na kulewa, na sadaka yangu niliyoifanya kwa ajili yenu.
20 Nanyi mtashibishwa mezani pangu kwa farasi, na magari ya vita, na mashujaa, na watu wote wa vita, asema Bwana MUNGU.
21 Nami nitauweka utukufu wangu kati ya mataifa, na mataifa wote wataiona hukumu yangu niliyoitekeleza, na mkono wangu niliouweka juu yao.
22 Basi, nyumba ya Israeli watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, Mungu wao, tangu siku hiyo na baadaye.
23 Nao mataifa watajua ya kuwa nyumba ya Israeli walihamishwa, na kwenda kifungoni, kwa sababu ya uovu wao; kwa sababu waliniasi, nami nikawaficha uso wangu; basi nikawatia katika mikono ya adui zao, nao wakaanguka kwa upanga, wote pia.
24 Kwa kadiri ya uchafu wao, kwa kadiri ya makosa yao, ndivyo nilivyowatenda, nami nikawaficha uso wangu.
25 Kwa sababu hiyo, Bwana MUNGU asema hivi, Sasa nitawarejeza watu wa Yakobo waliohamishwa, nitawahurumia nyumba yote ya Israeli; nami nitalionea wivu jina langu takatifu.
26 Nao watachukua aibu yao, na makosa yao yote waliyoniasi, watakapokaa salama katika nchi yao wenyewe, wala hapana mtu atakayewatia hofu;
27 nitakapokuwa nimewaleta tena kutoka kabila za watu, na kuwakusanya kwa kuwatoa katika nchi za adui zao, na kutakaswa kati yao mbele ya macho ya mataifa mengi.
28 Nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, Mungu wao, kwa kuwa naliwahamisha, waende utumwani kati ya mataifa, na mimi nikawakusanya, na kuwaingiza katika nchi yao wenyewe; wala sitawaacha tena huko kamwe, hata mmojawapo;
29 wala sitawaficha uso wangu tena; kwa maana nimemwaga roho yangu juu ya nyumba ya Israeli, asema Bwana MUNGU.

Ezekieli 40


1 Katika mwaka wa ishirini na tano wa kuhamishwa kwetu, mwanzo wa mwaka, siku ya kumi ya mwezi, katika mwaka wa kumi na nne baada ya kupigwa mji, siku iyo hiyo, mkono wa Bwana ulikuwa juu yangu, akanileta huko.
2 Katika maono ya Mungu alinileta mpaka nchi ya Israeli, akaniweka juu ya mlima mrefu sana, ambao juu yake palikuwapo kana kwamba ni umbo la mji upande wa kusini.
3 Akanileta huko, na tazama, alikuwapo mtu, ambaye kuonekana kwake kulikuwa kama kuonekana kwa shaba, naye alikuwa na uzi wa kitani mkononi mwake, na mwanzi wa kupimia; akasimama karibu na lango.
4 Mtu yule akaniambia, Mwanadamu, tazama kwa macho yako, sikia kwa masikio yako, ukaweke moyoni mwako, yote nitakayokuonyesha; maana umeletwa hapa kusudi nikuonyeshe haya; tangaza habari ya yote utakayoyaona kwa nyumba ya Israeli.
5 Na, tazama, kulikuwa na ukuta nje ya nyumba pande zote, na katika mkono wa mtu yule mwanzi wa kupimia, urefu wake dhiraa sita, kila dhiraa, dhiraa na shubiri; basi akaupima upana wa jengo lile, mwanzi mmoja, na urefu wake, mwanzi mmoja.
6 Kisha akaenda mpaka lango lielekealo upande wa mashariki, akapanda madaraja yake; akakipima kizingiti cha lango; upana wake mwanzi mmoja; na kizingiti cha pili, upana wake mwanzi mmoja.
7 Na kila chumba, upana wake mwanzi mmoja, na urefu wake mwanzi mmoja; na nafasi iliyokuwa kati ya vyumba ni dhiraa tano; na kizingiti cha lango lililokuwa karibu na ukumbi wa lango lililoielekea nyumba, mwanzi mmoja.
8 Akaupima na ukumbi wa lango lililoielekea nyumba, mwanzi mmoja.
9 Kisha akaupima ukumbi wa lango, dhiraa nane; na miimo yake, dhiraa mbili; na ukumbi wa lango uliielekea nyumba.
10 Na vyumba vya walinzi, vya lango upande wa mashariki, vilikuwa vitatu upande huu, na vitatu upande huu; vyote vitatu vya kipimo kimoja; nayo miimo ilikuwa na kipimo kimoja, upande huu na upande huu.
11 Akaupima upana wa mahali pa kuliingilia lango, dhiraa kumi; na urefu wa lango, dhiraa kumi na tatu.
12 Na mpaka, mbele ya vile vyumba, dhiraa moja upande huu, na mpaka, dhiraa moja upande huu; na vile vyumba, dhiraa sita upande huu, na dhiraa sita upande huu.
13 Akalipima lango, toka paa la chumba kimoja hata paa la chumba cha pili, upana wa dhiraa ishirini na tano; mlango mmoja ukielekea mlango wa pili.
14 Akafanya miimo pia, dhiraa sitini; na uwanda uliufikilia mwimo, lango lile likizungukwa pande zote.
15 Na toka mahali palipo mbele ya lango, penye maingilio yake, hata mahali palipo mbele ya ukumbi wa ndani ya lango, dhiraa hamsini.
16 Na kwa vile vyumba palikuwa na madirisha yaliyofungwa, na kwa miimo yake ndani ya lango pande zote, na kwa matao yake vivyo hivyo; na madirisha yalikuwako, pande zote upande wa ndani, tena palikuwa na mitende juu ya kila mwimo.
17 Ndipo akanileta mpaka ua wa nje, na tazama, palikuwa na vyumba, na sakafu iliyofanyizwa kwa ule ua pande zote; vyumba thelathini vilikuwako juu ya sakafu ile.
18 Na ile sakafu ilikuwa kando ya malango, urefu wake sawasawa na urefu wa malango, yaani, sakafu ya chini.
19 Kisha akaupima upana, toka mahali palipokuwa mbele ya lango la chini hata mahali palipokuwa mbele ya ua wa ndani, nje yake, dhiraa mia upande wa mashariki, na upande wa kaskazini.
20 Nalo lango la ua wa nje, lililoelekea kaskazini, akalipima urefu wake, na upana wake.
21 Na vyumba vyake vya walinzi vilikuwa vitatu upande huu, na vitatu upande huu; na miimo yake, na matao yake, kipimo chake ni sawasawa na kipimo cha lango la kwanza; urefu wake dhiraa hamsini, na upana wake dhiraa ishirini na tano.
22 Na madirisha yake, na matao yake, na mitende yake, kipimo chake ni sawasawa na kipimo cha lango lililoelekea upande wa mashariki; nao hupanda kwa madaraja saba; na matao yake yalikuwa mbele yake.
23 Na ule ua wa ndani ulikuwa na lango lililoelekea lile lango la pili, upande wa kaskazini, na upande wa mashariki; akapima toka lango hata lango, dhiraa mia.
24 Akanileta mpaka upande wa kusini, na tazama, lango lililoelekea kusini; akaipima miimo yake, na matao yake, sawasawa na vipimo hivyo.
25 Tena palikuwa na madirisha ndani yake, na katika matao yake pande zote kama madirisha hayo; urefu wake dhiraa hamsini, na upana wake dhiraa ishirini na tano.
26 Tena palikuwa na madaraja saba ya kulipandia, na matao yake yalikuwa mbele yake; nalo lilikuwa na mitende, mmoja upande huu, na mmoja upande huu, juu ya miimo yake.
27 Tena ua wa ndani ulikuwa na lango, lililoelekea kusini; akapima toka lango hata lango, kwa kuelekea upande wa kusini, dhiraa mia.
28 Kisha akanileta mpaka ua wa ndani karibu na lango lililoelekea kusini; akalipima lango la kusini kwa vipimo vivyo hivyo;
29 navyo vyumba vyake vya walinzi, na miimo yake, na matao yake, sawasawa na vipimo hivyo; tena palikuwa na madirisha ndani yake, na katika matao yake pande zote; urefu wake dhiraa hamsini, na upana wake dhiraa ishirini na tano.
30 Tena palikuwa na matao pande zote, urefu wake dhiraa ishirini na tano na upana wake dhiraa tano.
31 Na matao yake yaliuelekea ua wa nje, na mitende ilikuwa juu ya miimo yake; palikuwa na madaraja manane ya kuupandia.
32 Akanileta mpaka ua wa ndani ulioelekea upande wa mashariki, akalipima lango kwa vipimo vivyo hivyo;
33 navyo vyumba vyake vya walinzi, na miimo yake, na matao yake, kwa vipimo hivyo; tena palikuwa na madirisha ndani yake, na katika matao yake pande zote; urefu wake dhiraa hamsini, na upana wake dhiraa ishirini na tano.
34 Na matao yake yaliuelekea ua wa nje; na mitende ilikuwa juu ya miimo yake, upande huu na upande huu; tena palikuwa na madaraja manane ya kuupandia.
35 Akanileta mpaka lango lililoelekea upande wa kaskazini; akalipima kwa vipimo vivyo hivyo;
36 vyumba vyake vya walinzi, na miimo yake, na matao yake; tena palikuwa na madirisha ndani yake pande zote; urefu wake dhiraa hamsini, na upana wake dhiraa ishirini na tano.
37 Na miimo yake iliuelekea ua wa nje; na mitende ilikuwa juu ya miimo yake, upande huu na upande huu; tena palikuwa na madaraja manane ya kuupandia.
38 Na chumba, pamoja na lango lake, kilikuwa karibu na miimo ya malango; ndiko walikoiosha sadaka ya kuteketezwa.
39 Na katika ukumbi wa lango palikuwa na meza mbili upande huu, na meza mbili upande huu, ili kuichinja sadaka ya kuteketezwa, na sadaka ya dhambi, na sadaka ya hatia.
40 Na upande mmoja, nje, penye madaraja ya kuliingia lango lililoelekea kaskazini, palikuwa na meza mbili; na upande wa pili, ulio wa ukumbi wa lango hilo, palikuwa na meza mbili.
41 Palikuwa na meza nne upande huu, na meza nne upande huu, karibu na lango; meza nane ambazo juu yake walizichinja sadaka.
42 Tena palikuwa na meza nne kwa sadaka za kuteketezwa, za mawe yaliyochongwa; urefu wake dhiraa moja na nusu, na upana wake dhiraa moja na nusu, na kimo chake dhiraa moja; juu yake waliviweka vyombo vya kuchinjia sadaka za kuteketezwa na sadaka.
43 Tena hizo kulabu, ambazo urefu wake ni shubiri, zilifungwa ndani pande zote; na juu ya meza hizo ilikuwako nyama ya matoleo.
44 Tena nje ya lango la ndani palikuwa na vyumba kwa waimbaji, katika ua wa ndani, uliokuwa kando ya lango lililoelekea kaskazini, navyo vilikabili upande wa kusini; na kimoja kando ya lango lililoelekea upande wa mashariki, kilikabili upande wa kaskazini.
45 Akaniambia, Chumba hiki kinachokabili upande wa kusini ni kwa makuhani, yaani, hao walinzi wa malindo ya nyumba.
46 Nacho chumba kinachokabili upande wa kaskazini ni kwa makuhani, walinzi wa malindo ya madhabahu; hao ni wana wa Sadoki, ambao miongoni mwa wana wa Lawi wamkaribia Bwana, ili kumtumikia.
47 Akaupima huo ua, na urefu wake ulikuwa dhiraa mia, na upana wake dhiraa mia, mraba; nayo dhabahu ilikuwa mbele ya nyumba.
48 Ndipo akanileta mpaka ukumbi wa nyumba, akapima kila mwimo wa ukumbi, dhiraa tano upande huu, na dhiraa tano upande huu; na upana wa lango ulikuwa dhiraa tatu upande huu, na dhiraa tatu upande huu.
49 Urefu wa ukumbi ulikuwa dhiraa ishirini, na upana wake dhiraa kumi na moja; karibu na madaraja ambayo waliupandia; tena palikuwa na nguzo karibu na miimo, moja upande huu, na moja upande huu.

Ezekieli 41


1 Akanileta mpaka hekaluni, akaipima miimo, upana wake dhiraa sita upande mmoja, na upana wake dhiraa sita upande wa pili, ambao ulikuwa ni upana wa maskani.
2 Na upana wa maingilio yake ulikuwa dhiraa kumi; na mbavu za maingilio zilikuwa dhiraa tano upande huu, na dhiraa tano upande huu; akaupima urefu wake, dhiraa arobaini, na upana wake, dhiraa ishirini.
3 Kisha akaingia ndani, akapima kila mwimo wa maingilio, dhiraa mbili; nayo maingilio, dhiraa sita; na upana wa maingilio dhiraa saba.
4 Akaupima urefu wake; dhiraa ishirini, na upana wake, dhiraa ishirini, mbele ya hekalu; akaniambia, Hapa ndipo mahali patakatifu kuliko kila mahali.
5 Kisha akaupima ukuta wa nyumba, dhiraa sita; na upana wa kila chumba cha mbavuni, dhiraa nne, kuizunguka nyumba pande zote.
6 Na vile vyumba vya mbavuni vilikuwa na orofa tatu, moja juu ya mwenziwe; vilikuwa thelathini, safu baada ya safu; navyo viliingia ndani ya ukuta uliokuwa wa nyumba, kwa vile vyumba vya mbavuni pande zote vipate kushikamana nao, wala visishikamane na ukuta wa nyumba.
7 Na vile vyumba vya mbavuni vilizidi kuwa vipana, kwa kadiri vilivyoizunguka nyumba juu kwa juu; maana kule kuzunguka kwake kulikwenda juu kwa juu, kuizunguka nyumba; basi upana wa nyumba ulikuwa ule ule hata juu; basi hupanda juu toka chumba cha chini hata chumba cha juu, kwa njia ya kile chumba cha katikati.
8 Tena, nikaona ya kwamba nyumba ile ilikuwa na sakafu ya mawe, iliyoinuliwa pande zote; nayo misingi ya vyumba vya mbavuni ilikuwa mwanzi mzima wa dhiraa sita.
9 Unene wa ukuta uliokuwa wa vile vyumba vya mbavuni, upande wa nje, ulikuwa dhiraa tano; nayo nafasi iliyobaki ilikuwa dhiraa tano; na kati ya vyumba vya mbavuni vya nyumba,
10 na vyumba vya walinzi, upana wa dhiraa ishirini, kuizunguka nyumba pande zote.
11 Na milango ya vile vyumba vya mbavuni iliielekea nafasi ile iliyobaki, mlango mmoja ulielekea upande wa kaskazini, na mlango mmoja upande wa kusini; na upana wa nafasi iliyobaki ulikuwa dhiraa tano pande zote.
12 Nalo jengo lililokabili mahali palipotengeka upande wa magharibi, upana wake dhiraa sabini; na ukuta wa lile jengo, unene wake dhiraa tano pande zote, na urefu wake dhiraa tisini.
13 Basi akaipima nyumba, urefu wake dhiraa mia; na mahali pale palipotengeka na jengo lile, pamoja na kuta zake, urefu wake dhiraa mia;
14 tena upana wa uso wa nyumba, na wa mahali palipotengeka upande wa mashariki, dhiraa mia.
15 Akaupima urefu wa jengo lile lililokabili mahali palipotengeka, palipokuwa nyuma yake, na baraza zake upande huu na upande huu, dhiraa mia; na hekalu la ndani, na kumbi za ua;
16 na vizingiti, na madirisha yaliyofungwa, na baraza za pande zote za orofa zile tatu, zilizokikabili kizingiti, zilitiwa mabamba ya mti pande zote; na toka chini hata madirishani; (nayo madirisha yamefunikwa);
17 na mpaka juu ya mlango hata nyumba ya ndani, na nje, na juu ya kuta zote pande zote, katika nyumba ya ndani, na ya nje,
18 kulipambwa kwa makerubi na mitende; mtende mmoja kati ya kerubi na kerubi, na kila kerubi lilikuwa na nyuso mbili;
19 basi palikuwa na uso wa mwanadamu kuelekea mtende mmoja, na uso wa mwana-simba kuelekea mtende wa pili; ndivyo vilivyofanyika katika nyumba nzima pande zote.
20 Toka chini hata juu ya mlango makerubi yamefanyika, na mitende, na vivi hivi ukuta wa hekalu.
21 Na hilo hekalu, miimo ya milango yake ilikuwa ya miraba; na mbele ya patakatifu kuonekana kwake palionekana kama hapo kwanza.
22 Madhabahu ilikuwa ni ya miti, kimo chake dhiraa tatu, na urefu wake dhiraa mbili; na pembe zake, na msingi wake, na kuta zake zilikuwa za miti; akaniambia, Hii ndiyo meza iliyo mbele za Bwana.
23 Nalo hekalu na patakatifu palikuwa na milango miwili.
24 Na milango hiyo, kila mmoja ulikuwa na mbao mbili; mbao mbili zigeukazo; mbao mbili za mlango mmoja, na mbao mbili za mlango wa pili.
25 Na milango ya hekalu ilifanyiziwa makerubi na mitende vile vile, kama zile kuta zilivyofanyiziwa; tena palikuwa na boriti nene juu ya uso wa ukumbi, nje.
26 Tena palikuwa na madirisha yaliyofungwa, na mitende, upande huu na upande huu, katika pande za ukumbi; ndiyo habari ya vyumba vya mbavuni vya nyumba hiyo, na vya boriti zile nene.

Ezekieli 42


1 Ndipo akanileta mpaka ua wa nje, njia ya kuelekea upande wa kaskazini; akaniingiza katika chumba kilichopakabili mahali palipotengeka, na kilicholikabili jengo upande wa kaskazini;
2 kukabili urefu wa dhiraa mia palikuwa na mlango wa kaskazini, na upana wake ni dhiraa hamsini.
3 Kukabili zile dhiraa ishirini za ua wa ndani, na kukabili sakafu ya mawe ya ua wa nje, palikuwa na baraza kukabili baraza katika orofa ya tatu.
4 Na mbele ya vile vyumba palikuwa na njia, upana wake dhiraa kumi upande wa ndani, njia ya dhiraa mia, na milango yake ilielekea upande wa kaskazini.
5 Basi vile vyumba vya juu vilikuwa vifupi zaidi; kwa maana baraza zile zilivipunguza kuliko zilivyovipunguza vya chini na vya katikati.
6 Maana vilikuwa vina orofa tatu, wala havikuwa na nguzo kama nguzo za zile nyua; basi kila kilichokuwa cha juu kilikuwa chembamba kuliko cha chini na cha katikati, kutoka chini.
7 Na ukuta ule uliokuwa nje, ubavuni mwa vyumba vile, ulioelekea ua wa nje, kuvikabili vyumba vile, urefu wake ni dhiraa hamsini.
8 Maana urefu wa vyumba vile, vilivyokuwa katika ua wa nje, ulikuwa dhiraa hamsini; na tazama, mbele ya hekalu, dhiraa mia.
9 Na toka chini ya vyumba vile palikuwa na mahali pa kuingilia upande wa mashariki, mtu aviingiavyo toka ua wa nje.
10 Tena palikuwa na vyumba katika unene wa ukuta wa ua, kuukabili upande wa mashariki, kupaelekea mahali palipotengeka, na kulielekea jengo.
11 Nayo njia iliyokuwa mbele yake, kuonekana kwake kulikuwa kama kuonekana kwake vyumba vile vilivyokuwa upande wa kaskazini, urefu ule ule, na upana ule ule; na mahali pake pa kutokea palikuwa sawasawa na vipimo vyake, na sawasawa na milango yake.
12 Na sawasawa na milango ya vyumba, vilivyoelekea upande wa kusini, palikuwa na mlango katika mwisho wa njia ile; yaani, njia iliyoukabili ukuta upande wa mashariki, mtu akiingia.
13 Kisha akaniambia, Vyumba vya upande wa kaskazini, na vyumba vya upande wa kusini, ambavyo vyaelekea mahali palipotengeka, ni vyumba vitakatifu; humo makuhani, wamkaribiao Bwana, watakula vitu vilivyo vitakatifu sana; humo wataviweka vitu vilivyo vitakatifu sana, na sadaka ya unga, na sadaka ya dhambi, na sadaka ya hatia; kwa maana mahali hapo ni patakatifu.
14 Makuhani watakapoingia ndani, hawatatoka mahali patakatifu kwenda hata ua wa nje; lakini wataweka mavazi yao katika mahali wahudumiapo; maana ni matakatifu; nao watavaa mavazi mengine, na kupakaribia mahali palipo mahali pa watu.
15 Basi, alipokuwa amekwisha kuipima nyumba ya ndani, akanileta nje, kwa njia ya lango lililokabili upande wa mashariki, akalipima pande zote.
16 Akaupima upande wa mashariki kwa mwanzi wa kupimia, mianzi mia tano, kwa mwanzi wa kupimia pande zote.
17 Akaupima upande wa kaskazini, mianzi mia tano, kwa mwanzi wa kupimia pande zote.
18 Akaupima upande wa kusini, mianzi mia tano, kwa mwanzi wa kupimia.
19 Akageuka aelekee upande wa magharibi, akapima mianzi mia tano, kwa mwanzi wa kupimia.
20 Alipima pande zake zote nne; lilikuwa na ukuta pande zote, urefu wake mianzi mia tano, na upana wake mianzi mia tano, ili kupatenga mahali palipo patakatifu, na mahali palipo pa watu wote.

Ezekieli 43


1 Kisha akanileta mpaka langoni, yaani, lango lile lielekealo upande wa mashariki;
2 na tazama, huo utukufu wa Mungu wa Israeli ulitokea kwa njia ya mashariki; na sauti yake ilikuwa kama mshindo wa maji mengi, nayo nchi iling'aa kwa utukufu wake.
3 Na maono niliyoyaona yalikuwa kama maono niliyoyaona nilipokuja kuuharibu mji; nayo maono niliyoyaona yalikuwa kama maono niliyoyaona karibu na mto wa Kebari; nikaanguka kifudifudi.
4 Na huo utukufu wa Bwana ukaingia ndani ya nyumba, kwa njia ya lango lile lielekealo upande wa mashariki.
5 Kisha Roho ikaniinua, ikanichukua mpaka ua wa ndani; na tazama, utukufu wa Bwana uliijaza nyumba.
6 Nikasikia sauti ya mmoja asemaye nami, itokayo katika nyumba hiyo; na mtu akasimama karibu nami.
7 Akaniambia, Mwanadamu, hapa ni mahali pa kiti changu cha enzi, na mahali pa nyayo za miguu yangu, nitakapokaa kati ya wana wa Israeli milele; na nyumba ya Israeli hawatalinajisi jina langu takatifu tena, wao, wala wafalme wao, kwa mambo yao ya kikahaba, na kwa mizoga ya wafalme wao, katika mahali pao pa juu;
8 kwa kuweka kizingiti chao karibu na kizingiti changu; na mwimo wao karibu na mwimo wangu; tena palikuwa na ukuta tu kati ya mimi na wao; nao wamelinajisi jina langu takatifu kwa machukizo yao waliyoyatenda; basi, kwa sababu hiyo, nimewakomesha katika hasira yangu.
9 Basi sasa wayaondoe mambo yao ya kikahaba, na mizoga ya wafalme wao, yawe mbali nami, nami nitakaa kati yao milele.
10 Na wewe, mwanadamu, waonyeshe wana wa Israeli nyumba hii, ili wayatahayarikie maovu yao; na waipime hesabu yake.
11 Na ikiwa wameyatahayarikia yote waliyoyatenda, waonyeshe umbo la nyumba, na namna yake, na matokeo yake, na maingilio yake, na maumbo yake yote, na maagizo yake yote, na kawaida zake zote, na sheria zake zote, ukayaandike machoni pao; ili walishike umbo lake lote, na maagizo yake, na kuyatenda.
12 Hii ndiyo sheria ya nyumba; juu ya kilele cha mlima, mpaka wake wote pande zote patakuwa patakatifu sana. Tazama, hii ndiyo sheria ya nyumba.
13 Na vipimo vya madhabahu kwa dhiraa ni hivi; (dhiraa ni dhiraa na shubiri); tako lake ni dhiraa moja, na upana wake dhiraa moja; na pambizo yake karibu na ncha yake pande zote, shubiri moja; na hili litakuwa tako la madhabahu.
14 Tena toka chini, juu ya nchi, hata daraja ya chini, dhiraa mbili, na upana wake dhiraa moja; tena toka daraja ndogo hata daraja kubwa, dhiraa nne, na upana wake dhiraa moja.
15 Na madhabahu ya juu itakuwa dhiraa nne; na toka madhabahu pawashwapo moto na kwenda juu zitakuwa pembe nne.
16 Na pale pawashwapo moto, urefu wake dhiraa kumi na mbili, na upana wake kumi na mbili, mraba pande zake nne.
17 Na daraja, urefu wake dhiraa kumi na nne, na upana wake dhiraa kumi na nne, pande zake nne; na pambizo yake nusu dhiraa; na tako lake dhiraa moja, kote kote, na madaraja yake yataelekea upande wa mashariki.
18 Kisha akaniambia, Mwanadamu, Bwana MUNGU asema hivi; Hizi ndizo sheria za madhabahu katika siku ile watakapoifanya, ili watoe sadaka za kuteketezwa juu yake, na kunyunyiza damu juu yake.
19 Utawapa makuhani Walawi, walio wa uzao wa Sadoki, walio karibu nami, ili kunihudumu, asema Bwana MUNGU, ng'ombe mume mchanga awe sadaka ya dhambi.
20 Nawe utatwaa baadhi ya damu yake, na kuitia juu ya pembe zake nne, na juu ya ncha nne za daraja, na juu ya pambizo yake pande zote; ndivyo utakavyoitakasa, na kuifanyia upatanisho.
21 Tena utamtwaa ng'ombe wa sadaka ya dhambi, naye utamteketeza mahali palipoamriwa pa nyumba ile, nje ya mahali patakatifu.
22 Na siku ya pili utamtoa beberu mkamilifu awe sadaka ya dhambi; nao wataisafisha madhabahu, kama walivyoisafisha kwa ng'ombe huyo.
23 Utakapokwisha kuitakasa, utatoa ng'ombe mume mchanga mkamilifu, na kondoo mume wa kundini mkamilifu.
24 Nawe utawaleta karibu mbele za Bwana, na makuhani watamwaga chumvi juu yao, nao watawatoa wawe sadaka za kuteketezwa kwa Bwana.
25 Kwa muda wa siku saba utaweka tayari mbuzi kila siku awe sadaka ya dhambi; pia wataweka tayari ng'ombe mume mchanga, na kondoo mume wa kundini, wakamilifu.
26 Kwa muda wa siku saba wataifanyia madhabahu upatanisho, na kuitakasa; ndivyo watakavyoiweka wakfu.
27 Nao watakapozitimiza siku hizo, itakuwa, siku ya nane na baadaye, makuhani watatoa sadaka zenu za kuteketezwa juu ya madhabahu, na sadaka zenu za amani nami nitawakubali ninyi, asema Bwana MUNGU.

Ezekieli 44


1 Kisha akanirudisha kwa njia ya lango lile la nje, la mahali patakatifu lililoelekea upande wa mashariki; nalo lilikuwa limefungwa.
2 Bwana akaniambia, Lango hili litafungwa, halitafunguliwa, wala mtu awaye yote hataingia kwa lango hili, kwa maana Bwana, Mungu wa Israeli, ameingia kwa hilo; basi kwa sababu hiyo litafungwa.
3 Na mkuu, yeye ndiye atakayeketi ndani yake ale chakula mbele za Bwana; ataingia kwa njia ya ukumbi wa lango, naye atatoka kwa njia iyo hiyo.
4 Kisha akanileta, kwa njia ya lango la upande wa kaskazini, mbele ya nyumba; nikaangalia, na tazama, huo utukufu wa Bwana uliijaza nyumba ya Bwana; nikaanguka kifudifudi.
5 Bwana akaniambia, Mwanadamu, weka moyoni mwako, ukatazame kwa macho yako, ukasikie kwa masikio yako, maneno yote nitakayokuambia, katika habari ya kawaida zote za nyumba ya Bwana, na ya amri zake zote; nawe weka moyoni mwako maingilio ya nyumba, pamoja na matokeo yote ya mahali patakatifu.
6 Nawe utawaambia waasi, yaani nyumba ya Israeli, Bwana MUNGU asema hivi; Enyi nyumba ya Israeli, katika machukizo yenu yote, na iwatoshe,
7 kuwa mmewaingiza wageni, ambao mioyo yao haikutahiriwa, wala miili yao haikutahiriwa, wawe ndani ya patakatifu pangu, wapatie unajisi, naam, nyumba yangu, mtoapo sadaka ya chakula changu, mafuta na damu; nao wameyavunja maagano yangu, juu ya machukizo yenu yote.
8 Wala hamkuvilinda vitu vyangu vitakatifu bali mmejiwekea walinzi wa kawaida zangu, katika patakatifu pangu.
9 Bwana MUNGU asema hivi; Hapana mgeni, ambaye moyo wake haukutahiriwa, wala mwili wake haukutahiriwa, atakayeingia patakatifu pangu, miongoni mwa wageni walio kati ya wana wa Israeli.
10 Lakini Walawi waliofarakana nami, hapo Waisraeli walipopotea, waliopotea na kuvifuata vinyago vyao, watachukua uovu wao wenyewe.
11 Hata hivyo watakuwa wahudumu katika patakatifu pangu, wakiwa wasimamizi wa malango ya nyumba, wakihudumu humo nyumbani; watawachinjia watu sadaka za kuteketezwa na dhabihu, nao watasimama mbele yao ili kuwahudumia.
12 Kwa sababu waliwahudumia mbele ya vinyago vyao, wakawa kwazo la uovu kwa nyumba ya Israeli; basi nimeuinua mkono wangu juu yao, asema Bwana MUNGU, nao watachukua uovu wao.
13 Wala hawatanikaribia, kunihudumia katika kazi ya ukuhani, wala hawatakaribia vitu vyangu vitakatifu kimojawapo, vitu vilivyo vitakatifu sana; bali watachukua aibu yao, na machukizo yao yote waliyoyatenda.
14 Lakini nitawafanya kuwa walinzi katika ulinzi wa nyumba, kwa huduma yake yote, na kwa yote yatakayotendeka ndani yake.
15 Lakini makuhani Walawi, wana wa Sadoki, waliolinda ulinzi wa patakatifu pangu, hapo wana wa Israeli walipopotea na kuniacha, hao ndio watakaonikaribia ili kunihudumia; nao watasimama mbele zangu, kunitolea mafuta na damu, asema Bwana MUNGU;
16 wataingia patakatifu pangu, nao wataikaribia meza yangu, ili kunihudumia, nao watalinda ulinzi wangu.
17 Itakuwa, hapo watakapoingia kwa malango ya ua wa ndani, watavikwa mavazi ya kitani; wala sufu haitakuwa juu yao, maadamu wanahudumu katika malango ya ua wa ndani, na ndani ya nyumba.
18 Watakuwa na vilemba vya kitani juu ya vichwa vyao, nao watakuwa na suruali za kitani viunoni mwao; hawatajifunga kiunoni kitu cho chote kifanyacho jasho.
19 Nao watakapotoka kuingia ua wa nje, yaani, ua wa nje wa watu, ndipo watakapoyavua mavazi yao waliyovaa katika huduma yao, na kuyaweka katika vile vyumba vitakatifu, nao watavaa mavazi mengine, wasije wakawatakasa watu kwa mavazi yao.
20 Hawatanyoa vichwa vyao, wala hawataacha nywele zao kuwa ndefu sana; watazipunguza nywele za vichwa vyao tu.
21 Wala kuhani awaye yote hatakunywa mvinyo, aingiapo katika ua wa ndani.
22 Wala hawataoa wanawake wajane, wala mwanamke aliyeachwa na mume wake; lakini watatwaa mabikira wa wazao wa nyumba ya Israeli, au mjane aliyefiwa na mumewe kuhani.
23 Nao watawafundisha watu wangu tofauti iliyopo kati ya vitu vitakatifu na vitu vya sikuzote, na kuwafundisha kupambanua kati ya yaliyo machafu na yaliyo safi.
24 Na katika mashindano watasimama ili kuamua; wataamua sawasawa na hukumu zangu; nao watazishika sheria zangu, na amri zangu, katika sikukuu zangu zote zilizoamriwa; nao watazitakasa sabato zangu.
25 Wala hawatakaribia maiti na kujitia unajisi; ila kwa ajili ya baba, au mama, au mwana, au binti, au ndugu mwanamume, au ndugu mwanamke asiyeolewa bado, waweza kujitia unajisi.
26 Naye akiisha kutakaswa watamhesabia siku saba.
27 Na katika siku atakayoingia ndani ya patakatifu, katika ua wa ndani, ili kuhudumu ndani ya patakatifu, atatoa sadaka yake ya dhambi, asema Bwana MUNGU.
28 Nao watakuwa na urithi; mimi ni urithi wao; wala hamtawapa milki iwayo yote katika Israeli; mimi ni milki yao.
29 Wataila sadaka ya unga, na sadaka ya dhambi, na sadaka ya hatia, na kila kitu katika Israeli kilichowekwa wakfu kitakuwa chao.
30 Na kitu cha kwanza cha malimbuko yote ya vitu vyote, na kila toleo la kila kitu cha matoleo yenu, litakuwa la makuhani. Tena mtampa kuhani sehemu ya kwanza ya unga mbichi, ili kukalisha baraka juu ya nyumba yako.
31 Makuhani hawatakula nyamafu, au iliyoraruliwa, ikiwa ya ndege au ya mnyama.

Ezekieli 45


1 Tena, mtakapoigawanya nchi kwa kura iwe urithi, mtamtolea Bwana toleo, sehemu takatifu ya nchi, urefu wake utakuwa urefu wa mianzi ishirini na tano elfu, na upana wake elfu kumi; itakuwa takatifu ndani ya mipaka yake yote pande zote.
2 Katika hiyo itakuwako sehemu kwa mahali patakatifu, urefu wake mia tano, na upana wake mia tano, mraba pande zote; na dhiraa ishirini kwa viunga vyake pande zote.
3 Na kwa kipimo hicho utapima, urefu wa ishirini na tano elfu, na upana wa elfu kumi; na ndani yake patakuwa patakatifu, palipo patakatifu sana.
4 Hiyo ni sehemu takatifu ya nchi; itakuwa ya makuhani, wahudumu wa patakatifu, wakaribiao kumhudumia Bwana; nayo itakuwa mahali kwa nyumba zao, na patakatifu kwa mahali patakatifu.
5 Tena urefu wa ishirini na tano elfu, na upana wa elfu kumi, ni sehemu ya Walawi, wahudumu wa nyumba, iwe milki yao wenyewe kwa vyumba ishirini.
6 Nanyi mtaiandika milki ya mji, upana wake elfu tano, na urefu wake ishirini na tano elfu, kandokando ya mahali palipotolewa, iwe sehemu takatifu; nayo itakuwa ya nyumba yote ya Israeli.
7 Na sehemu itakayokuwa ya mkuu itakuwa upande huu, na upande huu, wa toleo takatifu, na wa milki ya mji, kulikabili toleo takatifu, na kuikabili milki ya mji, upande wa magharibi kuelekea magharibi, na upande wa mashariki kuelekea mashariki; na kwa urefu wake sawasawa na sehemu mojawapo, toka mpaka wa magharibi hata mpaka wa mashariki.
8 Katika nchi hiyo itakuwa milki kwake katika Israeli; wala wakuu wangu hawatawaonea watu wangu tena kabisa; bali watawapa nyumba ya Israeli nchi hiyo, kwa kadiri ya makabila yao.
9 Bwana MUNGU asema hivi; Na iwatoshe ninyi, enyi wakuu wa Israeli; ondoeni dhuluma na unyang'anyi; fanyeni hukumu na haki; ondoeni kutoza kwa nguvu kwenu katika watu wangu, asema Bwana MUNGU.
10 Mtakuwa na mizani ya haki, na efa ya haki, na bathi ya haki.
11 Efa na bathi zitakuwa za kipimo kimoja; ili kwamba bathi ichukue sehemu ya kumi ya homeri, na efa sehemu ya kumi ya homeri; kipimo chake kitakuwa kwa kadiri ya cheo cha kawaida cha homeri.
12 Nayo shekeli itakuwa gera ishirini; shekeli tano zitakuwa shekeli tano, shekeli kumi zitakuwa kumi, na shekeli hamsini zitakuwa mane yenu.
13 Toleo mtakalotoa ni hili; sehemu ya sita ya efa katika homeri moja ya ngano, nanyi mtatoa sehemu ya sita ya efa katika homeri ya shayiri;
14 na sehemu ya mafuta iliyoamriwa, katika bathi ya mafuta, itakuwa sehemu ya kumi ya bathi katika kori moja, ambayo ni bathi kumi, yaani homeri; maana bathi kumi ni homeri moja;
15 na mwana-kondoo mmoja wa kundi katika mia mbili, katika malisho ya Israeli yenye maji; kwa sadaka ya unga, na kwa sadaka ya kuteketezwa, na kwa sadaka za amani, ili kuwafanyia upatanisho, asema Bwana MUNGU.
16 Watu wote wa nchi watatoa toleo hili kwa ajili ya mkuu katika Israeli.
17 Tena itakuwa kazi ya mkuu kutoa hizo sadaka za kuteketezwa, na sadaka za unga, na sadaka za vinywaji, katika sikukuu, na katika mwezi mpya, na katika sabato, katika sikukuu zote za nyumba ya Israeli zilizoamriwa; atatengeneza sadaka ya dhambi, na sadaka ya unga, na sadaka ya kuteketezwa, na sadaka za amani, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya nyumba ya Israeli.
18 Bwana MUNGU asema hivi; Mwezi wa kwanza, siku ya kwanza ya mwezi, utatwaa ng'ombe mchanga mume mkamilifu; nawe utapatakasa mahali patakatifu.
19 Na kuhani atatwaa baadhi ya damu ya sadaka ya dhambi, na kuitia juu ya miimo ya milango ya nyumba, na juu ya pembe nne za daraja ya madhabahu, na juu ya miimo ya lango la ua wa ndani.
20 Nawe utafanya vivyo hivyo katika mwezi wa saba, siku ya kwanza ya mwezi kwa ajili ya kila mtu akosaye, na kwa ajili ya mtu aliye mjinga, ndivyo mtakavyoifanyia nyumba upatanisho.
21 Mwezi wa kwanza, siku ya kumi na nne ya mwezi, mtakuwa na Pasaka, sikukuu ya siku saba; mkate usiotiwa chachu utaliwa.
22 Na siku hiyo mkuu atatengeneza ng'ombe kuwa sadaka ya dhambi, kwa ajili ya nafsi yake, na kwa ajili ya watu wote wa nchi.
23 Tena, katika zile siku saba za sikukuu atamtengenezea Bwana sadaka ya kuteketezwa, ng'ombe saba na kondoo waume saba wakamilifu, kila siku kwa muda wa siku saba, na beberu mmoja kila siku kuwa sadaka ya dhambi.
24 Naye atatengeneza sadaka ya unga, efa moja kwa ng'ombe, na efa moja kwa kondoo mume, na hini moja ya mafuta kwa efa moja;
25 katika mwezi wa saba, siku ya kumi na tano ya mwezi, katika sikukuu atafanya vivyo hivyo kwa muda wa siku saba; sadaka ya dhambi vivyo hivyo, na sadaka ya kuteketezwa vivyo hivyo, na sadaka ya unga vivyo hivyo, na mafuta vivyo hivyo.

Ezekieli 46


1 Bwana MUNGU asema hivi; Lango la ua wa ndani, lielekealo upande wa mashariki litafungwa siku sita za kazi; lakini siku ya sabato litafunguliwa, na siku ya mwezi mpya litafunguliwa.
2 Naye mkuu ataingia kwa njia ya ukumbi wa lango lile, upande wa nje, naye atasimama karibu na mwimo wa lango, nao makuhani wataitengeneza sadaka yake ya kuteketezwa, na sadaka zake za amani, naye ataabudu penye kizingiti cha lango; kisha atatoka; lakini lango lile halitafungwa hata wakati wa jioni.
3 Watu wa nchi nao wataabudu mbele ya mlango wa lile lango mbele za Bwana, siku za sabato, na siku za mwezi mpya.
4 Nayo sadaka ya kuteketezwa, ambayo mkuu atamtolea Bwana siku ya sabato, itakuwa wana-kondoo sita wakamilifu, na kondoo mume mkamilifu.
5 Na sadaka ya unga itakuwa efa moja kwa kondoo mume, na sadaka ya unga kwa wale wana-kondoo, kiasi awezacho kutoa, na hini moja ya mafuta kwa efa moja.
6 Na siku ya mwezi mpya itakuwa ni ng'ombe mume mchanga mkamilifu; na wana-kondoo sita, na kondoo mume; nao watakuwa wakamilifu.
7 Naye atatengeneza sadaka ya unga, efa moja kwa ng'ombe mume, na efa moja kwa kondoo mume, na kwa wale wana-kondoo, kwa kiasi awezacho kutoa, na hini moja ya mafuta kwa efa moja.
8 Naye mkuu atakapoingia, ataingia kwa njia ya ukumbi wa lango lile, naye atatoka kwa njia iyo hiyo.
9 Lakini watu wa nchi watakapokuja mbele za Bwana katika sikukuu zilizoamriwa, yeye aingiaye kwa njia ya lango la upande wa kaskazini ili kuabudu, atatoka kwa njia ya lango la upande wa kusini; na yeye aingiaye kwa njia ya lango la upande wa kusini, atatoka kwa njia ya lango la upande wa kaskazini; hatarudi kwa njia ya lango aliloingia kwalo, lakini atatoka kwa kwenda mbele moja kwa moja.
10 Naye mkuu atakapoingia, ataingia katikati yao, nao, watakapotoka, watatoka wote pamoja.
11 Na katika sikukuu hizo, na sikukuu nyingine zilizoamriwa, sadaka ya unga itakuwa efa moja kwa ng'ombe mmoja, na efa moja kwa kondoo mume mmoja, na kwa wale wana-kondoo kiasi awezacho kutoa, na hini moja ya mafuta kwa efa moja.
12 Naye mkuu atakapotengeneza sadaka atoayo kwa hiari yake mwenyewe, sadaka ya kuteketezwa, au sadaka za amani, ziwe sadaka amtoleazo Bwana kwa hiari yake mwenyewe, mtu mmoja atamfungulia lango lile lielekealo upande wa mashariki, naye ataitengeneza sadaka yake ya kuteketezwa, na sadaka zake za amani, kama afanyavyo siku ya sabato; kisha atatoka; na baada ya kutoka kwake mtu mmoja atalifunga lango.
13 Nawe utatengeneza mwana-kondoo wa mwaka wa kwanza, mkamilifu, kuwa sadaka ya kuteketezwa kwa Bwana kila siku; kila siku asubuhi utamtengeneza.
14 Nawe utatengeneza sadaka ya unga pamoja nayo kila siku asubuhi, sehemu ya sita ya efa moja, na sehemu ya tatu ya hini moja ya mafuta; kuchanganya na unga ule mzuri; sadaka ya unga kwa Bwana daima, kwa amri ya milele.
15 Hivyo ndivyo watakavyomtengeneza mwana-kondoo, na sadaka ya unga, na mafuta, kila siku asubuhi, kuwa sadaka ya kuteketezwa ya daima.
16 Bwana MUNGU asema hivi; Mkuu akimpa mwanawe awaye yote zawadi, ni urithi wake, itakuwa mali ya wanawe; ni milki yao kwa kurithiwa.
17 Bali akimpa mmoja wa watumishi wake baadhi ya urithi wake, itakuwa mali yake mpaka mwaka wa kuacha huru; ndipo itakapomrudia mkuu; lakini urithi wake, huo utakuwa wa wanawe.
18 Tena mkuu hatawaondolea watu urithi wao, hata kuwatoa kwa nguvu katika milki yao; atawapa wanawe urithi katika mali yake mwenyewe, watu wangu wasije wakatawanyika, kila mtu mbali na milki yake.
19 Ndipo akanileta kati ya maingilio, yaliyokuwa kando ya lango, mpaka vyumba vitakatifu vya makuhani, vilivyoelekea upande wa kaskazini; na tazama, palikuwa na mahali, upande wa nyuma ulioelekea magharibi.
20 Akaniambia, Hapa ndipo mahali pa makuhani, watakapoitokosa sadaka ya hatia, na sadaka ya dhambi, watakapoioka sadaka ya unga; kusudi wasizilete nje katika ua wa nje, na kuwatakasa watu.
21 Kisha akanileta mpaka ua wa nje, akanipitisha karibu na pembe nne za ua huo; na tazama, katika kila pembe ya ua huo palikuwa na kiwanja.
22 Katika pembe nne za ua huo palikuwa na viwanja vilivyoungana, urefu wake dhiraa arobaini, na upana wake thelathini; viwanja hivyo vinne vya pembeni vilikuwa vya kipimo kimoja.
23 Tena palikuwa na safu ndani yake pande zote, kuvizunguka vile viwanja vinne; tena palifanywa meko ya kutokosea, chini ya safu pande zote.
24 Ndipo akaniambia, Hizi ni nyumba za kutokosea, ambamo wahudumu wa nyumba watatokosa sadaka za watu.

Ezekieli 47


1 Baadaye akanileta tena mpaka lango la nyumba; na tazama, maji yalitoka chini ya kizingiti cha nyumba, kwa njia ya mashariki, maana upande wa mbele wa nyumba ulielekea upande wa mashariki; nayo maji yakashuka toka chini ya upande wa kuume wa nyumba, upande wa kusini wa madhabahu.
2 Ndipo akanileta nje kwa njia ya lango upande wa kaskazini, akanizungusha kwa njia ya nje mpaka lango la nje, kwa njia yake iliyoelekea mashariki; na tazama, maji yalitoka upande wa kuume.
3 Na alipotoka mtu yule, mwenye uzi wa kupimia mkononi mwake, kwenda masharikini, akapima dhiraa elfu, akanivusha maji yale; maji yakafika mpaka viweko vya miguu.
4 Kisha akapima dhiraa elfu, akanivusha maji yale, maji yakafika mpaka magoti. Kisha akapima dhiraa elfu, akanivusha, maji yakafika mpaka viuno.
5 Kisha akapima dhiraa elfu, yakawa mto nisioweza kuuvuka; maana maji yamezidi, maji ya kuogelea, mto usiovukika.
6 Akaniambia, Mwanadamu, je! Umeona haya? Kisha akanichukua akanirudisha mpaka ukingo wa mto.
7 Basi nikiisha kurudi, tazama, kando ya ukingo wa mto ilikuwapo miti mingi sana, upande huu na upande huu.
8 Ndipo akaniambia, Maji haya yanatoka kwenda pande za nchi ya mashariki, nayo yanashuka mpaka Araba, na kuingia katika bahari maji yatokezwayo yataingia baharini ,na maji yake yataponyeka.
9 Tena itakuwa, kila kiumbe hai kisongamanacho, kila mahali itakapofika mito hiyo, kitaishi; kutakuwapo wingi mkubwa wa samaki, kwa sababu maji haya yamefika huko maana maji yale yataponyeka, na kila kitu kitaishi po pote utakapofikilia mto huo.
10 Tena itakuwa, wavuvi watasimama karibu nao; toka Engedi mpaka En-eglaimu, patakuwa ni mahali pa kutandazia nyavu; samaki wao watakuwa namna zao mbalimbali, kama samaki wa bahari kubwa, wengi sana.
11 Bali mahali penye matope, na maziwa yake, hayataponywa; yataachwa yawe ya chumvi.
12 Na karibu na mto, juu ya ukingo wake, upande huu na upande huu, utamea kila mti wa chakula, ambao majani yake hayatanyauka, wala matunda yake hayatatindika kamwe; utatoa matunda mapya kila mwezi, kwa sababu maji yake yanatoka mahali patakatifu; na matunda yake yatakuwa ni chakula; na majani yake yatakuwa ni dawa.
13 Bwana MUNGU asema hivi; Huu ndio mpaka ambao mtaigawanya nchi iwe urithi sawasawa na kabila kumi na mbili za Israeli; kwa Yusufu, mafungu mawili.
14 Nanyi mtaimiliki, mtu huyu sawasawa na huyu; ambayo naliuinua mkono wangu kuwapa baba zenu; na nchi hii itawaangukia kuwa urithi.
15 Na huu ndio mpaka wa nchi; upande wa kaskazini, toka bahari kubwa, kwa njia ya Hethloni, mpaka maingilio ya Sedada;
16 Hamathi, na Berotha, na Sibraimu, ulio katikati ya mpaka wa Dameski na mpaka wa Hamathi; na Haser-hatikoni, ulio karibu na mpaka wa Haurani.
17 Nao mpaka toka baharini utakuwa Hasar-enoni, penye mpaka wa Dameski, na kaskazini kuelekea upande wa kaskazini ndio mpaka wa Hamathi. Huu ndio upande wa kaskazini.
18 Na upande wa mashariki, kati ya Haurani na Dameski, na Gileadi na nchi ya Israeli, utakuwa mto Yordani; mtapima toka mpaka wa upande wa kaskazini hata bahari ya mashariki. Huu ndio upande wa mashariki.
19 Na upande wa kusini, kuelekea kusini, utakuwa ni kutoka Tamari mpaka maji ya Meriba-Kadeshi, mpaka kijito cha Misri, mpaka bahari kubwa. Huu ndio upande wa kusini, kuelekea kusini.
20 Na upande wa magharibi, utakuwa ni bahari kubwa, kutoka mpaka wa kusini mpaka mahali penye kuelekea maingilio ya Hamathi. Huu ndio upande wa magharibi.
21 Basi ndivyo mtakavyojigawanyia nafsi zenu nchi hii, sawasawa na kabila za Israeli.
22 Tena itakuwa mtaigawanya kwa kura, kuwa urithi kwenu, na kwa wageni wakaao kwenu hali ya ugeni, watakaozaa watoto kati yenu, nao watakuwa kwenu, kama wazaliwa miongoni mwa wana Israeli; watakuwa na urithi pamoja nanyi kati ya kabila za Israeli.
23 Tena itakuwa, mgeni akaaye katika kabila iwayo yote, atapewa urithi katika kabila asema Bwana MUNGU.

Ezekieli 48


1 Basi, haya ndiyo majina ya kabila hizo; toka mwisho wa pande za kaskazini, karibu na njia ya Hethloni, hata maingilio ya Hamathi, hata Hasar-enoni, penye mpaka wa Dameski, yaani, upande wa kaskazini karibu na Hamathi, watakuwa na upande wa mashariki, na upande wa magharibi; Dani fungu moja.
2 Tena mpakani mwake Dani, toka upande wa mashariki hata upande wa magharibi; Asheri, fungu moja.
3 Na mpakani mwa Asheri, toka upande wa mashariki hata upande wa magharibi; Naftali, fungu moja.
4 Na mpakani mwa Naftali, toka upande wa mashariki hata upande wa magharibi; Manase, fungu moja.
5 Na mpakani mwa Manase, toka upande wa mashariki hata upande wa magharibi; Efraimu, fungu moja.
6 Na mpakani mwa Efraimu, toka upande wa mashariki hata upande wa magharibi; Reubeni, fungu moja.
7 Na mpakani mwa Reubeni, toka upande wa mashariki hata upande wa magharibi; Yuda, fungu moja.
8 Na mpakani mwa Yuda, toka upande wa mashariki hata upande wa magharibi, yatakuwapo matoleo mtakayotoa, upana wake mianzi ishirini na tano elfu, na urefu wake sawasawa na moja la mafungu hayo, toka upande wa mashariki hata upande wa magharibi; na mahali patakatifu ni katikati yake.
9 Matoleo hayo, mtakayomtolea Bwana, urefu wake ni mianzi ishirini na tano elfu, na upana wake elfu kumi.
10 Matoleo hayo matakatifu yatakuwa kwa watu hawa, kwa makuhani; upande wa kaskazini urefu wake ishirini na tano elfu, na upande wa magharibi upana wake elfu kumi, na upande wa mashariki upana wake elfu kumi, na upande wa kusini urefu wake ishirini na tano elfu; na mahali patakatifu pa Bwana patakuwa katikati yake.
11 Patakuwa kwa makuhani wa wana wa Sadoki, waliotakasika, walioulinda ulinzi wangu, wasioasi, wana wa Israeli walipoasi, kama Walawi walivyoasi.
12 Na matoleo hayo ya nchi yatolewayo, yatakuwa kwao kitu kitakatifu sana, karibu na mpaka wa Walawi.
13 Na kuukabili mpaka wa makuhani, Walawi watakuwa na fungu, urefu wake ishirini na tano elfu, na upana wake elfu kumi; urefu wote utakuwa ishirini na tano elfu, na upana wake elfu kumi.
14 Wala hawatauza sehemu yake, wala kuibadili, wala hawatawapa wengine malimbuko ya nchi; maana ni matakatifu kwa Bwana.
15 Na mianzi elfu tano iliyosalia katika upana, kuikabili hiyo ishirini na tano elfu, itatumiwa na watu wote, kwa huo mji, na kwa maskani, na kwa viunga, na huo mji utakuwa katikati yake.
16 Na vipimo vyake ni hivi; upande wa kaskazini elfu nne na mia tano, na upande wa kusini elfu nne na mia tano, na upande wa mashariki elfu nne na mia tano, na upande wa magharibi elfu nne na mia tano.
17 Nao mji utakuwa na malisho; upande wa kaskazini mia mbili na hamsini, na upande wa kusini mia mbili na hamsini, na upande wa mashariki mia mbili na hamsini, na upande wa magharibi mia mbili na hamsini.
18 Na mabaki ya urefu wake yaelekeayo matoleo matakatifu, upande wa mashariki yatakuwa elfu kumi, na upande wa magharibi elfu kumi; nayo yatakuwa sawasawa na matoleo matakatifu; na mazao yake yatakuwa ni chakula cha watu wafanyao kazi humo mjini.
19 Na hao wafanyao kazi mjini, wa kabila zote za Israeli, watailima nchi hiyo.
20 Matoleo yote yatakuwa ishirini na tano elfu, kwa ishirini na tano elfu; mtatoa matoleo matakatifu, nchi ya mraba, pamoja na milki ya mji.
21 Nayo mabaki yake yatakuwa ya huyo mkuu, upande huu na upande huu wa matoleo matakatifu, na milki ya mji, kuikabili hiyo ishirini na tano elfu ya matoleo, kuelekea mpaka wa mashariki; tena upande wa magharibi kuikabili hiyo ishirini na tano elfu, upande wa kuelekea mpaka wa magharibi; sawa na yale mafungu, hayo yatakuwa ya huyo mkuu; na matoleo matakatifu na mahali patakatifu pa nyumba patakuwa katikati yake.
22 Tena tokea milki ya Walawi, na tokea milki ya mji, kwa kuwa ni katikati ya nchi iliyo ya mkuu, katikati ya mpaka wa Yuda na mpaka wa Benyamini, itakuwa ya mkuu.
23 Na katika habari za kabila zilizosalia; toka upande wa mashariki hata upande wa magharibi; Benyamini, fungu moja.
24 Tena mpakani mwa Benyamini, toka upande wa mashariki hata upande wa magharibi; Simeoni, fungu moja.
25 Tena mpakani mwa Simeoni, toka upande wa mashariki hata upande wa magharibi; Isakari, fungu moja.
26 Na mpakani mwa Isakari, toka upande wa mashariki hata upande wa magharibi; Zabuloni, fungu moja.
27 Na mpakani mwa Zabuloni, toka upande wa mashariki hata upande wa magharibi; Gadi, fungu moja.
28 Na mpakani mwa Gadi, upande wa kusini kuelekea kusini, mpaka wake utakuwa toka Tamari, mpaka maji ya Meriba-Kadeshi, mpaka kijito cha Misri, mpaka bahari kubwa.
29 Hiyo ndiyo nchi mtakayozigawanyia kabila za Israeli, kuwa urithi wao, na hayo ndiyo mafungu yao, asema Bwana MUNGU.
30 Na matokeo ya mji ndiyo haya; upande wa kaskazini, mianzi elfu nne na mia tano, kwa kupima;
31 na malango ya mji yatatajwa kwa majina ya kabila za Israeli, malango matatu upande wa kaskazini; lango la Reubeni, moja; lango la Yuda, moja; na lango la Lawi, moja.
32 Na upande wa mashariki, elfu nne na mia tano, kwa kupima; na malango matatu; lango la Yusufu, moja; lango la Benyamini, moja; lango la Dani, moja.
33 Na upande wa kusini, elfu nne na mia tano kwa kupima; na malango matatu; lango la Simeoni, moja; lango la Isakari, moja; lango la Zabuloni, moja.
34 Na upande wa magharibi, elfu nne na mia tano; pamoja na malango yake matatu; lango la Gadi, moja; lango la Asheri, moja; na lango la Naftali, moja.
35 Kuuzunguka ni mianzi kumi na nane elfu; na jina la mji huo tangu siku hiyo litakuwa hili, Bwana yupo hapa.