Isaya

Sura: 1, 2, 3, 4, 5, 6, 7, 8, 9, 10, 11, 12, 13, 14, 15, 16, 17, 18, 19, 20, 21, 22, 23, 24, 25, 26, 27, 28, 29, 30, 31, 32, 33, 34, 35, 36, 37, 38, 39, 40, 41, 42, 43, 44, 45, 46, 47, 48, 49, 50, 51, 52, 53, 54, 55, 56, 57, 58, 59, 60, 61, 62, 63, 64, 65, 66

Isaya 1


1 Haya ni maono ya Isaya, mwana wa Amozi, aliyoyaona katika habari za Yuda na Yerusalemu, siku za Uzia na Yothamu na Ahazi na Hezekia, wafalme wa Yuda.
2 Sikieni, enyi mbingu, tega sikio, Ee nchi, kwa maana Bwana amenena; Nimewalisha watoto na kuwalea, nao wameniasi.
3 Ng'ombe amjua bwana wake, Na punda ajua kibanda cha bwana wake; Bali Israeli hajui, watu wangu hawafikiri.
4 Ole wake, taifa lenye dhambi, watu wanaochukua mzigo wa uovu, wazao wa watenda mabaya, watoto wanaoharibu; wamemwacha Bwana, wamemdharau yeye aliye Mtakatifu wa Israeli, wamefarakana naye na kurudi nyuma.
5 Mbona mnataka kupigwa hata sasa, hata mkazidi kuasi? Kichwa chote ni kigonjwa, moyo wote umezimia.
6 Tangu wayo wa mguu hata kichwani hamna uzima ndani yake; bali jeraha na machubuko na vidonda vitokavyo usaha; havikufungwa, havikuzongwa-zongwa, wala havikulainishwa kwa mafuta.
7 Nchi yenu ni ukiwa; miji yenu imeteketezwa kwa moto; nchi yenu, wageni wameila mbele ya macho yenu; nayo ni ukiwa, kana kwamba imeangamizwa na wageni.
8 Na binti Sayuni ameachwa kama kibanda katika shamba la mizabibu, kama kipenu katika shamba la matango, kama mji uliohusuriwa.
9 Kama Bwana wa majeshi asingalituachia mabaki machache sana, tungalikuwa kama Sodoma, tungalifanana na Gomora.
10 Lisikieni neno la Bwana, enyi waamuzi wa Sodoma; tegeni masikio msikie sheria ya Mungu wetu, enyi watu wa Gomora.
11 Huu wingi wa sadaka zenu mnazonitolea una faida gani? Asema Bwana. Nimejaa mafuta ya kafara za kondoo waume, na mafuta ya wanyama walionona; nami siifurahii damu ya ng'ombe wala ya wana-kondoo wala ya mbuzi waume.
12 Mjapo ili kuonekana mbele zangu, ni nani aliyetaka neno hili mikononi mwenu, kuzikanyaga nyua zangu?
13 Msilete tena matoleo ya ubatili; uvumba ni chukizo kwangu; mwezi mpya na sabato, kuita makutano; siyawezi maovu hayo na makutano ya ibada.
14 Sikukuu zenu za mwezi mpya na karamu zenu zilizoamriwa, nafsi yangu yazichukia; mambo hayo yanilemea; nimechoka kuyachukua.
15 Nanyi mkunjuapo mikono yenu, nitaficha macho yangu nisiwaone; naam, mwombapo maombi mengi, sitasikia; mikono yenu imejaa damu.
16 Jiosheni, jitakaseni; ondoeni uovu wa matendo yenu usiwe mbele za macho yangu; acheni kutenda mabaya;
17 jifunzeni kutenda mema; takeni hukumu na haki; wasaidieni walioonewa; mpatieni yatima haki yake; mteteeni mjane.
18 Haya, njoni, tusemezane, asema Bwana. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu.
19 Kama mkikubali na kutii mtakula mema ya nchi;
20 bali kama mkikataa na kuasi mtaangamizwa kwa upanga; maana kinywa cha Bwana kimenena haya.
21 Mji huu uliokuwa mwaminifu umekuwaje kahaba! Yeye aliyejaa hukumu ya haki; haki ilikaa ndani yake, bali sasa wauaji!
22 Fedha yako imekuwa takataka, divai yako imechanganywa na maji.
23 Wakuu wako ni waasi, na rafiki za wevi; kila mtu hupenda rushwa, hufuata malipo; hawampatii yatima haki yake, wala maneno ya mjane hayawawasilii.
24 Kwa hiyo, asema Bwana, Bwana wa majeshi, Mwenye enzi, wa Israeli, Nitapata faraja kwa hao wanipingao, nitatwaa kisasi kwa adui zangu;
25 nami nitakuelekezea wewe mkono wangu, na kukutakasa takataka zako kabisa, na kukuondolea bati lako lote;
26 nami nitarejeza upya waamuzi wako kama walivyokuwa hapo kwanza, na washauri wako kama hapo mwanzo; baada ya hayo utaitwa, Mji wa haki, mji mwaminifu.
27 Sayuni itakombolewa kwa hukumu, na waongofu wake kwa haki.
28 Lakini kuharibika kwao wakosao nao wenye dhambi kutatokea wakati mmoja, nao wamwachao Bwana watateketezwa.
29 Kwa maana watatahayarika kwa sababu ya mialoni mliyoitamani, nanyi mtaaibishwa kwa sababu ya bustani mlizozichagua.
30 Maana mtakuwa kama mwaloni ambao majani yake yakauka, na kama bustani isiyo na maji.
31 Na mtu hodari atakuwa kama makumbi, na kazi yake kama cheche ya moto; nao watawaka pamoja, wala hapana atakayewazima.

Isaya 2


1 Hili ni neno aliloliona Isaya mwana wa Amozi katika habari za Yuda na Yerusalemu.
2 Na itakuwa katika siku za mwisho, mlima wa nyumba ya Bwana utawekwa imara juu ya milima, nao utainuliwa juu ya vilima; na mataifa yote watauendea makundi makundi.
3 Na mataifa mengi watakwenda na kusema, Njoni, twende juu mlimani kwa Bwana, nyumbani kwa Mungu wa Yakobo, naye atatufundisha njia zake, nasi tutakwenda katika mapito yake maana katika Sayuni itatoka sheria, na neno la Bwana katika Yerusalemu.
4 Naye atafanya hukumu katika mataifa mengi, atawakemea watu wa kabila nyingi; nao watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe miundu; taifa halitainua upanga juu ya taifa lingine, wala hawatajifunza vita tena kamwe.
5 Enyi wa nyumba ya Israeli, njoni, twende katika nuru ya Bwana.
6 Maana wewe umewaacha watu wako, nyumba ya Israeli, kwa sababu wamejaa kawaida za mashariki, nao ni wapiga ramli kama Wafilisti, na wanapana mikono na wana wa wageni.
7 Tena nchi yao imejaa fedha na dhahabu, wala hapana mwisho wa hazina zao; tena nchi yao imejaa farasi, wala hapana mwisho wa magari yao.
8 Tena nchi yao imejaa sanamu; huabudu kazi ya mikono yao, vitu vilivyofanywa kwa vidole vyao wenyewe.
9 Mtu mnyonge huinama, na mtu mkubwa hujidhili; kwa hiyo usiwasamehe.
10 Ingia ndani ya jabali; ukajifiche mavumbini mbele za utisho wa Bwana, mbele za utukufu wa enzi yake.
11 Macho ya mwanadamu yaliyoinuka yatashushwa chini, na kiburi cha mwanadamu kitainamishwa, naye Bwana, yeye peke yake, atatukuzwa siku hiyo.
12 Kwa maana kutakuwa siku ya Bwana wa majeshi juu ya watu wote wenye kiburi na majivuno, na juu ya yote yaliyoinuka; nayo yatashushwa chini.
13 Na juu ya mierezi yote ya Lebanoni iliyo mirefu na kuinuka, na juu ya mialoni yote ya Bashani;
14 na juu ya milima mirefu yote, na juu ya vilima vyote vilivyoinuka;
15 na juu ya kila mnara mrefu, na juu ya kila ukuta ulio na boma;
16 na juu ya merikebu zote za Tarshishi, na juu ya kila taswira ipendezayo.
17 Na majivuno ya mwanadamu yatainamishwa, na kiburi cha watu kitashushwa; naye Bwana, yeye peke yake, atatukuzwa siku hiyo.
18 Nazo sanamu zitatoweka kabisa.
19 Na watu wataingia ndani ya pango za majabali, na ndani ya mashimo ya nchi, mbele za utisho wa Bwana na utukufu wa enzi yake, atakapoondoka ili aitetemeshe mno dunia.
20 Siku hiyo kila mtu atazitupilia mbali sanamu zake za fedha, na sanamu zake za dhahabu, walizojifanyia ili kuziabudu, kwa fuko na popo;
21 ili aingie ndani ya pango za majabali, na ndani ya tundu za miamba iliyopasuka, mbele za utisho wa Bwana na utukufu wa enzi yake, atakapoondoka ili aitetemeshe mno dunia.
22 Mwacheni mwanadamu ambaye pumzi yake i katika mianzi ya pua yake; kwa maana hudhaniwaje kuwa ni kitu?

Isaya 3


1 Kwa maana, tazama, Bwana, Bwana wa majeshi, awaondolea Yerusalemu na Yuda egemeo na tegemeo; tegemeo lote la chakula na tegemeo lote la maji;
2 mtu hodari na mtu wa vita; mwamuzi na nabii; mpiga ramli na mzee;
3 jemadari aliye juu ya watu hamsini, na mtu mstahifu, na mshauri, na fundi aliye mstadi, na mganga ajuaye uganga sana.
4 Nami nitawapa watoto kuwamiliki, na watoto wachanga kuwatawala.
5 Nao watu wataonewa, kila mtu na mwenziwe, na kila mtu na jirani yake; mtoto atajivuna mbele ya mzee, na mtu mnyonge mbele ya mtu mwenye heshima.
6 Mtu atakapomshika ndugu yake ndani ya nyumba ya baba yake, akisema, Wewe una nguo, ututawale wewe; na mahali hapa palipobomoka pawe chini ya mkono wako;
7 basi, siku ile atainua sauti yake, akisema, Mimi sitakuwa mponya watu; kwa maana ndani ya nyumba yangu hamna chakula wala mavazi; wala hamtanifanya kuwa mtawala juu ya watu hawa.
8 Kwa maana Yerusalemu umebomolewa na Yuda wameanguka, kwa sababu ulimi wao na matendo yao ni kinyume cha Bwana, hata wayachukize macho ya utukufu wake.
9 Kuonekana kwa nyuso zao kwashuhudia juu yao, wafunua dhambi yao kama Sodoma, hawaifichi. Ole wa nafsi zao, kwa maana wamejilipa nafsi zao uovu.
10 Waambieni wenye haki ya kuwa watakuwa heri, kwa maana watakula matunda ya matendo yao
11 Ole wake mtu mbaya; shari itakuwa kwake, kwa maana atapewa ijara ya mikono yake.
12 Katika habari za watu wangu, watoto ndio wanaowaonea, na wanawake ndio wanaowatawala. Enyi watu wangu, wakuongozao wakukosesha, waiharibu njia ya mapito yako.
13 Bwana asimama ili atete, asimama ili awahukumu watu.
14 Bwana ataingia katika kuwahukumu wazee wa watu wake na wakuu wao; Ninyi ndinyi mliokula shamba la mizabibu; vitu mlivyowateka maskini vi ndani ya nyumba zenu.
15 Ni nini maana yake, ninyi kuwaonea watu wangu, na kuseta nyuso za maskini? Asema Bwana, Bwana wa majeshi.
16 Bwana akasema tena, Kwa sababu binti za Sayuni wana kiburi, na kuenenda na shingo zilizonyoshwa, na macho ya kutamani, wakienenda kwa hatua za madaha, na kuliza njuga kwa miguu yao;
17 Basi, kwa hiyo, Bwana atawapiga binti za Sayuni kwa pele za utosini, na Bwana ataifunua aibu yao.
18 Siku hiyo Bwana atawaondolea uzuri wa njuga zao, na kaya zao;
19 na pete za masikio, na vikuku, na taji zao;
20 na dusumali, na mafurungu, na vitambi, na vibweta vya marashi, na matalasimu;
21 na pete, na azama,
22 na mavazi ya sikukuu, na debwani; na shali, na vifuko;
23 na vioo vidogo, na kitani nzuri, na vilemba, na utaji.
24 Hata itakuwa ya kuwa badala ya manukato mazuri kutakuwa uvundo, na badala ya mishipi, kamba; na badala ya nywele zilizosukwa vizuri, upaa; na badala ya kisibau, mavazi ya kigunia; na kutiwa alama mwilini kwa moto badala ya uzuri.
25 Watu wako waume wataanguka kwa upanga, na mashujaa wako vitani.
26 Na malango yake yatalia na kuomboleza, naye atakuwa ukiwa, atakaa chini.

Isaya 4


1 Na siku hiyo wanawake saba watamshika mtu mume mmoja wakisema, Tutakula chakula chetu, na kuvaa nguo zetu wenyewe, lakini tuitwe tu kwa jina lako; utuondolee aibu yetu.
2 Siku hiyo chipukizi la Bwana litakuwa zuri, lenye utukufu, na matunda ya nchi yatakuwa mema sana, na kupendeza, kwa ajili ya Waisraeli wale waliookoka.
3 Tena itakuwa ya kwamba yeye aliyebaki katika Sayuni, na yeye aliyeachwa ndani ya Yerusalemu, ataitwa mtakatifu; yaani, kila mmoja aliyeandikwa miongoni mwa hao walio hai ndani ya Yerusalemu;
4 hapo Bwana atakapokuwa ameuosha uchafu wa hao binti za Sayuni na kuisafisha damu ya Yerusalemu kati yake, kwa roho ya hukumu na kwa roho ya kuteketeza.
5 Tena juu ya makao yote ya mlima Sayuni, na juu ya makusanyiko yake, Bwana ataumba wingu na moshi wakati wa mchana, na mwangaza wa miali ya moto wakati wa usiku; kwa maana juu ya utukufu wote itatandazwa sitara.
6 Kisha kutakuwa na hema kuwa uvuli wakati wa mchana kwa sababu ya hari, na kuwa mahali pa kukimbilia na kujificha wakati wa tufani na mvua.

Isaya 5


1 Na nimwimbie mpenzi wangu wimbo wa mpenzi wangu katika habari za shamba lake la mizabibu. Mpenzi wangu alikuwa na shamba la mizabibu, Kilimani penye kuzaa sana;
2 Akafanya handaki kulizunguka pande zote, Akatoa mawe yake, Akapanda ndani yake mzabibu ulio mzuri, Akajenga mnara katikati yake, Akachimba shinikizo ndani yake; Akatumaini ya kuwa utazaa zabibu, Nao ukazaa zabibu-mwitu.
3 Na sasa, enyi wenyeji wa Yerusalemu, nanyi watu wa Yuda, amueni, nawasihi, kati ya mimi na shamba langu la mizabibu.
4 Je! Ni kazi gani iliyoweza kutendeka ndani ya shamba langu la mizabibu nisiyoitenda? Basi, nilipotumaini ya kuwa litazaa zabibu, mbona lilizaa zabibu-mwitu?
5 Haya basi, sasa nitawaambieni nitakalolitenda shamba langu la mizabibu; nitaondoa kitalu chake, nalo litaliwa; nitabomoa ukuta wake, nalo litakanyagwa;
6 nami nitaliharibu; wala halitapogolewa wala kulimwa, bali litamea mbigili na miiba; nami nitayaamuru mawingu yasinyeshe mvua juu yake.
7 Kwa maana shamba la mizabibu la Bwana wa majeshi ndilo nyumba ya Israeli, na watu wa Yuda ni mche wake wa kupendeza; akatumaini kuona hukumu ya haki, na kumbe! Aliona dhuluma; alitumaini kuona haki, na kumbe! Alisikia kilio.
8 Ole wao waongezao nyumba baada ya nyumba, na kuweka shamba karibu na shamba, hata hapana nafasi tena, nanyi hamna budi kukaa peke yenu kati ya nchi!
9 Bwana wa majeshi asema katika masikio yangu, Hakika majumba mengi yatakuwa ukiwa, naam, majumba makubwa, mazuri, yatakuwa hayana watu.
10 Kwa maana shamba la mizabibu la eka kumi litatoa bathi moja tu, na homeri ya mbegu itatoa efa tu.
11 Ole wao waamkao asubuhi na mapema, wapate kufuata kileo; wakishinda sana hata usiku wa manane mpaka mvinyo imewaka kama moto ndani yao!
12 Na kinubi, na zeze, na matari, na filimbi, na mvinyo, zote ziko katika karamu zao; lakini hawaiangalii kazi ya Bwana wala kuyafikiri matendo ya mikono yake.
13 Kwa sababu hiyo watu wangu wamechukuliwa mateka, kwa kukosa kuwa na maarifa; na watu wao wenye cheo wana njaa, na wengi wao waona kiu sana.
14 Kwa hiyo kuzimu kumeongeza tamaa yake, kumefunua kinywa chake bila kiasi; na utukufu wao, na wingi wao, na ghasia yao, naye pia afurahiye miongoni mwao, hushuka na kuingia humo.
15 Na mtu mnyonge ainamishwa, na mtu mkubwa amedhilika, na macho yao walioinuka hunyenyekezwa,
16 bali Bwana wa majeshi ametukuzwa katika hukumu, na Mungu aliye Mtakatifu ametakaswa katika haki.
17 Ndipo wana-kondoo watakapolisha kama katika malisho yao wenyewe, na mahali pao waliowanda, palipoachwa ukiwa, wageni watakula.
18 Ole wao wavutao uovu kwa kamba za ubatili, na dhambi kama kwa kamba za gari!
19 Wasema, Na afanye haraka, aihimize kazi yake, tupate kuiona; na likaribie shauri lake aliye Mtakatifu wa Israeli, tupate kuliona.
20 Ole wao wasemao kwamba uovu ni wema, na kwamba wema ni uovu; watiao giza badala ya nuru, na nuru badala ya giza; watiao uchungu badala ya utamu, na utamu badala ya uchungu!
21 Ole wao walio wenye hekima katika macho yao wenyewe, na wenye busara katika fikira zao wenyewe!
22 Ole wao walio hodari kunywa kileo chenye nguvu, watu waume wenye nguvu kuchanganya vileo;
23 wampao haki mwenye uovu, ili wapewe ijara, na kumwondolea mwenye haki haki yake!
24 Kwa hiyo kama vile mwali wa moto uteketezavyo mabua makavu, na kama manyasi makavu yaangukavyo katika mwali wa moto; kadhalika shina lao litakuwa kama ubovu, na ua lao litapeperushwa juu kama mavumbi; kwa sababu wameikataa sheria ya Bwana wa majeshi, na kulidharau neno lake aliye Mtakatifu wa Israeli.
25 Kwa sababu hiyo hasira ya Bwana imewaka juu ya watu wake, naye amenyosha mkono wake juu yao; akawapiga, navyo vilima vilitetemeka, na mizoga yao ilikuwa kama takataka katika njia kuu. Pamoja na hayo yote hasira yake haikugeukia mbali, lakini mkono wake umenyoshwa hata sasa.
26 Naye atawatwekea bendera mataifa toka mbali, Naye atawapigia miunzi tokea mwisho wa nchi; Na tazama, watakuja mbio mbio upesi sana.
27 Miongoni mwao hakuna achokaye wala kukwaa; Hakuna asinziaye wala kulala usingizi; Wala mshipi wa viuno vyao hautalegea. Wala ukanda wa viatu vyao hautakatika;
28 Mishale yao ni mikali, na pindi zao zote zimepindika; Kwato za farasi zao zitahesabika kama gumegume; Na gurudumu zao kama kisulisuli;
29 Ngurumo yao itakuwa kama ya simba; Watanguruma kama wana-simba; Naam, watanguruma na kukamata mateka, Na kuyachukua na kwenda zao salama, Wala hakuna mtu atakayeokoa.
30 Nao watanguruma juu yao siku hiyo Kama ngurumo ya bahari; Na mtu akiitazama nchi, ataona giza na dhiki Nayo nuru imetiwa giza katika mawingu yake.

Isaya 6


1 Katika mwaka ule aliokufa mfalme Uzia nalimwona Bwana ameketi katika kiti cha enzi, kilicho juu sana na kuinuliwa sana, na pindo za vazi lake zikalijaza hekalu.
2 Juu yake walisimama maserafi; kila mmoja alikuwa na mabawa sita; kwa mawili alifunika uso wake, na kwa mawili alifunika miguu yake, na kwa mawili aliruka.
3 Wakaitana, kila mmoja na mwenzake, wakisema, Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, ni Bwana wa majeshi; dunia yote imejaa utukufu wake.
4 Na misingi ya vizingiti ikatikisika kwa sababu ya sauti yake aliyelia, nayo nyumba ikajaa moshi.
5 Ndipo niliposema, Ole wangu! Kwa maana nimepotea; kwa sababu mimi ni mtu mwenye midomo michafu, nami ninakaa kati ya watu wenye midomo michafu; na macho yangu yamemwona Mfalme, Bwana wa majeshi.
6 Kisha mmoja wa maserafi wale akaruka akanikaribia; naye alikuwa na kaa la moto mkononi mwake, ambalo alikuwa amelitwaa kwa makoleo toka juu ya madhabahu;
7 akanigusa kinywa changu kwa kaa hilo, akaniambia, Tazama, hili limekugusa midomo yako, na uovu wako umeondolewa, na dhambi yako imefunikwa.
8 Kisha nikaisikia sauti ya Bwana, akisema, Nimtume nani, naye ni nani atakayekwenda kwa ajili yetu? Ndipo niliposema, Mimi hapa, nitume mimi.
9 Naye akaniambia, Enenda, ukawaambie watu hawa, Fulizeni kusikia, lakini msifahamu; fulizeni kutazama, lakini msione.
10 Uunoneshe moyo wa watu hawa, ukayatie uzito masikio yao, ukayafumbe macho yao; wasije wakaona kwa macho yao, na kusikia kwa masikio yao, na kufahamu kwa mioyo yao, na kurejea na kuponywa.
11 Ndipo nilipouliza, Ee Bwana, hata lini? Naye akanijibu, Hata miji itakapokuwa ukiwa, haina wenyeji, na nyumba zitakapokuwa hazina watu, na nchi hii itakapokuwa ganjo kabisa;
12 hata Bwana atakapowahamisha watu waende mbali sana, na mahame yatakapokuwa mengi ndani ya nchi.
13 Na ijapokuwa imebaki sehemu moja katika sehemu kumi ndani yake, italiwa hii nayo; kama mvinje na kama mwaloni, ambao shina lake limebaki, ingawa imekatwa; kadhalika mbegu takatifu ndiyo shina lake.

Isaya 7


1 Hata ikawa katika siku za Ahazi, mwana wa Yothamu, mwana wa Uzia, mfalme wa Yuda, Resini, mfalme wa Shamu, na Peka, mwana wa Remalia, mfalme wa Israeli, wakapanda wakaenda Yerusalemu ili kupigana nao, lakini hawakuweza kuushinda.
2 Kisha watu wa nyumba ya Daudi wakaambiwa kwamba Shamu wamefanya mapatano na Efraimu. Na moyo wake ukataharuki, na moyo wa watu wake, kama miti ya mwituni itikiswavyo na upepo.
3 Basi Bwana akamwambia Isaya, Haya, toka, umlaki Ahazi, wewe na Shear-yashubu mwana wako, huko mwisho wa mfereji wa birika la juu, katika njia kuu ya uwanja wa dobi;
4 ukamwambie, Angalia, ukatulie; usiogope wala usife moyo, kwa sababu ya mikia hii miwili ya vinga hivi vitokavyo moshi; kwa sababu ya hasira kali ya Resini na Shamu, na mwana wa Remalia.
5 Kwa kuwa Shamu amekusudia mabaya juu yako, pamoja na Efraimu na mwana wa Remalia, wakisema,
6 Haya, na tupande ili kupigana na Yuda na kuwasumbua, tukabomoe mahali tupate kuingia, na kummilikisha mfalme ndani yake, huyo mwana wa Tabeeli.
7 Bwana MUNGU asema hivi, Neno hili halitasimama wala halitakuwa.
8 Kwa maana kichwa cha Shamu ni Dameski, na kichwa cha Dameski ni Resini; na katika muda wa miaka sitini na mitano Efraimu atavunjika vipande vipande, asiwe kabila ya watu tena;
9 tena kichwa cha Efraimu ni Samaria, na kichwa cha Samaria ni mwana wa Remalia. Kwamba hamtaki kusadiki, bila shaka hamtathibitika.
10 Tena Bwana akasema na Ahazi akinena,
11 Jitakie ishara ya Bwana, Mungu wako; itake katika mahali palipo chini sana, au katika mahali palipo juu sana.
12 Lakini Ahazi akasema, Sitaitaka, wala sitamjaribu Bwana.
13 Naye akasema, Sikilizeni sasa, enyi nyumba ya Daudi; Je! Ni neno dogo kwenu kuwachosha wanadamu, hata mkataka kumchosha Mungu wangu pia?
14 Kwa hiyo Bwana mwenyewe atawapa ishara. Tazama, bikira atachukua mimba, atazaa mtoto mwanamume, naye atamwita jina lake Imanueli.
15 Siagi na asali atakula, wakati ajuapo kuyakataa mabaya na kuyachagua mema.
16 Kwa maana kabla mtoto huyo hajajua kuyakataa mabaya na kuyachagua mema, nchi ile, ambayo wewe unawachukia wafalme wake wawili, itaachwa ukiwa.
17 Bwana ataleta juu yako, na juu ya watu wako, na juu ya nyumba ya baba yako, siku zisizokuja bado, tangu siku ile aliyoondoka Efraimu kutoka katika Yuda; yaani, mfalme wa Ashuru.
18 Tena itakuwa katika siku hiyo Bwana atampigia kelele inzi aliye katika pande za mwisho za mito ya Misri, na nyuki aliye katika nchi ya Ashuru
19 Nao watakuja na kutulia katika mabonde yaliyo ukiwa, na katika pango za majabali, na juu ya michongoma yote, na juu ya malisho yote.
20 Katika siku hiyo Bwana atanyoa kichwa na malaika ya miguuni, kwa wembe ulioajiriwa pande za ng'ambo ya Mto, yaani, kwa mfalme wa Ashuru, nao utazimaliza ndevu nazo.
21 Katika siku hiyo itakuwa ya kwamba mtu atalisha ng'ombe mke mchanga na kondoo wake wawili;
22 kisha itakuwa, kwa sababu wanyama hao watatoa maziwa mengi, atakula siagi; kwa maana kila mtu aliyesalia katika nchi hii atakula siagi na asali.
23 Tena itakuwa katika siku hiyo kila mahali palipokuwa na mizabibu elfu, iliyopata fedha elfu, patakuwa mahali pa mbigili na miiba tu.
24 Mtu atakayekwenda huko atakwenda na mishale na upinde; kwa sababu nchi yote itakuwa ina mibigili na miiba.
25 Na vilima vyote vilivyolimwa kwa jembe, hutafika huko kwa sababu ya kuiogopa mibigili na miiba, lakini hapo patakuwa mahali pa kupeleka ng'ombe, mahali pa kukanyagwa na kondoo.

Isaya 8


1 Bwana akaniambia, Ujipatie ubao mkubwa ukaandike juu yake kwa kalamu ya binadamu, Kwa Maher-shalal-hash-bazi;
2 nami nitajipatia mashahidi waaminifu ili kuandika habari, yaani, Uria, kuhani, na Zekaria, mwana wa Yeberekia.
3 Nami nikamwendea huyo nabii mke, naye akapata mimba, akazaa mtoto mwanamume. Kisha Bwana akaniambia, Mwite jina lake Maher-shalal-hash-bazi.
4 Kwa maana kabla mtoto huyo hajapata kujua kusema, Baba yangu, na Mama yangu, hazina za Dameski na mateka ya Samaria yatachukuliwa mbele ya mfalme wa Ashuru.
5 Kisha Bwana akasema nami mara ya pili, akaniambia,
6 Kwa sababu watu hawa wameyakataa maji ya Shiloa yapitayo polepole, na kufurahi kwa ajili ya Resini na huyo mwana wa Remalia,
7 basi sasa angalia; Bwana aleta juu yao maji ya huo Mto, yenye nguvu, mengi sana, nayo ni mfalme wa Ashuru na utukufu wake wote; naye atakuja, na kupita juu ya mifereji yake yote, atafurika juu ya kingo zake zote;
8 naye atapita, atapita kwa kasi na kuingia Yuda; atafurika na kupita katikati, atafika hata shingoni; na kule kuyanyosha mabawa yake kutaujaza upana wa nchi yako, Ee Imanueli.
9 Fanyeni ghasia, enyi kabila za watu, Nanyi mtavunjwa vipande vipande; Tegeni masikio, ninyi nyote wa nchi zilizo mbali; Jikazeni viuno, nanyi mtavunjwa vipande vipande; Jikazeni viuno, nanyi mtavunjwa vipande vipande.
10 Fanyeni shauri pamoja, nalo litabatilika; Semeni neno, lakini halitasimama; Kwa maana Mungu yu pamoja nasi.
11 Maana Bwana aliniambia hivi, kwa mkono hodari, akanifundisha nisiende katika njia ya watu hawa, akisema,
12 Msiseme, Ni fitina, katika habari za mambo yote ambayo watu hawa watasema, Ni fitina; msihofu kwa hofu yao, wala msiogope.
13 Bwana wa majeshi ndiye mtakayemtakasa; na awe yeye hofu yenu, na awe yeye utisho wenu.
14 Naye atakuwa ni mahali patakatifu; bali ni jiwe la kujikwaza na mwamba wa kujikwaa kwa nyumba za Israeli zote mbili, na mtego na tanzi kwa wenyeji wa Yerusalemu.
15 Na wengi watajikwaa juu yake, na kuanguka na kuvunjika, na kunaswa na kukamatwa.
16 Ufunge huo ushuhuda, ukaitie muhuri sheria kati ya wanafunzi wangu.
17 Nami nitamngojea Bwana, awafichaye uso wake nyumba ya Yakobo, nami nitamtazamia.
18 Angalieni, mimi na watoto hawa niliopewa na Bwana tu ishara na ajabu katika Israeli, zitokazo kwa Bwana wa majeshi, yeye akaaye katika mlima Sayuni.
19 Na wakati watakapokuambia, Tafuta habari kwa watu wenye pepo na kwa wachawi; waliao kama ndege na kunong'ona; je! Haiwapasi watu kutafuta habari kwa Mungu wao? Je! Waende kwa watu waliokufa kwa ajili ya watu walio hai?
20 Na waende kwa sheria na ushuhuda; ikiwa hawasemi sawasawa na neno hili, bila shaka kwa hao hapana asubuhi.
21 Nao watapita katikati yake, wamedhikika sana na kuwa na njaa; na itakuwa watakapoona njaa, watalalamika na kuapa kwa mfalme wao, na kwa Mungu wao, na kuelekeza nyuso zao juu;
22 nao wataiangalia nchi, na, tazama, shida na giza; hapana changamko kwa sababu ya dhiki; nao watafukuzwa na kuingia katika giza kubwa.

Isaya 9


1 Lakini yeye aliyekuwa katika dhiki hatakosa changamko. Hapo kwanza aliiingiza nchi ya Zabuloni na nchi ya Naftali katika hali ya kudharauliwa, lakini zamani za mwisho ameifanya kuwa tukufu, karibu na njia ya bahari; ng'ambo ya Yordani, Galilaya ya mataifa.
2 Watu wale waliokwenda katika giza Wameona nuru kuu; Wale waliokaa katika nchi ya uvuli wa mauti, Nuru imewaangaza.
3 Umeliongeza taifa, umezidisha furaha yao; Wanafurahi mbele zako, Kama furaha ya wakati wa mavuno, Kama watu wafurahivyo wagawanyapo nyara.
4 Kwa maana umeivunja nira ya mzigo wake, na gongo la bega lake, na fimbo yake yeye aliyemwonea, kama katika siku ya Midiani.
5 Maana silaha zote za mtu mwenye silaha wakati wa mshindo, na mavazi yaliyofingirishwa katika damu, yatakuwa tayari kuteketezwa, yatakuwa kuni za kutiwa motoni.
6 Maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, Tumepewa mtoto mwanamume; Na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake; Naye ataitwa jina lake, Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, Mfalme wa amani.
7 Maongeo ya enzi yake na amani Hayatakuwa na mwisho kamwe, Katika kiti cha enzi cha Daudi na ufalme wake; Kuuthibitisha na kuutegemeza Kwa hukumu na kwa haki, Tangu sasa na hata milele. Wivu wa Bwana wa majeshi ndio utakaotenda hayo.
8 Bwana alimpelekea Yakobo neno, likamfikilia Israeli.
9 Nao watu wote watajua, yaani, Efraimu na yeye akaaye Samaria, wasemao kwa kiburi na kwa kujisifu nafsi zao,
10 Matofali yameanguka, lakini sisi tutajenga kwa mawe yaliyochongwa; mikuyu imekatwa lakini sisi tutaweka mierezi badala yake.
11 Kwa sababu hiyo Bwana atawainua adui wa Resini juu yake, naye atawachochea adui zake;
12 Waashuri upande wa mbele, na Wafilisti upande wa nyuma, nao watamla Israeli kwa kinywa kilicho wazi. Pamoja na hayo yote hasira yake haikugeukia mbali, lakini mkono wake umenyoshwa hata sasa.
13 Lakini watu hao hawakumwelekea yeye aliyewapiga, wala kumtafuta Bwana wa majeshi.
14 Kwa sababu hiyo Bwana atakata katika Israeli kichwa na mkia, kuti na nyasi, katika siku moja.
15 Mzee mwenye kuheshimiwa ndiye kichwa, na nabii afundishaye uongo ndiye mkia.
16 Kwa maana wawaongozao watu hawa ndio wawakoseshao, na hao walioongozwa na watu hao wameangamia.
17 Kwa sababu hiyo Bwana hatawafurahia vijana wao, wala hatawahurumia yatima zao wala wajane wao; maana kila mtu ni mnajisi, dhalimu, na kila ulimi hunena upumbavu. Pamoja na hayo yote hasira yake haikugeukia mbali, lakini mkono wake umenyoshwa hata sasa.
18 Kwa maana uovu huteketeza kama moto; huila mibigili na miiba, naam, huwaka katika vichaka vya mwitu, nao hupaa juu katika mawingu mazito ya moshi.
19 Kwa sababu ya hasira ya Bwana wa majeshi nchi hii inateketea kabisa; watu hawa nao ni kama kuni zitiwazo motoni; hapana mtu amhurumiaye ndugu yake.
20 Hupokonya upande wa mkono wa kuume, nao huona njaa! Hula upande wa mkono wa kushoto, wala hawashibi! Watakula kila mtu nyama ya mkono wake mwenyewe.
21 Manase anamla Efraimu, naye Efraimu anamla Manase; nao wawili pamoja watakuwa juu ya Yuda. Pamoja na hayo yote hasira yake haikugeukia mbali, lakini mkono wake umenyoshwa hata sasa.

Isaya 10


1 Ole wao wawekao amri zisizo za haki, na waandishi waandikao maneno ya ushupavu;
2 ili kumpotosha mhitaji asipate haki yake, na kuwanyang'anya maskini wa watu wangu haki yao; ili wajane wawe mateka yao, na kuwafanya yatima waliofiwa na baba zao kuwa mawindo yao!
3 Nanyi mtafanya nini siku ya kujiliwa, na wakati wa uangamivu, utakaokuja kutoka mbali sana? Je! Mtamkimbilia nani mpate msaada? Na utukufu wenu mtauacha wapi?
4 Watainama chini ya wafungwa tu, wataanguka chini yao waliouawa. Pamoja na hayo yote hasira yake haikugeukia mbali, lakini mkono wake umenyoshwa hata sasa.
5 Ole wake Ashuru! Fimbo ya hasira yangu, ambaye gongo lililo mkononi mwake ni ghadhabu yangu!
6 Nitamtuma juu ya taifa lenye kukufuru, nitampa maagizo juu ya watu wa ghadhabu yangu, ateke nyara, na kuchukua mateka, na kuwakanyaga kama matope ya njiani.
7 Lakini hivyo sivyo akusudiavyo mwenyewe, wala sivyo moyo wake uwazavyo; maana katika moyo wake akusudia kuharibu, na kukatilia mbali mataifa, wala si mataifa machache.
8 Maana asema, Je! Wakuu wangu si wote wafalme?
9 Je! Kalno si kama Karkemishi? Hamathi si kama Arpadi? Samaria si kama Dameski?
10 Kama vile mkono wangu ulivyofikilia falme za sanamu, ambazo sanamu zao za kuchongwa zilikuwa bora kuliko sanamu za Yerusalemu na za Samaria;
11 je! Sitautenda Yerusalemu na sanamu zake vile vile kama nilivyoutenda Samaria na sanamu zake?
12 Basi, itakuwa, Bwana atakapokuwa ameitimiza kazi yake yote juu ya mlima Sayuni na juu ya Yerusalemu, nitayaadhibu matunda ya kiburi cha moyo wake mfalme wa Ashuru, na majivuno ya macho yake.
13 Kwa maana amesema, Kwa nguvu za mkono wangu nimetenda jambo hili, na kwa hekima yangu; maana mimi nina busara; nami nimeiondoa mipaka ya watu, nikaziteka akiba zao, nikawaangusha waketio juu ya viti vya enzi kama afanyavyo shujaa.
14 Na mkono wangu umezitoa mali za mataifa kama katika kioto cha ndege; na kama vile watu wakusanyavyo mayai yaliyoachwa, ndivyo nilivyokusanya dunia yote; wala hapana aliyetikisa bawa, wala kufumbua kinywa, wala kulia.
15 Je! Shoka lijisifu juu yake alitumiaye? Je! Msumeno ujitukuze juu yake auvutaye? Ingekuwa kana kwamba bakora ingewatikisa waiinuao, au fimbo ingemwinua yeye ambaye si mti.
16 Kwa hiyo Bwana, Bwana wa majeshi, atawapelekea kukonda watu wake walionona; na badala ya utukufu wake kutawashwa kuteketea kama kuteketea kwa moto.
17 Na mwanga wa Israeli utakuwa ni moto, na Mtakatifu wake atakuwa mwali wa moto; nao utateketeza na kula mbigili zake na miiba yake katika siku moja.
18 Naye atauteketeza utukufu wa msitu wake, na wa shamba lake linalositawi, tangu nafsi hata nyama ya mwili, itakuwa kama vile afapo mtu aliye mgonjwa.
19 Na miti ya msitu wake itakayosalia itakuwa michache, hata mtoto ataweza kuihesabu.
20 Tena itakuwa katika siku hiyo mabaki ya Israeli, na hao waliopona wa nyumba ya Yakobo, hawatamtegemea tena yeye aliyewapiga, bali watamtegemea Bwana, Mtakatifu wa Israeli, kwa kweli.
21 Mabaki, nao ni mabaki ya Yakobo, watamrudia Mungu, aliye mwenye nguvu.
22 Maana watu wako, Ee Israeli, wajapokuwa wengi kama mchanga wa pwani, ni mabaki tu watakaorudi; kuangamiza kumekusudiwa, kunakofurika kwa haki.
23 Kwa maana Bwana, Bwana wa majeshi, atayatimiza maangamizo yaliyokusudiwa katika nchi yote.
24 Kwa hiyo Bwana, Bwana wa majeshi, asema hivi, Enyi watu wangu mkaao katika Sayuni, msiogope Ashuru, ingawa akupiga kwa fimbo, na kuliinua gongo lake juu yako, kwa namna ya Kimisri.
25 Maana bado kitambo kidogo tu ghadhabu itakoma, na hasira yangu itageukia kuwaangamiza.
26 Na Bwana wa majeshi ataamsha mjeledi juu yake, kama vile alivyopiga Midiani karibu na jabali la Orebu; na fimbo yake itakuwa juu ya bahari, naye ataiinua kwa namna ya Kimisri.
27 Tena itakuwa katika siku hiyo mzigo wake utaondoka begani mwako, na nira yake shingoni mwako, nayo nira itaharibiwa, kwa sababu ya kutiwa mafuta.
28 Amefika Ayathi; amepita kati ya Migroni; ameweka mizigo yake huko Mikmashi;
29 wamevuka kivuko; wamekwenda kulala katika Geba; Rama unatetemeka; Gibea wa Sauli umekimbia.
30 Piga kelele sana, Ee binti Galimu; sikiliza, Ee Laisha; ole wako, maskini Anathothi!
31 Madmena ni mkimbizi; wenyeji wa Gebimu wamejikusanya wakimbie;
32 siku hii ya leo atasimama huko Nobu; anatikisa mkono wake juu ya mlima wa binti Sayuni, mlima wa Yerusalemu.
33 Angalia, Bwana, Bwana wa majeshi, atayakata matawi kwa nguvu za kutisha; nao walio warefu wa kimo watakatwa; na hao walioinuka wataangushwa chini;
34 naye atavikata vichaka vya msitu kwa chuma; na Lebanoni utaanguka kwa mkono wake aliye mwenye uweza.

Isaya 11


1 Basi litatoka chipukizi katika shina la Yese, na tawi litakalotoka katika mizizi yake litazaa matunda.
2 Na roho ya Bwana atakaa juu yake, roho ya hekima na ufahamu, roho ya shauri na uweza, roho ya maarifa na ya kumcha Bwana;
3 na furaha yake itakuwa katika kumcha Bwana; wala hatahukumu kwa kuyafuata ayaonayo kwa macho yake, wala hataonya kwa kuyafuata ayasikiayo kwa masikio yake;
4 bali kwa haki atawahukumu maskini, naye atawaonya wanyenyekevu wa dunia kwa adili; naye ataipiga dunia kwa fimbo ya kinywa chake, na kwa pumzi ya midomo yake atawaua wabaya.
5 Na haki itakuwa mshipi wa viuno vyake, na uaminifu mshipi wa kujifungia.
6 Mbwa-mwitu atakaa pamoja na mwana-kondoo, na chui atalala pamoja na mwana-mbuzi; ndama na mwana-simba na kinono watakuwa pamoja, na mtoto mdogo atawaongoza.
7 Ng'ombe na dubu watalisha pamoja; watoto wao watalala pamoja; na simba atakula majani kama ng'ombe.
8 Na mtoto anyonyaye atacheza penye tundu la nyoka, na mtoto aliyeachishwa atatia mkono wake katika pango la fira.
9 Hawatadhuru wala hawataharibu katika mlima wangu wote mtakatifu; maana dunia itajawa na kumjua Bwana, kama vile maji yanavyoifunika bahari.
10 Na itakuwa katika siku hiyo, shina la Yese lisimamalo kuwa ishara kwa kabila za watu, yeye ndiye ambaye mataifa watamtafuta; na mahali pake pa kupumzikia patakuwa na utukufu.
11 Na itakuwa katika siku hiyo, Bwana atapeleka mkono wake mara ya pili, ili ajipatie watu wake watakaosalia, kutoka Ashuru, na kutoka Misri, na kutoka Pathrosi, na kutoka Kushi, na kutoka Elamu, na kutoka Shinari, na kutoka Hamathi, na kutoka visiwa vya bahari.
12 Naye atawatwekea mataifa bendera, atawakutanisha watu wa Israeli waliotupwa, atawakusanya watu wa Yuda waliotawanyika, kutoka ncha nne za dunia.
13 Na wivu wa Efraimu utaondoka, na wale wanaomwudhi Yuda watakatiliwa mbali; Efraimu hatamhusudu Yuda, wala Yuda hatamwudhi Efraimu.
14 Nao watashuka, watalirukia bega la Wafilisti upande wa magharibi; nao pamoja watawateka wana wa mashariki; watanyosha mkono juu ya Edomu na Moabu; na wana wa Amoni watawatii.
15 Na Bwana atauangamiza kabisa ulimi wa bahari ya Misri; na kwa upepo wake uteketezao atatikisa mkono wake juu ya Mto, naye ataupiga, uwe vijito saba, na kuwavusha watu wenye viatu vikavu.
16 Itakuwako njia kuu kwa mabaki ya watu wake watakaobaki, watokao Ashuru, kama vile ilivyokuwako kwa Israeli, katika siku ile waliyotoka katika nchi ya Misri.

Isaya 12


1 Na katika siku hiyo utasema, Ee Bwana, nitakushukuru wewe; Kwa kuwa ijapokuwa ulinikasirikia, Hasira yako imegeukia mbali, Nawe unanifariji moyo.
2 Tazama, Mungu ndiye wokovu wangu; Nitatumaini wala sitaogopa; Maana Bwana YEHOVA ni nguvu zangu na wimbo wangu; Naye amekuwa wokovu wangu.
3 Basi, kwa furaha mtateka maji katika visima vya wokovu.
4 Na katika siku hiyo mtasema, Mshukuruni Bwana, liitieni jina lake; Yatangazeni matendo yake kati ya mataifa, Litajeni jina lake kuwa limetukuka.
5 Mwimbieni Bwana; kwa kuwa ametenda makuu; Na yajulikane haya katika dunia yote.
6 Paza sauti, piga kelele, mwenyeji wa Sayuni; Maana Mtakatifu wa Israeli ni mkuu kati yako.

Isaya 13


1 Ufunuo juu ya Babeli; maono aliyoyaona Isaya, mwana wa Amozi.
2 Haya! Juu ya mlima usio na miti inueni bendera, wapazieni sauti zenu, wapungieni mkono, kwamba waingie katika malango ya wakuu.
3 Mimi mwenyewe nimewaamuru watu wangu waliowekwa wakfu kwangu, naam, nimewaita watu wangu walio hodari kwa ajili ya hasira yangu, watu wangu wenye kutakabari.
4 Kelele milimani kama kelele za watu wengi sana; kelele za falme za mataifa waliokutana pamoja; Bwana wa majeshi anapanga jeshi kwa vita;
5 watu waliotoka katika nchi iliyo mbali, tokea upande wa mwisho wa mbingu; naam, Bwana na silaha za ghadhabu yake, ili aiangamize nchi yote.
6 Pigeni kelele za hofu; maana siku ya Bwana i karibu; itanyesha kama maangamizi yatokayo kwa Mwenyezi Mungu.
7 Kwa sababu hiyo mikono yote italegea, na moyo wa kila mtu utayeyuka.
8 Nao watafadhaika; watashikwa na utungu na maumivu; watakuwa na utungu kama mwanamke aliye karibu na kuzaa; watakodoleana macho; nyuso zao zitakuwa ni nyuso za moto.
9 Tazama, siku ya Bwana inakuja, siku kali, ya hasira na ghadhabu kuu, ili iifanye nchi kuwa ukiwa, na kuwaharibu watu wake, wenye dhambi, wasikae ndani yake.
10 Maana nyota za mbinguni na matangamano havitatoa nuru yake; jua litatiwa giza wakati wa kucha kwake, na mwezi utaacha nuru yake isiangaze.
11 Nami nitaadhibu ulimwengu kwa sababu ya ubaya wake, na wenye dhambi kwa sababu ya hatia yao; nami nitaikomesha fahari yao wenye kiburi; nami nitayaangusha chini majivuno yao walio wakali;
12 nitafanya wanadamu kuadimika kuliko dhahabu safi, na watu kuliko dhahabu ya Ofiri.
13 Kwa hiyo nitazitetemesha mbingu, na dunia itatikiswa itoke katika mahali pake, kwa sababu ya ghadhabu ya Bwana wa majeshi, na kwa sababu ya siku ya hasira yake kali.
14 Basi, itakuwa kama vile paa aliyetishwa, na kama kondoo wasio na mtu wa kuwakusanya; kila mtu atageukia watu wake; nao watakimbia, kila mtu aende nchi yake mwenyewe.
15 Kila mtu atakayeonekana atatumbuliwa, na kila mtu atakayepatikana ataanguka kwa upanga.
16 Na watoto wao wachanga watavunjwa-vunjwa mbele ya macho yao, nyumba zao zitatekwa nyara, na wake zao watatendwa jeuri.
17 Tazama, nitawaamsha Wamedi juu yao, ambao hawaoni fedha kuwa kitu, wala hawafurahii dhahabu.
18 Na nyuta zao zitawaangusha vijana; wala hawatahurumia mazao ya tumbo; jicho lao halitawahurumia watoto.
19 Na Babeli, huo utukufu wa falme, uzuri wa kiburi cha Wakaldayo, utakuwa kama Sodoma na Gomora hapo Mungu alipoiangamiza.
20 Hautakaliwa na watu tena kabisa, wala watu hawatakaa ndani yake tangu kizazi hata kizazi. Mwarabu hatapiga hema yake huko, wala wachungaji hawatalaza makundi yao huko.
21 Lakini huko watalala hayawani wakali wa nyikani; na nyumba zao zitajaa bundi; mbuni watakaa huko; na majini watacheza huko.
22 Na mbwa-mwitu watalia ndani ya ngome zake; na mbweha ndani ya majumba ya anasa; na wakati wake u karibu kufika, na siku zake hazitaongezeka.

Isaya 14


1 Maana Bwana atamhurumia Yakobo, atamchagua Israeli tena, naye atawaweka katika nchi yao wenyewe; na mgeni atajiunga nao, nao wataambatana na nyumba ya Yakobo.
2 Na hao mataifa watawatwaa na kuwaleta mpaka mahali pao wenyewe, na nyumba ya Israeli watawamiliki, na kuwafanya watumishi na wajakazi katika nchi ya Bwana; nao watawachukua hali ya kufungwa watu wale waliowafunga wao, nao watawamiliki watu wale waliowaonea.
3 Tena itakuwa katika siku ile, ambayo Bwana atakupa raha baada ya huzuni yako, na baada ya taabu yako, na baada ya utumishi ule mgumu uliotumikishwa;
4 utatunga mithali hii juu ya mfalme wa Babeli, na kusema, Jinsi alivyokoma mwenye kuonea; Jinsi ulivyokoma mji ule wenye jeuri!
5 Bwana amelivunja gongo la wabaya, Fimbo ya enzi yao wenye kutawala.
6 Yeye aliyewapiga mataifa kwa ghadhabu, Kwa mapigo yasiyokoma; Aliyewatawala mataifa kwa hasira, Ameadhibiwa asizuie mtu.
7 Dunia yote inastarehe na kutulia; Hata huanzilisha kuimba.
8 Naam, misunobari inakufurahia, Na mierezi ya Lebanoni, ikisema, Tokea wakati ulipolazwa chini wewe, Hapana mkata miti aliyetujia.
9 Kuzimu chini kumetaharuki kwa ajili yako, Ili kukulaki utakapokuja; Huwaamsha waliokufa kwa ajili yako, Naam, walio wakuu wote wa dunia; Huwainua wafalme wote wa mataifa, Watoke katika viti vyao vya enzi.
10 Hao wote watajibu na kukuambia, Je! Wewe nawe umekuwa dhaifu kama sisi! Wewe nawe umekuwa kama sisi!
11 Fahari yako imeshushwa hata kuzimu, Na sauti ya vinanda vyako; Funza wametandazwa chini yako, Na vidudu vinakufunika.
12 Jinsi ulivyoanguka kutoka mbinguni, Ewe nyota ya alfajiri, mwana wa asubuhi! Jinsi ulivyokatwa kabisa, Ewe uliyewaangusha mataifa!
13 Nawe ulisema moyoni mwako, Nitapanda mpaka mbinguni, Nitakiinua kiti changu juu kuliko nyota za Mungu; Nami nitaketi juu ya mlima wa mkutano, Katika pande za mwisho za kaskazini.
14 Nitapaa kupita vimo vya mawingu, Nitafanana na yeye Aliye juu.
15 Lakini utashushwa mpaka kuzimu; Mpaka pande za mwisho za shimo.
16 Wao wakuonao watakukazia macho, Watakuangalia sana, wakisema, Je! Huyu ndiye aliyeitetemesha dunia, Huyu ndiye aliyetikisa falme;
17 Aliyeufanya ulimwengu ukiwa, akaipindua miji yake; Asiyewafungua wafungwa wake waende kwao?
18 Wafalme wote wa mataifa wamezikwa wote kwa heshima, Kila mmoja ndani ya nyumba yake mwenyewe;
19 Bali wewe umetupwa mbali na kaburi lako, Kama chipukizi lililochukiza kabisa; Kama vazi la wale waliouawa, Wale waliochomwa kwa upanga, Wale washukao mpaka misingi ya shimo; Kama mzoga uliokanyagwa chini ya miguu.
20 Hutaungamanishwa pamoja nao katika mazishi, Kwa maana umeiharibu nchi yako, Umewaua watu wako; Kizazi chao watendao uovu hakitatajwa milele.
21 Fanyeni tayari machinjo kwa watoto wake. Kwa sababu ya uovu wa baba zao; Wasije wakainuka na kuitamalaki nchi, Na kuujaza miji uso wa ulimwengu.
22 Nami nitainuka, nishindane nao; asema Bwana wa majeshi; na katika Babeli nitang'oa jina na mabaki, mwana na mjukuu; asema Bwana.
23 Tena nitaifanya hiyo nchi kuwa makao ya nungu, na maziwa ya maji; nami nitaifagilia mbali kwa ufagio wa uharibifu; asema Bwana wa majeshi.
24 Bwana wa majeshi ameapa, akisema, Hakika yangu kama vile vilivyoazimia, ndivyo itakavyokuwa; na kama nilivyokusudia, ndivyo itakavyotokea;
25 kwamba nitamvunja huyo Mwashuri vipande vipande katika nchi yangu, na juu ya mlima wangu nitamkanyaga chini ya miguu yangu; ndipo nira yake iliyo juu yao itakapoondoka, na mzigo wake utatoka mabegani mwao.
26 Hilo ndilo kusudi lililokusudiwa duniani mwote, na huo ndio mkono ulionyoshwa juu ya mataifa yote.
27 Maana Bwana wa majeshi amekusudia, naye ni nani atakayelibatili? Na mkono wake ulionyoshwa, ni nani atakayeugeuza nyuma?
28 Ufunuo huu ulikuja mwaka ule alipokufa mfalme Ahazi.
29 Usifurahi, Ee Ufilisti, pia wote, Kwa sababu fimbo ile iliyokupiga imevunjika; Maana katika shina la nyoka atatoka fira, Na uzao wake ni joka la moto arukaye
30 Nao walio maskini kabisa watakula, Na wahitaji watajilaza salama; Nami nitatia shina lako kwa njaa, Na mabaki yako watauawa.
31 Piga yowe, Ee lango; lia, Ee mji; Ee Ufilisti, pia wote, umeyeyuka kabisa; Maana moshi unakuja toka kaskazini, Wala hakuna atakayechelewa katika majeshi yake.
32 Wajumbe wa taifa hilo waletewe jibu gani? Ya kuwa Bwana ameiweka misingi ya Sayuni, na ndani yake wale walioonewa katika watu wake wataona kimbilio.

Isaya 15


1 Ufunuo juu ya Moabu. Maana katika usiku mmoja Ari wa Moabu umeharibiwa kabisa na kuangamizwa; maana katika usiku mmoja Kiri wa Moabu umeharibiwa kabisa na kuangamizwa.
2 Wanapanda juu hata Bayithi na Diboni, mpaka mahali palipo juu ili walie; juu ya Nebo na juu ya Medeba Wamoabi wanalia; Wana upaa juu ya vichwa vyao vyote; kila ndevu zimenyolewa.
3 Wanajivika nguo za magunia katika njia kuu zao; juu ya dari zao, na katika mitaa yao, kila mtu analia, anamwaga machozi.
4 Heshboni analia na Eleale; mpaka Yahasa sauti ya kulia kwao inasikiwa; hata watu wa Moabu waliovaa silaha wanapiga kelele sana kwa sababu hiyo; nafsi yake inatetemeka ndani yake.
5 Moyo wangu unamlilia Moabu; wakuu wake wanakimbilia Soari kama ndama wa miaka mitatu; kwa maana wanapanda mbavu za Luhithi wakilia; maana katika njia iendayo hata Horonaimu wanapaliza sauti ya kukata tamaa.
6 Kwa maana maji ya Nimrimu yamekuwa mahali palipoharibika, kwa kuwa majani yamekauka, miche imenyauka, majani mabichi yamekoma.
7 Kwa hiyo vitu walivyojipatia tele, na akiba yao, wanavichukua hata kijito cha mierebi.
8 Maana kilio hicho kimezunguka mipaka ya Moabu, malalamiko yao yamefika hata Eglaimu, na malalamiko yao hata Beer-Elimu.
9 Maana maji ya Dimoni yamejaa damu; maana ninaweka tayari msiba mpya juu ya Dimoni, simba juu ya watu wa Moabu waliokimbia, na juu ya mabaki yao.

Isaya 16


1 Pelekeni wana-kondoo, kodi yake aitawalaye nchi toka Sela kuelekea jangwani, mpaka mlima wa binti Sayuni.
2 Na binti za Moabu watakuwa kama ndege warukao huko na huko, kama kioto cha ndege waliotiwa hofu, kwenye vivuko vya Arnoni.
3 Lete shauri; kata neno; fanya kivuli chako kuwa kama usiku kati ya mchana; wafiche waliofukuzwa; usiwachongee waliopotea.
4 Watu wangu waliofukuzwa waache wakae pamoja nawe; katika habari za Moabu, uwe sitara kwake mbele ya uso wake anayeharibu; maana yeye atozaye kwa nguvu amekoma; afanyaye ukiwa ametoweka; waliokanyaga watu wametoka katika nchi.
5 Na kiti cha enzi kitafanywa imara kwa rehema; na mmoja ataketi juu yake katika kweli, katika hema ya Daudi; akifanya hukumu, akitaka sana yaliyo haki, mwepesi wa kutenda haki.
6 Tumesikia habari za kiburi cha Moabu, ya kwamba ni mwenye kiburi kingi; habari za majivuno yake, na kiburi chake, na ghadhabu yake; majivuno yake si kitu.
7 Kwa sababu hiyo Moabu atalia kwa ajili ya Moabu, kila mmoja atalia, maana mtaiombolezea mikate ya zabibu ya Kir-Haresethi, mkipigwa sana.
8 Maana makonde ya Heshboni yamenyauka, na mzabibu wa Sibma; mabwana wa mataifa wameyavunja matawi yake mateule; yamefika hata Yazeri, yalitanga-tanga hata nyikani; matawi yake yalitapakaa, yaliivuka bahari.
9 Basi, naililia mizabibu ya Sibma kwa kilio cha Yazeri, nitawanyeshea machozi yangu, Ee Heshboni na Eleale, kwa kuwa kelele za vita zimeyaangukia mavuno ya matunda yako, na mavuno ya mizabibu yako.
10 Na furaha imeondolewa, na shangwe toka mashamba yaliyozaa sana; hapana kuimba katika mashamba ya mizabibu, wala sauti za furaha; akanyagaye hakanyagi divai katika mashinikizo; nimeikomesha sauti ya furaha yake akanyagaye.
11 Kwa sababu hiyo mtima wangu unamlilia Moabu kama kinubi, na matumbo yangu kwa ajili ya Kir-Heresi.
12 Tena itakuwa, Moabu akionekana, na kujichosha kwa kulia juu ya mahali pa juu, na kuingia katika patakatifu pake aombe, hatapata kushinda.
13 Hilo ndilo neno lile alilolisema Bwana juu ya Moabu zamani.
14 Lakini sasa Bwana asema hivi, Katika muda wa miaka mitatu, kama miaka ya mtu wa mshahara, utukufu wa Moabu utadharauliwa, pamoja na wingi wake wote; mabaki yake yatakuwa machache sana, kama si kitu kabisa.

Isaya 17


1 Ufunuo juu ya Dameski. Tazama, Dameski umeondolewa usiwe mji, nao utakuwa chungu ya magofu.
2 Miji ya Aroeri imeachwa; itakuwa kwa makundi ya kondoo, nao watajilaza huko wala hapana atakayewatia hofu.
3 Na ngome ya Efraimu itakomeshwa, na ufalme wa Dameski, na mabaki ya Shamu; watakuwa kama utukufu wa wana wa Israeli, asema Bwana wa majeshi.
4 Tena itakuwa katika siku hiyo, utukufu wa Yakobo utapungua-pungua, na kunona kwa mwili wake kutakonda.
5 Tena itakuwa kama hapo avunaye ashikapo mabua ya ngano, na mkono wake ukatapo masuke; tena itakuwa kama hapo mtu aokotapo masuke katika bonde la Warefai.
6 Lakini kilichosazwa na mvunaji kitakuwa ndani yake, kama vile wakati wa kupiga mizeituni, matunda mawili matatu yaliyo juu sana; matunda manne matano katika matawi, matawi ya mti wa matunda, asema Bwana, Mungu wa Israeli.
7 Katika siku hiyo mwanadamu atamwangalia Muumba wake, na macho yake yatamtazama Mtakatifu wa Israeli.
8 Wala hataziangalia madhabahu, kazi ya mikono yake; wala hatavitazama vilivyofanyika kwa vidole vyake, maashera na sanamu za jua.
9 Katika siku hiyo miji yake yenye maboma itakuwa kama mahali palipoachwa ndani ya mwitu, na juu ya kilele cha mlima, palipoachwa mbele ya wana wa Israeli; napo patakuwa ganjo.
10 Maana umemsahau Mungu wa wokovu wako, wala hukuukumbuka mwamba wa ngome yako; kwa sababu hiyo ulipanda mashamba yapendezayo, na kutia ndani yake mizabibu migeni.
11 Katika siku ile ulipopanda, ulifanya kitalu, na wakati wa asubuhi ulizimeesha mbegu zako, lakini mavuno yatatoweka siku ya huzuni, na ya sikitiko la moyo lifishalo.
12 Aha! Uvumi wa watu wengi! Wanavuma kama uvumi wa bahari; Aha! Ngurumo ya mataifa! Wananguruma kama ngurumo ya maji mengi;
13 Mataifa wananguruma kama ngurumo ya maji mengi; Lakini atawakemea, nao watakimbia mbali sana, Watafukuzwa kama makapi milimani mbele ya upepo, Na kama mavumbi vuruvuru mbele ya tufani.
14 Wakati wa jioni, tazama, kuna hofu; Na kabla ya mapambazuko hawako; Hilo ndilo fungu lao watutekao, Na ajali yao wanaotunyang'anya mali zetu.

Isaya 18


1 Ole wa nchi ya uvumi wa mabawa, Iliyoko mbali kupita mito ya Kushi;
2 Ipelekayo wajumbe wake kwa njia ya bahari, Na katika vyombo vya manyasi juu ya maji. Nendeni, wajumbe wepesi,kwa watu warefu,laini; Watu watishao tangu mwanzo wao hata sasa; Taifa la wenye nguvu,wakanyagao watu, Ambao mito inakata nchi yao.
3 Enyi watu mkaao katika ulimwengu wote, na wenyeji wa dunia, bendera ikiinuliwa milimani, angalieni; na wakipiga tarumbeta, sikieni.
4 Maana Bwana ameniambia hivi, Mimi nitatulia, na kuangalia katika makazi yangu, kama wakati wa mwangaza mweupe wa jua kali, mfano wa wingu la umande katika hari ya mavuno.
5 Maana kabla ya mavuno, maua yaangukapo, na maua yakawa zabibu zianzazo kuiva, ndipo atakapoyakata matawi kwa miundu, na kuviondoa vitawi vilivyopanuka na kuvikata.
6 Wote pamoja wataachiwa ndege wakali wa milimani, na hayawani wa nchi; ndege wakali watakaa juu yao wakati wa jua, na hayawani wote wa nchi watakaa juu yao wakati wa baridi.
7 Wakati huo Bwana wa majeshi ataletewa hedaya na watu warefu, laini; Watu watishao tangu mwanzo wao hata sasa; Taifa la wenye nguvu, wakanyagao watu, Ambao mito inakata nchi yao; mpaka mahali pa jina la Bwana wa majeshi,mlima Sayuni.

Isaya 19


1 Ufunuo juu ya Misri. Tazama, Bwana amepanda juu ya wingu jepesi, anafika Misri; na sanamu za Misri zinatikisika mbele zake, na moyo wa Misri unayeyuka ndani yake.
2 Nami nitawaamsha Wamisri juu ya Wamisri; nao watapigana, kila mtu na ndugu yake, na kila mtu na jirani yake, mji juu ya mji, na ufalme juu ya ufalme.
3 Na roho ya Misri itamwagika kabisa katikati yake, nami nitayabatilisha mashauri yake, nao watakwenda kwa sanamu zao, na kwa waganga, na kwa wapiga ramli, na kwa wachawi.
4 Nami nitawatoa hao Wamisri na kuwatia katika mikono ya bwana mgumu; na mfalme mkali atawatawala; asema Bwana, Bwana wa majeshi.
5 Na maji ya baharini yatapunguka, na huo mto utakauka na kuwa pakavu.
6 Na vijito vya mto vitatoa uvundo, na mifereji ya Misri itakuwa haina maji mengi, itakauka; manyasi na mianzi itanyauka.
7 Vitu vimeavyo karibu na Nile, katika ukingo wa Nile, na vyote vilivyopandwa karibu na Nile vitakauka na kuondolewa na kutoweka.
8 Na wavuvi wataugua, na wote wavuao kwa ndoana watahuzunika, nao watandao jarife juu ya maji watazimia.
9 Tena wao wafanyao kazi ya kuchana kitani watafadhaika, na hao pia wafumao bafta.
10 Na nguzo za nchi zitavunjika vipande vipande, wote wafanyao kazi ya mshahara watahuzunika nafsini mwao.
11 Wakuu wa Soani wamekuwa wapumbavu kabisa; washauri wenye hekima wa Farao, shauri lao limepumbazika; mwawezaje kumwambia Farao, Mimi ni mwana wa wenye hekima, ni mwana wa wafalme wa zamani?
12 Wako wapi, basi, watu wako wenye hekima? Na wakuambie sasa; na wajue mambo aliyokusudia Bwana wa majeshi juu ya Misri.
13 Wakuu wa Soani wamekuwa wapumbavu, wakuu wa Nofu wamedanganyika; na hao walio mawe ya pembeni ya kabila zake wameikosesha Misri.
14 Yeye Bwana ametia roho ya ushupavu katika moyo wa Misri, nao wameikosesha Misri katika matendo yake yote, kama mlevi aendavyo huko na huko akitapika.
15 Wala haitakuwako kazi yo yote katika Misri iwezayo kufanywa, ya kichwa au ya mkia, ya tawi au ya nyasi.
16 Katika siku hiyo Misri itakuwa kama wanawake; itatetemeka na kuogopa kwa sababu ya kutikiswa kwa mkono wa Bwana wa majeshi, autikisao juu yake.
17 Na nchi ya Yuda itakuwa sababu ya utisho kwa Misri; kila mtu atakayeambiwa habari zake ataingiwa na woga, kwa sababu ya kusudi la Bwana wa majeshi, analolikusudia juu yake.
18 Katika siku hiyo itakuwako miji mitano katika nchi ya Misri itumiayo lugha ya Kanaani, na kumwapia Bwana wa majeshi; mji mmoja utaitwa Mji wa uharibifu.
19 Katika siku hiyo itakuwako madhabahu katika nchi ya Misri kwa Bwana, na nguzo mpakani mwake kwa Bwana.
20 Nayo itakuwa ishara na ushuhuda kwa Bwana wa majeshi katika nchi ya Misri; kwa maana watamlilia Bwana kwa sababu ya watu wawaoneao, naye atawapelekea mwokozi mwenye kuwatetea, naye atawaokoa.
21 Na Bwana atajulikana na Misri, na Wamisri watamjua Bwana katika siku hiyo; naam watamtumikia kwa dhabihu na matoleo, nao watamwekea Bwana nadhiri, na kuzitekeleza.
22 Naye Bwana atapiga Misri, akipiga na kuponya; nao wakirudi kwa Bwana, atakubali maombi yao na kuwaponya.
23 Katika siku hiyo itakuwako njia kuu itokayo Misri na kufika hata Ashuru; Mwashuri atafika Misri, na Mmisri atafika Ashuru, na Wamisri wataabudu pamoja na Waashuri.
24 Katika siku hiyo Israeli atakuwa wa tatu pamoja na Misri na Ashuru, watakuwa baraka kati ya dunia;
25 kwa kuwa Bwana wa majeshi amewabariki, akisema, Wabarikiwe watu wangu Misri; na wewe Ashuru, kazi ya mikono yangu; na wewe Israeli, urithi wangu.

Isaya 20


1 Katika mwaka ule jemadari Yule alipofika Ashdodi,alipotumwa na Sargoni mfalme wa Ashuru;naye alipigana na Ashdodi akautwaa.
2 wakati huo Bwana alinena kwa kinywa cha Isaya, mwana wa Amozi, akisema, Haya, uvue nguo ya magunia viunoni mwako, na viatu vyako miguuni mwako.
3 Naye akafanya hivyo akaenda uchi, miguu yake haina viatu. Bwana akasema, Kama vile mtumishi wangu Isaya anavyokwenda uchi, hana viatu, awe ishara na ajabu kwa muda wa miaka mitatu juu ya Misri na juu ya Kushi;
4 vivyo hivyo mfalme wa Ashuru atawachukua uchi, wafungwa wa Misri, na watu wa Kushi waliohamishwa, watoto kwa wazee, hawana viatu, matako yao wazi, Misri iaibishwe.
5 Nao watafadhaika, na kuona haya kwa ajili ya Kushi, matumaini yao, na Misri, utukufu wao.
6 Na mwenyeji wa nchi ya pwani atasema katika siku hiyo, Angalia, haya ndiyo yaliyowapata watu wale tuliowatumaini, ambao tuliwakimbilia watuokoe na mfalme wa Ashuru; na sisi je! Twawezaje kupona?

Isaya 21


1 Ufunuo juu ya bara ya bahari. Kama tufani za Negebu zikaribiavyo kwa kasi,inakuja kutoka bara,toka nchi itishayo.
2 Nimeonyeshwa maono magumu; atendaye hila anatenda hila, mharibu anaharibu. Panda juu, Ee Elamu; husuru, Ee Umedi; mimi ninakomesha maombolezo yake yote.
3 Kwa sababu hiyo viuno vyangu vimejaa maumivu, utungu umenishika, kama utungu wa mwanamke azaaye; ninaumwa sana, nisiweze kusikia; nimefadhaishwa wa hofu, nisiweze kuona.
4 Moyo wangu unapiga-piga, utisho umenitaabisha, gizagiza la jioni nilipendalo limegeuka likanitetemesha.
5 Wanaandika meza, wanaweka ulinzi, wanakula, wanakunywa. Simameni, enyi wakuu, itieni ngao mafuta.
6 Maana Bwana ameniambia hivi, Enenda, weka mlinzi; aonayo na ayatangaze.
7 Naye akiona kundi la wapanda farasi, wakienda wawili wawili, na kundi la punda, na kundi la ngamia; asikilize sana, akijitahidi kusikiliza.
8 Ndipo akalia kama simba, Ee Bwana, mimi nasimama daima juu ya mnara wakati wa mchana, na kila usiku ninakaa katika zamu ya ulinzi wangu.
9 Na, tazama, linakuja kundi la watu, wapanda farasi, wakienda wawili wawili. Akajibu na kusema, Babeli umeanguka, umeanguka; na sanamu zote za miungu yake zimevunjwa chini.
10 Ewe niliyekufikicha, na nafaka ya sakafu yangu; Hayo niliyoyasikia kwa Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, nimewapasha habari zake.
11 Ufunuo juu ya Duma. Mtu ananililia toka Seiri, Ee mlinzi, habari gani za usiku? Ee mlinzi, habari gani za usiku?
12 Mlinzi akasema, Mchana unakuja na usiku pia; mkitaka kuuliza, ulizeni; njoni tena.
13 Ufunuo juu ya Arabuni. Ndani ya msitu wa Arabuni mtalala, Enyi misafara ya Wadedani.
14 Waleteeni wenye kiu maji, Enyi wenyeji wa nchi ya Tema; Nendeni kuwalaki wakimbiao na chakula chao.
15 Kwa maana wanakimbia mbele ya panga, Upanga uliofutwa, na upinde uliopindwa, Na mbele ya ukali wa vita.
16 Kwa sababu Bwana ameniambia hivi, Katika muda wa mwaka, kama miaka ya mtu mwenye kuajiriwa, utaangamia utukufu wote wa Kedari.
17 Na mabaki ya hesabu ya wavuta pinde, hao mashujaa wa Kedari watakuwa wachache; maana Bwana, Mungu wa Israeli, amenena neno hili.

Isaya 22


1 Ufunuo juu ya bonde la maono. Sasa una nini, wewe, Hata umepanda pia juu ya dari za nyumba?
2 Ewe uliyejaa makelele, Mji wa ghasia, mji wenye furaha; Watu wako waliouawa hawakuuawa kwa upanga, Wala hawakufa vitani.
3 Wakuu wako wote wamekimbia pamoja, Wamefungwa wasiutumie upinde. Wote walioonekana wamefungwa pamoja, Wamekimbia mbali sana.
4 Kwa sababu hiyo nasema, Geuza uso wako usinitazame, nipate kulia kwa uchungu; usijishughulishe kunifariji, kwa ajili ya kuharibika kwake binti ya watu wangu.
5 Kwa maana siku ya kutaabika, siku ya kukanyagwa, siku ya fujo inakuja, itokayo kwa Bwana, Bwana wa majeshi, katika bonde la Maono; inabomoa kuta; na kuililia milima.
6 Na Elamu wameshika podo, pamoja na magari ya vita, na watu wenye kupanda farasi; na Kiri wameifunua ngao.
7 Hata ikawa mabonde yako mateule yamejaa magari ya vita, nao wapandao farasi wamejipanga wakielekea malango.
8 Kisha alikiondoa kifuniko cha Yuda, nawe siku hiyo ulivitazama vyombo vya vita katika nyumba ya mwituni.
9 Nanyi mlipaona mahali palipobomoka katika mji wa Daudi ya kuwa ni pengi, nanyi mliyakusanya maji ya birika la chini.
10 Nanyi mlizihesabu nyumba za Yerusalemu, mkazibomoa nyumba ili kuutia nguvu ukuta.
11 Nanyi mlifanya birika la maji katikati ya kuta mbili, la kuwekea maji ya birika la kale; lakini hamkumwangalia yeye aliyeyafanya hayo, wala kumjali yeye aliyeyatengeneza zamani.
12 Siku hiyo Bwana, Bwana wa majeshi, akawaita watu walie na kuomboleza, na kung'oa nywele zao, na kuvaa nguo za magunia;
13 na kumbe! Furaha, na kuchekelea, na kuchinja ng'ombe, na kuchinja kondoo, na kula nyama, na kunywa mvinyo; tule, tunywe, kwa maana kesho tutakufa.
14 Na yeye Bwana wa majeshi akafunua haya masikioni mwangu, Ni kweli, uovu huu hautatakaswa wala kuwatokeni hata mfe; asema Bwana, Bwana wa majeshi.
15 Bwana, Bwana wa majeshi, asema hivi, Haya! Enenda kwa huyu mtunza hazina, yaani, Shebna, aliye juu ya nyumba, ukamwambie,
16 Unafanyaje hapa? Nawe una nani hapa? Hata ukachimba kaburi hapa; ukamchimbia kaburi huko juu, na kumchongea makao katika jabali!
17 Tazama, Bwana atakutupa kwa nguvu, kama mtu mwenye nguvu; naam, atakuzonga-zonga.
18 Hakika atakukunja na kukutupa kama mpira, mpaka nchi iliyo mbali; huko utakufa, na magari ya utukufu wako yatakuwa kuko huko, ewe uliye aibu ya nyumba ya bwana wako.
19 Nami nitakusukuma na kukutoa katika mahali pako, naye atakushusha utoke hapa usimamapo.
20 Na itakuwa katika siku ile nitamwita mtumishi wangu Eliakimu, mwana wa Hilkia;
21 nami nitamvika vazi lako, nitamtia nguvu kwa mshipi wako, nami nitamkabidhi yeye mamlaka yako; naye atakuwa baba kwa wenyeji wa Yerusalemu, na kwa nyumba ya Yuda.
22 Na ufunguo wa nyumba ya Daudi nitauweka begani mwake; yeye atafungua wala hapana atakayefunga; naye atafunga wala hapana atakayefungua.
23 Nami nitamkaza kama msumari mahali palipo imara; naye atakuwa kiti cha utukufu kwa nyumba ya baba yake.
24 Nao wataangika juu yake utukufu wote wa nyumba ya baba yake; wazao wake na watoto wao, kila chombo kidogo tangu vyombo vya vikombe hata vyombo vya makopo vyote pia.
25 Katika siku ile, asema Bwana wa majeshi, ule msumari uliokazwa katika mahali palipo imara utalegea; nao utakatwa na kuanguka chini, na ule mzigo uliokuwa juu yake utakatiliwa mbali; maana Bwana amesema haya.

Isaya 23


1 Ufunuo juu ya Tiro. Toeni sauti za uchungu, enyi merikebu za Tarshishi, kwa maana umeharibika kabisa, hata hapana nyumba, hapana mahali pa kuingia; toka nchi ya Kitimu wamefunuliwa habari.
2 Tulieni, enyi mkaao kisiwani; wewe ambaye wafanya biashara wa Sidoni, wavukao bahari, walikujaza.
3 Vitu vilivyopandwa, vya Shihori, mavuno ya Nile, yaliyokuja juu ya maji mengi, ndiyo pato lake, naye alikuwa soko la mataifa.
4 Tahayari, Ee Sidoni; kwa maana bahari imenena, hiyo ngome ya bahari ilisema, Sikuona utungu, wala sikuzaa, wala sikulea vijana, wala sikulea wanawali.
5 Habari itakapofika Misri wataona uchungu sana kwa sababu ya habari ya Tiro.
6 Piteni mpaka Tarshishi, enyi mkaao kisiwani, toeni sauti ya uchungu.
7 Je! Huu ndio mji wenu wa furaha, ambao mwanzo wake ulikuwako tangu siku za kale, ambao miguu yake ilimchukua akae mbali sana?
8 Ni nani aliyefanya shauri hili juu ya Tiro, uliotia watu taji, ambao wafanya biashara wake walikuwa wana wa wafalme, na wachuuzi wake ni watu wakuu wa dunia?
9 Bwana wa majeshi ndiye aliyefanya shauri hili, ili kuharibu kiburi cha utukufu wote, na kuwaaibisha watu wa duniani wote pia.
10 Pita katika nchi yako, kama Nile, Ee binti wa Tarshishi, hapana tena mshipi wa kukuzuia.
11 Amenyosha mkono wake juu ya bahari, amezitikisa falme; Bwana ametoa amri katika habari za Kanaani, kuziangamiza ngome zake.
12 Naye akasema, Usizidi kufurahi, ewe bikira uliyeaibishwa, binti wa Sidoni, haya, ondoka, uende hata Kitimu; huko nako hutapata raha.
13 Tazama, nchi ya Wakaldayo; watu hao hawako tena; Mwashuri ameiweka tayari kwa hayawani wa jangwani; wamesimamisha buruji zao za vita, wameyaharibu majumba yake ya enzi, akaufanya kuwa uharibifu.
14 Pigeni yowe, enyi merikebu za Tarshishi; maana ngome yenu imefanywa ukiwa.
15 Basi, itakuwa katika siku ile, Tiro utasahauliwa miaka sabini, kadiri ya siku za mfalme mmoja; hata mwisho wa miaka sabini, Tiro utakuwa kama vile ulivyo wimbo wa kahaba.
16 Twaa kinubi, tembea mjini, Ewe kahaba uliyesahauliwa; Piga vizuri, imba nyimbo nyingi, Upate kukumbukwa tena.
17 Hata itakuwa mwisho wa miaka sabini, Bwana ataizuru nchi ya Tiro, naye atarudi apate ujira wake, atafanya ukahaba pamoja na falme zote za ulimwengu juu ya uso wa dunia.
18 Na biashara yake na ujira wake utakuwa wakfu kwa Bwana, hautawekwa hazinani wala hautawekwa akiba; bali mapato ya biashara yake yatakuwa mali zao wakaao mbele za Bwana, wapate kula na kushiba, na kuvaa mavazi ya fahari.

Isaya 24


1 Tazama, Bwana ameifanya dunia kuwa tupu, aifanya ukiwa, aipindua, na kuwatawanya wakaao ndani yake.
2 Na itakuwa kama ilivyo hali ya watu, ndivyo itakavyokuwa hali ya kuhani; kama ilivyo hali ya mtumwa, ndivyo itakavyokuwa hali ya bwana wake; kama ilivyo hali ya mjakazi, ndivyo itakavyokuwa hali ya bibi yake; kama ilivyo hali yake anunuaye, ndivyo itakavyokuwa hali yake auzaye; kama ilivyo hali yake akopeshaye, ndivyo itakavyokuwa hali yake akopaye; kama ilivyo hali yake atwaaye faida, ndivyo itakavyokuwa hali yake ampaye faida.
3 Dunia hii itafanywa tupu kabisa, na kuharibiwa kabisa; maana Bwana amenena neno hilo.
4 Dunia inaomboleza, inazimia; ulimwengu unadhoofika, unazimia; watu wakuu wa dunia wanadhoofika.
5 Tena dunia imetiwa unajisi kwa watu wanaoikaa; kwa maana wameziasi sheria, wameibadili amri, wamelivunja agano la milele.
6 Ndiyo sababu laana imeila dunia hii, na hao wanaoikaa wameonekana kuwa na hatia, ndiyo sababu watu wanaoikaa dunia wameteketea, watu waliosalia wakawa wachache tu.
7 Divai mpya inaomboleza, mzabibu umedhoofika, watu wote waliochangamka moyo wanaugua.
8 Sauti ya furaha ya matoazi inakoma; kelele yao wafurahio imekwisha; furaha ya kinubi inakoma.
9 Hawatakunywa divai pamoja na nyimbo; kileo kitakuwa uchungu kwao wakinywao.
10 Mji wa machafuko umebomolewa; kila nyumba imefungwa, asipate kuingia mtu awaye yote.
11 Pana kilio katika njia kuu kwa sababu ya divai; furaha yote imetiwa giza, na changamko la nchi limetoweka.
12 Ndani ya mji umebaki ukiwa, na lango lake limepigwa kwa uharibifu.
13 Maana katikati ya dunia, katikati ya mataifa, itakuwa hivi; kama wakati utikiswapo mzeituni, kama wakati waokotapo zabibu baada ya mavuno yake.
14 Hawa watainua sauti zao, watapiga kelele; kwa sababu ya utukufu wa Bwana watapiga kelele toka baharini.
15 Basi, mtukuzeni Bwana katika mashariki, litukuzeni jina la Bwana, Mungu wa Israeli, katika visiwa vya bahari.
16 Toka pande za mwisho wa dunia tumesikia nyimbo, Atukuzwe mwenye haki. Ndipo niliposema, Kukonda kwangu! Kukonda kwangu! Ole wangu! Watenda hila wametenda hila, naam, watendao hila wametenda hila sana.
17 Hofu, na shimo, na mtego, vi juu yako, Ee mwenye kukaa duniani.
18 Itakuwa kila akimbiaye sauti ya hofu ataanguka katika shimo; na kila apandaye na kutoka shimoni atanaswa na mtego; kwa maana madirisha yaliyo juu yamewekwa wazi, na misingi ya dunia inatikisika.
19 Dunia kuvunjika, inavunjika sana; dunia kupasuka, imepasuka sana; dunia kutikisika, imetikisika sana.
20 Dunia inalewa-lewa kama mlevi, nayo inawaya-waya kama machela; na mzigo wa dhambi zake utailemea; nayo itaanguka, wala haitainuka tena.
21 Tena itakuwa katika siku hiyo, Bwana ataliadhibu jeshi la mahali palipo juu katika mahali palipo juu, na wafalme wa dunia katika dunia;
22 nao watakusanywa pamoja kama vile wakusanywavyo wafungwa katika shimo nao watafungwa katika gereza; na baada ya muda wa siku nyingi watajiliwa.
23 Ndipo mwezi utatahayari, na jua litaona haya; kwa kuwa Bwana wa majeshi atatawala katika mlima wa Sayuni, na katika Yerusalemu, na mbele ya wazee wake kwa utukufu.

Isaya 25


1 Ee Bwana, wewe u Mungu wangu; Nitakutukuza na kulihimidi jina lako; Kwa kuwa umetenda mambo ya ajabu, Mashauri ya kale, kwa uaminifu na kweli.
2 Kwa sababu umefanya mji kuwa ni chungu; Mji wenye boma kuwa ni magofu; Jumba la wageni kuwa si mji; Hautajengwa tena milele.
3 Kwa hiyo watu walio hodari watakutukuza, Mji wa mataifa watishao utakuogopa.
4 Maana umekuwa ngome ya maskini, Ngome ya mhitaji katika dhiki yake, Mahali pa kukimbilia wakati wa tufani, Kivuli wakati wa hari; Wakati uvumapo upepo wa watu watishao, Kama dhoruba ipigayo ukuta.
5 Kama vile hari katika mahali pakavu Utaushusha mshindo wa wageni; Kama ilivyo hari kwa kivuli cha wingu, Wimbo wa hao watishao utashushwa.
6 Na katika mlima huu Bwana wa majeshi atawafanyia mataifa yote karamu ya vitu vinono, karamu ya divai iliyokaa juu ya urojorojo wake, karamu ya vinono vilivyojaa mafuta, karamu ya divai iliyokaa juu ya urojorojo wake, iliyochujwa sana.
7 Naye katika mlima huu atauharibu uso wa sitara iliyowekwa juu ya watu wote, na utaji ule uliotandwa juu ya mataifa yote.
8 Amemeza mauti hata milele; na Bwana MUNGU atafuta machozi katika nyuso zote; na aibu ya watu wake ataiondoa katika ulimwengu wote; maana Bwana amenena hayo.
9 Katika siku hiyo watasema, Tazama, huyu ndiye Mungu wetu, Ndiye tuliyemngoja atusaidie; Huyu ndiye Bwana tuliyemngoja, Na tushangilie na kuufurahia wokovu wake.
10 Kwa maana mkono wa Bwana utatulia katika mlima huu, na Moabu atakanyagwa chini huko aliko, kama vile majani makavu yakanyagwavyo katika maji ya jaa.
11 Naye atanyosha mikono yake katikati yake, kama vile aogeleaye anyoshavyo mikono yake ili aogelee, naye atashusha kiburi chake, pamoja na hila za mikono yake.
12 Na boma la ngome ya kuta zako ameliinamisha, na kulilaza chini, na kulitupa chini hata mavumbini.

Isaya 26


1 Siku ile wimbo huu utaimbwa katika nchi ya Yuda; Sisi tunao mji ulio na nguvu; Ataamuru wokovu kuwa kuta na maboma.
2 Wekeni wazi malango yake, Taifa lenye haki, lishikalo kweli, liingie.
3 Utamlinda yeye ambaye moyo wake umekutegemea Katika amani kamilifu, kwa kuwa anakutumaini.
4 Mtumainini Bwana siku zote Maana Bwana YEHOVA ni mwamba wa milele.
5 Kwa kuwa amewashusha wakaao juu, Mji ule ulioinuka, aushusha, Aushusha hata nchi, auleta hata mavumbini.
6 Mguu utaukanyaga chini, Naam, miguu yao walio maskini, Na hatua zao walio wahitaji.
7 Njia yake mwenye haki ni unyofu; Wewe uliye mnyofu wainyosha njia ya mwenye haki.
8 Naam, katika njia ya hukumu zako Sisi tumekungoja, Ee Bwana; Shauku ya nafsi zetu inaelekea Jina lako na ukumbusho wako.
9 Kwa nafsi yangu nimekutamani wakati wa usiku; Naam, kwa nafsi yangu ndani yangu nitakutafuta mapema; Maana hukumu zako zikiwapo duniani, Watu wakaao duniani hujifunza haki.
10 Mtu mbaya ajapofadhiliwa, Hata hivyo hatajifunza haki; Katika nchi ya unyofu atatenda udhalimu, Wala hatauona utukufu wa Bwana.
11 Bwana, mkono wako umeinuliwa, lakini hawaoni; lakini watauona wivu wako kwa ajili ya watu wako, nao watatahayari; naam, moto utawala adui zako.
12 Bwana, utatuamuria amani; maana ni wewe pia uliyetutendea kazi zetu zote.
13 Ee Bwana, Mungu wetu, mabwana wengine zaidi ya wewe wametumiliki; lakini kwa msaada wako peke yako tutalitaja jina lako.
14 Wao wamekufa, hawataishi; wamekwisha kufariki, hawatafufuka; kwa sababu hiyo umewajilia, na kuwaangamiza, na kuupoteza ukumbusho wao.
15 Umeliongeza hilo taifa, Bwana, umeliongeza taifa; wewe umetukuzwa, umeipanua mipaka yote ya nchi hii.
16 Bwana, katika taabu zao walikwenda kwako; waliomba maombi mengi wakati adhabu yako ilipokuwa juu yao.
17 Kama vile mwanamke mwenye mimba anayekaribia wakati wake wa kuzaa, alivyo na utungu na kulia kwa sababu ya maumivu yake, ndivyo tulivyokuwa sisi mbele zako, Ee Bwana.
18 Tumekuwa na mimba, tumekuwa na utungu, tumekuwa kana kwamba tumezaa upepo; hatukufanya wokovu wo wote duniani, wala hawakuanguka wakaao duniani.
19 Wafu wako wataishi, maiti zangu zitafufuka; amkeni, kaimbeni, ninyi mnaokaa mavumbini, kwa maana umande wako ni kama umande wa mimea, nayo ardhi itawatoa waliokufa.
20 Njoni, watu wangu, ingia wewe ndani ya vyumba vyako, ukafunge mlango nyuma yako ujifiche kitambo kidogo, mpaka ghadhabu hii itakapopita.
21 Kwa maana, tazama, Bwana anakuja kutoka mahali pake, ili kuwaadhibu wakaao duniani, kwa sababu ya uovu wao; ardhi nayo itafunua damu yake, wala haitawafunika tena watu wake waliouawa.

Isaya 27


1 Katika siku hiyo Bwana, kwa upanga wake ulio mkali, ulio mkubwa, ulio na nguvu, atamwadhibu lewiathani, nyoka yule mwepesi, na lewiathani, nyoka yule mwenye kuzonga-zonga; naye atamwua yule joka aliye baharini.
2 Katika siku hiyo; Shamba la mizabibu la mvinyo, liimbieni.
3 Mimi, Bwana, nalilinda, Nitalitia maji kila dakika, Asije mtu akaliharibu; Usiku na mchana nitalilinda.
4 Hasira sinayo ndani yangu; Kama mibigili na miiba ingekuwa mbele zangu, Ningepanga vita juu yake, Ningeiteketeza yote pamoja.
5 Au azishike nguvu zangu, Afanye amani nami; Naam, afanye amani nami.
6 Siku zijazo Yakobo atatia mizizi; Israeli atatoa maua na kuchipuka; Nao watajaza uso wa ulimwengu matunda.
7 Je! Amempiga kama hilo pigo la hao waliompiga, au ameuawa kama walivyouawa wao waliouawa na yeye?
8 Umemwadhibu kwa kiasi, ulipomfukuza; ukampepeta kwa upepo mkali katika siku ya upepo wa mashariki.
9 Basi, uovu wa Yakobo utatakaswa hivyo, na hayo ndiyo matunda yote ya kumwondolea dhambi yake; afanyapo mawe yote ya madhabahu kuwa kama mawe ya chokaa yaliyopondwa, hata maashera na sanamu za jua havitasimama tena.
10 Kwa maana mji ulio na boma umekuwa peke yake, makao yaliyoachwa na ukiwa kama jangwa; huko ndiko atakakolisha ndama, na huko ndiko atakakolala, na kuyala matawi yake.
11 Matawi yake yatakapokauka yatavunjwa; wanawake watakuja na kuyachoma moto; kwa maana hawa si watu wenye akili; kwa sababu hiyo yeye aliyewaumba hatawahurumia, yeye aliyewafanya hatawasamehe.
12 Tena itakuwa katika siku hiyo, Bwana atayapiga-piga matunda yake toka gharika ya Mto hata kijito cha Misri, nanyi mtakusanywa mmoja mmoja, enyi wana wa Israeli.
13 Tena itakuwa katika siku hiyo, tarumbeta kubwa itapigwa, nao waliokuwa karibu na kuangamia katika nchi ya Ashuru watakuja; na hao waliotupwa katika nchi ya Misri; nao watamsujudu Bwana katika mlima mtakatifu huko Yerusalemu.

Isaya 28


1 Ole wa taji ya kiburi ya walevi wa Efraimu, na ua la uzuri wa fahari yake linalonyauka, lililo kichwani mwa bonde linalositawi, la hao walioshindwa na divai!
2 Tazama, Bwana ana mmoja aliye hodari, mwenye nguvu; kama dhoruba ya mvua ya mawe, tufani iharibuyo, kama dhoruba ya maji mengi yafurikayo, ndivyo atakavyotupa chini kwa mkono.
3 Taji ya kiburi ya walevi wa Efraimu itakanyagwa kwa miguu;
4 na ua la uzuri wa fahari yake linalonyauka, lililo kichwani mwa bonde linalositawi, litakuwa kama tini iliyotangulia kuiva kabla ya wakati wa hari, ambayo, aionapo yeye aiangaliaye, huila mara anapoishika mkononi mwake.
5 Katika siku ile Bwana wa majeshi atakuwa ni taji ya fahari, na kilemba cha uzuri, kwa mabaki ya watu wake.
6 Naye atakuwa roho ya hukumu kwake yeye aketiye ili ahukumu; naye atakuwa nguvu kwao wageuzao nyuma vita langoni.
7 Lakini hawa nao wamekosa kwa divai, wamepotea kwa kileo; kuhani na nabii wamekosa kwa kileo, wamemezwa kwa divai, wamepotea kwa kileo; hukosa katika maono, hujikwaa katika hukumu.
8 Maana meza zote zimejaa matapiko na uchafu, hapana mahali palipo safi.
9 Atamfundisha nani maarifa? Atamfahamisha nani habari hii? Je! Ni wale walioachishwa maziwa, walioondolewa matitini?
10 Kwa maana ni amri juu ya amri, amri juu ya amri; kanuni juu ya kanuni, kanuni juu ya kanuni; huku kidogo na huku kidogo.
11 La, bali kwa midomo ya watu wageni, na kwa lugha nyingine atasema na watu hawa;
12 ambao aliwaambia, Hii ndiyo raha yenu, mpeni raha yeye aliyechoka; huku ndiko kuburudika; lakini hawakutaka kusikia.
13 Kwa sababu hiyo neno la Bwana kwao litakuwa hivi, amri juu ya amri, amri juu ya amri; kanuni juu ya kanuni, kanuni juu ya kanuni; huku kidogo na huku kidogo; ili waende na kuanguka nyuma, na kuvunjwa, na kunaswa, na kuchukuliwa.
14 Basi, lisikieni neno la Bwana, enyi watu wenye dharau, mnaowatawala watu hawa walio ndani ya Yerusalemu.
15 Kwa sababu mmesema, Tumefanya agano na mauti, tumepatana na kuzimu; pigo lifurikalo litakapopita, halitatufikia sisi; kwa maana tumefanya maneno ya uongo kuwa kimbilio letu, tumejificha chini ya maneno yasiyo kweli;
16 kwa ajili ya hayo Bwana, MUNGU, asema hivi, Tazama, naweka jiwe katika Sayuni, liwe msingi, jiwe lililojaribiwa, jiwe la pembeni lenye thamani, msingi ulio imara; yeye aaminiye hatafanya haraka.
17 Nami nitafanya hukumu kuwa ndiyo kanuni, na haki kuwa ndiyo timazi; na mvua ya mawe itachukulia mbali hilo kimbilio la maneno ya uongo, na maji yatapagharikisha mahali pa kujisitiri.
18 Na agano lenu mliloagana na mauti litabatilika, tena mapatano yenu mliyopatana na kuzimu hayatasimama; pigo lifurikalo litakapopita, ndipo ninyi mtakapokanyagwa nalo.
19 Kila wakati litakapopita litawachukueni. Maana litapita asubuhi baada ya asubuhi, wakati wa mchana na wakati wa usiku; na kuifahamu habari ile kutakuwa kitisho tu.
20 Maana kitanda kile ni kifupi asiweze mtu kujinyosha juu yake, na nguo ile ya kujifunika ni nyembamba asipate mtu kujizingisha.
21 Maana Bwana ataondoka kama vile katika mlima Perasimu, ataghadhibika kama vile katika bonde la Gibeoni; apate kufanya kazi yake, kazi yake ya ajabu; na kulitimiza tendo lake, tendo lake la ajabu.
22 Basi sasa msiwe watu wenye kudharau, vifungo vyenu msije vikakazwa; maana nimesikia kwa Bwana, Bwana wa majeshi, habari ya hukumu itakayotimizwa, nayo imekusudiwa, itakayoipata dunia yote pia.
23 Tegeni masikio, sikieni sauti yangu, sikilizeni mkasikie neno langu.
24 Je! Mwenye kulima alima daima, ili apande? Afunua daima madongoa ya nchi yake, na kuyavunja?
25 Akiisha kuulainisha uso wa nchi yake, je! Hamwagi huko na huko kunde, na kutupa-tupa jira, na kuitia ngano safu safu, na shayiri mahali pake palipochaguliwa, na kusemethi karibu na mipaka yake?
26 Kwa maana Mungu wake anamwagiza vizuri na kumfundisha.
27 Kwa maana kunde zile hazipurwi kwa chombo kikali, wala gurudumu la gari halipitishwi huko na huko juu ya jira ile, bali kunde zile hupurwa kwa fimbo, na jira ile kwa ufito.
28 Ngano ya mkate husagwa; kwa maana haipuri siku zote bila kukoma; na ingawa gurudumu la gari lake na farasi wake huitawanya ngano ile, haisagi.
29 Hayo nayo yatoka kwa Bwana wa majeshi, mwenye shauri la ajabu, apitaye wote kwa hekima yake.

Isaya 29


1 Ole wa Arieli, Arieli, mji ambao Daudi alifanya kituo chake ndani yake; ongezeni mwaka baada ya mwaka; sikukuu na zirudi wakati wake,
2 ndipo nitamwudhi Arieli; kutakuwapo maombolezo na kilio; naye atakuwa kwangu kama Arieli.
3 Nami nitapiga kimo juu yako pande zote, nitakuhusuru kwa ngome, nami nitajenga maboma yakuzunguke.
4 Nawe utashushwa, nawe utanena toka chini ya nchi, na maneno yako yatakuwa chini toka mavumbini; na sauti yako itakuwa kama sauti ya mtu mwenye pepo, ikitoka katika nchi, na matamko yako yatanong'ona toka mavumbini.
5 Lakini wingi wa adui zako utakuwa kama mavumbi membamba, na wingi wao watishao utakuwa kama makapi yapitayo; naam, itakuwa mara na kwa ghafula.
6 Naye atajiliwa na Bwana wa majeshi kwa ngurumo, na tetemeko la nchi, na sauti kuu, na chamchela, na tufani, na mwali wa moto uteketezao.
7 Na wingi wa mataifa wapiganao na Arieli, wote wapiganao naye na ngome yake, nao wamwudhio, watakuwa kama ndoto, na maono ya usiku.
8 Tena itakuwa kama mtu mwenye njaa aotapo, kumbe, anakula; lakini aamkapo, nafsi yake haina kitu; na kama mtu mwenye kiu aotapo, kumbe, anakunywa; lakini aamkapo, kumbe, anazimia, na nafsi yake inatamani; hivyo ndivyo utakavyokuwa huo wingi wa mataifa waletao vita juu ya mlima Sayuni.
9 Ngojeni mstaajabu; fanyeni anasa zenu na kuwa vipofu; wamelewa wala si kwa mvinyo; wamewaya-waya wala si kwa sababu ya kileo.
10 Kwa maana Bwana amewamwagieni roho ya usingizi, amefumba macho yenu, yaani, manabii; amefunika vichwa vyenu, yaani, waonaji.
11 Na maono yote yamekuwa kwenu kama maneno ya chuo kilichotiwa muhuri, ambacho watu humpa mtu aliye na maarifa, wakisema, Tafadhali ukisome hiki; akasema, Siwezi, kwa kuwa kimetiwa muhuri;
12 kisha chuo hiki apewa mtu asiye na maarifa, akaambiwa, Kisome hicho tafadhali, akasema, Sina maarifa mimi.
13 Bwana akanena, Kwa kuwa watu hawa hunikaribia na kuniheshimu kwa vinywa vyao, bali mioyo yao wamefarakana nami, na kicho chao walicho nacho kwangu ni maagizo ya wanadamu waliyofundishwa;
14 kwa sababu hiyo mimi nitafanya tena kazi ya ajabu kati ya watu hawa, kazi ya ajabu na mwujiza; na akili za watu wao wenye akili zitapotea, na ufahamu wa wenye busara wao utafichwa.
15 Ole wao wanaojitahidi kumficha Bwana mashauri yao, na matendo yao yamo gizani, nao husema, Ni nani atuonaye? Nani atujuaye?
16 Ninyi mnapindua mambo; Je! Mfinyanzi ahesabiwe kuwa kama udongo; kitu kilichofinyangwa kimnene yeye aliyekifinyanga, Hakunifinyanga huyu; au kitu kilichoumbwa kimnene yeye aliyekiumba, Yeye hana ufahamu?
17 Je! Si muda mdogo uliobaki, na Lebanoni itageuzwa kuwa shamba lizaalo sana, na lile shamba lizaalo sana litahesabiwa kuwa msitu?
18 Na katika siku hiyo viziwi watasikia maneno ya hicho chuo, na macho ya vipofu yataona katika upofu na katika giza.
19 Wanyenyekevu nao wataongeza furaha yao katika Bwana, na maskini katika wanadamu watafurahi katika Mtakatifu wa Israeli.
20 Kwa maana mwenye kutisha ameangamizwa, naye mwenye dharau amekoma, nao wote watazamiao uovu wamekatiliwa mbali;
21 hao wamfanyao mtu kuwa amekosa katika neno, na kumtegea mtego yeye aonyaye langoni, na kumgeuza mwenye haki kwa kitu kisichofaa.
22 Basi, Bwana aliyemkomboa Ibrahimu asema hivi, katika habari za nyumba ya Yakobo; Yakobo hatatahayarika sasa, wala uso wake hautabadilika rangi yake.
23 Bali atakapowaona watoto wake, walio kazi ya mikono yangu, katikati yake, wao watalitakasa jina langu; naam, watamtakasa Mtakatifu wa Yakobo, nao watamcha Mungu wa Israeli.
24 Hao nao wakosao rohoni mwao watapata kufahamu, na hao wanung'unikao watajifunza elimu.

Isaya 30


1 Ole wa watoto waasi; asema Bwana; watakao mashauri lakini hawayataki kwangu mimi; wajifunikao kifuniko lakini si cha roho yangu; wapate kuongeza dhambi juu ya dhambi;
2 waendao kutelemkia Misri wala hawakuuliza kinywani mwangu; ili wajitie nguvu kwa nguvu za Farao, na kutumainia kivuli cha Misri.
3 Basi, nguvu za Farao zitakuwa aibu yenu, na kutumainia kivuli cha Misri kutakuwa kufadhaika kwenu.
4 Kwa maana wakuu wake wako Soani, na wajumbe wake wamefika Hanesi.
5 Wote watawaonea haya watu wasioweza kuwafaidia, wasio na msaada wala faida, bali ni aibu na sababu ya kushutumiwa.
6 Ufunuo juu ya hayawani wa Negebu. Katikati ya nchi ya taabu na dhiki, Ambayo hutoka huko simba jike na simba, Nyoka na joka la moto arukaye, Huchukua mali zao mabegani mwa punda wachanga, Na hazina zao juu ya nundu za ngamia Waende kwa watu ambao hawatawafaa kitu.
7 Kwa maana Misri huwasaidia bure, bila faida; Kwa hiyo nimemwita, Rahabu aketiye kimya.
8 Haya, enenda sasa, andika neno hili katika kibao mbele ya macho yao, lichore katika kitabu ili liwe kwa ajili ya majira yatakayokuja, kwa ushuhuda hata milele.
9 Kwa maana watu hawa ni watu waasi, watoto wasemao uongo, watoto wasiotaka kuisikia sheria ya Bwana;
10 wawaambiao waonaji, Msione; na manabii, Msitoe unabii wa mambo ya haki, tuambieni maneno laini, hubirini maneno yadanganyayo;
11 tokeni katika njia, geukeni mtoke katika mapito; mkomesheni Mtakatifu wa Israeli mbele yetu.
12 Basi kwa ajili ya hayo Mtakatifu wa Israeli asema hivi, Kwa sababu mwalidharau neno hili, na kutumainia jeuri na ukaidi, na kuyategemea hayo;
13 basi, uovu huu utakuwa kwenu kama mahali palipobomoka, palipo tayari kuanguka patokezapo katika ukuta mrefu, ambapo kuvunjika kwake huja ghafula kwa mara moja.
14 Naye atapavunja kama chombo cha mfinyanzi kivunjwavyo, akikivunja-vunja asiache kukivunja, hata hakipatikani katika vipande vyake kigae kitoshacho kutwaa moto jikoni, au kuteka maji kisimani.
15 Kwa maana Bwana MUNGU, Mtakatifu wa Israeli, asema hivi, Kwa kurudi na kustarehe mtaokolewa; nguvu zenu zitakuwa katika kutulia na kutumaini; lakini hamkukubali.
16 Bali ninyi mlisema, La! Maana tutakimbia juu ya farasi; basi, ni kweli, mtakimbia; tena, Sisi tutakimbia juu ya wanyama waendao upesi; basi, wale watakaowafuatia watakuwa wepesi.
17 Elfu moja watakimbia kwa kukemewa na mtu mmoja; kwa kukemewa na watano mtakimbia; hata mtakapoachwa kama mlingoti juu ya kilele cha mlima, na kama bendera juu ya kilima.
18 Kwa ajili ya hayo Bwana atangoja, ili awaonee huruma, na kwa ajili ya hayo atatukuzwa, ili awarehemu; kwa maana Bwana ni Mungu wa hukumu; heri wote wamngojao.
19 Kwa maana watu watakaa katika Sayuni huko Yerusalemu; wewe hutalia tena; hakika yake atakuonea rehema nyingi kwa sauti ya kilio chako; asikiapo ndipo atakapokujibu.
20 Na ingawa Bwana atawapeni chakula cha shida na maji ya msiba, lakini waalimu wako hawatafichwa tena, ila macho yako yatawaona waalimu wako;
21 na masikio yako yatasikia neno nyuma yako, likisema, Njia ni hii, ifuateni; mgeukapo kwenda mkono wa kulia, na mgeukapo kwenda mkono wa kushoto.
22 Nanyi mtakitia najisi kifuniko cha sanamu zenu za fedha zilizochongwa, na mabamba ya sanamu zenu za dhahabu zilizoyeyushwa; utazitupilia mbali kama kitu kilicho najisi; utasema, Haya, toka hapa.
23 Naye atatoa mvua juu ya mbegu zako, upate kuipanda nchi hii; na mkate wa mazao ya nchi, nayo itasitawi na kuzaa tele; katika siku hiyo ng'ombe zako watakula katika malisho mapana.
24 Ng'ombe pia na wana-punda wailimao nchi watakula chakula kilichokolea, kilichopepetwa kwa ungo na kwa pepeo.
25 Na juu ya kila mlima mrefu, na juu ya kila kilima kilichoinuka, itakuwapo mito na vijito vya maji, katika siku ya machinjo makuu itakapoanguka minara.
26 Na tena nuru ya mwezi itakuwa kama nuru ya jua, na nuru ya jua itaongezeka mara saba, kama nuru ya siku saba, katika siku ile Bwana atakapofunga mapigo ya watu wake, na kuliponya pigo la jeraha yao.
27 Tazama, jina la Bwana linakuja kutoka mbali sana, linawaka kwa hasira yake, kwa moshi mwingi sana unaopaa juu; midomo yake imejaa ghadhabu, na ulimi wake ni moto ulao;
28 na pumzi yake ni kijito kifurikacho, kifikacho hata shingoni, kupepeta mataifa kwa ungo wa ubatili; na lijamu ikoseshayo itakuwa katika taya za watu.
29 Mtakuwa na wimbo kama vile wakati wa usiku, ishikwapo sikukuu takatifu, mtakuwa na furaha ya moyo kama vile mtu aendapo na filimbi katika mlima wa Bwana, aliye Mwamba wa Israeli.
30 Naye Bwana atawasikizisha watu sauti yake ya utukufu, naye atawaonyesha jinsi mkono wake ushukavyo, na ghadhabu ya hasira yake, na mwako wa moto ulao, pamoja na dhoruba, na tufani, na mvua ya mawe ya barafu.
31 Maana kwa sauti ya Bwana, Mwashuri atavunjika-vunjika, yeye apigaye kwa bakora.
32 Na kila pigo la fimbo iliyoamriwa, ambayo Bwana ataliweka juu yake, litakuwa pamoja na matari na vinanda, na kwa mapigano yenye kutikisa atapigana nao.
33 Maana Tofethi imewekwa tayari tokea zamani, naam, imewekwa tayari kwa mfalme huyo; ameifanya kubwa, inakwenda chini sana; tanuru yake ni moto na kuni nyingi; pumzi ya Bwana, kama mto wa kiberiti, huiwasha.

Isaya 31


1 Ole wao watelemkao kwenda Misri wapate msaada, na kutegemea farasi; watumainio magari kwa kuwa ni mengi, na wapanda farasi kwa kuwa ni hodari sana; lakini hawamwangalii Mtakatifu wa Israeli, wala hawamtafuti Bwana!
2 Lakini yeye naye ana akili, naye ataleta uovu, wala hatayatangua maneno yake; bali ataondoka juu ya nyumba yao watendao mabaya, na juu ya msaada wa hao watendao maovu.
3 Basi Wamisri ni wanadamu wala si Mungu, na farasi zao ni nyama wala si roho; na Bwana atakaponyosha mkono wake, yeye asaidiaye atajikwaa, na yeye asaidiwaye ataanguka, nao wote pamoja watakoma.
4 Maana Bwana aniambia hivi, Kama vile ilivyo simba angurumapo na mwana-simba juu ya mawindo yake, wachungaji wengi wakiitwa ili kumpiga, lakini hatiwi hofu na sauti zao, wala kufanya woga kwa sababu ya mshindo wao; ndivyo Bwana wa majeshi atakavyoshuka ili kufanya vita juu ya mlima Sayuni, na juu ya kilima chake.
5 Kama ndege warukao, Bwana wa majeshi ataulinda Yerusalemu; ataulinda na kuuokoa, atapita juu yake na kuuhifadhi.
6 Mwelekeeni yeye mliyemwasi sana, enyi wana wa Israeli.
7 Maana katika siku hiyo kila mtu atatupa sanamu zake za fedha, na sanamu zake za dhahabu, ambazo mikono yenu imezifanya, zikawa dhambi kwenu.
8 Ndipo huyo Mwashuri ataanguka kwa upanga ambao si wa mtu; na upanga usio upanga wa mtu utamla; naye ataukimbia upanga, na vijana wake watatoa kodi.
9 Na mwamba wake utatoweka kwa sababu ya hofu, nao wakuu wake wataionea bendera hofu kuu, asema Bwana, ambaye moto wake u katika Sayuni, na tanuru yake katika Yerusalemu.

Isaya 32


1 Tazama, mfalme atamiliki kwa haki, na wakuu watatawala kwa hukumu.
2 Na mwanadamu atakuwa kama mahali pa kujificha na upepo, na mahali pa kujisitiri na dhoruba; kama mito ya maji mahali pakavu, kama kivuli cha mwamba mkubwa katika nchi yenye uchovu.
3 Tena macho yao waonao hayatakuwa na kiwi, na masikio yao wasikiao yatasikiliza.
4 Tena moyo wa mtu mwenye hamaki utafahamu maarifa, na ndimi zao wenye kigugumizi zitakuwa tayari kunena sawasawa.
5 Mpumbavu hataitwa tena mwungwana, wala ayari hatasemwa kwamba ni karimu.
6 Maana mpumbavu atanena yaliyo upumbavu, na moyo wake utafanya maovu, ili kutenda hila na kusema yasiyo kweli juu ya Bwana, ili kuziacha nafsi za watu wenye njaa hazina kitu, na kukikomesha kinywaji chake mwenye kiu.
7 Tena vyombo vyake ayari ni vibaya; hutunga hila mbaya, ili kuwaangamiza wanyonge kwa maneno ya uongo, mtu mhitaji ajaposema maneno yenye haki.
8 Bali mwungwana huwaza mambo ya kiungwana, naye hushika sana mambo ya kiungwana.
9 Inukeni, enyi wanawake wenye raha, isikieni sauti yangu; enyi binti za watu msiokuwa na uangalifu, tegeni masikio yenu msikie matamko yangu.
10 Maana mtataabishwa siku kadha wa kadha zaidi ya mwaka, enyi wanawake mliojikinai; kwa sababu mavuno ya mizabibu yatakoma, wakati wa kuvuna vitu vya mashamba hautakuja.
11 Tetemekeni, enyi wanawake wenye raha; taabikeni, enyi msiokuwa na uangalifu; jivueni, jivueni nguo zenu kabisa, jivikeni viuno nguo za magunia.
12 Watajipiga vifua kwa ajili ya mashamba mazuri, kwa ajili ya mzabibu uliozaa sana.
13 Juu ya nchi ya watu wangu itamea michongoma na mibigili; naam, juu ya nyumba za furaha katika mji ulio na shangwe;
14 maana jumba la mfalme litaachwa; mji uliokuwa na watu wengi utakuwa hauna mtu; kilima na mnara utakuwa makao ya wanyama milele, furaha ya punda-mwitu, malisho ya makundi ya kondoo;
15 hata roho itakapomwagwa juu yetu kutoka juu; hata jangwa litakapokuwa shamba lizaalo sana; nalo shamba lizaalo sana litakapohesabiwa kuwa msitu.
16 Ndipo hukumu itakaa katika jangwa, na haki itakaa katika shamba lizaalo sana.
17 Na kazi ya haki itakuwa amani; na mazao ya haki yatakuwa ni utulivu na matumaini daima.
18 Na watu wangu watakaa katika kao la amani; na katika maskani zilizo salama, na katika mahali pa kupumzikia penye utulivu.
19 Lakini mvua ya mawe itakunya, wakati wa kuangushwa miti ya msituni; na huo mji utadhilika.
20 Heri ninyi mpandao mbegu kando ya maji yote, na kuiacha miguu ya ng'ombe na punda waende ko kote.

Isaya 33


1 Ole wako uharibuye ila hukuharibiwa, utendaye hila wala hukutendwa hila! Utakapokwisha kuharibu, utaharibiwa wewe; na utakapokwisha kutenda kwa hila, wao watakutenda hila wewe.
2 Ee Bwana, uturehemu; tumekungoja wewe; uwe wewe mkono wetu kila asubuhi,na wokovu wetu pia wakati wa taabu.
3 Kabila za watu wamekimbia wakisikia kelele za fujo; mataifa wametawanyika ulipojiinua nafsi yako.
4 Na mateka yako yatakumbwa kama wadudu wakumbavyo, wataruka juu yake kama arukavyo nzige.
5 Bwana ametukuka; kwa maana anakaa juu; amejaza Sayuni hukumu na haki.
6 Nyakati zako zitakuwa nyakati za kukaa imara; za wokovu tele na hekima na maarifa; kumcha Bwana ni hazina yake ya akiba.
7 Angalia, mashujaa wao wanalia nje, wajumbe wa amani wanalia kwa uchungu.
8 Njia kuu zimeachwa, msafiri amekoma; ameyavunja maagano, ameidharau miji, hamjali mtu.
9 Nchi inaomboleza, na kulegea; Lebanoni imetahayarika na kunyauka; Sharoni imekuwa kama jangwa; Bashani na Karmeli zimepukutika majani.
10 Basi, sasa nitasimama; asema Bwana; sasa nitajiinua, sasa nitajitukuza.
11 Ninyi mtachukua mimba ya makapi, mtazaa majani makavu; pumzi yenu ni moto utakaowateketeza wenyewe.
12 Nao mataifa watakuwa kama kuchoma chokaa, kama miiba iliyokatika, iteketezwayo motoni.
13 Sikieni, ninyi mlio mbali, niliyoyatenda; na ninyi mlio karibu, kirini uweza wangu.
14 Wenye dhambi walio katika Sayuni wanaogopa; tetemeko limewashika wasiomcha Mungu; Ni nani kwetu sisi awezaye kukaa na moto ulao; ni nani kwetu sisi awezaye kukaa na moto uteketezao milele?
15 Ni yeye aendaye kwa haki, anenaye maneno ya adili; ni yeye anayedharau faida ipatikanayo kwa dhuluma; akung'utaye mikono yake asipokee rushwa; azibaye masikio yake asisikie habari za damu; afumbaye macho yake asitazame uovu.
16 Huyu ndiye atakayekaa juu; majabali ni ngome yake; atapewa chakula chake; maji yake hayatakoma.
17 Macho yako yatamwona mfalme katika uzuri wake, yataona nchi iliyoenea sana.
18 Moyo wako utatafakari hofu ile; Yuko wapi yeye aliyehesabu? Yuko wapi yeye aliyeupima ushuru? Yuko wapi yeye aliyeihesabu minara?
19 Hutawaona watu wale wakali; watu wa maneno magumu usiyoweza kuyafahamu; wenye lugha ya kigeni usiyoweza kuelewa nayo.
20 Angalia Sayuni, mji wa sikukuu zetu; macho yako yatauona Yerusalemu umekuwa kao la raha; hema isiyotanga-tanga; vigingi vyake havitang'olewa, wala kamba zake hazitakatika.
21 Bali huko Bwana atakuwa pamoja nasi, mwenye adhama; mahali penye mito mipana na vijito, pasipopita mashua na makasia yake; wala hapana merikebu ya vita itakayopita hapo.
22 Kwa maana Bwana ndiye mwamuzi wetu; Bwana ndiye mfanya sheria wetu; Bwana ndiye mfalme wetu; ndiye atakayetuokoa.
23 Kamba zako zimelegea; hawakuweza kukaza sana shina la mlingoti wao; hawakuweza kulikunjua tanga; ndipo mapato ya mateka yaligawanywa, hata wachechemeao walipata mateka.
24 Wala hapana mwenyeji atakayesema, Mimi mgonjwa; watu wakaao humo watasamehewa uovu wao.

Isaya 34


1 Karibuni, enyi mataifa, mpate kusikia; sikilizeni, enyi kabila za watu; dunia na isikie, nacho kiijazacho, ulimwengu na vitu vyote viutokavyo.
2 Maana Bwana ana ghadhabu juu ya mataifa yote, na hasira kali juu ya jeshi lao lote; amewaangamiza kabisa, amewatoa waende kuchinjwa.
3 Watu wao waliouawa watatupwa nje, na uvundo wa maiti zao utapaa juu, na milima itayeyushwa kwa damu yao.
4 Na jeshi lote la mbinguni litafumuliwa, na mbingu zitakunjwa kama karatasi, na jeshi lao lote litanyauka kama vile jani la mzabibu linyaukavyo na kupukutika, na kama jani la mtini linyaukavyo na kupukutika.
5 Maana upanga wangu umekunywa na kushiba mbinguni; tazama, utashukia Edomu, na juu ya watu wa laana yangu, ili kuwahukumu.
6 Upanga wa Bwana umeshiba damu, umenona kwa unono, kwa damu ya wana-kondoo na mbuzi, kwa mafuta ya figo za kondoo waume; maana Bwana ana dhabihu huko Bozra, machinjo makubwa katika nchi ya Edomu.
7 Na nyati watatelemka pamoja nao, na mahasai pamoja na mafahali, na nchi yao italewa kwa damu, na mavumbi yake yatanoneshwa kwa shahamu.
8 Maana ni siku ya kisasi cha Bwana, mwaka wa malipo, ili kushindania Sayuni.
9 Na vijito vyake vitageuzwa kuwa lami, na mavumbi yake yatageuzwa kuwa kiberiti, na ardhi yake itakuwa lami iwakayo.
10 Haitazimwa mchana wala usiku, moshi wake utapaa milele; tangu kizazi hata kizazi itakuwa ukiwa; hapana mtu atakayepita kati yake milele na milele.
11 Kaati na nungu wataimiliki, bundi na kunguru watakaa huko, naye atanyosha juu yake kamba ya ukiwa na timazi ya utupu.
12 Watawaitia wakuu wake ufalme, lakini hawatakuwapo; wakuu wake wote wamekuwa si kitu.
13 Miiba itamea majumbani mwake, upupu na mbigili ndani ya maboma yake; nayo itakuwa kao la mbweha, na ua la mbuni.
14 Na hayawani wa nyikani watakutana na mbwa-mwitu, na beberu anamwita mwenziwe; naam, babewatoto anakaa huko na kujipatia raha.
15 Huko pili atafanya kioto chake na kuzaa na kuotamia, na kukusanya watoto wake katika kivuli chake; naam, huko watakusanyika tai, kila mmoja na mwenzake.
16 Tafuteni katika kitabu cha Bwana mkasome; hapana katika hao wote atakayekosa kuwapo, hapana mmoja atakayemkosa mwenzake; kwa maana kinywa changu kimeamuru, na roho yake imewakusanya.
17 Naye amewapigia kura, na mkono wake umewagawanyia kwa kamba; wataimiliki hata milele, watakaa ndani yake kizazi hata kizazi.

Isaya 35


1 Nyika na mahali palipo ukiwa patafurahi; jangwa litashangilia na kuchanua maua kama waridi.
2 Litachanua maua mengi, na kufurahi, naam, kwa shangwe na kuimba; litapewa uzuri wa Lebanoni, utukufu wa Karmeli na Sharoni; watauona utukufu wa Bwana, ukuu wa Mungu wetu.
3 Itieni nguvu mikono iliyo dhaifu, yafanyeni imara magoti yaliyolegea.
4 Waambieni walio na moyo wa hofu, Jipeni moyo, msiogope; tazama, Mungu wenu atakuja na kisasi, na malipo ya Mungu; atakuja na kuwaokoa ninyi.
5 Ndipo macho ya vipofu yatafumbuliwa, na masikio ya viziwi yatazibuliwa.
6 Ndipo mtu aliye kilema ataruka-ruka kama kulungu, na ulimi wake aliye bubu utaimba; maana katika nyika maji yatabubujika; na vijito jangwani.
7 Na mchanga ung'aao mfano wa maji utakuwa ziwa la maji, na nchi yenye kiu itakuwa chemchemi za maji; katika makao ya mbweha, walipokuwa wamelala, patakuwa na majani, pamoja na mianzi na manyasi.
8 Na hapo patakuwa na njia kuu, na njia, nayo itaitwa, Njia ya utakatifu; wasio safi hawatapita juu yake; bali itakuwa kwa ajili ya watu hao; wasafirio, wajapokuwa wajinga, hawatapotea katika njia hiyo.
9 Hapo hapatakuwa na simba, wala mnyama mkali hatapanda juu yake; hawataonekana hapo; bali waliokombolewa watakwenda katika njia hiyo.
10 Na hao waliokombolewa na Bwana watarudi, watafika Sayuni wakiimba; na furaha ya milele itakuwa juu ya vichwa vyao; nao watapata kicheko na furaha, huzuni na kuugua zitakimbia.

Isaya 36


1 Ikawa, katika mwaka wa kumi na nne wa kumiliki kwake mfalme Hezekia, Senakeribu, mfalme wa Ashuru, akapanda ili kupigana na miji yote ya Yuda yenye boma, akaitwaa.
2 Mfalme wa Ashuru akamtuma amiri toka Lakishi hata Yerusalemu,kwa mfalme Hezekia,pamoja na jeshi kubwa. Naye akasimama karibu na mfereji wa birika ya juu,iliyo katika njia kuu ya kuuendea uwanda wa dobi.
3 Wakamtokea Eliakimu, mwana wa Hilkia, aliyekuwa msimamizi wa nyumba ya mfalme, na Shebna, mwandishi, na Yoa, mwana wa Asafu, mwenye kuandika tarehe.
4 Yule amiri akawaambia, Haya, mwambieni Hezekia, kwamba mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru, asema hivi, Ni tumaini gani hili unalolitumainia?
5 Nasema, mashauri yako, na nguvu zako kwa vita, ni maneno yasiyo na maana; basi, unamtumaini nani hata ukaniasi mimi?
6 Tazama, unaitumainia fimbo ya mwanzi huu uliopondeka, yaani, Misri, ambayo, mtu akitegemea juu yake, humwingia mkononi na kumchoma; ndivyo alivyo Farao, mfalme wa Misri, kwa wote wamtumainio.
7 Lakini ukiniambia, Tunamtumaini Bwana, Mungu wetu, je! Si yeye ambaye Hezekia ameondoa mahali pake mlimoinuka, na madhabahu zake, akawaambia watu wa Yuda na Yerusalemu, Sujuduni mbele ya madhabahu hii?
8 Basi sasa, tafadhali mpe bwana wangu, mfalme wa Ashuru, dhamana, nami nitakupa farasi elfu mbili, ikiwa wewe kwa upande wako waweza kupandisha watu juu yao.
9 Wawezaje, basi, kurudisha nyuma uso wa akida mmoja wa watumishi walio wadogo wa bwana wangu, na kuitumainia Misri upewe magari na farasi?
10 Je! Nimepanda mimi, ili kupigana na mahali hapa na kupaangamiza, bila shauri la Bwana? Bwana ndiye aliyeniambia, Panda upigane na nchi hii na kuiangamiza.
11 Ndipo Eliakimu, mwana wa Hilkia, na Shebna, na Yoa, wakamwambia yule amiri, Tafadhali, sema na watumishi wako kwa lugha ya Kiashuri; maana tunaifahamu; wala usiseme nasi kwa lugha ya Kiyahudi, masikioni mwa watu wote walio ukutani.
12 Lakini yule amiri akawaambia, Je! Bwana wangu amenituma kwa bwana wako, na kwako wewe, niseme maneno haya? Hakunituma kwa watu hawa walio ukutani, ili wale mavi yao wenyewe na kunywa mkojo wao pamoja nanyi?
13 Kisha yule amiri akasimama akalia kwa sauti kuu kwa lugha ya Kiyahudi, akisema, Lisikieni neno la mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru.
14 Mfalme asema hivi; Hezekia asiwadanganye, kwa maana hataweza kuwaokoa;
15 wala msimwache Hezekia kuwatia moyo wa kumtumaini Bwana; akisema, Bwana bila shaka atatuokoa, mji huu hautatiwa katika mkono wa mfalme wa Ashuru.
16 Msimsikilize Hezekia; maana mfalme wa Ashuru asema hivi, Fanyeni suluhu na mimi, mkatoke mnijie, mkale kila mtu matunda ya mzabibu wake na matunda ya mtini wake, mkanywe kila mmoja maji ya birika yake mwenyewe;
17 hata nije nikawachukue mpaka nchi iliyo kama nchi yenu wenyewe, nchi ya nafaka na divai, nchi ya mkate na mashamba ya mizabibu.
18 Jihadharini, asije Hezekia akawadanganya, akisema, Bwana atatuokoa. Je! Yuko mungu mmoja wa mataifa aliyewaokoa watu wake na mkono wa mfalme wa Ashuru?
19 Wako wapi miungu ya Hamathi na ya Arpadi? Wako wapi miungu ya Sefarvaimu? Je! Wameiokoa Samaria na mkono wangu?
20 Katika miungu yote ya nchi hizi ni nani waliookoa nchi yao na mkono wangu, hata Bwana auokoe Yerusalemu na mkono wangu?
21 Lakini watu wakanyamaza kimya; wala hawakumjibu hata neno moja; maana ilikuwa amri ya mfalme, kwamba, Msimjibu neno.
22 Ndipo Eliakimu, mwana wa Hilkia, aliyekuwa msimamizi wa nyumba ya mfalme, na Shebna, mwandishi, na Yoa, mwana wa Asafu mwenye kuandika tarehe, wakaenda kwa Hezekia, na nguo zao zimeraruliwa, wakamwambia Hezekia maneno ya yule amiri.

Isaya 37


1 Ikawa mfalme Hezekia aliposikia hayo, alizirarua nguo zake, akajivika nguo za magunia, akaingia katika nyumba ya Bwana.
2 Akamtuma Eliakimu aliyekuwa msimamizi wa nyumba yake na Shebna, mwandishi, na wazee wa makuhani, wamejivika nguo za magunia, waende kwa Isaya nabii, mwana wa Amozi.
3 Wakamwambia, Hezekia asema hivi, Siku hii ni siku ya dhiki, na aibu, na matukano; maana watoto wa tayari kuzaliwa, wala hapana nguvu za kuwazaa.
4 Yamkini Bwana, Mungu wako, atayasikia maneno ya huyo amiri ambaye mfalme wa Ashuru, bwana wake, amemtuma ili amtukane Mungu aliye hai; na Bwana, Mungu wako atayakemea maneno aliyoyasikia; basi, inua dua yako kwa ajili ya mabaki yaliyobakia.
5 Basi, watumishi wa mfalme Hezekia wakaenda kwa Isaya.
6 Isaya akawaambia, Mwambieni bwana wenu maneno haya; Bwana asema hivi, Usiyaogope maneno uliyoyasikia, ambayo watumishi wa mfalme wa Ashuru wamenitukana.
7 Tazama, nitatia roho ndani yake, naye atasikia kivumi, na kurudi hata nchi yake mwenyewe, nami nitamwangusha kwa upanga katika nchi yake mwenyewe.
8 Basi yule amiri akarudi, akamkuta mfalme wa Ashuru anafanya vita juu ya Libna; kwa maana alikuwa amesikia ya kwamba ameondoka, akaacha Lakishi.
9 Naye alisikia habari ya Tirhaka, mfalme wa Kushi, ya kwamba, Ametoka ili kupigana nawe; naye aliposikia hayo, akatuma wajumbe kwa Hezekia, kusema,
10 Mwambieni Hezekia, mfalme wa Yuda, maneno haya, mkisema, Asikudanganye Mungu wako unayemtumaini, akisema, Yerusalemu hautatiwa katika mikono ya mfalme wa Ashuru.
11 Tazama, umesikia habari ya mambo yote, ambayo wafalme wa Ashuru wamezitenda nchi zote, kwa kuziangamiza kabisa je! Utaokoka wewe?
12 Je! Miungu ya mataifa, ambao baba zangu waliwaangamiza, wamewaokoa? Gozani, na Harani, na Resefu, na wana wa Adini waliokuwa katika Telasari?
13 Yuko wapi mfalme wa Hamathi, na mfalme wa Arpadi, na mfalme wa mji wa Sefarvaimu, wa Hena, na wa Iva?
14 Basi Hezekia akaupokea waraka katika mikono ya wale wajumbe, akausoma; kisha Hezekia akapanda, akaingia katika nyumba ya Bwana, akaukunjua mbele za Bwana.
15 Hezekia akamwomba Bwana, akisema,
16 Ee Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, ukaaye juu ya makerubi, wewe, naam, wewe peke yako, ndiwe Mungu wa falme zote za dunia. Wewe ndiwe uliyeziumba mbingu na nchi.
17 Tega sikio lako, Bwana, usikie; funua macho yako, Bwana, uone; uyasikie maneno ya Senakeribu, aliyopeleka ili kumtukana Mungu aliye hai.
18 Ni kweli, Bwana, wafalme wa Ashuru wameziharibu nchi zote, na mashamba yao,
19 na kuwatupa miungu yao motoni; kwa maana hao hawakuwa miungu, bali kazi ya mikono ya wanadamu; walikuwa miti na mawe, ndiyo sababu wakawaharibu.
20 Basi sasa, Bwana, Mungu wetu, utuokoe na mkono wake, falme zote za dunia zipate kujua ya kuwa wewe ndiwe Bwana, wewe peke yako.
21 Ndipo Isaya, mwana wa Amozi, akapeleka ujumbe kwa Hezekia, akisema, Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Kwa kuwa umeniomba juu ya Senakeribu, mfalme wa Ashuru,
22 tamko alilolitamka Bwana katika habari zake ndilo hili; Bikira, binti Sayuni, anakudharau, anakudhihaki sana; binti Yerusalemu anatikisa kichwa chake juu yako.
23 Ni nani uliyemshutumu na kumtukana? Umeinua sauti yako juu ya nani, na kuinua macho yako juu? Juu ya Mtakatifu wa Israeli.
24 Umemshutumu Bwana kwa watumishi wako, kwa kuwa umesema, Kwa wingi wa magari yangu nimepanda juu ya vilele vya milima, mpaka mahali pa ndani ya Lebanoni; nami nitaikata mierezi yake mirefu, na misunobari yake mizuri, nami nitaingia ndani ya mahali pake palipoinuka, palipo mbali sana, msitu wa shamba lake lizaalo sana.
25 Nimechimba na kunywa maji, na kwa nyayo za miguu yangu nitaikausha mito yote ya Misri.
26 Je! Hukusikia? Ni mimi niliyeyatenda hayo tokea zamani, na kuyafanya tokea siku za kale; nikayatimiza sasa, iwe kazi yako kuangamiza miji yenye boma, ikawe chungu na magofu.
27 Ndiyo sababu wenyeji wao wakawa hawana nguvu, na kufadhaika, na kuhangaika, wakawa kama majani ya mashamba, kama miche mibichi, kama majani juu ya dari, kama shamba la ngano kabla haijaiva.
28 Lakini nakujua, kuketi kwako, na kutoka kwako, na kuingia kwako; na ghadhabu yako uliyonighadhibikia.
29 Kwa sababu ya kunighadhibikia kwako, na kwa sababu kutakabari kwako kumefika masikioni mwangu, nitatia kulabu yangu katika pua yako, na hatamu yangu midomoni mwako, nami nitakurudisha kwa njia ile ile uliyoijia.
30 Na kwako wewe dalili ndiyo hii; mwaka huu mtakula vitu vimeavyo vyenyewe; na mwaka wa pili mtakula mazao ya mbegu za vitu hivyo; na mwaka wa tatu pandeni mbegu, kavuneni; mkapande mizabibu katika mashamba, mkale matunda yake.
31 Na mabaki yaliyookoka, yaliyobakia ya nyumba ya Yuda, yatatia mizizi chini, na kuzaa matunda juu.
32 Maana katika Yerusalemu yatatoka mabaki, nao watakaookoka katika mlima Sayuni; wivu wa Bwana wa majeshi utatimiza mambo hayo.
33 Basi, Bwana asema hivi katika habari za mfalme wa Ashuru, Yeye hataingia ndani ya mji huu, wala hatapiga mshale hapa, wala hatakuja mbele yake kwa ngao, wala hatajenga boma juu yake.
34 Njia ile ile aliyoijia, kwa njia hiyo atarudi zake, wala hataingia ndani ya mji huu; asema Bwana.
35 Nami nitaulinda mji huu, niuokoe kwa ajili yangu mwenyewe, na kwa ajili ya Daudi, mtumishi wangu.
36 Basi malaika wa Bwana alitoka, akaua watu mia na themanini na tano elfu katika kituo cha Waashuri, na watu walipoamka asubuhi na mapema, kumbe, hao walikuwa maiti wote pia.
37 Basi Senakeribu, mfalme wa Ashuru akaenda zake, akarudi Ninawi, akakaa huko.
38 Ikawa alipokuwa akiabudu katika nyumba ya Nisroki, mungu wake, Adrameleki na Shareza, wanawe, wakampiga kwa upanga; wakakimbilia nchi ya Ararati; naye Esar-hadoni, mwanawe, akamiliki badala yake.

Isaya 38


1 Siku hizo Hezekia aliugua, akawa katika hatari ya kufa; na Isaya nabii, mwana wa Amozi, akaenda kwa mfalme, akamwambia, Bwana asema hivi, Tengeneza mambo ya nyumba yako; maana utakufa, wala hutapona.
2 Basi Hezekia akajigeuza, akaelekeza uso wake ukutani, akamwomba Bwana,
3 akasema, Ee Bwana, kumbuka haya, nakusihi, kwamba nimekwenda mbele zako katika kweli na kwa moyo mkamilifu, na kutenda yaliyo mema machoni pako. Hezekia akalia sana sana.
4 Ikawa, neno la Bwana likamjia Isaya, kusema,
5 Enenda ukamwambie Hezekia, Bwana, Mungu wa Daudi, baba yako, asema hivi, Mimi nimeyasikia maombi yako, nimeyaona machozi yako; tazama, nitaziongeza siku zako, kiasi cha miaka kumi na mitano.
6 Nami nitakuokoa wewe, na mji huu, na mkono wa mfalme wa Ashuru, nami nitaulinda mji huu.
7 Jambo hili liwe ishara kwako, itokayo kwa Bwana, ya kuwa Bwana atalitimiza jambo hili alilolisema;
8 Tazama, nitakirudisha nyuma kivuli madaraja kumi, ambayo kilishuka juu ya duara ya Ahazi kwa sababu ya jua. Basi jua likarudi madaraja kumi katika hiyo duara, ambayo limekwisha kushuka.
9 Haya ndiyo maandiko ya Hezekia, mfalme wa Yuda, alipokuwa hawezi, naye akapona ugonjwa wake.
10 Nalisema, Katika usitawi wa siku zangu nitakwenda kuingia malango ya kuzimu; Nimenyimwa mabaki ya miaka yangu.
11 Nalisema, Sitamwona Bwana, yeye Bwana, katika nchi ya walio hai; Sitamwona mwanadamu tena pamoja na hao wakaao duniani.
12 Kao langu limeondolewa kabisa, limechukuliwa kama hema ya mchungaji; Nimekunja maisha yangu kama mfumaji; atanikatilia mbali na kitanda cha mfumi; Tangu mchana hata usiku wanimaliza.
13 Nalijituliza hata asubuhi; kama simba, aivunja mifupa yangu yote; Tangu mchana hata usiku wanimaliza.
14 Kama mbayuwayu au korongo ndivyo nilivyolia; Naliomboleza kama hua; macho yangu yamedhoofu kwa kutazama juu; Ee Bwana, nimeonewa, na uwe mdhamini wangu.
15 Niseme nini? Yeye amenena nami, na yeye mwenyewe ametenda hayo; Nitakwenda polepole miaka yangu yote, kwa sababu ya uchungu wa nafsi yangu.
16 Ee Bwana, kwa mambo hayo watu huishi; Na uhai wa roho yangu u katika hayo yote; Kwa hiyo uniponye na kunihuisha.
17 Tazama; nalikuwa na uchungu mwingi kwa ajili ya amani yangu; Lakini kwa kunipenda umeniokoa na shimo la uharibifu; Kwa maana umezitupa dhambi zangu zote nyuma yako.
18 Kwa kuwa kuzimu hakuwezi kukusifu; mauti haiwezi kukuadhimisha; Wale washukao shimoni hawawezi kuitarajia kweli yako.
19 Aliye hai, naam, aliye hai, ndiye atakayekusifu, kama mimi leo; Baba atawajulisha watoto kweli yako.
20 Bwana yu tayari kunipa wokovu. Basi, kwa vinubi tutaziimba nyimbo zangu, Siku zote za maisha yetu nyumbani mwa Bwana.
21 Maana Isaya amesema, Na watwae mkate wa tini, wakauweke juu ya jipu, naye atapona.
22 Tena Hezekia alikuwa amesema, Iko ishara gani ya kunionyesha ya kuwa nitapanda niingie nyumbani mwa Bwana?

Isaya 39


1 Wakati huo Merodaki-baladani, mwana wa Baladani, mfalme wa Babeli, alipeleka barua na zawadi kwa Hezekia; kwa maana amepata habari kwamba amekuwa hawezi, na kwamba amepona.
2 Hezekia akawafurahia, akawaonyesha nyumba yake yenye vitu vyake vya thamani, fedha na dhahabu, na manukato, na marhamu ya thamani, na nyumba yote yenye silaha zake za vita, na vitu vyote vilivyoonekana katika hazina zake; hapakuwa na kitu nyumbani mwake wala katika ufalme wake asichowaonyesha.
3 Ndipo Isaya nabii akamwendea mfalme Hezekia, akamwambia, Watu hawa walisema nini? Nao wametoka wapi kuja kwako? Hezekia akasema, Wametoka katika nchi iliyo mbali, wakaja kwangu toka Babeli.
4 Ndipo akasema, Wameona nini katika nyumba yako? Hezekia akajibu, Wameviona vitu vyote vilivyomo nyumbani mwangu; hapana kitu katika hazina zangu nisichowaonyesha.
5 Ndipo Isaya akamwambia Hezekia, Basi, lisikie neno la Bwana wa majeshi.
6 Tazama, siku zinakuja, ambazo vitu vyote vilivyomo nyumbani mwako, na hivyo vilivyowekwa akiba na baba zako hata leo, vitachukuliwa mpaka Babeli; hapana kitu cho chote kitakachosalia; asema Bwana.
7 Na baadhi ya wana wako utakaowazaa, watakaotoka kwako, watawachukulia mbali; nao watakuwa matowashi katika jumba la mfalme wa Babeli.
8 Ndipo Hezekia akamwambia Isaya, Neno la Bwana ulilolinena ni jema. Tena akamwambia, Maana itakuwapo amani na kweli katika siku zangu mimi.

Isaya 40


1 Watulizeni mioyo, watulizeni mioyo, watu wangu, asema Mungu wenu.
2 Semeni na moyo wa Yerusalemu, kauambieni kwa sauti kuu ya kwamba vita vyake vimekwisha, uovu wake umeachiliwa; kwa kuwa amepokea kwa mkono wa Bwana adhabu maradufu kwa dhambi zake zote.
3 Sikiliza, ni sauti ya mtu aliaye, Itengenezeni nyikani njia ya Bwana; Nyosheni jangwani njia kuu kwa Mungu wetu.
4 Kila bonde litainuliwa, Na kila mlima na kilima kitashushwa; Palipopotoka patakuwa pamenyoka, Na palipoparuza patasawazishwa;
5 Na utukufu wa Bwana utafunuliwa, Na wote wenye mwili watauona pamoja; Kwa kuwa kinywa cha Bwana kimenena haya.
6 Sikiliza, ni sauti ya mtu asemaye, Lia! Nikasema, Nilie nini? Wote wenye mwili ni majani, Na wema wake wote ni kama ua la kondeni;
7 Majani yakauka, ua lanyauka; Kwa sababu pumzi ya Bwana yapita juu yake. Yakini watu hawa ni majani.
8 Majani yakauka, ua lanyauka; Bali neno la Mungu wetu litasimama milele.
9 Wewe uuhubiriye Sayuni habari njema, Panda juu ya mlima mrefu; Wewe uuhubiriye Yerusalemu habari njema, Paza sauti kwa nguvu; Paza sauti yako, usiogope; Iambie miji ya Yuda, Tazameni, Mungu wenu.
10 Tazameni, Bwana Mungu atakuja kama shujaa, Na mkono wake ndio utakaomtawalia; Tazameni, thawabu yake i pamoja naye, Na ijara yake i mbele zake.
11 Atalilisha kundi lake kama mchungaji, Atawakusanya wana-kondoo mikononi mwake; Na kuwachukua kifuani mwake, Nao wanyonyeshao atawaongoza polepole.
12 Ni nani aliyeyapima maji kwa konzi ya mkono wake, na kuzikadiri mbingu kwa shubiri, na kuyashika mavumbi ya dunia katika pishi, na kuipima milima kwa uzani, na vilima kama kwa mizani?
13 Ni nani aliyemwongoza roho ya Bwana, na kumfundisha kwa kuwa mshauri wake?
14 Alifanya shauri na nani, ni nani aliyemwelimisha na kumfunza njia ya hukumu, na kumfunza maarifa, na kumwonyesha njia ya fahamu?
15 Tazama, mataifa ni kama tone la maji katika ndoo, huhesabiwa kuwa kama mavumbi membamba katika mizani; tazama, yeye huvinyanyua visiwa kama ni kitu kidogo sana.
16 Lebanoni nayo hautoshi kwa kuni, wala wanyama wake hawatoshi kwa kafara.
17 Mataifa yote huwa kama si kitu mbele zake; huhesabiwa kwake kuwa duni ya si kitu, na ubatili.
18 Basi, mtamlinganisha Mungu na nani? Au mtamfananisha na mfano wa namna gani?
19 Sanamu fundi mmoja huiyeyusha, na mfua dhahabu huifunika dhahabu, huifulia mikufu ya fedha.
20 Yeye aliye maskini sana hata hawezi kutoa sadaka ya namna hii, huchagua mti usiooza, hujitafutia fundi mstadi wa kusimamisha sanamu ya kuchonga isiyoweza kutikisika.
21 Je! Hamkujua? Hamkusikia? Hamkuambiwa tokea mwanzo? Hamkufahamu tangu kuwekwa misingi ya dunia?
22 Yeye ndiye anayeketi juu ya duara ya dunia, na hao wanaokaa ndani yake huwa kama panzi; yeye ndiye azitandazaye mbingu kama pazia na kuzikunjua kama hema ya kukaliwa;
23 ndiye awatanguaye wakuu, na kuwabatilisha waamuzi wa dunia.
24 Naam, hawakupandwa; hawakutiwa katika ardhi kama mbegu; naam, shina lao halikutia mizizi katika ardhi; tena awapuzia tu, wakanyauka, upepo wa kisulisuli wawaondoa kama mabua makavu.
25 Mtanifananisha na nani, basi, nipate kuwa sawa naye? Asema yeye aliye Mtakatifu.
26 Inueni macho yenu juu, mkaone; ni nani aliyeziumba hizi; aletaye nje jeshi lao kwa hesabu; aziita zote kwa majina; kwa ukuu wa uweza wake, na kwa kuwa yeye ni hodari kwa nguvu zake; hapana moja isiyokuwapo mahali pake.
27 Mbona unasema, Ee Yakobo, mbona unanena, Ee Israeli, Njia yangu imefichwa, Bwana asiione, na hukumu yangu imempita Mungu wangu asiiangalie?
28 Je! Wewe hukujua? Hukusikia? Yeye Mungu wa milele, Bwana, Muumba miisho ya dunia, hazimii, wala hachoki; akili zake hazichunguziki.
29 Huwapa nguvu wazimiao, humwongezea nguvu yeye asiyekuwa na uwezo.
30 Hata vijana watazimia na kuchoka, na wanaume vijana wataanguka;
31 bali wao wamngojeao Bwana watapata nguvu mpya; watapanda juu kwa mbawa kama tai; watapiga mbio, wala hawatachoka; watakwenda kwa miguu, wala hawatazimia.

Isaya 41


1 Nyamazeni mbele zangu, enyi visiwa, na mataifa wajipatie nguvu mpya; na waje karibu wakanene; na tukaribiane pamoja kwa hukumu.
2 Ni nani aliyemwinua mmoja atokaye mashariki, ambaye katika haki amemwita mguuni pake? Ampa mataifa mbele yake, na kumtawaza juu ya wafalme; awatoa wawe kama mavumbi kwa upanga wake, kama makapi yaliyopeperushwa kwa upinde wake.
3 Awafuatia, apita salama hata kwa njia asiyoikanyaga kamwe kwa miguu yake.
4 Ni nani aliyetenda na kufanya jambo hilo, aviitaye vizazi tangu mwanzo? Mimi, Bwana, wa kwanza na wa mwisho, mimi ndiye.
5 Visiwa vimeona, vikaogopa; ncha za dunia zilitetemeka; walikaribia, walikuja.
6 Wakasaidiana, kila mtu na mwenzake, kila mtu akamwambia ndugu yake; Uwe na moyo mkuu.
7 Seremala akamtia moyo mfua dhahabu, na yeye alainishaye kwa nyundo akamhimiza yule apigaye fuawe, akiisifu kazi ya kuunga, akisema, Ni kazi njema; naye akaikaza kwa misumari isitikisike.
8 Nawe, Israeli, mtumishi wangu; Yakobo, niliyekuchagua; mzao wa Ibrahimu, rafiki yangu;
9 wewe niliyekushika toka miisho ya dunia, na kukuita toka pembe zake, nikikuambia, Wewe u mtumishi wangu; nimekuchagua wala sikukutupa;
10 usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako; nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, naam, nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu.
11 Tazama, wote walioona hasira juu yako watatahayarika na kufadhaika; watu washindanao nawe watakuwa si kitu, na kuangamia.
12 Utawatafuta wala hutawaona wale wapiganao nawe; watakuwa si kitu; watakuwa kama kitu kisichokuwa, wale waliofanya vita juu yako.
13 Kwa maana mimi, Bwana, Mungu wako, nitakushika mkono wako wa kuume, nikikuambia, Usiogope; mimi nitakusaidia.
14 Usiogope, Yakobo uliye mdudu, nanyi watu wa Israeli; mimi nitakusaidia, asema Bwana, na mkombozi wako ni Mtakatifu wa Israeli.
15 Tazama, nitakufanya kuwa chombo kikali kipya cha kupuria, chenye meno; utaifikicha milima, na kuisaga; nawe utafanya vilima kuwa kama makapi.
16 Utawapepeta, na upepo utawapeperusha; upepo wa kisulisuli utawatawanya; nawe utamfurahia Bwana, utajitukuza katika Mtakatifu wa Israeli.
17 Maskini na wahitaji wanatafuta maji, wala hapana; ndimi zao zimekauka kwa kiu; mimi, Bwana, nitawasikia, mimi, Mungu wa Israeli, sitawaacha.
18 Nitafunua vijito vya maji juu ya vilima, na chemchemi katikati ya mabonde; nitageuza jangwa kuwa ziwa la maji, na mahali pakavu kuwa vijito vya maji.
19 Nitapanda katika jangwa mwerezi, mshita, mhadasi, na mbono; nitatia katika nyika mberoshi, mtidhari, na mteashuri pamoja;
20 ili waone, na kujua, wakafikiri, na kufahamu pamoja, ya kuwa mkono wa Bwana ndio uliofanya jambo hilo. Mtakatifu wa Israeli ndiye aliyeliumba.
21 Haya, leteni maneno yenu, asema Bwana; toeni hoja zenu zenye nguvu, asema mfalme wa Yakobo.
22 Wayatangaze na kutujulisha yatakayokuwa; watuonyeshe mambo ya zamani, ni mambo gani, tukapate kuyatia moyoni, tukajue mwisho wake; au wamdhihirishie yatakayotokea baadaye.
23 Tujulisheni yatakayokuwa baadaye, nasi tutakiri ya kuwa ninyi ni miungu; naam, tendeni mema au tendeni mabaya, ili tujipime, tukaone pamoja.
24 Tazameni, ninyi si kitu, tena kazi yenu si kitu; awachaguaye ninyi ni chukizo.
25 Nimemwinua mtu toka kaskazini, naye amekuja; toka maawio ya jua amekuja anitajaye jina langu; naye atawajilia maliwali kama akanyagaye matope, na kama mfinyanzi afinyangaye udongo.
26 Ni nani aliyeihubiri habari tokea mwanzo, tupate kuijua? Na tokea zamani, tupate kusema, Yeye ni mwenye haki? Naam, hapana hata mmoja aliyetujulisha; naam, hapana hata mmoja aliyetuonyesha; naam, hapana hata mmoja aliyesikia maneno yenu.
27 Mimi kwanza nitauambia Sayuni, Tazama; hawa ndio; nami nitampa Yerusalemu mletaji wa habari njema.
28 Na nitazamapo, hapana mtu, hata katika watu hao hapana mshauri mmoja, ambaye, nikimwuliza, aweza kunijibu neno.
29 Tazama, hao wote ni ubatili; kazi zao si kitu; sanamu zao ni upepo na fujo.

Isaya 42


1 Tazama mtumishi wangu nimtegemezaye; mteule wangu, ambaye nafsi yangu imependezwa naye; nimetia roho yangu juu yake; naye atawatolea mataifa hukumu.
2 Hatalia, wala hatapaza sauti yake, wala kuifanya isikiwe katika njia kuu.
3 Mwanzi uliopondeka hatauvunja, wala utambi utokao moshi hatauzima; atatokeza hukumu kwa kweli.
4 Hatazimia, wala hatakata tamaa, hata atakapoweka hukumu duniani; na visiwa vitaingojea sheria yake.
5 Mungu Bwana anena, yeye aliyeziumba mbingu, na kuzitanda; yeye aliyeitandaza nchi na mazao yake; yeye awapaye pumzi watu walio juu yake; yeye awapaye roho wao waendao ndani yake.
6 Mimi, Bwana, nimekuita katika haki, nami nitakushika mkono, na kukulinda, na kukutoa uwe agano la watu, na nuru ya mataifa;
7 kuyafunua macho ya vipofu, kuwatoa gerezani waliofungwa, kuwatoa wale walioketi gizani katika nyumba ya kufungwa.
8 Mimi ni Bwana; ndilo jina langu; na utukufu wangu sitampa mwingine, wala sitawapa sanamu sifa zangu.
9 Tazama, mambo ya kwanza yamekuwa, nami nayahubiri mambo mapya; kabla hayajatokea nawapasheni habari zake.
10 Mwimbieni Bwana wimbo mpya, Na sifa zake tokea mwisho wa dunia; Ninyi mshukao baharini, na vyote vilivyomo, Na visiwa, nao wakaao humo.
11 Jangwa na miji yake na ipaze sauti zao, Vijiji vinavyokaliwa na Kedari; Na waimbe wenyeji wa Sela, Wapige kelele toka vilele vya milima.
12 Na wamtukuze Bwana, Na kutangaza sifa zake visiwani.
13 Bwana atatokea kama shujaa; Ataamsha wivu kama mtu wa vita; Atalia, naam, atapiga kelele; Atawatenda adui zake mambo makuu.
14 Siku nyingi nimenyamaza kimya; nimenyamaza, nikajizuia; sasa nitapiga kelele kama mwanamke aliye katika kuzaa; nitaugua na kutweta pamoja.
15 Nitaharibu milima na vilima, nitavikausha vyote vimeavyo; nitaifanya mito ya maji kuwa visiwa, na kuyakausha maziwa ya maji.
16 Nitawaleta vipofu kwa njia wasiyoijua; katika mapito wasiyoyajua nitawaongoza; nitafanya giza kuwa nuru mbele yao; na mahali palipopotoka kuwa pamenyoka. Haya nitayatenda, wala sitawaacha.
17 Watarudishwa nyuma, wataaibishwa sana, hao wanaotumainia sanamu za mawe, na kuziambia sanamu za madini, Ninyi ndinyi miungu yetu.
18 Sikilizeni, enyi viziwi; tazameni, enyi vipofu, mpate kuona.
19 Ni nani aliye kipofu, ila mtumishi wangu? Au aliye kiziwi, kama mjumbe wangu nimtumaye? Ni nani aliye kipofu, kama yeye aliye na amani? Naam, kipofu kama mtumishi wa Bwana?
20 Unaona mambo mengi, lakini huyatii moyoni; masikio yake ya wazi, lakini hasikii.
21 Bwana akapendezwa, kwa ajili ya haki yake, kuitukuza sheria, na kuiadhimisha.
22 Lakini watu hawa ni watu walioibiwa na kutekwa; wote wamenaswa katika mashimo, wamefichwa katika magereza; wamekuwa mawindo, wala hapana aokoaye; wamekuwa mateka, wala hapana asemaye, Rudisha.
23 Ni nani miongoni mwenu atakayetega sikio lake kuyasikia hayo? Atakayesikiliza na kusikia kwa wakati ujao?
24 Ni nani aliyemtoa Yakobo awe mateka, aliyemtia Israeli katika mikono ya wanyang'anyi? Si yeye, Bwana? Yeye tuliyemkosa, ambaye hawakutaka kwenda katika njia zake, wala hawakuitii sheria yake.
25 Kwa sababu hiyo alimwaga ukali wa hasira yake juu yake, na nguvu za vita; ukawasha moto wa kumzunguka pande zote, wala hakujua; ukamteketeza, wala hakuyatia hayo moyoni mwake.

Isaya 43


1 Lakini sasa, Bwana aliyekuhuluku, Ee Yakobo, yeye aliyekuumba, Ee Israeli, asema hivi, Usiogope, maana nimekukomboa; nimekuita kwa jina lako, wewe u wangu.
2 Upitapo katika maji mengi nitakuwa pamoja nawe; na katika mito, haitakugharikisha; uendapo katika moto, hutateketea; wala mwali wa moto hautakuunguza.
3 Maana mimi ni Bwana, Mungu wako; Mtakatifu wa Israeli, mwokozi wako, nimetoa Misri kuwa ukombozi wako; nimetoa Kushi na Seba kwa ajili yako.
4 Kwa kuwa ulikuwa wa thamani machoni pangu, na mwenye kuheshimiwa, nami nimekupenda; kwa sababu hiyo nitatoa watu kwa ajili yako; na kabila za watu kwa ajili ya maisha yako.
5 Usiogope; maana mimi ni pamoja nawe; nitaleta wazao wako toka mashariki, nitakukusanya toka magharibi;
6 nitaiambia kaskazi, Toa; nayo kusi, Usizuie; waleteni wana wangu kutoka mbali, na binti zangu kutoka miisho ya dunia.
7 Kila mmoja aliyeitwa kwa jina langu, niliyemwumba kwa ajili ya utukufu wangu; mimi nimemwumba, naam, mimi nimemfanya.
8 Walete vipofu walio na macho, na viziwi walio na masikio.
9 Na wakusanyike mataifa yote, kabila zote wakutanike; ni nani miongoni mwao awezaye kuhubiri neno hili, na kutuonyesha mambo ya zamani? Na walete mashahidi wao, wapate kuhesabiwa kuwa na haki; au na wasikie, wakaseme, Ni kweli.
10 Ninyi ni mashahidi wangu, asema Bwana, na mtumishi niliyemchagua; mpate kujua, na kuniamini, na kufahamu ya kuwa mimi ndiye; kabla yangu hakuumbwa Mungu awaye yote, wala baada yangu mimi hatakuwapo mwingine.
11 Mimi, naam, mimi, ni Bwana, zaidi yangu mimi hapana mwokozi.
12 Nimetangaza habari, nimeokoa, nimeonyesha, na hapakuwa mungu wa kigeni kati yenu; kwa sababu hiyo ninyi ni mashahidi wangu, asema Bwana, nami ni Mungu.
13 Naam, tangu siku ya leo, mimi ndiye; wala hapana awezaye kuokoa katika mkono wangu; mimi nitatenda kazi, naye ni nani awezaye kuizuia?
14 Bwana, Mkombozi wenu, Mtakatifu wa Israeli, asema hivi; Kwa ajili yenu nimetuma ujumbe Babeli nami nitawashusha wote mfano wa wakimbizi, naam, Wakaldayo, katika merikebu zao walizozifurahia.
15 Mimi ni Bwana, Mtakatifu wenu, Muumba wa Israeli, mfalme wenu.
16 Bwana asema hivi, yeye afanyaye njia katika bahari; na mahali pa kupita katika maji yenye nguvu;
17 atoaye gari na farasi, jeshi la askari na uwezo; wamelala, hawataondoka; wametoweka, wamezimwa mfano wa utambi.
18 Msiyakumbuke mambo ya kwanza, wala msiyatafakari mambo ya zamani.
19 Tazama, nitatenda neno jipya; sasa litachipuka; je! Hamtalijua sasa? Nitafanya njia hata jangwani, na mito ya maji nyikani.
20 Wanyama wa kondeni wataniheshimu, mbweha pia na mbuni; kwa sababu nimewapa maji jangwani, na mito nyikani, ili kuwanywesha watu wangu, wateule wangu;
21 watu wale niliojiumbia nafsi yangu, ili wazitangaze sifa zangu.
22 Lakini hukuniita, Ee Yakobo, bali umechoka nami, Ee Israeli.
23 Hukuniletea wana-kondoo kuwa kafara zako, wala hukuniheshimu kwa dhabihu zako. Sikukutumikisha kwa matoleo, wala sikukuchosha kwa ubani.
24 Hukuninunulia manukato kwa fedha, wala hukunishibisha kwa mafuta ya sadaka zako; bali umenitumikisha kwa dhambi zako, umenichosha kwa maovu yako.
25 Mimi, naam, mimi, ndimi niyafutaye makosa yako kwa ajili yangu mwenyewe, wala sitazikumbuka dhambi zako.
26 Unikumbushe, na tuhojiane; eleza mambo yako, upate kupewa haki yako.
27 Baba yako wa kwanza alifanya dhambi, na wakalimani wako wameniasi.
28 Kwa hiyo nitawatia unajisi wakuu wa patakatifu, nami nitamfanya Yakobo kuwalaani, na Israeli kuwa tukano.

Isaya 44


1 Lakini sikia sasa, Ee Yakobo, mtumishi wangu; na Israeli, niliyekuchagua;
2 Bwana, aliyekufanya, na kukuumba toka tumboni, yeye atakayekusaidia, asema hivi; Usiogope, Ee Yakobo, mtumishi wangu; na wewe, Yeshuruni, niliyekuchagua.
3 Kwa maana nitamimina maji juu yake aliye na kiu, na vijito vya maji juu ya mahali pakavu; nitamwaga roho yangu juu ya wazao wako, na baraka yangu juu yao utakaowazaa;
4 nao watatokea katika manyasi, kama mierebi karibu na mifereji ya maji.
5 Mmoja atasema, Mimi ni wa Bwana; na mwingine atajiita kwa jina la Yakobo; na mwingine ataandika juu ya mkono wake, Kwa Bwana, na kujiita kwa jina la Israeli.
6 Bwana, Mfalme wa Israeli, Mkombozi wako, Bwana wa majeshi, asema hivi; Mimi ni wa kwanza, na mimi ni wa mwisho; zaidi yangu mimi hapana Mungu.
7 Naye ni nani kama mimi atakayeita, na kuyahubiri haya, na kunitengenezea, tangu nilipowaweka watu wa kale? Na mambo yanayokuja na yatakayotokea, wayatangaze.
8 Msiogope wala msifanye hofu; je! Sikukuhubiri haya zamani na kuyaonyesha? Na ninyi ni mashahidi wangu. Je! Yuko Mungu zaidi yangu mimi? Hakika hapana Mwamba; mimi sijui mwingine.
9 Wachongao sanamu, wote ni ubatili; wala mambo yao yawapendezayo hayatafaa kitu; wala mashahidi wao wenyewe hawaoni, wala hawajui; ili watahayarike.
10 Ni nani aliyejichongea mungu mmoja, au aliyesubu sanamu isiyofaa kitu?
11 Tazama, wenziwe wote watatahayari; na mafundi, hao ni wanadamu; na wakusanyike pamoja, wakasimame; wataogopa na kutahayari pamoja.
12 Mfua chuma hufanza shoka, hufanya kazi kwa makaa, huitengeneza sanamu kwa nyundo, huifanyiza kwa nguvu za mkono wake; naam, huona njaa, nguvu zake zikampungukia; asipokunywa maji huzimia.
13 Seremala hunyosha uzi; huiandika kwa kalamu ya mate; huitengeneza kwa randa, huiandika kwa bikari, huifanza kwa mfano wa mwanadamu, sawasawa na uzuri wa mwanadamu, ili ikae nyumbani.
14 Yeye hujikatia mierezi, hutwaa mtiriza, na mwaloni, hujichagulia mti mmoja katika miti ya msituni; hupanda mvinje, mvua ikausitawisha.
15 Kisha utamfaa mwanadamu kwa kuni; hutwaa kipande, akaota moto; naam, huuwasha moto, akaoka mkate; naam, huufanya mungu, akauabudu; huifanya sanamu ya kuchonga, akaisujudia.
16 Sehemu moja huiteketeza; kwa sehemu nyingine hula nyama; huoka chakula kiokwacho, akashiba; naam, huota moto, akasema, Aha, nimeota moto, nimeona moto;
17 na kwa sehemu iliyobakia hufanya mungu, yaani, sanamu yake ya kuchonga; husujudu mbele yake akaiabudu, akaiomba, akasema, Uniokoe; maana wewe u mungu wangu.
18 Hawajui wala hawafikiri; maana amewafumba macho, wasione, na mioyo yao, wasiweze kufahamu.
19 Wala hapana atiaye moyoni, wala hapana maarifa, wala fahamu kusema, Nimeteketeza sehemu motoni, naam, pia nimeoka mkate juu ya makaa yake; nimeoka nyama nikaila; nami, je! Kilichobaki nikifanye kuwa chukizo? Je! Nisujudie shina la mti?
20 Hula majivu; moyo uliodanganyika umempotosha, asiweze kuiokoa nafsi yake, wala kusema, Je! Sio uongo mkononi mwangu?
21 Kumbuka haya, Ee Yakobo; nawe Israeli, maana wewe u mtumishi wangu; nimekuumba; u mtumishi wangu; Ee Israeli, hutasahauliwa na mimi.
22 Nimeyafuta makosa yako kama wingu zito, na dhambi zako kama wingu; unirudie; maana nimekukomboa.
23 Imbeni, enyi mbingu, maana Bwana ametenda hayo; Pigeni kelele, enyi mabonde ya nchi; Pazeni nyimbo, enyi milima; Nawe, msitu, na kila mti ndani yake. Maana Bwana amemkomboa Yakobo, Naye atajitukuza katika Israeli.
24 Bwana, mkombozi wako, yeye aliyekuumba tumboni, asema hivi; Mimi ni Bwana, nifanyaye vitu vyote; nizitandaye mbingu peke yangu; niienezaye nchi; ni nani aliye pamoja nami?
25 Nizitanguaye ishara za waongo, na kuwatia waganga wazimu; niwarudishaye nyuma wenye hekima, na kuyageuza maarifa yao kuwa ujinga;
26 nilithibitishaye neno la mtumishi wangu, na kuyafikiliza mashauri ya wajumbe wangu; niuambiaye Yerusalemu, Utakaliwa na watu, nayo miji ya Yuda, Itajengwa, nami nitapainua mahali pake palipobomoka;
27 niviambiaye vilindi, Kauka, nami nitaikausha mito yako;
28 nimwambiaye Koreshi, Mchungaji wangu, naye atayatenda mapenzi yangu; hata ataunena Yerusalemu, Utajengwa; na hilo hekalu, Msingi wako utawekwa.

Isaya 45


1 Haya ndiyo Bwana amwambiayo Koreshi, masihi wake,ambaye nimemshika mkono wake wa kuume,ili kutiisha mataifa mbele yake, nami nitalegeza viuno vya wafalme; ili kufungua milango mbele yake, hata malango hayatafungwa.
2 Nitakwenda mbele yako, na kupasawazisha mahali palipoparuza; nitavunja vipande vipande milango ya shaba, na kukata-kata mapingo ya chuma;
3 nami nitakupa hazina za gizani, na mali zilizofichwa za mahali pa siri, upate kujua ya kuwa mimi ni Bwana, nikuitaye kwa jina lako, naam, Mungu wa Israeli.
4 Kwa ajili ya Yakobo, mtumishi wangu, na Israeli, mteule wangu, nimekuita kwa jina lako; nimekupa jina la sifa; ijapokuwa hukunijua.
5 Mimi ni Bwana, wala hapana mwingine; zaidi yangu mimi hapana Mungu; nitakufunga mshipi ijapokuwa hukunijua;
6 ili wapate kujua toka maawio ya jua, na toka magharibi, ya kuwa hapana mwingine zaidi ya mimi; Mimi ni Bwana, wala hapana mwingine.
7 Mimi naiumba nuru, na kulihuluku giza; mimi nafanya suluhu, na kuhuluku ubaya; Mimi ni Bwana, niyatendaye hayo yote.
8 Dondokeni, enyi mbingu, toka juu, Mawingu na yamwage haki; Nchi na ifunuke, ili kutoa wokovu, Nayo itoe haki ikamee pamoja; Mimi, Bwana, nimeiumba.
9 Ole wake ashindanaye na Muumba wake! Kigae kimoja katika vigae vya dunia! Je! Udongo umwambie yeye aufinyangaye; Unafanya nini? Au kazi yako, Hana mikono?
10 Ole wake amwambiaye baba yake, Wazaa nini? Au mwanamke, Una utungu wa nini?
11 Bwana, Mtakatifu wa Israeli, na Muumba wake, asema hivi; Niulize habari za mambo yatakayokuja; mambo ya wana wangu, na habari ya kazi ya mikono yangu; haya! Niagizeni.
12 Mimi nimeiumba dunia, nimemhuluku mwanadamu juu yake; Mimi, naam, mikono yangu mimi, imezitanda mbingu, na jeshi lake lote nimeliamuru.
13 Mimi nimemwinua katika haki, nami nitazinyosha njia zake zote; ataujenga mji wangu, naye atawaacha huru watu wangu waliohamishwa, si kwa kulipwa fedha, wala kwa kupewa zawadi, asema Bwana wa majeshi.
14 Bwana asema hivi, Kazi ya Misri, na bidhaa ya Kushi, na Waseba, watu walio warefu, watakujilia, nao watakuwa wako; watakufuata; watakuja katika minyororo; wataanguka chini mbele yako, watakuomba, wakisema, Hakika Mungu yu ndani yako; wala hapana mwingine, hapana Mungu tena.
15 Hakika wewe u Mungu ujifichaye nafsi yako, Ee Mungu wa Israeli, Mwokozi.
16 Watatahayarika, naam, watafadhaika, wote pia; wale wafanyao sanamu wataingia fadhaa pamoja.
17 Bali Israeli wataokolewa na Bwana kwa wokovu wa milele; ninyi hamtatahayarika, wala kufadhaika, milele na milele.
18 Maana Bwana, aliyeziumba mbingu, asema hivi; Yeye ni Mungu; ndiye aliyeiumba dunia na kuifanya; ndiye aliyeifanya imara; hakuiumba ukiwa, aliiumba ili ikaliwe na watu; Mimi ni Bwana, wala hapana mwingine.
19 Sikusema kwa siri, katika mahali pa nchi ya giza; sikuwaambia wazao wa Yakobo; Nitafuteni bure; Mimi, Bwana, nasema haki; nanena mambo ya adili.
20 Jikusanyeni mje; na kukaribia pamoja, ninyi wa mataifa mliookoka; hawana maarifa wale wachukuao mti wa sanamu yao ya kuchonga; wamwombao mungu asiyeweza kuokoa.
21 Hubirini, toeni habari; naam, na wafanye mashauri pamoja; ni nani aliyeonyesha haya tangu zamani za kale? Ni nani aliyeyahubiri hapo zamani? Si mimi, Bwana? Wala hapana Mungu zaidi ya mimi; Mungu mwenye haki, mwokozi; hapana mwingine zaidi ya mimi.
22 Niangalieni mimi, mkaokolewe, enyi ncha zote za dunia; maana mimi ni Mungu; hapana mwingine.
23 Kwa nafsi yangu nimeapa, neno hili limetoka kinywani mwangu katika haki, wala halitarudi, ya kwamba mbele zangu kila goti litapigwa, kila ulimi utaapa.
24 Mmoja ataniambia, Kwa Bwana, peke yake, iko haki na nguvu; naam, watu watamwendea yeye, na wote waliomkasirikia watatahayarika.
25 Katika Bwana wazao wote wa Israeli watapewa haki, na kutukuka.

Isaya 46


1 Beli anaanguka chini, Nebo anainama; sanamu zao ziko juu ya wanyama, na juu ya ng'ombe; vitu vile mlivyokuwa mkivichukua huku na huku vimekuwa mzigo, mzigo wa kumlemea mnyama aliyechoka.
2 Wanajiinamisha, wanainama pamoja; hawakuweza kuutua mzigo, bali wao wenyewe wamekwenda kufungwa.
3 Nisikilizeni, enyi wa nyumba ya Yakobo, ninyi mlio mabaki ya nyumba ya Israeli, mliochukuliwa nami tangu tumboni, mlioinuliwa tangu mimbani;
4 na hata uzee wenu mimi ndiye, na hata wakati wenu wa mvi nitawachukueni; nimefanya, nami nitachukua; naam, nitachukua na kuokoa.
5 Mtanifananisha na nani, na kunisawazisha naye, na kunilinganisha naye, ili tuwe sawasawa?
6 Watu wamwagao dhahabu kutoka mfukoni, na kupima fedha katika mizani, huajiri mfua dhahabu, akaifanya mungu; huanguka, naam, huabudu.
7 Humchukua begani, humchukua, wakamsimamisha mahali pake, akasimama; hataondoka katika mahali pake, naam, mmoja atamwita, lakini hawezi kujibu, wala kumwokoa na taabu yake.
8 Kumbukeni haya, mkajionyeshe kuwa waume; jifahamisheni haya, ninyi mkosao;
9 kumbukeni mambo ya zamani za kale; maana mimi ni Mungu, wala hapana mwingine; mimi ni Mungu, wala hapana aliye kama mimi;
10 nitangazaye mwisho tangu mwanzo, na tangu zamani za kale mambo yasiyotendeka bado; nikisema, Shauri langu litasimama, nami nitatenda mapenzi yangu yote.
11 Nikiita ndege mkali kutoka mashariki, mtu wa shauri langu toka nchi iliyo mbali; naam, nimenena, nami nitatekeleza; nimekusudia, nami nitafanya.
12 Nisikilizeni, ninyi mlio na moyo mshupavu, mlio mbali na haki;
13 Mimi ninaleta karibu haki yangu, haitakuwa mbali, na wokovu wangu hautakawia; nami nitaweka wokovu katika Sayuni kwa ajili ya Israeli, utukufu wangu.

Isaya 47


1 Haya, shuka, keti mavumbini, Ewe bikira, binti Babeli; Keti chini pasipo kiti cha enzi, Ewe binti wa Wakaldayo; Maana hutaitwa tena mwororo, mpenda anasa.
2 Twaa mawe ya kusagia, usage unga; Vua utaji wako, ondoa mavazi yako, Funua mguu wako, pita katika mito ya maji.
3 Uchi wako utafunuliwa, Naam, aibu yako itaonekana. Nitalipa kisasi; simkubali mtu ye yote.
4 Mkombozi wetu, Bwana wa majeshi ndilo jina lake, Mtakatifu wa Israeli.
5 Kaa kimya, ingia gizani, Ee binti wa Wakaldayo; Maana hutaitwa tena Malkia wa falme.
6 Nalikuwa nimekasirika na watu wangu, naliutia unajisi urithi wangu, nikawatia mkononi mwako; wewe hukuwatendea rehema; uliwatia wazee nira yako, nayo nzito sana.
7 Ukasema, Mimi nitakuwa bibi milele; hata hukuyatia hayo moyoni mwako, wala hukukumbuka mwisho wa mambo hayo.
8 Sasa, basi, sikia haya, wewe upendaye anasa, ukaaye na kujiona salama, wewe usemaye moyoni mwako, Mimi ndiye, wala hapana mwingine zaidi yangu mimi; sitaketi mfano wa mjane, wala sitajua kufiwa na watoto;
9 lakini mambo haya mawili yatakupata katika dakika moja siku moja, kufiwa na watoto, na ujane; yatakupata kiasi kitimilifu, uchawi wako ujapokuwa mwingi, na uganga wako mwingi mno.
10 Maana umeutumainia ubaya wako; umesema, Hapana anionaye; hekima yako, na maarifa yako yamekupotosha, nawe umesema moyoni mwako, Mimi ndiye, wala hapana mwingine zaidi yangu mimi.
11 Kwa sababu hiyo ubaya utakupata; wala hutajua kutopoa kwake; na msiba utakuangukia; hutaweza kuuondoa; na ukiwa utakupata kwa ghafula, usioujua.
12 Simama sasa na uganga wako, na wingi wa uchawi wako, uliojitaabisha nao tangu ujana wako; labda utaweza kupata faida, labda utaweza kushinda.
13 Umechoka kwa wingi wa mashauri yako; basi, na wasimame hao wajuao falaki, wazitazamao nyota, watabirio kila mwezi mambo ya mwezi huo, wakakuokoe na mambo yatakayokupata.
14 Tazama, watakuwa kama mabua makavu; moto utawateketeza; hawatajiokoa na nguvu za mwali wa moto; hautakuwa kaa la kukota moto, wala moto wa kukaa karibu nao.
15 Ndivyo yatakavyokuwa mambo hayo uliyojitaabisha nayo; wale waliofanya biashara nawe tangu ujana wako watatanga-tanga mbali nawe, kila mtu akienda zake; hapatakuwa na mtu wa kukuokoa.

Isaya 48


1 Sikieni haya, enyi watu wa nyumba ya Yakobo, mnaoitwa kwa jina la Israeli, mliotoka katika maji ya Yuda; mnaoapa kwa jina la Bwana, na kumtaja Mungu wa Israeli, lakini si kwa kweli, wala si kwa haki.
2 Maana hujiita wenyeji wa mji mtakatifu, hujitegemeza juu ya Mungu wa Israeli; Bwana wa majeshi ni jina lake.
3 Mimi nimehubiri mambo ya kale tangu zamani; naam, yalitoka katika kinywa changu, nikayadhihirisha; naliyatenda kwa ghafula, yakatokea.
4 Kwa sababu nalijua ya kuwa wewe u mkaidi, na shingo yako ni shingo ya chuma, na kipaji cha uso wako ni shaba;
5 basi nimekuonyesha tangu zamani; kabla hayajatukia nalikuonyesha; usije ukasema, Sanamu yangu imetenda haya; sanamu yangu ya kuchonga, na sanamu yangu ya kuyeyusha, imeyaamuru.
6 Umesikia haya; tazama haya yote; nanyi, je! Hamtayahubiri? Nimekuonyesha mambo mapya tangu wakati huu, naam, mambo yaliyofichwa, usiyoyajua.
7 Yameumbwa sasa, wala si tokea zamani; na kabla ya siku hii ya leo hukusikia habari yake; usije ukasema, Tazama, naliyajua.
8 Naam, hukusikia; naam, hukujua; naam, tokea zamani sikio lako halikuzibuka; maana nalijua ya kuwa wewe watenda kwa hila nyingi, nawe umeitwa mkosaji tangu kuzaliwa kwako;
9 kwa ajili ya jina langu nitaahirisha hasira yangu, na kwa ajili yako nitajizuia, ili nisifiwe, wala nisikukatilie mbali.
10 Tazama, nimekusafisha, lakini si kama fedha; nimekuchagua katika tanuru ya mateso.
11 Kwa ajili ya nafsi yangu, kwa ajili ya nafsi yangu, nitatenda haya; je! Litiwe unajisi jina langu? Wala sitampa mwingine utukufu wangu.
12 Nisikilize mimi, Ee Yakobo; na Israeli, niliyekuita; mimi ndiye. Mimi ni wa kwanza, na mimi ni wa mwisho pia.
13 Naam, mkono wangu umeuweka msingi wa dunia, na mkono wangu wa kuume umezitanda mbingu; niziitapo husimama pamoja.
14 Kusanyikeni, ninyi nyote, mkasikie; ni nani miongoni mwao aliyehubiri haya? Bwana amempenda; atatimiza mapenzi yake juu ya Babeli, na mkono wake utakuwa juu ya Wakaldayo.
15 Mimi, naam, mimi, nimenena; naam, nimemwita; nimemleta, naye ataifanikisha njia yake.
16 Nikaribieni, sikieni haya; tokea mwanzo sikunena kwa siri; tangu yalipokuwapo, mimi nipo; na sasa Bwana MUNGU amenituma, na roho yake.
17 Bwana, mkombozi wako, mtakatifu wa Israeli, asema hivi; Mimi ni Bwana, Mungu wako, nikufundishaye ili upate faida, nikuongozaye kwa njia ikupasayo kuifuata.
18 Laiti ungalisikiliza amri zangu! Ndipo amani yako ingalikuwa kama mto wa maji, na haki yako kama mawimbi ya bahari;
19 Tena wazao wako wangalikuwa kama mchanga, na hao waliotoka katika tumbo lako kama chembe zake; jina lake lisingalikatika, wala kufutwa mbele zangu.
20 Haya, tokeni katika Babeli, Kimbieni kutoka kwa Wakaldayo; Hubirini kwa sauti ya kuimba, tangazeni haya, Yatamkeni mpaka mwisho wa dunia, semeni, Bwana amemkomboa mtumishi wake, Yakobo.
21 Wala hawakuona kiu alipowaongoza jangwani; Alitoa maji katika mwamba kwa ajili yao; Pia akaupasua mwamba, maji yakatoka kwa nguvu.
22 Hapana amani kwa wabaya, asema Bwana.

Isaya 49


1 Nisikilizeni, enyi visiwa; tegeni masikio yenu, enyi kabila za watu mlio mbali sana; Bwana ameniita tangu tumboni; toka tumbo la mama yangu amenitaja jina langu.
2 Naye anifanya kinywa changu kuwa kama upanga mkali; katika kivuli cha mkono wake amenisitiri; naye amenifanya kuwa mshale uliosuguliwa; katika podo lake amenificha;
3 akaniambia; Wewe u mtumishi wangu, Israeli, ambaye katika wewe nitatukuzwa.
4 Lakini nikasema, Nimejitaabisha bure, nimetumia nguvu zangu bure bila faida; lakini hakika hukumu yangu ina Bwana, na thawabu yangu ina Mungu wangu.
5 Na sasa Bwana asema hivi, yeye aliyeniumba tangu tumboni niwe mtumishi wake, ili nimletee Yakobo tena, na Israeli wakusanyike mbele zake tena; (maana mimi nimepata heshima mbele ya macho ya Bwana, na Mungu wangu amekuwa nguvu zangu);
6 naam, asema hivi, Ni neno dogo sana wewe kuwa mtumishi wangu ili kuziinua kabila za Yakobo, na kuwarejeza watu wa Israeli waliohifadhiwa; zaidi ya hayo nitakutoa uwe nuru ya mataifa, upate kuwa wokovu wangu hata miisho ya dunia.
7 Bwana, mkombozi wa Israeli, Mtakatifu wake, amwambia hivi yeye anayedharauliwa na wanadamu; yeye anayechukiwa na taifa hili; yeye aliye mtumishi wao watawalao; Wafalme wataona, watasimama; wakuu nao watasujudu; kwa sababu ya Bwana aliye mwaminifu, Mtakatifu wa Israeli aliyekuchagua
8 Bwana asema hivi, Wakati uliokubalika nimekujibu, na siku ya wokovu nimekusaidia; nami nitakuhifadhi, nitakutoa uwe agano la watu hawa, ili kuiinua nchi hii, na kuwarithisha urithi uliokuwa ukiwa;
9 kuwaambia waliofungwa, Haya, tokeni; na hao walio katika giza, Jionyesheni. Watajilisha katika njia, na juu ya majabali watapata malisho.
10 Hawataona njaa, wala hawataona kiu; hari haitawapiga, wala jua; kwa maana yeye aliyewarehemu atawatangulia, naam, karibu na chemchemi za maji atawaongoza.
11 Nami nitafanya milima yangu yote kuwa njia, na njia kuu zangu zitatukuzwa zote.
12 Tazama, hawa watakuja kutoka mbali; na tazama, hawa kutoka kaskazini, na kutoka magharibi, na hawa kutoka nchi ya Sinimu.
13 Imbeni, enyi mbingu; ufurahi, Ee nchi; Pazeni sauti ya kuimba, enyi milima; Kwa kuwa Bwana amewafariji watu wake, Naye atawahurumia watu wake walioteswa.
14 Bali Sayuni alisema, YEHOVA ameniacha, Bwana amenisahau.
15 Je! Mwanamke aweza kumsahau mtoto wake anyonyaye, hata asimhurumie mwana wa tumbo lake? Naam, hawa waweza kusahau, lakini mimi sitakusahau wewe.
16 Tazama, nimekuchora katika vitanga vya mikono yangu; kuta zako ziko mbele zangu daima.
17 Watoto wako wafanya haraka, hao wakuharibuo, nao waliokufanya ukiwa, watatoka kwako.
18 Inua macho yako, ukatazame pande zote; hao wote wanajikusanya na kukujia. Kama niishivyo, asema Bwana, hakika utajivika na hao wote, kama kwa uzuri, nawe utajifungia hao, kama bibi arusi.
19 Maana katika habari za mahali pako palipokuwa ukiwa, pasipokaliwa na watu, na nchi yako iliyoharibika hakika sasa utakuwa mwembamba usiwatoshe wenyeji wako, nao waliokumeza watakuwa mbali.
20 Watoto ulionyang'anywa watasema masikioni mwako, Mahali hapa ni pembamba, hapanitoshi; nipe nafasi nipate kukaa.
21 Ndipo utasema moyoni mwako, Ni nani aliyenizalia watoto hawa, na mimi nimefiwa na watoto wangu, nami ni peke yangu, nimehamishwa, ninatanga-tanga huko na huku? Tena ni nani aliyewalea hawa? Tazama, naliachwa peke yangu; hawa je! Walikuwa wapi?
22 Bwana MUNGU asema hivi, Tazama, nitawainulia mataifa mkono wangu, na kuwatwekea kabila za watu bendera yangu; nao wataleta wana wako vifuani mwao, na binti zako watachukuliwa mabegani mwao.
23 Na wafalme watakuwa baba zako za kulea, na malkia zao mama zako za kulea; watainama mbele yako kifudifudi, na kuramba mavumbi ya miguu yako; nawe utajua ya kuwa mimi ni Bwana, tena waningojeao hawatatahayarika.
24 Je! Aliye hodari aweza kunyang'anywa mateka yake, au jeshi lao waliofungwa halali wataokoka?
25 Naam, Bwana asema hivi, Hata jeshi la wafungwa wake aliye hodari watapokonywa mikononi mwake, na mateka yake aliye jabari wataokoka; kwa maana nitateta na yeye atetaye nawe, nami nitawaletea wana wako wokovu.
26 Na hao wanaokuonea nitawalisha nyama yao wenyewe, nao watalewa kwa kuinywa damu yao wenyewe, kama kwa mvinyo mpya; na wote wenye mwili watajua ya kuwa mimi, Bwana, ni mwokozi wako, na Mkombozi wako ni Mwenye enzi wa Yakobo.

Isaya 50


1 Bwana asema hivi, Iko wapi hati ya talaka ya mama yenu, ambayo kwa hiyo naliachana naye? Au nimewauza ninyi kwa nani katika watu wanaoniwia? Ninyi mliuzwa kwa sababu ya maovu yenu; tena mama yenu ameachwa kwa sababu ya makosa yenu.
2 Basi, nilipokuja, mbona hapakuwa na mtu? Nilipoita, mbona hapakuwa na mtu aliyenijibu? Je! Mkono wangu ni mfupi, hata nisiweze kukomboa? Au je! Mimi sina nguvu za kuponya? Tazama, kwa kukemea kwangu naikausha bahari, mito ya maji naifanya kuwa jangwa; samaki wao wanuka kwa sababu hapana maji, nao wafa kwa kiu.
3 Mimi nazivika mbingu weusi, nami nafanya nguo ya magunia kuwa kifuniko chao.
4 Bwana MUNGU amenipa ulimi wa hao wafundishwao, nipate kujua jinsi ya kumtegemeza kwa maneno yeye aliyechoka, huniamsha asubuhi baada ya asubuhi; huniamsha, sikio langu lipate kusikia kama watu wafundishwao.
5 Bwana MUNGU amenizibua sikio langu, wala sikuwa mkaidi, wala sikurudi nyuma.
6 Naliwatolea wapigao mgongo wangu, na wang'oao ndevu mashavu yangu; sikuficha uso wangu usipate fedheha na kutemewa mate.
7 Maana Bwana MUNGU atanisaidia; kwa sababu hiyo sikutahayari, kwa sababu hiyo nimekaza uso wangu kama gumegume, nami najua ya kuwa sitaona haya.
8 Yeye anipatiaye haki yangu yu karibu; ni nani atakayeshindana nami? Na tusimame pamoja; ni nani aliye hasimu yangu? Na anikaribie basi.
9 Tazama, Bwana MUNGU atanisaidia; ni nani atakayenihukumu kuwa mkosa? Tazama hao wote watachakaa kama vazi; nondo atawala.
10 Ni nani miongoni mwenu amchaye Bwana, aitiiye sauti ya mtumishi wake? Yeye aendaye katika giza, wala hana nuru, naye alitumainia jina la Bwana, na kumtegemea Mungu wake.
11 Tazama, ninyi nyote mwashao moto, mjifungiao hiyo mienge; endeni ninyi katika mwali wa moto wenu, na katikati ya mienge mliyoiwasha. Mtayapata haya kwa mkono wangu; mtalala kwa huzuni.

Isaya 51


1 Nisikilizeni, ninyi mnaoifuatia haki; ninyi mnaomtafuta Bwana; uangalieni mwamba ule ambao mlitolewa kwa kuchongwa, na tundu la shimo ambalo mlitolewa kwa kuchimbuliwa.
2 Mwangalieni Ibrahimu, baba yenu, na Sara, aliyewazaa; kwa maana alipokuwa mmoja tu nalimwita, nikambariki, nikamfanya kuwa wengi.
3 Maana Bwana ameufariji Sayuni; amepafariji mahali pake palipokuwa ukiwa; amefanya jangwa lake kuwa kama bustani ya Edeni, na nyika yake kama bustani ya Bwana; furaha na kicheko zitaonekana ndani yake, kushukuru, na sauti ya kuimba.
4 Nisikilizeni mimi, enyi watu wangu; nisikieni, taifa langu; maana sheria itatoka kwangu, nami nitaistarehesha hukumu yangu iwe nuru ya mataifa.
5 Haki yangu i karibu, wokovu wangu umekuwa wazi, na mikono yangu itawahukumu kabila za watu; visiwa vitaningoja, navyo vitautumainia mkono wangu.
6 Inueni macho yenu mbinguni, mkaitazame nchi chini; maana mbingu zitatoweka kama moshi, na nchi itachakaa kama vazi, nao wakaao ndani yake watakufa kadhalika; bali wokovu wangu utakuwa wa milele, na haki yangu haitatanguka.
7 Nisikilizeni, ninyi mjuao haki, watu ambao mioyoni mwenu mna sheria yangu; msiogope matukano ya watu, wala msifadhaike kwa sababu ya dhihaka zao.
8 Maana nondo itawala kama vazi, na funza atawala kama sufu; bali haki yangu itakuwa ya milele, na wokovu wangu hata vizazi vyote.
9 Amka, amka, jivike nguvu, Ee mkono wa Bwana; Amka kama katika siku zile za kale, Katika vizazi vile vya zamani.
10 Si wewe uliyemkata-kata Rahabu? Uliyemchoma yule joka? Si wewe uliyeikausha bahari, Na maji ya vilindi vikuu; Uliyevifanya vilindi kuwa njia, Ili wapite watu waliokombolewa?
11 Nao waliokombolewa na Bwana watarejea, Watafika Sayuni, wakiimba; Furaha ya milele itakuwa juu ya vichwa vyao; Watapata shangwe na furaha; Huzuni na kuugua zitakimbia.
12 Mimi, naam, mimi, ndimi niwafarijiye; wewe u nani hata ukamwogopa mtu atakayekufa, na mwanadamu atakayefanywa kuwa kama majani?
13 Ukamsahau Bwana, Muumba wako, yeye aliyezitanda mbingu, na kuiweka misingi ya dunia; nawe unaogopa daima mchana kutwa kwa sababu ya ghadhabu yake yeye aoneaye, hapo afanyapo tayari kuharibu; nayo i wapi ghadhabu yake aoneaye?
14 Yeye aliyehamishwa na kufungwa atafunguliwa kwa haraka; wala hatakufa na kushuka shimoni, wala chakula chake hakitapunguka.
15 Maana mimi ni Bwana, Mungu wako, niichafuaye bahari, mawimbi yake yakavuma.
16 Bwana wa majeshi ndilo jina lake. Nami nimetia maneno yangu kinywani mwako, nami nimekusitiri katika kivuli cha mkono wangu, ili nizipande mbingu, na kuiweka misingi ya dunia, na kuuambia Sayuni, Ninyi ni watu wangu.
17 Amka, amka, simama, Ee Yerusalemu, Wewe uliyenywea, mkononi mwa Bwana, Kikombe cha hasira yake; Bakuli la kikombe cha kulevya-levya Umelinywea na kulimaliza.
18 Hapana hata mmoja wa kumwongoza Miongoni mwa wana wote aliowazaa, Wala hapana hata mmoja wa kumshika mkono Miongoni mwa wana wote aliowalea.
19 Mambo haya mawili yamekupata; Ni nani awezaye kukusikitikia? Ukiwa na uharibifu, na njaa na upanga; Niwezeje kukutuliza?
20 Wana wako wamezimia, Wamelala penye pembe za njia kuu zote Kama kulungu wavuni; Wamejaa hasira ya Bwana, Lawama ya Mungu wako.
21 Basi, kwa sababu ya hayo, ulisikilize neno hili, ewe uliyeteswa, na kulewa, lakini si kwa mvinyo;
22 Bwana, Bwana wako na Mungu wako, awateteaye watu wake, asema hivi, Tazama, nimeondoa mkononi mwako kikombe cha kulevya-levya, hilo bakuli la kikombe cha hasira yangu; hutakinywea tena;
23 nami nitakitia mikononi mwao wakutesao; waliokuambia nafsi yako, Inama, tupate kupita; nawe uliufanya mgongo wako kuwa kama nchi, na kama njia, kwa hao wapitao juu yake.

Isaya 52


1 Amka, amka, jivike nguvu zako, Ee Sayuni; Jivike mavazi yako mazuri, Ee Yerusalemu, mji mtakatifu; Kwa maana tokea sasa hataingia ndani yako Asiyetahiriwa, wala aliye najisi.
2 Jikung'ute mavumbi; uondoke, Uketi, Ee Yerusalemu; Jifungulie vifungo vya shingo yako, Ee binti Sayuni uliyefungwa.
3 Maana Bwana asema hivi, Mliuzwa bure; nanyi mtakombolewa bila fedha.
4 Maana Bwana MUNGU asema hivi, Watu wangu hapo kwanza walishuka Misri ili wakae huko hali ya ugeni; na Mwashuri akawaonea bila sababu.
5 Basi sasa, nafanya nini hapa, asema Bwana, ikiwa watu wangu wamechukuliwa bure? Hao wanaowatawala wanapiga yowe, asema Bwana, na jina langu linatukanwa daima mchana kutwa.
6 Kwa hiyo watu wangu watalijua jina langu kwa hiyo watajua siku ile ya kuwa mimi ndimi ninenaye; tazama ni mimi.
7 Jinsi ilivyo mizuri juu ya milima Miguu yake aletaye habari njema, Yeye aitangazaye amani, Aletaye habari njema ya mambo mema, Yeye autangazaye wokovu, Auambiaye Sayuni, Mungu wako anamiliki!
8 Sauti ya walinzi wako! Wanapaza sauti zao, wanaimba pamoja; Maana wataona jicho kwa jicho, Jinsi Bwana arejeavyo Sayuni.
9 Pigeni kelele za furaha, imbeni pamoja, Enyi mahali pa Yerusalemu palipokuwa ukiwa; Kwa kuwa Bwana amewafariji watu wake, Ameukomboa Yerusalemu.
10 Bwana ameweka wazi mkono wake mtakatifu Machoni pa mataifa yote; Na ncha zote za dunia Zitauona wokovu wa Mungu wetu.
11 Nendeni zenu, nendeni zenu, tokeni huko, msiguse kitu kichafu; tokeni kati yake; iweni safi ninyi mnaochukua vyombo vya Bwana.
12 Maana hamtatoka kwa haraka, wala hamtakwenda kwa kukimbia, kwa sababu Bwana atawatangulia; na Mungu wa Israeli atawafuata nyuma; awalinde.
13 Tazama, mtumishi wangu atatenda kwa busara, atatukuzwa, na kuinuliwa juu, naye atakuwa juu sana.
14 Kama vile wengi walivyokustaajabia, (uso wake ulikuwa umeharibiwa sana zaidi ya mtu ye yote, na umbo lake zaidi ya wanadamu),
15 ndivyo atakavyowasitusha mataifa mengi; wafalme watamfumbia vinywa vyao; maana mambo wasiyoambiwa watayaona; na mambo wasiyoyasikia watayafahamu.

Isaya 53


1 Ni nani aliyesadiki habari tuliyoileta? Na mkono wa Bwana amefunuliwa nani?
2 Maana alikua mbele zake kama mche mwororo, Na kama mzizi katika nchi kavu; Yeye hana umbo wala uzuri; Na tumwonapo hana uzuri hata tumtamani.
3 Alidharauliwa na kukataliwa na watu; Mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko; Na kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao, Alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu.
4 Hakika ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa, Amepigwa na Mungu, na kuteswa.
5 Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.
6 Sisi sote kama kondoo tumepotea; Kila mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyewe; Na Bwana ameweka juu yake Maovu yetu sisi sote.
7 Alionewa, lakini alinyenyekea, Wala hakufunua kinywa chake; Kama mwana-kondoo apelekwaye machinjoni, Na kama vile kondoo anyamazavyo Mbele yao wakatao manyoya yake; Naam, hakufunua kinywa chake.
8 Kwa kuonewa na kuhukumiwa aliondolewa; Na maisha yake ni nani atakayeisimulia? Maana amekatiliwa mbali na nchi ya walio hai; Alipigwa kwa sababu ya makosa ya watu wangu.
9 Wakamfanyia kaburi pamoja na wabaya; Na pamoja na matajiri katika kufa kwake; Ingawa hakutenda jeuri, Wala hapakuwa na hila kinywani mwake.
10 Lakini Bwana aliridhika kumchubua; Amemhuzunisha; Utakapofanya nafsi yake kuwa dhabihu kwa dhambi, Ataona uzao wake, ataishi siku nyingi, Na mapenzi ya Bwana yatafanikiwa mkononi mwake;
11 Ataona mazao ya taabu ya nafsi yake, na kuridhika. Kwa maarifa yake mtumishi wangu mwenye haki Atawafanya wengi kuwa wenye haki; Naye atayachukua maovu yao.
12 Kwa hiyo nitamgawia sehemu pamoja na wakuu, Naye atagawanya nyara pamoja nao walio hodari; Kwa sababu alimwaga nafsi yake hata kufa, Akahesabiwa pamoja na hao wakosao. Walakini alichukua dhambi za watu wengi, Na kuwaombea wakosaji.

Isaya 54


1 Imba, wewe uliye tasa, wewe usiyezaa; paza sauti yako kwa kuimba, piga kelele, wewe usiyekuwa na utungu; maana watoto wake aliyeachwa ni wengi kuliko watoto wake yeye aliyeolewa, asema Bwana.
2 Panua mahali pa hema yako, na wayatandaze mapazia ya maskani yako; usiwakataze; ongeza urefu wa kamba zako; vikaze vigingi vya hema yako.
3 Kwa maana utaenea upande wa kuume na upande wa kushoto; na wazao wako watawamiliki mataifa; wataifanya miji iliyokuwa ukiwa kukaliwa na watu.
4 Usiogope; maana hutatahayarika; wala usifadhaike; maana hutaaibishwa; kwa kuwa utaisahau aibu ya ujana wako, pia mashutumu ya ujane wako hutayakumbuka tena.
5 Kwa sababu Muumba wako ni mume wako; Bwana wa majeshi ndilo jina lake; na Mtakatifu wa Israeli ndiye Mkombozi wako; Yeye ataitwa Mungu wa dunia yote.
6 Maana Bwana amekuita kama mke aliyeachwa na kuhuzunishwa rohoni, kama mke wakati wa ujana, atupwapo, asema Mungu wako.
7 Kwa kitambo kidogo nimekuacha; lakini kwa rehema nyingi nitakukusanya.
8 Kwa ghadhabu ifurikayo nalikuficha uso wangu dakika moja; lakini kwa fadhili za milele nitakurehemu, asema Bwana, Mkombozi wako.
9 Kwa maana jambo hili limekuwa kama maji ya Nuhu kwangu; maana kama nilivyoapa ya kwamba maji ya Nuhu hayatapita juu ya dunia tena, kadhalika nimeapa ya kwamba sitakuonea hasira, wala kukukemea.
10 Maana milima itaondoka, na vilima vitaondolewa; bali wema wangu hautaondoka kwako, wala agano langu la amani halitaondolewa; asema Bwana akurehemuye.
11 Ewe uliyeteswa, uliyerushwa na tufani, usiyetulizwa, tazama, nitaweka mawe yako kwa rangi nzuri, nitaweka misingi yako kwa yakuti samawi.
12 Nami nitaifanya minara yako ya akiki nyekundu, na malango yako ya almasi, na mipaka yako yote ya mawe yapendezayo.
13 Na watoto wako wote watafundishwa na Bwana; na amani ya watoto wako itakuwa nyingi.
14 Utathibitika katika haki; utakuwa mbali na kuonewa, kwa maana hutaogopa; na mbali na hofu, kwa maana haitakukaribia.
15 Tazama, yamkini watakusanyana; lakini si kwa shauri langu. Watu wo wote watakaokusanyana juu yako wataanguka kwa ajili yako.
16 Tazama, nimemwumba mhunzi avukutaye moto wa makaa, akatoa silaha kwa kazi yake; nami nimemwumba mharibu ili aharibu.
17 Kila silaha itakayofanyika juu yako haitafanikiwa na kila ulimi utakaoinuka juu yako katika hukumu utauhukumu kuwa mkosa. Huu ndio urithi wa watumishi wa Bwana, na haki yao inayotoka kwangu mimi, asema Bwana.

Isaya 55


1 Haya, kila aonaye kiu, njoni majini, Naye asiye na fedha; njoni, nunueni mle; Naam, njoni, nunueni divai na maziwa, Bila fedha na bila thamani.
2 Kwani kutoa fedha kwa ajili ya kitu ambacho si chakula? Na mapato yenu kwa kitu kisichoshibisha? Nisikilizeni kwa bidii, mle kilicho chema, Na kujifurahisha nafsi zenu kwa unono.
3 Tegeni masikio yenu, na kunijia; Sikieni, na nafsi zenu zitaishi; Nami nitafanya nanyi agano la milele, Naam, rehema za Daudi zilizo imara.
4 Angalieni, nimemweka kuwa shahidi kwa kabila za watu; kuwa kiongozi na jemadari kwa kabila za watu.
5 Tazama, utaita taifa usilolijua, na taifa lisilokujua wewe litakukimbilia, kwa sababu ya Bwana, Mungu wako, na kwa ajili yake Mtakatifu wa Israeli; maana amekutukuza.
6 Mtafuteni Bwana, maadamu anapatikana, Mwiteni, maadamu yu karibu;
7 Mtu mbaya na aache njia yake, Na mtu asiye haki aache mawazo yake; Na amrudie Bwana, Naye atamrehemu; Na arejee kwa Mungu wetu, Naye atamsamehe kabisa.
8 Maana mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu; asema Bwana.
9 Kwa maana kama vile mbingu zilivyo juu sana kuliko nchi, kadhalika njia zangu zi juu sana kuliko njia zenu, na mawazo yangu kuliko mawazo yenu.
10 Maana kama vile mvua ishukavyo, na theluji, kutoka mbinguni, wala hairudi huko; bali huinywesha ardhi, na kuizalisha na kuichipuza, ikampa mtu apandaye mbegu, na mtu alaye chakula;
11 ndivyo litakavyokuwa neno langu, litokalo katika kinywa changu; halitanirudia bure, bali litatimiza mapenzi yangu, nalo litafanikiwa katika mambo yale niliyolituma.
12 Maana mtatoka kwa furaha, Mtaongozwa kwa amani; Mbele yenu milima na vilima vitatoa nyimbo; Na miti yote ya kondeni itapiga makofi.
13 Badala ya michongoma utamea msunobari, Na badala ya mibigili, mhadesi; Jambo hili litakuwa la kumpatia Bwana jina, Litakuwa ishara ya milele isiyokatiliwa mbali.

Isaya 56


1 Bwana asema hivi, Shikeni hukumu, mkatende haki; kwa maana wokovu wangu u karibu kuja, na haki yangu kufunuliwa.
2 Heri afanyaye haya, na mwanadamu ayashikaye sana; azishikaye sabato asizivunje, auzuiaye mkono wake usifanye uovu wo wote.
3 Wala mgeni, aambatanaye na Bwana, asiseme hivi, Hakika yake Bwana atanitenga na watu wake; wala towashi asiseme, Mimi ni mti mkavu.
4 Kwa maana Bwana awaambia hivi matowashi, wanaozishika sabato zangu, na kuyachagua mambo yanipendezayo, na kulishika sana agano langu;
5 Nitawapa hawa nyumbani mwangu, na ndani ya kuta zangu, kumbukumbu na jina, lililo jema kuliko kuwa na wana na binti; nitawapa jina lidumulo milele, lisilokatiliwa mbali.
6 Na wageni, walioandamana na Bwana ili wamhudumu, na kulipenda jina la Bwana, kuwa watumishi wake; kila aishikaye sabato asiivunje, na kulishika sana agano langu;
7 Nitawaleta hao nao hata mlima wangu mtakatifu, na kuwafurahisha katika nyumba yangu ya sala; makafara yao na dhabihu zao zitakubaliwa juu ya madhabahu zangu; kwa maana nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote.
8 Bwana MUNGU, akusanyaye waliofukuzwa katika Israeli asema, Pamoja na hayo nitamkusanyia na wengine, zaidi ya hao walio wake waliokusanywa.
9 Enyi hayawani wote wa nyikani, njoni, Mle, enyi hayawani wote wa mwituni.
10 Walinzi wake ni vipofu, wote pia hawana maarifa; wote ni mbwa walio bubu, hawawezi kulia; huota ndoto, hulala, hupenda usingizi.
11 Naam, mbwa hao wana choyo sana, hawashibi kamwe; na hao ni wachungaji wasioweza kufahamu neno; wote pia wamegeuka upande, wazifuate njia zao wenyewe, kila mmoja kwa faida yake, toka pande zote.
12 Husema, Njoni, nitaleta divai, Na tunywe sana kileo; Na kesho itakuwa kama leo, Sikukuu kupita kiasi.

Isaya 57


1 Mwenye haki hupotea, wala hakuna atiaye hayo moyoni; na watu watauwa huondolewa, wala hakuna afikiriye ya kuwa mwenye haki ameondolewa asipatikane na mabaya.
2 Yeye huingia katika amani; wao hustarehe katika vitanda vyao, kila mtu aendaye katika unyofu wake.
3 Lakini ninyi karibuni hapa, enyi wana wa mwanamke mchawi, uzao wa mzinzi na kahaba.
4 Mnafanya dhihaka yenu juu ya nani? Mmepanua vinywa vyenu, na kutoa ndimi zenu? Je, ninyi si wana wa uasi, uzao wa uongo;
5 ninyi mnaowasha tamaa zenu kati ya mialoni, chini ya kila mti wenye majani mabichi; ninyi mnaoua watoto mabondeni, chini ya mianya ya majabali?
6 Sehemu yako i katika makokoto ya bonde; hayo ndiyo kura yako; umeyamwagia hayo sadaka ya kinywaji, umeyatolea sadaka ya unga; je! Niwe radhi na mambo hayo?
7 Umeweka kitanda chako juu ya mlima mrefu ulioinuka sana; ukaenda huko ili kutoa dhabihu.
8 Na nyuma ya milango na miimo umeweka kumbukumbu lako; kwa maana umejifunua nafsi yako kwa ajili ya mwingine, si kwa ajili yangu, ukakwea juu; umekipanua kitanda chako, nawe umefanya maagano na hao; ulikipenda kitanda chao hapo ulipokiona.
9 Ulimwendea mfalme na mafuta ya marhamu, ukaongeza manukato yako, ukawatuma wajumbe wako waende mbali, ukajidhili sana hata kuzimu.
10 Ulikuwa umechoka kwa ajili ya urefu wa njia yako; lakini hukusema, Hapana matumaini; ulipata kuhuishwa nguvu zako; kwa sababu hiyo hukuugua.
11 Tena ni nani uliyemwogopa na kumhofu, hata ukasema uongo, wala hukunikumbuka mimi, wala kuweka hayo moyoni? Je! Mimi sikunyamaza tangu zamani, hata huniogopi?
12 Mimi nitatangaza haki yako, na matendo yako hayatakufaa.
13 Utakapolia, na wakuponye hao uliowakusanya; lakini upepo utawachukua; uvuvio tu utawachukulia mbali; lakini yeye anayenitumaini ataimiliki nchi, na kuurithi mlima wangu mtakatifu.
14 Naye atasema, Tutieni, tutieni, Itengenezeni njia, Kiondoeni kila kikwazacho Katika njia ya watu wangu.
15 Maana yeye aliye juu, aliyetukuka, akaaye milele; ambaye jina lake ni Mtakatifu; asema hivi; Nakaa mimi mahali palipoinuka, palipo patakatifu; tena pamoja na yeye aliye na roho iliyotubu na kunyenyekea, ili kuzifufua roho za wanyenyekevu, na kuifufua mioyo yao waliotubu.
16 Kwa kuwa sitashindana na watu siku zote, wala sitakuwa na hasira siku zote; maana roho ingezimia mbele zangu, na hizo nafsi nilizozifanya.
17 Kwa sababu ya uovu wa kutamani kwake naliona hasira, nikampiga; nalificha uso wangu, nikaona ghadhabu; naye akaendelea kwa ukaidi, kuifuata njia ya moyo wake mwenyewe.
18 Nimeziona njia zake; nami nitamponya; nitamwongoza pia, nitamrudishia faraja zake, yeye na hao wanaomlilia.
19 Mimi nayaumba matunda ya midomo; Amani, amani, kwake yeye aliye mbali, na kwake yeye aliye karibu; asema Bwana; nami nitamponya.
20 Bali wabaya wanafanana na bahari iliyochafuka; maana haiwezi kutulia, na maji yake hutoa tope na takataka.
21 Hapana amani kwa wabaya; asema Mungu wangu.

Isaya 58


1 Piga kelele, usiache, Paza sauti yako kama tarumbeta; Uwahubiri watu wangu kosa lao, Na nyumba ya Yakobo dhambi zao.
2 Walakini wanitafuta kila siku; hupenda kujua njia zangu; kama vile taifa waliotenda haki, wasioacha sheria ya Mungu wao, hutaka kwangu amri za haki; hufurahi kumkaribia Mungu.
3 Husema, Mbona tumefunga, lakini huoni? Mbona tumejitaabisha nafsi zetu, lakini huangalii? Fahamuni, siku ya kufunga kwenu mnatafuta anasa zenu wenyewe, na kuwalemea wote watendao kazi kwenu.
4 Tazama, ninyi mwafunga mpate kushindana na kugombana, na kupiga kwa ngumi ya uovu. Hamfungi siku hii ya leo hata kuisikizisha sauti yenu juu.
5 Je! Kufunga namna hii ni saumu niliyoichagua mimi? Je! Ni siku ya mtu kujitaabisha nafsi yake? Ni kuinama kichwa kama unyasi, na kutanda nguo za magunia na majivu chini yake? Je! Utasema ni siku ya kufunga, na ya kukubaliwa na Bwana?
6 Je! Saumu niliyoichagua, siyo ya namna hii? Kufungua vifungo vya uovu, kuzilegeza kamba za nira, kuwaacha huru walioonewa, na kwamba mvunje kila nira?
7 Je! Siyo kuwagawia wenye njaa chakula chako, na kuwaleta maskini waliotupwa nje nyumbani kwako? Umwonapo mtu aliye uchi, umvike nguo; wala usijifiche na mtu mwenye damu moja nawe?
8 Ndipo nuru yako itakapopambazuka kama asubuhi, na afya yako itatokea mara; na haki yako itakutangulia; utukufu wa Bwana utakufuata nyuma ukulinde.
9 Ndipo utaita, na Bwana ataitika; utalia, naye atasema, Mimi hapa. Kama ukiiondoa nira; isiwepo kati yako, wala kunyosha kidole, wala kunena maovu;
10 na kama ukimkunjulia mtu mwenye njaa nafsi yako, na kuishibisha nafsi iliyoteswa; ndipo nuru yako itakapopambazuka gizani; na kiwi chako kitakuwa kama adhuhuri.
11 Naye Bwana atakuongoza daima, ataishibisha nafsi yako mahali pasipokuwa na maji, na kuitia nguvu mifupa yako; nawe utakuwa kama bustani iliyotiwa maji, na kama chemchemi ambayo maji yake hayapungui.
12 Na watu wako watapajenga mahali palipokuwa ukiwa; utaiinua misingi ya vizazi vingi; nawe utaitwa, Mwenye kutengeneza mahali palipobomoka; na, Mwenye kurejeza njia za kukalia.
13 Kama ukigeuza mguu wako usihalifu sabato, usifanye anasa yako siku ya utakatifu wangu; ukiita sabato siku ya furaha, na siku takatifu ya Bwana yenye heshima; ukiitukuza, kwa kutokuzifanya njia zako mwenyewe, wala kuyatafuta yakupendezayo, wala kusema maneno yako mwenyewe;
14 ndipo utakapojifurahisha katika Bwana; nami nitakupandisha mahali pa nchi palipoinuka; nitakulisha urithi wa Yakobo baba yako; kwa maana kinywa cha Bwana kimenena hayo.

Isaya 59


1 Tazama, mkono wa Bwana haukupunguka, hata usiweze kuokoa wala sikio lake si zito, hata lisiweze kusikia;
2 lakini maovu yenu yamewafarikisha ninyi na Mungu wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia.
3 Kwa maana mikono yenu imetiwa unajisi kwa damu, na vidole vyenu vimetiwa unajisi kwa uovu; midomo yenu imenena uongo, ndimi zenu zimenong'ona ubaya.
4 Hapana adaiye kwa haki, wala hapana atetaye kwa kweli; hutumainia ubatili, hunena uongo; hupata mimba ya madhara, na kuzaa uovu.
5 Huangua mayai ya fira, na kusuka wavu wa buibui; yeye alaye mayai yao hufa, na hilo livunjwalo hutoka nyoka.
6 Nyavu zao hazitakuwa mavazi, wala hawatajifunika kwa kazi zao; kazi zao ni kazi za uovu, na vitendo vya udhalimu vimo mikononi mwao.
7 Miguu yao hukimbilia mabaya, nao hufanya haraka kumwaga damu isiyo na hatia; mawazo yao ni mawazo ya uovu; ukiwa na uharibifu zaonekana katika njia kuu zao.
8 Njia ya amani hawaijui; wala hapana hukumu ya haki katika miendo yao; wamejifanyizia njia zilizopotoka; kila apitaye katika njia hizo hajui amani.
9 Kwa sababu hiyo hukumu ya haki i mbali nasi, wala haki haitufikilii; twatazamia nuru, na kumbe! Latokea giza; twatazamia mwanga, lakini twaenda katika giza kuu.
10 Twapapasa-papasa kutafuta ukuta kama kipofu, naam, twapapasa kama watu wasio na macho; twajikwaa wakati wa adhuhuri, kana kwamba ni wakati wa ukungu wa alfajiri; kati yao waliowanda tumekuwa kama wafu.
11 Sisi sote twanguruma kama dubu; twaomboleza kama hua; twatazamia hukumu ya haki, lakini hapana; na wokovu, lakini u mbali nasi.
12 Maana makosa yetu yamezidi kuwa mengi mbele zako, na dhambi zetu zashuhudia juu yetu; maana makosa yetu tunayo pamoja nasi, na maovu yetu tumeyajua;
13 katika kukosa na kumkana Bwana, na katika kugeuka tusimfuate Mungu wetu, tukinena jeuri na uasi, na kukusudia maneno ya uongo na kuyatoa moyoni.
14 Na hukumu imegeuka ikaenda nyuma, na haki inasimama mbali sana; maana kweli imeanguka katika njia kuu, na unyofu hauwezi kuingia.
15 Naam, kweli imepunguka kabisa, na yeye auachaye uovu ajifanya kuwa mateka; naye Bwana akaona hayo, akachukizwa kwa kuwa hapana hukumu ya haki.
16 Akaona ya kuwa hapana mtu, akastaajabu kwa kuwa hapana mwombezi; basi, mkono wake mwenyewe ndio uliomletea wokovu; na haki yake ndiyo iliyomsaidia.
17 Akajivika haki kama deraya kifuani, na chapeo cha wokovu kichwani pake, akajivika mavazi ya kisasi yawe mavazi yake, naye alivikwa wivu kama joho.
18 Kadiri ya matendo yao, kwa kadiri iyo hiyo atawalipa, ukali kwao wampingao, malipo kwa adui zake; naye atavirudishia visiwa malipo.
19 Basi, wataliogopa jina la Bwana toka magharibi, na utukufu wake toka maawio ya jua; maana yeye atakuja kama mkondo wa mto ufurikao, uendeshwao kwa pumzi ya Bwana.
20 Na Mkombozi atakuja Sayuni, kwao waachao maasi yao katika Yakobo, asema Bwana.
21 Tena katika habari zangu, hili ndilo agano langu nao, asema Bwana; roho yangu iliyo juu yako, na maneno yangu niliyoyatia kinywani mwako, hayataondoka kinywani mwako, wala kinywani mwa wana wako, wala kinywani mwa wajukuu wako, asema Bwana, tangu leo na hata milele.

Isaya 60


1 Ondoka, uangaze; kwa kuwa nuru yako imekuja, Na utukufu wa Bwana umekuzukia.
2 Maana, tazama, giza litaifunika dunia, Na giza kuu litazifunika kabila za watu; Bali Bwana atakuzukia wewe, Na utukufu wake utaonekana juu yako.
3 Na mataifa wataijilia nuru yako, Na wafalme kuujia mwanga wa kuzuka kwako.
4 Inua macho yako, utazame pande zote; Wote wanakusanyana; wanakujia wewe; Wana wako watakuja kutoka mbali. Na binti zako watabebwa nyongani.
5 Ndipo utakapoona na kutiwa nuru, Na moyo wako utatetemeka na kukunjuka; Kwa kuwa wingi wa bahari utageuzwa kukujia, Utajiri wa mataifa utakuwasilia.
6 Wingi wa ngamia utakufunika, Ngamia vijana wa Midiani na Efa; Wote watakuja kutoka Sheba; Wataleta dhahabu na uvumba; Na kuzitangaza sifa za Bwana.
7 Makundi yote ya Kedari yatakusanyika kwako, Kondoo waume wa Nebayothi watakutumikia; Watapanda juu ya madhabahu yangu kwa kibali, Nami nitaitukuza nyumba ya utukufu wangu.
8 Ni nani hawa warukao kama wingu, Na kama njiwa waendao madirishani kwao?
9 Hakika yake visiwa vitaningojea, Na merikebu za Tarshishi kwanza, Ili kuleta wana wako kutoka mbali, Na fedha yao na dhahabu yao pamoja nao, Kwa ajili ya jina la Bwana, Mungu wako, Kwa ajili yake Mtakatifu wa Israeli, Kwa kuwa amekutukuza wewe.
10 Na wageni watajenga kuta zako, Na wafalme wao watakuhudumu; Maana katika ghadhabu yangu nalikupiga, Lakini katika upendeleo wangu nimekurehemu.
11 Malango yako nayo yatakuwa wazi daima; Hayatafungwa mchana wala usiku; Ili watu wapate kukuletea utajiri wa mataifa, Na wafalme wao wakiongozwa pamoja nao.
12 Kwa maana kila taifa na ufalme wa watu Wasiotaka kukutumikia wataangamia; Naam, mataifa hayo wataharibiwa kabisa.
13 Utukufu wa Lebanoni utakujia wewe, Mberoshi na mtidhari na mteashuri pamoja; Ili kupapamba mahali pangu patakatifu, Nami nitapatukuza mahali pa miguu yangu.
14 Na wana wa watu wale waliokutesa Watakuja kwako na kukuinamia; Nao wote waliokudharau Watajiinamisha hata nyayo za miguu yako; Nao watakuita, Mji wa Bwana, Sayuni wa Mtakatifu wa Israeli.
15 Na kwa kuwa umeachwa na kuchukiwa, Hata ikawa hapana mtu aliyepita ndani yako, Nitakufanya kuwa fahari ya milele, Furaha ya vizazi vingi.
16 Utanyonya maziwa ya mataifa, Utanyonya matiti ya wafalme; Nawe utajua ya kuwa mimi, Bwana, ni mwokozi wako, Na mkombozi wako, Mwenye enzi wa Yakobo.
17 Badala ya shaba nitaleta dhahabu, Na badala; ya chuma nitaleta fedha, Na badala ya mti, shaba, Na badala ya mawe, chuma; Tena nitawafanya wasimamizi wako wawe amani, Na hao wakutozao fedha kuwa haki.
18 Jeuri haitasikiwa tena katika nchi yako, Ukiwa na uharibifu hazitakuwa mipakani mwako; Bali utaziita kuta zako, Wokovu, Na malango yako, Sifa.
19 Jua halitakuwa nuru yako tena wakati wa mchana, Wala mwezi hautakupa nuru kwa mwangaza wake; Bali Bwana atakuwa nuru ya milele kwako, Na Mungu wako atakuwa utukufu wako.
20 Jua lako halitashuka tena, Wala mwezi wako hautajitenga; Kwa kuwa Bwana mwenyewe atakuwa nuru yako ya milele; Na siku za kuomboleza kwako zitakoma.
21 Watu wako nao watakuwa wenye haki wote, Nao watairithi nchi milele;
22 Mdogo atakuwa elfu, Na mnyonge atakuwa taifa hodari; Mimi, Bwana, nitayahimiza hayo wakati wake.

Isaya 61


1 Roho ya Bwana MUNGU i juu yangu; kwa sababu Bwana amenitia mafuta niwahubiri wanyenyekevu habari njema; amenituma ili kuwaganga waliovunjika moyo, kuwatangazia mateka uhuru wao, na hao waliofungwa habari za kufunguliwa kwao.
2 Kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa, na siku ya kisasi cha Mungu wetu; kuwafariji wote waliao;
3 kuwaagizia hao waliao katika Sayuni, wapewe taji ya maua badala ya majivu, mafuta ya furaha badala ya maombolezo, vazi la sifa badala ya roho nzito; wapate kuitwa miti ya haki, iliyopandwa na Bwana, ili atukuzwe.
4 Nao watajenga mahali pa kale palipoharibiwa, watapainua mahali palipokuwa ukiwa zamani, watatengeneza miji iliyoharibiwa, mahali palipoachwa kizazi baada ya kizazi.
5 Na wageni watasimama na kulisha makundi yenu, na watu wa kabila nyingine watakuwa wakulima wenu, na watunzaji wa mizabibu yenu.
6 Bali ninyi mtaitwa makuhani wa Bwana; watu watawaiteni wahudumu wa Mungu wetu; mtakula utajiri wa mataifa, na kujisifia utukufu wao.
7 Badala ya aibu yenu mtapata maradufu, na badala ya fedheha wataifurahia sehemu yao; basi katika nchi yao watamiliki maradufu; furaha yao itakuwa ya milele.
8 Maana mimi, Bwana, naipenda hukumu ya haki, nauchukia wivi na uovu; nami nitawalipa malipo katika kweli, nitaagana nao agano la milele.
9 Na kizazi chao kitajulikana katika mataifa, na uzao wao katika kabila za watu; wote wawaonao watakiri ya kuwa wao ni kizazi kilichobarikiwa na Bwana.
10 Nitafurahi sana katika Bwana, nafsi yangu itashangilia katika Mungu wangu; maana amenivika mavazi ya wokovu, amenifunika vazi la haki, kama bwana arusi ajipambavyo kwa kilemba cha maua, na kama bibi arusi ajipambavyo kwa vyombo vya dhahabu.
11 Maana kama nchi itoavyo machipuko yake, na kama bustani ioteshavyo vitu vilivyopandwa ndani yake; ndivyo Bwana MUNGU atakavyootesha haki na sifa mbele ya mataifa yote.

Isaya 62


1 Kwa ajili ya Sayuni sitanyamaza, na kwa ajili ya Yerusalemu sitatulia, hata haki yake itakapotokea kama mwangaza, na wokovu wake kama taa iwakayo.
2 Na mataifa wataiona haki yako, na wafalme wote watauona utukufu wako; nawe utaitwa jina jipya, litakalotajwa na kinywa cha Bwana.
3 Nawe utakuwa taji ya uzuri katika mkono wa Bwana, na kilemba cha kifalme mkononi mwa Mungu wako.
4 Hutaitwa tena Aliyeachwa, wala nchi yako haitaitwa tena, Ukiwa; bali utaitwa Hefsiba; na nchi yako Beula;kwa kuwa Bwana anakufurahia ,na nchi yako itaolewa.
5 Maana kama vile kijana amwoavyo mwanamwali, ndivyo wana wako watakavyokuoa wewe; na kama vile bwana arusi amfurahiavyo bibi arusi, ndivyo Mungu wako atakavyokufurahia wewe.
6 Nimeweka walinzi juu ya kuta zako, Ee Yerusalemu; hawatanyamaza mchana wala usiku; ninyi wenye kumkumbusha Bwana, msiwe na kimya;
7 wala msimwache akae kimya, mpaka atakapoufanya imara Yerusalemu, na kuufanya kuwa sifa duniani.
8 Bwana ameapa kwa mkono wake wa kuume, na kwa mkono wa nguvu zake, Hakika sitawapa adui zako nafaka yako tena kuwa chakula chao; wala wageni hawatakunywa divai yako, uliyoifanyia kazi.
9 Lakini walioivuna, ndio watakaoila, na kumhimidi Bwana; na walioichuma, ndio watakaoinywa, ndani ya nyua za patakatifu pangu.
10 Piteni, piteni, katika malango; Itengenezeni njia ya watu; Tutieni, tutieni barabara; toeni mawe yake; Twekeni bendera kwa ajili ya kabila za watu.
11 Tazama, Bwana ametangaza habari mpaka mwisho wa dunia, Mwambieni binti Sayuni, Tazama, wokovu wako unakuja; Tazama, thawabu yake i pamoja naye, Na malipo yake yako mbele zake.
12 Nao watawaita, Watu watakatifu, Waliokombolewa na Bwana; Nawe utaitwa, Aliyetafutwa, Mji usioachwa.

Isaya 63


1 Ni nani huyu atokaye Edomu, Mwenye mavazi ya kutiwa damu kutoka Bosra? Huyu aliye na nguo za fahari, Anayekwenda katika ukuu wa uweza wake?
2 Kwani mavazi yako kuwa mekundu, Na nguo zako kama za mtu akanyagaye zabibu?
3 Nalikanyaga shinikizoni peke yangu; Wala katika watu hakuwapo mtu pamoja nami; Naam, naliwakanyaga kwa hasira yangu, Naliwaponda kwa ghadhabu yangu; Na mavazi yangu yametiwa madoa kwa damu yao, Nami nimezichafua nguo zangu zote.
4 Maana siku ya kisasi ilikuwamo moyoni mwangu, Na mwaka wao niliowakomboa umewadia.
5 Nikatazama, wala hakuna wa kusaidia; Nikashangaa kwa kuwa hakuna mwenye kutegemeza; Basi, mkono wangu mwenyewe uliniletea wokovu, Ghadhabu yangu ndiyo iliyonitegemeza.
6 Nikazikanyaga kabila za watu kwa hasira yangu, Nikawalevya kwa ghadhabu yangu, Nami nikaimwaga damu yao chini.
7 Nitautaja wema wa Bwana, sifa za Bwana kwa yote aliyotukirimia Bwana; na wingi wa wema wake kwa nyumba ya Israeli, aliowakirimia kwa rehema zake, na kwa wingi wa wema wake.
8 Maana alisema, Hakika ndio watu wangu hawa, wana wasio na hila; akawa Mwokozi wao.
9 Katika mateso yao yote yeye aliteswa, na malaika wa uso wake akawaokoa; kwa mapenzi yake, na huruma zake, aliwakomboa mwenyewe; akawainua, akawachukua siku zote za kale.
10 Lakini wakaasi, wakamhuzunisha Roho yake Mtakatifu; kwa hiyo akawageukia, akawa adui, akapigana nao.
11 Ndipo alipozikumbuka siku za kale, za Musa, na watu wake, akisema, Yuko wapi yeye aliyewapandisha toka baharini pamoja na wachungaji wa kundi lake? Yuko wapi yeye aliyetia kati yao Roho yake Mtakatifu?
12 Aliyewaongoza kwa mkono wake mtukufu, kwa mkono wa kuume wa Musa? Aliyeyatenga maji mbele yao, ili ajifanyie jina la milele?
13 Aliyewaongoza vilindini, kama farasi jangwani, wasijikwae?
14 Kama ng'ombe washukao bondeni, Roho ya Bwana akawastarehesha; ndivyo ulivyowaongoza watu wako, ili ujifanyie jina lenye utukufu.
15 Tazama toka mbinguni, ukaone toka makao ya utukufu wako na fahari yako; uko wapi wivu wako, na uweza wako? Shauku ya moyo wako, na huruma zako zimezuiliwa kwangu.
16 Maana wewe ndiwe Baba yetu, ijapokuwa Ibrahimu hatujui, wala Israeli hatukiri; wewe, Bwana, ndiwe Baba yetu, mkombozi wetu tangu milele ndilo jina lako.
17 Ee Bwana, mbona umetukosesha njia zako, ukatufanyiza kuwa na mioyo migumu hata tusikuogope? Urudi kwa ajili ya watumishi wako, kabila za urithi wako.
18 Watu wako watakatifu waliumiliki kwa kitambo tu; adui zetu wamepakanyaga patakatifu pako.
19 Tumekuwa kama watu usiowamiliki kamwe; kama watu wasioitwa kwa Jina lako.

Isaya 64


1 Laiti ungepasua mbingu, na kushuka, ili milima iteteme mbele zako;
2 kama vile moto uchomapo vichaka, na moto uchemshapo maji; ili kuwajulisha adui zako jina lako, mataifa wakatetemeke mbele zako!
3 Ulipofanya mambo ya kutisha tusiyoyatazamia, ulishuka, milima ikatetema mbele zako.
4 Maana tangu zamani za kale watu hawakusikia, wala kufahamu kwa masikio, wala jicho halikuona Mungu, ila wewe, atendaye mambo kwa ajili yake amngojaye.
5 Wewe wamlaki yeye afurahiaye yaliyo haki na kuyatenda, watu wale wakukumbukao katika njia zako; tazama, ulikuwa na hasira, nasi tulitenda dhambi; tumekuwa katika mambo haya muda mwingi; nasi, je! Tutaokolewa?
6 Kwa maana sisi sote tumekuwa kama mtu aliye mchafu, na matendo yetu yote ya haki yamekuwa kama nguo iliyotiwa unajisi; sisi sote twanyauka kama jani, na maovu yetu yatuondoa, kama upepo uondoavyo.
7 Tena hapana aliitiaye jina lako, ajitahidiye akushike; kwa kuwa umetuficha uso wako, nawe umetukomesha kwa njia ya maovu yetu.
8 Lakini sasa, Ee Bwana, wewe u baba yetu; sisi tu udongo, nawe u mfinyanzi wetu; sisi sote tu kazi ya mikono yako.
9 Ee Bwana, usione hasira nyingi, wala usiukumbuke uovu siku zote; tazama, angalia, twakusihi, sisi sote tu watu wako.
10 Miji yako mitakatifu imekuwa jangwa, Sayuni umekuwa jangwa, Yerusalemu umekuwa ukiwa.
11 Nyumba yetu takatifu, nzuri, walimokusifu baba zetu, imeteketea moto; vitu vyetu vyote vyenye kupendeza vimeharibika.
12 Utajizuia usiyaangalie mambo haya, Ee Bwana? Utanyamaza, na kututesa sana?

Isaya 65


1 Watu wasionitaka wanauliza habari zangu; nimeonekana na hao wasionitafuta; naliliambia taifa lisiloitwa kwa jina langu,
2 Nitazameni, nitazameni. Mchana kutwa nimewanyoshea mikono yangu watu walioasi, watu waendao katika njia isiyo njema, wakifuata mawazo yao wenyewe;
3 watu wanikasirishao mbele za uso wangu daima, wakitoa dhabihu katika bustani zao, na kufukiza uvumba juu ya matofali;
4 waketio kati ya makaburi, na kulala katika mahali pao pa siri; walao nyama ya nguruwe, na mchuzi wa vitu vinichukizavyo u katika vyombo vyao;
5 watu wasemao, Simama peke yako, usinikaribie mimi, kwa maana mimi ni mtakatifu kuliko wewe; watu hao ni moshi puani mwangu, moto uwakao mchana kutwa.
6 Tazama, neno hili limeandikwa mbele zangu. Sitanyamaza, lakini nitalipa, naam, mimi nitawalipa ujira wao vifuani mwao;
7 maovu yenu na maovu ya baba zenu pamoja, asema Bwana, ninyi mliofukiza uvumba juu ya milima, na kunitukana juu ya vilima; basi, kwa ajili ya hayo nitawapimia kwanza kazi yao vifuani mwao.
8 Bwana asema hivi, Kama vile divai mpya ipatikanavyo katika kichala, na mtu mmoja husema, Usikiharibu kwa maana mna baraka ndani yake; ndivyo nitakavyotenda kwa ajili ya watumishi wangu, ili nisiwaharibu wote.
9 Nami nitaleta uzao toka Yakobo, na mrithi wa milima yangu toka Yuda, na mteule wangu atairithi, na watumishi wangu watakaa huko.
10 Na Sharoni itakuwa zizi la makundi ya kondoo, na bonde la Akori mahali pa kulala makundi ya ng'ombe, kwa ajili ya watu wangu walionitafuta.
11 Bali ninyi mmwachao Bwana, na kuusahau mlima wangu mtakatifu, na kuandika meza kwa ajili ya Bahati, na kuijazia Ajali vyombo vya divai iliyochanganyika;
12 mimi nitawaandikia kuuawa kwa upanga, na ninyi nyote mtainama ili kuchinjwa; kwa sababu nilipoita hamkuitika; niliponena, hamkusikia; bali mlitenda yaliyo mabaya machoni pangu, mlichagua mambo nisiyoyafurahia.
13 Kwa hiyo Bwana MUNGU asema hivi, Tazama, watumishi wangu watakula, bali ninyi mtaona njaa; tazama, watumishi wangu watakunywa, bali ninyi mtaona kiu; tazama, watumishi wangu watafurahi, bali ninyi mtatahayarika;
14 tazama, watumishi wangu wataimba kwa furaha ya moyo, bali ninyi mtalia kwa huzuni ya moyo; mtapiga kelele kwa sababu ya uchungu wa roho zenu.
15 Nanyi mtaliacha jina lenu kuwa laana kwa wateule wangu. Na Bwana MUNGU atakuua; naye atawaita watumishi wake kwa jina lingine.
16 Hata itakuwa yeye atakayejibariki duniani, atajibariki kwa Mungu wa kweli; naye atakayeapa duniani, ataapa kwa Mungu wa kweli. Kwa kuwa taabu za kwanza zimesahauliwa, na kwa kuwa zimefichwa machoni pangu.
17 Maana, tazama, mimi naumba mbingu mpya na nchi mpya, na mambo ya kwanza hayatakumbukwa, wala hayataingia moyoni.
18 Lakini furahini, mkashangilie daima, kwa ajili ya hivi niviumbavyo; maana, tazama, naumba Yerusalemu uwe shangwe, na watu wake wawe furaha.
19 Nami nitaufurahia Yerusalemu, nitawaonea shangwe watu wangu; sauti ya kulia haitasikiwa ndani yake tena, wala sauti ya kuomboleza.
20 Hatakuwapo tena mtoto wa siku chache, wala mzee asiyetimia siku zake; kwa maana mtoto atakufa mwenye umri wa miaka mia; bali mtenda dhambi mwenye umri wa miaka mia atalaaniwa.
21 Nao watajenga nyumba, na kukaa ndani yake; watapanda mizabibu, na kula matunda yake.
22 Hawatajenga, akakaa mtu mwingine ndani yake; hawatapanda, akala mtu mwingine; maana kama siku za mti ndivyo zitakavyokuwa siku za watu wangu, na wateule wangu wataifurahia kazi ya mikono yao muda wa siku nyingi.
23 Hawatajitaabisha kwa kazi bure, wala hawatazaa kwa taabu; kwa sababu wao ni wazao wa hao waliobarikiwa na Bwana, na watoto wao pamoja nao.
24 Na itakuwa ya kwamba, kabla hawajaomba, nitajibu; na wakiwa katika kunena, nitasikia.
25 Mbwa-mwitu na mwana-kondoo watalisha pamoja, na simba atakula majani kama ng'ombe; na mavumbi yatakuwa chakula cha nyoka. Hawatadhuru wala kuharibu katika mlima wangu mtakatifu wote, asema Bwana.

Isaya 66


1 Bwana asema hivi, Mbingu ni kiti changu cha enzi, na dunia ni mahali pa kuweka miguu yangu; mtanijengea nyumba ya namna gani? Na mahali pangu pa kupumzikia ni mahali gani?
2 Maana mkono wangu ndio uliofanya hivi vyote, vitu hivi vyote vikapata kutokea, asema Bwana; lakini mtu huyu ndiye nitakayemwangalia, mtu aliye mnyonge, mwenye roho iliyopondeka, atetemekaye asikiapo neno langu.
3 Yeye achinjaye ng'ombe ni kama yeye amwuaye mtu; na yeye atoaye dhabihu ya mwana-kondoo ni kama yeye avunjaye shingo ya mbwa; na yeye atoaye matoleo ni kama yeye atoaye damu ya nguruwe; na yeye afukizaye uvumba ni kama yeye abarikiye sanamu; naam, wamezichagua njia zao wenyewe, na nafsi zao zafurahia machukizo yao.
4 Mimi nami nitachagua mapigo yao, nitaleta hofu zao juu yao; kwa sababu nilipoita, hawakuitika; na niliponena, hawakusikia; bali walifanya yaliyo maovu machoni pangu, na kuyachagua nisiyoyafurahia.
5 Lisikilizeni neno la Bwana, ninyi mtetemekao kwa sababu ya neno lake; Ndugu zenu wawachukiao ninyi, waliowatupa kwa ajili ya jina langu, wamesema, Na atukuzwe Bwana, tupate kuiona furaha yenu; lakini watatahayarika.
6 Sauti ya fujo itokayo mjini! Sauti itokayo hekaluni! Sauti ya Bwana awalipaye adui zake adhabu!
7 Kabla hajaona utungu alizaa; Kabla maumivu yake hayajampata, Alizaa mtoto mwanamume.
8 Ni nani aliyesikia neno kama hili? Ni nani aliyeona mambo kama haya? Je! Nchi yaweza kuzaliwa siku moja? Taifa laweza kuzaliwa mara? Maana Sayuni, mara alipoona utungu, Alizaa watoto wake.
9 Je! Mimi nilete wana karibu na kuzaliwa, nisizalishe? Asema Bwana; mimi nizalishaye, je! Nilifunge tumbo? Asema Mungu wako.
10 Furahini pamoja na Yerusalemu, shangilieni kwa ajili yake, ninyi nyote mmpendao; furahini pamoja naye kwa furaha, ninyi nyote mliao kwa ajili yake;
11 mpate kunyonya, na kushibishwa kwa maziwa ya faraja zake, mpate kukama, na kufurahiwa kwa wingi wa utukufu wake.
12 Maana Bwana asema hivi, Tazama, nitamwelekezea amani kama mto, na utukufu wa mataifa kama kijito kifurikacho, nanyi mtapata kunyonya; mtabebwa; na juu ya magoti mtabembelezwa.
13 Mfano wa mtu ambaye mama yake amfariji, ndivyo nitakavyowafariji ninyi; nanyi mtafarijiwa katika Yerusalemu.
14 Nanyi mtaona, na mioyo yenu itafurahi, na mifupa yenu itasitawi kama majani mabichi; na mkono wa Bwana utajulikana, uwaelekeao watumishi wake, naye atawaonea adui zake ghadhabu.
15 Maana Bwana atakuja na moto, na magari yake ya vita kama upepo wa kisulisuli; ili atoe malipo ya ghadhabu yake kwa moto uwakao, na maonyo yake kwa miali ya moto.
16 Kwa maana Bwana atateta na wote wenye mwili, kwa moto na kwa upanga wake; nao watakaouawa na Bwana watakuwa wengi.
17 Watu wale wajitakasao, na kujisafisha katika bustani, nyuma yake aliye katikati; wakila nyama ya nguruwe, na machukizo, na panya; watakoma pamoja, asema Bwana.
18 Nami nayajua matendo yao na mawazo yao; wakati unakuja nitakapokusanya mataifa yote na lugha zote; nao watakuja, nao watauona utukufu wangu.
19 Nami nitaweka ishara kati yao, nami nitawatuma hao waliookoka kwa mataifa, Tarshishi, na Puli, na Ludi, wavutao upinde, kwa Tubali na Yavani, visiwa vilivyo mbali; watu wasioisikia habari yangu, wala kuuona utukufu wangu; nao watahubiri utukufu wangu katika mataifa.
20 Nao watawaleta ndugu zenu wote kutoka mataifa yote, kuwa sadaka kwa Bwana, juu ya farasi, na katika magari, na katika machela, na juu ya nyumbu, na juu ya wanyama wepesi, mpaka mlima wangu mtakatifu Yerusalemu, asema Bwana; kama vile wana wa Israeli waletavyo sadaka yao nyumbani kwa Bwana katika chombo safi.
21 Na baadhi ya hao nitawatwaa kuwa makuhani na Walawi, asema Bwana.
22 Kama vile mbingu mpya na nchi mpya, nitakazofanya, zitakavyokaa mbele zangu, asema Bwana, ndivyo uzao wenu na jina lenu litakavyokaa.
23 Na itakuwa, mwezi mpya hata mwezi mpya, na sabato hata sabato, wanadamu wote watakuja kuabudu mbele zangu, asema Bwana.
24 Nao watatoka nje na kuitazama mizoga ya watu walioniasi; maana funza wao hatakufa, wala moto wao hautazimika nao watakuwa chukizo machoni pa wote wenye mwili.