Maombolezo

Sura: 1, 2, 3, 4, 5

Maombolezo 1


1 Jinsi mji huu ukaavyo ukiwa, Huo uliokuwa umejaa watu! Jinsi alivyokuwa kama mjane, Yeye aliyekuwa mkuu kati ya mataifa! Binti mfalme kati ya majimbo, Jinsi alivyoshikwa shokoa!
2 Hulia sana wakati wa usiku, Na machozi yake yapo mashavuni; Miongoni mwa wote waliompenda Hakuna hata mmoja amfarijiye; Rafiki zake wote wamemtenda hila, Wamekuwa adui zake.
3 Yuda amehamishwa kwa sababu ya kuonewa, Na kwa sababu ya utumwa mkuu; Anakaa kati ya makafiri, Haoni raha iwayo yote; Wote waliomfuata wamempata Katika dhiki yake.
4 Njia za Sayuni zaomboleza, Kwa kuwa hakuna ajaye kwa sikukuu; Malango yake yote yamekuwa ukiwa, Makuhani wake hupiga kite; Wanawali wake wanahuzunika; Na yeye mwenyewe huona uchungu.
5 Watesi wake wamekuwa kichwa, Adui zake hufanikiwa; Kwa kuwa Bwana amemtesa Kwa sababu ya wingi wa makosa yake; Watoto wake wadogo wamechukuliwa mateka Mbele yake huyo mtesi.
6 Naye huyo binti Sayuni Enzi yake yote imemwacha; Wakuu wake wamekuwa kama ayala Wasioona malisho; Nao wamekwenda zao hawana nguvu Mbele yake anayewafuatia.
7 Siku za mateso na misiba yake, Yerusalemu huyakumbuka matamaniko yake yote Yaliyokuwa tangu siku za kale; Hapo watu wake walipoanguka mikononi mwa mtesi, Wala hakuna hata mmoja wa kumsaidia; Hao watesi wake walimwona, Wakafanya sabato zake kuwa mzaha.
8 Yerusalemu amefanya dhambi sana; Kwa hiyo amekuwa kama kitu kichafu; Wote waliomheshimu wanamdharau, Kwa sababu wameuona uchi wake; Naam, yeye anaugua, Na kujigeuza aende nyuma.
9 Uchafu wake ulikuwa katika marinda yake; Hakukumbuka mwisho wake; Kwa hiyo ameshuka kwa ajabu; Yeye hana mtu wa kumfariji; Tazama, Bwana, teso langu; Maana huyo adui amejitukuza.
10 Huyo mtesi amenyosha mkono wake Juu ya matamaniko yake yote; Maana ameona ya kuwa makafiri wameingia Ndani ya patakatifu pake; Ambao kwa habari zao wewe uliamuru Wasiingie katika kusanyiko lako.
11 Watu wake wote hupiga kite, Wanatafuta chakula; Wameyatoa matamaniko yao wapate chakula Cha kuihuisha nafsi; Ee Bwana, tazama, uangalie; Kwa maana mimi nimekuwa mnyonge.
12 Je! Si kitu kwenu, enyi nyote mpitao njia, Angalieni, mtazame Kama kuna majonzi yo yote mfano wa majonzi yangu, Niliyotendwa mimi, Ambayo Bwana amenihuzunisha kwa hayo Siku ya hasira yake iwakayo.
13 Toka juu amepeleka moto mifupani mwangu, Nao umeishinda; Ametandika wavu aninase miguu, Amenirudisha nyuma; Amenifanya kuwa mtu wa pekee, Na mgonjwa mchana kutwa.
14 Kongwa la makosa yangu limefungwa na mkono wake; Hayo yameshikamana; Yamepanda juu shingoni mwangu; Amezikomesha nguvu zangu;
15 Bwana amenitia mikononi mwao, Ambao siwezi kupingamana nao. Bwana amewafanya mashujaa wangu wote Kuwa si kitu kati yangu; Ameita mkutano mkuu kinyume changu Ili kuwaponda vijana wangu; Bwana amemkanyaga kama shinikizoni Huyo bikira binti Yuda.
16 Mimi ninayalilia mambo hayo; Jicho langu, jicho langu linachuruzika maji; Kwa kuwa mfariji yu mbali nami, Ambaye ilimpasa kunihuisha nafsi; Watoto wangu wameachwa peke yao, Kwa sababu huyo adui ameshinda.
17 Sayuni huinyosha mikono yake; Hakuna hata mmoja wa kumfariji; Bwana ametoa amri juu ya Yakobo, Kwamba wamzungukao wawe watesi wake; Yerusalemu amekuwa kati yao Kama kitu kichafu.
18 Bwana ndiye mwenye haki; Maana nimeiasi amri yake; Sikieni, nawasihi, enyi watu wote, Mkayatazame majonzi yangu; Wasichana wangu na wavulana wangu Wamechukuliwa mateka.
19 Naliwaita hao walionipenda Lakini walinidanganya; Makuhani wangu na wazee wangu Walifariki mjini; Hapo walipokuwa wakitafuta chakula ili kuzihuisha nafsi zao.
20 Angalia, Ee Bwana; maana mimi ni katika dhiki; Mtima wangu umetaabika; Moyo wangu umegeuka ndani yangu; Maana nimeasi vibaya sana; Huko nje upanga hufisha watu; Nyumbani mna kama mauti.
21 Wamesikia kwamba napiga kite; Hakuna hata mmoja wa kunifariji; Adui zangu wote wamesikia habari ya mashaka yaliyonipata; Hufurahi kwa kuwa umeyafanya hayo; Utaileta siku ile uliyoitangaza, Nao watakuwa kama mimi.
22 Huo uovu wao wote Na uje mbele zako wewe; Ukawatende wao kama ulivyonitenda mimi Kwa dhambi zangu zote; Kwa maana mauguzi yangu ni mengi sana, Na moyo wangu umezimia.

Maombolezo 2


1 Jinsi Bwana alivyomfunika binti Sayuni Kwa wingu katika hasira yake! Ameutupa toka mbinguni hata nchi Huo uzuri wa Israeli; Wala hakukikumbuka kiti cha miguu yake Katika siku ya hasira yake.
2 Bwana ameyameza makao yote ya Yakobo, Wala hakuona huruma; Ameziangusha ngome za binti Yuda Katika ghadhabu yake; Amezibomoa hata nchi Ameunajisi ufalme na wakuu wake.
3 Ameikata pembe yote ya Israeli Katika hasira yake kali; Ameurudisha nyuma mkono wake wa kuume Mbele ya hao adui, Naye amemteketeza Yakobo kama moto uwakao, Ulao pande zote.
4 Ameupinda upinde wake kama adui, Amesimama na mkono wake wa kuume kama mtesi; Naye amewaua hao wote Waliopendeza macho; Katika hema ya binti Sayuni Amemimina kani yake kama moto.
5 Bwana amekuwa mfano wa adui, Amemmeza Israeli; Ameyameza majumba yake yote, Ameziharibu ngome zake; Tena amemzidishia binti Yuda Matanga na maombolezo.
6 Naye ameondoa maskani yake kwa nguvu, Kana kwamba ni ya bustani tu; Ameziharibu sikukuu zake; Bwana amezisahauzisha katika Sayuni Sikukuu za makini na sabato; Naye amewadharau mfalme na kuhani Katika uchungu wa hasira yake.
7 Bwana ameitupilia mbali madhabahu yake, Amepachukia patakatifu pake; Amezitia katika mikono ya hao adui Kuta za majumba yake; Wamepiga kelele ndani ya nyumba ya Bwana Kama katika siku ya kusanyiko la makini.
8 Bwana amekusudia kuuharibu Ukuta wa binti Sayuni; Ameinyosha hiyo kamba, Hakuuzuia mkono wake usiangamize; Bali amefanya boma na ukuta kuomboleza; Zote pamoja hudhoofika.
9 Malango yake yamezama katika nchi; Ameyaharibu makomeo yake na kuyavunja; Mfalme wake na wakuu wake wanakaa Kati ya mataifa wasio na sheria; Naam, manabii wake hawapati maono Yatokayo kwa Bwana.
10 Wazee wa binti Sayuni huketi chini, Hunyamaza kimya; Wametupa mavumbi juu ya vichwa vyao, Wamejivika viunoni nguo za magunia; Wanawali wa Yerusalemu huinama vichwa vyao Kuielekea nchi.
11 Macho yangu yamechoka kwa machozi, Mtima wangu umetaabika; Ini langu linamiminwa juu ya nchi Kwa uharibifu wa binti ya watu wangu; Kwa sababu watoto wachanga na wanyonyao, Huzimia katika mitaa ya mji.
12 Wao huwauliza mama zao, Zi wapi nafaka na divai? Hapo wazimiapo kama waliojeruhiwa Katika mitaa ya mji, Hapo walipomiminika nafsi zao Vifuani mwa mama zao.
13 Nikushuhudie nini? Nikufananishe na nini, Ee Binti Yerusalemu? Nikusawazishe na nini, nipate kukufariji, Ee bikira binti Sayuni? Kwa maana uvunjifu wako ni mkuu kama bahari, Ni nani awezaye kukuponya?
14 Manabii wako wameona maono kwa ajili yako Ya ubatili na upumbavu Wala hawakufunua uovu wako, Wapate kurudisha kufungwa kwako; Bali wameona mabashiri ya ubatili kwa ajili yako Na sababu za kuhamishwa.
15 Hao watu wote wapitao Hukupigia makofi; Humzomea binti Yerusalemu, Na kutikisa vichwa vyao; Je! Mji huu ndio ulioitwa, Ukamilifu wa uzuri, Furaha ya dunia yote?
16 Juu yako adui zako wote Wamepanua vinywa vyao; Huzomea, husaga meno yao, Husema, Tumemmeza; Hakika siku hii ndiyo tuliyoitazamia; Tumeipata, tumeiona.
17 Bwana ameyatenda aliyoyakusudia; amelitimiza neno lake, Aliloliamuru siku za kale; Ameangusha hata chini, Wala hakuona huruma; Naye amemfurahisha adui juu yako, Ameitukuza pembe ya watesi wako.
18 Mioyo yao ilimlilia Bwana; Ee ukuta wa binti Sayuni! Machozi na yachuruzike kama mto Mchana na usiku; Usijipatie kupumzika; Mboni ya jicho lako isikome.
19 Inuka, ulalamike usiku, Mwanzo wa makesha yake; Mimina moyo wako kama maji usoni pa Bwana; Umwinulie mikono yako; Kwa uhai wa watoto wako wachanga wazimiao kwa njaa, Mwanzo wa kila njia kuu.
20 Tazama, Bwana, uangalie, Ni nani uliyemtenda hayo! Je! Wanawake wale mazao yao, Watoto waliowabeba? Je! Kuhani na nabii wauawe Katika patakatifu pa Bwana?
21 Kijana na mzee hulala chini Katika njia kuu; Wasichana wangu na wavulana wangu Wameanguka kwa upanga; Umewaua katika siku ya hasira yako; Umeua, wala hukuona huruma.
22 Umeziita kama katika siku ya mkutano wa makini; Hofu zangu zije pande zote; Wala hapana hata mmoja aliyepona wala kusalia Katika siku ya hasira ya Bwana; Hao niliowabeba na kuwalea Huyo adui yangu amewakomesha.

Maombolezo 3


1 Mimi ni mtu aliyeona mateso Kwa fimbo ya ghadhabu yake.
2 Ameniongoza na kuniendesha katika giza Wala si katika nuru.
3 Hakika juu yangu augeuza mkono wake Mara kwa mara mchana wote.
4 Amechakaza nyama yangu na ngozi yangu; Ameivunja mifupa yangu.
5 Amejenga boma juu yangu, Na kunizungusha uchungu na uchovu.
6 Amenikalisha penye giza, Kama watu waliokufa zamani.
7 Amenizinga pande zote hata siwezi kutoka; Ameufanya mnyororo wangu mzito.
8 Naam, nikilia na kuomba msaada, Huyapinga maombi yangu.
9 Ameziziba njia zangu kwa mawe yaliyochongwa; Ameyapotosha mapito yangu.
10 Alivyo kwangu ni kama dubu aoteaye, Kama simba aliye mafichoni.
11 Amezigeuza njia zangu, na kunirarua-rarua; Amenifanya ukiwa.
12 Ameupinda upinde wake, Na kunifanya niwe shabaha kwa mshale.
13 Amenichoma viuno Kwa mishale ya podo lake.
14 Nimekuwa dhihaka kwa watu wangu wote; Wimbo wao mchana kutwa.
15 Amenijaza uchungu, Amenikinaisha kwa pakanga.
16 Amenivunja meno kwa changarawe; Amenifunika majivu.
17 Umeniweka nafsi yangu mbali na amani; Nikasahau kufanikiwa.
18 Nikasema, Nguvu zangu zimepotea, Na tumaini langu kwa Bwana.
19 Kumbuka mateso yangu, na msiba wangu, Pakanga na nyongo.
20 Nafsi yangu ikali ikiyakumbuka hayo, Nayo imeinama ndani yangu.
21 Najikumbusha neno hili, Kwa hiyo nina matumaini.
22 Ni huruma za Bwana kwamba hatuangamii, Kwa kuwa rehema zake hazikomi.
23 Ni mpya kila siku asubuhi; Uaminifu wako ni mkuu.
24 Bwana ndiye fungu langu, husema nafsi yangu, Kwa hiyo nitamtumaini yeye.
25 Bwana ni mwema kwa hao wamngojeao, Kwa hiyo nafsi imtafutayo.
26 Ni vema mtu autarajie wokovu wa Bwana Na kumngojea kwa utulivu.
27 Ni vema mwanadamu aichukue nira Wakati wa ujana wake.
28 Na akae peke yake na kunyamaza kimya; Kwa sababu Bwana ameweka hayo juu yake.
29 Na atie kinywa chake mavumbini; Ikiwa yamkini liko tumaini.
30 Na amwelekezee yule ampigaye shavu lake; Ashibishwe mashutumu.
31 Kwa kuwa Bwana hatamtupa mtu Hata milele.
32 Maana ajapomhuzunisha atamrehemu, Kwa kadiri ya wingi wa huruma zake.
33 Maana moyo wake hapendi kuwatesa wanadamu. Wala kuwahuzunisha.
34 Kuwaseta chini kwa miguu Wafungwa wote wa duniani,
35 Kuipotosha hukumu ya mtu Mbele zake Aliye juu,
36 Na kumnyima mtu haki yake, Hayo Bwana hayaridhii kabisa.
37 Ni nani asemaye neno nalo likafanyika, Ikiwa Bwana hakuliagiza?
38 Je! Katika kinywa chake Aliye juu Hayatoki maovu na mema?
39 Mbona anung'unika mwanadamu aliye hai Mtu akiadhibiwa kwa dhambi zake?
40 Na tuchunguze njia zetu na kuzijaribu, Na kumrudia Bwana tena.
41 Na tumwinulie Mungu aliye mbinguni Mioyo yetu na mikono.
42 Sisi tumekosa na kuasi; Wewe hukusamehe.
43 Umetufunika kwa hasira na kutufuatia; Umeua, wala hukuona huruma.
44 Umejifunika nafsi yako kwa wingu, Maombi yetu yasipite.
45 Umetufanya kuwa takataka, na vifusi Katikati ya mataifa.
46 Juu yetu adui zetu wote Wametupanulia vinywa vyao.
47 Hofu imetujilia na shimo, Ukiwa na uharibifu.
48 Jicho langu lachuruzika mito ya maji Kwa ajili ya uvunjifu wa binti ya watu wangu.
49 Jicho langu latoka machozi lisikome, Wala haliachi;
50 Hata Bwana atakapoangalia Na kutazama toka mbinguni.
51 Jicho langu lanitia huzuni nafsini mwangu, Kwa sababu ya binti zote za mji wangu.
52 Walio adui zangu bila sababu Wameniwinda sana kama ndege;
53 Wameukatilia mbali uhai wangu gerezani, Na kutupa jiwe juu yangu.
54 Maji mengi yalipita juu ya kichwa changu, Nikasema, Nimekatiliwa mbali.
55 Naliliitia jina lako, Bwana, kutoka lile shimo Liendalo chini kabisa.
56 Ukaisikia sauti yangu; usifiche sikio lako Ili usisikie pumzi yangu, kwa kilio changu.
57 Ulinikaribia siku ile nilipokulilia; Ukasema, Usiogope.
58 Ee Bwana umenitetea mateto ya nafsi yangu; Umeukomboa uhai wangu.
59 Umekuona kudhulumiwa kwangu, Ee Bwana; Unihukumie neno langu.
60 Umekiona kisasi chao chote, Na mashauri yao yote juu yangu.
61 Ee Bwana, umeyasikia matukano yao, Na mashauri yao yote juu yangu;
62 Midomo yao walioinuka juu yangu Na maazimio yao juu yangu mchana kutwa.
63 Uangalie kuketi kwao, na kuinuka kwao; Wimbo wao ndio mimi.
64 Utawalipa malipo, Ee Bwana, Sawasawa na kazi ya mikono yao.
65 Utawapa ushupavu wa moyo; Laana yako juu yao.
66 Utawafuatia kwa hasira, na kuwaangamiza Wasiwe tena chini ya mbingu za Bwana.

Maombolezo 4


1 Jinsi dhahabu ilivyoacha kung'aa, Na dhahabu iliyo safi ilivyobadilika! Mawe ya patakatifu yametupwa Mwanzo wa kila njia.
2 Wana wa Sayuni wenye thamani, Walinganao na dhahabu safi, Jinsi wanavyodhaniwa kuwa vyombo vya udongo, Kazi ya mikono ya mfinyanzi!
3 Hata mbwa-mwitu hutoa matiti, Huwanyonyesha watoto wao; Binti ya watu wangu amekuwa mkali, Mfano wa mbuni jangwani.
4 Ulimi wa mtoto anyonyaye Wagandamana na kaakaa lake kwa kiu; Watoto wachanga waomba chakula, Wala hakuna hata mmoja awamegeaye.
5 Wale waliokula vitu vya anasa Wameachwa peke yao njiani; Wale waliokuzwa kuvaa nguo nyekundu Wakumbatia jaa.
6 Maana uovu wa binti ya watu wangu ni mkubwa Kuliko dhambi ya Sodoma, Uliopinduliwa kama katika dakika moja, Wala mikono haikuwekwa juu yake.
7 Wakuu wake walikuwa safi kuliko theluji, Walikuwa weupe kuliko maziwa; Miili yao, walikuwa wekundu kuliko marijani, Na umbo lao kama yakuti samawi.
8 Nyuso zao ni nyeusi kuliko makaa; Hawajulikani katika njia kuu; Ngozi yao yagandamana na mifupa yao Imekauka, imekuwa kama mti.
9 Heri wale waliouawa kwa upanga Kuliko wao waliouawa kwa njaa; Maana hao husinyaa, wakichomwa Kwa kukosa matunda ya mashamba.
10 Mikono ya wanawake wenye huruma Imewatokosa watoto wao wenyewe; Walikuwa ndio chakula chao Katika uharibifu wa binti ya watu wangu.
11 Bwana ameitimiza kani yake, Ameimimina hasira yake kali; Naye amewasha moto katika Sayuni Ulioiteketeza misingi yake.
12 Wafalme wa dunia hawakusadiki, Wala wote wakaao duniani, Ya kwamba mtesi na adui wangeingia Katika malango ya Yerusalemu.
13 Ni kwa sababu ya dhambi za manabii wake Na maovu ya makuhani wake, Walioimwaga damu ya wenye haki Katikati yake.
14 Hutanga-tanga njiani kama vipofu, Wametiwa unajisi kwa damu; Hata ikawa watu wasiweze Kuyagusa mavazi yao.
15 Watu waliwapigia kelele, Ondokeni, Uchafu, Ondokeni, ondokeni, msiguse; Walipokimbia na kutanga-tanga, watu walisema kati ya mataifa, Hawatakaa hapa tena.
16 Hasira ya Bwana imewatenga, Yeye hatawaangalia tena; Hawakujali nafsi za wale makuhani, Hawakuwaheshimu wazee wao.
17 Macho yetu yamechoka Kwa kuutazamia bure msaada wetu; Katika kungoja kwetu tumengojea taifa Lisiloweza kutuokoa.
18 Wanatuvizia hatua zetu, Hata hatuwezi kwenda katika njia zetu; Mwisho wetu umekaribia, siku zetu zimetimia; Maana mwisho wetu umefika.
19 Waliotufuatia ni wepesi Kuliko tai za mbinguni; Hao walitufuatia milimani, Nao walituotea jangwani.
20 Pumzi ya mianzi ya pua zetu, masihi wa BWANA, Alikamatwa katika marima yao;Ambaye kwa habari zake tulisema,Chini ya kivuli chake tukakaa kati ya mataifa.
21 Furahi, ushangilie, Ee binti Edomu, Ukaaye katika nchi ya Usi; Hata kwako kikombe kitapita, Utalewa, na kujifanya uchi.
22 Uovu wako umetimia, Ee binti Sayuni; Hatakuhamisha tena; Atapatiliza uovu wako, Ee binti Edomu; Atazivumbua dhambi zako.

Maombolezo 5


1 Ee Bwana, kumbuka yaliyotupata; Utazame na kuiona aibu yetu.
2 Urithi wetu umegeuka kuwa mali ya wageni; Na nyumba zetu kuwa mali ya makafiri.
3 Tumekuwa yatima waliofiwa na baba; Mama zetu wamekuwa kama wajane.
4 Tumekunywa maji yetu kwa fedha; Kuni zetu twauziwa.
5 Watufuatiao wa juu ya shingo zetu; Tumechoka tusipate raha yo yote.
6 Tumewapa hao Wamisri mkono; Na Waashuri nao, ili tushibe chakula.
7 Baba zetu walitenda dhambi hata hawako; Na sisi tumeyachukua maovu yao.
8 Watumwa wanatutawala; Hakuna mtu wa kutuokoa na mikono yao.
9 Twapata chakula kwa kujihatarisha nafsi zetu; Kwa sababu ya upanga wa nyikani.
10 Ngozi yetu ni nyeusi kama tanuu; Kwa sababu ya hari ya njaa ituteketezayo.
11 Huwatia jeuri wanawake katika Sayuni; Na mabikira katika miji ya Yuda.
12 Wakuu hutungikwa kwa mikono yao; Nyuso za wazee hazipewi heshima.
13 Vijana huyachukua mawe ya kusagia; Na watoto hujikwaa chini ya kuni.
14 Wazee wameacha kwenda langoni; Na vijana kwenda ngomani.
15 Furaha ya mioyo yetu imekoma; Machezo yetu yamegeuka maombolezo.
16 Taji ya kichwa chetu imeanguka; Ole wetu! Kwa kuwa tumetenda dhambi.
17 Kwa sababu hiyo mioyo yetu imezimia; Kwa ajili ya hayo macho yetu hayaoni vema.
18 Kwa ajili ya mlima Sayuni ulio ukiwa, Mbweha hutembea juu yake.
19 Wewe, Bwana, unadumu milele; Kiti chako cha enzi ni tangu kizazi hata kizazi.
20 Mbona watusahau sikuzote; Na kutuacha muda huu mwingi?
21 Ee Bwana, utugeuze kwako, nasi tutageuka; Zifanye mpya siku zetu kama siku za kale.
22 Isipokuwa wewe umetukataa kabisa; Nawe una hasira nyingi sana juu yetu.