Kutoka

Sura: 1, 2, 3, 4, 5, 6, 7, 8, 9, 10, 11, 12, 13, 14, 15, 16, 17, 18, 19, 20, 21, 22, 23, 24, 25, 26, 27, 28, 29, 30, 31, 32, 33, 34, 35, 36, 37, 38, 39, 40

Kutoka 1


1 Basi majina ya wana wa Israeli walioingia Misri ni haya; kila mtu pamoja na jamaa zake walikuja pamoja na Yakobo.
2 Reubeni, na Simeoni na Lawi, na Yuda;
3 na Isakari, na Zabuloni, na Benyamini;
4 na Dani, na Naftali, na Gadi, na Asheri.
5 Na nafsi zile zote zilizotoka viunoni mwa Yakobo zilikuwa ni nafsi sabini; na huyo Yusufu alikuwa huko ndani ya Misri tangu hapo.
6 Yusufu akafa, na ndugu zake wote, na watu wote wa kizazi kile.
7 Na wana wa Israeli walikuwa na uzazi sana, na kuongezeka mno, na kuzidi kuwa wengi, nao wakaendelea na kuongezeka nguvu; na ile nchi ilikuwa imejawa na wao.
8 Basi akainuka mfalme mpya kutawala Misri, asiyemjua Yusufu.
9 Akawaambia watu wake, Angalieni, watu wa wana wa Israeli ni wengi tena wana nguvu kuliko sisi.
10 Haya! Na tuwatendee kwa akili, wasije wakaongezeka; tena, ikitokea vita, wao nao wasije wakashikamana na adui zetu na kupigana nasi, na kutoka katika nchi hii.
11 Basi wakaweka wasimamizi juu yao wawatese kwa mizigo yao. Nao wakamjengea Farao miji ya kuwekea akiba, Pithomu na Ramesesi.
12 Lakini kwa kadiri ya walivyowatesa ndivyo walivyoongezeka na kuzidi kuenea. Nao walichukiwa kwa sababu ya wana wa Israeli.
13 Wamisri wakawatumikisha wana wa Israeli kwa ukali;
14 wakafanya maisha yao kuwa uchungu kwa kazi ngumu; kazi ya chokaa na ya matofali, na kila namna ya kazi ya mashamba; kwa kazi zao zote walizowatumikisha kwa ukali.
15 Kisha mfalme wa Misri akasema na wazalisha wa Waebrania, mmoja jina lake aliitwa Shifra, na wa pili jina lake aliitwa Pua;
16 akasema, Wakati mwazalishapo wanawake wa Kiebrania na kuwaona wa katika kuzaa, ikiwa ni mtoto mwanamume, basi mwueni, bali ikiwa ni mtoto mwanamke, na aishi.
17 Lakini wale wazalisha walikuwa wakimcha Mungu, wasifanye kama walivyoamriwa na huyo mfalme wa Misri, lakini wakawahifadhi hai wale wanaume.
18 Basi mfalme wa Misri akawaita wale wazalisha na kuwauliza, Kwa nini kufanya jambo hili, na kuwahifadhi watoto waume wawe hai?
19 Wazalisha wakamwambia Farao, Ni kwa sababu hao wanawake wa Kiebrania si kama wanawake wa Kimisri; kwa kuwa ni hodari hao, nao huzaa kabla mzalisha hajapata kuwafikilia.
20 Basi Mungu akawatendea mema wale wazalisha; na hao watu wakaongezeka sana, wakaendelea na kuzidi kuwa na nguvu nyingi.
21 Ilikuwa kwa sababu wale wazalisha walikuwa wakimcha Mungu, akawasimamishia nyumba.
22 Kisha huyo Farao akawaagiza watu wake, akisema, Kila mtoto mwanamume atakayezaliwa mtamtupa mtoni, na kila mtoto mwanamke mtamhifadhi hai.

Kutoka 2


1 Mtu mmoja wa nyumba ya Lawi akaondoka akaoa binti mmoja wa Lawi.
2 Yule mwanamke akachukua mimba akazaa mwana, na alipoona ya kuwa ni mtoto mzuri akamficha miezi mitatu.
3 Na alipokuwa hawezi kumficha tena, akampatia kisafina cha manyasi akakipaka sifa na lami, akamtia mtoto ndani yake, akakiweka katika majani kando ya mto.
4 Umbu lake mtoto akasimama mbali ili ajue yatakayompata.
5 Basi binti Farao akashuka, aoge mtoni, na vijakazi wake wakatembea kando ya mto; naye akakiona kile kisafina katika majani, akamtuma kijakazi wake kwenda kukileta.
6 Akakifungua, akamwona mtoto, na tazama, mtoto yule analia. Basi akamhurumia, akasema, Huyu ni mmojawapo wa watoto wa Waebrania.
7 Basi umbu lake mtoto akamwambia binti Farao, Je! Niende nikamwite mlezi katika wanawake wa Kiebrania, aje kwako, akunyonyeshee mtoto huyu?
8 Binti Farao akamwambia, Haya! Enenda. Yule kijana akaenda akamwita mama yake yule mtoto.
9 Binti Farao akamwambia, Mchukue mtoto huyu, ukaninyonyeshee, nami nitakupa mshahara wako. Yule mwanamke akamtwaa mtoto, akamnyonyesha.
10 Mtoto akakua, naye akamleta kwa binti Farao, akawa mwanawe. Akamwita jina lake Musa, akasema, Ni kwa sababu nalimtoa majini.
11 Hata siku zile, Musa alipokuwa mtu mzima, akatoka kuwaendea ndugu zake, akatazama mizigo yao. Akamwona Mmisri anampiga Mwebrania, mmojawapo wa ndugu zake.
12 Basi akatazama huko na huko, na alipoona ya kuwa hapana mtu, akampiga Mmisri yule, akamficha ndani ya mchanga.
13 Akatoka siku ya pili, na tazama, watu wawili wa Waebrania walikuwa wakipigana. Akamwambia yule aliyemdhulumu mwenzake, Mbona unampiga mwenzako?
14 Yule akasema, Ni nani aliyekuweka wewe kuwa mkuu wetu, na mwamuzi juu yetu? Je! Wataka kuniua mimi kama ulivyomwua yule Mmisri? Musa akaogopa, akasema, Kumbe! Jambo lile limejulikana.
15 Basi Farao alipopata habari, akataka kumwua Musa; lakini Musa akakimbia mbele ya Farao, akakaa katika nchi ya Midiani; akaketi karibu na kisima.
16 Basi kuhani wa Midiani alikuwa na binti saba, nao wakaja wakateka maji, wakazijaza birika maji, wapate kunywesha kundi la baba yao.
17 Wachungaji wakaja wakawafukuza; lakini Musa akasimama, akawasaidia, akalinywesha kundi lao.
18 Walipofika kwa Reueli baba yao, akasema, Imekuwaje hata mkarejea mapema leo?
19 Wakasema, Mmisri mmoja alituokoa katika mikono ya wachungaji, tena zaidi ya hayo, akatutekea maji, akalinywesha kundi.
20 Akawaambia binti zake, Yuko wapi basi? Mbona mmemwacha mtu huyo? Mwiteni, ale chakula.
21 Musa akawa radhi kukaa kwake mtu yule, naye akampa Musa binti yake, Sipora.
22 Huyo akamzalia mwana, akamwita jina lake Gershomu, maana alisema, Nimekuwa mgeni katika nchi ya ugeni.
23 Hata baada ya siku zile nyingi mfalme wa Misri akafa; wana wa Israeli wakaugua kwa sababu ya ule utumwa, wakalia; kilio chao kikafika juu kwa Mungu kwa sababu ya ule utumwa.
24 Mungu akasikia kuugua kwao, Mungu akakumbuka agano lake alilolifanya na Ibrahimu na Isaka na Yakobo.
25 Mungu akawaona wana wa Israeli, na Mungu akawaangalia.

Kutoka 3


1 Basi huyo Musa alikuwa akilichunga kundi la Yethro mkwewe, kuhani wa Midiani; akaliongoza kundi nyuma ya jangwa, akafika mpaka mlima wa Mungu, hata Horebu.
2 Malaika wa Bwana akamtokea, katika mwali wa moto uliotoka katikati ya kijiti; akatazama, na kumbe! Kile kijiti kiliwaka moto, nacho kijiti hakikuteketea.
3 Musa akasema, Nitageuka sasa, niyaone maono haya makubwa, na sababu kijiti hiki hakiteketei.
4 Bwana alipoona ya kuwa amegeuka ili atazame, Mungu akamwita kutoka katikati ya kile kijiti, akasema, Musa! Musa! Akasema, Mimi hapa.
5 Naye akasema, Usikaribie hapa; vua viatu vyako miguuni mwako; maana mahali hapo unaposimama ni nchi takatifu.
6 Tena akasema, Mimi ni Mungu wa baba yako, Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo. Musa akaficha uso wake; kwa maana aliogopa kumwangalia Mungu.
7 Bwana akasema, Hakika nimeyaona mateso ya watu wangu walioko Misri, nami nimekisikia kilio chao kwa sababu ya wasimamizi wao; maana nayajua maumivu yao;
8 nami nimeshuka ili niwaokoe na mikono ya Wamisri, niwapandishe kutoka nchi ile, hata nchi njema, kisha pana; nchi ijaayo maziwa na asali; hata mahali pa Mkanaani, na Mhiti, na Mwamori, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi.
9 Basi, tazama, kilio cha wana wa Israeli kimenifikilia; tena nimeyaona hayo mateso ambayo Wamisri wanawatesa.
10 Haya, basi, nitakutuma sasa kwa Farao, ili upate kuwatoa watu wangu, hao wana wa Israeli, katika Misri.
11 Musa akamwambia Mungu, Mimi ni nani, hata niende kwa Farao, nikawatoe wana wa Israeli watoke Misri?
12 Akasema, Bila shaka mimi nitakuwa pamoja nawe; na dalili ya kuwa nimekutuma ndiyo hii; utakapokuwa umekwisha kuwatoa hao watu katika Misri, mtamwabudu Mungu katika mlima huu.
13 Musa akamwambia Mungu, Tazama, nitakapofika kwa wana wa Israeli, na kuwaambia, Mungu wa baba zenu amenituma kwenu; nao wakaniuliza, Jina lake n'nani? Niwaambie nini?
14 Mungu akamwambia Musa, MIMI NIKO AMBAYE NIKO;akasema,Ndivyo utakavyowaambia wana wa Israeli;MIMI NIKO amenituma kwenu.
15 Tena Mungu akamwambia Musa, Waambie wana wa Israeli maneno haya, Bwana, Mungu wa baba zenu, Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, Mungu wa Yakobo, amenituma kwenu; hili ndilo jina langu hata milele, nalo ni kumbukumbu langu hata vizazi vyote.
16 Enenda, ukawakusanye wazee wa Israeli pamoja, ukawaambie, Bwana, Mungu wa baba zenu, Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, Mungu wa Yakobo, amenitokea, akaniambia, Hakika nimewajilieni, tena nimeyaona mnayotendewa huko Misri;
17 Nami nimesema, Nitawapandisha kutoka katika mateso ya Misri na kuwaingiza katika nchi ya Mkanaani, na Mhiti, na Mwamori, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi, nchi ijaayo maziwa na asali.
18 Nao watakusikia sauti yako; nawe utakwenda, wewe na wazee wa Israeli kwa mfalme wa Misri, na kumwambia, Bwana Mungu wa Waebrania, amekutana nasi; basi sasa twakuomba, tupe ruhusa twende mwendo siku tatu jangwani, ili tumtolee dhabihu Bwana Mungu wetu.
19 Nami najua ya kuwa huyo mfalme wa Misri hatawapa ruhusa mwende zenu, la, hata kwa mkono wa nguvu.
20 Nami nitaunyosha mkono wangu, na kuipiga Misri kwa ajabu zangu zote, nitakazofanya kati yake, kisha baadaye atawapa ruhusa kwenda.
21 Nami nitawapa watu hao kufadhiliwa mbele ya Wamisri; hata itakuwa, hapo mtakapokwenda zenu hamtakwenda kitupu;
22 Lakini kila mwanamke ataomba kwa jirani, na kwa huyo akaaye naye nyumbani, vyombo vya fedha, na vyombo vya dhahabu, na mavazi; nanyi mtawavika wana wenu na binti zenu; nanyi mtawateka nyara Wamisri.

Kutoka 4


1 Musa akajibu akasema, Lakini, tazama, hawataniamini, wala hawataisikia sauti yangu; maana watasema, Bwana hakukutokea.
2 Bwana akamwambia, Ni nini hiyo uliyo nayo mkononi mwako? Akasema, Ni fimbo.
3 Akamwambia, Itupe chini; akaitupa chini, nayo ikawa nyoka; Musa akakimbia mbele yake.
4 Bwana akamwambia Musa, Nyosha mkono wako, kamshike mkia; (akaunyosha mkono wake akamshika, naye akageuka kuwa fimbo mkononi mwake;)
5 ili kwamba wapate kusadiki ya kwamba Bwana, Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, Mungu wa Yakobo, amekutokea.
6 Bwana akamwambia tena, Sasa tia mkono wako kifuani mwako. Akautia mkono wake kifuani mwake; naye alipoutoa, kumbe! Mkono wake ulikuwa una ukoma, umekuwa mweupe kama theluji.
7 Akasema, Tia mkono wako kifuani mwako tena. Akautia mkono wake kifuani mwake tena, na alipoutoa kifuani mwake, kumbe! Umerudia hali ya mwili wake.
8 Basi itakuwa, wasipokusadiki, wala kuisikiliza sauti ya ishara ya kwanza, wataisikiliza sauti ya ishara ya pili.
9 Kisha itakuwa wasipoamini hata ishara hizo mbili, wala kuisikiliza sauti yako, basi, yatwae maji ya mtoni uyamwage juu ya nchi kavu, na yale maji uyatwaayo mtoni yatakuwa damu juu ya nchi kavu.
10 Musa akamwambia Bwana Ee Bwana, mimi si msemaji, tokea zamani, wala tokea hapo uliposema na mtumishi wako; maana mimi si mwepesi wa kusema, na ulimi wangu ni mzito.
11 Bwana akamwambia, Ni nani aliyekifanya kinywa cha mwanadamu? Au ni nani afanyaye mtu kuwa bubu au kiziwi, au mwenye kuona, au kuwa kipofu? Si mimi, Bwana?
12 Basi sasa, enenda, nami nitakuwa pamoja na kinywa chako, na kukufundisha utakalolinena.
13 Akasema, Ee Bwana, nakuomba, tuma kwa mkono wake huyo utakayemtuma.
14 Hasira ya Bwana ikawaka juu ya Musa, akasema, Je! Hayuko Haruni, ndugu yako, Mlawi? Najua ya kuwa yeye aweza kusema vizuri. Pamoja na hayo, tazama, anakuja kukulaki; naye atakapokuona, atafurahi moyoni mwake.
15 Nawe utasema naye, na kuyatia maneno kinywani mwake; nami nitakuwa pamoja na kinywa chako, na pamoja na kinywa chake, na kuwafundisheni mtakayofanya.
16 Naye atakuwa msemaji wako kwa watu, hata yeye atakuwa mfano wa kinywa kwako, nawe utakuwa mfano wa Mungu kwake.
17 Nawe utatwaa fimbo hii mkononi mwako, na kwa hiyo utazifanya zile ishara.
18 Basi Musa akaenda na kurejea kwa Yethro mkwewe, na kumwambia, Nipe ruhusa niende, nakusihi, niwarudie hao ndugu zangu walioko Misri, nipate kuwaona kwamba wako hai hata sasa. Yethro akamwambia Musa, Haya, nenda kwa amani.
19 Bwana akamwambia Musa huko Midiani, Haya, nenda, karudi Misri; kwa kuwa wale watu wote waliokutaka uhai wako wamekwisha kufa.
20 Basi Musa akamchukua mkewe na wanawe, na kuwapandisha juu ya punda, naye akarudi mpaka nchi ya Misri; na Musa akaichukua ile fimbo ya Mungu mkononi mwake.
21 Bwana akamwambia Musa, Hapo utakaporudi Misri, angalia ukazifanye mbele ya Farao zile ajabu zote nilizozitia mkononi mwako; lakini nitaufanya mgumu moyo wake, naye hatawapa ruhusa hao watu waende zao.
22 Nawe umwambie Farao, Bwana asema hivi, Israeli ni mwanangu mimi, mzaliwa wa kwanza wangu;
23 nami nimekuambia, Mpe mwanangu ruhusa aende, ili apate kunitumikia, nawe umekataa kumpa ruhusa aende; angalia basi, mimi nitamwua mwanao, mzaliwa wa kwanza wako.
24 Ilikuwa walipokuwa njiani mahali pa kulala, Bwana akakutana naye akataka kumwua.
25 Ndipo Sipora akashika jiwe gumu na kuikata govi ya zunga la mwanawe, na kuibwaga miguuni pake akasema. Hakika wewe u bwana arusi wa damu kwangu mimi.
26 Basi akamwacha. Ndipo huyo mkewe akanena, U bwana arusi wa damu wewe, kwa ajili ya kutahiri.
27 Bwana akamwambia Haruni, Nenda jangwani uonane na Musa. Naye akaenda, akamkuta katika mlima wa Mungu, akambusu.
28 Musa akamwambia Haruni hayo maneno yote ya Bwana ambayo alimtuma aende nayo, na ishara hizo zote alizomwagiza.
29 Musa na Haruni wakaenda, wakawakusanya wazee wote wa watu wa Israeli.
30 Haruni akawaambia maneno yote Bwana aliyonena na Musa akazifanya zile ishara mbele ya watu.
31 Watu wakaamini, na waliposikia ya kuwa Bwana amewajilia wana wa Israeli, na ya kuwa ameyaona mateso yao, wakainama vichwa vyao wakasujudu.

Kutoka 5


1 Hata baadaye, Musa na Haruni wakaenda wakamwambia Farao, wakasema, Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Wape watu wangu ruhusa waende, ili kunifanyia sikukuu jangwani.
2 Farao akasema, Bwana ni nani, hata niisikilize sauti yake, na kuwapa Israeli ruhusa waende zao? Mimi simjui Bwana, wala sitawapa Israeli ruhusa waende zao.
3 Wakasema, Mungu wa Waebrania amekutana nasi; twakuomba, tupe ruhusa twende safari ya siku tatu jangwani, tumtolee dhabihu Bwana, Mungu wetu; asije akatupiga kwa tauni, au kwa upanga.
4 Mfalme wa Misri akawaambia Enyi Musa na Haruni, mbona mnawaachisha watu kazi zao? Enendeni zenu kwa mizigo yenu.
5 Kisha Farao akasema, Tazameni, watu wa nchi sasa ni wengi, nanyi mnawapumzisha, wasichukue mizigo yao.
6 Na siku ile ile Farao akawaamuru wasimamizi wa watu, na wanyapara wao, akisema,
7 Msiwape watu tena majani ya kufanyia matofali, kama mlivyofanya tangu hapo; na waende wakatafute majani wenyewe.
8 Lakini hesabu ya matofali waliyokuwa wakifanya tokea hapo, wawekeeni iyo hiyo, msiipunguze hata kidogo, kwa maana ni wavivu hao; kwa hiyo wanapiga kelele, wakisema, Tupe ruhusa twende kumtolea Mungu wetu dhabihu.
9 Wapeni watu hao kazi nzito zaidi, waitaabikie; wala wasiangalie maneno ya uongo.
10 Hao wasimamizi wa watu na wanyapara wao wakatoka, wakasema na watu, wakanena, Farao asema hivi, Mimi siwapi majani.
11 Enendeni wenyewe, jipatieni majani hapo mtakapoyaona; kwa maana kazi yenu haitapunguzwa hata kidogo.
12 Basi hao watu wakatawanyika katika nchi yote ya Misri ili wapate kukusanya matakataka ya mashamba badala ya majani.
13 Wasimamizi wao wakawahimiza, wakisema, Timizeni kazi zenu, shughuli zenu za kila siku, kama wakati ule majani yalipokuwapo.
14 Na wanyapara wa wana wa Israeli, ambao wasimamizi wa Farao wamewaweka juu yao, wakapigwa, wakiambiwa, Kwa nini hamkutimiza kazi yenu jana na leo; kwa kufanya matofali kama hapo kwanza?
15 Basi wanyapara wa wana wa Israeli wakaenda, wakamlilia Farao, wakisema, Mbona umetutendea hivi, sisi watumwa wako?
16 Watumwa wako hawapewi majani, nao wanatuambia, Fanyeni matofali; na tazama, watumwa wako wapigwa; lakini kosa hilo ni la watu wako mwenyewe.
17 Akasema, Wavivu ninyi; wavivu; kwa ajili hii mwasema, Tupe ruhusa twende kumtolea Bwana dhabihu.
18 Basi, enendeni sasa, mkafanye kazi; kwa maana hamtapewa majani, na pamoja na hayo mtaleta hesabu ile ile ya matofali.
19 Basi wanyapara wa wana wa Israeli wakaona ya kwamba wa katika hali mbaya, walipoambiwa, Hamtapunguza hesabu ya matofali yenu hata kidogo; ndizo shughuli zenu za kila siku.
20 Wakakutana na Musa na Haruni, waliokuwa wanasimama njiani, hapo walipotoka kwa Farao;
21 wakawaambia, Bwana awaangalie na kuamua; kwa kuwa mmefanya harufu yetu kuwa chukizo mbele ya Farao, na mbele ya watumishi wake, mkatia upanga mikononi mwao, watuue.
22 Musa akarudi kwa Bwana, akasema, Bwana, mbona umewatenda mabaya watu hawa? Kwani kunituma mimi?
23 Kwa maana tangu nilipokwenda kwa Farao, kusema naye kwa jina lako, amewatenda mabaya watu hawa; wala hukuwaokoa watu wako hata kidogo.

Kutoka 6


1 Bwana akamwambia Musa, Sasa utaona nitakavyomtenda Farao; maana kwa mkono hodari atawapa ruhusa kwenda zao, na kwa mkono hodari atawafukuza katika nchi yake.
2 Kisha Mungu akasema na Musa, akamwambia, Mimi ni YEHOVA;
3 nami nilimtokea Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, kama Mungu Mwenyezi, bali kwa jina langu YEHOVA sikujulikana kwao.
4 Tena nimelithibitisha agano langu nao, la kuwapa nchi ya Kanaani; nchi ya kukaa kwao hali ya ugeni.
5 Na zaidi ya hayo, nimesikia kuugua kwao wana wa Israeli, ambao Wamisri wanawatumikisha, nami nimelikumbuka agano langu.
6 Basi waambie wana wa Israeli, Mimi ni YEHOVA, nami nitawatoa ninyi mtoke chini ya mizigo ya Wamisri, nami nitawaokoa na utumwa wao, nami nitawakomboa kwa mkono ulionyoshwa, na kwa hukumu kubwa;
7 nami nitawatwaeni kuwa watu wangu, nitakuwa Mungu kwenu; nanyi mtajua ya kuwa mimi ni YEHOVA, Mungu wenu, niwatoaye mtoke chini ya mizigo ya Wamisri.
8 Nami nitawaleta hata nchi ile ambayo naliinua mkono wangu, niwape Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo; nitawapa iwe urithi wenu; Mimi ni YEHOVA.
9 Musa akawaambia wana wa Israeli maneno haya; lakini hawakumsikiliza Musa kwa ajili ya uchungu wa moyo, na kwa ajili ya utumwa mgumu.
10 Bwana akasema na Musa, akamwambia,
11 Ingia ndani, ukaseme na Farao, mfalme wa Misri, ili awape ruhusa wana wa Israeli watoke nchi yake.
12 Musa akanena mbele ya Bwana, akasema, Tazama, hao wana wa Israeli hawakunisikiza mimi; basi huyo Farao atanisikizaje, mimi niliye na midomo isiyo tohara?
13 Bwana akanena na Musa na Haruni, akawaagiza wawaendee wana wa Israeli, na Farao, mfalme wa Misri, ili awatoe hao wana wa Israeli katika nchi ya Misri.
14 Hawa ndio vichwa vya nyumba za baba zao: wana wa Reubeni, mzaliwa wa kwanza wa Israeli; ni Hanoki, na Palu, na Hesroni, na Karmi; hao ni jamaa za Reubeni.
15 Na wana wa Simeoni; ni Yemueli, na Yamini, na Ohadi, na Yakini, na Sohari, na Shauli mwana wa mwanamke wa Kikanaani; hao ni jamaa za Simeoni.
16 Na haya ndiyo majina ya wana wa Lawi, sawasawa na vizazi vyao; Gershoni, na Kohathi, na Merari; na miaka ya maisha yake Lawi ilikuwa ni miaka mia na thelathini na saba.
17 Wana wa Gershoni; ni Libni, na Shimei, sawasawa na jamaa zao.
18 Na wana wa Kohathi; ni Amramu, na Ishari, na Hebroni, na Uzieli; na miaka ya maisha ya huyo Kohathi ilikuwa ni miaka mia na thelathini na mitatu.
19 Na wana wa Merari; ni Mali, na Mushi. Hizi ni jamaa za hao Walawi sawasawa na vizazi vyao.
20 Huyo Amramu akamwoa Yokebedi ndugu ya baba yake; naye akamzalia Haruni, na Musa; na miaka ya maisha yake Amramu ilikuwa ni miaka mia na thelathini na saba.
21 Na wana wa Ishari; ni Kora, na Nefegi, na Zikri.
22 Na wana wa Uzieli; ni Mishaeli, na Elisafani, na Sithri.
23 Haruni akamwoa Elisheba, binti ya Aminadabu, umbu lake Nashoni; naye akamzalia Nadabu, na Abihu, na Eleazari, na Ithamari.
24 Na wana wa Kora; ni Asiri, na Elkana, na Abiasafu; hizo ni jamaa za hao Wakora.
25 Na Eleazari mwana wa Haruni akamwoa mmoja miongoni mwa binti za Putieli; naye akamzalia Finehasi. Hawa ndio vichwa vya nyumba za mababa ya Walawi sawasawa na jamaa zao.
26 Hawa ni Haruni ye yule, na Musa ye yule, Bwana aliowaambia, akisema, Watoeni wana wa Israeli watoke nchi ya Misri sawasawa na majeshi yao.
27 Ni hao walionena na Farao mfalme wa Misri ili wawatoe wana wa Israeli watoke Misri; hao ni Musa ye yule, na Haruni ye yule.
28 Ilikuwa siku hiyo Bwana aliponena na Musa katika nchi ya Misri,
29 Bwana akamwambia Musa, akasema, Mimi ni Bwana; mwambie Farao mfalme wa Misri maneno yote nikuambiayo.
30 Musa akanena mbele ya Bwana, Mimi ni mtu mwenye midomo isiyo tohara, Farao atanisikizaje?

Kutoka 7


1 Bwana akamwambia Musa, Angalia, nimekufanya wewe kuwa kama Mungu kwa Farao; na huyo ndugu yako Haruni atakuwa nabii wako.
2 Utanena hayo yote nikuagizayo; na ndugu yako Haruni atanena na Farao, ili awape wana wa Israeli ruhusa watoke nchi yake.
3 Nami nitaufanya mgumu moyo wa Farao, nami nitazifanya kuwa nyingi ishara zangu na ajabu zangu katika nchi ya Misri.
4 Lakini Farao hatawasikiza ninyi, nami nitaweka mkono wangu juu ya Misri, na kuyatoa majeshi yangu, watu wangu, hao wana wa Israeli, watoke nchi ya Misri kwa hukumu zilizo kuu.
5 Na Wamisri watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, hapo nitakapounyosha mkono wangu juu ya Misri na kuwatoa wana wa Israeli watoke kati yao.
6 Musa na Haruni wakafanya vivyo; kama Bwana alivyowaambia, ndivyo walivyofanya.
7 Huyo Musa alikuwa ni mtu wa miaka themanini umri wake, na Haruni alikuwa ni mtu wa miaka themanini na mitatu, hapo waliponena na Farao.
8 Bwana akanena na Musa na Haruni, akawaambia,
9 Farao atakaponena nanyi, na kuwaambia, Jifanyieni miujiza; ndipo utakapomwambia Haruni, Shika fimbo yako, uibwage chini mbele ya Farao, ili iwe nyoka.
10 Basi Musa na Haruni wakaingia kwa Farao, wakafanya vivyo kama Bwana alivyowaambia; Haruni akaibwaga fimbo yake chini mbele ya Farao, mbele ya watumishi wake, ikawa nyoka.
11 Ndipo Farao naye akawaita wenye akili na wachawi; na hao waganga wa Misri wakafanya vivyo kwa uganga wao.
12 Wakabwaga chini kila mtu fimbo yake, nazo zikawa nyoka; lakini fimbo ya Haruni ikazimeza fimbo zao.
13 Moyo wa Farao ukawa ni mgumu asiwasikize; kama Bwana alivyonena.
14 Bwana akamwambia Musa, Moyo wa Farao ni mzito, anakataa kuwapa watu ruhusa waende zao.
15 Mwendee Farao asubuhi; tazama, atoka kwenda majini; nawe simama karibu na ufuo wa mto ili upate kuonana naye; na ile fimbo iliyogeuzwa kuwa nyoka utaichukua mkononi mwako.
16 Nawe umwambie, Bwana, Mungu wa Waebrania, amenituma nije kwako, kusema, Wape watu wangu ruhusa, ili wapate kunitumikia jangwani; nawe, tazama! Hujasikia hata sasa.
17 Bwana asema, Katika jambo hili utanijua ya kuwa mimi ndimi Bwana; tazama, nitayapiga haya maji yaliyo mtoni kwa fimbo hii niliyo nayo mkononi mwangu, nayo yatageuzwa kuwa damu.
18 Na hao samaki walio mtoni watakufa, na huo mto utatoa uvundo; nao Wamisri watachukizwa kuyanywa maji ya mtoni.
19 Bwana akamwambia Musa, Mwambie Haruni, Shika fimbo yako, kaunyoshe mkono wako juu ya maji ya Misri, juu ya mito yao, juu ya vijito vyao, na juu ya maziwa ya maji yao, na juu ya visima vyao vyote vya maji, ili yageuke kuwa damu, nako kutakuwa na damu katika nchi yote ya Misri, katika vyombo vya mti, na katika vyombo vya jiwe.
20 Musa na Haruni wakafanya hivyo, kama Bwana alivyowaambia; naye akaiinua ile fimbo, na kuyapiga maji yaliyokuwa mtoni, mbele ya Farao, mbele ya watumishi wake; na hayo maji yote yaliyokuwa katika mto yakageuzwa kuwa damu.
21 Hao samaki waliokuwa mtoni nao wakafa; na ule mto ukatoa uvundo, Wamisri wasipate kunywa maji ya mtoni; na ile damu ilikuwa katika nchi yote na Misri.
22 Lakini waganga wa Misri wakafanya mfano wa hayo kwa uganga wao; na moyo wake Farao ukawa mgumu, wala hakuwasikiza, kama Bwana alivyonena.
23 Farao akazunguka na kuingia nyumbani mwake, wala hata hilo hakuliweka moyoni.
24 Wamisri wote wakachimba-chimba kando ya mto ili wapate maji ya kunywa; maana, hawakuweza kuyanywa yale maji ya mtoni.
25 Zikatimia siku saba, baada ya Bwana kuupiga ule mto.

Kutoka 8


1 Bwana akamwambia Musa, Ingia kwa Farao, ukamwambie, Bwana asema hivi, Wape watu wangu ruhusa, ili wapate kunitumikia.
2 Tena kama ukikataa kuwapa ruhusa, tazama, nitaipiga mipaka yako yote kwa kuleta vyura;
3 na huo mto utafurika vyura, nao watakwea juu na kuingia ndani ya nyumba yako, na ndani ya chumba chako cha kulala, na juu ya kitanda chako, na ndani ya nyumba ya watumishi wako, na juu ya watu wako, na ndani ya meko yako, na ndani ya vyombo vyako vya kukandia unga.
4 Kisha hao vyura watakwea juu yako wewe, na juu ya watu wako, na juu ya watumishi wako wote.
5 Bwana akamwambia Musa, Mwambie Haruni, Nyosha mkono wako na fimbo yako juu ya mito, juu ya vijito, na juu ya maziwa ya maji, ukawalete vyura waje juu ya nchi yote ya Misri.
6 Basi Haruni akaunyosha mkono wake juu ya maji yote ya Misri; na hao vyura wakakwea juu, wakaifunika nchi ya Misri.
7 Waganga nao wakafanya mfano wa hayo kwa uganga wao; na kuwaleta vyura juu ya nchi ya Misri.
8 Ndipo Farao akawaita Musa na Haruni na kuwaambia, Mwombeni Bwana, ili awaondoe vyura hawa kwangu mimi na kwa watu wangu; nami nitawapa watu ruhusa waende zao, ili wamtolee Bwana dhabihu.
9 Musa akamwambia Farao, Haya, ujitukuze juu yangu katika jambo hili; sema ni lini unapotaka nikuombee wewe, na watumishi wako, na watu wako, ili hao vyura waangamizwe watoke kwako wewe na nyumba zako, wakae ndani ya mto tu.
10 Akamwambia, Kesho, Akasema, Na yawe kama neno lako; ili upate kujua ya kwamba hapana mwingine mfano wa Bwana, Mungu wetu.
11 Hao vyura wataondoka kutoka kwako wewe na nyumba zako, na watumishi wako, na watu wako; watasalia mtoni tu.
12 Basi Musa na Haruni wakatoka kwa Farao; Musa akamlilia Bwana katika jambo la hao vyura aliokuwa amewaleta juu ya Farao.
13 Bwana akafanya sawasawa na neno la Musa; na hao vyura wakafa kutoka katika zile nyumba, na katika viwanja, na katika mashamba.
14 Wakawakusanya chungu chungu; na nchi ikatoa uvundo.
15 Lakini Farao alipoona ya kuwa pana nafuu, akaufanya moyo wake kuwa mzito, asiwasikize; kama Bwana alivyonena.
16 Bwana akamwambia Musa, Mwambie Haruni, Nyosha fimbo yako, ukayapige mavumbi ya nchi, ili kwamba yawe chawa katika nchi yote ya Misri.
17 Nao wakafanya; Haruni akaunyosha mkono wake na fimbo yake, na kuyapiga mavumbi ya nchi, nayo yakawa chawa juu ya wanadamu na juu ya wanyama; mavumbi yote ya nchi yakawa ni chawa katika nchi yote ya Misri.
18 Hao waganga nao wakafanya mfano wa hayo kwa uganga wao, ili kwamba walete chawa, lakini wasiweze; nako kulikuwa na chawa juu ya wanadamu, na juu ya wanyama.
19 Ndipo wale waganga wakamwambia Farao, Jambo hili ni chanda cha Mungu; na moyo wake Farao ukawa mgumu asiwasikize; vile vile kama Bwana alivyonena.
20 Bwana akamwambia Musa, Inuka asubuhi na mapema usimame mbele ya Farao; angalia! Atoka aende majini; kamwambie, Bwana asema, Wape watu wangu ruhusa waende zao, ili wanitumikie mimi.
21 Au kwamba huwapi ruhusa watu wangu, tazama, nitaleta wingi wa mainzi juu yako wewe, na juu ya watumishi wako, na juu ya watu wako, nao wataingia ndani ya nyumba zako; na nyumba za Wamisri zitajawa na wingi wa mainzi, na nchi nayo ambayo wa juu yake.
22 Nami siku hiyo nitatenga nchi ya Gosheni, watu wangu wanayokaa, ili hao mainzi wasiwe huko; ili kwamba upate kujua wewe ya kuwa mimi ndimi Bwana kati ya dunia.
23 Nami nitatia mpaka kati ya watu wangu na watu wako; ishara hiyo italetwa kesho.
24 Bwana akafanya; wakaja wingi wa mainzi kwa uzito sana, wakaingia nyumbani mwa Farao, na katika nyumba za watumishi wake, tena katika nchi yote ya Misri; nayo nchi iliharibiwa kwa ajili ya wale mainzi.
25 Farao akawaita Musa na Haruni akawaambia, Endeni mkamtolee Mungu wenu dhabihu ndani ya nchi hii.
26 Musa akasema, Haitupasi kufanya hivyo; kwa kuwa tutamchinjia sadaka Bwana, Mungu wetu, na hayo machukizo ya Wamisri; je! Tutachinja sadaka ya hayo machukizo ya Wamisri mbele ya macho yao, wasitupige kwa mawe?
27 La, tutakwenda safari ya siku tatu jangwani, tumchinjie dhabihu Bwana, Mungu wetu, kama atakavyotuagiza.
28 Farao akasema, Mimi nitawapa ruhusa mwende, ili mmchinjie dhabihu Bwana, Mungu wenu, jangwani; lakini hamtakwenda mbali sana; haya niombeeni.
29 Musa akasema, Tazama, mimi natoka kwako, nami nitamwomba Bwana ili hao mainzi wamtoke Farao, na watumishi wake, na watu wake kesho; lakini Farao asitende kwa udanganyifu tena, kwa kutowaacha watu waende kumchinjia Bwana dhabihu.
30 Musa akatoka kwa Farao, akamwomba Bwana.
31 Bwana akafanya kama neno la Musa, akawaondoa wale mainzi wabaya kwake Farao, na kwa watumishi wake, na watu wake; hakusalia hata mmoja.
32 Farao akaufanya moyo wake kuwa mzito mara hiyo nayo, wala hakuwapa ruhusa hao watu waende zao.

Kutoka 9


1 Ndipo Bwana akamwambia Musa, Ingia wewe kwa Farao, umwambie, Bwana, Mungu wa Waebrania, yuasema, Wape ruhusa watu wangu ili waende wanitumikie.
2 Kwani ukikataa kuwapa ruhusa waende, na kuzidi kuwazuia,
3 tazama, mkono wa Bwana u juu ya wanyama wako wa mifugo walioko kondeni, juu ya farasi, na juu ya punda, na juu ya ngamia, na juu ya ng'ombe, na juu ya kondoo; kutakuwa na tauni nzito sana.
4 Kisha Bwana atawatenga wanyama wa Israeli na wanyama wa Misri; wala hakitakufa kitu cho chote cha wana wa Israeli.
5 Naye Bwana akaweka muda, akasema, Kesho Bwana atalifanya jambo hili katika nchi.
6 Bwana akalifanya jambo hilo siku ya pili, na wanyama wote wa kufugwa wa Misri wakafa; lakini katika wanyama wa wana wa Israeli hakufa hata mmoja.
7 Farao akatuma watu, na tazama, hapana mmoja aliyekufa katika wanyama wa wana wa Israeli. Lakini moyo wa Farao ulikuwa mzito, wala hakuwapa hao watu ruhusa waende zao.
8 Bwana akawaambia Musa na Haruni, Jitwalieni konzi za majivu ya tanuuni, kisha Musa na ayarushe juu kuelekea mbinguni mbele ya Farao.
9 Nayo yatakuwa ni mavumbi membamba juu ya nchi yote ya Misri, nayo yatakuwa majipu yenye kufura na kutumbuka juu ya wanadamu na juu ya wanyama, katika nchi yote ya Misri.
10 Basi wakatwaa majivu ya tanuuni, na kusimama mbele ya Farao; na Musa akayarusha juu mbinguni nayo yakawa ni majipu yenye kufura na kutumbuka juu ya wanadamu na juu ya wanyama.
11 Nao wale waganga hawakuweza kusimama mbele ya Musa kwa sababu ya hayo majipu, kwa maana hao waganga walikuwa na majipu, na Wamisri wote walikuwa nayo.
12 Bwana akaufanya mgumu moyo wa Farao, asiwasikize; vile vile kama Bwana alivyomwambia Musa.
13 Bwana akamwambia Musa, Ondoka asubuhi na mapema, ukasimame mbele ya Farao, umwambie, Bwana, Mungu wa Waebrania, asema, Wape watu wangu ruhusa waende ili wanitumikie.
14 Kwani wakati huu nitaleta mapigo yangu yote juu ya moyo wako, na juu ya watumishi wako, na juu ya watu wako; ili upate kujua ya kuwa hapana mmoja mfano wa mimi ulimwenguni mwote.
15 Kwa kuwa wakati huu ningekwisha kuunyosha mkono wangu, na kukupiga wewe na watu wako, kwa tauni, nawe ungekatiliwa mbali na kuondolewa katika nchi;
16 lakini, nilikusimamisha wewe kwa sababu hii hii, ili nikuonyeshe uweza wangu, tena kwamba jina langu litangazwe katika dunia yote.
17 Nawe, je! Hata sasa wajitukuza juu ya watu wangu, usiwape ruhusa waende zao?
18 Tazama, kesho wakati kama huu, nitanyesha mvua ya mawe nzito sana, ambayo mfano wake haujakuwa huko Misri tangu siku ile ilipoanza kuwa hata hivi sasa.
19 Basi sasa tuma wahimize waingie ndani wanyama wako na hayo yote uliyo nayo mashambani; kwani kila mtu na kila mnyama apatikanaye mashambani, wasioletwa nyumbani, hiyo mvua ya mawe itanyesha juu yao, nao watakufa.
20 Yeye aliyelicha neno la Bwana miongoni mwa watumishi wa Farao aliwakimbiza watumishi wake na wanyama wake waingie nyumbani;
21 na yeye asiyelitia moyoni neno la Bwana akawaacha watumishi wake na wanyama wake mashambani.
22 Bwana akamwambia Musa, Nyosha mkono wako kuelekea mbinguni, ili iwe mvua ya mawe katika nchi yote ya Misri, juu ya wanadamu na juu ya wanyama, na juu ya mboga zote za mashamba, katika nchi yote ya Misri.
23 Musa akaunyosha mkono wake kuelekea mbinguni; na Bwana akaleta ngurumo na mvua ya mawe, na moto ukashuka juu ya nchi; Bwana akanyesha mvua ya mawe juu ya nchi yote ya Misri.
24 Basi palikuwa na mvua ya mawe, na moto uliochanganyikana na ile mvua ya mawe, nzito sana, ambayo mfano wake haukuwapo katika nchi yote ya Misri tangu ilipoanza kuwa taifa.
25 Na ile mvua ya mawe ikapiga kila kilichokuwako mashambani, binadamu na mnyama, katika nchi yote ya Misri; hiyo mvua ya mawe ikapiga kila mmea wa mashambani, na kuuvunja kila mti wa mashamba.
26 Katika nchi ya Gosheni peke yake, walikokaa wana wa Israeli, haikuwako mvua ya mawe.
27 Farao akatuma watu, na kuwaita Musa na Haruni, na kuwaambia, Mimi nimekosa wakati huu; Bwana ni mwenye haki, na mimi na watu wangu tu waovu.
28 Mwombeni Bwana; kwa kuwa zimekuwa za kutosha ngurumo hizo kuu na hii mvua ya mawe; nami nitawapa ninyi ruhusa mwende zenu, msikae zaidi.
29 Musa akamwambia, Mara nitakapotoka mjini nitamwinulia Bwana mikono yangu; na hizo ngurumo zitakoma, wala haitanyesha mvua ya mawe tena; ili upate kujua ya kuwa dunia hii ni ya Bwana.
30 Lakini, wewe na watumishi wako, najua ya kuwa ninyi hamtamcha Bwana Mungu bado.
31 Kitani na shayiri zilipigwa; maana shayiri zilikuwa na masuke na kitani zilikuwa katika kutoa maua.
32 Lakini ngano na kusemethu hazikupigwa; maana, zilikuwa hazijakua bado.
33 Musa akatoka mjini, kutoka kwa Farao, akamwinulia Bwana mikono yake; na zile ngurumo na ile mvua ya mawe zikakoma, wala mvua haikunyesha juu ya nchi.
34 Farao alipoona ya kwamba mvua na mvua ya mawe na ngurumo zimekoma, akazidi kufanya dhambi, na kuufanya moyo wake mzito, yeye na watumishi wake.
35 Moyo wa Farao ukawa ni mgumu naye hakuwapa wana wa Israeli ruhusa waende zao; kama Bwana alivyonena kwa kinywa cha Musa.

Kutoka 10


1 Bwana akamwambia Musa, Ingia wewe kwa Farao; kwa kuwa mimi nimeufanya moyo wake mzito, nipate kuzionyesha ishara zangu hizi kati yao;
2 nawe upate kusema masikioni mwa mwanao, na masikioni mwa mjukuu wako, ni mambo gani niliyotenda juu ya Misri, na ishara zangu nilizozifanya kati yao; ili mpate kujua ya kuwa mimi ndimi Bwana.
3 Basi Musa na Haruni wakaingia kwa Farao, na kumwambia, Bwana, Mungu wa Waebrania, asema hivi, Je! Utakataa hata lini kujinyenyekeza mbele zangu? Wape watu wangu ruhusa waende zao, ili wanitumikie.
4 Au, kwamba wakataa kuwapa hao watu wangu ruhusa waende zao, tazama, kesho nitaleta nzige waingie ndani ya mipaka yako;
5 nao wataufunika uso wa nchi, mtu asipate kuona hiyo nchi; nao watakula mabaki ya hayo yaliyopona yaliyowasalia baada ya ile mvua ya mawe, watakula kila mti umeao kwa ajili yenu mashambani;
6 na nyumba zako, na nyumba za watumishi wako, na nyumba za Wamisri wote zitajawa na nzige; mfano wake baba zako wala baba za baba zako hawakuona, tangu siku walipoanza kuwapo juu ya nchi hata hivi leo. Basi akageuka na kutoka kwa Farao.
7 Ndipo watumishi wa Farao wakamwambia, Mtu huyu atakuwa tanzi kwetu sisi hata lini? Wape hawa watu ruhusa waende zao, wamtumikie Bwana, Mungu wao; hujatambua bado ya kuwa Misri imekwisha haribika?
8 Musa na Haruni wakaletwa tena kwa Farao; naye akawaambia, Nendeni, mkamtumikie Bwana, Mungu wenu; lakini ni kina nani watakaokwenda?
9 Musa akamjibu, Tutakwenda na vijana wetu na wazee wetu, na wana wetu, na binti zetu, tutakwenda na kondoo zetu na ng'ombe zetu; kwa kuwa inatupasa kumfanyia Bwana sikukuu.
10 Lakini akawaambia, Ehe, Bwana na awe pamoja nanyi, kama nitakavyowapa ruhusa kwenda zenu pamoja na watoto wenu; angalieni, kwa kuwa pana uovu huko mbele yenu.
11 Sivyo; endeni ninyi mlio watu wazima, mkamtumikie Bwana; kwa kuwa ndilo jambo mtakalo. Nao walifukuzwa usoni pa Farao.
12 Bwana akamwambia Musa, Nyosha mkono wako juu ya nchi ya Misri kwa hao nzige, ili wakwee juu ya nchi ya Misri, waile mimea yote ya nchi, yaani, vyote vilivyosazwa na ile mvua ya mawe.
13 Basi Musa akainyosha fimbo yake juu ya nchi ya Misri, na Bwana akaleta upepo kutoka mashariki juu ya nchi, mchana kutwa, na usiku kucha; kulipopambazuka ule upepo wa mashariki ukawaleta nzige.
14 Na hao nzige wakakwea juu ya nchi yote ya Misri, wakatua ndani ya mipaka yote ya Misri, walikuwa wabaya mno; hawajakuwapo nzige kama hao majira yo yote, wala baada yao hawatakuwa wengine jinsi hiyo.
15 Kwa kuwa waliufunika uso wote wa nchi, hata nchi iliingia giza; wakala mimea yote ya nchi, na matunda yote ya miti yaliyosazwa na ile mvua ya mawe; hapakusalia hata jani moja, mti wala mmea wa mashamba, katika nchi yote ya Misri.
16 Ndipo Farao akawaita Musa na Haruni haraka; akasema, Nimemfanyia dhambi Bwana, Mungu wenu na ninyi pia.
17 Basi sasa, nawasihi, nisameheni dhambi yangu mara hii moja tu, mkamwombe Bwana, Mungu wenu, aniondolee kifo hiki tu.
18 Akatoka kwa Farao, na kumwomba Bwana.
19 Bwana akaugeuza upepo wa magharibi wenye nguvu nyingi, ambao uliwaondoa wale nzige na kuwapeleka katika Bahari ya Shamu; hakusalia hata nzige mmoja ndani ya mipaka yote ya Misri.
20 Lakini Bwana akaufanya ule moyo wa Farao uwe mgumu, asiwape wana wa Israeli ruhusa waende zao.
21 Bwana akamwambia Musa, Nyosha mkono wako kuelekea mbinguni, kuwe giza juu ya nchi ya Misri, watu wapapase-papase gizani.
22 Basi Musa akaunyosha mkono wake kuelekea mbinguni; kukawa na giza nene katika nchi yote ya Misri muda wa siku tatu;
23 hawakupata kuonana mtu na mwenziwe, wala hakuondoka mtu mahali alipokuwa muda wa siku tatu; lakini wana wa Israeli wote walikuwa na mwanga makaoni mwao.
24 Farao akamwita Musa, na kumwambia, Haya, nendeni, mkamtumikie Bwana; kondoo zenu na ng'ombe zenu tu na waachwe; watoto wenu nao na waende pamoja nanyi.
25 Musa akasema, Ni lazima utupe mikononi mwetu na wanyama wa dhabihu na wa sadaka za kuteketezwa, ili tupate kumchinjia Bwana Mungu wetu dhabihu.
26 Makundi yetu pia watakwenda pamoja nasi; hautasalia nyuma hata ukwato mmoja; kwa maana inampasa kutwaa katika hao tupate kumtumikia Bwana, Mungu wetu; nasi hatujui, hata tutakapofika huko, ni kitu gani ambacho kwa hicho inatupasa kumtumikia Bwana.
27 Lakini Bwana akaufanya kuwa mgumu moyo wa Farao, asikubali kuwapa ruhusa waende zao.
28 Farao akamwambia Musa, Nenda zako, ujiangalie, usinione uso tena; kwani siku hiyo utakayoniangalia uso wangu utakufa.
29 Musa akasema, Umenena vema; mimi sitakuangalia uso wako tena.

Kutoka 11


1 Bwana akamwambia Musa, Liko pigo moja bado, nitakaloleta juu ya Farao na juu ya Misri; baadaye atawapa ninyi ruhusa mtoke huku; naye hapo atakapowapa ruhusa, atawafukuza mtoke huku kabisa kabisa.
2 Basi nena wewe masikioni mwa watu hawa, na kila mtu mume na atake kwa jirani yake, na kila mwanamke atake kwa jirani yake, vyombo vya fedha, na vyombo vya dhahabu.
3 Bwana akawapa watu hao kibali machoni pa Wamisri. Zaidi ya hayo, huyo Musa alikuwa ni mkuu sana katika nchi ya Misri, machoni pa watumishi wa Farao, na machoni pa watu wake.
4 Musa akasema, Bwana asema hivi, Kama usiku wa manane mimi nitatoka nipite kati ya Misri;
5 na wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri watakufa, tangu yule mzaliwa wa kwanza wa Farao aketiye katika kiti chake cha enzi, hata mzaliwa wa kwanza wa huyo kijakazi aliye pale nyuma ya jiwe la kusagia; na wazaliwa wa kwanza wote wa wanyama.
6 Ndipo kutakuwa na kilio kikuu katika nchi yote ya Misri, ambacho mfano wake haujakuwa bado majira yo yote, wala hautakuwako mfano wake tena kabisa.
7 Lakini katika wana wa Israeli hapana hata mbwa atakayetoa ulimi juu yao, juu ya mtu wala juu ya mnyama; ili kwamba mpate kujua jinsi Bwana anavyowatenga Wamisri na Waisraeli.
8 Tena hao watumishi wako wote watanitelemkia kwangu mimi, nao watanisujudia, wakisema, Toka wewe, na hawa watu wote wakufuatao; na baada ya hayo nitatoka. Basi akatoka kwa Farao na hasira kuu.
9 Bwana akamwambia Musa, Farao hatawasikiza ninyi; kusudi ajabu zangu ziongezeke katika nchi ya Misri.
10 Musa na Haruni walifanya ajabu hizo zote mbele ya Farao; Bwana akaufanya moyo wa Farao kuwa mgumu, asiwape wana wa Israeli ruhusa watoke nchi yake.

Kutoka 12


1 Bwana akanena na Musa na Haruni katika nchi ya Misri, akawaambia,
2 Mwezi huu utakuwa mwanzo wa miezi kwenu; utakuwa ni mwezi wa kwanza wa mwaka kwenu.
3 Semeni na mkutano wote wa Israeli, mkawaambie, Siku ya kumi ya mwezi huu kila mtu atatwaa mwana-kondoo, kwa hesabu ya nyumba ya baba zao, mwana-kondoo kwa watu wa nyumba moja;
4 na ikiwa watu wa nyumba ni wachache kwa mwana-kondoo, basi yeye na jirani yake aliye karibu na nyumba yake na watwae mwana-kondoo mmoja, kwa kadiri ya hesabu ya watu; kwa kadiri ya ulaji wa kila mtu, ndivyo mtakavyofanya hesabu yenu kwa yule mwana-kondoo.
5 Mwana-kondoo wenu atakuwa hana ila, mume wa mwaka mmoja; mtamtwaa katika kondoo au katika mbuzi.
6 Nanyi mtamweka hata siku ya kumi na nne ya mwezi ule ule; na kusanyiko lote la mkutano wa Israeli watamchinja jioni.
7 Nao watatwaa baadhi ya damu yake na kuitia katika miimo miwili na katika kizingiti cha juu, katika zile nyumba watakazomla.
8 Watakula nyama yake usiku ule ule, imeokwa motoni, pamoja na mkate usiotiwa chachu; tena pamoja na mboga zenye uchungu.
9 Msiile mbichi, wala ya kutokoswa majini, bali imeokwa motoni; kichwa chake pamoja na miguu yake, na nyama zake za ndani.
10 Wala msisaze kitu chake cho chote hata asubuhi, bali kitu kitakachosalia hata asubuhi mtakichoma kwa moto.
11 Tena mtamla hivi; mtakuwa mmefungwa viuno vyenu, mmevaa viatu vyenu miguuni, na fimbo zenu mikononi mwenu; nanyi mtamla kwa haraka; ni pasaka ya Bwana.
12 Maana nitapita kati ya nchi ya Misri usiku huo, nami nitawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri, wa mwanadamu na wa mnyama; nami nitafanya hukumu juu ya miungu yote ya Misri; Mimi ndimi Bwana.
13 Na ile damu itakuwa ishara kwenu katika zile nyumba mtakazokuwamo; nami nitakapoiona ile damu, nitapita juu yenu, lisiwapate pigo lo lote likawaharibu, nitakapoipiga nchi ya Misri.
14 Na siku hii itakuwa ukumbusho kwenu, nanyi mtaifanya iwe sikukuu kwa Bwana; mtaifanya iwe sikukuu katika vizazi vyenu vyote, kwa amri ya milele
15 Mtakula mikate isiyochachwa muda wa siku saba; siku hiyo ya kwanza mtaondoa chachu yote isiwe katika nyumba zenu kabisa; kwa kuwa mtu ye yote atakayekula mkate uliochachwa tangu siku hiyo ya kwanza hata siku ya saba, nafsi hiyo atakatiliwa mbali na Israeli.
16 Siku ya kwanza kutakuwa kwenu na kusanyiko takatifu, na siku ya saba kutakuwa kusanyiko takatifu; haitafanywa kazi yo yote katika siku hizo, isipokuwa kwa hiyo ambayo kila mtu hana budi kula, hiyo tu ifanyike kwenu.
17 Nanyi mtaitunza ile sikukuu ya mikate isiyochachwa; kwa kuwa katika siku iyo hiyo mimi nimeyatoa majeshi yenu katika nchi ya Misri; kwa hiyo mtaitunza siku hiyo katika vizazi vyenu vyote, kwa amri ya milele.
18 Mwezi wa kwanza, siku ya mwezi kumi na nne, wakati wa jioni, mtakula mikate isiyochachwa, hata siku ya mwezi ishirini na moja jioni.
19 Muda wa siku saba isionekane chachu katika nyumba zenu kabisa; kwa kuwa mtu ye yote atakayekula hiyo iliyotiwa chachu, nafsi hiyo atakatiliwa mbali na mkutano wa Israeli, akiwa mwenye kukaa hali ya ugeni, au akiwa mtu aliyezaliwa katika nchi.
20 Msile kitu chochote kilichochachwa; mtakula mikate isiyochachwa katika makao yenu yote.
21 Hapo ndipo Musa akawaita wazee wa Israeli, na kuwaambia, Nendeni, mkajitwalie wana-kondoo kama jamaa zenu zilivyo mkamchinje pasaka.
22 Nanyi twaeni tawi la hisopu, mkalichovye katika ile damu iliyo bakulini na kukipiga kizingiti cha juu, na miimo miwili ya mlango, kwa hiyo damu iliyo katika bakuli; tena mtu ye yote miongoni mwenu asitoke mlangoni mwa nyumba yake hata asubuhi.
23 Kwa kuwa Bwana atapita ili awapige hao Wamisri; na hapo atakapoiona hiyo damu katika kizingiti cha juu, na katika ile miimo miwili, Bwana atapita juu ya mlango, wala hatamwacha mwenye kuharibu aingie nyumbani mwenu kuwapiga ninyi.
24 Nanyi mtalitunza jambo hili kuwa ni amri kwako na kwa wanao milele.
25 Itakuwa hapo mtakapoifikilia hiyo nchi, Bwana atakayowapa, kama alivyoahidi, ndipo mtakapoushika utumishi huu.
26 Kisha itakuwa, hapo watoto wenu watakapowauliza, N'nini maana yake utumishi huu kwenu?
27 Ndipo mtawaambia, Ni dhabihu ya pasaka ya Bwana, kwa kuwa alipita juu ya nyumba za wana wa Israeli huko Misri, hapo alipowapiga Wamisri, akaziokoa nyumba zetu. Hao watu wakainama vichwa na kusujudia.
28 Basi wana wa Israeli wakaenda na kufanya mambo hayo; vile vile kama Bwana alivyowaamuru Musa na Haruni, ndivyo walivyofanya.
29 Hata ikawa, usiku wa manane Bwana akawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri, tangu mzaliwa wa kwanza wa Farao aliyeketi katika kiti chake cha enzi, hata mzaliwa wa kwanza wa mtu aliyefungwa katika nyumba ya wafungwa; na wazaliwa wa kwanza wote wa wanyama.
30 Farao akaondoka usiku, yeye na watumishi wake wote, na Wamisri wote; pakawa na kilio kikuu katika Misri; maana hapakuwa na nyumba hata moja asimokufa mtu.
31 Akawaita Musa na Haruni usiku, akasema, Ondokeni tokeni katika watu wangu, ninyi na wana wa Israeli; enendeni, kamtumikieni Bwana kama mlivyosema.
32 Twaeni kondoo zenu na ng'ombe zenu kama mlivyosema, enendeni zenu, mkanibariki mimi pia.
33 Wamisri nao wakawahimiza watu, kuwatoa katika nchi kwa haraka, maana walisema, Tumekwisha kufa sote.
34 Watu wakauchukua unga wa mikate yao kabla haijatiwa chachu, na vyombo vyao vya kukandia wakavitia ndani ya nguo zao mabegani.
35 Wana wa Israeli wakafanya kama neno lile la Musa; wakataka kwa Wamisri vyombo vya fedha na vyombo vya dhahabu, na mavazi.
36 Bwana akawajalia kupendelewa na Wamisri hata wakawapa kila walichokitaka. Nao wakawateka Wamisri nyara.
37 Wana wa Israeli wakasafiri kutoka Ramesesi mpaka Sukothi, walipata hesabu yao kama watu sita mia elfu watu waume waliokwenda kwa miguu, bila kuhesabu watoto.
38 Na kundi kubwa la watu waliochangamana mno wakakwea pamoja nao; na kondoo na ng'ombe, wanyama wengi sana.
39 Nao wakaoka mikate isiyochachwa ya ule unga waliouchukua walipotoka Misri, maana, haukutiwa chachu, kwa sababu walitolewa watoke Misri, wasiweze kukawia, nao walikuwa hawajajifanyia tayari chakula.
40 Basi wana wa Israeli kukaa kwao, maana, muda waliokaa ndani ya Misri, ulikuwa ni miaka mia nne na thelathini.
41 Ilikuwa mwisho wa miaka hiyo mia nne na thelathini, ilikuwa siku ile ile, ya kwamba majeshi yote ya Bwana yalitoka nchi ya Misri.
42 Ni usiku wa kuangaliwa sana mbele za Bwana kwa sababu ya kuwatoa katika nchi ya Misri; huu ndio usiku wa Bwana, ambao wapasa kuangaliwa sana na wana wa Israeli wote katika vizazi vyao.
43 Bwana akawaambia Musa na Haruni, Amri ya pasaka ni hii; mtu mgeni asimle;
44 lakini mtumishi wa mtu awaye yote aliyenunuliwa kwa fedha, ukiisha kumtahiri, ndipo hapo atamla pasaka.
45 Akaaye kwenu hali ya ugeni, na mtumishi aliyeajiriwa, wasimle pasaka.
46 Na aliwe ndani ya nyumba moja; usiichukue nje ya nyumba nyama yake yo yote; wala msivunje mfupa wake uwao wote.
47 Na wafanye jambo hili mkutano wa Israeli wote.
48 Na mgeni atakapoketi pamoja nawe, na kupenda kumfanyia Bwana pasaka, waume wake wote na watahiriwe, ndipo hapo akaribie na kufanya pasaka; naye atakuwa mfano mmoja na mtu aliyezaliwa katika nchi; lakini mtu ye yote asiyetahiriwa asimle.
49 Sheria ni hiyo moja kwa mtu aliyezaliwa kwenu, na kwa mgeni akaaye kati yenu ugenini.
50 Ndivyo walivyofanya wana wa Israeli wote; kama Bwana alivyowaagiza Musa na Haruni, ndivyo walivyofanya.
51 Ilikuwa siku ile ile moja, Bwana akawatoa wana wa Israeli katika nchi ya Misri kwa majeshi yao.

Kutoka 13


1 Bwana akasema na Musa, akamwambia,
2 Nitakasie mimi wazaliwa wa kwanza wote, kila afunguaye tumbo katika wana wa Israeli, wa binadamu na wa mnyama; ni wangu huyo.
3 Musa akawaambia hao watu, Kumbukeni siku hii, mliyotoka nchi ya Misri, kutoka nyumba ya utumwa; kwa kuwa Bwana aliwatoa mahali hapa kwa nguvu za mkono wake; na usiliwe mkate uliochachwa.
4 Ninyi mwatoka leo katika mwezi wa Abibu.
5 Itakuwa hapo Bwana atakapowaleta mpaka nchi ya Wakanaani, na Wahiti, na Waamori, na Wahivi, na Wayebusi, nchi hiyo aliyowaapia baba zako kwamba atakupa wewe, ni nchi imiminikayo maziwa na asali, ndipo mtakapoushika utumishi huu katika mwezi huu.
6 Mtakula mikate isiyochachwa muda wa siku saba, nayo siku ya saba itakuwa ni sikukuu ya Bwana.
7 Mikate isiyochachwa italiwa katika hizo siku saba; mkate uliotiwa chachu usionekane kwako, wala chachu isionekane kwako, ndani ya mipaka yako yote.
8 Nawe utamwambia mwanao siku hiyo, ukisema, Ni kwa sababu ya hayo Bwana aliyonifanyia hapo nilipotoka Misri.
9 Nayo itakuwa ishara kwako katika mkono wako, na kwa ukumbusho kati ya macho yako, ili kwamba sheria ya Bwana ipate kuwa kinywani mwako; kwani Bwana alikutoa utoke Misri kwa mkono wenye uwezo.
10 Kwa hiyo utaitunza amri hii kwa wakati wake mwaka baada ya mwaka.
11 Itakuwa hapo Bwana atakapokuleta katika nchi ya Wakanaani, kama alivyokuapia wewe na baba zako, na kukupa,
12 ndipo utamwekea Bwana kila afunguaye tumbo, na kila mzaliwa wa kwanza uliye naye, azaliwaye na mnyama; hao waume watakuwa ni wa Bwana.
13 Kila mzaliwa wa kwanza wa punda utamkomboa kwa mwana-kondoo; na kwamba hutaki kumkomboa, utamvunja shingo; na kila mzaliwa wa kwanza wa binadamu katika wanao utamkomboa.
14 Kisha itakuwa hapo mwanao atakapokuuliza keshoni, akisema, Ni nini hivi? Utamwambia, Bwana alimtoa Misri, kutoka ile nyumba ya utumwa, kwa uwezo wa mkono wake;
15 basi ilikuwa hapo Farao alipojifanya kuwa mgumu ili asitupe ruhusa kuondoka, Bwana akawapiga wazaliwa wa kwanza wote waliokuwa katika nchi ya Misri, wa binadamu na wa mnyama; kwa ajili ya hayo namtolea Bwana wote wafunguao tumbo, wakiwa waume; lakini wazaliwa wa kwanza wote wa wana wangu nawakomboa.
16 Jambo hilo litakuwa ni ishara mkononi mwako, na utepe katikati ya macho yako; kwa kuwa Bwana alitutoa Misri kwa uwezo wa mkono wake.
17 Ilikuwa hapo Farao alipokwisha kuwaacha watu hao waende zao, Mungu hakuwaongoza kwa njia ya nchi ya Wafilisti, ijapokuwa ilikuwa ni ya karibu; maana Mungu alisema, Wasije wakaghairi watu hawa hapo watakapokutana na vita, na kurudi Misri;
18 lakini Mungu akawazungusha hao watu kwa njia ya bara kando ya Bahari ya Shamu; wana wa Israeli wakakwea kutoka nchi ya Misri hali wamevaa silaha.
19 Musa akaichukua ile mifupa ya Yusufu pamoja naye; maana, alikuwa amewaapisha sana wana wa Israeli, akisema, Mungu hana budi atawajilia ninyi; nanyi mtaichukua mfupa yangu kutoka hapa pamoja nanyi.
20 Nao wakasafiri kutoka Sukothi, wakapiga kambi Ethamu, kwenye mpaka wa ile jangwa.
21 Bwana naye akawatangulia mchana ndani ya wingu mfano wa nguzo, ili awaongoze njia; na usiku, ndani ya moto mfano wa nguzo, ili kuwapa nuru; wapate kusafiri mchana na usiku;
22 ile nguzo ya wingu haikuondoka mchana, wala ile nguzo ya moto haikuondoka usiku, mbele ya hao watu.

Kutoka 14


1 Bwana akasema na Musa, akamwambia,
2 Waambie wana wa Israeli, kwamba warudi na kupiga kambi yao mbele ya Pi-hahirothi, kati ya Migdoli na bahari, kukabili Baal-sefoni; mtapanga mbele yake karibu na bahari.
3 Naye Farao atasema katika habari za wana wa Israeli, Wametatanishwa katika nchi, ile jangwa imewazuia wasitoke.
4 Nami nitaufanya uwe mgumu moyo wa Farao, naye atafuata nyuma yao; nami nitajipatia utukufu kwa Farao, na kwa jeshi lake lote; na Wamisri watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana. Basi wakafanya hivyo.
5 Mfalme wa Misri aliambiwa ya kuwa wale watu wamekwisha kimbia; na moyo wa Farao, na mioyo ya watumishi wake, iligeuzwa iwe kinyume cha hao watu, nao wakasema, Ni nini jambo hili tulilotenda, kwa kuwaacha Waisraeli waende zao wasitutumikie tena?
6 Akaandalia gari lake, akawachukua watu wake pamoja naye;
7 tena akatwaa magari mia sita yaliyochaguliwa, na magari yote ya Wamisri, na maakida juu ya magari hayo yote.
8 Na Bwana akaufanya moyo wake Farao mfalme wa Misri kuwa mgumu, naye akawafuata wana wa Israeli; kwa sababu wana wa Israeli walitoka kwa ujeuri.
9 Wamisri wakafuata nyuma yao, farasi zote na magari yote ya Farao, na askari zake wenye kupanda farasi, na jeshi lake, nao wakawapata hali wamepanga pale karibu na bahari, karibu na Pi-hahirothi, kukabili Baal-sefoni.
10 Hata Farao alipokaribia, wana wa Israeli wakainua macho yao, na tazama, Wamisri wanakuja nyuma yao; wakaogopa sana; wana wa Israeli wakamlilia Bwana.
11 Wakamwambia Musa, Je! Kwa sababu hapakuwa na makaburi katika Misri umetutoa huko ili tufe jangwani? Mbona umetutendea haya, kututoa katika nchi ya Misri?
12 Neno hili silo tulilokuambia huko Misri, tukisema, Tuache tuwatumikie Wamisri? Maana ni afadhali kuwatumikia Wamisri kuliko kufa jangwani.
13 Musa akawaambia watu, Msiogope, simameni tu, mkauone wokovu wa Bwana atakaowafanyia leo; kwa maana hao Wamisri mliowaona leo hamtawaona tena milele.
14 Bwana atawapigania ninyi, nanyi mtanyamaza kimya.
15 Bwana akamwambia Musa, Mbona unanililia mimi? Waambie wana wa Israeli waendelee mbele.
16 Nawe inua fimbo yako, ukanyoshe mkono wako juu ya bahari, na kuigawanya; nao wana wa Israeli watapita kati ya bahari katika nchi kavu.
17 Nami, tazama, nitaifanya mioyo ya Wamisri kuwa migumu, nao wataingia na kuwafuatia, nami nitajipatia utukufu kwa Farao, na kwa jeshi lake lote, kwa magari yake na kwa wapanda farasi wake.
18 Na Wamisri watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, nitakapokwisha kujipatia utukufu kwa Farao, na magari yake, na farasi zake.
19 Kisha malaika wa Mungu, aliyetangulia mbele ya jeshi la Israeli, akaondoka akaenda nyuma yao; na ile nguzo ya wingu ikaondoka hapo mbele yao, ikasimama nyuma yao;
20 ikafika kati ya jeshi la Misri na jeshi la Israeli; napo palikuwa na lile wingu na lile giza, lakini lilitoa nuru wakati wa usiku; na hawa hawakuwakaribia hawa usiku kucha.
21 Musa; akanyosha mkono wake juu ya bahari; Bwana akaifanya bahari irudi nyuma kwa upepo wa nguvu utokao mashariki, usiku kucha, akaifanya bahari kuwa nchi kavu, maji yakagawanyika.
22 Wana wa Israeli wakaenda ndani kati ya bahari katika nchi kavu; nayo maji yalikuwa ukuta kwao mkono wa kuume, na mkono wa kushoto.
23 Na wale Wamisri wakawafuatia, wakaingia ndani kati ya bahari, farasi zote za Farao, na magari yake, na wapanda farasi wake.
24 Ikawa katika zamu ya alfajiri, Bwana akalichungulia jeshi la Wamisri katika ile nguzo ya moto na ya wingu, akalifadhaisha jeshi la Wamisri.
25 Akayaondoa magurudumu ya magari yao, hata yakaenda kwa uzito; na Wamisri wakasema, Na tukimbie mbele ya Israeli; kwa kuwa Bwana anawapigania, kinyume cha Wamisri.
26 Bwana akamwambia Musa, Nyosha mkono wako juu ya bahari, ili maji yarudi tena juu ya Wamisri, juu ya magari yao, na juu ya farasi zao.
27 Musa akaunyosha mkono wake juu ya bahari, na kulipopambazuka, bahari ikarudi kwa nguvu zake; Wamisri wakakimbia mbele yake; na Bwana akawakukutia mbali hao Wamisri kati ya bahari.
28 Yale maji yakarudi yakafunikiza magari na wapanda farasi, hata jeshi lote la Farao lililoingia katika bahari nyuma yao; hakusalia hata mtu mmoja.
29 Lakini wana wa Israeli wakaenda katika nchi kavu katikati ya bahari; na hayo maji yalikuwa ni kuta upande wao wa kuume, na upande wao wa kushoto.
30 Ndivyo Bwana alivyowaokoa Israeli siku ile mikononi mwa Wamisri; Waisraeli wakawaona Wamisri ufuoni kwa bahari, wamekufa.
31 Israeli akaiona ile kazi kubwa aliyoifanya Bwana juu ya Wamisri, ndipo hao watu wakamcha Bwana, wakamwamini Bwana, na Musa mtumishi wake.

Kutoka 15


1 Ndipo Musa na wana wa Israeli wakamwimbia Bwana wimbo huu wakanena, na kusema, Nitamwimbia Bwana, kwa maana ametukuka sana; Farasi na mpanda farasi amewatupa baharini.
2 Bwana ni nguvu zangu, na wimbo wangu; Naye amekuwa wokovu wangu. Yeye ni Mungu wangu, nami nitamsifu; Ni Mungu wa baba yangu, nami nitamtukuza.
3 Bwana ni mtu wa vita, Bwana ndilo jina lake.
4 Magari ya Farao na jeshi lake amewatupa baharini, Maakida yake wateule wamezama katika bahari ya Shamu.
5 Vilindi vimewafunikiza, Walizama vilindini kama jiwe.
6 Bwana, mkono wako wa kuume umepata fahari ya uwezo, Bwana, mkono wako wa kuume wawaseta-seta adui.
7 Kwa wingi wa ukuu wako wawaangusha chini wanaokuondokea, Wapeleka hasira yako, nayo huwateketeza kama mabua makavu.
8 Kwa upepo wa mianzi ya pua yako maji yalipandishwa, Mawimbi yakasimama juu wima mfano wa chungu, Vilindi vikagandamana ndani ya moyo wa bahari.
9 Adui akasema, Nitafuatia, nitapata, nitagawanya nyara, Nafsi yangu itashibishwa na wao; Nitaufuta upanga wangu, mkono wangu utawaangamiza.
10 Ulivuma kwa upepo wako, bahari ikawafunikiza; Wakazama kama risasi ndani ya maji makuu.
11 Ee Bwana, katika miungu ni nani aliye kama wewe? Ni nani aliye kama wewe, mtukufu katika utakatifu, Mwenye kuogopwa katika sifa zako, mfanya maajabu?
12 Ulinyosha mkono wako wa kuume, Nchi ikawameza.
13 Wewe kwa rehema zako umewaongoza watu uliowakomboa, Kwa uweza wako uliwaelekeza hata makao yako matakatifu.
14 Kabila za watu wamesikia, wanatetemeka, Wakaao Ufilisti utungu umewashika.
15 Ndipo majumbe wa Edomu wakashangaa, Watu wa Moabu wenye nguvu tetemeko limewapata, Watu wote wakaao Kanaani wameyeyuka.
16 Hofu na woga umewaangukia; Kwa uweza wa mkono wako wanakaa kimya kama jiwe; Hata watakapovuka watu wako, Ee Bwana, Hata watakapovuka watu wako uliowanunua.
17 Utawaingiza, na kuwapanda katika mlima wa urithi wako, Mahali pale ulipojifanyia, Ee Bwana, ili upakae, Pale patakatifu ulipopaweka imara, Bwana, kwa mikono yako.
18 Bwana atatawala milele na milele.
19 Kwa maana farasi za Farao na magari yake na wapanda farasi wake waliingia ndani ya bahari, Bwana akayarudisha maji ya bahari juu yao; bali wana wa Israeli walikwenda katika nchi kavu katikati ya bahari.
20 Na Miriamu, nabii mke, ndugu yake Haruni, akatwaa tari mkononi mwake; wanawake wakatoka wote wakaenda nyuma yake, wenye matari na kucheza.
21 Miriamu akawaitikia,Mwimbieni Bwana ,kwa maana ametukuka sana;Farasi na mpanda farasi amewatupa baharini.
22 Musa akawaongoza Israeli waende mbele kutoka Bahari ya Shamu, nao wakatokea kwa jangwa la Shuri; wakaenda safari ya siku tatu jangwani wasione maji.
23 Walipofika mahali palipoitwa Mara hawakupata kuyanywa yale maji ya Mara, kwa kuwa yalikuwa machungu; kwa ajili ya hayo jina lake likaitwa Mara.
24 Ndipo watu wakamnung'unikia Musa, wakisema, Tunywe nini?
25 Naye akamlilia Bwana; Bwana akamwonyesha mti, naye akautia katika hayo maji, maji yakawa matamu. Basi akawawekea amri na hukumu huko, akawaonja huko;
26 akawaambia, Kwamba utaisikiza kwa bidii sauti ya Bwana, Mungu wako, na kuyafanya yaliyoelekea mbele zake, na kutega masikio usikie maagizo yake, na kuzishika amri zake, mimi sitatia juu yako maradhi yo yote niliyowatia Wamisri; kwa kuwa Mimi ndimi Bwana nikuponyaye.
27 Wakafikilia Elimu, palipokuwa na chemchemi kumi na mbili, na mitende sabini; wakapanga hapo, karibu na maji.

Kutoka 16


1 Kisha wakasafiri kutoka Elimu, na mkutano wote wa wana wa Israeli wakafikilia bara ya Sini, iliyoko kati ya Elimu na Sinai, siku ya kumi na tano ya mwezi wa pili baada ya kutoka kwao nchi ya Misri.
2 Na mkutano mzima wa wana wa Israeli ukawanung'unikia Musa na Haruni, huko barani;
3 wana wa Israeli wakawaambia, Laiti tungalikufa kwa mkono wa Bwana katika nchi ya Misri, hapo tulipoketi karibu na zile sufuria za nyama, tulipokula vyakula hata kushiba; kwani mmetutoa huko na kututia katika bara hii, ili kutuua kwa njaa kusanyiko hili lote.
4 Ndipo Bwana akamwambia Musa, Tazama, mimi nitawanyeshea ninyi mvua ya mkate kutoka mbinguni; na hao watu watatoka nje na kuokota kila siku sehemu ya siku; ili nipate kuwajaribu, kwamba watakwenda katika sheria yangu, ama sivyo.
5 Kisha itakuwa siku ya sita, ya kwamba watayaandaa hayo watakayoleta ndani, nayo yatakuwa ni mara mbili kuliko wayaokotayo kila siku.
6 Musa na Haruni wakawaambia wana wote wa Israeli, Jioni ndipo mtakapojua ya kuwa Bwana amewaleta kutoka nchi ya Misri;
7 na asubuhi ndipo mtakapouona utukufu wa Bwana; kwa kuwa yeye asikia manung'uniko yenu mliyomnung'unikia Bwana; na sisi tu nani, hata mkatunung'unikia?
8 Musa akasema, Ndilo litakalokuwa, hapo Bwana atakapowapa nyama wakati wa jioni mle, na asubuhi mikate hata mkakinai; kwa kuwa Bwana asikia manung'uniko yenu mliyomnung'unikia yeye; na sisi tu nani? Manung'uniko yenu hayakuwa juu yetu sisi, ila juu ya Bwana.
9 Musa akamwambia Haruni, Haya, sema na mkutano wote wa wana wa Israeli, Njoni karibu mbele ya Bwana; kwa kuwa yeye ameyasikia manung'uniko yenu.
10 Ilikuwa Haruni aliponena na huo mkutano wote wa wana wa Israeli, wakaangalia upande wa bara, na tazama, utukufu wa Bwana ukaonekana katika hilo wingu.
11 Bwana akasema na Musa, akinena,
12 Nimeyasikia manung'uniko ya wana wa Israeli; haya sema nao, ukinena, Wakati wa jioni mtakula nyama, na wakati wa asubuhi mtashiba mkate; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.
13 Ikawa wakati wa jioni, kware wakakaribia, wakakifunikiza kituo; na wakati wa asubuhi umande ulikuwa juu ya nchi pande zote za kituo.
14 Na ulipoinuka ule umande uliokuwa juu ya nchi, kumbe! Juu ya uso wa bara kitu kidogo kilichoviringana, kidogo kama sakitu juu ya nchi.
15 Wana wa Israeli walipokiona, wakaambiana, Nini hiki? Maana hawakujua ni kitu gani. Musa akawaambia, Ndio mkate ambao Bwana amewapa ninyi, mle.
16 Neno hili ndilo aliloagiza Bwana, Okoteni ninyi kitu hicho kila mtu kama ulaji wake ulivyo; kichwa pishi,kama hesabu ya watu wenu ilivyo ;ndivyo mtakavyotwaa,kila mtu kwa ajili ya hao walioko hemani mwake.
17 Wana wa Israeli wakafanya hivyo, wakaokota wengine zaidi, wengine kupungua.
18 Nao walipoipima kwa pishi, yeye aliyekuwa ameokota kingi hakubakiwa na kitu, na yeye aliyekuwa ameokota kichache hakupungukiwa; wakaokota kila mtu kama ulaji wake ulivyokuwa.
19 Musa akawaambia, Mtu awaye yote asikisaze hata asubuhi.
20 Lakini hawakumsikiza Musa; wengine miongoni mwao wakakisaza hata asubuhi, nacho kikaingia mabuu na kutoa uvundo; Musa akawakasirikia sana.
21 Basi wakaokota asubuhi baada ya asubuhi, kila mtu kama ulaji wake ulivyokuwa; na hapo jua lilipokuwa ni kali, kikayeyuka.
22 Basi ikawa siku ya sita wakaokota kile chakula sehemu maradufu, kila mtu pishi mbili; na wazee wote wa mkutano wakaenda na kumwambia Musa.
23 Akawaambia, Ndilo neno alilonena Bwana Kesho ni starehe takatifu, Sabato takatifu kwa Bwana; okeni mtakachooka, na kutokosa mtakachotokosa; na hicho kitakachowasalia jiwekeeni kilindwe hata asubuhi.
24 Basi wakakiweka hata asubuhi, kama Musa alivyowaagiza; nacho hakikutoa uvundo wala kuingia mabuu.
25 Musa akasema, Haya, kuleni hiki leo; kwa kuwa leo ni Sabato ya Bwana; leo hamtakiona nje barani.
26 Siku sita mtaokota; lakini siku ya saba ni Sabato, siku hiyo hakitapatikana.
27 Ikawa siku ya saba wengine wakatoka kwenda kukiokota, wasikione.
28 Bwana akamwambia Musa, Mtakataa kuyashika maagizo yangu na sheria zangu hata lini?
29 Angalieni, kwa kuwa Bwana amewapa ninyi hiyo Sabato, kwa sababu hii huwapa siku ya sita chakula cha siku mbili; kaeni kila mtu mahali pake, mtu awaye yote asiondoke mahali pake kwa siku ya saba.
30 Basi hao watu wakapumzika kwa siku ya saba.
31 Na nyumba ya Israeli wakakiita jina lake Mana; nacho kilikuwa mfano wa chembe za mtama, nyeupe; na tamu yake ilikuwa kama tamu ya maandazi membamba yaliyoandaliwa kwa asali.
32 Musa akasema, Hili ni neno Bwana aliloliamuru, Pishi moja ya kitu hicho na kiwekwe kwa ajili ya vizazi vyenu; ili kwamba wao wapate kukiona kile chakula nilichowalisha ninyi barani, hapo nilipowaleta kutoka nchi ya Misri.
33 Basi Musa akamwambia Haruni, Twaa kopo, ukatie pishi moja ya hiyo Mana ndani yake, uiweke mbele ya Bwana, ilindwe kwa ajili ya vizazi vyenu.
34 Kama vile Bwana alivyomwagizia Musa ndivyo Haruni alivyoiweka hapo mbele ya Ushahidi, ili ilindwe.
35 Na wana wa Israeli walikula Mana muda wa miaka arobaini, hata walipofikilia nchi iliyo na watu, wakala ile Mana, hata walipofikilia mipakani mwa nchi ya Kanaani.
36 Hiyo omeri ni sehemu kumi ya efa.

Kutoka 17


1 Mkutano wote wa wana wa Israeli ukasafiri, kutoka bara ya Sini kwa safari zao, kama Bwana alivyowaagiza, wakatua Refidimu; napo hapakuwa na maji, watu wanywe.
2 Kwa hiyo hao watu wakateta na Musa, wakasema, Tupe maji tunywe. Musa akawaambia, Kwani kuteta na mimi? Mbona mnamjaribu Bwana?
3 Watu wakawa na kiu huko; nao wakamnung'unikia Musa, wakasema, Mbona umetupandisha kutoka Misri, kutuua sisi na watoto wetu na wanyama wetu kwa kiu?
4 Musa akamlilia Bwana, akisema, Niwatendee nini watu hawa? Bado kidogo nao watanipiga kwa mawe.
5 Bwana akamwambia Musa, Pita mbele ya watu, ukawachukue baadhi ya wazee wa Israeli pamoja nawe; na ile fimbo yako ambayo uliupiga mto kwayo, uitwae mkononi mwako, ukaende.
6 Tazama, nitasimama mbele yako huko, juu ya lile jabali katika Horebu; nawe utalipiga jabali, na maji yatatoka, watu wapate kunywa. Musa akafanya hivyo mbele ya wazee wa Israeli.
7 Akapaita mahali pale jina lake Masa, na Meriba; kwa sababu ya mateto ya wana wa Israeli, na kwa sababu walimjaribu Bwana, wakisema, Je! Bwana yu kati yetu au sivyo?
8 Wakati huo Waamaleki wakatokea, wakapigana na Israeli huko Refidimu.
9 Musa akamwambia Yoshua, Tuchagulie watu, ukatoke upigane na Waamaleki; kesho nitasimama juu ya kilele kile, na ile fimbo ya Mungu nitakuwa nayo mkononi mwangu.
10 Basi Yoshua akafanya kama Musa alivyomwambia, akapigana na Amaleki; na Musa na Haruni na Huri wakapanda juu ya kile kilima.
11 Ikawa, Musa alipouinua mkono wake, Israeli walishinda; na alipoushusha mkono wake, Amaleki walishinda.
12 Lakini mikono ya Musa ilikuwa mizito; basi wakatwaa jiwe, wakaliweka chini yake akalikalia. Haruni na Huri wakaitegemeza mikono yake, mmoja upande huu na mmoja upande huu; mikono yake ikathibitika hata jua lilipokuchwa.
13 Yoshua akawaangamiza Amaleki na watu wake kwa ukali wa upanga.
14 Bwana akamwambia Musa, Andika habari hii katika kitabu iwe ukumbusho, kisha ihubiri masikioni mwa Yoshua; ya kuwa nitaufuta ukumbusho wa Amaleki kabisa, usiwe tena chini ya mbingu.
15 Musa akajenga madhabahu, akaiita jina lake Yehova-nisi;
16 akasema, Bwana ameapa; Bwana atakuwa na vita na Amaleki kizazi baada ya kizazi.

Kutoka 18


1 Basi Yethro, kuhani wa Midiani, mkwewe Musa, alisikia habari ya mambo hayo yote Mungu aliyokuwa amemtendea Musa, na Waisraeli watu wake, jinsi Bwana alivyowaleta Israeli watoke Misri.
2 Ndipo Yethro mkwewe Musa akamtwaa Sipora, mke wa Musa, baada ya yeye kumrudisha,
3 pamoja na wanawe wawili; katika hao, jina la mmoja ni Gershomu, maana alisema, Mimi nimekuwa mgeni katika nchi ya ugenini;
4 na jina la wa pili ni Eliezeri, kwa kuwa alisema, Yeye Mungu wa baba yangu alikuwa msaada wangu, akaniokoa na upanga wa Farao.
5 Basi Yethro, mkwewe Musa, pamoja na mke wa Musa na wanawe wawili wakamwendea Musa huko nyikani, hapo alipokuwa amepanga, kwenye mlima wa Mungu;
6 naye akamwambia Musa, Mimi Yethro mkweo nimekuja kwako, na mkeo, na wanawe wawili pamoja naye.
7 Basi Musa akatoka nje ili amlaki mkwewe, akasujudia na kumbusu; nao wakaulizana habari; kisha wakaingia hemani.
8 Musa akamwambia mkwewe mambo hayo yote Bwana aliyomtenda Farao na Wamisri kwa ajili ya Israeli, na mambo mazito yote yaliyowapata njiani, na jinsi Bwana alivyowaokoa.
9 Yethro alifurahi kwa ajili ya wema wote Bwana aliowatendea Israeli, kwa alivyo waokoa mikononi mwa Wamisri.
10 Kisha Yethro akasema, Na ahimidiwe Bwana aliyewaokoa na mikono ya Wamisri, na mkono wa Farao; aliyewaokoa watu hao watoke mikononi mwa Wamisri.
11 Sasa najua ya kuwa Bwana ni mkuu kuliko miungu yote; naam, katika jambo hilo walilowatenda kwa unyeti.
12 Yethro mkwewe Musa akamletea Mungu sadaka ya kuteketezwa na dhabihu; na Haruni akaja, na wazee wote wa Israeli, wale chakula pamoja na mkwewe Musa mbele za Mungu.
13 Asubuhi yake Musa akaketi ili awapishie hukumu watu; na hao watu wakasimama kumzunguka Musa tangu asubuhi hata jioni.
14 Mkwewe Musa alipoyaona yote aliyowafanyia watu, akasema, Ni jambo gani hili uwatendealo hao watu? Kwani wewe kuketi hapo peke yako, na watu wote kusimama kwako tangu asubuhi hata jioni?
15 Musa akamwambia mkwewe, Ni kwa sababu watu hunijilia mimi wapate kumwuliza Mungu;
16 wakiwa na neno, hunijilia; nami naamua kati ya mtu na mwenziwe, nami nawajuvisha amri za Mungu, na sheria zake.
17 Mkwewe Musa akamwambia, Jambo hili ufanyalo si jema.
18 Huna budi utadhoofika wewe, na hawa watu walio pamoja nawe pia; maana jambo hili ni zito mno kwako; huwezi wewe kulitenda peke yako.
19 Sikiza sasa neno langu, nitakupa shauri, na Mungu na awe pamoja nawe; uwe wewe kwa ajili ya watu mbele ya Mungu, nawe umletee Mungu maneno yao;
20 nawe utawafundisha zile amri na sheria, nawe utawaonyesha njia ambayo inawapasa kuiendea, na kazi ambayo inawapasa kuifanya.
21 Zaidi ya hayo utajipatia katika watu hawa watu walio na uwezo, wenye kumcha Mungu, watu wa kweli, wenye kuchukia mapato ya udhalimu; ukawaweka juu yao, wawe wakuu wa maelfu, na wakuu wa mia, na wakuu wa hamsini, na wakuu wa kumi;
22 nao wawaamue watu hawa sikuzote; kisha, kila neno lililo kubwa watakuletea wewe, lakini kila neno dogo wataliamua wenyewe; basi kwako wewe mwenyewe utapata nafasi zaidi, nao watauchukua huo mzigo pamoja nawe.
23 Kwamba utafanya jambo hili, na Mungu akikuagiza hivyo, basi utaweza kusimama wewe, na watu hawa wote nao watakwenda mahali pao kwa amani.
24 Basi Musa akasikiza neno la mkwewe, akayafanya yote aliyokuwa amemwambia.
25 Musa akawachagua watu wenye uwezo katika Israeli yote, akawaweka wawe vichwa juu ya watu, wakuu wa maelfu, na wakuu wa mia, na wakuu wa hamsini, na wakuu wa kumi.
26 Nao wakawaamua watu sikuzote; mashauri magumu wakamletea Musa, lakini kila neno dogo wakaliamua wenyewe.
27 Kisha Musa akaagana na mkwewe; naye akaenda zake, mpaka nchi yake mwenyewe.

Kutoka 19


1 Mwezi wa tatu baada ya kutoka Waisraeli katika nchi ya Misri, siku iyo hiyo wakafika jangwa la Sinai.
2 Nao walipokuwa wameondoka Refidimu na kufika jangwa la Sinai, wakatua katika lile jangwa; Israeli wakapiga kambi huko wakiukabili mlima.
3 Musa akapanda kwa Mungu, na Bwana akamwita toka mlima ule, akisema, Utawaambia nyumba ya Yakobo, na kuwaarifu wana wa Israeli, maneno haya;
4 Mmeona jinsi nilivyowatendea Wamisri, na jinsi nilivyowachukua ninyi juu ya mbawa za tai, nikawaleta ninyi kwangu mimi.
5 Sasa basi ikiwa mtaitii sauti yangu kweli kweli, na kulishika agano langu, hapo ndipo mtakapokuwa tunu kwangu kuliko makabila yote ya watu; maana dunia yote pia ni mali yangu,
6 nanyi mtakuwa kwangu ufalme wa makuhani, na taifa takatifu. Hayo ndiyo maneno utakayowaambia wana wa Israeli.
7 Musa akaenda akawaita wazee wa watu, akawafunulia maneno hayo yote, Bwana aliyokuwa amemwagiza.
8 Watu wote wakaitika pamoja wakisema, Hayo yote aliyoyasema Bwana tutayatenda. Naye Musa akamwambia Bwana maneno ya hao watu.
9 Bwana akamwambia Musa, Tazama, mimi naja kwako katika wingu zito ili watu hawa wasikie nitakaposema nawe, nao wapate kukuamini wewe nawe hata milele. Musa akamwambia Bwana hayo maneno ya watu.
10 Bwana akamwambia Musa, Enenda kwa watu hawa, ukawatakase leo na kesho, wakazifue nguo zao,
11 wawe tayari kwa siku ya tatu; maana siku ya tatu Bwana atashuka katika mlima wa Sinai machoni pa watu hawa wote.
12 Nawe utawawekea mipaka watu hawa pande zote, ukisema, Jihadharini, msipande mlima huu, wala msiuguse, hata mapambizo yake; kila mtu atakayeugusa mlima huu, bila shaka atauawa.
13 Mkono wa mtu awaye yote usimguse mtu huyo, ila hakika yake atapigwa kwa mawe, au kupigwa kwa mkuki; kwamba ni mnyama au kwamba ni mwanadamu, hataishi. Hapo panda itakapotoa sauti kwa kufuliza ndipo watakapoukaribia mlima.
14 Musa akatelemka mlimani akawaendea watu akawatakasa, nao wakafua nguo zao.
15 Akawaambia watu; Mwe tayari siku ya tatu; msimkaribie mwanamke.
16 Ikawa siku ya tatu, wakati wa asubuhi, palikuwa na ngurumo na umeme, na wingu zito juu ya mlima, na sauti ya baragumu iliyolia sana. Watu wote waliokuwa kituoni wakatetemeka.
17 Musa akawatoa hao watu katika kituo, akawaleta ili waonane na Mungu; wakasimama pande za chini za kile kilima.
18 Mlima wa Sinai wote pia ukatoa moshi, kwa sababu Bwana alishuka katika moto; na ule moshi wake ukapanda juu kama moshi wa tanuu, mlima wote ukatetemeka sana.
19 Na hapo sauti ya baragumu ilipozidi kulia sana, Musa akanena, naye Mungu akamwitikia kwa sauti.
20 Bwana akaushukia mlima, juu ya kilele cha mlima; Bwana akamwita Musa aende hata kilele cha mlima; Musa akapanda juu.
21 Ndipo Bwana akamwambia Musa, Shuka chini, uwaonye watu wasije wakapasua njia waje kwa Bwana kutazama, kisha wengi miongoni mwao wakaangamia.
22 Makuhani nao, wamkaribiao Bwana, na wajitakase, Bwana asije akawafurikia.
23 Musa akamwambia Bwana, Watu hawa hawawezi kuukaribia mlima wa Sinai; kwa kuwa wewe ulituusia, ukisema, Wekeni mipaka kando-kando ya mlima, na kuutenga.
24 Bwana akamwambia, Nenda, ushuke wewe; nawe utakwea, wewe, na Haruni pamoja nawe; lakini wale makuhani na watu wasipenye kumkaribia Bwana, asije yeye akawafurikia juu yao.
25 Basi Musa akawatelemkia hao watu na kuwaambia hayo.

Kutoka 20


1 Mungu akanena maneno haya yote akasema,
2 Mimi ni Bwana, Mungu wako, niliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa.
3 Usiwe na miungu mingine ila mimi.
4 Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia.
5 Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi, Bwana, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu; nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao,
6 nami nawarehemu maelfu elfu wanipendao, na kuzishika amri zangu.
7 Usilitaje bure jina la Bwana, Mungu wako, maana Bwana hatamhesabia kuwa hana hatia mtu alitajaye jina lake bure.
8 Ikumbuke siku ya Sabato uitakase.
9 Siku sita fanya kazi, utende mambo yako yote;
10 lakini siku ya saba ni Sabato ya Bwana, Mungu wako, siku hiyo usifanye kazi yo yote, wewe, wala mwana wako, wala binti yako, wala mtumwa wako, wala mjakazi wako, wala mnyama wako wa kufuga, wala mgeni aliye ndani ya malango yako.
11 Maana, kwa siku sita Bwana alifanya mbingu, na nchi, na bahari, na vyote vilivyomo, akastarehe siku ya saba; kwa hiyo Bwana akaibarikia siku ya Sabato akaitakasa.
12 Waheshimu baba yako na mama yako; siku zako zipate kuwa nyingi katika nchi upewayo na Bwana, Mungu wako.
13 Usiue.
14 Usizini.
15 Usiibe.
16 Usimshuhudie jirani yako uongo.
17 Usiitamani nyumba ya jirani yako, usimtamani mke wa jirani yako; wala mtumwa wake, wala mjakazi wake, wala ng'ombe wake, wala punda wake, wala cho chote alicho nacho jirani yako.
18 Watu wote wakaona umeme na ngurumo na sauti ya baragumu, na ule mlima kutoka moshi; na watu walipoona hayo wakatetemeka, wakasimama mbali.
19 Wakamwambia Musa, Sema nasi wewe, nasi tutasikia, bali Mungu asiseme nasi, tusije tukafa.
20 Musa akawaambia watu, Msiogope, maana Mungu amekuja ili awajaribu, na utisho wake uwe mbele yenu, ili kwamba msifanye dhambi.
21 Basi hao watu wakasimama mbali, naye Musa akalikaribia lile giza kuu Mungu alipokuwapo.
22 Bwana akamwambia Musa, Waambie wana wa Israeli hivi, Ninyi wenyewe mmeona ya kuwa nimenena nanyi kutoka mbinguni.
23 Msifanye miungu mingine pamoja nami; miungu ya fedha, wala miungu ya dhahabu, msijifanyie.
24 Utanifanyia madhabahu ya udongo, nawe utatoa dhabihu zako juu yake; sadaka za kuteketezwa, na sadaka za amani, kondoo zako, na ng'ombe zako, kila mahali nitakapotia ukumbusho wa jina langu, hapo ndipo nitakapokujilia na kukubarikia.
25 Nawe ukinifanyia madhabahu ya mawe, hutaijenga ya mawe yaliyochongwa; kwa kuwa ukiwa wewe umetumia chombo chako katika kuichonga umeitia unajisi.
26 Tena hutapanda kwenda madhabahuni kwangu kwa daraja, uchi wako usidhihirike juu yake.

Kutoka 21


1 Basi hukumu utakazoziweka mbele ya watu ni hizi
2 Ukimnunua mtumwa wa Kiebrania, atakutumikia muda wa miaka sita; mwaka wa saba atatoka kwako huru bure.
3 Kwamba aliingia kwako peke yake tu, atatoka hivyo peke yake; kwamba ameoa, mkewe atatoka aende pamoja naye.
4 Kwamba ni bwana wake aliyempa huyo mke, naye amemzalia wana, wa kiume au wa kike; yule mke na wanawe watakuwa ni mali ya bwana wake, naye mume atatoka peke yake.
5 Lakini huyo mtumwa akisema waziwazi, Mimi nampenda bwana wangu, na mke wangu na watoto wangu; sitaki mimi kutoka niwe huru;
6 ndipo hapo huyo bwana wake atamleta mbele ya Mungu na kumleta mlangoni, au penye mwimo wa mlango; na bwana wake atalitoboa sikio lake kwa uma; ndipo atamtumikia sikuzote.
7 Mtu akimwuza binti yake awe kijakazi, hatatoka yeye kama watumwa wa kiume watokavyo.
8 Kwamba bwana wake hakupendezewa naye, akiwa amemposa, ndipo atakubali akombolewe; hana amri yeye kumwuza aende kwa watu wageni maana amemtenda kwa udanganyifu.
9 Kwamba amposa mwanawe, atamtendea kama desturi zipasazo binti zake.
10 Kwamba ajitwalia mke mwingine, chakula chake huyo, na nguo zake, na ngono yake, hatampunguzia.
11 Kwamba hamfanyii mambo haya matatu, ndipo atatoka aende bure, pasipo kutolewa mali.
12 Mtu awaye yote ampigaye mtu, hata akafa, hana budi atauawa huyo.
13 Lakini kama hakumvizia, ila Mungu amemtia mkononi mwake; basi nitakuonyesha mahali atakapopakimbilia.
14 Lakini, mtu akimwendea mwenziwe kwa kujikinai, kusudi apate kumwua kwa hila; huyo utamwondoa hata madhabahuni pangu, auawe.
15 Ampigaye baba yake au mama yake, sharti atauawa.
16 Yeye amwibaye mtu, na kumwuza, au akipatikana mkononi mwake, sharti atauawa huyo
17 Yeye amwapizaye baba yake au mama yake, sharti atauawa.
18 Watu wakigombana, na mmoja akimpiga mwenziwe kwa jiwe, au kwa konde, asife, lakini yualazwa kitandani mwake;
19 atakapoinuka tena na kuenenda nje kwa kutegemea fimbo, ndipo hapo yule aliyempiga ataachwa; ila atamlipa kwa ajili ya hayo majira yake yaliyompotea, naye atamwuguza hata apone kabisa.
20 Mtu akimpiga mtumwa wake, au kijakazi chake, kwa fimbo, naye akifa mkononi mwake, hana budi ataadhibiwa.
21 Lakini akipona siku moja au mbili hataadhibiwa; maana, ni mali yake.
22 Watu waume wakiteta pamoja, wakamwumiza mwanamke mwenye mimba hata akaharibu mimba, tena yasiwe madhara zaidi; sharti atatozwa mali kama atakavyomwandikia mumewe huyo mwanamke; atalipa kama hao waamuzi watakavyosema.
23 Lakini kwamba pana madhara zaidi, ndipo utatoza uhai kwa uhai,
24 jicho kwa jicho, jino kwa jino, mkono kwa mkono, mguu kwa mguu,
25 kuteketeza kwa kuteketeza, jeraha kwa jeraha, chubuko kwa ajili ya chubuko.
26 Mtu akimpiga mtumwa wake jicho, au jicho la kijakazi chake, na kuliharibu; atamwacha huru kwa ajili ya jicho lake.
27 Au akimpiga mtumwa wake jino likang'oka, au jino la kijakazi chake, atamwacha huru kwa ajili ya jino lake.
28 Ng'ombe akipiga pembe mtu mume au mtu mke, nao wakafa, huyo ng'ombe atauawa kwa kupigwa kwa mawe, nyama yake isiliwe; lakini mwenye huyo ng'ombe ataachiliwa.
29 Lakini kwamba huyo ng'ombe alizoea kupiga watu tangu hapo, naye mwenyewe ameonyeshwa jambo hilo, wala asimzuie, naye amemwua mtu mume au mwanamke; huyo ng'ombe atauawa kwa kupigwa kwa mawe, na huyo mwenyewe naye atauawa.
30 Lakini akiandikiwa ukombozi, ndipo atakapotoa kwa ajili ya uhai wake hicho atakachoandikiwa.
31 Akiwa ng'ombe amempiga pembe mtoto wa kiume na kumtumbua, au akiwa amempiga mtoto wa kike, atatendwa kama hukumu hiyo.
32 Ng'ombe akimtumbua mtumwa mume au kijakazi; mwenye ng'ombe atampa bwana wao shekeli thelathini za fedha, naye ng'ombe atauawa kwa kupigwa kwa mawe.
33 Kwamba mtu atafunua shimo, au kuchimba shimo, naye asilifunike, kisha ikawa ng'ombe au punda kutumbukia humo,
34 mwenye shimo atalipa; atampa huyo mwenye mnyama fedha, na mnyama aliyekufa atakuwa ni wake.
35 Ng'ombe wa mtu akimwumiza ng'ombe wa mtu mwingine hata akafa; ndipo watamwuza huyo ng'ombe aliye hai na kugawanya thamani yake; na ng'ombe aliyekufa pia watamgawanya.
36 Au kwamba ilijulikana ya kuwa ng'ombe tangu hapo amezoea kupiga kwa pembe, wala mwenyewe asimzuie; ndipo atakapolipa yeye, ng'ombe kwa ng'ombe, na huyo ng'ombe aliyekufa atakuwa ni wake.

Kutoka 22


1 Mtu akiiba ng'ombe au kondoo, na kumchinja, au kumwuza; atalipa ng'ombe watano badala ya ng'ombe mmoja, na kondoo wanne badala ya kondoo mmoja.
2 Mwivi akipatikana akiwa yu hali ya kuvunja mahali, naye akapigwa hata akafa, hapatakuwa na malipizo ya damu kwa ajili yake.
3 Lakini kama jua limekucha juu yake, ndipo patakuwa na malipizo ya damu kwa ajili yake; ingempasa kutoa malipo kamili; akiwa hana kitu, na auzwe kwa ajili ya wivi wake.
4 Kama hicho kitu kilichoibwa chapatikana hai mkononi mwake, kama ni ng'ombe, au punda, au kondoo; atalipa thamani yake mara mbili.
5 Mtu akilisha katika shamba, au shamba la mizabibu, akimwacha mnyama wake, akala katika shamba la mtu mwingine; atalipa katika vitu vilivyo vizuri vya shamba lake mwenyewe, au vya mizabibu yake.
6 Ukiwaka moto, na kushika penye miiba, na ngano zilizofungwa miganda, au ngano ambazo hazijakatwa, au shamba, likateketea; yeye aliyeuwasha huo moto lazima atalipa.
7 Mtu akimpa mwenziwe amana ya fedha au vitu vingine amtunzie, na vitu vile vikaibwa katika nyumba ya mtu huyo; mwivi akipatikana, atalipa thamani yake mara mbili.
8 Mwivi asipopatikana, ndipo mwenye nyumba atakaribia mbele ya Mungu, ionekane kwamba si yeye aliyetia mkono na kutwaa vyombo vya mwenziwe.
9 Kila jambo la kukosana, kama ni la ng'ombe, au la punda, au la kondoo, au la mavazi, au la kitu cho chote kilichopotea, ambacho mtu mmoja asema ni chake, hilo jambo la watu wote wawili litaletwa mbele ya Mungu; na yeye atakayehukumiwa na Mungu kuwa ni mkosa atamlipa mwenziwe thamani yake mara mbili.
10 Mtu akimpa mwenziwe punda, au ng'ombe, au kondoo, au mnyama ye yote, ili amtunzie; yule mnyama akafa, au akaumia, au akachukuliwa mtu asione;
11 patakuwa na kiapo cha Bwana katikati ya watu hao wawili, kwamba alipeleka mkono wake kutwaa mali ya mwenziwe, na mwenyewe atakubali hayo, wala hatalipa.
12 Lakini kwamba aliibiwa mnyama huyo, sharti amlipe yule mwenyewe.
13 Kwamba aliraruliwa na mnyama mkali, na amlete uwe ushahidi; hatalipa kwa ajili ya mnyama aliyeraruliwa.
14 Mtu akiazima mnyama kwa mwenziwe, naye akaumia huyo mnyama, au akafa, mwenyewe asipokuwapo, lazima atalipa.
15 Kama huyo mwenyewe alikuwapo pamoja na mnyama wake, hatalipa; kama ni mnyama aliyeajiriwa, alikwenda kwa ajili ya ujira wake.
16 Mtu akimshawishi mwanamwali, aliyeposwa na mume, na kulala naye, lazima atatoa mahari kwa ajili yake ili awe mkewe.
17 Ikiwa baba yake huyo mwanamwali akataa kabisa kumpa, atalipa fedha kama hesabu ya mahari ya mwanamwali ilivyo.
18 Usimwache mwanamke mchawi kuishi.
19 Mtu awaye yote alalaye na mnyama sharti atauawa.
20 Mtu atakayemchinjia sadaka mungu ye yote, isipokuwa ni yeye Bwana peke yake, na angamizwe kabisa.
21 Usimwonee mgeni, wala kumtendea jeuri; kwa kuwa ninyi mlikuwa wageni katika nchi ya Misri.
22 Usimtese mjane ye yote aliyefiwa na mumewe, wala mtoto yatima.
23 Ukiwatesa watu hao katika neno lo lote, nao wakanililia mimi, hakika yangu nitasikia kilio chao,
24 na hasira yangu itawaka moto, nami nitawaua ninyi kwa upanga; na wake wenu watakuwa wajane, na watoto wenu mayatima.
25 Ukimkopesha mtu aliye maskini, katika watu wangu walio pamoja nawe; usiwe kwake mfano wa mwenye kumdai; wala hutamwandikia faida.
26 Ikiwa wewe kwa njia yo yote wapokea nguo ya jirani yako rehani, lazima utamrudishia mbele ya jua kuchwa;
27 maana hiyo nguo ni kifuniko chake, hiyo peke yake ni nguo ya ngozi yake; je! Atalalia nini? Itakuwa, hapo atakaponililia mimi, nitasikia; kwa kuwa mimi ni mwenye rehema.
28 Usimtukane Mungu, wala usimlaani mkuu wa watu wako.
29 Usikawie kuleta malimbuko ya matunda yako na ya vinywaji vyako. Mzaliwa wa kwanza katika wanao waume utanipa mimi.
30 Nawe utafanya vivyo katika ng'ombe zako, na kondoo zako; utamwacha siku saba pamoja na mama yake; siku ya nane utanipa mimi.
31 Nanyi mtakuwa watu watakatifu kwangu mimi; kwa hiyo msiile nyama yo yote iliyoraruliwa huko kondeni na mnyama wa mwitu; mtawatupia mbwa nyama hiyo.

Kutoka 23


1 Usivumishe habari za uongo; usitie mkono wako pamoja na mwovu, kuwa shahidi wa udhalimu.
2 Usiandamane na mkutano kutenda uovu; wala usitie ushahidi wako katika neno lo lote kwa kugeukia kando na kuandamana na mkutano ili kupotoa hukumu;
3 wala usimpendelee mtu mnyonge katika neno lake.
4 Ukimwona ng'ombe wa adui wako, au punda wake, amepotea, sharti umrudishie mwenyewe tena.
5 Ukimwona punda wake huyo akuchukiaye hali ameanguka chini ya mzigo wake, nawe ungejizuia usimsaidie, lazima umsaidie.
6 Usipotoe hukumu ya mtu maskini katika neno lake.
7 Jitenge mbali na neno uongo; wala wasio hatia na wenye haki usiwaue; kwa kuwa mimi sitamhesabia haki yeye aliye mwovu.
8 Nawe usipokee rushwa; kwani hiyo rushwa huwapofusha macho hao waonao, na kuyapotoa maneno ya wenye haki.
9 Usimwonee mgeni; maana, ninyi mwajua moyo wa mgeni ulivyo, kwa kuwa ninyi mlikuwa wageni katika nchi ya Misri.
10 Utapanda mbegu katika nchi yako muda wa miaka sita na kuyavuna maongeo yake;
11 lakini mwaka wa saba utaiacha nchi ipumzike na kutulia; hao maskini miongoni mwa watu wako wapate kula; na hicho watakachosaza wao, wapate kula wanyama wa kondeni. Utafanya vivyo katika shamba lako la mizabibu, na katika shamba lako la mizeituni.
12 Siku sita utafanya kazi yako, na siku ya saba utapumzika; ili kwamba ng'ombe wako na punda wako wapate kupumzika, kisha mwana wa mjakazi wako na mgeni wapate kuburudika.
13 Yaangalieni hayo yote niliyowaambia; wala msitaje kabisa majina ya miungu mingine, wala yasisikizwe kutoka kinywani mwako.
14 Mara tatu kila mwaka utaniwekea sikukuu.
15 Utaiweka sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu; utakula mikate isiyochachwa muda wa siku saba kama nilivyokuagiza, kwa wakati uliowekwa, mwezi wa Abibu (kwa maana ndio mwezi uliotoka Misri); wala hapana mtu atakayeonekana mbele yangu na mikono mitupu;
16 tena, sikukuu ya mavuno, hayo malimbuko ya kazi zako za kupanda mashambani; tena, sikukuu ya kukusanya, mwisho wa mwaka, hapo utakapokusanya hayo uliyoyataabikia shambani.
17 Mara tatu katika mwaka watu waume wako wote watahudhuria mbele ya Bwana MUNGU.
18 Usisongeze damu ya dhabihu zangu pamoja na mkate uliotiwa chachu, wala mafuta ya sikukuu yangu usiyaache kusalia hata asubuhi.
19 Ya kwanza ya malimbuko ya nchi yako utayaleta na kuyatia ndani ya nyumba ya Bwana, Mungu wako. Usimtokose mwana-mbuzi katika maziwa ya mama yake.
20 Tazama, mimi namtuma malaika aende mbele yako, ili akulinde njiani na kukupeleka mpaka mahali pale nilipokutengezea.
21 Jitunzeni mbele yake, mwisikize sauti yake; wala msimtie kasirani; maana, hatawasamehe makosa yenu; kwa kuwa jina langu limo ndani yake.
22 Lakini ukiisikiza sauti yake kweli, na kuyatenda yote ninenayo mimi; ndipo mimi nitakuwa ni adui wa adui zako, na mtesi wa hao wakutesao.
23 Kwa kuwa malaika wangu atatangulia mbele yako, na kukufikisha kwenye Mwamori, na Mhiti, na Mperizi, na Mkanaani, na Mhivi, na Myebusi; nami nitawakatilia mbali.
24 Usiisujudie miungu yao, wala kuitumikia; wala usitende mfano wa matendo yao; bali utaiangamiza kabisa, na nguzo zao utazivunja vipande vipande.
25 Nanyi mtamtumikia Bwana, Mungu wenu, naye atakibarikia chakula chako, na maji yako; nami nitakuondolea ugonjwa kati yako.
26 Hapatakuwa na mwenye kuharibu mimba, wala aliye tasa, katika nchi yako; na hesabu ya siku zako nitaitimiza.
27 Nitatuma utisho wangu utangulie mbele yako, nami nitawafadhaisha watu wote utakaowafikilia, nami nitawafanya hao adui zako wote wakuonyeshe maungo yao.
28 Nami nitapeleka mavu mbele yako, watakaomfukuza Mhivi, na Mkanaani, na Mhiti, watoke mbele yako.
29 Sitawafukuza mbele yako katika mwaka mmoja; nchi isiwe ukiwa, na wanyama wa bara wakaongezeka kukusumbua.
30 Nitawafukuza kidogo kidogo mbele yako, hata utakapoongezeka wewe, na kuirithi hiyo nchi.
31 Nami nitakuwekea mpaka wako tangu Bahari ya Shamu hata bahari ya Wafilisti, tena tangu jangwani hata huo Mto; kwa kuwa nitawatia wenyeji wa nchi mkononi mwako; nawe utawafukuza mbele yako.
32 Usifanye maagano pamoja nao, wala pamoja na miungu yao.
33 Wasikae katika nchi yako, wasije wakakufanya kunitendea mimi dhambi; kwa sababu ukiitumikia miungu yao, jambo hili halikosi litakuwa ni tanzi kwako.

Kutoka 24


1 Kisha Bwana akamwambia Musa, Kweeni wewe, na Haruni, na Nadabu, na Abihu, na watu sabini wa wazee wa Israeli, mkamfikilie Bwana; mkasujudie kwa mbali;
2 na Musa peke yake ndiye atakayekaribia karibu na Bwana; lakini hao hawatakaribia karibu; wala hao watu hawatakwea pamoja naye.
3 Musa akaenda akawaambia watu maneno yote ya Bwana, na hukumu zake zote; watu wote wakajibu kwa sauti moja, wakasema, Maneno yote aliyoyanena Bwana tutayatenda.
4 Basi Musa akayaandika maneno yote ya Bwana, akaondoka asubuhi na mapema, akajenga madhabahu chini ya mlima, na nguzo kumi na mbili, kwa hesabu ya kabila kumi na mbili za Israeli,
5 akapeleka vijana wa wana wa Israeli, waliotoa sadaka za kuteketezwa, wakamchinjia Bwana sadaka za amani za ng'ombe.
6 Musa akatwaa nusu ya ile damu, akaitia katika mabakuli; na nusu ya ile damu akainyunyiza juu ya madhabahu.
7 Kisha akakitwaa kitabu cha agano akakisoma masikioni mwa watu; wakasema, Hayo yote aliyoyanena Bwana tutayatenda, nasi tutatii.
8 Musa akaitwaa ile damu, akawanyunyizia watu, akasema, Hii ndiyo damu ya agano alilolifanya Bwana pamoja nanyi katika maneno haya yote.
9 Ndipo akakwea juu, Musa, na haruni, na Nadabu, na Abihu, na watu sabini miongoni mwa wazee wa Israeli;
10 wakamwona Mungu wa Israeli; chini ya miguu yake palikuwa na kama sakafu iliyofanyizwa kwa yakuti samawi, kama zile mbingu zenyewe kwa usafi wake.
11 Naye hakuweka mkono wake juu ya hao wakuu wa wana wa Israeli; nao wakamwona Mungu, wakala na kunywa.
12 Bwana akamwambia Musa, Njoo huku juu kwangu mlimani, uwe huku; nami nitakupa mbao za mawe na ile sheria na hiyo amri niliyoiandika ili uwafundishe.
13 Musa akaondoka na Yoshua, mtumishi wake, Musa akapanda mlimani kwa Mungu.
14 Akawaambia hao wazee, Tungojeeni hapa, mpaka tutakaporudi kwenu; na tazameni, Haruni na Huri wapo pamoja nanyi; kila mtu aliye na neno na awaendee.
15 Musa akapanda mlimani, lile wingu likaufunikiza mlima.
16 Na huo utukufu wa Bwana ukakaa juu ya mlima wa Sinai; lile wingu likaufunikiza siku sita; na siku ya saba akamwita Musa toka kati ya lile wingu.
17 Na kuonekana kwake ule utukufu wa Bwana kulikuwa kama moto uteketezao, juu ya mlima machoni pa wana wa Israeli.
18 Musa akaingia ndani ya lile wingu, akapanda mlimani; Musa akawa humo katika ule mlima siku arobaini, mchana na usiku.

Kutoka 25


1 Bwana akanena na Musa, akamwambia,
2 Waambie wana wa Israeli kwamba wanitwalie sadaka; kila mtu ambaye moyo wake wampa kupenda mtatwaa kwake sadaka yangu.
3 Sadaka utakayopokea mikononi mwao ni hii; dhahabu, na fedha, na shaba,
4 na nyuzi za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na za rangi nyekundu, na nguo za kitani safi, na singa za mbuzi;
5 na ngozi za kondoo waume zilizotiwa rangi nyekundu, na ngozi za pomboo, na miti ya mshita,
6 na mafuta ya ile taa, na viungo vya manukato kwa yale mafuta ya kupaka, na kwa ule uvumba wenye harufu nzuri;
7 na vito vya shohamu, na vito vingine vya kutiwa kwa ile naivera, na kwa kile kifuko cha kifuani.
8 Nao na wanifanyie patakatifu; ili nipate kukaa kati yao.
9 Sawasawa na haya yote nikuonyeshayo, mfano wa maskani, na mfano wa vyombo vyake vyote, ndivyo mtakavyovifanya.
10 Nao na wafanye sanduku la mti wa mshita; urefu wake na uwe dhiraa mbili na nusu, na upana wake dhiraa moja na nusu, na kwenda juu kwake dhiraa moja na nusu.
11 Nawe ulifunike kwa dhahabu safi, ulifunike ndani na nje, nawe tia na ukingo wa dhahabu kulizunguka pande zote.
12 Nawe subu vikuku vinne vya dhahabu kwa ajili yake, na kuvitia katika miguu yake minne; vikuku viwili upande mmoja, na vikuku viwili upande wake wa pili.
13 Nawe fanya miti mirefu ya mshita na kuifunika dhahabu.
14 Nawe tia hiyo miti katika vile vikuku vilivyo katika pande mbili za sanduku ili kulichukua hilo sanduku.
15 Hiyo miti itakaa katika vile vikuku vya sanduku; haitaondolewa.
16 Kisha tia ndani ya sanduku huo ushuhuda nitakaokupa.
17 Nawe fanya kiti cha rehema cha dhahabu safi; urefu wake utakuwa dhiraa mbili na nusu, na upana wake dhiraa moja na nusu.
18 Nawe fanya makerubi mawili ya dhahabu; uyafanye ya kazi ya kufua, katika hiyo miisho ya kiti cha rehema, huku na huku.
19 Weka kerubi moja mwisho mmoja, na kerubi la pili mwisho wa pili; fanya hayo makerubi ya kitu kimoja na kiti cha rehema, mwisho huku na mwisho huku.
20 Na hayo makerubi yatainua mabawa yao juu, na kukifunika hicho kiti cha rehema kwa mabawa yao, na nyuso zao zitaelekeana hili na hili; nyuso za hayo makerubi zitaelekea kiti cha rehema.
21 Weka kiti cha rehema juu ya hilo sanduku, kisha utie huo ushuhuda nitakaokupa ndani ya sanduku.
22 Nami nitaonana nawe hapo, na kuzungumza nawe pale nilipo juu ya kiti cha rehema, katikati ya hayo makerubi mawili yaliyo juu ya sanduku la ushuhuda, katika mambo yote nitakayokuagiza kwa ajili ya wana wa Israeli.
23 Nawe fanya meza ya mti wa mshita; urefu wake utakuwa dhiraa mbili, na upana wake dhiraa moja, na kwenda juu kwake dhiraa moja na nusu.
24 Uifunike dhahabu safi, na kuifanyia ukingo wa dhahabu wa kuizunguka pande zote.
25 Kisha ifanyie upapi wa kuizunguka pande zote, upana wake utakuwa nyanda nne, nawe uufanyie ule upapi ukingo wa urembo wa dhahabu wa kuuzunguka pande zote.
26 Uifanyie vikuku vinne vya dhahabu, na kuvitia vile vikuku katika pembe zake nne, katika miguu yake minne.
27 Vile vikuku na viwe karibu na ule upapi, ili viwe mahali pa kutilia ile miti, ya kuichukulia meza.
28 Fanya ile miti ya mti wa mshita, na kuifunika dhahabu, kwamba ile meza ichukuliwe kwayo.
29 Nawe fanya sahani zake, na miiko yake, na makopo yake, na vikombe vyake vya kumiminia; vifanye vyote vya dhahabu safi.
30 Nawe utaiweka mikate ya wonyesho juu ya meza mbele yangu daima.
31 Nawe fanya kinara cha taa cha dhahabu safi; hicho kinara na kifanywe cha kazi ya kufua, tako lake, na mti wake, vikombe vyake, na matovu yake, na maua yake, vyote vitakuwa vya kitu kimoja nacho;
32 nacho kitakuwa na matawi sita yenye kutoka ubavuni mwake; matawi matatu ya kinara upande wake mmoja, na matawi matatu ya kinara upande wake wa pili
33 vikombe vitatu vilivyofanywa mfano wa maua ya mlozi katika tawi moja; tovu na ua; na vikombe vitatu vilivyofanywa mfano wa maua ya mlozi katika tawi la pili, tovu na ua; vivyo hivyo hayo matawi yote sita yatokayo katika kile kinara;
34 na katika hicho kinara vikombe vinne vilivyofanywa mfano wa maua ya mlozi, matovu yake, na maua yake;
35 na tovu chini ya matawi mawili la kitu kimoja nacho, na tovu chini ya matawi mawili la kitu kimoja nacho, na tovu chini ya matawi mawili la kitu kimoja nacho, kwa hayo matawi sita yatokayo katika kile kinara.
36 Matovu yake na matawi yake yatakuwa ya kitu kimoja nacho; kiwe chote pia kazi moja ya kufua, ya dhahabu safi.
37 Nawe zifanye taa zake saba; nao wataziwasha hizo taa zake, zitoe nuru mbele yake.
38 Na makoleo yake, na visahani vyake, vyote vitakuwa vya dhahabu safi.
39 Kitafanywa cha talanta moja ya dhahabu safi, pamoja na vyombo hivi vyote.
40 Nawe angalia ya kwamba uvifanye kama mfano wake, ulioonyeshwa mlimani.

Kutoka 26


1 Kisha fanya hiyo maskani iwe na mapazia kumi; ifanye ya nguo ya kitani nzuri ya kusokota, pamoja na nyuzi za rangi ya samawi, na ya zambarau, na nyekundu, pamoja na makerubi; kazi ya fundi stadi.
2 Urefu wa kila pazia utakuwa dhiraa ishirini na nane, na upana wa kila pazia utakuwa dhiraa nne; mapazia yote yatakuwa ya kipimo kimoja.
3 Mapazia matano yataungwa pamoja, hili na hili; na mapazia matano mengine yataungwa pamoja, hili na hili.
4 Kisha utafanya tanzi za rangi ya samawi upande wa mwisho wa pazia moja katika ule upindo wa fungu lake, vivyo utafanya upande wa mwisho wa ile pazia iliyo, katika fungu la pili.
5 Fanya matanzi hamsini katika pazia moja, na matanzi hamsini katika upande wa mwisho wa ile pazia iliyo katika kuungana kwa pili; hizo tanzi zitaelekeana.
6 Kisha ufanye vifungo hamsini vya dhahabu, na kuunganya hayo mapazia pamoja kwa vile vifungo; na hiyo maskani itakuwa ni moja.
7 Nawe fanya mapazia ya singa za mbuzi yawe hema juu ya maskani; fanya mapazia kumi na moja.
8 Urefu wa kila pazia utakuwa dhiraa thelathini, na upana wa kila pazia utakuwa dhiraa nne; hayo mapazia kumi na moja yatakuwa ya kipimo kimoja.
9 Kisha utaunganya mapazia matano mbali, na mapazia sita mbali, na lile pazia la sita utalipeta hapo upande wa mbele wa ile hema.
10 Fanya tanzi hamsini upande wa mwisho wa pazia lile lililo la mwisho katika hayo yaliyounganywa pamoja, na tanzi hamsini upande wa mwisho wa lile pazia lililo nje katika hayo ya pili yaliyounganywa pamoja.
11 Tena ufanye vifungo hamsini vya shaba, na kuvitia vile vifungo katika zile tanzi, na kuiunganya ile hema pamoja, ili iwe hema moja.
12 Na kipande kile kilichosalia, kile kiangukacho, cha yale mapazia ya hema, ile nusu ya pazia iliyosalia, itaanguka huko upande wa nyuma wa maskani.
13 Na hiyo dhiraa moja upande mmoja, na ile dhiraa moja upande wa pili, ya urefu wa mapazia ya hema uliosalia, zitaanguka katika ubavu wa maskani upande huu na upande huu, ili kuifunika.
14 Nawe fanya kifuniko cha ile hema, cha ngozi za kondoo waume zilizotiwa rangi nyekundu, na juu yake kifuniko cha ngozi za pomboo.
15 Nawe fanya hizo mbao za maskani za mti wa mshita, zenye kusimama.
16 Kila ubao utakuwa na urefu wa dhiraa kumi, na upana wake kila ubao utakuwa dhiraa moja na nusu.
17 Kila ubao utakuwa na ndimi mbili, zenye kuunganywa huu na huu; ndivyo utakavyozifanya mbao zote za maskani.
18 Kisha ufanye zile mbao za maskani, mbao ishirini kwa upande wa kusini kuelekea kusini.
19 Nawe ufanye matako arobaini ya fedha chini ya zile mbao ishirini, matako mawili chini ya ubao mmoja, kupokea zile ndimi zake mbili, na matako mawili chini ya ubao mwingine kupokea zile ndimi zake mbili;
20 na upande wa pili wa maskani, upande wa kaskazini, mbao ishirini;
21 na matako yake ya fedha arobaini; matako mawili chini ya ubao mmoja, na matako mawili chini ya ubao mwingine.
22 Kisha ufanye mbao sita kwa ajili ya upande wa nyuma wa maskani kuelekea magharibi.
23 Tena ufanye mbao mbili kwa ajili ya hizo pembe za maskani zilizo upande wa nyuma.
24 Upande wa chini zitakuwa ni mbili mbili; vivyo zitaungwa pamoja mbao pacha hata ncha ya juu katika pete ya kwanza; zote mbili ndivyo zitakavyokuwa; zitakuwa kwa ajili ya hizo pembe mbili.
25 Mbao zitakuwa ni nane, na matako yake ya fedha, matako kumi na sita; matako mawili chini ya ubao mmoja, na matako mawili chini ya ubao wa pili.
26 Nawe fanya mataruma ya mti wa mshita; mataruma matano kwa ajili ya mbao za upande mmoja wa maskani,
27 na mataruma matano kwa ajili ya mbao za upande wa pili wa maskani, na mataruma matano kwa ajili ya mbao za upande wa maskani ulio nyuma kuelekea magharibi.
28 Na hilo taruma la katikati, lililo katikati ya zile mbao litapenya toka mwisho huu hata mwisho huu.
29 Na hizo mbao utazifunika dhahabu, na pete zake za kutilia yale mataruma utazifanya za dhahabu; na hayo mataruma utayafunika dhahabu.
30 Nawe utaisimamisha hiyo maskani sawasawa na mfano wake ulioonyeshwa mlimani.
31 Nawe fanya pazia la nyuzi za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na za rangi nyekundu, na nguo za kitani nzuri zenye kusokotwa, litafumwa na kutiwa makerubi, kazi ya fundi stadi;
32 kisha litungike katika nguzo nne za mti wa mshita zilizofunikwa dhahabu, vifungo vyake vitakuwa vya dhahabu, katika matako ya fedha manne.
33 Nawe tungika lile pazia chini ya vile vifungo, nawe lete lile sanduku la ushuhuda na kulitia humo nyuma ya pazia; na lile pazia litawagawanyia kati ya patakatifu, na mahali patakatifu sana.
34 Nawe utaweka kiti cha rehema juu ya lile sanduku la ushuhuda ndani ya mahali pale patakatifu sana.
35 Na ile meza utaiweka nje ya pazia, na kinara cha taa kuikabili ile meza upande wa maskani wa kuelekea kusini; na ile meza utaiweka upande wa kaskazini.
36 Kisha utafanya kisitiri kwa mlango wa Hema, cha nyuzi za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na za rangi nyekundu, na kitani nzuri yenye kusokotwa, kazi ya mshona taraza.
37 Nawe fanya nguzo tano za mti wa mshita kwa kile kisitiri, na kuzifunika dhahabu; kulabu zake zitakuwa za dhahabu; nawe utasubu matako ya shaba matano kwa ajili yake.

Kutoka 27


1 Nawe fanya madhabahu ya mti wa mshita; urefu wake utakuwa ni dhiraa tano, na upana wake dhiraa tano; hiyo madhabahu itakuwa mraba; na kwenda juu kwake kutakuwa dhiraa tatu.
2 Nawe fanya pembe nne katika pembe zake nne; hizo pembe zitakuwa za kitu kimoja na madhabahu; nawe utayafunika shaba.
3 Na vyombo vyake vya kuyaondoa majivu yake utavifanya, na majembe yake, na mabakuli yake, na uma zake, na meko yake; vyombo vyake vyote utavifanya vya shaba.
4 Nawe uifanyie hiyo madhabahu wavu wa shaba; kisha utie pete nne za shaba katika hizo pembe nne za ule wavu.
5 Nawe tia huo wavu chini ya kizingo kiizungukacho madhabahu upande wa chini, ili huo wavu ufikilie katikati ya hiyo madhabahu.
6 Nawe fanya miti kwa ajili ya madhabahu, miti ya mshita, na kuifunika shaba.
7 Na hiyo miti itatiwa katika pete, na ile miti itakuwa katika pande mbili za madhabahu, wakati wa kuichukua.
8 Uifanye ya mbao, yenye mvungu ndani yake; kama ulivyoonyeshwa mlimani, ndivyo watakavyoifanya.
9 Nawe fanya ua wa maskani; upande wa kusini wa kuelekea kusini kutakuwa na chandarua ya nguo ya kitani nzuri yenye kusokotwa, kwa huo ua, urefu wake upande mmoja utakuwa ni dhiraa mia;
10 na nguzo zake zitakuwa nguzo ishirini, na matako yake ishirini, matako yake yatakuwa ya shaba; kulabu za zile nguzo na vitanzi vyake vitakuwa vya fedha.
11 Ni vivyo upande wa kaskazini, urefu wake hiyo chandarua utakuwa ni dhiraa mia, na nguzo zake ishirini, na matako yake ishirini yatakuwa ya shaba; kulabu za zile nguzo na vitanzi vyake vitakuwa vya fedha.
12 Na upande wa magharibi, upana wa ua kutakuwa na chandarua ya dhiraa hamsini; nguzo zake kumi, na matako yake kumi.
13 Na upana wa ule ua upande wa mashariki kuelekea mashariki utakuwa ni dhiraa hamsini.
14 Chandarua upande mmoja wa lango itakuwa dhiraa kumi na tano upana wake; nguzo zake zitakuwa tatu na matako yake matatu.
15 Upande wa pili ni vivyo chandarua ya dhiraa kumi na tano; nguzo zake tatu, na matako yake matatu.
16 Na kwa lile lango la ua patakuwa na kisitiri cha dhiraa ishirini, kitakuwa cha nguo ya rangi ya samawi, na ya rangi ya zambarau, na nyekundu, na kitani nzuri yenye kusokotwa, kazi ya mshona taraza; nguzo zake zitakuwa nne, na matako yake manne.
17 Nguzo zote za ule ua ziuzungukazo pande zote zitakuwa na vitanzi vya fedha; kulabu zake za fedha, na matako yake ya shaba.
18 Urefu wa huo ua utakuwa dhiraa mia, na upana wake utakuwa dhiraa hamsini kotekote, na kwenda juu kwake dhiraa tano; yawe ya nguo ya kitani nzuri, na matako yake yatakuwa ya shaba.
19 Vyombo vyote vya maskani vitumiwavyo katika utumishi wake wote, na vigingi vyake vyote, na vigingi vyote vya ule ua, vitakuwa vya shaba.
20 Nawe waamuru wana wa Israeli wakuletee mafuta ya zeituni safi ya kupondwa kwa ajili ya nuru, ili kufanya ile taa kuwaka daima.
21 Ndani ya ile hema ya kukutania, nje ya hilo pazia, lililo mbele ya huo ushuhuda, Haruni na wanawe wataitengeza tangu jioni hata asubuhi mbele ya Bwana; itakuwa ni amri ya milele katika vizazi vyao vyote kwa ajili ya wana wa Israeli.

Kutoka 28


1 Nawe umlete Haruni ndugu yako karibu nami, na wanawe pamoja naye, miongoni mwa wana wa Israeli, ili anitumikie katika kazi ya ukuhani. Haruni, na Nadabu, na Abihu, na Eleazari, na Ithamari, wana wa Haruni.
2 Nawe utamfanyia Haruni ndugu yako mavazi matakatifu, kwa utukufu na kwa uzuri.
3 Nawe utawaambia watu wote wenye moyo wa hekima, niliowajaza na roho ya hekima wamfanyie Haruni mavazi ili kumtakasa anitumikie katika kazi ya ukuhani.
4 Na mavazi watakayoyafanya ni haya; kifuko cha kifuani, na naivera, na joho, na kanzu ya kazi ya urembo; na kilemba, na mshipi; nao watawafanyia Haruni nduguyo, na wanawe, mavazi matakatifu ili anitumikie katika kazi ya ukuhani.
5 Nao wataitwaa dhahabu, na nguo ya rangi ya samawi, na ya rangi ya zambarau, na ya rangi nyekundu, na nguo ya kitani nzuri.
6 Nao waifanye naivera kwa nyuzi za dhahabu, na za samawi, na za zambarau, na nyekundu, na kitani nzuri yenye kusokotwa kwa kazi ya mstadi.
7 Itakuwa na vipande viwili vya mabegani, vilivyoungana kwenye ncha zake mbili; ili ipate kuunganywa.
8 Na mshipi wa kazi ya ustadi ulio juu yake, ili kuifunga mahali pake; utakuwa wa kazi kama ile ya naivera, ya vitu vile vile ya nyuzi za dhahabu, na za rangi ya samawi, na ya zambarau, na nyekundu, na kitani nzuri yenye kusokotwa.
9 Nawe utatwaa vito viwili vya shohamu, ya rangi ya chani-kiwiti, nawe utachora juu yake majina ya wana wa Israeli;
10 majina yao sita katika kito kimoja, na majina sita yaliyosalia katika kile kito cha pili, kwa utaratibu wa kuzaliwa kwao.
11 Kwa kazi mtu mwenye kuchora mawe kama vile muhuri ichorwavyo, utavichora hivi vito viwili, sawasawa na majina ya wana wa Israeli, nawe utavitia katika vijalizo vya dhahabu.
12 Nawe utavitia vile vito viwili juu ya vipande vya mabegani vya hiyo naivera, viwe vito vya ukumbusho kwa ajili ya wana wa Israeli; naye Haruni atayachukua majina yao mbele za Bwana juu ya mabega yake mawili ili kuwa ukumbusho.
13 Nawe fanya vijalizo viwili vya dhahabu;
14 na mikufu miwili ya dhahabu safi; utaifanya iwe mfano wa kamba, ya kazi ya kusokotwa; nawe uitie ile mikufu ya kazi ya kusokotwa katika vile vijalizo.
15 Nawe utafanya kifuko cha kifuani cha hukumu, kazi ya fundi stadi; utakifanya kwa kuiandama ile kazi ya hiyo naivera; ya nyuzi za dhahabu, na za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na nyekundu, na kitani safi yenye kusokotwa, ndivyo utakavyokifanya.
16 Kitakuwa mraba, tena cha kukunjwa; urefu wake utakuwa shibiri moja, na upana wake shibiri moja.
17 Nawe ukijaze viweko vya vito, safu nne za vito; safu moja itakuwa ni akiki, na yakuti ya rangi ya manjano, na baharamani, hivi vitakuwa safu ya kwanza;
18 na safu ya pili itakuwa zumaridi, na yakuti samawi, na almasi;
19 na safu ya tatu itakuwa hiakintho, na akiki nyekundu, na amethisto;
20 na safu ya nne itakuwa ni zabarajadi, na shohamu, na yaspi; vito hivyo vitakazwa ndani ya dhahabu kwa kujaa mahali pake.
21 Na vile vito vitakuwa sawasawa na majina ya wana wa Israeli, kumi na viwili, sawasawa na majina yao; mfano wa kuchora kwa muhuri kila kimoja sawasawa na jina lake, vitakuwa vya hizo kabila kumi na mbili.
22 Nawe utie katika kile kifuko cha kifuani mikufu mfano wa kamba, ya kazi ya kusokotwa, ya dhahabu safi.
23 Nawe utie pete mbili za dhahabu katika kile kifuko cha kifuani, na kuzitia hizo pete mbili katika ncha mbili za kifuko cha kifuani.
24 Nawe utie hiyo mikufu miwili ya dhahabu iliyosokotwa katika zile pete mbili zilizo katika ncha za kifuko cha kifuani.
25 Na ncha zile nyingine za hiyo mikufu miwili ya kusokotwa utazitia katika vile vijalizo viwili, na kuvitia katika vile vipande vya mabegani vya naivera upande wa mbele.
26 Nawe utafanya pete mbili za dhahabu, uzitie katika hizo ncha mbili za kifuko cha kifuani, katika ukingo wake, ulio upande wa naivera ulio ndani.
27 Nawe fanya pete mbili za dhahabu, na kuzitia katika vile vipande viwili vya mabegani vya ile naivera chini yake, upande wa mbele, karibu na kifungo chake, juu ya huo mshipi wa naivera uliosukwa kwa ustadi.
28 Nao watakikaza kile kileso kwa zile pete zake kwenye pete za naivera kwa ukanda wa rangi ya samawi, ili kwamba kikae pale juu ya ule mshipi wa naivera uliosukwa kwa ustadi, ili kwamba kifuko cha kifuani kisiachane na naivera.
29 Na Haruni atayachukua majina ya wana wa Israeli katika kile kifuko cha kifuani cha hukumu juu ya moyo wake, hapo atakapoingia ndani ya mahali patakatifu, kuwa ukumbusho mbele ya Bwana daima.
30 Nawe utie hizo Urimu na Thumimu katika kile kifuko cha kifuani cha hukumu; nazo zitakuwa juu ya moyo wa Haruni, hapo atakapoingia ndani mbele ya Bwana; na Haruni atachukua hukumu ya hao wana wa Israeli juu ya moyo wake mbele ya Bwana daima.
31 Nawe fanya hiyo joho ya naivera ya rangi ya samawi yote.
32 Nayo itakuwa na tundu katikati yake kwa kupitisha kichwa; itakuwa na utepe wa kazi ya kusokotwa kuzunguka hilo tundu lake, mfano wa tundu lililo katika kanzu ya chuma, ili lisipasuke.
33 Nawe katika pindo zake utatia makomamanga ya rangi ya samawi, na ya rangi ya zambarau, na ya rangi nyekundu, kuzunguka pindo zake kotekote; na njuga za dhahabu kati ya hayo makomamanga pande zote;
34 njuga ya dhahabu na komamanga, njuga ya dhahabu na komamanga, katika pindo za joho kuizunguka pande zote.
35 Nayo itakuwa juu ya Haruni akitumika; na sauti ya hizo njuga itasikilikana hapo aingiapo ndani ya mahali patakatifu mbele ya Bwana na hapo atokapo nje, ili kwamba asife.
36 Nawe fanya bamba la dhahabu safi na kuchora juu yake, mfano wa machoro ya muhuri, MTAKATIFU KWA Bwana.
37 Nawe ulitie hilo bamba katika ukanda wa rangi ya samawi, nalo litakuwa katika kile kilemba; litakuwa upande wa mbele wa kile kilemba.
38 Nalo litakuwa katika kipaji cha uso cha Haruni, na Haruni atauchukua uovu wa vile vitu vitakatifu, watakavyovitakasa hao wana wa Israeli katika vipawa vyao vyote vitakatifu, nalo litakuwa katika kipaji chake cha uso sikuzote, ili kwamba vipate kukubaliwa mbele za Bwana.
39 Na hiyo kanzu utaifuma ya kitani nzuri ya kazi ya urembo, ufanye na kilemba cha nguo ya kitani nzuri, nawe utafanya mshipi wa kazi ya mwenye kutia taraza.
40 Kisha utafanya kanzu kwa ajili ya wana wa Haruni, nawe wafanyie mishipi, wafanyie na kofia kwa utukufu na uzuri.
41 Nawe mvike huyo nduguyo Haruni na wanawe nao mavazi hayo; nawe watie mafuta, na kuwaweka kwa kazi takatifu, na kuwatakasa, ili wapate kunitumikia mimi katika kazi ya ukuhani.
42 Nawe wafanyie suruali za nguo ya kitani, ili kufunika tupu ya miili yao; suruali hizo zitafika tangu kiunoni hata mapajani;
43 na Haruni na wanawe watazivaa, hapo watakapoingia katika hema ya kukutania, au hapo watakapoikaribia madhabahu ili watumike katika mahali patakatifu; wasije wakachukua uovu, wakafa; hii itakuwa ni amri ya milele kwake yeye, na kwa wazao wake.

Kutoka 29


1 Nawe uwafanyie jambo hili, ili kuwatakasa, wapate kunitumikia mimi katika kazi ya ukuhani; twaa ng'ombe mmoja mume kijana, na kondoo waume wawili walio wakamilifu,
2 na mkate usiotiwa chachu, na maandazi yasiyotiwa chachu yaliyokandwa kwa mafuta, na kaki zisizotiwa chachu zilizotiwa mafuta; utazifanya za unga mzuri mwembamba wa ngano.
3 Nawe vitie vyote katika kikapu, uvilete ndani ya kikapu, pamoja na huyo ng'ombe, na hao kondoo waume wawili.
4 Kisha mlete Haruni na wanawe hata mlangoni pa hema ya kukutania, ukawaoshe kwa maji.
5 Kisha twaa hayo mavazi na kumvika Haruni; itie kanzu, na joho ya naivera, na naivera, na kifuko cha kifuani, na kumkaza kwa huo mshipi wa naivera uliosukwa kwa ustadi;
6 nawe mvike kile kilemba kichwani, na ile taji takatifu utaitia katika kile kilemba.
7 Ndipo utakapotwaa hayo mafuta ya kutiwa, na kummiminia kichwani mwake, na kumtia mafuta.
8 Kisha walete hao wanawe na kuwavika kanzu.
9 Nawe uwakaze mishipi, Haruni na wanawe, na kuwavika kofia; nao watakuwa na huo ukuhani kwa amri ya milele; nawe utawaweka Haruni na wanawe kwa kazi takatifu.
10 Kisha utamleta huyo ng'ombe mbele ya hema ya kukutania; na Haruni na wanawe wataweka mikono yao juu ya kichwa cha huyo ng'ombe.
11 Kisha utamchinja huyo ng'ombe mbele ya Bwana, mlangoni pa hema ya kukutania.
12 Kisha twaa baadhi ya damu ya ng'ombe, uitie katika pembe za madhabahu kwa kidole chako; na kuimimina damu yote chini ya madhabahu.
13 Kisha twaa mafuta yote yafunikayo matumbo, na kitambi kilicho katika ini, na figo mbili, na mafuta yaliyo juu yake, uyateketeze yote juu ya madhabahu.
14 Lakini nyama yake huyo ng'ombe, na ngozi yake, na mavi yake, utayachoma kwa moto nje ya marago; ni sadaka kwa ajili ya dhambi.
15 Pia mtwae kondoo mume mmoja; na Haruni na wanawe wataweka mikono yao juu ya kichwa chake huyo kondoo mume.
16 Kisha utamchinja huyo kondoo mume, na kuitwaa damu yake, na kuinyunyiza katika madhabahu kuizunguka kando-kando.
17 Kisha utamkata-kata kondoo vipande vyake, na kuyaosha matumbo yake na miguu yake, na kuiweka pamoja na vipande vyake na kichwa chake.
18 Nawe mteketeze kondoo mzima juu ya madhabahu; ni sadaka ya kuteketezwa kwa ajili ya Bwana; ni harufu nzuri, sadaka iliyosongezwa kwa Bwana kwa njia ya moto.
19 Kisha mtwae huyo kondoo wa pili; na Haruni na wanawe wataweka mikono yao juu ya kichwa chake huyo kondoo.
20 Kisha utamchinja kondoo, na kuitwaa damu yake, na kuitia katika ncha ya sikio la Haruni la upande wa kuume, na katika ncha za masikio ya kuume ya wanawe, na katika vyanda vya gumba vya mikono yao ya kuume, na katika vidole vikuu vya miguu yao ya kuume, na kuinyunyiza hiyo damu katika madhabahu kuizunguka kando-kando.
21 Kisha twaa katika hiyo damu iliyo juu ya madhabahu, na katika hayo mafuta ya kutiwa, na kumnyunyizia Haruni, juu ya mavazi yake, na wanawe, na mavazi yao pia, pamoja naye; naye atatakaswa, na mavazi yake, na wanawe, na mavazi ya wanawe, pamoja naye.
22 Tena yatwae mafuta ya huyo kondoo mume, na mkia wake wa mafuta, na mafuta yafunikayo matumbo, na kitambi kilicho katika ini, na figo mbili, na mafuta yaliyo katika hizo figo, na paja la kuume; kwani ni kondoo ambaye ni wa kuwekwa kwa kazi takatifu;
23 utwae na mkate mmoja wa unga, na mkate mmoja ulioandaliwa kwa mafuta, na kaki moja katika kile kikapu cha mikate isiyotiwa chachu, kilichowekwa mbele ya Bwana;
24 nawe utavitia hivi vyote katika mikono ya Haruni, na katika mikono ya wanawe; nawe utavitikisa-tikisa viwe sadaka ya kutikiswa mbele za Bwana.
25 Kisha uvitwae vile vitu mikononi mwao, na kuviteketeza juu ya madhabahu, juu ya ile sadaka ya kuteketezwa, viwe harufu nzuri mbele ya Bwana; ni sadaka iliyosongezwa kwa Bwana kwa njia ya moto.
26 Kisha twaa kidari cha huyo kondoo wa kuwekwa kwake Haruni kwa kazi takatifu, na kukitikisa-tikisa kiwe sadaka ya kutikiswa mbele za Bwana; nacho kitakuwa ni sehemu yako.
27 Nawe kitakase kile kidari cha ile sadaka ya kutikiswa, na lile paja la sadaka ya kuinuliwa, lililotikiswa, na lililoinuliwa juu, vya yule kondoo wa kuwekwa kwa kazi takatifu, huyo aliyekuwa kwa ajili ya Haruni, na huyo aliyekuwa kwa ajili ya wanawe;
28 navyo vitakuwa vya Haruni na wanawe posho ya lazima sikuzote itokayo kwa hao wana wa Israeli; kwa kuwa ni sadaka ya kuinuliwa; nayo itakuwa ni sadaka ya kuinuliwa itokayo kwa hao wana wa Israeli katika dhabihu zao za sadaka za amani, ni sadaka yao ya kuinuliwa kwa ajili ya Bwana.
29 Na hayo mavazi matakatifu ya Haruni yatakuwa ya wanawe baada yake, wayavae watakapotiwa mafuta, na watakapowekwa kwa kazi takatifu.
30 Huyo mwanawe atakayekuwa kuhani badala yake atayavaa muda wa siku saba, hapo atakapoingia ndani ya hiyo hema ya kukutania, ili atumike ndani ya mahali patakatifu.
31 Nawe twaa huyo kondoo mume aliyekuwa wa kuwekwa kwa kazi takatifu, na kuitokosa nyama yake katika mahali patakatifu.
32 Na Haruni na wanawe wataila ile nyama ya kondoo, na mikate iliyo katika kile kikapu, hapo mbele ya mlango wa hema ya kukutania.
33 Nao watakula vile vitu ambavyo upatanisho ulifanywa kwa hivyo, ili kuwaweka kwa kazi takatifu na kuwatakasa; lakini mgeni asivile, maana, ni vitu vitakatifu.
34 Na kwamba kitu cho chote cha ile nyama, iliyo kwa ajili ya kuweka kwa kazi takatifu, au cho chote cha hiyo mikate, kikisalia hata asubuhi, ndipo utavichoma kwa moto hivyo vilivyosalia; havitaliwa, maana, ni vitu vitakatifu.
35 Ni hivyo utakavyowatendea Haruni na wanawe, sawasawa na hayo yote niliyokuagiza; utawaweka kwa kazi takatifu siku saba.
36 Kila siku utamtoa ng'ombe wa sadaka ya dhambi kwa ajili ya upatanisho; nawe utaisafisha hiyo madhabahu, hapo utakapofanya upatanisho kwa ajili ya hiyo madhabahu; nawe utaitia mafuta, ili kuitakasa.
37 Utafanya upatanisho kwa ajili ya hiyo madhabahu muda wa siku saba, na kuitakasa; ndipo madhabahu itakapokuwa takatifu sana; kila kitu kiigusacho madhabahu kitakuwa kitakatifu.
38 Basi sadaka utakazozitoa juu ya madhabahu ni hizi; wana-kondoo wa mwaka mmoja wawili siku baada ya siku daima.
39 Mwana-kondoo mmoja utamchinja asubuhi; na mwana-kondoo wa pili utamchinja jioni;
40 tena, pamoja na mwana-kondoo mmoja utatoa vibaba vitatu vya unga mzuri uliochanganyika na mafuta yenye kupondwa, kiasi cha kibaba na robo kibaba; na divai kiasi cha kibaba na robo kibaba, iwe sadaka ya kinywaji.
41 Na huyo mwana-kondoo wa pili utamchinja wakati wa jioni, nawe utamfanyia vivyo kama ile sadaka ya unga ya asubuhi, na kama ile sadaka yake ya kinywaji, iwe harufu nzuri, ni dhabihu ya kusongezwa kwa Bwana kwa njia ya moto.
42 Itakuwa ni sadaka ya kuteketezwa milele katika vizazi vyenu vyote mlangoni pa ile hema ya kukutania mbele ya Bwana; hapo nitakapokutana nanyi, ili ninene na wewe hapo.
43 Nami nitakutana na wana wa Israeli hapo, na hiyo Hema itafanywa takatifu na utukufu wangu.
44 Nami nitaitakasa hiyo hema ya kukutania, na hiyo madhabahu; pia Haruni na wanawe nitawatakasa, ili wanitumikie katika kazi ya ukuhani.
45 Na mimi nitakaa kati ya wana wa Israeli, nami nitakuwa Mungu wao.
46 Nao watanijua kuwa mimi ndimi Bwana, Mungu wao, niliyewaleta watoke katika nchi ya Misri, nipate kukaa kati yao; ni mimi Bwana Mungu wao.

Kutoka 30


1 Nawe fanya madhabahu ya kufukizia uvumba; utaifanyiza kwa mti wa mshita.
2 Urefu wake utakuwa dhiraa moja, na upana wake dhiraa moja; itakuwa mraba; na kwenda juu kwake dhiraa mbili; pembe zake zitakuwa za kitu kimoja nayo.
3 Nawe utaifunikiza dhahabu safi juu yake, na mbavu zake kando kando, na pembe zake; nawe utaifanyia ukingo wa dhahabu kuizunguka.
4 Kisha utaifanyia pete mbili za dhahabu, chini ya ukingo wake katika mbavu zake mbili, katika pande zake mbili utazifanya; nazo zitakuwa mahali pa kuitia miti ya kuichukulia.
5 Na ile miti utaifanya kwa mti wa mshita, na kuifunikiza dhahabu safi.
6 Nawe utaitia mbele ya lile pazia lililo karibu na sanduku la ushuhuda mbele ya kiti cha rehema kilicho juu ya ushuhuda, hapo nitakapokutana nawe.
7 Na Haruni atafukiza uvumba wa manukato juu yake; kila siku asubuhi atakapozitengeneza zile taa, ataufukiza.
8 Na Haruni atakapoziwasha zile taa wakati wa jioni, ataufukiza, uwe uvumba wa daima mbele za Bwana katika vizazi vyenu vyote.
9 Hamtafukiza juu yake uvumba mgeni, wala sadaka ya kuteketezwa, wala sadaka ya unga, wala hamtamimina juu yake sadaka ya kinywaji.
10 Naye Haruni atafanya upatanisho juu ya pembe zake mara moja kila mwaka; kwa damu ya ile sadaka ya dhambi ya kufanya upatanisho, mara moja kila mwaka ataifanyia upatanisho, katika vizazi vyenu vyote; ni takatifu sana kwa Bwana.
11 Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
12 Utakapowahesabu wana wa Israeli, kama itakavyotokea hesabu yao, ndipo watakapompa Bwana kila mtu ukombozi kwa ajili ya roho yake, hapo utakapowahesabu; ili kwamba yasiwe maradhi kati yao, hapo utakapowahesabu.
13 Nacho watakachotoa ni hiki, kila mtu apitaye kwa wale waliohesabiwa atatoa nusu shekeli kwa kuiandama shekeli ya mahali patakatifu; (shekeli ni gera ishirini;) nusu shekeli kwa sadaka ya Bwana.
14 Kila mtu apitaye kwa wale waliohesabiwa tangu huyo ambaye umri wake ni miaka ishirini, au zaidi, atatoa hiyo sadaka ya Bwana.
15 Matajiri hawataleta zaidi, wala maskini hawataleta kilichopungua, katika hiyo nusu shekeli, watakapotoa hiyo sadaka ya Bwana, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya roho zenu.
16 Nawe utapokea hizo fedha za upatanisho mikononi mwa hao wana wa Israeli, na kuziweka kwa ajili ya utumishi wa hema ya kukutania; ili kwamba ziwe ukumbusho kwa ajili ya wana wa Israeli mbele ya Bwana, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya roho zenu.
17 Bwana akanena na Musa, na kumwambia
18 Fanya na birika la shaba, na tako lake la shaba, ili kuogea; nawe utaliweka kati ya hema ya kukutania na madhabahu, nawe utalitia maji.
19 Na Haruni na wanawe wataosha mikono yao na miguu yao humo;
20 hapo waingiapo ndani ya hema ya kukutania; watajiosha majini, ili wasife; au hapo watakapoikaribia madhabahu ili watumike, kumteketezea Bwana sadaka ya moto;
21 basi wataosha mikono yao na miguu yao ili kwamba wasife; na neno hili litakuwa amri kwao milele, kwake yeye na kwa wazao wake katika vizazi vyao vyote.
22 Kisha Bwana akasema na Musa, na kumwambia,
23 Jitwalie manukato yaliyo bora, manemane mbichi shekeli mia tano, na mdalasini wenye harufu nzuri nusu ya kiasi hicho, yaani, shekeli mia mbili na hamsini, na kane shekeli mia mbili na hamsini,
24 na kida shekeli mia tano, kwa kuiandama shekeli ya mahali patakatifu, na mafuta ya zeituni kiasi cha vibaba vitano;
25 nawe utayafanya mafuta ya kutiwa matakatifu, marhamu iliyochanganywa kwa kazi ya ustadi ya mtengezaji manukato; yatakuwa ni mafuta matakatifu ya kutiwa.
26 Nawe utaipaka hema ya kukutania kwa mafuta hayo, na hilo sanduku la ushuhuda,
27 na hiyo meza, na vyombo vyake vyote, na kinara cha taa, na vyombo vyake, na madhabahu ya kufukizia uvumba,
28 na madhabahu ya kuteketezea sadaka, pamoja na vyombo vyake vyote, na birika, na tako lake.
29 Nawe utavitakasa vitu hivyo, ili viwe vitakatifu sana; tena kila kivigusacho vyombo vile kitakuwa kitakatifu.
30 Nawe utawatia mafuta Haruni na wanawe, na kuwatakasa, ili wanitumikie katika kazi ya ukuhani.
31 Nawe utanena na wana wa Israeli na kuwaambia, Haya yatakuwa ni mafuta matakatifu ya kutiwa kwa ajili yangu mimi katika vizazi vyenu vyote.
32 Hayatamiminwa katika kiwiliwili cha binadamu, wala msifanye mengine mfano wa haya kama yalivyoungwa kwa viungo vyake; ni matakatifu, na kwenu ninyi yatakuwa matakatifu.
33 Mtu awaye yote atakayechanganya mafuta mfano wa haya, au mtu awaye yote atakayetia mafuta haya juu ya mgeni, mtu huyo atakatiliwa mbali na watu wake.
34 Bwana akamwambia Musa, Jitwalie manukato mazuri, yaani, natafi, na shekelethi, na kelbena; viungo vya manukato vizuri pamoja na ubani safi; vitu hivyo vyote na viwe vya kipimo kimoja;
35 nawe utafanya uvumba wa vitu hivyo, manukato ya kazi ya ustadi wa mtengenazaji manukato, yatakuwa yamekolea, safi, matakatifu;
36 nawe baadhi yake utayaponda sana, na kuyaweka mbele ya ushuhuda ndani ya hema ya kukutania, hapo nitakapokutana nawe; nayo yatakuwa kwenu matakatifu sana.
37 Na uvumba utakaofanya, hamtajifanyia uvumba wenye viungo sawasawa na uvumba huo; utakuwa kwenu mtakatifu kwa ajili ya Bwana.
38 Mtu ye yote atakayefanya mfano wa huo, ili kuunusa, mtu huyo atakatiliwa mbali na watu wake.

Kutoka 31


1 Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
2 Angalia, nimemwita kwa jina lake Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa kabila ya Yuda;
3 nami nimemjaza roho ya Mungu, katika hekima, na maarifa, na ujuzi, na mambo ya kazi ya kila aina,
4 ili abuni kazi za ustadi, kuwa fundi wa dhahabu, na wa fedha, na wa shaba,
5 na kukata vito kwa kutiwa mahali, na kuchora miti, na kufanya kazi ya ustadi iwayo yote.
6 Tena, tazama, nimemchagua, awe pamoja naye, huyo Oholiabu, mwana wa Ahisamaki, wa kabila ya Dani; nami nimetia hekima katika mioyo ya wote wenye moyo wa hekima, ili wapate kufanya vyote nilivyokuagiza;
7 yaani, hema ya kukutania na sanduku la ushuhuda, na kiti cha rehema kilicho juu yake, na vyombo vyote vya Hema;
8 na meza, na vyombo vyake, na kinara cha taa safi pamoja na vyombo vyake vyote, na madhabahu ya kufukizia uvumba;
9 na madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa na vyombo vyake vyote, na birika na tako lake;
10 na mavazi yenye kufumwa kwa uzuri, na mavazi matakatifu ya Haruni kuhani, na mavazi ya wanawe, ili kutumika katika kazi ya ukuhani;
11 na mafuta ya kutiwa, na uvumba wa manukato mazuri, kwa ajili ya mahali patakatifu; sawasawa na yote niliyokuagiza ndivyo watakavyofanya wao.
12 Bwana akasema na Musa, na kumwambia,
13 Kisha, nena wewe na wana wa Israeli, na kuwaambia, Hakika mtazishika Sabato zangu, kwa kuwa ni ishara kati ya mimi na ninyi katika vizazi vyenu vyote; ili mpate kujua ya kuwa mimi ndimi Bwana niwatakasaye ninyi.
14 Basi mtaishika hiyo Sabato; kwa kuwa ni takatifu kwenu; kila mtu atakayeitia unajisi hakika yake atauawa; kwa kuwa kila mtu afanyaye kazi katika siku hiyo, nafsi hiyo itakatiliwa mbali na watu wake.
15 Kazi itafanywa siku sita; lakini siku ya saba ni Sabato ya kustarehe kabisa, takatifu kwa Bwana; kila mtu atakayefanya kazi yo yote katika siku ya Sabato, hakika yake atauawa.
16 Kwa ajili ya hayo wana wa Israeli wataishika Sabato, kuiangalia sana hiyo Sabato katika vizazi vyao vyote, ni agano la milele.
17 Ni ishara kati ya mimi na wana wa Israeli milele; kwani kwa siku sita Bwana alifanya mbingu na nchi, akastarehe kwa siku ya saba na kupumzika.
18 Hapo Bwana alipokuwa amekwisha zungumza na Musa katika mlima wa Sinai, akampa hizo mbao mbili za ushuhuda, mbao mbili za mawe, zilizoandikwa kwa chanda cha Mungu.

Kutoka 32


1 Hata watu walipoona ya kuwa Musa amekawia kushuka katika mlima, wakakusanyana wakamwendea Haruni, wakamwambia, Haya! Katufanyizie miungu itakayokwenda mbele yetu, kwa maana Musa huyo aliyetutoa katika nchi ya Misri hatujui yaliyompata.
2 Haruni akawaambia, Zivunjeni pete za dhahabu zilizo katika masikio ya wake zenu, na wana wenu, na binti zenu, mkaniletee.
3 Watu wote wakazivunja pete za dhahabu zilizo katika masikio yao, wakamletea Haruni.
4 Akaipokea mikononi mwao akaitengeneza kwa patasi, akaifanya iwe sanamu ya ndama kwa kuiyeyusha; nao wakasema, Hiyo ndiyo miungu yako, Ee Israeli, iliyokutoa katika nchi ya Misri.
5 Naye Haruni alipoona jambo hili, akajenga madhabahu mbele yake; Haruni akatangaza akasema, Kesho itakuwa sikukuu kwa Bwana.
6 Wakaondoka asubuhi na mapema, wakatoa dhabihu, wakaleta sadaka za amani, watu wakaketi kula na kunywa, wakaondoka wacheze.
7 Bwana akamwambia Musa, Haya! Shuka; kwa maana watu wako uliowatoa katika nchi ya Misri wamejiharibu nafsi zao,
8 wamepotoka upesi kuiacha ile njia niliyowaamuru, wamejifanyizia ndama ya kuyeyusha wakaiabudu na kuitolea dhabihu, wakasema, Hiyo ndiyo miungu yako, Ee Israeli, iliyokutoa katika nchi ya Misri.
9 Tena Bwana akamwambia Musa, Mimi nimewaona watu hawa, na tazama, ni watu wenye shingo ngumu
10 basi sasa niache, ili hasira zangu ziwake juu yao, niwaangamize, nami nitakufanya wewe uwe taifa kuu.
11 Musa akamsihi sana Bwana, Mungu wake, na kusema, Bwana, kwa nini hasira zako kuwaka juu ya watu wako uliowaleta kutoka nchi ya Misri kwa uweza mkuu, na kwa mkono wenye nguvu?
12 Kwa nini Wamisri kunena, wakisema, Amewatoa kwa kuwatenda uovu, ili apate kuwaua milimani, na kuwaondoa watoke juu ya uso wa nchi? Geuka katika hasira yako kali, ughairi uovu huu ulio nao juu ya watu wako.
13 Mkumbuke Ibrahimu, na Isaka, na Israeli, watumishi wako, ambao uliwaapia kwa nafsi yako, na kuwaambia, Nitazidisha kizazi chenu mfano wa nyota za mbinguni; tena nchi hii yote niliyoinena nitakipa kizazi chenu nao watairithi milele.
14 Na Bwana akaughairi ule uovu aliosema ya kwamba atawatenda watu wake.
15 Basi, Musa akageuka akashuka katika mlima, na zile mbao mbili za mawe mikononi mwake; mbao zilizoandikwa pande zote mbili, upande huu na upande huu ziliandikwa.
16 Na zile mbao zilikuwa kazi ya Mungu nayo maandiko yalikuwa maandiko ya Mungu, yaliyochorwa katika zile mbao.
17 Na Yoshua aliposikia kelele za watu walipokuwa wakipiga kelele, akamwambia Musa, Kuna kelele ya vita maragoni.
18 Akasema, Hiyo si sauti ya watu wapigao kelele kwa sababu ya kushinda vitani, wala si sauti ya watu wapigao kelele kwa sababu ya kushindwa; bali kelele za watu waimbao ndizo ninazozisikia mimi.
19 Hata alipoyakaribia marago akaiona ile ndama, na ile michezo. Hasira ya Musa ikawaka, akazitupa zile mbao mikononi mwake, akazivunja chini ya mlima.
20 Akaitwaa ile ndama waliyoifanya, akaichoma moto, akaisaga hata ikawa mavumbi, akainyunyiza juu ya maji, akawanywesha wana wa Israeli.
21 Musa akamwambia Haruni Watu hawa wamekufanyani hata ukaleta dhambi hii kuu juu yao?
22 Haruni akasema, Hasira ya bwana wangu isiwake, wewe unawajua watu hawa, ya kuwa wamejielekeza kwa mabaya.
23 Maana waliniambia, Katufanyie miungu, itakayokwenda mbele yetu, kwa maana mtu huyo Musa, aliyetutoa katika nchi ya Misri, hatujui yaliyompata.
24 Nikawaambia, Mtu ye yote aliye na dhahabu na aivunje; basi wakanipa, nami nikaitupa ndani ya moto, akatoka ndama huyu.
25 Basi Musa alipoona ya kuwa watu hawa wameasi, maana Haruni amewaacha waasi, ili wawe dhihaka kati ya adui zao,
26 ndipo Musa akasimama katika mlango wa marago, akasema, Mtu awaye yote aliye upande wa Bwana, na aje kwangu. Wana wa Lawi wote wakamkusanyikia
27 Akawaambia, Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Kila mtu na ajifunge upanga wake pajani mwake, akapite huko na huko toka mlango hata mlango kati ya marago, mkamchinje kila mtu ndugu yake, na kila mtu mwenziwe na kila mtu jirani yake.
28 Na hao wana wa Lawi wakafanya kama vile alivyosema Musa, wakaanguka siku ile kama watu elfu tatu.
29 Musa akasema, Jiwekeni wakfu kwa Bwana leo, naam, kila mtu juu ya mwanawe na juu ya ndugu yake; ili awape baraka leo.
30 Hata asubuhi yake Musa akawaambia watu, Mmetenda dhambi kuu; na sasa nitakwenda juu kwa Bwana, labda nitafanya upatanisho kwa ajili ya dhambi yenu.
31 Musa akarejea kwa Bwana akasema, Aa! Watu hawa wametenda dhambi kuu wamejifanyia miungu ya dhahabu.
32 Walakini sasa, ikiwa utawasamehe dhambi yao -- na kama sivyo, unifute, nakusihi, katika kitabu chako ulichoandika.
33 Bwana akamwambia Musa, Mtu ye yote aliyenitenda dhambi ndiye nitakayemfuta katika kitabu changu.
34 Basi sasa uende ukawaongoze watu hawa mpaka mahali pale ambapo nimekwambia habari zake; tazama, malaika wangu atakutangulia; pamoja na hayo siku nitakayowajilia nitawapatiliza kwa ajili ya dhambi yao.
35 Bwana akawapiga hao watu, kwa walivyoifanya ile ndama, ambayo Haruni aliifanya.

Kutoka 33


1 Bwana akanena na Musa, Haya, ondokeni, katokeni hapo, wewe na hao watu uliowaleta wakwee kutoka nchi ya Misri, waende nchi hiyo niliyomwapia Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, niliposema, Nitakipa kizazi chako nchi hii;
2 nami nitamtuma malaika aende mbele yako; nami nitawafukuza Mkanaani, na Mwamori, na Mhiti, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi;
3 waifikilie nchi imiminikayo maziwa na asali; kwa maana mimi sitakwenda kati yenu; kwa sababu ninyi ni watu wenye shingo ngumu; nisiwaangamize ninyi katika njia.
4 Watu waliposikia habari hizo mbaya wakaomboleza wala hapana mtu aliyevaa vyombo vyake vya uzuri.
5 Bwana akamwambia Musa, Waambie wana wa Israeli, Ninyi ni watu wenye shingo ngumu; kama mimi nikiingia kati yenu dakika moja, nitawaangamiza; basi sasa vueni vyombo vyenu vya uzuri ili nipate kujua nitakalowatenda.
6 Basi wana wa Israeli wakavua vyombo vyao vyote vya uzuri, tangu mlima wa Horebu na mbele.
7 Basi desturi ya Musa, ilikuwa kuitwaa ile hema, na kuikita nje ya marago mbali na hayo marago; akaiita, hema ya kukutania. Hata kila mtu aliyekuwa akitaka neno kwa Bwana, akatoka, akaenda hata hema ya kukutania, iliyokuwa nje ya marago.
8 Hata Musa alipotoka kuiendea ile hema, watu wote waliondoka wakasimama, kila mtu mlangoni pa hema yake, akamtazama Musa, hata alipokwisha kuingia hemani.
9 Ikawa Musa alipoingia humo hemani, ile nguzo ya wingu ikashuka, ikasimama mlangoni pa ile hema; naye Bwana akasema na Musa.
10 Watu wote wakaiona nguzo ya wingu ikisimama penye mlango wa hema; watu wote wakaondoka wakasujudu, kila mtu mlangoni pa hema yake.
11 Naye Bwana akasema na Musa uso kwa uso, kama vile mtu asemavyo na rafiki yake. Kisha akageuka akarejea hata maragoni; bali mtumishi wake Yoshua, mwana wa Nuni, naye ni kijana, hakutoka mle hemani.
12 Musa akamwambia Bwana, Angalia, wewe waniambia, Wachukue watu hawa; nawe hukunijulisha ni nani utakayemtuma pamoja nami. Walakini umesema, Nakujua jina lako, nawe umepata neema mbele zangu.
13 Basi, sasa nakuomba, ikiwa nimepata neema mbele zako, unionyeshe njia zako, nipate kukujua, ili nipate neema mbele zako; ukakumbuke ya kuwa taifa hilo ndilo watu wako.
14 Akasema, Uso wangu utakwenda pamoja nawe, nami nitakupa raha.
15 Naye akamwambia, Uso wako usipokwenda pamoja nami, usituchukue kutoka hapa.
16 Kwa maana itajulikanaje kuwa nimepata neema mbele zako, mimi na watu wako? Siyo kwa sababu unakwenda pamoja nasi, hata mimi na watu wako tutengwe na watu wote walio juu ya uso wa nchi?
17 Bwana akamwambia Musa, Nitafanya na neno hili ulilolinena, kwa maana umepata neema mbele zangu, nami nakujua jina lako.
18 Akasema, Nakusihi unionyeshe utukufu wako.
19 Akasema, Nitapitisha wema wangu wote mbele yako, nami nitalitangaza jina la Bwana mbele yako; nami nitamfadhili yeye nitakayemfadhili; nitamrehemu yeye nitakayemrehemu.
20 Kisha akasema, Huwezi kuniona uso wangu, maana mwanadamu hataniona akaishi.
21 Bwana akasema, Tazama, hapa pana mahali karibu nami, nawe utasimama juu ya mwamba;
22 kisha itakuwa wakati unapopita utukufu wangu, nitakutia katika ufa wa ule mwamba, na kukufunika kwa mkono wangu hata nitakapokuwa nimekwisha kupita;
23 nami nitaondoa mkono wangu, nawe utaniona nyuma yangu, bali uso wangu hautaonekana.

Kutoka 34


1 Kisha Bwana akamwambia Musa, Chonga mbao mbili za mawe mfano wa zile za kwanza; nami nitaandika juu ya mbao hizo maneno hayo yaliyokuwa juu ya mbao za kwanza, hizo ulizozivunja.
2 Nawe uwe tayari asubuhi, na asubuhi ukwee juu katika mlima wa Sinai, nawe hudhurisha nafsi yako kwangu huko katika kilele cha mlima.
3 Asikwee mtu pamoja nawe, wala asionekane mtu awaye yote katika huo mlima; wala kondoo na ng'ombe wasilishe mbele ya huo mlima.
4 Naye akachonga mbao mbili za mawe mfano wa zile za kwanza; na Musa akainuka na mapema asubuhi, naye akakwea katika mlima wa Sinai, kama Bwana alivyomwamuru, akazichukua hizo mbao mbili za mawe mkononi mwake.
5 Bwana akashuka ndani ya lile wingu, akasimama pamoja naye huko, akalitangaza jina la Bwana.
6 Bwana akapita mbele yake, akatangaza, Bwana, Bwana, Mungu mwingi wa huruma, mwenye fadhili, si mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema na kweli;
7 mwenye kuwaonea huruma watu elfu elfu, mwenye kusamehe uovu na makosa na dhambi; wala si mwenye kumhesabia mtu mwovu kuwa hana hatia kamwe; mwenye kuwapatiliza watoto uovu wa baba zao, na wana wa wana wao pia, hata kizazi cha tatu na cha nne.
8 Musa akafanya haraka, akainamisha kichwa chake hata nchi, akasujudu.
9 Akasema, Ikiwa sasa nimepata neema mbele zako, Bwana, nakuomba, Bwana, uende kati yetu, maana ni watu wenye shingo ngumu; ukasamehe uovu wetu na dhambi yetu, ukatutwae tuwe urithi wako.
10 Akasema, Tazama, nafanya agano; mbele ya watu wangu wote nitatenda miujiza, ya namna isiyotendeka katika dunia yote, wala katika taifa lo lote; na watu wote ambao unakaa kati yao wataona kazi ya Bwana, kwa maana ni neno la kutisha nikutendalo.
11 Liangalie neno hili ninalokuamuru leo; tazama, mbele yako namtoa Mwamori, na Mkanaani, na Mhiti, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi.
12 Ujihadhari nafsi yako, usije ukafanya agano na wenyeji wa nchi ile unayoiendea, lisiwe mtego katikati yako.
13 Bali utabomoa madhabahu zao, na kuvunja-vunja nguzo zao, na kuyakata-kata maashera yao.
14 Maana hutamwabudu mungu mwingine, kwa kuwa Bwana, ambaye jina lake ni mwenye wivu, ni Mungu mwenye wivu.
15 Usije ukafanya agano na wenyeji wa nchi, watu wakaenda kufanya uzinzi na miungu yao, na kuitolea sadaka miungu yao; mtu mmoja akakuita, ukaila sadaka yake.
16 Ukawaoza wana wako binti zao, nao binti zao wakaenda kufanya uzinzi na miungu yao, wakawavuta wana wenu wafanye uzinzi na miungu yao.
17 Usijifanyizie miungu ya kuyeyusha.
18 Hiyo sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu utaitunza. Utakula mikate isiyotiwa chachu muda wa siku saba, kama nilivyokuagiza, kwa majira yaliyoaganwa katika mwezi wa Abibu; kwa kuwa ulitoka Misri katika mwezi huo wa Abibu.
19 Kila kifunguacho mimba ni changu mimi; na wanyama wako wote walio waume, wazaliwa wa kwanza wa ng'ombe na wa kondoo.
20 Na mzaliwa wa kwanza wa punda utamkomboa kwa mwana-kondoo; tena kwamba hutaki kumkomboa, ndipo utamvunja shingo. Wazaliwa wa kwanza wote wa wanao utawakomboa. Wala hapana atakayehudhuria mbele zangu mikono mitupu.
21 Utafanya kazi siku sita, lakini katika siku ya saba utapumzika; wakati wa kulima mashamba, na wakati wa kuvuna pia, utapumzika.
22 Nawe utaitunza sikukuu ya majuma, nayo ni ya malimbuko ya mavuno ya ngano, na sikukuu ya kukusanya vitu mwisho wa mwaka.
23 Mara tatu kila mwaka watu waume wako wote watahudhuria mbele za Bwana MUNGU, Mungu wa Israeli.
24 Kwa kuwa mimi nitazitupa nje taifa za watu mbele yako, na kuipanua mipaka yako; wala hapana mtu ye yote atakayeitamani nchi yako, hapo utakapokwea kwenda kuhudhuria mbele za Bwana Mungu wako mara tatu kila mwaka.
25 Usisongeze damu ya sadaka yangu pamoja na mkate uliotiwa chachu; wala hiyo sadaka ya sikukuu ya pasaka haitasazwa hata asubuhi.
26 Vitu vya kwanza vya malimbuko ya nchi yako utavileta na kuvitia ndani ya nyumba ya Bwana Mungu wako. Usimtokose mwana-mbuzi katika maziwa ya mama yake.
27 Bwana akamwambia Musa, Andika maneno haya; kwa kuwa mimi nimefanya agano nawe, na pamoja na Israeli, kwa mujibu wa maneno haya.
28 Naye alikuwa huko pamoja na Bwana siku arobaini na masiku yake; hakula chakula, wala hakunywa maji. Naye akaandika katika hizo mbao, hayo maneno ya maagano, hizo amri kumi.
29 Hata ikawa, Musa aliposhuka katika mlima Sinai, na zile mbao mbili za ushuhuda zilikuwa mkononi mwa Musa, hapo aliposhuka katika mlima, Musa hakujua ya kuwa ngozi ya uso wake iling'aa kwa sababu amesema naye.
30 Basi Haruni na wana wote wa Israeli walipomwona Musa, tazama, ngozi ya uso wake iling'aa; nao wakaogopa kumkaribia.
31 Musa akawaita; Haruni na wakuu wote wa kusanyiko wakarudi kwake; Musa akasema nao.
32 Baadaye wana wa Israeli wote wakakaribia; akawausia maneno yote ambayo Bwana amemwambia katika mlima Sinai.
33 Na Musa alipokuwa amekwisha kusema nao, akatia utaji juu ya uso wake.
34 Lakini desturi ya Musa ilikuwa alipoingia mbele za Bwana kusema naye, kuuvua huo utaji mpaka atoke; akatoka akawaambia wana wa Israeli maneno yote aliyoambiwa.
35 Wana wa Israeli wakauona uso wa Musa ya kuwa ngozi ya uso wake Musa iling'aa; naye Musa akautia utaji juu ya uso wake tena, hata alipoingia kusema naye.

Kutoka 35


1 Musa akakutanisha mkutano wote wa wana wa Israeli, na kuwaambia, Maneno aliyoyausia Bwana ni haya, kwamba myafanye.
2 Fanyeni kazi siku sita, lakini siku ya saba itakuwa siku takatifu kwenu; ni Sabato ya kustarehe kabisa kwa Bwana; mtu awaye yote atakayefanya kazi yo yote katika siku hiyo atauawa.
3 Hamtawasha moto katika nyumba zenu kwa siku ya Sabato.
4 Kisha Musa akanena na mkutano wote wa wana wa Israeli, akawaambia, Neno hili ndilo aliloliamuru Bwana, akisema,
5 Katwaeni kati yenu matoleo kwa Bwana; mtu awaye yote aliye na moyo wa kupenda, ayalete matoleo; dhahabu na fedha na shaba;
6 na nyuzi za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na za rangi nyekundu, na kitani nzuri, na singa za mbuzi;
7 na ngozi za kondoo waume zilizotiwa rangi nyekundu, na ngozi za pomboo, na mbao za mshita;
8 na mafuta kwa hiyo taa, na viungo vya manukato kwa hayo mafuta ya kutiwa, na kwa huo uvumba mzuri;
9 na vito vya shohamu, na vito vya kutiwa kwa hiyo naivera, na kwa hicho kifuko cha kifuani.
10 Na kila mtu kati yenu aliye na moyo wa hekima na aje, na kuyafanya hayo yote ambayo Bwana ameyaagiza;
11 yaani, hiyo maskani na hema yake, na kifuniko chake, na vifungo vyake, na mbao zake, na mataruma yake, na viguzo vyake, na matako yake;
12 hilo sanduku, na miti yake, na hicho kiti cha rehema, na lile pazia la sitara;
13 na hiyo meza, na miti yake, na vyombo vyake vyote, na hiyo mikate ya wonyesho;
14 na hicho kinara cha taa kwa mwanga, na vyombo vyake, na taa zake, na hayo mafuta kwa nuru;
15 na hiyo madhabahu ya kufukizia uvumba, na miti yake, na hayo mafuta ya kupaka, na huo uvumba mzuri, na hicho kisitiri cha mlango, mlangoni mwa hiyo maskani;
16 na hiyo madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, pamoja na wavu wake wa shaba, na miti yake, na vyombo vyake vyote, na hilo birika na tako lake;
17 na hizo kuta za nguo za ua, na viguzo vyake, na matako yake, na pazia la lango la ua;
18 na vile vigingi vya maskani, na vigingi vya ua, na kamba zake
19 na mavazi yenye kufumwa kwa uzuri, kwa ajili ya kutumika ndani ya mahali patakatifu, hayo mavazi matakatifu ya Haruni kuhani, na mavazi ya wanawe, ili kutumika katika kazi ya ukuhani.
20 Basi mkutano wote wa wana wa Israeli wakaondoka hapo mbele ya Musa.
21 Wakaja kila mtu ambaye moyo wake ulimhimiza, na kila mtu ambaye roho yake ilimfanya kuwa apenda, nao wakaleta sadaka za kumpa Bwana, kwa kazi ya hema ya kukutania, na kwa utumishi wake, na kwa hayo mavazi matakatifu.
22 Nao wakaja, waume kwa wake, wote waliokuwa na moyo wa kupenda, wakaleta vipini, na hazama, na pete za muhuri, na vikuku, na vyombo vyote vya dhahabu; kila mtu aliyetoa toleo la dhahabu la kumpa Bwana.
23 Tena kila mtu aliyeona kwake nyuzi za rangi ya samawi, na nyuzi za rangi ya zambarau, na nyekundu, na kitani nzuri, na singa za mbuzi, na ngozi za kondoo waume zilizotiwa rangi nyekundu, na ngozi za pomboo, akavileta.
24 Kila mtu aliyetoa toleo la fedha, na la shaba, akaileta sadaka ya Bwana; na kila mtu, aliyeona kwake mti wa mshita kwa kazi yo yote ya huo utumishi, akauleta.
25 Na wanawake wote waliokuwa na mioyo ya hekima, walisokota kwa mikono yao, nao wakaleta hizo walizokuwa wamezisokota, nguo za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na hizo nyuzi nyekundu, na hiyo nguo ya kitani nzuri.
26 Na wanawake wote ambao mioyo yao iliwahimiza katika hekima wakasokota hizo singa za mbuzi.
27 Na hao wakuu wakavileta vile vito vya shohamu, na vito vya kutiwa, kwa hiyo naivera, na kwa hicho kifuko cha kifuani,
28 na viungo vya manukato, na mafuta; kwa hiyo taa, na kwa hayo mafuta ya kutiwa, na kwa huo uvumba mzuri.
29 Wana wa Israeli wakaleta sadaka za kumpa Bwana kwa moyo wa kupenda; wote, waume kwa wake, ambao mioyo yao iliwafanya kuwa wapenda kuleta kwa hiyo kazi, ambayo Bwana aliamuru ifanywe kwa mkono wa Musa.
30 Kisha Musa akawaambia wana wa Israeli, Angalieni, Bwana amemwita kwa jina lake Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa kabila ya Yuda;
31 naye amemjaza roho ya Mungu, katika hekima, na akili, na ujuzi, na kazi ya ustadi kila aina;
32 na kuvumbua kazi za werevu, na kufanya kazi ya dhahabu, na fedha, na shaba,
33 na kukata vito vya kutilia, na kuchora miti, atumike katika kazi za werevu kila aina.
34 Naye amemtilia moyoni mwake ili apate kufundisha, yeye, na Oholiabu mwana wa Ahisamaki, wa kabila ya Dani.
35 Amewajaza watu hao akili za moyoni, ili watumike katika kazi kila aina, ya mwenye kuchora mawe, na kazi ya werevu, na ya mwenye kutia taraza, katika nyuzi za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na nyekundu, na kitani nzuri, na ya mwenye kufuma nguo; ya hao wafanyao kazi yo yote, na ya wenye kuvumbua kazi za werevu.

Kutoka 36


1 Basi Bezaleli na Oholiabu watatenda kazi, na kila mtu mwenye moyo wa hekima, ambaye Bwana amemtia akili na hekima ili ajue kufanya kazi hiyo yote kwa huo utumishi wa mahali patakatifu, kama hayo yote Bwana aliyoyaagiza.
2 Basi Musa akawaita Bezaleli na Oholiabu, na kila mtu aliyekuwa na moyo wa akili, ambaye Bwana alimtia moyoni mwake hekima, kila mtu ambaye moyo wake ulimhimiza ili aende kuifanya kazi hiyo;
3 nao wakapokea mkononi mwa Musa matoleo yote, ambayo hao wana wa Israeli walikuwa wameyaleta kwa ajili ya huo utumishi wa mahali patakatifu, ili wapafanye. Kisha wakamletea matoleo kila siku asubuhi kwa moyo wa kupenda.
4 Na hao watu wote wenye hekima, waliotumika katika kazi yote ya mahali patakatifu, wakaenda kila mtu kutoka katika kazi yake aliyokuwa akiifanya;
5 nao wakasema na Musa, na kumwambia, Watu waleta vitu vingi sana zaidi ya hivyo vitoshavyo kwa ajili ya utumishi wa hiyo kazi, ambayo Bwana aliagiza ifanywe.
6 Basi Musa akatoa amri, nao wakatangaza mbiu katika marago yote, wakisema, Wasifanye kazi tena, mtu mume wala mwanamke, kwa ajili ya matoleo kwa mahali patakatifu. Basi watu wakazuiwa wasilete tena.
7 Kwani vile vitu walivyokuwa navyo vilikuwa vyatosha kwa kuifanya kazi hiyo yote, kisha vilizidi.
8 Basi kila mtu mwenye moyo wa hekima miongoni mwa hao waliofanya kazi, akaifanya hiyo maskani ya mapazia kumi; ya nguo ya kitani nzuri ya kusokotwa, na nyuzi za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na nyekundu; pamoja na makerubi, kazi ya fundi stadi; ndivyo alivyoyafanya.
9 Urefu wa kila pazia ulikuwa ni dhiraa ishirini na nane, na upana wa kila pazia ulikuwa ni dhiraa nne; mapazia yote yalikuwa ya kipimo kimoja.
10 Naye akaunganisha mapazia matano hili na hili; na mapazia matano mengine akayaunganisha hili na hili.
11 Kisha akafanya matanzi ya rangi ya samawi katika ncha za pazia moja, katika upindo wa kiungo chake; akafanya vivyo katika ncha ya pazia lililokuwa upande wa nje katika kiungo cha pili.
12 Akafanya matanzi hamsini katika pazia moja, na matanzi hamsini katika upindo wa pazia lililokuwa katika kiungo cha pili; hayo matanzi yalikuwa yakabiliana hili na hili.
13 Kisha akafanya vifungo hamsini vya dhahabu, na kuyaunganya hayo mapazia hili na hili kwa vile vifungo; hivi ile maskani ilikuwa ni moja.
14 Kisha akafanya vifuniko vya singa za mbuzi kuwa hema ya kuifunika hiyo maskani; akafanya mapazia kumi na moja.
15 Urefu wa kila pazia ulikuwa ni dhiraa thelathini, na upana wa kila pazia ulikuwa ni dhiraa nne; hayo mapazia yote kumi na moja yalikuwa ya kipimo kimoja.
16 Naye akaunganya mapazia matano mbali, na mapazia sita mbali.
17 Kisha akafanya matanzi hamsini katika upindo wa pazia lililo upande wa nje katika kile kiungo, naye akafanya matanzi hamsini katika ncha ya pazia lililokuwa upande wa nje katika kiungo cha pili.
18 Kisha akafanya vifungo hamsini vya shaba aiunganye ile hema pamoja, ili iwe hema moja.
19 Kisha akafanya kifuniko kwa ajili ya hiyo hema cha ngozi za kondoo waume zilizotiwa rangi nyekundu; tena juu yake akafanya kifuniko cha ngozi za pomboo.
20 Kisha akafanya mbao za mti wa mshita kwa hiyo maskani, zilizosimama.
21 Urefu wa kila ubao ulikuwa ni dhiraa kumi, na upana wa kila ubao ulikuwa ni dhiraa moja na nusu.
22 Kila ubao ulikuwa na ndimi mbili, zilizounganywa pamoja; ndivyo alivyozifanya hizo mbao zote za maskani.
23 Naye akazifanya hizo mbao kwa ajili ya hiyo maskani; mbao ishirini kwa upande wa kusini kuelekea kusini;
24 naye akafanya matako ya fedha arobaini yawe chini ya hizo mbao ishirini; matako mawili chini ya ubao mmoja kwa hizo ndimi zake mbili, na matako mawili chini ya ubao mwingine kwa ndimi zake mbili.
25 Na kwa upande wa pili wa maskani upande wa kaskazini, akafanya mbao ishirini,
26 na matako yake ya fedha arobaini; matako mawili chini ya ubao mmoja, na matako mawili chini ya ubao mwingine.
27 Na kwa upande wa nyuma wa hiyo maskani kuelekea magharibi akafanya mbao sita.
28 Naye akafanya mbao mbili kwa pembe za maskani upande wa nyuma.
29 Nazo zilikuwa mbao pacha upande wa chini, vivyo zilishikamana pamoja hata ncha ya juu kufikilia pete ya kwanza; ndivyo alivyofanya zote mbili katika hizo pembe mbili.
30 Hivyo zilikuwa mbao nane, na matako yake ya fedha, matako kumi na sita, matako mawili chini ya kila ubao.
31 Kisha akafanya mataruma ya miti ya mshita; matano kwa mbao za upande mmoja wa maskani;
32 na mataruma matano kwa mbao za upande wa pili wa maskani, na mataruma matano kwa hizo mbao za maskani zilizokuwa upande wa nyuma kuelekea magharibi.
33 Naye akalifanya hilo taruma la katikati lipenye kati ya hizo mbao kutoka upande huu hata upande huu.
34 Naye akazifunika hizo mbao dhahabu, akazifanya zile pete zake za dhahabu ziwe mahali pa hayo mataruma, akayafunika dhahabu hayo mataruma.
35 Kisha akafanya hilo pazia la nyuzi za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na nyekundu, na kitani nzuri zilizosokotwa; akatia na makerubi kazi ya fundi stadi, ndivyo alivyofanya.
36 Naye akafanya kwa ajili yake nguzo nne za mti wa mshita, akazifunika dhahabu; na kulabu zake zilikuwa za dhahabu; naye akasubu kwa ajili yake matako manne ya fedha.
37 Kisha akafanya pazia la sitara kwa ajili ya mlango wa Hema, la nguo ya rangi ya samawi, na ya rangi ya zambarau, na nyekundu, na nguo ya kitani nzuri ya kusokotwa, kazi ya mwenye kutia taraza,
38 na nguzo zake tano pamoja na kulabu zake; naye akavifunika dhahabu vichwa vyake na vifungo vyake; na matako yake matano yalikuwa ya shaba.

Kutoka 37


1 Kisha Bezaleli akalifanya lile sanduku la mti wa mshita, urefu wake ulikuwa dhiraa mbili na nusu, na upana wake ulikuwa dhiraa moja na nusu, na kwenda juu kwake kulikuwa ni dhiraa moja na nusu;
2 akalifunika dhahabu safi, ndani na nje, akafanya na ukingo wa dhahabu kulizunguka pande zote.
3 Naye akasubu pete nne za dhahabu kwa ajili yake, katika miguu yake minne; pete mbili upande wake mmoja na pete mbili upande wake wa pili.
4 Akafanya na miti ya kulichukulia, ya mti wa mshita akaifunika dhahabu.
5 Naye akaitia hiyo miti katika zile pete zilizokuwa ubavuni mwa sanduku, ili kulichukua hilo sanduku.
6 Kisha akafanya kiti cha rehema cha dhahabu safi; urefu wake ulikuwa dhiraa mbili na nusu na upana wake ulikuwa dhiraa moja na nusu.
7 Kisha akafanya makerubi mawili ya dhahabu; akayafanya ya kazi ya kufua, yawe katika miisho miwili ya kiti cha rehema;
8 kerubi moja mwisho huu, na kerubi moja mwisho huu; alifanya hayo makerubi mawili ya kitu kimoja na hicho kiti cha rehema katika miisho yake miwili.
9 Na hayo makerubi yakayanyosha mabawa yao juu, na kukifunika hicho kiti cha rehema kwa mabawa yao, na nyuso zao zilikuwa zaelekeana hili na hili; nyuso za hayo makerubi zilikuwa zikielekea kiti cha rehema.
10 Kisha akafanya hiyo meza ya mti wa mshita; urefu wake ulikuwa ni dhiraa mbili, na upana wake ulikuwa ni dhiraa moja, na kwenda juu kwake kulikuwa ni dhiraa moja na nusu;
11 naye akaifunika dhahabu safi, akaifanyia ukingo wa dhahabu kuizunguka pande zote.
12 Kisha akaifanyia upapi wa upana wa shibiri kuizunguka pande zote, akauzungushia ukingo wa urembo wa dhahabu ule upapi.
13 Naye akasubu vikuku vinne vya dhahabu kwa ajili yake, akavitia vile vikuku katika pembe nne, katika miguu yake minne.
14 Vile vikuku vilikuwa karibu na ule upapi, ili viwe mahali pa kutilia ile miti, ya kuichukulia meza.
15 Naye akaifanya hiyo miti ya kuichukulia, ya mti wa mshita, akaifunika dhahabu, ili kuichukua hiyo meza.
16 Kisha, vile vyombo vilivyokuwa juu ya meza, sahani zake, na miiko yake, na bakuli zake, na makopo yake ya kumiminia, akavifanya vya dhahabu safi.
17 Kisha akakifanya kile kinara cha taa cha dhahabu safi, akakifanya kile kinara cha taa cha kazi ya kufua, tako lake, na mti wake; vikombe vyake, na matovu yake, na maua yake, vyote vilikuwa vya kitu kimoja nacho,
18 nacho kilikuwa na matawi sita yaliyotoka ubavuni mwake; matawi matatu ya kinara yalikuwa upande huu, na matawi matatu ya kinara yalikuwa upande huu;
19 vikombe vitatu, vilivyofanywa mfano wa maua ya mlozi vilikuwa katika tawi moja, tovu na ua; na vikombe vitatu, vilivyofanywa mfano wa maua ya mlozi, katika tawi la pili, tovu na ua; yalikuwa ni vivyo hivyo yale matawi sita yaliyokuwa katika hicho kinara.
20 Katika kinara mlikuwa na vikombe vinne, vilivyofanywa mfano wa maua ya mlozi, matovu yake na maua yake;
21 kisha chini ya matawi mawili mlikuwa na tovu iliyokuwa ya kitu kimoja nacho, na chini ya matawi mawili mengine mlikuwa na tovu ya kitu kimoja nacho, tena chini ya matawi mawili hayo mengine mlikuwa na tovu ya kitu kimoja nacho; kwa ajili ya hayo matawi sita, yaliyotokana nacho.
22 Hayo matovu yake na matawi yake yalikuwa ya kitu kimoja nacho; kinara hicho kizima chote pia ni kazi moja ya kufua ya dhahabu safi.
23 Kisha akafanya taa zake saba, na makoleo yake, na visahani vyake, vya dhahabu safi.
24 Akakifanya cha talanta moja ya dhahabu safi, pamoja na vyombo vyake vyote.
25 Kisha akafanya hiyo madhabahu ya kufukizia uvumba ya mti wa mshita; urefu wake ulikuwa ni dhiraa moja, na upana wake ulikuwa ni dhiraa moja, ilikuwa mraba; na kwenda juu kwake kulikuwa ni dhiraa mbili; na pembe zake zilikuwa za kitu kimoja nayo.
26 Naye akaifunika dhahabu safi, upande wa juu, na mbavu zake pande zote, na hizo pembe zake; akaifanyia na ukingo wa dhahabu kuizunguka pande zote.
27 Naye akaifanyia vikuku viwili vya dhahabu na kuvitia chini ya ukingo wake, katika mbavu zake mbili, katika pande zake mbili, viwe ni mahali pa hiyo miti ya kuichukulia.
28 Kisha akafanya hiyo miti kwa mti wa mshita, na kuifunika dhahabu.
29 Kisha akayafanya hayo mafuta matakatifu ya kutiwa, na ule uvumba safi wa viungo vya manukato vizuri, kwa kuandama kazi ya mtengezaji manukato.

Kutoka 38


1 Kisha akafanya hiyo madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, ya mti wa mshita urefu wake ulikuwa dhiraa tano, na upana wake ulikuwa dhiraa tano, ilikuwa mraba; na kwenda juu kwake kulikuwa dhiraa tatu.
2 Naye akazifanya pembe zake katika ncha zake nne; hizo pembe zilikuwa za kitu kimoja nayo; naye akaifunika shaba.
3 Kisha akafanya vyombo vyote vya madhabahu, yaani sufuria zake, na majembe yake, na mabakuli yake, na uma zake, na meko yake; vyombo vyake vyote akavifanya vya shaba.
4 Naye akaifanyia madhabahu wavu wa shaba, akautia chini ya ukingo kuizunguka pande zote, ukawa katikati ya hiyo madhabahu.
5 Naye akasubu vikuku vinne kwa kutiwa katika pembe nne za huo wavu wa shaba, viwe mahali pa kutia ile miti ya kuichukulia.
6 Naye akaifanya hiyo miti kwa mti wa mshita na kuifunika shaba.
7 Naye akaitia ile miti katika vile vikuku vilivyokuwa katika mbavu za hiyo madhabahu, ili kuichukua; akaifanya yenye mvungu ndani, kwa zile mbao.
8 Kisha akafanya hilo birika la shaba, na tako lake la shaba; shaba hiyo ilikuwa ni ya vioo vya wanawake wenye kutumika, waliokuwa wakitumika mlangoni mwa hema ya kukutania.
9 Naye akafanya ule ua; upande wa kusini kwa kuelekea kusini, chandarua ya ua ilikuwa ya nguo ya kitani nzuri ya kusokotwa, kiasi cha dhiraa mia;
10 nguzo zake zilikuwa ishirini, na matako yake yalikuwa ishirini, yalikuwa ya shaba; kulabu za nguzo na vitanzi vyake vilikuwa vya fedha.
11 Upande wa kaskazini ulikuwa ni dhiraa mia vivyo, nguzo zake ishirini na matako yake ishirini, yalikuwa ni ya shaba; kulabu za nguzo na vitanzi vyake vilikuwa vya fedha.
12 Upande wa magharibi mlikuwa na chandarua ya dhiraa hamsini, nguzo zake zilikuwa ni kumi, na matako yake kumi; kulabu za hizo nguzo na vitanzi vyake vilikuwa vya fedha.
13 Upande wa mashariki kuelekea mashariki dhiraa hamsini.
14 Chandarua ya upande mmoja wa lango ilikuwa dhiraa kumi na tano urefu wake; na nguzo zake tatu, na matako yake matatu;
15 ni vivyo upande wa pili; upande huu na huu langoni mwa ua mlikuwa na chandarua ya dhiraa kumi na tano urefu wake; nguzo zake zilikuwa ni tatu, na matako yake matatu.
16 Chandarua za nguo zote za ule ua zilizouzunguka pande zote zilikuwa za nguo ya kitani nzuri iliyosokotwa.
17 Na matako ya zile nguzo yalikuwa ya shaba; kulabu za hizo nguzo na vitanzi vyake vilikuwa vya fedha; na vichwa vya zile nguzo vilikuwa ni vya fedha; na nguzo zote za huo ua ziliungwa kwa vitanzi vya fedha.
18 Na hilo pazia la lango la ua, lilikuwa ni kazi ya mwenye kutia taraza, lilikuwa la nyuzi za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na nyekundu, na kitani nzuri ya kusokotwa; lilikuwa na urefu wake dhiraa ishirini, na kutukuka kwake katika huo upana wake kulikuwa dhiraa tano, kupatana na ile chandarua ya ua.
19 Na nguzo zake zilikuwa nne, na matako yake manne, yalikuwa ya shaba; kulabu zake zilikuwa za fedha, na vichwa vyake na vitanzi vyake vilikuwa vya fedha.
20 Na vigungi vyote vya maskani, na vya ua ulioizunguka pande zote vilikuwa vya shaba.
21 Jumla ya vile vyombo vilivyofanywa kwa ajili ya hiyo maskani, hiyo maskani ya ushuhuda ni hii, kama vilivyohesabiwa, kama maagizo ya Musa yalivyokuwa, kwa ajili ya utumishi wa Walawi kwa mkono wa Ithamari, mwana wa Haruni, kuhani.
22 Na Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa kabila ya Yuda, akafanya yote Bwana aliyomwagiza Musa.
23 Na pamoja naye alikuwa na Oholiabu, mwana wa Ahisamaki, wa kabila ya Dani, aliyekuwa fundi wa kuchora nakshi, mfanyaji wa kazi mwerevu, naye alikuwa mwenye kutia taraza za nyuzi za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na nyekundu, na kitani nzuri.
24 Dhahabu yote iliyotumiwa kwa ajili ya hiyo kazi, katika kazi hiyo yote ya mahali patakatifu, hiyo dhahabu ya matoleo, ilikuwa ni talanta ishirini na kenda, na shekeli mia saba na thelathini, kwa kadiri ya shekeli ya mahali patakatifu.
25 Na fedha ya hao waliohesabiwa, watu wa huo mkutano ilikuwa talanta mia, na shekeli elfu moja na mia saba na sabini na tano kwa kadiri ya shekeli ya mahali patakatifu;
26 kichwa beka, maana, nusu shekeli, kwa kadiri ya shekeli ya mahali patakatifu, kwa ajili ya kila mtu aliyepita kwa wale waliohesabiwa, aliyekuwa wa umri wa miaka ishirini au zaidi, kwa ajili ya watu waume sita mia na tatu elfu, na mia tano na hamsini (603,550).
27 Na hizo talanta mia za fedha zilikuwa kwa kusubu yale matako ya mahali patakatifu na matako ya hilo pazia; matako mia kwa hizo talanta mia, talanta moja tako moja.
28 Na kwa hizo shekeli elfu moja na mia saba, na sabini na tano, akafanya vifungo vya hizo nguzo, na kuvifunika fedha vile vichwa vyake, na kufanya vitanzi vyake.
29 Na hiyo shaba iliyoletwa ilikuwa ni talanta sabini, na shekeli elfu mbili na mia nne.
30 Naye akafanya ya hiyo shaba matako kwa ajili ya lango la hema ya kukutania, na hiyo madhabahu ya shaba, na ule wavu wa shaba kwa ajili yake na vyombo vyote vya hiyo madhabahu,
31 na matako ya ua kuuzunguka pande zote, na matako ya lango la huo ua, na vigingi vyote vya maskani, na vigingi vyote vya huo ua uliozunguka pande zote.

Kutoka 39


1 Na zile nyuzi za rangi ya samawi, na nyuzi za rangi ya zambarau, na nyekundu, wakafanya mavazi yaliyofumwa kwa ustadi sana kwa ajili ya kutumika katika mahali patakatifu, na kuyafanya hayo mavazi matakatifu ya Haruni, vile vile kama Bwana alivyomwagiza Musa.
2 Naye akaifanya hiyo naivera, ya nyuzi za dhahabu, na za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na za rangi nyekundu, na kitani nzuri ya kusokotwa.
3 Nao wakaifua hiyo dhahabu hata ikawa mabamba membamba sana, kisha wakaikata iwe nyuzi, ili wapate kuifuma pamoja na hizo nyuzi za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na nyuzi nyekundu na za kitani nzuri, kazi ya fundi stadi sana.
4 Nao wakafanya na vipande vya mabegani kwa ajili yake, vilivyoungwa pamoja; viliungwa pamoja kwa ncha zake mbili.
5 Na huo mshipi wa kazi ya werevu, uliokuwa juu yake ili kuifunga mahali pake; ulikuwa wa kitu kimoja, na wa kazi moja na naivera ya dhahabu, na rangi ya samawi, na rangi ya zambarau, na nyekundu, na kitani nzuri ya kusokotwa; vile vile kama Bwana alivyomwagiza Musa.
6 Nao wakavitengeza vile vito vya shohamu, vilivyotiwa katika vijalizo vya dhahabu, vilivyochorwa mfano wa kuchora kwake muhuri, kwa majina ya hao wana wa Israeli.
7 Naye akavitia katika vile vipande vya mabegani vya hiyo naivera, viwe vito vya ukumbusho kwa wana wa Israeli, kama Bwana alivyomwagiza Musa.
8 Naye akafanya kile kifuko cha kifuani, kazi ya fundi stadi, kama hiyo kazi ya naivera; ya nyuzi za dhahabu, na za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na nyekundu, na kitani nzuri ya kusokotwa.
9 Kilikuwa mraba; wakakifanya kile kifuko cha kifuani kwa kukikunja; urefu wake ulikuwa shibiri, na upana wake ulikuwa shibiri, tena kilikuwa ni cha kukunjwa.
10 Nao wakatia safu nne za vito ndani yake, safu moja ilikuwa ni akiki, na yakuti ya rangi ya manjano, na baharamani, vilikuwa ni safu ya kwanza.
11 Na safu ya pili ilikuwa zumaridi, na yakuti samawi, na almasi.
12 Na safu ya tatu ilikuwa ni hiakintho, na akiki nyekundu, na amethisto.
13 Na safu ya nne ilikuwa ni zabarajadi, na shohamu, na yaspi: vito hivyo vilikuwa vimetiwa katika vijalizo vya dhahabu, kila kimoja mahali pake.
14 Na hivyo vito vilikuwa vyaandama majina ya wana wa Israeli, kumi na mawili, sawasawa na majina yao; mfano wa kuchora muhuri, kila moja kwa jina lake, kwa zile kabila kumi na mbili.
15 Nao wakafanya katika kile kifuko cha kifuani mikufu mfano wa kamba, ya kazi ya kusokotwa ya dhahabu safi.
16 Nao wakafanya vijalizo viwili vya dhahabu, na pete mbili za dhahabu; nao wakazitia hizo pete mbili katika ncha mbili za hicho kifuko.
17 Nao wakaitia hiyo mikufu miwili iliyosokotwa katika hizo pete mbili zilizokuwa katika ncha mbili za hicho kifuko.
18 Na ncha hizo mbili nyingine, za hiyo mikufu miwili ya kusokotwa, wakazitia katika vile vijalizo viwili, na kuvitia katika vile vipande vya mabegani vya naivera, upande wa mbele.
19 Nao wakafanya pete mbili za dhahabu, na kuzitia katika ncha mbili za kifuko cha kifuani, katika ukingo wake, ulio upande wa naivera ulio ndani.
20 Nao wakafanya pete mbili za dhahabu, na kuzitia katika vile vipande viwili vya ile naivera chini yake, upande wa mbele, karibu na kifungo chake, juu ya huo mshipi wa naivera uliosukwa kwa ustadi.
21 Nao wakakikaza kile kifuko kwa pete zake kwenye naivera kwa ukanda wa rangi ya samawi, ili kikae pale juu ya mshipi wa naivera uliosukwa kwa ustadi, na ya kwamba kifuko cha kifuani kisiachane na naivera; vile vile kama Bwana alivyomwagiza Musa.
22 Naye akafanya hiyo joho ya naivera ya kazi ya kusuka, rangi ya samawi yote;
23 na hilo tundu lililokuwa katikati yake, mfano wa tundu lililo katika kanzu ya chuma, na utepe wake kulizunguka hilo tundu, ili lisipasuke.
24 Nao wakatia katika upindo wa joho makomamanga ya nyuzi za rangi ya samawi, na rangi ya zambarau, na rangi nyekundu, na kitani iliyosokotwa.
25 Nao wakafanya njuga za dhahabu safi, na kuzitia hizo njuga kati ya hayo makomamanga pande zote, kati ya hayo makomamanga;
26 njuga na komamanga, njuga na komamanga katika pindo za joho kuizunguka pande zote, ili kutumika kwa hiyo; vile vile kama Bwana alivyomwagiza Musa.
27 Nao wakafanya hizo kanzu za nguo ya kitani nzuri ya kufumwa, kwa Haruni, na kwa wanawe
28 na hicho kilemba cha nguo ya kitani nzuri, na zile kofia nzuri za kitani, na hizo suruali za nguo ya kitani nzuri iliyosokotwa,
29 na huo mshipi wa nguo nzuri ya kitani iliyosokotwa, na rangi ya samawi, na rangi ya zambarau, na nyekundu, kazi ya fundi mwenye kutia taraza; vile vile kama Bwana alivyomwagiza Musa.
30 Nao wakafanya hilo bamba la hiyo taji takatifu la dhahabu safi, na kuandika juu yake andiko, mfano wa kuchorwa kwa muhuri, MTAKATIFU KWA Bwana.
31 Nao wakatia ukanda wa rangi ya samawi ili kulifunga katika hicho kilemba upande wa juu; vile vile kama Bwana alivyomwagiza Musa.
32 Basi ndivyo ilivyomalizwa kazi yote ya maskani ya hema ya kukutania; na wana wa Israeli walifanya kama yote Bwana aliyomwagiza Musa, ndivyo walivyofanya.
33 Nao wakamletea Musa hiyo maskani; yaani Hema, na vyombo vyake vyote, vifungo vyake, na mbao zake, na mataruma yake, na nguzo zake, na matako yake;
34 na kifuniko chake cha ngozi za kondoo waume zilizotiwa rangi nyekundu, na kifuniko cha ngozi za pomboo, na pazia la sitara;
35 na sanduku la ushuhuda, na miti yake, na kiti cha rehema;
36 na meza, na vyombo vyake vyote, na mikate ya wonyesho;
37 na kinara cha taa safi, na taa zake, hizo taa za kuwekwa mahali pake, na vyombo vyake vyote, na mafuta ya taa,
38 na madhabahu ya dhahabu, na mafuta ya kutiwa, na uvumba mzuri, na pazia kwa mlango wa hema;
39 na madhabahu ya shaba, na wavu wake wa shaba, na miti yake, na vyombo vyake vyote, na birika na tako lake;
40 na ukuta wa nguo wa ua, na nguzo zake na matako yake, na pazia la lango la ua, na kamba zake, na vigingi vyake, na vyombo vyote vya kutumiwa katika utumishi wa maskani, kwa hiyo hema ya kukutania,
41 na mavazi ya kazi nzuri kwa utumishi katika mahali patakatifu, na mavazi matakatifu ya Haruni kuhani, na mavazi ya wanawe, ili kutumika katika kazi ya ukuhani.
42 Sawasawa na yote Bwana aliyomwagiza Musa, ndivyo walivyoifanya hiyo kazi yote wana wa Israeli.
43 Musa akaiona hiyo kazi yote, na tazama, walikuwa wameimaliza; vile vile kama Bwana alivyoagiza, walikuwa wameifanya vivyo; basi Musa akawaombea heri.

Kutoka 40


1 Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
2 Siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza utaisimamisha hiyo maskani ya hema ya kukutania.
3 Nawe utatia ndani yake sanduku la ushuhuda, nawe utalisitiri hilo sanduku kwa pazia.
4 Nawe utaleta meza na kuitia ndani, na kuviweka sawasawa vile vitu juu yake; kisha utakileta ndani kile kinara cha taa, na kuziwasha taa zake.
5 Kisha utaisimamisha madhabahu ya dhahabu kwa kufukizia uvumba mbele ya sanduku la ushuhuda, na kulitia pazia mlangoni mwa hiyo maskani.
6 Kisha utaweka madhabahu ya kuteketeza sadaka mbele ya mlango wa maskani ya hema ya kukutania.
7 Kisha utaliweka birika kati ya hema ya kukutania na hiyo madhabahu, nawe utatia maji ndani yake.
8 Kisha utausimamisha ukuta wa ua kuuzunguka pande zote, na kuitundika sitara ya lango la ua.
9 Kisha utayatwaa mafuta ya kutiwa, na kuitia mafuta hiyo maskani, na kila kitu kilicho ndani yake, na kuiweka iwe takatifu, na vyombo vyake vyote; nayo itakuwa takatifu.
10 Kisha utaitia mafuta madhabahu ya kuteketeza sadaka, na vyombo vyake vyote; na kuiweka takatifu madhabahu; na hiyo madhabahu itakuwa takatifu sana.
11 Kisha utalitia mafuta birika na tako lake, na kuliweka liwe takatifu.
12 Kisha utamleta Haruni na wanawe hapo mlangoni pa hema ya kukutania, nawe utawaosha kwa maji.
13 Kisha utamvika Haruni mavazi matakatifu; nawe utamtia mafuta, na kumweka awe mtakatifu, ili apate kunitumikia katika kazi ya ukuhani.
14 Kisha utawaleta wanawe, na kuwavika kanzu zao;
15 nawe utawatia mafuta kama ulivyomtia mafuta baba yao, ili wanitumikie katika kazi ya ukuhani; na huko kutiwa mafuta kwao kutakuwa ni kwa ukuhani wa milele katika vizazi vyao vyote.
16 Musa akafanya hayo yote; kama yote Bwana aliyoagiza ndivyo alivyofanya.
17 Hata mwezi wa kwanza wa mwaka wa pili, siku ya kwanza ya mwezi ile maskani ilisimamishwa.
18 Musa akaisimamisha maskani, akayaweka matako yake, akazisimamisha mbao zake akayatia mataruma yake, akazisimamisha nguzo zake.
19 Akaitanda hema juu ya maskani, akakitia kifuniko cha hema juu yake; kama Bwana alivyomwamuru Musa.
20 Akautwaa ule ushuhuda, akautia ndani ya sanduku, akaiweka miti ya kuchukulia juu ya sanduku, akakiweka kiti cha rehema juu ya sanduku;
21 kisha akalileta sanduku akalitia ndani ya maskani, naye akalitundika pazia la sitara, akalisitiri sanduku la ushuhuda; kama Bwana alivyomwamuru Musa.
22 Akaitia meza ndani ya hema ya kukutania, upande wa maskani ulioelekea kaskazini, nje ya pazia.
23 Akaipanga ile mikate juu yake mbele za Bwana; kama Bwana alivyomwamuru Musa.
24 Kisha akakitia kinara cha taa ndani ya hema ya kukutania, kuikabili ile meza, upande wa maskani ulioelekea kusini.
25 Kisha akaziwasha taa zake mbele za Bwana, kama Bwana alivyomwamuru Musa.
26 Akaitia madhabahu ya dhahabu ndani ya hema ya kukutania mbele ya pazia.
27 Akafukiza juu yake uvumba wa manukato kama Bwana alivyomwamuru Musa.
28 Akalitia pazia la mlango wa maskani.
29 Akaiweka madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa mlangoni pa maskani ya kukutania, akatoa sadaka ya kuteketezwa juu yake, na sadaka ya unga; kama Bwana alivyomwamuru Musa.
30 Akaliweka birika kati ya hema ya kukutania na madhabahu, akatia maji ndani yake ya kuoshea.
31 Musa na Haruni, na wanawe wakanawa mikono yao na miguu yao ndani yake;
32 hapo walipoingia hema ya kukutania, na hapo walipoikaribia madhabahu walinawa kama Bwana alivyomwamuru Musa.
33 Akausimamisha ukuta wa ua kuizunguka maskani na madhabahu, akalitundika pazia la mlango wa ule ua. Basi Musa akaimaliza hiyo kazi.
34 Ndipo lile wingu likaifunikiza hema ya kukutania, na huo utukufu wa Bwana ukaijaza maskani.
35 Wala Musa hakuweza kuliingia hema la kukutania, kwa sababu lile wingu lilikaa juu yake, na huo utukufu wa Bwana ukaijaza maskani.
36 Na hapo lile wingu lilipoinuliwa kutoka juu ya maskani, wana wa Israeli wakaenda mbele katika safari zao zote,
37 bali kama lile wingu halikuinuliwa, wakati ule hawakusafiri hata siku ile lilipoinuliwa tena.
38 Kwa maana lile wingu la Bwana lilikuwa juu ya maskani wakati wa mchana, na mlikuwa na moto ndani yake wakati wa usiku, mbele ya macho ya nyumba ya Israeli katika safari zao zote.