2 Samweli

Sura: 1, 2, 3, 4, 5, 6, 7, 8, 9, 10, 11, 12, 13, 14, 15, 16, 17, 18, 19, 20, 21, 22, 23, 24

2 Samweli 1


1 Ikawa baada ya kufa kwake Sauli, hapo Daudi aliporudi katika kuwaua Waamaleki, naye Daudi amekaa siku mbili katika Siklagi;
2 hata siku ya tatu ikawa, tazama! Akaja mtu kutoka kambi ya Sauli, nguo zake zimeraruliwa, tena ana mavumbi kichwani mwake; basi, ikawa alipomfikia Daudi, akaanguka chini, akamsujudia.
3 Daudi akamwambia, Umetoka wapi? Akamwambia, Nimeokoka katika kambi ya Israeli.
4 Daudi akamwambia, Yalikwendaje? Tafadhali uniambie. Akajibu, Watu wamekimbia vitani, tena watu wengi wameanguka wamekufa; hata Sauli naye na Yonathani, mwanawe, wamekufa.
5 Daudi akamwambia yule kijana aliyempa habari, Umejuaje ya kuwa Sauli na Yonathani mwanawe wamekufa?
6 Yule kijana aliyempa habari akasema, Nalikuwapo kwa nasibu juu ya kilima cha Gilboa, na tazama, Sauli alikuwa ameegemea fumo lake; na tazama, magari na wapanda farasi wanamfuatia kwa kasi.
7 Naye alipotazama nyuma, akaniona, akaniita. Nikajibu, Mimi hapa.
8 Akaniambia, U nani wewe? Nikamjibu, Mimi ni Mwamaleki.
9 Akaniambia, Tafadhali simama karibu nami, ukaniue, maana shida imenipata; kwa sababu roho yangu ingali hai ndani yangu.
10 Basi, nikasimama karibu naye, nikamwua, kwa sababu nalijua hakika ya kuwa hawezi kupona baada ya kuanguka; kisha nikaitwaa ile taji iliyokuwa kichwani mwake, na kikuku kilichokuwa mkononi mwake, nami nimevileta hapa kwa bwana wangu.
11 Ndipo Daudi akashika nguo zake akazirarua na kadhalika watu wote waliokuwa pamoja naye;
12 wakaomboleza, wakalia, wakafunga hata jioni, kwa ajili ya Sauli, na kwa ajili ya Yonathani mwanawe, na kwa ajili ya watu wa Bwana na kwa ajili ya nyumba ya Israeli; kwa sababu wameanguka kwa upanga.
13 Naye Daudi akamwambia yule kijana aliyempa habari, Watoka wapi wewe? Akajibu, Mimi ni mwana wa mgeni, Mwamaleki.
14 Daudi akamwambia, Jinsi gani hukuogopa kuunyosha mkono wako umwangamize masihi wa BWANA?
15 Ndipo Daudi akamwita mmoja wa vijana, akamwambia, Mwendee, ukamwangukie. Basi akampiga hata akafa.
16 Daudi akamwambia, Damu yako na iwe juu ya kichwa chako mwenyewe; maana umejishuhudia nafsi yako ukisema, Nimemwua masihi wa Bwana.
17 Basi Daudi akamwomboleza Sauli, na Yonathani, mwanawe, maombolezo haya;
18 (kama ilivyoandikwa katika kitabu cha Yashari), akasema, Wana wa Yuda na wafundishwe haya,
19 Walio fahari yako, Ee Israeli Juu ya mahali pako palipoinuka wameuawa; Jinsi mashujaa walivyoanguka!
20 Msiyahubiri mambo haya katika Gathi, Msiyatangaze katika njia za Ashkeloni; Wasije wakashangilia binti za Wafilisti, Binti za wasiotahiriwa wakasimanga.
21 Enyi milima ya Gilboa, visiwepo juu yenu Umande wala mvua, wala mashamba ya matoleo; Maana ndipo ilipotupwa kwa aibu ngao ya shujaa, Ngao yake Sauli, pasipo kutiwa mafuta.
22 Kutoka kwa damu yao waliouawa, Kutoka kwa shahamu yao mashujaa, Upinde wa Yonathani haukurudi nyuma, Wala upanga wa Sauli haukurudi bure.
23 Sauli na Yonathani walipendwa na kupendeza Maishani wala mautini hawakutengwa; Walikuwa wepesi kuliko tai, Walikuwa hodari kuliko simba.
24 Enyi binti za Israeli, mlilieni Huyo Sauli, ambaye aliwavika Mavazi mekundu kwa anasa, Akazipamba nguo zenu dhahabu.
25 Jinsi mashujaa walivyoanguka Katikati ya vita! Ee Yonathani, wewe umeuawa Juu ya mahali pako palipoinuka
26 Nimesikitika kwa ajili yako, Yonathani, ndugu yangu, Ulikuwa ukinipendeza sana; Upendo wako kwangu ulikuwa wa ajabu, Kupita upendo wa wanawake.
27 Jinsi mashujaa walivyoanguka, Na silaha za vita zilivyoangamia!

2 Samweli 2


1 Ikawa baada ya hayo, Daudi akauliza kwa Bwana, akasema, Je! Niupandie mji wo wote wa Yuda? Bwana akamwambia, Haya! Panda. Daudi akasema, Niupandie mji upi? Akasema, Hebroni.
2 Basi Daudi akapanda aende huko, pamoja na wakeze wawili, Ahinoamu wa Yezreeli, na Abigaili, mkewe Nabali, wa Karmeli.
3 Daudi naye akawapandisha watu wake waliokuwa pamoja naye, kila mtu na watu wa nyumbani mwake; wakakaa katika miji ya Hebroni.
4 Basi watu wa Yuda wakaenda, wakamtia Daudi mafuta huko, awe mfalme juu ya nyumba ya Yuda. Wakamwambia Daudi wakasema, Watu wa Yabesh-gileadi ndio waliomzika Sauli.
5 Basi Daudi akatuma wajumbe kwa watu wa Yabesh-gileadi, na kuwaambia, Na mbarikiwe ninyi na Bwana, kwa kuwa mmemtendea bwana wenu fadhili hii, yaani Sauli, mkamzika.
6 Bwana naye sasa awatendee ninyi fadhili na kweli; mimi nami nitawalipeni fadhili hiyo, kwa sababu mmetenda jambo hilo.
7 Basi sasa, mikono yenu na itiwe nguvu, nanyi iweni mashujaa; maana Sauli, bwana wenu, amekufa, tena nyumba ya Yuda wamenitia mimi mafuta niwe mfalme juu yao.
8 Basi Abneri, mwana wa Neri, amiri wa jeshi la Sauli, alikuwa amemtwaa Ishboshethi, mwana wa Sauli, na kumvusha na kumpeleka Mahanaimu;
9 akamweka awe mfalme juu ya Gileadi, na Waasheri, na Yezreeli, na Efraimu, na Benyamini, na juu ya Israeli wote.
10 (Huyo Ishboshethi, mwana wa Sauli, umri wake alikuwa amepata miaka arobaini alipoanza kutawala juu ya Israeli, akatawala miaka miwili.) Lakini nyumba ya Yuda waliandamana na Daudi.
11 Na wakati Daudi alipotawala Hebroni juu ya nyumba ya Yuda ulikuwa miaka saba na miezi sita.
12 Basi Abneri, mwana wa Neri, na watumishi wa Ishboshethi, mwana wa Sauli, wakatoka Mahanaimu kwenda Gibeoni.
13 Huyo Yoabu naye, mwana wa Seruya, na watumishi wa Daudi, wakatoka, wakakutana nao karibu na ziwa la Gibeoni; wakaketi, hawa upande huu wa ziwa, na hawa upande huu wa ziwa.
14 Abneri akamwambia Yoabu, Tafadhali vijana hawa na waondoke na kucheza mbele yetu. Yoabu akasema, Haya! Na waondoke.
15 Basi wakaondoka, wakaenda upande wa pili kwa hesabu yao watu kumi na wawili wa Benyamini, na wa Ishboshethi, mwana wa Sauli na watu kumi na wawili wa watumishi wa Daudi.
16 Wakakamatana, kila mtu akimshika mwenziwe kichwa chake, na kutia upanga wake katika ubavu wa mwenzake; wakaanguka pamoja; hata mahali pale pakaitwa Helkath-hasurimu, napo ni katika Gibeoni.
17 Vita vile vilikuwa vikali sana siku ile; naye Abneri akashindwa, na watu wa Israeli, mbele ya watumishi wa Daudi.
18 Na wana watatu wa Seruya walikuwako huko, Yoabu, na Abishai, na Asaheli; na Asaheli alikuwa mwepesi wa miguu kama kulungu.
19 Naye Asaheli akamfuatia Abneri; na katika kwenda kwake hakugeuka kwenda mkono wa kuume wala mkono wa kushoto katika kumfuatia Abneri.
20 Basi Abneri akatazama nyuma yake, akasema, Ni wewe, Asaheli? Akajibu, Ni mimi.
21 Basi Abneri akamwambia, Geuka mkono wa kuume au mkono wa kushoto, ukamshike mmoja wa vijana, ukazitwae silaha zake. Lakini Asaheli hakukubali kugeuka na kuacha kumfuata.
22 Abneri akamwambia Asaheli mara ya pili, Geuka, acha kunifuatia mimi; kwa nini nikupige hata chini? Hapo ningewezaje kuinua uso wangu mbele ya Yoabu, ndugu yako?
23 Lakini akakataa kugeuka; kwa hiyo Abneri akampiga tumboni kwa ncha ya nyuma ya mkuki wake, ule mkuki ukamtoka kwa nyuma; naye akaanguka hapo, akafa papo hapo; ikawa, watu wote waliofika hapo, alipoanguka Asaheli na kufa, wakasimama.
24 Ila Yoabu na Abishai wakamfuatia Abneri; na jua likachwa hapo walipoufikilia mlima wa Ama, uelekeao Gia, katika njia ya nyika ya Gibeoni.
25 Nao wana wa Benyamini wakakusanyika pamoja nyuma ya Abneri, wakawa kikosi kimoja, wakasimama juu ya mlima.
26 Ndipo huyo Abneri akamwita Yoabu, akasema, Je! Upanga uwale watu sikuzote? Je! Hujui ya kwamba utakuwa uchungu mwisho wake? Basi itakuwa hata lini usijewaamuru watu warudi na kuacha kuwafuatia ndugu zao?
27 Naye Yoabu akasema, Aishivyo Mungu, usingalinena, basi asubuhi wangalikwenda zao, wasiwafuatie kila mtu ndugu yake.
28 Basi Yoabu akapiga tarumbeta, na watu wote wakasimama, wasiwafuatie Israeli tena, wala hawakupigana tena.
29 Wakaenda Abneri na watu wake usiku ule wote kati ya ile Araba; wakavuka Yordani, wakapita kati ya Bithroni yote, wakaja Mahanaimu.
30 Akarudi Yoabu naye kutoka kumfuatia Abneri; na alipokwisha kuwakusanya watu wote pamoja, wa hao watumishi wa Daudi walipungukiwa na watu kumi na kenda pamoja na Asaheli.
31 Ila watumishi wa Daudi walikuwa wamewapiga watu wa Benyamini, na watu wa Abneri, hata wakafa watu mia tatu na sitini.
32 Nao wakamwinua Asaheli, wakamzika katika kaburi la baba yake, lililokuwako Bethlehemu. Yoabu na watu wake wakaenda usiku kucha, wakapambazukiwa huko Hebroni.

2 Samweli 3


1 Basi kulikuwa na vita siku nyingi kati ya nyumba ya Sauli na nyumba ya Daudi; Daudi akaendelea akasitawi, lakini nyumba ya Sauli ikaendelea kudhoofika.
2 Naye Daudi akazaliwa wana huko Hebroni; mzaliwa wake wa kwanza alikuwa Amnoni, wa Ahinoamu wa Yezreeli;
3 na wa pili wake Danieli, wa Abigaili mkewe Nabali wa Karmeli; na wa tatu Absalomu, mwana wa Maaka binti Talmai, mfalme wa Geshuri,
4 na wa nne Adoniya, mwana wa Hagithi; na wa tano Shefatia, mwana wa Abitali;
5 na wa sita Ithreamu, wa Egla, mkewe Daudi. Hawa walizaliwa kwa Daudi huko Hebroni.
6 Ikawa, wakati vilipokuwapo vita kati ya nyumba ya Sauli na nyumba ya Daudi, Abneri akajipatia nguvu nyumbani kwa Sauli.
7 Basi Sauli alikuwa na suria, jina lake akiitwa Rispa, binti Aya; Ishboshethi akamwuliza Abneri, Kwa nini umeingia kwa suria ya babangu?
8 Basi Abneri akakasirika kwa maneno ya Ishboshethi, akasema, Je! Mimi ni kichwa cha mbwa, aliye wa Yuda? Hata leo hivi nawafanyia fadhili nyumba ya Sauli babako, na ndugu zake, na rafiki zake, nisikutie wewe mkononi mwa Daudi; nawe hata hivyo wanitia hatiani leo kwa mwanamke huyu.
9 Mungu amfanyie Abneri vivyo, na kuzidi, nisipomtendea Daudi kama vile Bwana alivyomwapia;
10 kuupitisha ufalme toka nyumba ya Sauli, na kukisimamisha kiti cha Daudi juu ya Israeli, na juu ya Yuda, toka Dani mpaka Beer-sheba.
11 Wala hakuweza kumjibu Abneri tena, kwa sababu alimwogopa.
12 Basi Abneri akatuma wajumbe kwa Daudi mahali alipokuwapo, akisema, Nchi hii ni ya nani? Fanya agano nami, na tazama, mkono wangu utakuwa pamoja nawe, ili kuwaleta Israeli wote kwako.
13 Daudi akasema, Vema, nitafanya agano nawe, lakini nina sharti moja nitakalo kwako, nalo ni hili; Hutaniona uso wangu, isipokuwa uniletee Mikali, binti Sauli, hapo ujapo kuniona uso wangu.
14 Basi Daudi akatuma wajumbe kwa Ishboshethi, mwana wa Sauli, kusema, Nipe mke wangu Mikali, niliyemposa kwa govi mia za Wafilisti.
15 Basi Ishboshethi akatuma watu, akamnyang'anya Paltieli, mwana wa Laishi, mumewe, mwanamke huyo.
16 Huyo mumewe akafuatana naye, akiendelea na kulia, akamfuata mpaka Bahurimu. Ndipo Abneri akamwambia, Haya, rudi. Naye akarudi.
17 Basi Abneri akafanya mashauri na wazee wa Israeli, akasema, Zamani mlitaka Daudi awamiliki;
18 basi, sasa, fanyeni hayo; kwa maana Bwana amemtaja Daudi, akisema, kwa mkono wa mtumishi wangu, Daudi, nitawaokoa watu wangu Israeli katika mikono ya Wafilisti, na katika mikono ya adui zao wote.
19 Tena Abneri alinena masikioni mwa Benyamini; kisha Abneri akaenda ili kunena masikioni mwa Daudi huko Hebroni maneno yote yaliyoonekana kuwa mema machoni pa Israeli, na machoni pa nyumba yote ya Benyamini.
20 Basi Abneri akamwendea Daudi huko Hebroni, na watu ishirini pamoja naye. Daudi akamfanyia karamu Abneri, na watu wote waliokuwa pamoja naye.
21 Kisha Abneri akamwambia Daudi, Nitaondoka, niende zangu; nami nitamkusanyia bwana wangu mfalme Israeli wote, ili wafanye agano nawe, ukamiliki juu ya wote inaowatamani roho yako. Basi Daudi akamruhusu Abneri; naye akaenda zake kwa amani.
22 Na tazama, watumishi wa Daudi pamoja na Yoabu walitoka jeshini, wakaleta mateka mengi pamoja nao; lakini Abneri hakuwako Hebroni kwa Daudi; maana alikuwa amemruhusu, naye amekwisha kwenda zake kwa amani.
23 Hata Yoabu, na jeshi lote waliokuwa pamoja naye, walipofika, watu wakamwambia Yoabu, wakisema, Abneri, mwana wa Neri, alikuja kwa mfalme, naye amemruhusu, naye amekwenda zake kwa amani.
24 Basi Yoabu akamwendea mfalme, akasema, Umefanyaje? Tazama, Abneri amekuja kwako; mbona umemruhusu, naye amekwisha kwenda zake?
25 Wewe wamjua Abneri, mwana wa Neri, ya kuwa alikuja ili kukudanganya, apate kujua kutoka kwako, na kuingia kwako, akajue yote uyatendayo.
26 Naye Yoabu alipotoka kwa Daudi, akapeleka wajumbe kumfuata Abneri, wakamrudisha kutoka kisima cha Sira; lakini Daudi alikuwa hana habari.
27 Basi Abneri alipokuwa amerudi Hebroni, Yoabu akamchukua kando hata katikati ya lango, ili aseme naye kwa faragha; akampiga mkuki wa tumbo huko, hata akafa; kwa ajili ya damu ya Asaheli, ndugu yake.
28 Hata baadaye Daudi aliposikia, akasema, Mimi na ufalme wangu hatuna hatia milele mbele za Bwana, kwa sababu ya damu ya Abneri, mwana wa Neri;
29 na imwangukie Yoabu kichwani pake, na nyumba yote ya babaye, tena hiyo nyumba ya Yoabu isikose kuwa na mtu mwenye kutoka damu, au aliye na ukoma, au mwenye kutegemea fimbo, au mwenye kuanguka kwa upanga au mwenye kuhitaji chakula.
30 Basi Yoabu, na Abishai nduguye, walimwua Abneri, kwa sababu yeye alimwua ndugu yao Asaheli katika vita huko Gibeoni.
31 Kisha Daudi alimwambia Yoabu, na watu wote waliokuwa pamoja naye, Rarueni nguo zenu, mkajivike nguo za magunia, mkamlilie Abneri. Naye mfalme Daudi akaifuata jeneza.
32 Wakamzika Abneri katika Hebroni; naye mfalme akapaza sauti yake, akalia kaburini kwa Abneri, nao watu wote wakalia.
33 Ndipo mfalme akamwomboleza Abneri, akasema, Ilimpasaje Abneri kufa afavyo mpumbavu?
34 Mikono yako haikufungwa, Wala miguu yako haikutiwa pingu; Aangukavyo mtu mbele ya wana wa uovu, ndivyo ulivyoanguka. Na watu wote wakaongeza kumlilia.
35 Wakaja na watu wote wamshurutishe Daudi kula chakula, ukalipo bado mchana; lakini Daudi akaapa, akasema Mungu anitendee vivyo, na kuzidi, nikionja mkate, au kingine cho chote kabla lichwapo jua.
36 Wakaangalia watu wote, yakawa mema machoni pao; kama yalivyokuwa mema machoni pao yote aliyoyatenda mfalme.
37 Wakajua watu wote, na Israeli wote, siku ile, ya kuwa si nia ya mfalme kwamba auawe Abneri, mwana wa Neri.
38 Kisha mfalme akawaambia watumishi wake, Hamjui ya kuwa mkuu mmoja, naye ni mtu mkubwa ameanguka leo katika Israeli?
39 Nami leo nimedhoofika, hata nijapotiwa mafuta niwe mfalme; na watu hao, wana wa Seruya, ni wagumu kwangu mimi; Bwana amlipie mwovu sawasawa na uovu wake.

2 Samweli 4


1 Hata Ishboshethi mwana wa Sauli aliposikia ya kuwa Abneri amekufa huko Hebroni, mikono yake ilikuwa dhaifu, na Waisraeli wote wakataabika.
2 Na huyo mwana wa Sauli alikuwa na watu wawili, maakida wa vikosi; jina lake mmoja akiitwa Baana, na jina la wa pili Rekabu wana wa Rimoni, Mbeerothi, wa wana wa Benyamini; (kwa maana Beerothi umehesabiwa kuwa wa Benyamini;
3 na hao Wabeerothi walikimbia kwenda Githaimu, ndipo wanapokaa hali ya ugeni hata hivi leo.)
4 Naye Yonathani, mwana wa Sauli alikuwa na mwana aliyekuwa na kilema cha miguu. Alikuwa amepata miaka mitano, habari za Sauli na Yonathani zilipofika Yezreeli, na yaya wake akamchukua akakimbia ikawa, alipokimbia kwa haraka, huyo mtoto akaanguka, akawa kilema. Na jina lake aliitwa Mefiboshethi.
5 Na wale wana wa Rimoni, Mbeerothi, Rekabu na Baana, wakaenda wakafika nyumbani kwa Ishboshethi, wakati wa hari ya mchana, alipokuwa akipumzika adhuhuri.
6 Wakafikia kati ya nyumba, kana kwamba wanataka kuchukua ngano, wakampiga mkuki wa tumbo; kisha Rekabu na Baana nduguye wakakimbia.
7 Basi walipoingia katika ile nyumba, alipokuwa amelala kitandani mwake, katika chumba chake cha kulala, wakampiga, wakamwua, wakamkata kichwa, wakachukua kichwa chake, wakaenda zao kwa njia ya Araba usiku kucha.
8 Wakamletea Daudi kichwa cha Ishboshethi huko Hebroni, wakamwambia mfalme, Tazama, hiki ni kichwa cha Ishboshethi, mwana wa Sauli, adui yako, aliyekutafuta roho yako; Bwana amemlipia kisasi bwana wangu mfalme hivi leo, juu ya Sauli, na juu ya wazao wake.
9 Naye Daudi akawajibu Rekabu na Baana, nduguye, wana wa Rimoni, Mbeerothi, akawaambia, Aishivyo Bwana, aliyenihifadhi roho yangu katika shida zote,
10 mtu mmoja aliponiambia, akasema, Tazama, Sauli amekufa, akidhani ya kuwa ameleta habari njema, nalimshika, nikamwua, huko Siklagi, ndio ujira niliompa kwa habari zake.
11 Basi, iwapo watu waovu wamemwua mtu mwenye haki kitandani mwake, je! Sasa nisitake zaidi damu yake mikononi mwenu, na kuwaondoa ninyi katika nchi?
12 Ndipo Daudi akawaagiza vijana wake, wakawaua, wakawakata mikono na miguu, wakawatundika kando ya ziwa katika Hebroni. Nao wakakitwaa kichwa cha Ishboshethi wakakizika katika kaburi la Abneri huko Hebroni.

2 Samweli 5


1 Ndipo kabila zote za Israeli wakamwendea Daudi huko Hebroni, wakasema naye, wakinena, Tazama, sisi tu mfupa wako na nyama yako.
2 Zamani za kale, hapo Sauli alipokuwa mfalme juu yetu, wewe ndiwe uliyewaongoza Israeli watoke nje, na kuingia ndani. Naye Bwana akakuambia, Wewe utawalisha watu wangu Israeli, nawe utakuwa mkuu juu ya Israeli.
3 Basi wazee wote wa Israeli wakamwendea mfalme huko Hebroni, naye mfalme Daudi akapatana nao huko Hebroni mbele za Bwana; wakamtia Daudi mafuta awe mfalme juu ya Israeli.
4 Daudi alikuwa amepata miaka thelathini alipoanza kutawala, akatawala miaka arobaini.
5 Huko Hebroni alitawala miaka saba na miezi sita; na katika Yerusalemu alitawala miaka thelathini na tatu juu ya Israeli wote na Yuda.
6 Kisha mfalme na watu wake wakaenda Yerusalemu ili kupigana na Wayebusi, wenyeji wa nchi ile; hao ndio waliomwambia Daudi, wakisema, Usipowaondoa vipofu, na viwete, hutaingia humu kamwe; huku wakidhania ya kuwa Daudi hawezi kuingia humo.
7 Lakini Daudi aliipiga ngome ya Sayuni; huu ndio mji wa Daudi.
8 Naye Daudi alisema siku hiyo, Yeye atakayewapiga Wayebusi, na apande kwenye mfereji wa maji, na kuwapiga viwete, na hao vipofu, ambao roho yake Daudi inawachukia. Kwa sababu hii watu husema, Wako vipofu na viwete hawawezi kuingia nyumbani.
9 Basi Daudi akakaa ndani ya ngome hiyo, akaiita mji wa Daudi. Kisha Daudi akajenga toka Milo na pande za ndani.
10 Naye Daudi akazidi kuwa mkuu; kwa maana Bwana, Mungu wa majeshi, alikuwa pamoja naye.
11 Kisha Hiramu, mfalme wa Tiro, akatuma wajumbe kwa Daudi, akampelekea na mierezi, na maseremala, na waashi; nao wakamjengea Daudi nyumba.
12 Akajua Daudi ya kwamba Bwana amemweka imara awe mfalme juu ya Israeli, na ufalme wake ameutukuza kwa ajili ya watu wake, Israeli.
13 Naye Daudi akazidi kujitwalia masuria na wake huko Yerusalemu baada ya kutoka Hebroni; wakazaliwa zaidi kwa Daudi wana na binti.
14 Na haya ndiyo majina ya hao waliozaliwa kwake huko Yerusalemu; Shamua, na Shobabu, na Nathani, na Sulemani,
15 na Ibhari, na Elishua; na Nefegi, na Yafia;
16 na Elishama, na Eliada, na Elifeleti.
17 Na hao Wafilisti waliposikia kwamba wamemtia Daudi mafuta ili awe mfalme juu ya Israeli, Wafilisti wote wakapanda kumtafuta Daudi; naye Daudi akapata habari, akashuka akaenda ngomeni.
18 Basi Wafilisti walikuwa wamekuja na kujitawanya bondeni mwa Warefai.
19 Basi Daudi akauliza kwa Bwana, akisema, Je! Nipande juu ya Wafilisti? Utawatia mkononi mwangu? Naye Bwana akamwambia Daudi, Panda; kwa kuwa hakika nitawatia Wafilisti mikononi mwako.
20 Basi Daudi akaja Baal-perasimu, naye Daudi akawapiga huko; akasema, Bwana amewafurikia adui zangu mbele yangu, kama mafuriko ya maji. Basi akapaita mahali pale Baal-perasimu.
21 Nao wakaziacha sanamu zao huko, na Daudi na watu wake wakaziondolea mbali.
22 Lakini wakapanda hao Wafilisti tena mara ya pili, wakajitawanya bondeni mwa Warefai.
23 Naye Daudi alipouliza kwa Bwana, alisema, Usipande; zunguka nyuma yao, ukawajie huko mbele ya miforsadi.
24 Kisha itakuwa, hapo utakapoisikia sauti ya kwenda katika vilele vya miforsadi, ndipo nawe ujitahidi; kwa maana ndipo Bwana ametoka mbele yako awapige jeshi la Wafilisti.
25 Ndivyo alivyotenda Daudi, vile vile kama Bwana alivyomwagiza; naye akawapiga Wafilisti toka Geba hata ujapo Gezeri.

2 Samweli 6


1 Basi Daudi akakusanya tena wateule wote wa Israeli, watu thelathini elfu.
2 Akaondoka Daudi akaenda pamoja na watu wote waliokuwa naye, mpaka Baala wa Yuda, ili kulipandisha kutoka huko sanduku la Mungu lililoitwa kwa jina, naam, jina la Bwana wa majeshi akaaye juu ya makerubi.
3 Wakaliweka sanduku la Mungu juu ya gari jipya, wakalitoa katika nyumba ya Abinadabu, iliyoko kilimani; nao Uza na Ahio wana wa Abinadabu wakaliendesha lile gari jipya.
4 Wakalitoa katika nyumba ya Abinadabu iliyoko kilimani, pamoja na sanduku la Bwana; na huyo Ahio akatangulia mbele ya sanduku.
5 Daudi na nyumba yote ya Israeli wakacheza mbele za Bwana kwa nguvu zao zote, kwa nyimbo, na kwa vinubi, na kwa vinanda, na kwa matari, na kwa kayamba, na kwa matoazi.
6 Hata walipofika kwa uga ya Nakoni, Uza akalinyoshea mkono sanduku la Mungu, akalikamata kwa maana wale ng'ombe walikunguwaa.
7 Ndipo hasira ya Bwana ikawaka juu ya Uza; naye Mungu akampiga huko kwa kosa lake; hata akafa pale pale penye sanduku la Mungu.
8 Daudi akaona uchungu kwa kuwa Bwana amemfurikia Uza; akapaita mahali pale Peres-uza hata leo.
9 Naye Daudi akamwogopa Bwana siku ile; akasema, Litanijiaje sanduku la Bwana?
10 Basi Daudi hakutaka kulileta sanduku la Bwana kwake mjini mwa Daudi; ila Daudi akalihamisha nyumbani kwa Obed-edomu, Mgiti.
11 Sanduku la Bwana akalitia katika nyumba ya Obed-edomu, Mgiti, muda wa miezi mitatu; naye Bwana akambarikia Obed-edomu, na nyumba yake yote.
12 Kisha mfalme Daudi akaambiwa ya kwamba, Bwana ameibarikia nyumba ya Obed-edomu, na vitu vyote alivyo navyo kwa ajili ya sanduku la Mungu. Daudi akaenda, akalileta sanduku la Mungu, toka nyumba ya Obed-edomu mpaka mji wa Daudi, kwa shangwe.
13 Hata ikawa, watu waliolichukua sanduku la Bwana walipokwisha kwenda hatua sita, akachinja ng'ombe na kinono.
14 Daudi akacheza mbele za Bwana kwa nguvu zake zote; na Daudi alikuwa amevaa naivera ya kitani.
15 Basi Daudi na nyumba yote ya Israeli wakalileta sanduku la Bwana kwa shangwe, na kwa sauti ya tarumbeta.
16 Ikawa, sanduku la Bwana lilipoingia mji wa Daudi Mikali, binti Sauli, akachungulia dirishani, akamwona mfalme Daudi akiruka-ruka na kucheza mbele za Bwana; akamdharau moyoni mwake.
17 Wakaliingiza sanduku la Bwana, na kuliweka mahali pake, katikati ya hema aliyoipiga Daudi kwa ajili yake, naye Daudi akatoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani mbele za Bwana.
18 Kisha Daudi alipokwisha kutoa sadaka ya kuteketezwa na sadaka za amani akawabarikia watu kwa jina la Bwana wa majeshi.
19 Akawagawia watu wote, mkutano wote wa Israeli, wanaume kwa wanawake, kila mtu mkate wa ngano, na kipande cha nyama, na mkate wa zabibu. Basi watu wote wakaenda zao, kila mtu nyumbani kwake.
20 Ndipo Daudi akarudi ili awabarikie watu wa nyumbani mwake. Na Mikali, binti Sauli, akatoka nje aende kumlaki Daudi, naye akasema, Mfalme wa Israeli alikuwa mtukufu leo namna gani, akijifunua mwili wake mbele ya vijakazi vya watumishi wake, mfano wa watu baradhuli mmojawapo, ajifunuavyo mwili wake mbele ya watu, asipokuwa na haya!
21 Daudi akamwambia Mikali, Ilikuwa mbele za Bwana, aliyenichagua mimi juu ya baba yako, na juu ya nyumba yake, ili kuniweka niwe mkuu juu ya watu wa Bwana, juu ya Israeli; kwa hiyo mimi nitacheza mbele za Bwana.
22 Kisha nitakuwa hafifu zaidi, nami nitakuwa mnyonge machoni pangu mimi mwenyewe; lakini kwa wale vijakazi uliowanena, kwao nitaheshimiwa.
23 Basi Mikali, binti Sauli, hakuwa na mtoto hata siku ya kufa kwake.

2 Samweli 7


1 Ikawa, mfalme alipokuwa akikaa katika nyumba yake, hapo Bwana alipomstarehesha, asiudhiwe na adui zake waliomzunguka pande zote,
2 mfalme akamwambia Nathani, nabii, Angalia sasa, mimi ninakaa katika nyumba ya mierezi, bali sanduku la Mungu linakaa ndani ya mapazia.
3 Nathani akamwambia mfalme, Haya, fanya yote yaliyomo moyoni mwako; maana Bwana yu pamoja nawe.
4 Ikawa usiku uo huo, neno la Bwana likamfikia Nathani kusema,
5 Enenda, ukamwambie mtumishi wangu, Daudi, Bwana asema hivi, Je! Wewe utanijengea nyumba, nikae ndani yake?
6 Kwa maana mimi sikukaa ndani ya nyumba, tangu siku ile niliyowatoa wana wa Israeli katika Misri, hata leo, lakini nimekaa katika hema na maskani.
7 Mahali mwote nilimokwenda na wana wa Israeli wote, je! Nimesema neno lo lote na mtu ye yote wa waamuzi wa Israeli, niliyemwagiza kuwalisha watu wangu Israeli, nikisema, Mbona hamkunijengea nyumba ya mierezi?
8 Basi, sasa, mwambie mtumishi wangu, Daudi, maneno haya, Bwana wa majeshi asema hivi, Nalikutwaa katika zizi la kondoo, katika kuwaandama kondoo, ili uwe mkuu juu ya watu wangu, juu ya Israeli;
9 nami nimekuwa pamoja nawe kila ulikokwenda, na kuwakatilia mbali adui zako wote mbele yako; nami nitakufanyia jina kuu, kama jina la wakuu walioko duniani.
10 Tena nitawaagizia mahali watu wangu Israeli, nami nitawapanda, wapate kukaa mahali pao wenyewe, wasiondolewe tena; wala wana wa uovu hawatawatesa tena, kama hapo kwanza;
11 naam, kama vilivyokuwa tangu siku ile nilipowaamuru waamuzi, wawe juu ya watu wangu Israeli; nami nitakustarehesha mbele ya adui zako wote. Tena Bwana anakuambia ya kwamba Bwana atakujengea nyumba.
12 Nawe siku zako zitakapotimia, ukalala na baba zako, nitainua mzao wako nyuma yako, atakayetoka viunoni mwako, nami nitaufanya imara ufalme wake.
13 Yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa jina langu, nacho kiti cha enzi cha ufalme wake nitakifanya imara milele.
14 Mimi nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu; akitenda maovu nitamwadhibu kwa fimbo ya binadamu na kwa mapigo ya wanadamu;
15 lakini fadhili zangu hazitamwondoka, kama vile nilivyomwondolea Sauli, niliyemwondoa mbele yako.
16 Na nyumba yako, na ufalme wako, vitathibitishwa milele mbele yako. Nacho kiti chako kitafanywa imara milele.
17 Kwa maneno hayo yote, na kwa maono hayo yote, ndivyo Nathani alivyonena na Daudi.
18 Ndipo Daudi, mfalme, akaingia, akaketi mbele za Bwana, akasema, Mimi ni nani, Bwana MUNGU, na nyumba yangu ni nini, hata umenileta hata hapa?
19 Tena jambo hili lilikuwa dogo machoni pako, Ee Bwana MUNGU; hata umeleta habari ya nyumba yangu mimi, mtumwa wako, kwa miaka mingi inayokuja baadaye; na hayo kwa namna ya kibinadamu, Ee Bwana MUNGU.
20 Na mimi, Daudi, nikuambie nini tena zaidi? Iwapo wewe umemjua mtumwa wako, Ee Bwana MUNGU.
21 Kwa ajili ya neno lako, na kwa moyo wako mwenyewe, umetenda makuu hayo yote, ili umjulishe mtumwa wako.
22 Kwa hiyo, wewe ndiwe mkuu, Ee Bwana Mungu, kwa maana hakuna kama wewe, wala hapana Mungu mwingine ila wewe, kwa kadiri tulivyosikia kwa masikio yetu.
23 Tena ni taifa lipi duniani lililo kama watu wako, kama Israeli, ambalo Mungu alikwenda kuwakomboa kwa ajili yake, wawe watu wake mwenyewe, akajifanyie jina, na kutenda mambo makuu kwa ajili yenu, na mambo ya kuogofya kwa ajili ya nchi yako, mbele ya watu wako, uliowakomboa kutoka Misri wawe wako, kutoka katika mataifa na miungu yao.
24 Nawe ulijifanyia imara watu wako Israeli, wawe watu wako milele; nawe, Bwana, umekuwa Mungu wao.
25 Basi sasa, Ee Bwana Mungu, neno lile ulilolinena katika habari za mtumwa wako, na katika habari za nyumba yangu, ulifanye imara milele, ukatende kama ulivyosema.
26 Jina lako na litukuzwe milele, kusema, Bwana wa majeshi ndiye Mungu juu ya Israeli; na nyumba ya mtumwa wako, Daudi, itakuwa imara mbele zako.
27 Kwa kuwa wewe, Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli umenifunulia mimi, mtumwa wako, ukisema, Nitakujengea nyumba; kwa hiyo mimi, mtumwa wako, nimeona vema moyoni mwangu nikuombe dua hii.
28 Na sasa, Ee Bwana MUNGU, wewe ndiwe Mungu, na maneno yako ndiyo kweli, nawe umemwahidia mtumwa wako jambo hili jema
29 basi, sasa, uwe radhi, ukaibarikie nyumba ya mtumwa wako, ipate kudumu milele mbele zako; kwa maana wewe, Ee Bwana MUNGU, umelinena na kwa baraka yako nyumba ya mtumwa wako na ibarikiwe milele.

2 Samweli 8


1 Ikawa baadaye, Daudi akawapiga Wafilisti, akawashinda; Daudi akautwaa Gathi na vijiji vyake mikononi mwa hao Wafilisti.
2 Akapiga Moabu, akawapima kwa kamba hali wamelazwa chini; akapima kamba mbili za kuuawa, na kamba moja nzima ya kuhifadhi hai. Wamoabi wakawa watumwa wa Daudi, wakaleta zawadi.
3 Tena Daudi akampiga Hadadezeri mwana wa Rehobu, mfalme wa Soba, alipokwenda kujipatia tena mamlaka yake huko Mtoni.
4 Daudi akampokonya wapanda farasi elfu na mia saba na askari waliokwenda kwa miguu ishirini elfu; Daudi akawakata mshipa farasi wote wa magari, ila farasi wa magari mia akawasaza.
5 Na Washami wa Dameski walipokuja kumsaidia Hadadezeri, mfalme wa Soba, Daudi akawapiga wa Washami watu ishirini na mbili elfu.
6 Daudi akaweka ngome katika Shamu ya Dameski, na hao Washami wakawa watumwa wa Daudi, wakaleta zawadi. Naye Bwana akampa Daudi kushinda kila alikokwenda.
7 Tena Daudi akazitwaa ngao za dhahabu zilizovaliwa na watumwa wa Hadadezeri, akazileta Yerusalemu.
8 Tena toka Tebhathi na toka Berothai, miji ya Hadadezeri, Daudi akatwaa shaba nyingi mno.
9 Na Tou, mfalme wa Hamathi, aliposikia ya kwamba Daudi amewapiga jeshi lote la Hadadezeri,
10 Tou akamtuma kwa Daudi Hadoramu mwanawe kusalimia, na kumbarikia, kwa sababu amepigana na Hadadezeri, na kumpiga; kwa maana Hadadezeri alikuwa amepigana vita juu ya Tou. Na mkononi mwake akaleta vyombo vya fedha, na vyombo vya dhahabu, na vyombo vya shaba;
11 hivi pia mfalme Daudi akavifanya wakfu kwa Bwana, pamoja na hiyo fedha, na dhahabu alizofanya wakfu za mataifa yote aliowashinda;
12 za Edomu, na za Moabu, na za wana wa Amoni, na za Wafilisti, na za Amaleki, na za nyara za Hadadezeri, mwana wa Rehobu, mfalme wa Soba.
13 Basi Daudi akajipatia jina, aliporudi kutoka kuwapiga Waedomi katika Bonde la Chumvi, watu kumi na nane elfu.
14 Akaweka askari wenye kulinda ngome katika Edomu; katikati ya Edomu yote akaweka ngome, na Waedomi wote wakawa watumwa wa Daudi. Naye Bwana akampa Daudi kushinda kila alikokwenda.
15 Daudi akatawala juu ya Israeli wote; naye Daudi akawafanyia hukumu na haki watu wake wote.
16 Huyo Yoabu, mwana wa Seruya alikuwa juu ya jeshi; na Yehoshafati, mwana wa Ahiludi, mwenye kuandika tarehe;
17 na Sadoki, mwana wa Ahitubu, na Ahimeleki, mwana wa Abiathari walikuwa makuhani; na Shausha mwandishi;
18 na Benaya, mwana wa Yehoyada, alikuwa juu ya Wakerethi na Wapelethi; nao wana wa Daudi wakawa makuhani.

2 Samweli 9


1 Kisha Daudi akasema, Je! Amesalia mtu mmoja katika nyumba ya Sauli, nipate kumtendea mema kwa ajili ya Yonathani?
2 Palikuwa na mtumishi mmoja wa nyumba ya Sauli, jina lake Siba, basi wakamwita aende kwa Daudi; na mfalme akamwuliza, Wewe ndiwe Siba? Naye akasema Mimi, mtumwa wako ndiye.
3 Mfalme akasema, Je! Hakuna hata sasa mtu ye yote wa nyumba ya Sauli, nipate kumtendea mema ya Mungu? Siba akamwambia mfalme, Yonathani anaye mwana hata sasa, aliye na kilema cha mguu.
4 Mfalme akamwambia, Yuko wapi? Siba akamwambia mfalme, Tazama, yumo katika nyumba ya Makiri, mwana wa Amieli, katika Lo-debari.
5 Basi mfalme Daudi akatuma watu, akamwondoa katika nyumba ya Makiri, mwana wa Amieli, katika Lo-debari.
6 Basi Mefiboshethi, mwana wa Yonathani, mwana wa Sauli akaenda kwa Daudi, akaanguka kifudifudi, akasujudu. Daudi akasema, Mefiboshethi! Naye akaitika, Mimi hapa, mtumwa wako!
7 Daudi akamwambia, Usiogope, maana bila shaka nitakutendea mema; kwa ajili ya Yonathani, baba yako, nami nitakurudishia mashamba yote ya Sauli, baba yako; nawe utakula chakula mezani pangu daima.
8 Akasujudu, akasema, Mimi mtumwa wako ni nini, hata ukamwangalia mbwa mfu kama mimi?
9 Ndipo mfalme akamwita Siba, mtumwa wa Sauli, akamwambia, Mali yote yaliyokuwa ya Sauli na ya nyumba yake nimempa mwana wa bwana wako.
10 Nawe utamlimia nchi hiyo, wewe, na wanao, na watumwa wako; nawe utamletea mwana wa bwana wako matunda yake, apate chakula ale; lakini Mefiboshethi, mwana wa bwana wako, atakula chakula mezani pangu sikuzote. Basi huyo Siba alikuwa na wana kumi na watano na watumwa ishirini.
11 Ndipo Siba akamwambia mfalme, Mimi, mtumwa wako, nitatenda hayo yote kama bwana wangu, mfalme, alivyoniamuru. Na kwa habari za Mefiboshethi, mfalme alisema, Atakula mezani pangu, kama mmojawapo wa wana wa mfalme.
12 Huyo Mefiboshethi alikuwa na mwana mdogo, jina lake akiitwa Mika. Na watu wote waliokaa nyumbani mwa Siba walikuwa watumwa wa Mefiboshethi.
13 Basi Mefiboshethi akakaa Yerusalemu; maana alikuwa akila chakula sikuzote mezani pa mfalme; naye alikuwa na kilema cha miguu yote miwili.

2 Samweli 10


1 Ikawa baadaye, mfalme wa wana wa Amori akafa, akamiliki Hanuni, mwanawe, mahali pake.
2 Naye Daudi akasema, Nitamtendea wema Hanuni, mwana wa Nahasi, kama babaye alivyonitendea wema mimi. Basi Daudi akatuma kwa mkono wa watumishi wake, ili kumtuliza kwa habari za babaye. Wakaja watumishi wa Daudi katika nchi ya wana wa Amoni.
3 Lakini wakuu wa wana wa Amoni wakamwambia Hanuni, bwana wao, Je! Waona ya kuwa Daudi amemheshimu babayo kwa kutuma kwako wafariji? Je! Daudi hakuwapeleka watumishi wake kwako ili kuuangalia mji, na kuupeleleza, na kuuangamiza?
4 Basi Hanuni akawatwaa hao watumishi wa Daudi, akawanyoa nusu ya ndevu zao, akawakatia nguo zao katikati, hata matakoni, akawatoa waende zao.
5 Watu walipomwambia Daudi habari hizo, akatuma watu kuwalaki; kwa sababu watu hao walikuwa wametahayarika sana. Mfalme akasema, Ngojeni Yeriko, hata mtakapoota ndevu zenu, ndipo mrudi.
6 Na wana wa Amoni walipoona ya kuwa wamekuwa machukizo kwa Daudi, wana wa Amoni wakatuma na kuwaajiri Washami wa Bethrehobu, na Washami wa Soba, askari ishirini elfu, na mfalme wa Maaka mwenye watu elfu, na watu wa Tobu watu kumi na mbili elfu.
7 Naye Daudi aliposikia akamtuma Yoabu, na jeshi lote la mashujaa.
8 Wana wa Amoni wakatoka, wakapanga vita mahali pa kuingilia lango; na Washami wa Soba, na wa Rehobu, na watu wa Tobu, na wa Maaka, walikuwa peke yao uwandani.
9 Basi Yoabu alipoona ya kwamba uso wa vita umekuwa juu yake mbele na nyuma, akachagua baadhi ya wateule wote wa Israeli, akawapanga juu ya Washami;
10 akawatia nguvu watu waliosalia mkononi mwa Abishai, nduguye, akawapanga juu ya wana wa Amoni.
11 Akasema, Wakiwa Washami hodari mno kwangu, ndipo wewe utanisaidia, lakini wana wa Amoni wakiwa ni hodari mno kwako, ndipo mimi nitakuja nikusaidie wewe.
12 Uwe hodari, tukajitie moyo mkuu, kwa ajili ya watu wetu, na kwa ajili ya miji ya Mungu wetu; naye Bwana afanye yaliyo mema machoni pake.
13 Basi Yoabu na watu waliokuwa pamoja naye wakakaribia kupigana na Washami; nao wakakimbia mbele yake.
14 Na wana wa Amoni walipoona ya kwamba Washami wamekimbia, wakakimbia nao mbele ya Abishai, wakaingia mjini. Ndipo Yoabu akarudi kutoka kwa wana wa Amoni, akaja Yerusalemu.
15 Na Washami walipojiona kuwa wameshindwa mbele ya Israeli, wakakusanyika.
16 Naye Hadadezeri akatuma na kuwaleta Washami waliokuwako ng'ambo ya Mto; nao wakaja Helamu, naye Shobaki, jemadari wa jeshi la Hadadezeri, akawaongoza.
17 Alipoambiwa Daudi, akakusanya Israeli wote, akavuka Yordani, akaja Helamu. Nao Washami wakajipanga kinyume cha Daudi, wakapigana naye.
18 Wakakimbia Washami mbele ya Israeli; naye Daudi akawaua katika Washami, watu wa magari mia saba, na wapanda farasi arobaini elfu, naye akampiga huyo Shobaki, jemadari wa jeshi lao, hata akafa huko.
19 Na wafalme wote waliomtumikia Hadadezeri walipojiona kuwa wameshindwa mbele ya Israeli, walifanya amani na Israeli, wakawatumikia. Basi Washami wakaogopa kuwasaidia wana wa Amoni tena.

2 Samweli 11


1 Hata ikawa, mwanzo wa mwaka mpya, wakati watokapo wafalme kwenda vitani, Daudi akampeleka Yoabu, na watumishi wake pamoja naye, na Israeli wote; wakawaangamiza wana wa Amoni, wakauhusuru Raba. Lakini Daudi mwenyewe akakaa Yerusalemu.
2 Ikawa wakati wa jioni, Daudi akaondoka kitandani, akatembea juu ya dari ya jumba la mfalme; na alipokuwa juu ya dari aliona mwanamke anaoga; naye huyo mwanamke alikuwa mzuri sana, wa kupendeza macho.
3 Naye Daudi akapeleka, akauliza habari za yule mwanamke. Mtu mmoja akasema, Je! Huyu siye Bath-sheba, binti Eliamu, mkewe Uria, Mhiti?
4 Basi Daudi akapeleka wajumbe, akamtwaa; naye akaingia kwake; naye akalala naye; (maana yule mwanamke amekwisha kutakasika unajisi wake); kisha akarudi nyumbani kwake.
5 Yule mwanamke akachukua mimba; basi akapeleka na kumwambia Daudi, akasema, Ni mja-mzito.
6 Ndipo Daudi akapeleka kwa Yoabu, akisema, Unipelekee Uria, Mhiti. Naye Yoabu akampeleka Uria kwa Daudi.
7 Uria alipomwendea Daudi, Daudi alimwuliza habari za Yoabu, na habari za watu, na habari za vita.
8 Daudi akamwambia Uria, Haya, shuka nyumbani kwako, ukanawe miguu yako. Basi Uria akatoka katika nyumba ya mfalme, na tunu ya vyakula ikamfuata, iliyotoka kwa mfalme.
9 Lakini Uria akalala mlangoni pa nyumba ya mfalme, pamoja na watumishi wote wa bwana wake, wala hakushuka nyumbani kwake.
10 Watu walipomwambia Daudi ya kwamba, Uria hakushuka nyumbani kwake, Daudi akamwambia Uria, Je! Hukutoka safarini? Mbona hukushuka nyumbani kwako?
11 Naye Uria akamwambia Daudi, Sanduku, na Israeli, na Yuda, wanakaa vibandani; na bwana wangu Yoabu, na watumishi wa bwana wangu, wamepiga kambi waziwazi uwandani; nami niende nyumbani kwangu, kula na kunywa, na kulala na mke wangu? Uishivyo, na kama roho yako iishivyo, mimi sitafanya jambo hili.
12 Basi Daudi akamwambia Uria, Ngoja hapa leo tena, na kesho nitakuacha kwenda zako. Basi Uria akakaa Yerusalemu siku ile, na siku ya pili yake.
13 Naye Daudi akamwalika, akala, akanywa mbele yake; naye akamlevya; hata wakati wa jioni akatoka kwenda kulala kitandani mwake pamoja na watumishi wa bwana wake, lakini hakushuka nyumbani kwake.
14 Hata ikawa asubuhi, Daudi akamwandikia Yoabu waraka, akaupeleka kwa mkono wa Uria.
15 Akaandika katika waraka huo, kusema, Mwekeni Uria mbele ya watu penye vita vikali, kisha ondokeni, mmwache, ili apigwe akafe.
16 Ikawa, Yoabu alipokuwa akiuhusuru mji, akamweka Uria mahali alipojua ya kuwa pana mashujaa.
17 Watu wa mji wakatoka, wakapigana na Yoabu; na baadhi ya watu, watumishi wa Daudi, wakaanguka; Uria Mhiti naye akafa.
18 Ndipo Yoabu akapeleka na kumwarifu Daudi habari zote za vita;
19 akamwagiza yule mjumbe, akisema, Ukiisha kumpa mfalme habari zote za vita,
20 itakuwa, hasira ya mfalme ikiwaka, akakuambia, Kwani mliukaribia mji namna ile ili kuupiga? Je! Hamkujua ya kuwa watapiga mishale toka ukutani?
21 Ni nani aliyempiga Ahimeleki, mwana wa Yeru-beshethi? Je! Si mwanamke aliyemtupia jiwe la kusagia la juu kutoka ukutani? Hata akafa huko Thebesi? Kwani kuukaribia ukuta namna ile? Ndipo utakaposema, Mtumishi wako Uria, Mhiti, amekufa naye.
22 Basi yule mjumbe akaenda, akafika na kumwonyesha Daudi yote aliyomtuma Yoabu.
23 Yule mjumbe akamwambia Daudi, Watu hao walitushinda, wakatutokea nje hata uwandani, tukashindana nao hata mahali pa kuingilia langoni.
24 Wapiga mishale wakatupiga sisi, watumishi wako, toka juu ya ukuta; na baadhi ya watumishi wa mfalme wamekufa, na Uria, Mhiti, mtumishi wako, amekufa naye.
25 Basi Daudi akamwambia yule mjumbe, Basi, mwambie Yoabu maneno haya, Jambo hili lisiwe baya machoni pako, maana upanga hula huyu kama unavyomla huyu; zidi kutia nguvu vita vyako juu ya mji ukauangushe; nawe mtie moyo.
26 Na yule mke wa Uria alipopata habari ya kuwa Uria mumewe amekufa, akamwombolezea mumewe.
27 Hata maombolezo hayo yalipokwisha, Daudi akatuma mtu, akamtwaa, akamtia nyumbani mwake; naye akawa mkewe, akamzalia mwana. Lakini jambo lile alilolitenda Daudi likamchukiza Bwana.

2 Samweli 12


1 Ndipo Bwana akamtuma Nathani aende kwa Daudi. Naye akamwendea, akamwambia, Palikuwa na watu wawili katika mji mmoja; mmoja wao alikuwa tajiri, wa pili maskini.
2 Yule tajiri alikuwa na kondoo na ng'ombe wengi sana;
3 bali yule maskini hakuwa na kitu, ila mwana kondoo mmoja, mdogo, ambaye amemnunua na kumlea; naye akakua pamoja naye, na pamoja na wanawe; hula sehemu ya posho lake, na kukinywea kikombe chake, na kulala kifuani mwake, akawa kwake kama binti.
4 Hata msafiri mmoja akamfikilia yule tajiri, naye akaacha kutwaa mmoja wa kondoo zake mwenyewe au mmoja wa ng'ombe zake mwenyewe, ili kumwandalia yule msafiri aliyemfikilia, bali alimnyang'anya yule maskini mwana-kondoo wake, akamwandalia yule mtu aliyemfikilia.
5 Ndipo hasira ya Daudi ikawaka sana juu ya mtu yule; akamwambia Nathani, Aishivyo Bwana, mtu huyo aliyetenda jambo hili, hakika yake astahili kufa;
6 naye atamrudishia yule mwana-kondoo mara nne, kwa sababu ametenda neno hili, na kwa sababu hakuwa na huruma.
7 Basi Nathani akamwambia Daudi, Wewe ndiwe mtu huyo. Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Nalikutia mafuta, uwe mfalme juu ya Israeli, nikakuokoa na mkono wa Sauli;
8 nami nikakupa nyumba ya bwana wako, na wake za bwana wako kifuani mwako; nikakupa nyumba ya Israeli na ya Yuda; na kama hayo yangalikuwa machache, ningalikuongezea mambo kadha wa kadha.
9 Kwa nini umelidharau neno la Bwana, na kufanya yaliyo mabaya machoni pake? Umempiga Uria, Mhiti, kwa upanga, nawe umemtwaa mkewe awe mke wako, nawe umemwua huyo kwa upanga wa wana wa Amoni.
10 Basi, sasa upanga hautaondoka nyumbani mwako, kwa sababu umenidharau, ukamtwaa mkewe Uria, Mhiti, kuwa mke wako.
11 Bwana asema hivi, Angalia, nitakuondokeshea uovu katika nyumba yako, nami nitawatwaa wake zako mbele ya macho yako, na kumpa jirani yako, naye atalala na wake zako mbele ya jua hili.
12 Maana wewe ulifanya jambo lile kwa siri; bali mimi nitalifanya jambo hili mbele ya Israeli wote na mbele ya jua.
13 Daudi akamwambia Nathani, Nimemfanyia Bwana dhambi. Nathani akamwambia Daudi, Bwana naye ameiondoa dhambi yako; hutakufa.
14 Lakini, kwa kuwa kwa tendo hili umewapa adui za Bwana nafasi kubwa ya kukufuru, mtoto atakayezaliwa kwako hakika yake atakufa.
15 Naye Nathani akaondoka kwenda nyumbani kwake. Basi Bwana akampiga yule mtoto ambaye mkewe Uria alimzalia Daudi naye akawa hawezi sana.
16 Basi Daudi akamwomba Mungu kwa ajili ya mtoto; Daudi akafunga, akaingia, akalala usiku kucha chini.
17 Nao wazee wa nyumba yake wakaondoka, wakasimama karibu naye, ili wamwinue katika nchi; lakini hakukubali, wala hakula chakula pamoja nao.
18 Ikawa siku ya saba, yule mtoto akafa. Nao watumishi wa Daudi wakaogopa kumwambia ya kuwa mtoto amekufa, maana, walisema, Angalieni, yule mtoto alipokuwa angali hai, tulisema naye, asitusikilize sauti zetu; basi hatazidi kujisumbua, tukimwambia ya kuwa mtoto amekufa?
19 Lakini alipoona ya kuwa watumishi wake wananong'onezana, Daudi alitambua ya kuwa mtoto amekufa; basi Daudi akawauliza watumishi wake, Je! Mtoto amekufa? Nao wakasema, Amekufa.
20 Ndipo Daudi akainuka pale chini akaoga, akajipaka mafuta, akabadili mavazi yake; akaingia nyumbani mwa Bwana, akasali; kisha akaenda nyumbani kwake, na alipotaka wakamwandalia chakula, naye akala.
21 Watumishi wake wakamwambia, Ni neno gani hili ulilolitenda? Ulifunga na kulia kwa ajili ya mtoto, alipokuwa hai; lakini mtoto alipokuwa amekufa, uliinuka ukala chakula.
22 Akasema, Mtoto alipokuwa hai, nalifunga, nikalia; kwa maana nalisema, Ni nani ajuaye kwamba Bwana atanihurumia, mtoto apate kuishi?
23 Lakini sasa amekufa nifungie nini? Je! Naweza kumrudisha tena? Mimi nitakwenda kwake lakini yeye hatanirudia mimi.
24 Naye Daudi akamfariji Bath-sheba mkewe, akaingia kwake, akalala naye; naye akazaa mwana, akamwita jina lake Sulemani. Naye Bwana akampenda;
25 akapeleka kwa mkono wa Nathani, nabii, naye akamwita jina lake Yedidia, kwa ajili ya Bwana.
26 Yoabu akapigana juu ya Raba wa wana wa Amoni, akautwaa mji wa kifalme.
27 Yoabu akatuma wajumbe waende kwa Daudi, kusema Nimeshindana na Raba, hata nimeutwaa huo mji wa maji.
28 Basi sasa kusanya watu waliobaki, ukauzunguke mji, na kuutwaa; nisije mimi nikautwaa mji, ukaitwe jina langu.
29 Basi Daudi akawakusanya watu wote akaenda Raba, akapigana nao, akautwaa.
30 Kisha akamnyang'anya mfalme wao taji toka kichwani pake; na uzani wake ulikuwa talanta ya dhahabu, nayo ilikuwa na vito vya thamani ndani yake; akavikwa Daudi kichwani. Akazitoa nyara za huo mji, nyingi sana.
31 Naye akawatoa watu waliokuwamo, akawaweka kwenye kazi ya misumeno,na sululu za chuma,na mashoka ya chuma,akawatumikisha,tanuuni mwa matofali ndivyo alivyoifanya miji yote ya wana wa Amoni.Kisha Daudi akarudi na watu wote Yerusalemu.

2 Samweli 13


1 Ikawa baada ya hayo, Absalomu, mwana wa Daudi, alikuwa na umbu mzuri, jina lake akiitwa Tamari, naye Amnoni, mwana wa Daudi, akampenda.
2 Akasononeka Amnoni, hata akaugua, kwa ajili ya umbu lake Tamari, maana huyu msichana alikuwa mwanamwali, Amnoni akaona ni vigumu kumtendea neno lo lote.
3 Lakini Amnoni alikuwa na rafiki, jina lake Yonadabu, mwana wa Shama, nduguye Daudi; naye Yonadabu alikuwa mtu mwerevu sana.
4 Naye akamwambia, Kwa nini, Ee mwana wa mfalme, unakonda hivi siku kwa siku? Hutaki kuniambia? Amnoni akamwambia, Nampenda Tamari, umbu la ndugu yangu, Absalomu.
5 Yonadabu akamwambia, Lala kitandani mwako ujifanye mgonjwa na babako atakapokuja kukutazama, umwambie, Mwache ndugu yangu, Tamari, aje, nakusihi, anipe mkate nile, akaandae chakula machoni pangu nikione, nikakile mkononi mwake.
6 Basi Amnoni akalala, akajifanya mgonjwa; na mfalme alipokuja kumtazama, Amnoni akamwambia mfalme Mwache ndugu yangu, Tamari, aje, nakusihi, aniandalie mikate miwili machoni pangu, nipate kula mkononi mwake.
7 Basi Daudi akatuma mjumbe aende nyumbani kwa Tamari, akasema, Nenda sasa nyumbani kwa Amnoni, ndugu yako, ukamwandalie chakula.
8 Akaenda Tamari nyumbani kwa nduguye Amnoni; naye alikuwa amelala. Akachukua unga, akaukanda, akaiandaa mikate machoni pake, akaioka mikate.
9 Akalitwaa kaango, akaisongeza mbele yake; lakini alikataa kula. Naye Amnoni akasema, Toeni watu wote kwangu. Wakatoka kila mtu kwake.
10 Amnoni akamwambia Tamari, Kilete chakula chumbani, nipate kula mkononi mwako. Basi Tamari akaitwaa mikate aliyoifanyiza, akamletea Amnoni nduguye mle chumbani.
11 Naye alipokwisha kuileta karibu naye, ili ale, Amnoni akamkamata, akamwambia, Njoo ulale nami, ndugu yangu.
12 Naye akamjibu, La, sivyo, ndugu yangu, usinitenze nguvu; kwani haifai kutendeka hivi katika Israeli; usitende upumbavu huu.
13 Nami nichukue wapi aibu yangu? Wewe nawe utakuwa kama mmoja wa wapumbavu wa Israeli. Basi, sasa, nakusihi, useme na mfalme; kwa maana hatakukataza kunioa.
14 Walakini yeye hakukubali kusikiliza sauti yake; naye akiwa na nguvu kuliko yeye, akamtenza nguvu, akalala naye.
15 Kisha Amnoni akamchukia machukio makuu sana; kwa kuwa machukio aliyomchukia yakawa makuu kuliko yale mapenzi aliyokuwa amempenda kwanza. Amnoni akamwambia, Ondoka, nenda zako.
16 Naye akamwambia, Sivyo, kwa kuwa mabaya haya ya kunitoa ni makuu kuliko yale uliyonitendea. Lakini alikataa kumsikiliza.
17 Ndipo akamwita mtumishi wake aliyemtumikia, akasema, Mtoe sasa mwanamke huyu kwangu, ukafunge mlango nyuma yake.
18 Naye alikuwa amevaa kanzu ndefu; kwa kuwa kwa nguo hizo huvikwa binti za mfalme waliokuwa wanawali. Ndipo mtumishi wake akamleta nje, akafunga mlango nyuma yake.
19 Naye Tamari akatia majivu kichwani mwake, akairarua hiyo kanzu ndefu yake aliyoivaa, akaweka mkono kichwani akaenda zake huku akilia kwa sauti.
20 Huyo Absalomu nduguye akamwambia, je! Amekuwa nawe Amnoni nduguyo? Ila sasa tulia, dada; ni nduguyo; usilitie moyoni jambo hili. Basi Tamari akakaa hali ya ukiwa nyumbani mwa nduguye Absalomu.
21 Na mfalme Daudi alipoyasikia maneno hayo yote, alikasirika sana.
22 Ila Absalomu hakusema na Amnoni wala kwa heri wala kwa shari; kwa maana Absalomu alimchukia Amnoni kwa kumtenza nguvu umbu lake Tamari.
23 Ikawa baada ya miaka miwili mizima, Absalomu alikuwa na wenye kukata manyoya ya kondoo huko Baal-hasori uliopo upande wa Efraimu; naye Absalomu akawaalika wana wote wa mfalme.
24 Absalomu akamjia mfalme, akasema, Tazama sasa, mimi mtumwa wako ninao wakata manyoya ya kondoo; basi mfalme na aende, nakusihi, na watumishi wake pamoja nami mtumwa wako.
25 Mfalme akamwambia Absalomu, Sivyo, mwanangu, tusiende sote, tusije tukakulemea. Akamsihi sana; asikubali kwenda, ila akambariki.
26 Ndipo akasema Absalomu, Kwamba huji, nakusihi, mwache ndugu yangu Amnoni aende nasi.
27 Mfalme akamwambia, Kwa nini aende nawe? Lakini Absalomu akamsihi sana, naye akamwacha Amnoni na wana wote wa mfalme waende naye.
28 Kisha Absalomu akawaamuru watumishi wake, akasema, Angalieni basi, moyo wake Amnoni utakapofurahiwa kwa mvinyo; nami nitakapowaambia, Mpigeni Amnoni, ndipo mwueni, msiogope; si mimi niliyewaamuru? Iweni hodari, iweni na ujasiri.
29 Basi watumishi wa Absalomu wakamfanyia Amnoni kama alivyoamuru Absalomu. Ndipo wakaondoka wana wote wa mfalme, wakapanda kila mtu nyumbu wake, wakakimbia.
30 Ikawa, walipokuwa njiani, habari zikamwasilia Daudi, kusema, Absalomu amewaua wana wote wa mfalme, wala hata mmoja wao hakusalia.
31 Ndipo mfalme akainuka, akararua nguo zake, akalala chini; nao watumishi wake wote wakasimama karibu naye, wenye nguo zao zimeraruliwa.
32 Akajibu Yonadabu, mwana wa Shama, nduguye Daudi, akasema, Asidhani bwana wangu ya kwamba wamewaua vijana wote, wana wa mfalme; maana ndiye Amnoni peke yake aliyekufa; yakini haya yamekusudiwa kwa kinywa chake Absalomu tangu siku ile alipotenzwa nguvu umbu lake, Tamari.
33 Basi sasa bwana wangu mfalme asilitie neno hili moyoni, kudhani ya kwamba wana wote wa mfalme wamekufa maana ni Amnoni peke yake aliyekufa.
34 Lakini Absalomu akakimbia. Na kijana yule aliyekuwa mlinzi akainua macho yake, akaona, na tazama, kuna watu wengi wanakuja kwa njia ya upande wa kilima nyuma yake.
35 Ndipo Yonadabu akamwambia mfalme, Tazama, wana wa mfalme wamekuja; kama mimi mtumwa wako nilivyosema, ndivyo ilivyo.
36 Ikawa alipokwisha kusema, tazama, wana wa mfalme walikuja, nao wakapaza sauti zao wakalia; mfalme naye akalia, na watumishi wake wote, kilio kikubwa mno.
37 Lakini Absalomu akakimbia, akamwendea Talmai, mwana wa Amihuri, mfalme wa Geshuri. Naye Daudi akamlilia mwanawe kila siku.
38 Basi Absalomu akakimbia, akaenda Geshuri, akakaa huko muda wa miaka mitatu.
39 Mfalme Daudi akatamani kutoka kumwendea Absalomu kwa kuwa ametulizwa kwa habari ya Amnoni, kwa maana amekufa.

2 Samweli 14


1 Basi Yoabu, mwana wa Seruya, akatambua ya kuwa moyo wa mfalme unamwelekea Absalomu.
2 Yoabu akatuma watu waende Tekoa, akaleta kutoka huko mwanamke mwenye akili, akamwambia, Nakusihi, ujifanye kama unakaa matanga, ukavae nguo za kufiwa, nakusihi, wala usijitie mafuta, ila ukafanane na mwanamke aliyeomboleza siku nyingi kwa ajili yake aliyefariki;
3 kisha uingie kwa mfalme ukamwambie maneno haya. Hivyo Yoabu akamtia maneno kinywani.
4 Naye yule mwanamke wa Tekoa aliponena na mfalme, akaanguka kifulifuli chini, akamsujudia, akasema, Nisaidie, Ee mfalme.
5 Mfalme akamwuliza, Una nini? Naye akajibu, Hakika ni mjane mimi, niliyefiwa na mume wangu.
6 Nami mjakazi wako nalikuwa na wana wawili, na hao wawili wakashindana uwandani, wala hapakuwa na mtu wa kuwaamua, lakini mmoja akampiga mwenzake, akamwua.
7 Na tazama, jamaa yote wameniinukia mimi mjakazi wako, wakasema, Mtoe yule aliyempiga nduguye, ili tupate kumwua yeye kwa maisha ya nduguye aliyemwua, hata na kumfisha mrithi pia; ndivyo watakavyolizima kaa langu lililobaki, wasimwachie mume wangu jina wala masalio usoni pa nchi.
8 Mfalme akamwambia huyo mwanamke, Nenda nyumbani kwako, nami nitakufanyia agizo.
9 Ndipo huyo mwanamke wa Tekoa akamwambia mfalme, Na uwe juu yangu, Ee bwana wangu mfalme, na juu ya nyumba ya baba yangu uovu huu; wala kwa mfalme na kwa kiti chake cha enzi pasiwepo hatia.
10 Mfalme akasema, Ye yote atakaye kuambia neno, mlete kwangu, naye hatakugusa tena.
11 Ndipo akajibu, Nakusihi, mfalme na amkumbuke Bwana, Mungu wako, ili mlipiza kisasi cha damu asizidi kuharibu, wasije kumharibu mwanangu. Naye akasema, Aishivyo Bwana, hautaanguka chini hata unywele mmoja wa mwanao.
12 Mwanamke akasema, Mwache mjakazi wako, nakusihi, niseme neno moja kwa bwana wangu mfalme. Akasema, Haya nena.
13 Mwanamke akasema, Kwa nini basi wewe umewafikiria mambo kama hayo watu wa Mungu? Kwani kwa kunena neno hili mfalme ni kama mwenye hatia, kwa kuwa mfalme hamleti kwao tena yule mfukuzwa wake.
14 Kwa kuwa hatuna budi kufa, nasi tu kama maji yaliyomwagika chini, yasiyowezekana kuzoleka tena; wala Mungu haondoi maisha ila hufikiri shauri, kwamba yeye aliyefukuzwa asiwe mkimbizi kwake.
15 Hata sasa nilivyokuja mimi kunena neno hili na bwana wangu mfalme, ni kwa sababu watu wamenitisha; nami, mjakazi wako, nikasema, Mimi nitanena sasa kwa mfalme; labda itakuwa mfalme atanifanyia haja yangu mimi mtumwa wake.
16 Kwa kuwa mfalme atasikia, ili amwokoe mtumwa wake mkononi mwa yule mtu atakaye kuniharibu mimi na mwanangu pia katika urithi wa Mungu.
17 Ndipo mimi mjakazi wako nikasema, Neno la bwana wangu mfalme na liwe la kustarehesha; kwa kuwa kama malaika wa Mungu ndivyo alivyo bwana wangu mfalme, kuyapambanua yaliyo mema na yaliyo mabaya; naye Bwana, Mungu wako na awe pamoja nawe.
18 Ndipo mfalme akajibu, akamwambia yule mwanamke, usinifiche, nakusihi, neno lo lote nitakalokuuliza. Na mwanamke akasema, Na anene sasa bwana wangu mfalme.
19 Mfalme akasema, Je! Si mkono wa Yoabu ulio pamoja nawe katika haya yote? Mwanamke akajibu, akasema, Kama iishivyo roho yako, bwana wangu, mfalme, hapana mtu awezaye kugeuka kwa kuume, au kwa kushoto, kukana neno lo lote alilolisema bwana wangu mfalme; kwani mtumwa wako Yoabu ndiye aliyeniamuru, na kuyaweka maneno haya yote kinywani mwa mjakazi wako;
20 mtumwa wako Yoabu ameyatenda haya ili kubadili uso wa jambo hili; na bwana wangu anayo akili, kama akili ya malaika wa Mungu, hata ajue mambo yote ya duniani.
21 Basi mfalme akamwambia Yoabu, Angalia sasa, nimekata shauri hili; nenda, ukamrudishe tena yule kijana Absalomu.
22 Naye Yoabu akaanguka kifulifuli hata nchi, akasujudu, akambariki mfalme, Yoabu akasema, Leo mimi mtumwa wako najua ya kwamba nimepata neema machoni pako, bwana wangu mfalme, kwa kuwa mfalme amemfanyia mtumwa wake haja yake.
23 Basi Yoabu akaondoka, akaenda Geshuri, akamleta Absalomu Yerusalemu.
24 Naye mfalme akasema, Ageukie nyumbani kwake, asinione uso wangu. Basi Absalomu akarejea nyumbani kwake, asimwone uso mfalme.
25 Basi katika Israeli wote hapakuwa na mtu hata mmoja mwenye kusifiwa kwa uzuri wake kama huyo Absalomu; tangu nyayo za miguu yake hata utosi wa kichwa chake hapakuwa na ila kwake.
26 Naye aliponyoa kichwa, (basi mwisho wa kila mwaka hunyoa; na kwa sababu nywele zilikuwa nzito kwake, kwa hiyo akanyoa;) hupima nywele za kichwa chake shekeli mia mbili kwa uzani wa mfalme.
27 Kisha wakazaliwa kwake Absalomu wana watatu na binti mmoja, ambaye jina lake aliitwa Tamari; naye alikuwa mwanamke mzuri wa uso.
28 Absalomu akakaa miaka miwili mizima katika Yerusalemu; asimwone uso mfalme.
29 Ndipo Absalomu akatuma kumwita Yoabu, ampeleke kwa mfalme, lakini yeye akakataa kumjia; akatuma tena mara ya pili, lakini akakataa kuja.
30 Kwa hiyo akawaambia watumishi wake, Tazameni, shamba la Yoabu liko karibu na shamba langu, naye ana shayiri huko; nendeni mkalitie moto. Basi watumishi wa Absalomu wakalitia moto lile shamba.
31 Ndipo akaondoka Yoabu, akamwendea Absalomu nyumbani kwake, akamwambia, Kwa nini watumishi wako wamelitia moto shamba langu?
32 Absalomu akamjibu Yoabu, Angalia, nilituma kwako, kusema, Njoo kwangu, ili nikupeleke kwa mfalme kunena, Mbona nimekuja kutoka Geshuri? Ingekuwa heri kwangu kama ningekuwako huko hata sasa; basi sasa na nimtazame uso mfalme; na ukiwapo uovu kwangu, na aniue.
33 Basi Yoabu akamwendea mfalme, akamwambia hayo, naye alipomwita Absalomu, yeye akaja kwa mfalme, akainama kifulifuli hata nchi mbele ya mfalme; naye mfalme akambusu Absalomu.

2 Samweli 15


1 Ikawa baada ya hayo, Absalomu akajiwekea tayari gari na farasi, na watu hamsini wa kupiga mbio mbele yake.
2 Tena Absalomu huondoka asubuhi na mapema, na kusimama kando ya njia ya lango; kisha ikawa, mtu ye yote aliyekuwa na neno, lililokuwa halina budi kufika kwa mfalme ili kuhukumiwa, Absalomu humwita mtu huyo kwake, na kumwuliza, Wewe u mtu wa mji gani? Naye akasema, Mtumwa wako ni mtu wa kabila fulani ya Israeli.
3 Naye Absalomu humwambia, Tazama, maneno yako ni mema yenye haki; lakini hapana mtu aliyeagizwa na mfalme kukusikiliza.
4 Tena Absalomu husema, Laiti mimi ningewekwa kuwa mwamuzi katika nchi hii, ili kila mtu mwenye neno au daawa aje kwangu, nimpatie haki yake!
5 Tena ikawa hapo alipokaribia mtu ye yote kumsujudia, hunyosha mkono wake, na kumshika, na kumbusu.
6 Hivyo ndivyo Absalomu alivyowatendea Israeli wote, waliomwendea mfalme ili wapate hukumu; na hivyo Absalomu akawadanganya watu wa Israeli.
7 Hata ikawa mwisho wa miaka minne, Absalomu akamwambia mfalme Tafadhali uniache niende nikaondoe nadhiri yangu, niliyomwekea Bwana huko Hebroni.
8 Maana mimi mtumishi wako naliweka nadhiri hapo nilipokuwa nikikaa Geshuri katika Shamu, nikasema, Kama Bwana akinirudisha Yerusalemu kweli, ndipo nitamtumikia Bwana.
9 Naye mfalme akamwambia, Enenda na amani. Basi akaondoka, akaenda Hebroni.
10 Lakini Absalomu akapeleka wapelelezi katika kabila zote za Israeli kusema, Mara mtakaposikia sauti ya tarumbeta, ndipo mtakaposema Absalomu anamilikl huko Hebroni.
11 Na watu mia mbili walioalikwa wakatoka Yerusalemu pamoja na Absalomu, wakaenda katika ujinga wao wasijue neno lo lote.
12 Absalomu naye akatuma kumwita Ahithofeli Mgiloni, mshauri wake Daudi, kutoka katika mji wake, yaani, Gilo, alipokuwa akitoa dhabihu. Fitina yao ikawa na nguvu; maana watu waliokuwa pamoja na Absalomu wakazidi kuwa wengi.
13 Mjumbe akamfikilia Daudi, akasema, Mioyo ya watu wa Israeli inashikamana na Absalomu.
14 Basi Daudi akawaambia watumishi wake wote waliokuwa pamoja naye Yerusalemu, Ondokeni, tukakimbie kwa kuwa tusipokimbia hapana mtu miongoni mwetu atakayeokoka mikononi mwa Absalomu; haya! Fanyeni haraka, tuondoke, asitupate kwa upesi, na kutuletea maovu, na kuupiga mji huu kwa makali ya upanga.
15 Hao watumishi wa mfalme wakamwambia mfalme, Angalia, sisi watumishi wako tu tayari kutenda lo lote atakalolichagua bwana wetu mfalme.
16 Basi mfalme akatoka na watu wa nyumbani mwake wote wakafuatana naye. Mfalme akaacha wanawake kumi, masuria, ili kuitunza nyumba.
17 Mfalme akatoka, na watu wote wakamfuata; wakakaa kidogo katika Beth-merhaki.
18 Watumishi wake wote wakapita karibu naye; na Wakerethi wote, na Wapelethi wote, na Wagiti wote, watu mia sita walioandamana naye kutoka Gathi, wakapita mbele ya mfalme.
19 Ndipo mfalme akamwambia Itai, Mgiti, Mbona wewe unakwenda pamoja nasi? Rudi, ukakae na mfalme; maana wewe u mgeni, tena u mtu uliyefukuzwa mahali pako mwenyewe.
20 Kwa kuwa umekuja jana tu kwa nini nikusumbue leo, na kukuzungusha huko na huko pamoja nasi nami hapa naenda niwezapo kwenda? Rudi wewe, ukawarudishe na ndugu zako; rehema na kweli ziwe pamoja nawe.
21 Naye Itai akamjibu mfalme akasema, Kama aishivyo Bwana, na bwana wangu mfalme aishivyo, hakika yake kila mahali atakapokuwapo mfalme, bwana wangu, ikiwa ni kwa kufa au ikiwa ni kwa kuishi, ndipo atakapokuwapo na mtumwa wako.
22 Basi Daudi akamwambia Itai, Haya, enenda ukavuke. Akavuka Itai, Mgiti na watu wake wote, na watoto wadogo wote waliokuwa pamoja naye.
23 Na nchi yote ikalia kwa sauti kuu, nao watu wote wakavuka, mfalme mwenyewe naye akavuka kile kijito Kidroni, na hao watu wote wakavuka, wakielekea njia ya nyika.
24 Na tazama, Sadoki naye akaja, na Walawi wote pamoja naye, huku wakilichukua sanduku la agano la Mungu; kisha wakalitua hilo sanduku la Mungu; Abiathari naye akapanda juu, hata watu wote walipokwisha kuutoka mji.
25 Naye mfalme akamwambia Sadoki, Rudisha sanduku la Mungu mjini; nikipata kibali machoni pa Bwana atanirudisha, na kunionyesha tena sanduku hili, na maskani yake;
26 lakini akisema kama hivi, Mimi si radhi nawe kabisa; basi, mimi hapa, na anitendee kama aonavyo kuwa vyema.
27 Kisha mfalme akamwambia Sadoki, kuhani, Angalia, rudini mjini kwa amani, na wana wenu wawili pamoja nanyi,Ahimaasi,mwana wako, na Yonathani,mwana wa Abiathari.
28 Angalia, mimi nitangoja penye vivuko vya jangwani, hata litakaponifikilia neno la kunipasha habari kutoka kwenu.
29 Basi Sadoki na Abiathari wakalichukua sanduku la Mungu, wakalirudisha Yerusalemu; wakakaa huko.
30 Daudi akapanda akishika njia ya kuupandia mlima wa Mizeituni, akilia alipokuwa akipanda; naye alikuwa amejifunika kichwa chake, akaenda hana viatu; na watu wote waliokuwa pamoja naye wakajifunika vichwa vyao, kila mmoja wao, wakapanda juu, wakilia walipopanda.
31 Mtu mmoja akamwambia Daudi ya kwamba, Ahithofeli yu katika hao waliopatana na Absalomu; Daudi akasema, Ee Bwana, nakusihi, uligeuze shauri la Ahithofeli liwe ubatili.
32 Ikawa, Daudi alipofika juu, hapo Mungu alipoabudiwa, tazama, Hushai, Mwarki, akaja kumlaki na joho lake limeraruliwa, tena ana udongo kichwani mwake.
33 Daudi akamwambia, Ukienda mbele pamoja nami, utakuwa mzigo kwangu;
34 lakini ukirudi mjini, na kumwambia Absalomu, Nitakuwa mtumishi wako, Ee mfalme; kama vile nilivyokuwa mtumishi wa baba yako tokea zamani, ndivyo nitakavyokuwa mtumishi wako sasa; ndipo utayavunja mashauri ya Ahithofeli kwa ajili yangu.
35 Je! Hawako Sadoki na Abiathari, makuhani, pamoja nawe huko? Basi itakuwa, kila neno utakalolisikia katika jumba la mfalme, utawaambia Sadoki na Abiathari, makuhani.
36 Angalia, wanao huko pamoja nao wana wao wawili, Ahimaasi, mwana wa Sadoki, na Yonathani, mwana wa Abiathari; nanyi kwa mikono yao mtanipelekea habari ya kila neno mtakalolisikia.
37 Basi Hushai, rafiki wa Daudi, akaingia ndani ya mji; naye Absalomu akafika akaingia Yerusalemu.

2 Samweli 16


1 Naye Daudi alipokipita punde hicho kilele cha mlima, tazama, Siba, mtumwa wa Mefiboshethi, akamkuta, na punda wawili waliotandikwa, na juu yao mikate mia mbili ya ngano, na vishada mia vya zabibu kavu, na matunda mia ya wakati wa hari, na kiriba cha divai.
2 Mfalme akamwambia Siba, Ni za nini hizi? Siba akasema, Punda ni za jamaa ya mfalme wazipande; na mkate na matunda ni chakula cha hawa vijana; na divai ni kwamba wanywe hao wazimiao nyikani.
3 Mfalme akasema, Na mwana wa bwana wako yuko wapi? Siba akamwambia mfalme, Angalia, anakaa Yerusalemu; kwani alisema, Leo nyumba ya Israeli watanirudishia ufalme wa baba yangu.
4 Ndipo mfalme akamwambia Siba, Tazama, yote yaliyokuwa ni mali ya Mefiboshethi ni yako. Siba akasema, Mimi nasujudu; na nione kibali machoni pako, Ee bwana wangu, mfalme.
5 Basi mfalme Daudi alipofika Bahurimu, tazama, kulitoka huko mtu wa jamaa ya nyumba ya Sauli, jina lake akiitwa Shimei, mwana wa Gera; alitoka, akalaani alipokuwa akienda.
6 Tena akamtupia Daudi mawe, na watumishi wote wa mfalme Daudi; na watu wote na mashujaa wote walikuwako mkono wake wa kuume na mkono wake wa kushoto.
7 Na Shimei alipolaani, alisema hivi, Nenda zako! Nenda zako! Ewe mtu wa damu! Ewe mtu usiyefaa!
8 Bwana amerudisha juu yako damu yote ya nyumba ya Sauli ambaye umetawala badala yake; naye Bwana ametia ufalme katika mkono wa Absalomu mwanao; kisha, angalia, wewe umetwaliwa katika uovu wako mwenyewe, kwa sababu umekuwa mtu wa damu.
9 Ndipo Abishai mwana wa Seruya, akamwambia mfalme, Mbona mbwa mfu huyu amlaani mfalme bwana wangu? Na nivuke, nakusihi, nikaondoe kichwa chake.
10 Mfalme akasema, Nina nini na ninyi, enyi wana wa Seruya? Kwa sababu yeye analaani, na kwa sababu Bwana amemwambia, Mlaani Daudi, basi, ni nani atakayesema, Mbona umetenda haya?
11 Daudi akamwambia Abishai, na watumishi wake wote, Angalieni, huyu mwanangu, aliyetoka viunoni mwangu, anautafuta uhai wangu; si zaidi Mbenyamini huyu sasa? Mwacheni alaani, kwa sababu Bwana ndiye aliyemwagiza.
12 Labda Bwana atayaangalia mabaya yaliyonipata, naye Bwana atanilipa mema kwa sababu ya kunilaani kwake leo.
13 Basi wakaendelea njiani Daudi na watu wake; Shimei naye akaaendelea juu ya ubavu wa kile kilima, kwa kumkabili, huku akiendelea, akilaani, akimtupia mawe, na kurusha mavumbi.
14 Naye mfalme na watu wake wote waliokuwa pamoja naye wakafika, wamechoka sana; naye akajiburudisha huko.
15 Absalomu, na hao watu wote wa Israeli, wakafika Yerusalemu, naye Ahithofeli alikuwa pamoja naye.
16 Ikawa, Hushai, Mwarki, rafiki wa Daudi, alipomjia Absalomu, Hushai akamwambia Absalomu, Na aishi mfalme, aishi mfalme.
17 Naye Absalomu akamwambia Hushai, Je! Huu ndio wema wako kwa rafiki yako? Mbona hukutoka pamoja na rafiki yako?
18 Hushai akamwambia Absalomu, La, sivyo; lakini yule Bwana aliyemchagua, na watu hawa, na watu wote wa Israeli, mimi nitakuwa wake, na pamoja naye nitakaa.
19 Na tena, Ni nani ambaye yanipasa nimtumikie? Hainipasi kutumika mbele ya mwanawe? Kama nilivyotumika mbele ya baba yako, ndivyo nitakavyokuwa mbele yako.
20 Kisha Absalomu akamwambia Ahithofeli, Haya, toa shauri lako, tufanyeje.
21 Naye Ahithofeli akamwambia Absalomu, Ingia wewe kwa masuria ya baba yako, hao aliowaacha ili kutunza nyumba; na Israeli wote watasikia ya kuwa umechukizwa kabisa na baba yako; ndipo itatiwa nguvu mikono yao wote walio pamoja nawe.
22 Basi wakamtandikia Absalomu hema juu ya nyumba darini; naye Absalomu akaingia kwa masuria ya babaye machoni pa Israeli wote.
23 Na shauri lake Ahithofeli, alilokuwa akilitoa siku zile, lilikuwa kama mtu aulizapo kwa neno la Mungu; ndivyo yalivyokuwa mashauri yote ya Ahithofeli, kwa Daudi, na kwa Absalomu.

2 Samweli 17


1 Zaidi ya hayo Ahithofeli akamwambia Absalomu, Niache nichague watu kumi na mbili elfu, nami nitaondoka na kumfuatia Daudi usiku huu;
2 nami nitamshambulia wakati atakaokuwa amechoka, na mikono yake imekuwa dhaifu, nami nitamtia hofu; na watu wote walio pamoja naye watakimbia; nami nitampiga mfalme peke yake;
3 na hao watu wote nitawarejeza kwako; mtu yule umtafutaye ni kana kwamba wamerudi wote; na hivyo watu wote watakuwa katika amani.
4 Shauri hili likawa jema machoni pa Absalomu, na machoni pa wazee wote wa Israeli.
5 Ndipo Absalomu akasema, Basi, mwiteni Hushai, Mwarki, naye, tukasikie atakayosema yeye pia.
6 Basi Hushai alipofika kwa Absalomu, Absalomu akamwambia, akasema, Ahithofeli amesema hivi; je! Tufanye kama alivyosema? Kama sivyo, sema maneno yako.
7 Hushai akamwambia Absalomu, Shauri hili alilolitoa Ahithofeli si jema wakati huu.
8 Hushai akafuliza kusema, Wamjua baba yako na watu wake, ya kuwa ni watu mashujaa hawa, nao wana uchungu katika mioyo yao, kama dubu aliyenyang'anywa watoto wake nyikani; tena baba yako ni mtu wa vita, hatalala pamoja na watu wake.
9 Angalia, amefichwa sasa katika shimo, au penginepo; kisha itakuwa, watakapoanguka baadhi yao mwanzo, kila mtu atakayesikia, atasema, Kuna machinjo katika watu wanaofuatana na Absalomu.
10 Basi hata yeye aliye shujaa, mwenye moyo kama moyo wa simba, atayeyuka kabisa; maana Israeli wote wanajua ya kuwa baba yako ni shujaa, na ya kuwa watu wale walio pamoja naye ni mashujaa.
11 Kwa hiyo shauri langu ni hili, Waisraeli wote toka Dani mpaka Beer-sheba wakusanyike kwako, kama mchanga wa bahari kwa wingi; na wewe uende vitani mwenyewe.
12 Hivyo tutamfikia mahali po pote atakapoonekana, na kumwangukia kama vile umande uangukavyo juu ya nchi; wala hatutaacha hata mmoja wao, yeye na watu wote walio pamoja naye.
13 Tena, ikiwa amejitia katika mji uwao wote, basi Israeli wote wataleta kamba, na kuuendea mji ule, nasi tutaukokota mpaka mtoni, wala halitaonekana huko hata jiwe dogo moja la mawe yake.
14 Naye Absalomu na watu wote wa Israeli wakasema, Shauri la Hushai, Mwarki, ni jema kuliko shauri la Ahithofeli. Kwa maana Bwana alikuwa amekusudia kulivunja shauri jema la Ahithofeli, ili Bwana alete mabaya juu ya Absalomu.
15 Ndipo Hushai akawaambia Sadoki na Abiathari, makuhani, Ahithofeli amempa Absalomu na wazee wa Israeli mashauri kadha wa kadha; na mimi nimetoa mashauri kadha wa kadha.
16 Basi sasa pelekeni habari upesi kamwambieni Daudi ya kwamba, Usilale usiku huu karibu na vivuko vya jangwani; bali usikose kuvuka; asije akamezwa mfalme, na watu wote walio pamoja naye.
17 Basi Yonathani na Ahimaasi walikuwa wakikaa karibu na Enrogeli; na mjakazi mmoja alikuwa akienda na kuwapa habari; nao huenda kumwambia mfalme Daudi; maana ilikuwa lazima wasionekane wakiingia mjini.
18 Lakini kijana mmoja aliwaona, akamwambia Absalomu; basi wakaenda wote wawili kwa haraka, wakafika Bahurimu, nyumbani kwa mtu aliyekuwa na kisima uani mwake; wakashuka ndani yake.
19 Na mwanamke akatwaa kifuniko akakiweka juu ya mdomo wa kile kisima, akaanika ngano iliyotwangwa juu yake; wala halikujulikana neno lo lote.
20 Nao watumishi wa Absalomu wakamwendea yule mwanamke mle nyumbani; wakasema, Wako wapi Yonathani na Ahimaasi? Yule mwanamke akawaambia, Wamevuka kijito cha maji. Basi walipokwisha kuwatafuta wasiwaone, wakarudi Yerusalemu.
21 Kisha ikawa, baada ya kuondoka kwao, wale wakatoka kisimani, wakaenda wakamwarifu mfalme Daudi; wakamwambia Daudi, Ondokeni, mkavuke maji haya upesi; maana ndivyo alivyotoa shauri Ahithofeli juu yenu.
22 Ndipo Daudi, na watu wote waliokuwa pamoja naye, wakaondoka, wakavuka Yordani; na kulipopambazuka hakubaki mmojawapo wao asiyevuka Yordani.
23 Naye Ahithofeli alipoona ya kuwa shauri lake halikufuatwa, akatandika punda wake, akaondoka, akaenda nyumbani kwake, mjini mwake, akaitengeneza nyumba yake, akajisonga; akafa, akazikwa kaburini mwa babaye.
24 Basi Daudi akaja Mahanaimu. Naye Absalomu akauvuka Yordani yeye na watu wote wa Israeli pamoja naye.
25 Naye Absalomu akamweka Amasa awe juu ya jeshi mahali pa Yoabu. Basi huyo Amasa alikuwa mwana wa mtu, jina lake Yetheri, Mwishmaeli, aliyeingia kwa Abigali, binti Nahashi, nduguye Seruya, mamaye Yoabu.
26 Israeli na Absalomu wakapiga kambi katika nchi ya Gileadi.
27 Ikawa, Daudi alipofika Mahanaimu, Shobi, mwana wa Nahashi wa Raba, wa wana wa Amoni, na Makiri, mwana wa Amieli wa Lo-debari, na Barzilai, Mgileadi wa Rogelimu,
28 wakaleta magodoro, na mabakuli, na vyungu, na ngano, na shayiri, na unga, na bisi, na kunde, na dengu,
29 na asali, na siagi, na kondoo, na samli ya ng'ombe, wapate kula Daudi na watu waliokuwa pamoja naye; kwani walisema, Watu hao waona njaa, tena wamechoka, nao wana kiu huku nyikani.

2 Samweli 18


1 Kisha Daudi akawahesabu watu waliokuwa pamoja naye, akaweka maakida wa elfu elfu, na maakida wa mia mia juu yao.
2 Daudi akawapeleka hao watu vitani, theluthi moja chini ya mkono wa Yoabu, na theluthi ya pili chini ya mkono wa Abishai, mwana wa Seruya nduguye Yoabu, na theluthi ya tatu chini ya mkono wa Itai, Mgiti. Mfalme akawaambia watu, Bila shaka mimi mwenyewe nami nitatoka pamoja nanyi.
3 Lakini watu wakasema, Wewe usitoke nje; kwa maana tukikimbia, hawatatuona sisi kuwa kitu; au tukifa nusu yetu, hawatatuona kuwa kitu; lakini wewe u wa thamani kuliko watu elfu kumi katika sisi; kwa hivyo sasa ni afadhali ukae tayari kutusaidia toka mjini.
4 Mfalme akawaambia, Yaliyo mema machoni penu ndiyo nitakayofanya. Basi mfalme akasimama kando ya lango, na hao watu wakatoka kwa elfu zao na mia zao.
5 Mfalme akawaamuru Yoabu na Abishai na Itai, akasema, Mtendeeni yule kijana, Absalomu, kwa upole kwa ajili yangu. Nao watu wote wakasikia, mfalme alipowaagiza maakida wote katika habari za Absalomu.
6 Hivyo watu wakatoka waende nyikani ili kupigana na Israeli; na vita vikatokea ndani ya msitu wa Efraimu.
7 Watu wa Israeli wakapigwa huko mbele ya watumishi wa Daudi, kukawa na maangamizo makuu huko siku ile, ya watu ishirini elfu.
8 Kwa maana vita vilienea huko juu ya uso wote wa nchi; na siku ile huo msitu ukala watu wengi kuliko wale walioliwa na upanga.
9 Na kwa bahati Absalomu akakutana na watumishi wa Daudi. Naye Absalomu alikuwa amepanda nyumbu wake, na yule nyumbu akapita chini ya matawi manene ya mwaloni mkubwa, hata kichwa chake kikakwama katika mwaloni huo, akanyakuliwa juu kati ya mbingu na nchi; na yule nyumbu aliyekuwa chini yake akaenda mbele.
10 Basi mtu mmoja akaona hayo, akaenda akamwambia Yoabu, akasema, Tazama, mimi nalimwona Absalomu ametundikwa katika mwaloni.
11 Naye Yoabu akamwambia mtu yule aliyempasha habari, Je! Wewe umeona haya; Mbona, basi, hukumpiga hata nchi papo hapo? Nami ningalikupa fedha kumi na mshipi.
12 Yule mtu akamwambia Yoabu, Kama ningalipata fedha elfu mkononi mwangu, hata hivyo singalinyosha mkono wangu juu ya mwana wa mfalme; kwa maana mfalme masikioni mwetu alikuagiza wewe, na Abishai na Itai, akisema, Angalieni sana mtu awaye yote asimguse yule kijana, Absalomu.
13 Na tena, kama ningaliitendea roho yake kwa hila; (wala hapana neno lo lote liwezalo kufichwa mbele ya mfalme); ndipo wewe mwenyewe ungalijitenga.
14 Ndipo Yoabu akasema, Siwezi kungoja na kusema nawe hivi. Akachukua vyemba vitatu mkononi mwake, akamchoma Absalomu moyoni, alipokuwa akali hai katikati ya ule mwaloni.
15 Kisha vijana kumi, waliomchukulia Yoabu silaha zake wakamzunguka, wakampiga Absalomu, na kumwua.
16 Kisha Yoabu akapiga tarumbeta, wakarudi watu toka kuwafuatia Israeli; kwani Yoabu akawazuia watu.
17 Nao wakamtwaa Absalomu wakamtupa katika shimo kubwa mle msituni, wakaweka juu yake chungu kubwa sana la mawe; kisha Israeli wote wakakimbia kila mtu hemani mwake.
18 Huyo Absalomu alipokuwa yu hai alikuwa ameitwaa na kujiinulia ile nguzo iliyoko bondeni mwa mfalme; kwa maana alisema, Mimi sina mtoto wa kulikumbusha jina langu; akaiita hiyo nguzo kwa jina lake mwenyewe nayo inaitwa ziara la Absalomu hata hivi leo.
19 Basi Ahimaasi, mwana wa Sadoki, akasema, Niende mbio sasa, nikampelekee mfalme habari, jinsi Bwana alivyomlipiza kisasi juu ya adui zake.
20 Yoabu akamwambia, Wewe hutakuwa mchukua habari leo, siku nyingine utachukua habari; lakini leo hutachukua habari, kwa sababu mwana wa mfalme amekufa.
21 Ndipo Yoabu akamwambia Mkushi mmoja, Nenda ukamwambie mfalme hayo uliyoyaona. Na huyo Mkushi akajiinamisha mbele ya Yoabu, akaenda zake mbio.
22 Ndipo Ahimaasi, mwana wa Sadoki, akamwambia Yoabu mara ya pili, Haidhuru, tafadhali nipe ruhusa, nipige mbio na mimi nyuma ya huyo Mkushi. Naye Yoabu akasema, Mbona wewe unataka kupiga mbio, mwanangu, kwa maana hutapata kitu kwa habari hizo unazopeleka?
23 Akasema, Haidhuru, nitapiga mbio. Akamwambia, Haya, piga mbio. Ndipo Ahimaasi akapiga mbio, akishika njia ya uwandani, akampita yule Mkushi.
24 Basi Daudi alikuwa ameketi kati ya malango mawili; mlinzi akapanda juu hata dari ya lile lango hata ukutani, akainua macho yake, akaangalia, na tazama, mtu anakuja mbio peke yake.
25 Mlinzi akalia, akamwambia mfalme. Naye mfalme akasema, Kama yu peke yake, ana habari kinywani mwake. Akaja mbio, akakaribia.
26 Kisha huyo mlinzi akaona mtu mwingine anapiga mbio; mlinzi akamwita bawabu, akasema, Angalia, mtu mwingine anakuja mbio peke yake. Mfalme akasema, Huyu naye analeta habari.
27 Na huyo mlinzi akasema, Nionavyo mimi, kupiga mbio kwake yule wa kwanza ni kama kupiga mbio kwake Ahimaasi, mwana wa Sadoki. Naye mfalme akasema, Yeye ni mtu mwema, anakuja na habari njema.
28 Ahimaasi akainua sauti yake, akamwambia mfalme, Amani. Akainama mbele ya mfalme kifudifudi, akasema, Ahimidiwe Bwana, Mungu wako, aliyewatoa watu hao walioiinua mikono yao juu ya bwana wangu, mfalme.
29 Mfalme akauliza, Je! Yule kijana, Absalomu, yu salama? Ahimaasi akajibu, Yoabu aliponituma mimi mtumishi wa mfalme, mimi mtumishi wako, naliona kishindo kikubwa, lakini sikujua sababu yake.
30 Naye mfalme akasema, Geuka, usimame hapa. Akageuka, akasimama.
31 Na tazama, yule Mkushi akafika; Mkushi akasema, Nina habari kwa bwana wangu mfalme; kwa maana Bwana amekulipizia kisasi leo juu ya hao wote walioinuka kupigana nawe.
32 Naye mfalme akamwambia yule Mkushi, Yule kijana, Absalomu, je! Yu salama? Yule Mkushi akajibu, Adui za bwana wangu mfalme, na wote wainukao ili kukudhuru, na wawe kama alivyo yule kijana.
33 Naye mfalme akataabika sana, akapanda juu, akaingia kile chumba kilichokuwa juu ya lango, akalia; na katika kwenda kwake alisema hivi, Mwanangu Absalomu! Ee mwanangu! Mwanangu Absalomu! Laiti ningalikufa badala yako, Absalomu, mwanangu, mwanangu!

2 Samweli 19


1 Kisha Yoabu akaambiwa, Angalia, mfalme anamlilia Absalomu na kumwombolezea.
2 Na kushinda kwao vitani siku ile kukageuzwa kuwa maombolezo kwa watu wote; maana watu walisikia siku ile ya kwamba, Mfalme anahuzunika kwa ajili ya mwanawe.
3 Watu wakajificha siku ile, wakaingia mjini kama vile watu waonao fedheha wajifichavyo, hapo wakimbiapo vitani.
4 Mfalme akajifunika uso; na mfalme akalia kwa sauti kuu, Mwanangu Absalomu, Absalomu, mwanangu, mwanangu!
5 Basi Yoabu akaingia nyumbani kwa mfalme, akasema, Wewe leo umefedhehesha nyuso za watumishi wako wote, waliokuokoa leo roho yako, na roho za wanao, na za binti zako, na roho za wakezo, na roho za masuria wako;
6 kwa kuwa unawapenda wakuchukiao, na unawachukia wakupendao. Maana umetangaza leo ya kuwa wakuu na watumishi wako si kitu kwako; maana leo nimetambua hivi; kama Absalomu angaliishi, na sisi sote tungalikufa leo, ingalikuwa vyema machoni pako.
7 Basi sasa, ondoka, utoke nje, ukaseme na watumishi wako maneno ya kuwatuliza roho zao; maana mimi nakuapia kwa Bwana, usipotoka, hatabaki hata mtu mmoja pamoja nawe usiku huu; na mambo haya yatakuwa mabaya kwako kuliko mabaya yote yaliyokupata tokea ujana wako hata sasa.
8 Ndipo mfalme akaondoka, akaketi langoni. Nao wote wakaambiwa ya kwamba, Angalieni, mfalme ameketi langoni; watu wote wakaenda huko mbele ya mfalme. Basi, Israeli wote walikuwa wamekimbia kila mtu hemani kwake.
9 Wakashindana watu wote katika kabila zote za Israeli, wakisema, Mfalme alitutoa mikononi mwa adui zetu, akatuokoa mikononi mwa Wafilisti; naye sasa amekimbia kutoka nchi hii mbele ya Absalomu.
10 Na huyo Absalomu, tuliyemtia mafuta ili awe juu yetu, amekufa vitani. Basi sasa mbona ninyi hamsemi neno lo lote juu ya kumrudisha tena mfalme?
11 Naye mfalme Daudi akatuma kwa Sadoki na Abiathari, makuhani, kusema, Neneni na wazee wa Yuda, mkisema, Kwa nini ninyi mmekuwa wa mwisho wa kumrudisha tena mfalme nyumbani kwake? Kwa maana maneno ya Israeli wote yamemjia mfalme, ili kumleta nyumbani kwake.
12 Ninyi ni ndugu zangu, ninyi ni mfupa wangu na nyama yangu; mbona basi ninyi mmekuwa wa mwisho wa kumrudisha tena mfalme.
13 Kisha mkamwambie Amasa, Je! Si wewe uliye mfupa wangu, na nyama yangu? Mungu anifanyie hivyo, na kuzidi, usipokuwa wewe jemadari wa jeshi mbele yangu daima mahali pa Yoabu.
14 Akawainamisha mioyo watu wote wa Yuda, kama mtu mmoja; basi wakatuma kwa mfalme, Rudi wewe na watumishi wako wote.
15 Hivyo mfalme akarudi, akafika Yordani. Kisha Yuda wakaja Gilgali kwenda kumlaki mfalme, na kumvusha mfalme Yordani.
16 Akafanya haraka Shimei, mwana wa Gera, Mbenyamini, wa Bahurimu akashuka pamoja na watu wa Yuda ili kumlaki mfalme Daudi.
17 Na Watu elfu wa Benyamini walikuwa pamoja naye, na huyo Siba mtumwa, nyumba ya Sauli, na hao wanawe kumi na watano, na watumwa wake ishirini pamoja naye; wakavuka Yordani mbele ya mfalme.
18 Tena ikavuka mashua ili kuwavusha jamaa ya mfalme, na kufanya aliyoyaona kuwa mema. Ndipo Shimei, mwana wa Gera, akamwangukia mfalme alipokuwa amevuka Yordani.
19 Akamwambia mfalme, Bwana wangu asinihesabie uovu, wala usiyakumbuke yale niliyoyatenda mimi mtumwa wako kwa upotoe siku ile alipotoka Yerusalemu bwana wangu mfalme, hata mfalme ayatie moyoni mwake.
20 Kwa kuwa mimi mtumwa wako najua ya kwamba nimekosa; kwa hiyo, tazama, nimekuja leo, wa kwanza wa nyumba yote ya Yusufu, kushuka ili nimlaki bwana wangu mfalme.
21 Lakini Abishai, mwana wa Seruya, akajibu na kusema, Je! Shimei hatauawa kwa sababu hii, kwa kuwa amemlaani masihi wa BWANA?
22 Lakini Daudi akasema, Mimi nina nini nanyi, enyi wana wa Seruya, hata mmekuwa adui zangu leo? Je! Atauawa mtu ye yote leo katika Israeli? Kwa maana sijui mimi leo ya kwamba ndimi mfalme juu ya Israeli?
23 Kisha mfalme akamwambia Shimei, Hutakufa. Mfalme akamwapia.
24 Kisha Mefiboshethi, mwana wa Sauli, akashuka ili amlaki mfalme; alikuwa hakukata kucha za miguu yake wala kukata ndevu zake, wala kufua nguo zake, tangu siku alipoondoka mfalme, hata siku hiyo aliporudi kwake kwa amani.
25 Basi ikawa, alipofika Yerusalemu kumlaki mfalme, mfalme akamwambia, Mbona hukwenda pamoja nami, Mefiboshethi?
26 Naye akajibu, Bwana wangu, Ee mfalme, mtumwa wangu alinidanganya; kwa kuwa mimi mtumwa wako nilisema, Nitajitandikia punda, nipate kumpanda, na kwenda pamoja na mfalme; kwa sababu mimi mtumwa wako ni kiwete.
27 Naye amenisingizia mimi mtumwa wako kwa bwana wangu mfalme; lakini bwana wangu mfalme ni kama malaika wa Mungu; utende basi yaliyo mema machoni pako.
28 Kwa kuwa jamaa yote ya baba yangu walikuwa kama watu wa kufa tu mbele ya bwana wangu mfalme; ila uliniweka mimi mtumwa wako kati ya hao walao mezani pako. Basi ni haki gani sasa niliyo nayo, hata nimlilie mfalme zaidi?
29 Basi mfalme akamwambia, Kwa nini unazidi kuyanena mambo yako? Mimi naamua, Wewe na Siba mwigawanye hiyo nchi.
30 Naye Mefiboshethi akamwambia mfalme, Naam, hata yote na atwae yeye, kwa kuwa bwana wangu mfalme amekuja kwa amani nyumbani kwake.
31 Tena Barzilai, Mgileadi, akashuka kutoka Rogelimu; akavuka Yordani pamoja na mfalme, amvushe Yordani.
32 Naye huyo Barzilai alikuwa mzee sana, amepata umri wa miaka themanini; naye amemlisha mfalme hapo alipokuwapo Mahanaimu; kwa kuwa alikuwa mtu mwenye cheo kikubwa.
33 Naye mfalme akamwambia Barzilai, Uvuke pamoja nami; nami nitakulisha kwangu huko Yerusalemu.
34 Lakini Barzilai akamjibu mfalme, Siku ni ngapi za miaka ya maisha yangu, hata mimi nipande pamoja na mfalme kwenda Yerusalemu?
35 Nimepata leo miaka themanini; nami je! Naweza kupambanua mema na mabaya? Mimi mtumwa wako, je! Naweza kuonja nilacho au ninywacho? Naweza kusikia tena sauti ya waimbaji waume na wake? Kwa nini basi mtumwa wako amlemee bado bwana wangu mfalme?
36 Mtumwa wako ataka kuvuka Yordani tu pamoja na mfalme; tena mbona mfalme anilipie thawabu ya namna hii?
37 Niache nirudi basi, mimi mtumwa wako, ili nife katika mji wangu mwenyewe, karibu na kaburi la baba yangu na la mama yangu. Lakini tazama, mtumwa wako Kimhamu; na avuke yeye pamoja na bwana wangu mfalme; nawe ukamtendee yeye yaliyo mema machoni pako.
38 Mfalme akajibu, Haya, Kimhamu na avuke pamoja nami, nami nitamtendea yaliyo mema machoni pako wewe; na kila utakalotaka kwangu, mimi nitalifanya kwa ajili yako.
39 Basi watu wote wakavuka Yordani, naye mfalme akavuka; kisha mfalme akambusu Barzilai, akambariki; naye akarejea mahali pake.
40 Hivyo mfalme akavuka, akafika Gilgali; Kimhamu akavuka pamoja naye; na watu wote wa Yuda wakamvusha mfalme, na nusu ya watu wa Israeli.
41 Tena, angalia, watu wote wa Israeli wakamjia mfalme wakamwambia mfalme, Kwa nini ndugu zetu, watu wa Yuda wamekuiba, na kumvusha Yordani mfalme, na jamaa yake, na watu wote wa Daudi pamoja naye?
42 Ndipo watu wote wa Yuda wakawajibu hao watu wa Israeli, Ni kwa sababu mfalme ndiye wa jamaa yetu; mbona basi ninyi mmekasirika kwa ajili ya jambo hili? Je! Sisi tumekula kitu cha mfalme? Ama ametupa sisi zawadi yo yote?
43 Hao watu wa Israeli wakawajibu watu wa Yuda, wakasema, Sisi tunazo sehemu kumi katika mfalme, tena tunayo haki yetu katika Daudi zaidi kuliko ninyi; mbona basi ninyi mmetudharau sisi, lisitakwe kwanza shauri letu katika kumrudisha tena mfalme wetu? Na maneno ya watu wa Yuda yakawa makali kuliko maneno ya watu wa Israeli.

2 Samweli 20


1 Basi ilitukia ya kwamba kulikuwapo mtu asiyefaa, jina lake akiitwa Sheba, mwana wa Bikri, Mbenyamini; naye akapiga tarumbeta, akasema, Sisi hatuna sehemu katika Daudi, wala hatuna urithi katika mwana wa Yese; nendeni kila mtu hemani kwake, enyi Israeli.
2 Basi wakapanda watu wote wa Israeli kutoka kumfuata Daudi, wakamfuata Sheba, mwana wa Bikri; lakini watu wa Yuda wakaambatana na mfalme wao, toka Yordani hata kufika Yerusalemu.
3 Basi Daudi akaja Yerusalemu nyumbani kwake; kisha mfalme akawatwaa wale wanawake kumi, masuria, aliowaacha kuitunza nyumba, akawatia nyumbani mwa kulindwa, akawalisha, ila asiingie kwao. Basi wakafungwa hata siku ya kufa kwao, huku wakiishi hali ya ujane.
4 Ndipo mfalme akamwambia Amasa, Uwakusanye pamoja kwangu kwa siku tatu watu wa Yuda, na uwepo wewe hapa.
5 Amasa akaenda kuwakusanya Yuda; lakini akakawia zaidi ya huo muda aliowekewa.
6 Basi Daudi akamwambia Abishai, Sasa Sheba, mwana wa Bikri, atatudhuru, kuliko Absalomu; twaa wewe watumishi wa bwana wako, ukamfuatie, asiingie katika miji yenye boma, na kujiponya machoni petu.
7 Ndipo wakatoka nyuma yake watu wa Yoabu, na Wakerethi na Wapelethi, na mashujaa wote; wakatoka Yerusalemu, ili kumfuatia Sheba, mwana wa Bikri.
8 Basi walipokuwako kwenye lile jiwe kubwa lililoko Gibeoni, Amasa akaja kuwalaki. Naye Yoabu alikuwa amefungwa mavazi yake ya vita aliyoyavaa, na juu yake alikuwa na mshipi, na upanga uliotiwa viunoni mwake ndani ya ala yake; naye alipokuwa akiendelea, ukaanguka.
9 Naye Yoabu akamwambia Amasa, Amani kwako, ndugu yangu. Kisha Yoabu akamshika Amasa ndevu kwa mkono wake wa kuume ili ambusu.
10 Wala Amasa hakuangalia huo upanga uliomo mkononi mwa Yoabu; basi akampiga nao wa tumbo, akamwaga matumbo yake chini, asimpige mara ya pili; naye akafa. Kisha Yoabu na Abishai, nduguye, wakamfuata Sheba, mwana wa Bikri.
11 Akasimama karibu naye mmojawapo wa vijana wa Yoabu, huyo akasema, Ampendaye Yoabu, na aliye wa Daudi, na amfuate Yoabu.
12 Lakini Amasa alikuwa anagaagaa katika damu yake katikati ya njia kuu. Basi yule mtu alipowaona watu wote wamesimama, akamwondoa Amasa toka njia kuu akamtia kondeni, akamfunika nguo, hapo alipoona ya kuwa kila mtu aliyefika kwake amesimama.
13 Na alipoondolewa katika njia kuu, watu wote wakapita, wakamwandama Yoabu ili kumfuatia Sheba, mwana wa Bikri.
14 Naye akapita kati ya kabila zote za Israeli mpaka Abeli, na kwa Bethmaaka na Wabikri wote; nao wakakusanyika, wakaenda pia kumwandama.
15 Na hao wakaja wakamhusuru katika Abeli wa Bethmaaka, wakafanya chuguu mbele ya mji, nayo ikasimama kuielekea ngome; na watu wote waliokuwa pamoja na Yoabu wakavunja-vunja ukuta, wapate kuubomoa.
16 Ndipo akalia mwanamke mmoja mwenye akili toka mjini, Sikieni, sikieni; mwambieni na Yoabu, aje hapa karibu, niseme naye.
17 Basi akamkaribia; na yule mwanamke akasema, Ndiwe Yoabu? Akajibu, Ndimi. Ndipo akamwambia Sikia maneno ya mjakazi wako. Akajibu, Mimi nasikia.
18 Kisha akanena, akisema, Watu hunena zamani za kale, wakisema, Wasikose kuuliza huko Abeli; ndivyo walivyomaliza shauri.
19 Mimi ni wa hao wenye amani, walio waaminifu katika Israeli; wewe unatafuta kuuharibu mji, na mama wa Israeli; mbona wataka kuumeza urithi wa Bwana?
20 Yoabu akajibu, akasema, Isiwe, isiwe kwangu, niumeze wala kuuharibu.
21 Neno hili silo hivyo; lakini mtu mmoja wa milima ya Efraimu, Sheba, mwana wa Bikri, jina lake, ameinua mkono wake juu ya mfalme, naam, Daudi, basi mtoeni yeye tu, nami nitaondoka katika mji huu. Basi yule mwanamke akamwambia Yoabu, Tazama, kichwa chake utatupiwa juu ya ukuta.
22 Ndipo yule mwanamke akawaendea watu wote katika akili zake. Nao wakamkata kichwa Sheba, mwana wa Bikri, wakamtupia Yoabu huko nje. Ndipo akapiga tarumbeta, nao wakatawanyika kutoka mjini kila mtu hemani kwake. Naye Yoabu akarudi mpaka Yerusalemu kwa mfalme.
23 Basi Yoabu alikuwa juu ya jeshi lote la Israeli; na Benaya, mwana wa Yehoyada, alikuwa juu ya Wakerethi, na juu ya Wapelethi;
24 na Adoramu alikuwa juu ya shokoa; na Yehoshafati, mwana wa Ahiludi, alikuwa mkumbushi;
25 na Shausha mwandishi; na Sadoki na Abiathari walikuwa makuhani.
26 Tena na Ira, Myairi, alikuwa kuhani kwa Daudi.

2 Samweli 21


1 Kulikuwa na njaa siku za Daudi muda wa miaka mitatu, mwaka kwa mwaka; naye Daudi akautafuta uso wa Bwana. Bwana akasema, Ni kwa ajili ya Sauli, na kwa nyumba yake yenye damu, kwa kuwa aliwaua hao Wagibeoni.
2 Ndipo mfalme akawaita Wagibeoni akawaambia; (basi Wagibeoni si wa wana wa Israeli, ila ni wa masalio ya Waamori; na wana wa Israeli walikuwa wamewaapia; lakini Sauli akatafuta kuwaua katika juhudi yake kwa ajili ya wana wa Israeli na Yuda;)
3 basi Daudi akawaambia hao Wagibeoni, Niwatendee nini? Na kwa tendo gani nifanye upatanisho, mpate kuubariki urithi wa Bwana?
4 Na hao Wagibeoni wakamwambia, Si jambo la fedha wala dhahabu lililo kati ya sisi na Sauli, au nyumba yake; wala si juu yetu kumwua mtu ye yote katika Israeli. Akasema Mtakayoyanena, ndiyo nitakayowatendea ninyi.
5 Wakamwambia mfalme, Yule mtu aliyetupoteza, na kutufanyia shauri la kutuharibu, tusikae katika mipaka yo yote ya Israeli,
6 basi, na tutolewe watu saba katika wanawe, nasi tutawatundika mbele za Bwana katika Gibeoni, katika mlima wa Bwana. Mfalme akasema, Nitawatoa.
7 Lakini mfalme akamwachilia Mefiboshethi, mwana wa Yonathani, mwana wa Sauli, kwa ajili ya kiapo cha Bwana kilichokuwa kati yao, yaani, kati ya Daudi na Yonathani, mwana wa Sauli.
8 Ila mfalme akawatwaa hao wana wawili wa Rispa, binti Aya, aliomzalia Sauli, Armoni na Mefiboshethi; na wana watano wa Merabu binti Sauli, aliomzalia Adrieli, mwana wa Barzilai, Mmeholathi;
9 akawatia mikononi mwa Wagibeoni, nao wakawatundika mlimani mbele za Bwana, nao wakaangamia wote saba pamoja; wakauawa siku za mavuno, za kwanza, mwanzo wa mavuno ya shayiri.
10 Naye Rispa, binti Aya, akatwaa nguo ya magunia akajitandikia mwambani, tangu mwanzo wa mavuno hata waliponyeshewa mvua toka mbinguni; wala hakuacha ndege wa angani kukaa juu yao mchana, wala wanyama wa mwitu usiku.
11 Kisha akaambiwa Daudi hayo aliyoyafanya huyo Rispa binti Aya, suria wa Sauli.
12 Akaenda Daudi, akaitwaa mifupa ya Sauli na mifupa ya Yonathani mwanawe mikononi mwa watu wa Yabesh-gileadi; waliyoiiba katika njia ya Bethshani, hapo Wafilisti walipowatungika, katika siku hiyo waliyomwua Sauli huko Gilboa;
13 naye akaileta toka huko hiyo mifupa ya Sauli, na mifupa ya Yonathani mwanawe; nao wakaizoa mifupa yao waliotundikwa.
14 Kisha wakaizika mifupa ya Sauli na ya Yonathani mwanawe katika nchi ya Benyamini, huko Zela, kaburini mwa Kishi babaye; wakafanya yote aliyoyaamuru mfalme. Na baadaye Mungu aliiridhia hiyo nchi.
15 Basi kulikuwa na vita tena kati ya Wafilisti na Israeli; Daudi akashuka mpaka Gobu, na watumishi wake pamoja naye, akapigana na Wafilisti; naye Daudi akaishiwa na nguvu.
16 Naye Ishi-benobu, aliyekuwa mmojawapo wa Warefai, ambaye uzito wa mkuki wake ulikuwa shekeli mia tatu za shaba kwa uzani ,naye amejifungia upanga mpya,alijaribu kumwua Daudi.
17 Lakini Abishai, mwana wa Seruya, akamsaidia, akampiga Mfilisti, akamwua. Ndipo watu wa Daudi wakamwapia, wakasema, Wewe hutatoka tena pamoja nasi kwenda vitani, usije ukaizima taa ya Israeli.
18 Ikawa baada ya hayo, kulikuwa na vita tena na Wafilisti huko Gobu; ndipo Sibekai, Mhushathi, alipomwua Safu, aliyekuwa mmojawapo wa Warefai.
19 Kulikuwa na vita tena na Wafilisti huko Gobu; na Elhanani, mwana wa Yairi, Mbethlehemi, alimwua Goliathi, Mgiti, ambaye mti wa mkuki wake ulikuwa kama mti wa mfumaji.
20 Kulikuwa na vita tena huko Gathi; ambako kulikuwa na mtu mrefu sana, mwenye vidole sita katika kila mkono, na vidole sita katika kila mguu, jumla yake ishirini na vinne; yeye naye alizaliwa kwa Mrefai.
21 Naye huyo alipowatukana Israeli, ndipo Yonathani, mwana wa Shama, nduguye Daudi, akamwua.
22 Hao wanne walizaliwa kwake huyo Mrefai wa Gathi; wakaanguka kwa mkono wa Daudi, na kwa mikono ya watumishi wake.

2 Samweli 22


1 Basi Daudi akamwambia Bwana maneno ya wimbo huu, siku ile Bwana alipomwokoa mikononi mwa adui zake zote, na mkononi mwa Sauli;
2 akasema, Bwana ndiye jabali langu, na ngome yangu, na mwokozi wangu, naam, wangu;
3 Mungu wa mwamba wangu, nitamwamini yeye; Ngao yangu, na pembe ya wokovu wangu, mnara wangu, na makimbilio yangu; Mwokozi wangu, waniokoa na jeuri.
4 Nitamwita Bwana astahiliye kusifiwa; Hivyo nitaokoka na adui zangu.
5 Maana mawimbi ya mauti yalinizunguka, Mafuriko ya uovu yakanitia hofu.
6 Kamba za kuzimu zilinizunguka; Mitego ya mauti ikanikabili.
7 Katika shida yangu nalimwita Bwana, Naam, nikamlalamikia Mungu wangu;
8 Ndipo nchi ilipotikisika na kutetemeka, Misingi ya mbinguni ikasuka-suka Na kutikisika, kwa sababu alikuwa na ghadhabu.
9 Kukapanda moshi kutoka puani mwake, Moto ukatoka kinywani mwake ukala; Makaa yakawashwa nao.
10 Aliziinamisha mbingu akashuka; Kukawa na giza kuu chini ya miguu yake.
11 Akapanda juu ya kerubi akaruka; Naam, alionekana juu ya mabawa ya upepo.
12 Akafanya giza hema zake za kumzunguka, Makusanyiko ya maji, mawingu makuu ya mbinguni.
13 Toka mwangaza uliokuwa mbele zake Makaa ya moto yakawashwa.
14 Bwana alipiga radi toka mbinguni, Naye Aliye juu akaitoa sauti yake.
15 Akapiga mishale, akawatawanya; Umeme, naye akawatapanya.
16 Ndipo ilipoonekana mikondo ya bahari, Misingi ya ulimwengu ikafichuliwa, Kwa kukemea kwake Bwana, Kwa mvumo wa pumzi ya puani mwake.
17 Alipeleka kutoka juu, akanishika; Akanitoa katika maji mengi;
18 Akaniokoa na adui yangu mwenye nguvu, Na wale walionichukia; Maana walikuwa na nguvu kuliko mimi.
19 Walinikabili siku ya msiba wangu; Lakini Bwana alikuwa tegemeo langu.
20 Akanitoa akanipeleka panapo nafasi; Aliniponya kwa kuwa alipendezwa nami.
21 Bwana alinitendea sawasawa na haki yangu; Sawasawa na usafi wa mikono yangu akanilipa.
22 Maana nimezishika njia za Bwana, Wala sikumwasi Mungu wangu.
23 Maana hukumu zake zote zilikuwa mbele yangu; Na kwa habari za amri zake, sikuziacha.
24 Nami nalikuwa mkamilifu kwake, Nikajilinda na uovu wangu.
25 Basi Bwana amenilipa sawasawa na haki yangu; Sawasawa na usafi wa mikono yangu mbele zake.
26 Kwa mtu mwenye fadhili utakuwa mwenye fadhili Kwa mkamilifu utajionyesha kuwa mkamilifu;
27 Kwake ajitakasaye utajionyesha kuwa mtakatifu; Na kwa mpotovu utajionyesha kuwa mkaidi.
28 Na watu wanaoonewa wewe utawaokoa; Ila macho yako ni juu ya wenye kiburi, uwadhili.
29 Kwa kuwa wewe u taa yangu, Ee Bwana; Na Bwana ataniangazia giza langu.
30 Maana kwa msaada wako nafuatia jeshi; Kwa msaada wa Mungu wangu naruka ukuta.
31 Mungu njia yake ni kamilifu; Ahadi ya Bwana imehakikishwa; Yeye ndiye ngao yao Wote wanaomkimbilia.
32 Maana ni nani aliye Mungu, ila Bwana? Ni nani aliye mwamba, ila Mungu wetu?
33 Mungu ndiye ngome yangu yenye nguvu; Naye huwaongoza wakamilifu katika njia yake.
34 Huifanya miguu yangu kuwa kama ya kulungu; Na kunisimamisha mahali pangu pa juu.
35 Ananifundisha mikono yangu vita; Hata mikono yangu yaupinda upinde wa shaba.
36 Nawe umenipa ngao ya wokovu wako; Na unyenyekevu wako umenikuza.
37 Umezifanyizia nafasi hatua zangu, Wala miguu yangu haikuteleza.
38 Nimewafuatia adui zangu, na kuwaangamiza; Wala sikurudi nyuma hata walipokomeshwa.
39 Nami nimewakomesha na kuwapiga-piga wasiweze kusimama; Naam, wameanguka chini ya miguu yangu.
40 Maana umenifunga mshipi wa nguvu kwa vita; Umenitiishia chini yangu walioniondokea.
41 Naam, adui zangu umewafanya wanipe visogo, Ili niwakatilie mbali wanaonichukia.
42 Walitazama, lakini hakuna wa kuokoa; Walimwita Bwana, lakini hakuwajibu.
43 Ndipo nikawaponda kama mavumbi ya nchi, Nikawakanyaga kama matope ya njiani, nikawatawanya.
44 Nawe umeniokoa na mashindano ya watu wangu; Umenihifadhi niwe kichwa cha mataifa; Watu nisiowajua watanitumikia.
45 Wageni watanijia wakinyenyekea; Kwa kusikia tu habari zangu, Mara watanitii.
46 Wageni nao watatepetea, Watatoka katika ngome zao wakitetemeka.
47 Bwana ndiye aliye hai; Na ahimidiwe mwamba wangu; Na atukuzwe Mungu wa mwamba wa wokovu wangu;
48 Naam, Mungu anipatiaye kisasi, Na kuwatweza watu chini yangu,
49 Na kunileta nje nitoke kwa adui zangu; Naam, waniinua juu yao walioniinukia; Waniponya na mtu wa jeuri.
50 Basi, Bwana, nitakushukuru kati ya mataifa, Nami nitaliimbia jina lako.
51 Ampa mfalme wake wokovu mkuu; Amfanyia fadhili masihi wake Daudi na mzao wake ,hata milele.

2 Samweli 23


1 Basi haya ndiyo maneno ya mwisho ya Daudi. Daudi, mwana wa Yese, anena, anena huyo mtu aliyeinuliwa juu, Yeye, masihi wake Mungu wa Yakobo,Mtungaji wa nyimbo za Israeli mwenye kupendeza;
2 Roho ya Bwana ilinena ndani yangu, Na neno lake likawa ulimini mwangu.
3 Mungu wa Israeli alisema, Mwamba wa Israeli aliniambia, Atawalaye wanadamu kwa haki, Akitawala katika kicho cha Mungu,
4 Atakuwa kama nuru ya asubuhi jua lichapo, Asubuhi isiyo na mawingu.
5 Je! Sivyo ilivyo nyumba yangu mbele za Bwana? Kwa kuwa amefanya nami agano la milele; Ina taratibu katika yote, ni thabiti, Maana ni wokovu wangu wote, na shauku langu lote.
6 Lakini hatawachipuza watu wa ubatili; Watakuwa wote kama miiba ya nyikani ya kutupwa, Ambayo haivuniki kwa mkono,
7 Mtu atakayeigusa hiyo, Na awe na chuma na mpini wa mkuki, Nao watateketezwa papo hapo kwa moto.
8 Haya ndiyo majina ya mashujaa aliokuwa nao Daudi; Yashobeamu Mhakmoni,mkuu wa maakida ;huyo aliliinua shoka lake juu ya watu mia nane waliouawa pamoja.
9 Na baada yake kulikuwa na Eleazari, mwana wa Dodai, Mwahohi, mmojawapo wa wale mashujaa watatu waliokuwa pamoja na Daudi; walipowatukana Wafilisti waliokuwa wamekusanyika huko ili kupigana, na watu wa Israeli walikuwa wamekwenda zao;
10 huyo aliinuka, akawapiga Wafilisti hata mkono wake ukachoka, na mkono wake ukaambatana na upanga; naye Bwana akafanya wokovu mkuu siku ile; nao watu wakarudi nyuma yake ili kuteka nyara tu.
11 Na baada yake kulikuwa na Shama, mwana wa Agee, Mharari; nao Wafilisti walikuwa wamekusanyika huko Lehi, palipokuwapo konde lililojaa midengu; nao watu wakawakimbia Wafilisti;
12 ila huyo alisimama katikati ya konde lile, akalipigania, akawaua Wafilisti; naye Bwana akafanya wokovu mkuu.
13 Tena, watatu miongoni mwa wale thelathini waliokuwa wakuu wakashuka, wakamwendea Daudi wakati wa mavuno mpaka pango la Adulamu, na kikosi cha Wafilisti walikuwa wamefanya kambi katika bonde la Warefai.
14 Naye Daudi wakati ule alikuwako ngomeni, na jeshi la Wafilisti wakati ule walikuwako Bethlehemu.
15 Daudi akatamani, akasema, Laiti mtu angeninywesha maji ya kisima cha Bethlehemu, kilicho karibu na lango!
16 Basi hao mashujaa watatu wakapenya jeshi la Wafilisti, wakateka maji kutoka kile kisima cha Bethlehemu, kilicho karibu na lango, wakayachukua, wakamletea Daudi; walakini yeye hakukubali kuyanywa, akayamimina mbele za Bwana.
17 Akasema, Hasha, Bwana, nisifanye hivi; je! Si damu hii ya watu hao waliohatirisha nafsi zao? Kwa hiyo hakukubali kuyanywa. Hayo ndiyo waliyoyafanya wale mashujaa watatu.
18 Tena, Abishai, nduguye Yoabu, mwana wa Seruya, alikuwa mkuu wa wale watatu. Huyo aliuinua mkuki wake juu ya watu mia tatu, akawaua, akawa na jina kati ya wale watatu.
19 Je! Huyo hakuwa na heshima maalumu miongoni mwa wale watatu? Kwa hiyo akawekwa kuwa akida wao; ila hakudiriki kuwamo katika wale watatu.
20 Tena Benaya, mwana wa Yehoyada, mtu hodari wa Kabseeli aliyekuwa amefanya mambo makuu; aliwaua simba wakali wawili wa Moabu, pia akashuka akamwua simba katikati ya shimo wakati wa theruji.
21 huyo naye akamwua Mmisri, mtu mrefu; naye huyo Mmisri alikuwa na mkuki mkononi; lakini yeye alimshukia na gongo, akamnyakulia Mmisri mkuki mkononi mwake, akamwua kwa mkuki wake mwenyewe.
22 Hayo ndiyo aliyoyafanya Benaya, mwana wa Yehoyada, akawa na jina kati ya wale mashujaa watatu.
23 Alikuwa mwenye heshima kuliko wale thelathini, ila hakudiriki kuwamo katika wale watatu. Naye Daudi akamweka juu ya walinzi wake.
24 Asaheli, nduguye Yoabu, alikuwa mmojawapo wa wale thelathini; na Elhanani, mwana wa Dodo, wa Bethlehemu;
25 na Shama, Mharodi, na Elika, Mharodi;
26 na Helesi, Mpeloni, na Ira, mwana wa Ikeshi, Mtekoi;
27 na Abiezeri, Mwanathothi, na Sibekai, Mhushathi;
28 na Salmoni, Mwahohi, na Maharai, Mnetofathi;
29 na Heledi, mwana wa Baana, Mnetofathi, na Itai, mwana wa Ribai, wa Gibea wa wana wa Benyamini;
30 na Benaya, Mpirathoni, na Hurai, wa vijito vya Gaashi;
31 na Abieli, Mwarbathi, na Azmawethi, Mbarhumi;
32 na Eliaba, Mshaalboni, na wana wa Yasheni; na Yonathani,
33 mwana wa Shama, Mharari, na Ahiamu, mwana wa Shalali, Mharari;
34 na Elifeleti, mwana wa Ahasbai, na Heferi, Mmaakathi, na Eliamu, mwana wa Ahithofeli, Mgiloni;
35 na Hezro, Mkarmeli, na Paarai, Mwarbi;
36 na Igali, mwana wa Nathani, wa Soba, na Bani, Mgadi;
37 na Seleki, Mwamoni, na Naharai, Mbeerothi, ambao ni wachukua silaha wa Yoabu, mwana wa Seruya;
38 na Ira, Mwithri, na Garebu, Mwithri;
39 na Uria, Mhiti; jumla yao ilikuwa watu thelathini na saba.

2 Samweli 24


1 Tena hasira ya Bwana ikawaka juu ya Israeli, akamtia Daudi nia juu yao, akisema, Nenda, ukawahesabu Israeli na Yuda.
2 Basi mfalme akamwambia Yoabu, jemadari wa jeshi la askari, waliokuwa pamoja naye, Zunguka sasa katikati ya kabila zote za Israeli, tangu Dani mpaka Beer-sheba, mkawahesabu watu, nipate kujua jumla ya hao watu.
3 Naye Yoabu akamwambia mfalme, Bwana, Mungu wako, na awaongeze watu, hesabu yao ikiwa yo yote, mara mia, tena macho ya bwana wangu mfalme na yawaone; ila kwa nini neno hili limempendeza bwana wangu mfalme?
4 Lakini neno la mfalme likawa na nguvu juu ya Yoabu, na juu ya majemadari wa jeshi. Basi Yoabu akatoka na majemadari wa jeshi machoni pa mfalme, kwenda kuwahesabu watu wa Israeli.
5 Wakavuka Yordani, wakapiga kambi huko Aroeri, upande wa kuume wa mji ulioko kati ya bonde la Gadi, na mpaka Yazeri;
6 kisha wakaja Gileadi, na nchi ya Wahiti huko Kadeshi; kisha wakaja Dani, na kutoka Dani wakazunguka mpaka Sidoni,
7 wakaja ngomeni kwa Tiro, na kwa miji yote ya Wahivi, na ya Wakanaani; tena wakatoka kusini kwa Yuda huko Beer-sheba.
8 Nao walipokwisha kuzunguka nchi yote, wakaja Yerusalemu mwisho wa miezi kenda na siku ishirini.
9 Naye Yoabu akamtolea mfalme jumla ya hesabu ya watu; nao walikuwa wa Israeli mashujaa wenye kufuta panga mia nane elfu; nao wa Yuda walikuwa watu mia tano elfu.
10 Ndipo moyo wake Daudi ukamchoma baada ya kuwahesabu hao watu. Naye Daudi akamwambia Bwana, Nimekosa sana kwa haya niliyoyafanya; lakini sasa, Ee Bwana, nakusihi uuondolee mbali uovu wa mtumishi wako; kwani nimefanya upumbavu kabisa.
11 Na Daudi alipoondoka asubuhi, neno la Bwana likamjia nabii Gadi, mwonaji wake Daudi, kusema,
12 Nenda, ukanene na Daudi, Bwana asema hivi, Nakuwekea mambo matatu; katika haya uchague moja, nikutendee hilo.
13 Basi Gadi akamwendea Daudi, akamweleza, akamwambia, Basi, miaka saba ya njaa ikujie katika nchi yako? Au miezi mitatu ukimbie mbele ya adui zako, huku wakikufuatia? Au siku tatu iwe tauni katika nchi yako? Fanya shauri sasa, ufikiri, ni jawabu gani nimrudishie yeye aliyenituma.
14 Naye Daudi akamwambia Gadi, Nimeingia katika mashaka sana; basi sasa na tuanguke katika mkono wa Bwana; kwa kuwa rehema zake ni nyingi; wala nisianguke katika mkono wa wanadamu.
15 Basi Bwana akawaletea Israeli tauni tangu asubuhi hata wakati ulioamriwa; nao wakafa watu toka Dani mpaka Beer-sheba sabini elfu.
16 Lakini huyo malaika aliponyosha mkono wake kuelekea Yerusalemu ili auharibu, Bwana akaghairi katika mabaya, akamwambia huyo malaika mwenye kuwaharibu watu, Yatosha, sasa ulegeze mkono wako. Naye yule malaika wa Bwana alikuwako karibu na kiwanja cha kupuria cha Arauna, Myebusi.
17 Daudi, alipomwoma malaika aliyewapiga watu, akanena na Bwana, akasema, Tazama, ni mimi niliyekosa, ni mimi niliyepotoka; lakini kondoo hawa, wamefanya nini? Mkono wako na uwe juu yangu, na juu ya nyumba ya baba yangu.
18 Siku hiyo Gadi akamwendea Daudi, akamwambia, Haya! Kwea wewe, ukamwinulie Bwana madhabahu penye kiwanja cha Arauna, Myebusi.
19 Basi Daudi akakwea sawasawa na neno la Gadi, kama Bwana alivyoamuru.
20 Huyo Arauna akatazama, akamwona mfalme na watumishi wake wakimjia; Arauna akatoka, akasujudu mbele ya mfalme kifulifuli hata nchi.
21 Arauna akasema, Bwana wangu mfalme amemjia mtumwa wake kwa kusudi gani? Naye Daudi akasema, Makusudi ninunue kwako kiwanja hiki, ili nimjengee Bwana madhabahu, ili kwamba tauni ipate kuzuiliwa katika watu.
22 Arauna akamwambia Daudi, Bwana wangu mfalme na akitwae, akatolee yaliyo mema machoni pake; tazama, ng'ombe hawa kwa sadaka ya kuteketezwa, tena vyombo vya kupuria, na vyombo vya ng'ombe, viko kwa kuni,
23 vitu hivi vyote, Ee mfalme, mimi Arauna nakupa wewe mfalme. Kisha Arauna akamwambia mfalme, Bwana, Mungu wako, na akukubali.
24 Lakini mfalme akamwambia Arauna, La, sivyo; lakini kweli nitavinunua kwako kwa thamani yake; wala sitamtolea Bwana, Mungu wangu, sadaka za kuteketezwa nisizozigharimia. Hivyo Daudi akakinunua hicho kiwanja cha kupuria na wale ng'ombe kwa shekeli hamsini za fedha.
25 Naye Daudi akamjengea Bwana madhabahu huko, akatoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani. Basi Bwana aliiridhia nchi, na tauni ikazuiliwa katika Israeli.